read

Tatizo La Masunni Halitanzuki Kwa Hadithi Mbili:

Tukiyafumbia macho yote hayo na tusalimu amri kimjadala, ilimradi tu mjadala uchukue nafasi yake kuwa Hadithi mbili hizi: “Ni juu yenu Sunna yangu” na “Kitabu cha Mwenyezi Munguu na Sunna yangu” ni sahihi, bado hali hiyo haiwaokoi Masunni wala kuondoa taabu yao, bali kwa kila njia na mwelekeo yatilia nguvu na kuyaunga mkono madhehebu ya Ahlul- Bayt (Ushia), hiyo ni kwa sababu zifuatazo:

Hadithi ya kwanza:

Ni juu yenu kuishika Sunna yangu na Sunna ya makhalifa waongofu wenye kuongoza baada yangu.”

Makhalifa Ni Wao Maimam Wa Kiahlul-Bait:

Kwa kweli neno ‘Makhalifa’ hapa lina maana ya jenasi sio mahsusi kwa kikundi maalumu. Hivyo basi Sunni kulitafsiri kwa maana ya makhalifa wanne tu ni tafsiri isiyo na asili wala dalili, kwa kuwa kadhia ni kubwa zaidi kuliko madai.

Bali dalili za tamko zaonyesha kinyume na madai hayo, kwa sababu makhalifa au makhalifa waongofu ni maimamu kumi na wawili katoka Ahlul-Bayt. Hiyo ni kulingana na dalili zilizothibiti na riwaya thabiti kuwa makhalifa baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ni makhalifa kumi na wawili.

Al-Qunduziy al-Hanafiy katika kitabu Yanabii’ul-Mawaddah, amesema: “Yahya bin Hasan amesema katika kitabu Al-Umdah kupitia njia ishirini kuwa makhalifa baada ya Nabii (s.a.w.w.) ni makhalifa kumi na wawili, wote ni makuraishi.

Ndani ya Bukhari ni kwa njia tatu. Na katika Muslim ni kwa njia tisa. Na katika Abu Daudi ni kwa njia tatu. Na katika Tirmidhiy ni kwa njia moja na katika Al-Hamidiy ni kwa njia tatu.

“Hivyo katika Bukhari imetoka kwa Jabir ameisimulia akiwa ameacha nyororo ya wapokezi: ‘Baada yangu watakuwa maamiri kumi na wawili.’ Na akasema neno sikulisikia, hivyo nilimuuliza baba yangu: Je amesema nini? Alijibu: ‘Wote kutoka kwa makuraishi.’

“Na katika Sahih Muslim ni kutoka kwa Aamir bin Saad, amesema: Nilimwandikia Ibnu Samrah: Nipe habari ya kitu ulichosikia kutoka kwa Nabii (s.a.w.w), kwa hiyo aliniandikia: ‘Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) akisema siku ya Ijumaa jioni, siku ya kupigwa mijeledi

Al-Aslamiy:

‘Dini itaendelea imara mpaka kije Kiyama, na wawe juu yao makhalifa kumi na wawili, wote kutoka kwa wakuraishi.’ 1

Baada ya hivyo haiwezekani mtoa hoja atoe hoja kwa hadithi ya “Na Sunna ya makhalifa...” akiibebesha riwaya hiyo makhalifa wanne, hiyo ni kwa ajili ya kuwepo riwaya mutawatiri ambayo imefikia njia ishirini na zote hizo zikibainisha kuwa makhalifa ni kumi na wawili.

Wala hatuwezi kuipata tafsiri ya riwaya hizi kwa ukweli wake wa kivitendo isipokuwa kwa Maimamu wa madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) kumi na wawili.

Kwa hiyo Shia wanakuwa ndiyo kikundi pekee ambacho imepatikana maana ya kivitendo ya Hadithi hizi, kwa sababu ya kumtawaza kwao Imam Ali (a.s.) na baada yake Hasan na Husein, na baada ya Hasan na Husein Maimamu tisa kutoka dhuriya ya Imam Husein, idadi inakuwa baada ya hivyo ni Maimamu kumi na wawili.
Japokuwa neno ‘Kurayshi’ katika riwaya hizi ni jumuishi la wazi lisilo na mipaka, ambalo linaruhusu kuingia Makurayshi wengine ambao si katika Ahlul-Bayt, lakini kwa kuambatanisha na riwaya kadhaa na vielelezo vingine, yaani ishara zingine, inabainika kuwa makusudio ya hizo riwaya ni Ahlul-Bayt.

Hivyo ni kwa sababu ya kupatikana riwaya kadhaa zinazosaidiana zikithibitisha uimamu wa Ahlul-Bayt (a.s.). Tutazipitia baadhi yao katika utafiti ujao.

Na hapa mwaweza kutosheka na riwaya:

“Kwa hakika mimi ni mwenye kukuachieni katika ninyi ambalo endapo mtashikamana nalo hamtopotea baada yangu: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu watu wa nyumba yangu.”2

Madam kuimarika kwa dini ni kwa wilaya ya makhalifa kumi na wawili kama zilivyobainisha riwaya hizo zilizotangulia, na wakati huo huo kuna riwaya zinatilia mkazo wa kuambatana na Ahlul-Bayt na Kitabu, kwa hiyo ni dalili bora kuwa makusudio ya ‘Makhalifa kumi na wawili’ ni Maimamu wa Ki-Ahlul-Bayt.

Ama ibara isemayo: ‘Wote kutoka kwa wakuraishi’ si chochote ila ni kubadilisha na kughushi katika Hadithi, imewekwa ili dalili iliyo wazi iwajibishayo kuwafuata Ahlul-Bayt ipotoshwe, kwa kuwa ibara sahihi ni: “Wote ni kutoka kizazi cha Hashim.”

Lakini mkono mdanganyifu na wa khiyana ulizifuatilia fadhila za Ahlul-Bayt ukazificha miongoni mwazo kiasi cha uwezo wake, na ukabadilisha ulichoweza kukibadilisha.3

Na riwaya hii ni mojawapo ya riwaya zilizokuwa muhanga wa kugeuzwa na kubadilishwa. Lakini Mwenyezi Mungu anakataa mpaka aidhihirishe nuru yake. Al-Qunduziy Al-Hanafiy mwenyewe amenakili ndani ya kitabu Yanabiul-Mawaddah: “Na katika mawada ya kumi katika kitabu Mawadatulqurba cha Sayyid Ali al-Hamdaniy, Mwenyezi Mungu aitukuze siri yake na atububujishie baraka zake, amenukuu kutoka kwa Abdul Malik kutoka kwa Umayr kutoka kwa Jaabir bin Samrah kuwa amesema: ‘Mimi na baba yangu tulikuwa kwa Nabii (s.a.w.w) naye (s.a.w.w.) alikuwa anasema: ‘Baada yangu kutakuwa makhalifa kumi na wawili.’ Halafu alihafifisha sauti yake, na nilimuuliza baba yangu: Alisema nini alipohafi- fisha sauti yake? Akajibu: Wote kutoka kizazi cha Hashim.”4

Bali Al-Qunduziy ameeleza Hadithi zenye uwazi zaidi kuliko hiyo, ameeleza kutoka kwa Abayah bin Rab’iy kutoka kwa Jabir, amesema: “Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w): ‘Mimi ni bwana wa manabii na Ali ni bwana wa mawasii na hakika ya mawasii wa baada yangu ni kumi na wawili, wa kwanza wao ni Ali na wa mwisho wao ni al- Qaim al-Mahdiy.”5

Al-Qunduziy Al-Hanafiy hakupata njia nyingine baada ya kuitaja Hadithi hii, ila ni kukiri na akawa anasema: “Kwa kweli Hadithi zinazojulisha kuwa makhalifa baada yake (s.a.w.w) ni makhalifa kumi na wawili, zimekuwa mashuhuri kwa njia nyingi, kwa hiyo kwa ufafanuzi wa zama na utambulisho wa ulimwengu na mahali, imejulikana kuwa makusudio ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) katika Hadithi hii ya maimamu kumi na wawili, ni kutoka Ahlul-Bayt wake na kizazi chake. Kwa sababu hatuwezi kuibebesha Hadithi hii juu ya wafalme wa kizazi cha Umayyah, kwa sababu ya kuzidi idadi yao kumi na wawili na dhulma yao mbaya, isipokuwa Umar bin Abdul-Azizi.

“Na kwa sababu wao si kizazi cha Hashim, kwa kuwa Nabii (s.a.w.w) alisema: “Wote kutoka kizazi cha Hashim,” katika riwaya ya Abdul-Malik kutoka kwa Jabir. Na kitendo cha (s.a.w.w) kuihafifisha sauti yake katika kauli hii, kinaipa uzito riwaya hii, kwa kuwa wao hawaufanyii vyema ukhalifa wa kizazi cha Hashim. Na wala hatuwezi kuibebesha juu ya wafalme wa kizazi cha Abbas kwa sababu ya kuzidi kwao idadi iliyotajwa, na kwa kutochunga kwao Aya hii “Sema sikuombeni ujira ila upendo kwa karaba wangu.” Na pia Hadithi ya Kishamia.

“Kwa hiyo hapana budi ibebeshwe Hadithi hii juu ya Maimamu kumi na wawili kutoka Ahlul-Bayt wake na kizazi chake (s.a.w.w), kwa kuwa wao walikuwa wataalamu zaidi kuliko watu wote wa zama zao na watukufu mno na wanadini mno na wacha Mungu mno, na ni wenye nasaba ya juu mno na wabora wa jamii yao, na wenye heshima mno kwa Mwenyezi Mungu. Elimu yao ilikuwa kutoka kwa baba zao na yaungana na ya babu yao (s.a.w.w). Kwa hiyo kuibebesha Hadithi: “Ni juu yenu kuishika Sunna yangu na Sunna ya makhalifa waongofu wenye kuongoza baada yangu,” juu ya Maimamu kutoka Ahlul-Bayt ni karibu mno kuliko kuibebesha juu ya makhalifa wanne, kwa ubainifu uliopatikana kuwa makhalifa baada ya Mtume (s.a.w.w) ni kumi na wawili na ni kutoka kizazi cha Hashim.”

Ahlul-Baiyt Ndio Njia Ya Kushikamana Na Kitabu Na Sunna:

Ama kuhusu hadithi:

“Mimi nimekuachieni kati yenu kile ambacho endapo mtakishika hamtopotea baada yangu kamwe: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu.”

Hii haipingani na hadith “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu.” Wala hatukimbilii kwenye maamuzi ya kuwa zinapingana, isipokuwa kama kupingana kumeimarika na kuoanisha kati ya hadithi mbili kumeshindikana, lakini ikiwa yawezekana kuoanisha kati ya hadithi mbili basi hapo hakuna kupingana asilan.

Ibnu Hajar ametutosheleza juhudi ya kutafuta uwezekano wa kuoanisha kati ya mbili hizo, kwa kuwa amesema katika Swawaiq yake: “‘Mimi ni mwenye kuacha katika ninyi mambo mawili hamtopotea mkiyafuata. Navyo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlul-Bayt wangu, kizazi changu.’ Tabraniy amezidisha: ‘Kwa hakika mimi nimewaombea hilo kwa Mwenyezi Mungu, hivyo basi msiwatangule mtahiliki, wala msizembee mbali nao mtahiliki, wala msiwaelimishe kwa kuwa wao ni wajuzi mno kuliko ninyi.’

Na katika riwaya nyingine: ‘Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu.’ nayo ndiyo iliyokusudiwa katika hadithi zinazoishia na kitabu peke yake, kwa sababu Sunna hukifafanua, kwa hiyo kukitaja (Kitabu) kumetosheleza haja ya kuitaja (Sunna). Matokeo yake ni kuwa, mkazo umekuja katika kushikamana na Kitabu na Sunna na kushikamana na wanavyuoni wa Kitabu na Sunna miongoni mwa Ahlul-Bayt. Tija ipatikanayo kwa jumla ya hayo yote ni kubakia kwa mambo matatu mpaka Kiyama kitakaposimama….”6

Na kwa ibara ya kina zaidi kuliko aliyoisema Ibnu Hajar ni kuwa: Hakika amri ya kushikamana na Sunna haiwezi kutekelezeka ila kupitia wahifadhi wake, nao ni Ahlul-Bayt, na Ahlul-Bayt ni wajuzi mno wa yaliyo ndanimwe, kama ambavyo riwaya imelithibitisha hilo na historia imelitolea ushahidi.

Hivyo basi himizo kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) limekita kwenye kushikamana na Kitabu na Ahlul-Bayt, hivyo basi kushikamana na Sunna huwa ni jambo la kawaida linalazimiana na kushikamana na Ahlul-Bayt, wala si kama alivyosema Ibnu Hajar kuwa: “Himizo limekita juu ya kushikamana na Sunna.” Kwa kuwa riwaya zilizokuja za ulazima wa kushikamana na kizazi ambao ni Ahlul-Bayt zimefikia kiwango cha tawatur.

Ukiongeza juu ya hilo ni kuwa umekwishajua yaliyojiri kuihusu Sunna, ikiwemo kuunguzwa, kuificha na kuipotosha. Kwa hiyo Ahlul-Bayt ni njia pekee ya kuijua Qur’ani na Sunna, kama alivyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w): “Wala msiwatangulie mtahiliki, wala msizembee mbali nao mtahiliki, wala msiwaelimishe kwa kuwa wao ni wajuzi mno kuliko ninyi.” Kama alivyoiandika Hadithi hii Tabaraniy, hivyo inakuwa hakuna upenyo baada ya hayo, wa kuukwepa wajibu wa kushikamana na Ahlul- Bayt.

  • 1. Yanabiiul-Mawaddah cha al-Qunduziy al-Hanafiy Uk.104 - manshuratu Muasasatil Aalamiy lilmatbuati, Beirut – Lebanon .
  • 2. Kwa hakika Ali (a.s.) ni wa kwanza miongoni mwa maimamu kumi na wawili. Linalojadiliwa na kitabu hiki hapa ni nadharia mbili: Je hivi wao ni makhalifa wanne au makhalifa kumi na wawili? Hawa kumi na wawili ni akina nani na wanaungana na nani?
  • 3. Rejea mlango wa wasimulizi wazibadili hadithi
  • 4. Chanzo kilichopita, Uk.104.
  • 5. Chanzo kilichopita, Uk.105.
  • 6. Al- Swawaiqul-Muhrriqah. Uk. 150.