read

Ukweli Wa Kihistoria Na Hadithi: ‘Na Sunna Yangu’

Ama ukweli wa kihistoria pia unaikanusha Hadithi hii. Historia yasema kuwa Sunna takatifu haikuwa imeandikwa zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), bali kuna Hadithi kwa njia ya Ahlu Sunnah inaonyesha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) anakataza kuandika Hadithi, mfano wa kauli yake (s.a.w.w): “Msiandike kitu kutoka kwangu, na aliyeandika kutoka kwangu ambacho si Qur’ani basi naakifute.” Kama ilivyo katika Sunan Daarmiy1 na Musnad Ahmad.

Na katika riwaya nyingine ni kuwa wao waliomba idhini kwa Nabii (s.a.w.w) ili waandike, na hakuwapa idhini. Na zisizo hizo miongoni mwa riwaya zinazoonyesha kuzuia kuandika Hadithi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).

Yote hayo yalikuwa ndani ya mpango ambao ulitekelezwa ili kuzuia kuenea kwa Hadithi na ziwe zimefichwa ili haki isidhihiri.

Hawakusimama hapo, bali Umar alifanya juhudi ya wazi kuifutilia mbali Sunna. Urwa bin Zubayr ametoa riwaya kuwa Umar bin Khattabi alitaka kuziandika Sunna, aliwataka ushauri kwa hilo swahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), nao walimshauri aziandike, ikawa Umar anafanya istikhara kwa Mwenyezi Mungu kuhusu hilo mwezi mzima, kisha asubuhi moja aliamka akiwa amemwazimia Mwenyezi Mungu akasema:

“Kwa hakika mimi nilitaka kuandika Sunna, na kwa kweli mimi nilikumbuka kaumu walikuwa kabla yenu waliandika maandiko na wakajishughulisha nayo na waliacha kitabu cha Mwenyezi Mungu, na kwa kweli abadan mimi sikifuniki kitabu cha Mwenyezi Mungu na kitu.”2

Na kutoka kwa Yahya bin Jaadata kuwa Umar bin Al Khattab alitaka kuandika Sunna halafu ikamjia asiiandike. Halafu aliandika katazo na kupeleka mikoani: “Mwenye kuwa na kitu - miongoni mwa Hadithi - naakifutilie mbali.”3

Ibnu Jarir ameeleza kuwa Khalifa Umar bin al-Khattab alikuwa kila amtumapo hakimu au liwali kwenye mkoa au nchi humuusia, katika jumla ya anayomuusia ni: “Itenge mbali Qur’ani, na fanya riwaya kutoka kwa Muhammad ziwe chache na mimi ni mshirika wenu.”4

Historia imehifadhi kuwa Khalifa alimwambia Abu Dharr na Abdullah bin Mas’ud na Abu Darda’a kuwa: “Hadithi gani hizi mnazieneza kutoka kwa Muhammad?!”5

Kama ilivyoelezwa kuwa Umar bin al-Khattab alizikusanya Hadithi kutoka kwa watu, wao wakidhania kuwa anataka kuziangalia na kuzisawazisha ili jambo moja lisiwe na tofauti. Walimletea maandiko yao na yeye akayachoma moto, kisha akasema: “Tumaini kama tumaini la Ahlul’kitabi.”

Kama alivyoeleza al-Khatib kutoka kwa al-Qasim katika kitabu Taqyidul-Ilmi.

Ama sababu alizozisema Umar za kuhalalisha kuiondoa Sunna, ni sababu ambazo hata mjinga hazikubali sembuse mwanachuoni, kwa kuwa ni kinyume na Qur’ani, na roho ya dini na akili, basi vipi aseme:

“Itenge mbali Qur’ani, na fanya riwaya kutoka kwa Muhammad ziwe chache..” hali Qur’ani yenyewe yatilia mkazo kuwa hoja yake hutimia kwa Sunna, kwa kuwa Sunna ni muweka wazi na mfafanuzi, na Sunna ndio inayojulisha kuwa hukumu hii ya Qur’ani ni mahsusi na yenye kufungika na yasiyo kuwa hayo, na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema: “Na tumeuteremsha kwako utajo (Qur’ani) ili uwabainishie watu walichoteremshiwa ili wawe wanafikiri.”

Hivyo basi ni vipi Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ataibainisha Qur’ani kama si kwa Sunna?! Na amesema (s.w.t.):

مَا ضَلَّ صَاحِبُكُمْ وَمَا غَوَىٰ {2}

وَمَا يَنْطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ {3}

إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ {4}

“Kwamba mtu wenu hakupotea wala hakukosa. Wala hasemi kwa utashi binafsi. Hayakuwa haya ila ni Wahyi uliofunuliwa.” (Surat Najmi: 2 4).

Basi ni faida gani ya wahyi endapo tutaamrisha ufichwe na uunguzwe. Na hii Sunna muitoleayo hoja kuwa ni lazima kuifuata imepitiwa na mlolongo wa njama, mwendo huu umeanzia kutoka kwa Abu Bakr, yeye ameunguza Hadithi mia tano alizokuwa ameziandika kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) wakati wa zama za ukhalifa wake. Bibi Aisha amesema:

“Baba yangu alikusanya Hadithi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), zilikuwa Hadithi mia tano, alikesha anajigeuzageuza alipopambazukiwa na asubuhi akasema:

‘Ee binti yangu zilete Hadithi zilizo kwako.’ Nilimletea na aliziunguza na akasema: ‘Nimeogopa nisijekufa nazo zipo kwako, hivyo hadithi kutoka kwa mtu niliyemwamini na nimemshiba zitakuwa kinyume na alivyonihadithia, kwa hiyo nitakuwa nimelibeba hilo.”6

Na Umar aliandika barua akiwa katika enzi ya ukhalifa wake na alizituma sehemu za miji mbalimbali, katika barua hizo aliandika: “Aliyekuwa ameandika Hadithi na aifute.”7

Uthman naye alipita njia hiyo hiyo; kwa sababu alichukua ahadi kuwa atakwernda mwendo wa masheikh wawili – Abu Bakr na Umar – akasema akiwa juu ya mimbari:

“Si halali kwa yeyote aieleze Hadith ambayo haikusikika katika zama za Abu Bakr wala zama za Umar.”8

Baada ya Uthman aliendeleza mwendo huo Muawiyah bin Abi Sufian, akisema: “Ee ninyi watu punguzeni riwaya kutoka kwa Mtume, na ikiwa munahadithia hadithieni zilizokuwa zinahadithiwa zama za Umar.”9

Kwa mujibu huo kuacha kuandika Hadithi kunakuwa ni Sunna ya kufuatwa, na kuiandika kukahesabika kuwa ni kitu cha munkari.
Kudhalilishwa na kupotoshwa kama huku kwa njia ya habari kulikokuwa kunafanywa na mamlaka tawala juu ya kuandika hadithi, si kwa jingine ila ni kwa ajili ya kuzificha fadhila za Ahlul-Bayt na kuzuia zisienee.

Hii ndio sababu ambayo walio wengi hawaridhiki, lakini ndio ukweli mchungu ambao anagongana nao mfuatiliaji katika historia na aliyeyasoma matukio yake.

Baada ya hali hiyo ni Sunna gani ambayo Mtume (s.a.w.w) aliamrisha ifuatwe?! Je ni ile aliyoifutilia mbali Umar? Au aliyoiunguza Abu Bakr?!

Ikiwa kulikuwa na amri ya kuifuata Sunna basi ni kwa nini hawakuitii amri hii hawa makhalifa waongofu, kwa kukithirisha riwaya zake na kutilia hima ya kuziandika?!

Afanyeje atakaye kushikamana na Sunna baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w)?! Tufanye mfano mtu huyo aliishi na Swahaba, je awe anawatafuta maswahaba wote ili achukue Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kutoka kwao hali kati yao kuna maliwali, mahakimu, viongozi, na askari wakiwa kwenye msitari wa mbele?!

Je awatafute wote ili awaulize hali ya analotaka kulijua miongoni mwa hukumu, au atosheke na kurejea kwa wanaopatikana, na yeye haijuzishi hiyo – Sunnah - kwa tazamio la kutokea Naasikhu10 au Muqayyadu11 au Mukhaswasu12 kwa kule kuhudhuria mmoja au wawili miongoni mwa ambao hawapo Madina? Na hoja kama asemavyo Ibnu Haazim: ‘Haiwi ila kwa wao.’

Na ikiwa tatizo ni kama hili kwa aliyewakuta maswahaba, hali wao ni wachache, basi vipi itakuwa baada ya dola ya kiislamu kupanuka na kukithiri kwa nchi zilizopatikana kwa ushindi, na kukithiri kwa maswali kuhusu matukio na mabadiliko. Nini watajibiwa?

Na pia Hadithi nyingi na hukumu zimepotea, na hili ndilo lililolengwa na njama. Umar alilieleza hilo bayana wakati wa zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), pale aliposema karibu na kifo chake Mtume aliposema: “Nileteeni karatasi na kidau cha wino niwaandikieni maandishi ambayo kwamba hamtopotea kabisa baada yangu.” Umar akasema: “Kwa kweli yeye anaweweseka, kitabu cha Mwenyezi Mungu kinatutosha.”13

Hivyo basi lengo lililozuia karatasi na wino visiletwe kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ili awaandikie maandiko yatakayowazuia wasipotee ni lilelile liliwaziwia wasizikusanye Hadithi na kuziandika. Basi vipi ielezwe baada ya hayo kuwa “Shikamaneni na Sunna zangu?”

Maswahaba hawakushikamana nazo wala makhalifa, bali walitangaza kinyume na hivyo, kama alivyoeleza Dhahabi katika kitabu Tadhkiratul’hufaadh, amesema: “Kwa hakika Sidiq (Abu Bakr) aliwakusanya watu baada ya kutawafu Nabii wao, na akasema: ’Kwa kweli ninyi mnahadithia kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) Hadithi nyingi, mnatofautiana humo, na watu baada yenu watakuwa wenye kutofautiana sana, hivyo basi msihadithie kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kitu chochote, na atakayewauliza semeni: Kati yetu na ninyi kuna kitabu cha Mwenyezi Mungu, halalisheni halali yake na haramisheni haramu yake.”14
Ni kitu cha kawaida pasiwajibishwe chanzo chochote cha kisheria juu ya umma maadamu haijasajiliwa na kuwekewa mpaka wa ufahamu, au kuwa na mbeba jukumu la kuwa yeye ndiye rejea wa hiyo sheria.15

Umma umeafikiana kuwa Sunna haikuwa imesajiliwa zama za Mtume (s.a.w.w) wala zama za makhalifa na haikuwa imesajiliwa ila baada ya karne na nusu tokea kutawafu kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Hivyo ni kwa sababu zipi aseme msemaji: “Ni juu yenu kuishika Sunna yangu”.

Hadithi Nyingine:

Tamko lake:

“Nimeacha kati yenu mambo mawili ambayo hamtopotea endapo mtashikamana nayo: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Nabii wake.”

Hadithi hii ni dhaifu mno haina haja ya kuijadili, na lolote laweza kusemwa kuhusiana nayo, ukiachilia mbali yaliyotangulia ni kuwa:

a) Kwa hakika Hadithi hii hawakuieleza waandishi wa Sahih-Sita za Ahlu Sunna. Na hilo latosha kuifanya iwe dhaifu, basi vipi jamani wameshikamana na Hadithi isiyokuwa katika vitabu vyao Sahihi wala vitabu vyao vya rejea.

Na mwangalizi wa nafasi ya Hadithi kwa Ahlu Sunna haimuingii shaka kuwa je, Hadithi hii imeelezwa na vitabu Sahihi, na vilivyo msitari wa mbele ni Bukhari na Muslim, hali ukweli wa mambo ni kuwa haipo kabisa.

b) Kwa kweli vyanzo vya mwanzo kabisa ambavyo vimeitaja Hadithi hii ni Muwatau ya Imam Malik, na Siira ya Ibnu Hisham, na Sawa’iqu ya Ibnu Hajar. Sikukipata kitabu kingine kilichoeleza Hadithi hii kisichokuwa hivyo. Na vitabu hivi vimeshirikiana katika kunakili Hadithi mbili hizi isipokuwa Muwatau.

c) Riwaya ya Hadithi hii ni isiyo na nyororo ya wapokezi (mursalah) katika Sawa’iqu, na yenye Sanad iliyo pungufu katika Siira ya Ibnu Hisham.16 Na Ibin Hisham anadai kuwa yeye ameichukua Hadithi hii kutoka katika Siira ya Ibnu Is’haqa, na nilitafuta katika Siira ya Ibnu Is’haqa sikuikuta Hadithi hii katika chapa zote, basi ni wapi ameitoa Ibnu Hisham jamani?!

d) Ama riwaya ya Malik ya Hadithi hii, ni habari isiyo na nyororo ya wapokezi, haina Sanad. Mpokezi wa al-Muwatau amesema: “Amenisimulia kutoka kwa Malik kuwa zilimfikia habari kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema…”17

Kama uonavyo Hadithi hii haina sanad, haiwezi kutegemewa. Kwa nini Malik amekuwa wa pekee kuieleza Hadithi hii na wala ustadhi wake Abu Hanifa hakuieleza au mwanafunzi wake Shafiiy na Ahmad bin Hanbali? Lau Hadithi ingekuwa sahihi kwa nini maimamu wa madhehebu na maimamu wa Hadithi wameikwepa?!

e) Al-Haakim ameiandika Hadithi hii katika Mustadrak yake18 kwa njia mbili: Ya kwaza yumo Zaydu Ad-Daylisiy akinukuu kutoka kwa Ikrimah kutoka kwa Ibnu Abbas. Wala hatuwezi kuikubali Hadithi hii kwa kuwa katika sanad yake kuna huyu Ikrimah muongo,19 na yeye ni miongoni mwa maadui wa Ahlu-Bayt (a.s.) na ni miongoni mwa ambao walitoka dhidi ya Ali na walimkufurisha.

Ama njia nyingine yenyewe yumo Swaleh bin Musa al-Talhiy akinukuu kutoka kwa Abdul-Azizi bin Rafiiu kutoka kwa Ibnu Swaalih kutoka kwa Abu Hurayra. Na Hadithi hii pia haiwezi kukubaliwa, kwa kuwa Hadithi hii kwa mujibu wa riwaya ya Abu Said al-Khidriy, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) aliitamka akiwa amelala katika tandiko la ugonjwa aliotawafu nao, na muda huu Abu Hurayra alikuwa Bahrayni, alitumwa pamoja na Al-Alaa Al-Hadhramiy mwaka na nusu kabla hajatawafu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w). Hivyo ni wakati gani alimsikia Nabii akiwa mgonjwa mahututi juu ya tandiko?!

f) Sunanul-Kubra ya al-Bayhaqiy Juz. 1, Uk. 4, chapa ya Darul-Maarifah, Beirut – Lebanon. Imeinakili Hadithi ya Muslim: “Nimewaachieni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu watu wa nyumba yangu.” Kisha inazinakili Hadithi mbili za Mustadrak kwa tamko.

g) Kitabu Al-Faqiihul-Mutafaqihu cha Al-Khatiib Al-Baghdady Jalada la 1. Uk. 94 kilichosahihishwa na kutolewa maelezo na mstahiki Sheikh Ismail Al-Answariy, yeye ni mwanachama wa baraza la fat’wa –Darul- Kutubil-Ilmiyah – Beirut – Lebanon.

Amezinakili Hadithi mbili, ya kwaza ni Hadithi ya Al-Mustadrak, (kutoka kwa Abu Swalih kutoka kwa Abu Hurayra). Ama ni Hadithi mpya ambayo aliinakili. Alisema: Seifu bin Umar amenihadithia kutoka kwa Abu Is’haqah Al-Asadiy kutoka kwa As- Swabahi bin Muhammad kutoka kwa Abu Haazim, kutoka kwa Abu Said Al-Khudriy…..

Na sanad hii haiwezi kukubaliwa kulingana na ushahidi wa wanavyuoni wa Jarhu na Taadil kumhusu Seifu bin Umar, wameafikiana kuwa ni muongo na mzushi, itakujia hivi punde kauli ya wanachuoni kumhusu yeye.

h) Kitabu Al-Ilmaau ila Maarifati Usuulir-Riwayah Wataqdiisu Sumaai cha Kadhi Iyadh (479 – 544 A .H.) kilicho hakikiwa na Sayyid Ahmad Swaqiir, chapa ya kwanza, mchapishaji akiwa ni Darur-Rasun-Naaswira – Maktaba ya Al-Atiiqah – Tunis, Uk. 9. Amenukuu tamko la Hadith kutoka katika kitabu Al-Faqiihul-Mutafaqihu, ambayo sanad yake kuna Seifu bin Umar.

Mbali na tulivyovitaja hakuna kitabu kilichonakili Hadith: “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu.” Hivyo basi Hadith hii haijapatikana ila kwa njia tatu: Kutoka kwa Ibnu Abbas, Abu Said al-Khudriy na Abu Huraira. Na njia hizi pamoja na udhaifu wake hazikujitokeza ila katikati ya karne ya tano ya Hijria, yaani baada ya al-Haakim, na hakijakuja kitabu cha zamani kuliko hicho kikitaja njia hizi. Hilo ni la kwanza.

Pili, kwa kweli maswahaba hawa watatu: Abu Huraira, Ibnu Abbas, na Abu Said al-Khudriy, wameieleza Hadith ya “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu.” katika karne ya pili ya Hijriya kama alivyoeleza Muslim, je, ni ipi kati ya hizi mbili tuikubali?20

Kwa mujibu huo riwaya hii si zaidi ya kuwa ni riwaya miongoni mwa riwaya za mpokezi mmoja, zisizo na nyororo ya wapokezi au zisizo na sanadi.

Na miongoni mwa sababu zinazojulisha kuwa riwaya hii ni ya kuzua, ni kuwa Hadith mfano wa Hadith hii ni ya muhimu mkubwa nayo ni kanuni ambayo umma utatakiwa uende nayo baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.), kwani “Hamtopotea endapo mtashikamana na viwili hivi: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Nabii wake.”

Hivyo yapaswa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) awe ameirudia rudia mahali pengi, na maswahaba waichukue kuieleza na kuihifadhi kama ilivyo katika Hadithi “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu.”

Haiwezekani Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) awe ametufanyia Hadithi hii kuwa chimbuko la kisheria baada yake, kwa kuwa ni Hadith isiyojulikana, haina dalili, achia mbali ile dhana ya chimbuko lake.

 • 1. Ameipokea Ahmad, Muslim, Daramii, Tirmidhi na Nasaaiy, wameieleza Hadithi hii kutoka kwa Abi
  Said al-Khidriy.
 • 2. Ameipokea Al-Bayhaqiy ndani ya Al-Madkhali kutoka kwa Ur’wat, na pia kaipokea Hafidhul-Maghrib bin Abdul-Bari.
 • 3. Jaamiu-Bayanil-ilmi wa fadhlihi, Jalada 1, Uk. 64-65. Tabaqati Ibn Saad Uk.3.s
 • 4. Tarikhut-Tabari Jalada 3, Uk. 273.
 • 5. Kanzul Ummal, Jalada 1, Uk. 293.
 • 6. Tadhkiratul-Hufadh Jalada 1, Uk. 5.
 • 7. Musnad Ahmad Jalada, 3, Uk. 12 -14.
 • 8. Kanzul Ummal, Juz.10, Uk. 295, Hadith namba 2949.
 • 9. Kanzul Ummal, Juz.1, Uk. 291, Hadith namba 29413.
 • 10. Naasikhu: Iliyofuta hukumu fulani.
 • 11. Muqayyadu: Iliyofungika kwa kadhia fulani.
 • 12. Mukhaswasu: Iliyofanya hukumu mahsusi kwa kadhia fulani.
 • 13. Al-Bukhari, kitabul’ilmi, Jalada 1, Uk. 30.
 • 14. Adhuwaau Ala Sunnati Muhammadiyya, Muhammad Abu Rayyah, Uk. 53.
 • 15. Usulul’fiqhi, li Muhammad Taqiyyu al Hakii, Uk. 73.
 • 16. Siirat Ibnu Hisham chapa ya zamani Juz. 2, Uk. 603. Chapa ya pili Juz. 4, Uk.185 na chapa ya mwisho ni Juz. 2, Uk. 221.
 • 17. Al-Muwatau cha Imam Malik aliyefariki 179 A.H. Jalada 2, Uk. 46, amekisahihisha, na kukiweka namba, kuzitoa Hadithi zake na kuzitolea maelezo Muhammad Abdul Baaqiy.
 • 18. Mustadrak Jalada 1, Uk. 93, usimamizi wa Dr.Yusuf Abdur Rahman al- Mar’ashiy, chapa ya Darul’maarifa, Beiruth – Lebanon.
 • 19. Yatakujia hivi punde maneno ya wanazuoni wa jarhu na taadiil kuhusu Ikrimah.
 • 20. Hakika amenipa faida sana Samahatu Allamah Sayyid Ali Badriy katika matoleo yake ya Hadith “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu.”