read

Neno La Mchapishaji

Kitabu kilichoko mikononi mwako ni tarjuma ya kitabu cha Kiarabu kiitwacho al-Haqiqatu ‘dh-Dha’i’ah kilichoandikwa na Sheikh Mu’tasim Sayyid Ahmad. Sisi tumekiita, Ukweli Uliopotea. Kwa vile kitabu hiki ni kikubwa, sisi tumekigawa katika juzuu tano ili kiwe chepesi kusomwa na wasomaji wetu wa Kiswahili. Hiki ulichonacho mkononi mwako ni juzuu ya kwanza.

Kitabu hiki ni utafiti uliofanywa na mwanachuoni huyo wa Kiislamu kuhusu madhehebu za Kiislamu. Utafiti wake huu ulihusisha pia mahojiano na mijadala baina yake na na masheikh wa Kiwahabi na maustadh wake katika chuo alikosoma.

Kama kawaida katika utafiti wake, ametumia sana vitabu vya historia ya Kiislamu na vya hadithi vilivyoondikwa na wanavyuoni wa Sunni na Shia, kisha akahitimisha kwa Qur’ani Tukufu na Sunna. Baadhi ya vitabu hivyo ameviorodhesha ndani ya kitabu hiki ili msomaji aweze kuvirejelea. Lakini bahati mbaya sana mengi ya matoleo mapya ya vitabu hivyo yamefanyiwa mabadiliko na baadhi ya sehemu kuondolewa, hususan zile zinazounga mkono madai ya Shia. Ufuatao hapa chini ni mfano mdogo tu wa yanay- ofanywa katika vitabu hivyo:

Katika ukurasa wa 301 wa juzuu ya 3 ya Tafsir al-Kashshaaf iliyokusany- wa chini ya maelekezo ya Sheikh Mustafa al-Halabi (toleo la pili, 1319 A.H. liliochapishwa na Main Government Printing House ya Amiriah Bulaq ya Misri), beti zinazojitokeza ambazo kwazo Jarallah Zamakhshari, mfasiri wa al-Kashshaaf, alitangaza wazi imani yake katika uhalali wa Ushia. Lakini katika toleo la mwaka wa 1373 A.H. kutoka Printing House Istiqamah bi ‘l-Qahara, shairi lililotajwa halionekani tena.

Marehemu Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi katika kitabu chake kiitwa- cho, Uimamu, ukurasa wa 37, anaandika kushangazwa kwake kutokana na maneno yaliyoondolewa katika kitabu cha at-Tarikhat-Tabari, chapa ya Leiden (ya mwaka 1879 Miladia). Chapa hii ya Leiden imeyanakili maneno ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w) aliyoyatumia wakati wa karamu mashuhuri ya ndugu wa karibu aliyoitayarisha ambapo katika khutba yake alisema: “Enyi watu wangu! Huyu Ali ni ndugu yangu, Wasii wangu na Khalifa wangu miongoni mwenu; msikilizeni na mtiini.” Lakini katika chapa ya Misri ya mwaka 1963, (chapa inayodaiwa kuwa imechekiwa na ile ya Leiden) maneno haya muhimu: “Wasii wangu na Khalifa wangu” yamebadilishwa na kuandikwa “kadha wa kadha” na kusomeka hivi: “Huyu Ali ni ndugu yangu na kadha wa kadha.” Huu ni msiba mkubwa.

Huu ni mchezo umefanywa na unaendelea kufanywa mpaka leo. Na lengo ni kuficha ukweli. Lakini hata hivyo, ‘ukweli siku zote unaelea’; matoleo ya zamani yapo mengi na yamehifadhiwa kwenye maktaba zetu. Ni muhimu kufikia kila aina ya maoni katika kujaribu kuamua ukweli. Uislamu kimsingi uko dhidi ya kufuata kibubusa. Utafiti huu umefanywa ili kuwaelemisha Waislamu kwa ujumla juu ya madhehebu za Kiislamu ili kujenga maoni yao kuhusu mtazamo mzuri wa mtu mwenyewe, na ni muhimu mtu kuelewa hoja za wale ambao hakubaliani nao. Inawezekana kusemwa kwamba wale ambao hawaelewi kabisa mtazamo wa maoni tofauti, hawaelewi kwa ukamilifu (mtazamo) wa kwao wenyewe.

Tumekiona kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote, ambapo uwongo, ngano za kale na upotoshaji wa historia ni mambo ambayo hayana nafasi tena katika akili za watu.

Kutokana na ukweli huo, taasisi yetu ya Al-Itrah Foundation imeamua kukichapisha kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili kwa madhumuni yake yaleyale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili.

Tunamshukuru ndugu yetu, Sheikh Harun Pingili kwa kukubali jukumu hili la kukitarjumi kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwake.

Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam,
Tanzania.