read

Mlango Wa Sita

Shura Na Ukhalifa Wa Kiislaam

Kwanza: Utafiti Kuhudu Dalili Ya Aya Ya Shura

Waislamu wametofautiana kwa tofauti kubwa mno kuhusu jinsi ya kumwainisha Imam na Khalifa, hiyo ni tangu zamani na hadi hii leo.

Na tofauti hapo zamani ilijikita zaidi katika ukweli wa kiutendaji na utekelezaji wa nje kuliko upande wa nadharia na kifikra. Ama hii leo tofauti imezingirwa na wigo wa kifikra na dhana, hauvuki mzozo wa kupaza sauti na thibitisho za kinadharia.

Na mchango wetu ili kupata ufumbuzi wa mzozo huu tungependa kuija- jadili dalili ya Aya ya Shura katika Qur’ani ambayo Ahlu Sunnah wanaitegemea katika nadharia yao.

Halafu kuiendea Shura yenyewe katika ukweli wake kiutendaji baada ya kutawafu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na mapinduzi yaliyotokea baada yake.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema:

فَبِمَا رَحْمَةٍ مِنَ اللَّهِ لِنْتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنْتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانْفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ ۖ فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمْ وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ ۖ فَإِذَا عَزَمْتَ فَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُتَوَكِّلِينَ {159}

“Basi kwa ajili ya rehema ya Mwenyezi Mungu umekuwa laini kwao na lau ungekuwa mkali mshupavu wa moyo, wangekukimbia. Basi wasamehe na waombee msamaha na ushauriane nao katika mambo, na unapoazimia basi mtegemee Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wenye kumtegemea.” (Surat al-Imran:159).

Na amesema tena:

وَالْوَالِدَاتُ يُرْضِعْنَ أَوْلَادَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ ۖ لِمَنْ أَرَادَ أَنْ يُتِمَّ الرَّضَاعَةَ ۚ وَعَلَى الْمَوْلُودِ لَهُ رِزْقُهُنَّ وَكِسْوَتُهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۚ لَا تُكَلَّفُ نَفْسٌ إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَا تُضَارَّ وَالِدَةٌ بِوَلَدِهَا وَلَا مَوْلُودٌ لَهُ بِوَلَدِهِ ۚ وَعَلَى الْوَارِثِ مِثْلُ ذَٰلِكَ ۗ فَإِنْ أَرَادَا فِصَالًا عَنْ تَرَاضٍ مِنْهُمَا وَتَشَاوُرٍ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا ۗ وَإِنْ أَرَدْتُمْ أَنْ تَسْتَرْضِعُوا أَوْلَادَكُمْ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِذَا سَلَّمْتُمْ مَا آتَيْتُمْ بِالْمَعْرُوفِ ۗ وَاتَّقُوا اللَّهَ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ {233}

“Na watakapopendelea kumwachisha maziwa, kwa kuridiana na kushauriana, basi hakuna lawama juu yao. Na kama mkitaka kuwap- atia watoto wenu mama wa kuwanyonyeshea, basi hakuna lawama juu yenu kama mkitoa mliyoyaahidi kwa wema. Na mcheni Mwenyez Mungu na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.” (Surat Al-Baqarah: 233)

Na akasema:

وَالَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنْفِقُونَ {38}

“Na wale waliomwitikia Mola Wao na wakasimamisha Swala, na mwendo wao ni kushauriana wao kwa wao, na wanatoa katika yale tuliyowaruzuku. (Surat Shura: 38).

Ahlu Sunna wanategemea chanzo cha suala la ukhalifa kiwe kwa Shura, yaani mashauriano. Na maoni yao ni kwamba ukhalifa wa waislamu hauwezi kuwa ila kwa Shura, kwa mantiki hiyo wanauona ukhalifa wa Abu Bakr kuwa ni sahihi kwa sababu amechaguliwa kwa njia ya Shura, iliyofanyika katika ukumbi wa Saqifa wa Bani Saidah.

Na upande wa pili, yaani safu ya wafuasi wa Ahlul-Bayt, wao wanaona ni dharura uainishaji na usimikaji wa khalifa uwe wa kiungu, kwa kuwa hakuna dhamana ya kuchaguliwa anayefaa zaidi katika nadharia ya kwanza (Shura).

Hivyo ni kwa sababu suala la Shura huwa linaathiriwa na mielemeo ya watu, upendeleo wao na mwelekeo wao kifikra, kinafsi, na uambatano wao kiitikadi, kijamii, na kisiasa, kama ambavyo nadharia ya uchaguzi inahitajia kiwango fulani cha usafi na mahala pafaapo na kujikomboa kwa kuwa mbali na taathira za hisia na bila ya hisia.

Kwa ajili hiyo wanasema hapana budi Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) awe na usia ulio wazi kuhusu suala la Ukhalifa. Na umedai kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alimtaja khalifa wake, si hivyo tu bali aliwataja makhalifa wake watakaokuwa baada yake.

Kwa mujibu huo wamesema kuwa ukhalifa ni wa Ali bin Abu Talib (a.s.), na kuwa Shura ambayo Qur’ani imeiteremsha bila shaka imekuja katika baadhi ya maudhui ambazo zahusika na utekelezaji wa hukumu, na sio katika suala la kuainisha hakimu ambaye wadhifa wake ni cheo cha kiungu.

Na kwa kuwa tofauti imezingirwa kati ya pande hizi mbili; basi endapo mojawapo ikithibiti kuwa iko batili upande mwingine utathibiti kuwa sahihi, jambo ambalo natija yake itakuwa usahihi au ubatili wa ukhalifa wa khalifa, sawa awe Abu Bakr na walio kuwa nyuma yake miongoni mwa makhalifa au Ali (a.s.) na walio nyuma yake miongoni mwa mawasii.

Na kwa kweli tumekwishathibitisha kwa kiwango kisicho acha nafasi ya shaka katika milango iliyotangulia usahihi wa nadharia ya wasemao kuwa ukhalifa inabidi uthibiti kwa tamko rasmi, na kuwa ukhalifa wa kiislamu ni haki ya Ahlul-Bayt, bali ni haki iliyo mahsusi kwao tu haivuki na kuwaendea wengine, lakini kwa ajili ya kukamilisha faida na kubainisha ukweli zaidi na zaidi, imekuwa hapana budi kuijadili nadharia ya Shura, hali ikiwa ni nadharia tu na kufaa kwake katika kumchagua khalifa wa waislamu.

Na wana-Shura wamezitegemea sana Aya za Qur’ani ambazo tumezifanya taji la mwanzo wa utafiti, kwa hiyo zenyewe ndio mdhamini katika mlan- go huu. Endapo tutarejea kwenye Aya hizo inatuwia wazi kuwa Shura ya kiislamu inaweza kufanyiwa taswira katika aina mbili:

Iwe maudhui ya Shura ambayo yakusudiwa kufanyiwa ushauri ni sehemu tu ya jambo zima, yaani sehemu ya jambo katika nukta ndogo yenye ukomo, mfano wa maudhui ya kumwachisha ziwa mtoto anyonyaye kama inavyoashiria Aya: “Na watakapopendelea kumwachisha maziwa,” na aina hii ya Shura si mahali pa kuzozaniwa, kwa hiyo tunapafumbia macho kupajadili.

Au iwe maudhui ya Shura ikusudiwayo kufanyiwa ushauri ni suala lenye maana ya ujumuishi na la ujumla, lina umuhimu kwa waislamu wote, kama kutangaza vita dhidi ya adui au kumchagua khalifa wa waislamu…n.k.

Hapana shaka wala wasiwasi kuwa hapana budi kurejea kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) katika maudhui kama hii kwa kuwa haiingii akilini kwamba ifanyike Shura kama hii na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) asiwe na rai yeyote, bali ni miongoni mwa mabaya kwa kawaida na ni maasi kisheria Shura ikamilike bila ya kurejea kwake au kurejea kwa ambaye anachukua nafasi yake naye ni walii wa mamlaka:

وَلَوْ رَدُّوهُ إِلَى الرَّسُولِ وَإِلَىٰ أُولِي الْأَمْرِ مِنْهُمْ لَعَلِمَهُ الَّذِينَ يَسْتَنْبِطُونَهُ مِنْهُمْ ۗ {83}

“Na lau wangelipeleka kwa Mtume na Wenye mamlaka katika wao, bila shaka wangelilijua wale wanaochunguza miongoni mwao.” (Surat Nisai: 83)

Na aina hii ya Shura kulingana na Aya: “Na ushauriane nao katika mambo, na unapoazimia basi mtegemee Mwenyezi Mungu” ina nguzo tatu:

1. Dharura ya kuwepo washauri ili shauri litimie, na hili lajulishwa na tamko “Nao” katika “Na ushauriane nao”

2. Kuwepo kwa mada ya ushauriano na maudhui yake ili ushauriano huu uwepo.

3. Walii atakayeiongoza Shura, na mwishowe suala litaambatana na rai yake. Na hili lajulishwa na nomino “Una” ya nafsi ya pili katika “Unapoazimia basi mtegemee Mwenyezi Mungu,”

Wala hapana shaka kama maudhui itakuwa ni jambo la wote linalomgusa kila mwislamu kwa hakika yule mwenye haki ya kukata shauri ni walii mwenye mamlaka juu ya suala la waislamu. Wala haiwezekani kwa Shura ya kisheria kwa tamko la kiislamu itimiye kwa kuibomoa nguzo moja miongoni mwa nguzo zake tatu.

Kwani ni ima iwe Walii mwenye mamlaka yupo na washauri wapo, na maudhui ya Shura haipo, hapo shauri halitokuwepo aslan, kwa kuwa hakuna jambo la kujadiliwa na kufanyiwa mashauri.

Au iwe Walii mwenye mamlaka yupo na maudhui ipo lakini jamaa wa kushauriana nao hawapo, na katika hali hii anuani inabadilika kutoka Shura na kuwa tamko rasmi au iwe amri.

Au iwe jamaa wa kushauriana nao wapo na maudhui ya Shauri ipo na Walii mwenye mamlaka hayupo, katika hali hii Shura haiwi kwa tamko lake la kisheria ambalo Mwenyezi Mungu amelipitisha katika kitabu chake, pindi alipofaradhisha Shura iwe kwenye jambo linalorejea kwake, kwani anapotoa kila mmoja miongoni mwao rai yake basi wapi yatakuwa marejeo ya rai?!

Wala haiwezekani kwa Shura kama hii isiyo ya kisheria itowe maamuzi ya kisheria ambayo waislamu wawe wanalazimika nayo, kwa kuwa hiyo wazi kabisa ni kinyume na Aya ambayo imetilia mkazo kuwa suala mwishowe lahusika na Walii mwenye mamlaka: “Unapoazimia basi mtegemee Mwenyezi Mungu,”

Na yawezekana ikapatikana ishkali ikasemwa:

Kwa kweli Aya hii: “Na ushauriane nao katika mambo, na unapoazimia basi mtegemee Mwenyezi Mungu” ni mahsusi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kwa hiyo si lazima kuwepo kwa Walii mwenye mamlaka katika Shura, wala hakuna kizuizi kufanyika Shura bila ya kuwepo humo Walii mwenye mamlaka, kwa dalili ya Aya: “Na mwendo wao ni kushauriana wao kwa wao,” kwa kuwa maana ya dhahiri ya Aya hakuna ndani yake walii wa amri anayeazimia na anatawakali, kama ilivyo katika Aya ya mwanzo.

Huondolewa Ishkali Hii Kwa Yafuatayo:

1. Kila ambalo limethibiti kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) katika haki ya utii lathibiti kwa Walii mwenye mamlaka, kwa dalili ya kauli yake (s.w.t.): “Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye madaraka miongoni mwenu.”

Kwa hilo inabainika kuwa utii wa dhati wa Walii mwenye mamlaka ni uleule utii wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), kwa kuwepo kwa herufi ya kiungo moja kwa moja.

Kama alivyotumia tamko moja kwa ajili ya wote wawili: “Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye madaraka miongoni mwenu.”

Lau angetumia tamko ‘Mtiini’ mara ya tatu kwa ajili ya Walii mwenye mamlaka kauli ya kuwa kuna hitilafu katika utii wa hawa wawili ingekuwa sahihi.

2 Kwa kweli namna ya Shura ambayo Mwenyezi Mungu ameipitisha kati- ka mambo yenye ujumla, ambayo yanawahusu waislamu kwa sura ya jumla, ni namna moja: “Na ushauriane nao katika mambo, na unapoazimia basi mtegemee Mwenyezi Mungu.” Hivyo basi kuileta namna nyingine dalili ya kisheria yahitajika, kwa sababu ya kuambatana kwake na mambo ya kisheria kama vile, wajibu wa kuyatii yatolewayo na hii Shura. Na kuitumia Aya “Na mwendo wao ni kushauriana wao kwa wao,” kama dalili juu ya aina ya pili ya Shura, utumiaji huo si timamu.

Jibu litarudi dhidi yake kuwa Aya hii bila ya ishkali wala tofauti ilimteremkia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), kwa maana ya kuwa ilishuka na yeye akiwa hai kati ya waislamu, hali ikiwa akili na sheria zinawazuia waislamu wasishauriane kulihusu jambo la wote linalowahusu waislamu bila ya kuwepo Mtume (s.a.w.w) kati yao na bila ya wao kurejea kwake, na hili ni baya na liko mbali sana. Jambo ambalo hujulisha kuwa hapana budi awe pamoja nao, na nomino “Wao” katika “Na mwendo wao” inamuingiza ndani yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).

Na zaidi ya hapo ni kuwa muundo wa Aya unaelezea sifa za waumini waliofuzu:

فَمَا أُوتِيتُمْ مِنْ شَيْءٍ فَمَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَمَا عِنْدَ اللَّهِ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ لِلَّذِينَ آمَنُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ {36}

وَالَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ وَإِذَا مَا غَضِبُوا هُمْ يَغْفِرُونَ {37}

وَالَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنْفِقُونَ {38}

“Basi vyote hivi mlivyopewa ni starehe ya maisha ya dunia tu, lakini kilicho kwa Mwenyezi Mungu ni bora na cha kudumu zaidi kwa wale walioamini na wanamtegemea Mola Wao. Na wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na mambo mabaya na wanapokasirika husamehe. Na wale waliomwitikia Mola Wao na wakasimamisha swala na mwendo wao ni kushauriana wao kwa wao, na wanatoa katika yale tuliyowaruzuku. (Surat Ashura: 36-38),

Na ni jambo lisilo na shaka kuwa kielelezo bora cha waumini ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), hapana shaka kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ni mmoja wa hao wana-Shura, na ikiwa imethibiti kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ni katika jumla ya hii Shura itajulikana kuwa suala la Shura katika Aya larejea kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na haitimii ila kwa azma yake: “Na unapoazimia basi mtegemee Mwenyezi Mungu.” Kwa mujibu huo kwa kweli hii Shura ni ile aina ya kwanza, na kwa yote hayo ni kuwa Aya: “Na mwendo wao ni kushauriana wao kwa wao,” ni Aya yenye maana kwa sura ya jumla na ya jenasi, na kwamba Aya: “Na ushauriane nao katika mambo, na unapoazimia basi mtegemee Mwenyezi Mungu” yenyewe ni mfafanuzi na mpambanuzi wake.

Baada ya kuwa nimebainisha haya haraka naongeza juu yake kuwa sisi tunaifikia natija iliyozingirwa na wigo wa lau tungejilazimisha na wazo la kuwa Aya ya “Na ushauriane nao katika mambo,” kuwa ni mahsusi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) bila ya kumjumuisha Walii mwenye mamlaka, kwa sababu wakati huo Shura haitokuwa kamili ila kwa kuwepo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), na hivyo akifa hapatakuwa na Shura kwa sababu ya kukosekana kwa nguzo ya msingi katika hiyo Shura, na nguzo hiyo ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).

Na endapo hatutajilazimisha na wazo la Aya kukomea kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) pekee, tutaizingatia kuwa Aya inavuka na kuwaingiza Mawalii wenye mamlaka, kwa hiyo Shura itakuwa ipo na ni jambo la kisheria, kwa sharti ya kuwepo Walii mwenye mamlaka ndani yake, na yeye ana haki ileile aliyostahiki Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) katika Shura kwa kuwa Walii mwenye mamlaka anachukua nafasi yake.

Hivyo basi maana ya “Na mwendo wao ni kushauriana wao kwa wao,” yaani hawafanyi jambo bila kumshauri Mtume na Walii mwenye mamlaka katika walihitajialo miongoni mwa mambo ya dini yao, kama Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alivyosema: “Na lau wangelipeleka kwa Mtume na Wenye mamlaka katika wao.”

Na kwa rai hizi mbili zote nadharia ya Shura ya kumsimika khalifa inakuwa katika mkwamo na ni jambo lisilowezekana, yalazimu liwe batili.

Na kulingana na rai ya kwanza: Nayo ni kuwa Aya “Na ushauriane nao katika mambo,” ni mahsusi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), ni kuwa inajulikana fika kuwa Shura ambayo ilifanyika kumtawaza khalifa wa kwanza ilikuwa baada ya kutawafu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), hivyo basi inakuwa Shura hiyo si ya kisheria kwa hukumu ya kiislamu, na kwa nadharia ya rai ya Qur’ani. Na kila tija itakayotokea kutokana nayo si ya kisheria.

Na miongoni mwa tija iliyotokea ni kumsimika khalifa wa kwanza, kama ambavyo vitabu vya historia na riwaya vinaonyesha jinsi gani alivyosimikwa pale panapoitwa Saqifa Bani Saidah, na Dhahabi ameieleza katika kitabu chake cha historia. Kama tukio hili lilivyokuja kulingana na riwaya ya Umar bin al-Khattab katika kitabu Sahih Bukhariy kwenye kitabul- hudud, mlango wa Rajmul-Hubla Minazzina.

Kama pia alivyoeleza Tabariy katika kitabu chake cha historia, alipoelezea matukio ya mwaka 11 A.H. Jalada la pili. Na Ibnu Al-Athir na Ibnu Qutaybah katika Tarikhul- Khulafaa, Jalada la 1, na vitabu vingine miongoni mwa rejea mbalimbali za kihistoria.

Na kwa mujibu wa rai ya pili, yaani kuwa Aya “Na ushauriane nao katika mambo,” yaonyesha kuwa Shura hutimia kwa kuwepo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) au kwa kuwepo anayeshika nafasi yake, naye ni Walii mwenye mamlaka.
Kwa hakika Shura ya kisheria haitimii ila kwa kuwepo Walii mwenye mamlaka, na Walii mwenye mamlaka hawezi kutawazwa ila kwa Shura ya kisheria. Na hii ni mzunguko,1 na mzunguko ni batili kwa mujibu wa nadharia ya wanamantiki. Kwa kuwa haiwezekani kufanyika kwa Shura kisheria ila baada ya kuwepo Walii mwenye mamlaka, na haiwezekani awepo Walii mwenye mamlaka ila baada ya kufanyika Shura ya kisheria. Kwa hiyo jambo hili linasimama lenyewe binafsi, hivyo haitowezekana kufanyika Shura ya kisheria milele na milele.

Ila kama itasemwa kuwa kuna Walii mwenye mamlaka aliyeainishwa na Mtume (s.a.w.w) ambaye kuwepo kwake kumeitangulia Shura, na huku ni kusalimu amri mbele ya nadharia ya kuwepo kwa tamko rasmi kunakodaiwa na kambi ya Ahlulu-Bayt.

Na inawezekana ikasemwa kuwa si lazima kuwepo na Walii mwenye mamlaka katika Shura bali yatosha kuwepo kwa mwenye shauri yaani mfanyaji shauri na si sharti awe walii. Na endapo shaka ikijitokeza kuwa nomino katika: “Na unapoazimia” inajulisha haki ya mshauri kukata shauri, jambo linalojulisha kuwa ni walii katika suala la Shura! Yawezekana kuipa jibu shaka hii kuwa, ukiazimia kwa maana ya azma ile iliyofikiwa na ushauri katika kupitisha jambo lake.

Kuna walakini katika jibu hilo: Kwa kuwa dhahiri siyo hiyo, kwani lionekalo dhahiri mno katika Aya ni kuwepo kwa haki ya kukata shauri upande wake, na kwa maana nyingine ni kuwa kwa kweli maneno yanatengenea endapo itakuwa rai ya wanaoshauriana ni moja, lakini zikitofautiana rai za wanaoshauriana basi vipi litakatwa suala la Shura? Na endapo mwenye shaka atasema litakatwa kulingana na rai ya wengi, basi dalili iko wapi? Si hivyo tu ikumbukwe kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amelaumu wingi katika Aya nyingi

وَإِنْ تُطِعْ أَكْثَرَ مَنْ فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ {116}

Wengi walio ardhini watakupoteza. (Surat al-An’aam: 116)

Bali ni kuwa kauli yake hii iko kinyume na maana halisi ya Aya ambayo inawakilisha suala la azma kwa mshauri pindi rai zinaposigana. Tukikubali hilo atakuwa ametoka nje ya sifa ya mshauri na kwenda kwenye sifa za walii wa Shura hii. Na hata kama rai za wanaoshauriana ziafikiane kwenye rai moja yeye bado ana haki ya kuazimia na kutoazimia. Ndio lililopo ni kuwa hawezi kuazimia jambo lililo kinyume na rai ya walioshauriana, hata hivyo hili halimpokonyi sifa ya uwalii. Na hivyo kulingana na yaliyotangulia inakuwa wazi kuwa nadharia ya Shura huwa kati ya mawili yaliyo hadharishwa.

a) Iwe Shura imefanyika bila ya kuwepo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na Walii mwenye mamlaka, Shura hii ni batili si ya kisharia, na kauli isemayo kuwa yawezekana kufanya Shura bila ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na bila ya Walii mwenye mamlaka yahita- jia dalili ya kisheria, na dalili haipo.

b) Au iwe Shura imefanyika kwa kuwepo Walii mwenye mamlaka ambaye kwake wanarejea, na Shura kama hii ina taswira kadhaa:

1 Ima huyu Walii mwenye mamlaka awe amejitawaza mwenyewe kutawalia suala la waislamu, mwenendo kama huu hauhalalishwi na chochote kisheria, ni tendo lisilo la kisheria kwa ajili ya haki za waisla- mu, basi utii kwake utakuwaje wajibu kisheria juu ya kundi la waislamu akiazimia jambo baada ya shura?

2 Au kiwe kikundi kidogo cha waislamu kimemtawaza juu ya jambo la waislamu, hivyo tunaangukia katika hadhari zilezile mbili tulizozionge- lea. Kwa kuwa wamemtawaza vipi?
Hivyo mushkili wa ziada utaingia katika sura hii, yaani ni uhalali gani kisharia kuwatii hawa na dalili iko wapi?

3 Iwe Mwenyezi Mungu na Mtume wake wametoa agizo la kumsimika awe Walii mwenye mamlaka, basi hapo hapatokuwa na haja ya Shura, kwa kuwa haiwezekani kumkhalifu Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na rai hii dhati yake ni nadharia ya kuwepo kwa tamko rasmi, kwa hiyo Shura imetoweka, na kutokana na athari yake umetoweka na kubatilika ukhalifa wa wa kwanza (Abu Bakr).

Kwa minajili hiyo inakuwa wazi kubatilika kwa nadharia ya Shura katika kuainisha ukhalifa kwa njia zote, hivyo yapasa kuiondoa maudhui ya Shura mbali na Aya za Qur’ani na kuipa maana nyingine isiyokuwa kumwainisha Walii mwenye mamlaka ya waislamu, na itabaki maana ya Shura kwenye ushauri katika mbinu za hukumu na vita… Kama ulivyo muktadha wa Aya: “Na ushauriane nao katika mambo….” Na haujabakia mlango kwa ajili yao, ila ikiwa watadai kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na Mtume wake (s.a.w.w) wamebainisha ukhalifa wa wakwanza kwa tamko rasmi. Hili hakupata kulidai Abu Bakr mwenyewe, lau lingekuwa sahihi angelitolea hoja dhidi ya maanswari katika ukumbi wa Saqifa ya Bani Saidah.

Na miongoni mwa yanayowekwa wazi pia kutoka katika Aya ya Shura ni kuwa Mwenyezi Mungu hakupata kuwaamini katika mbinu za kivita ambazo ushauri hauwezi kuwa nje ya wigo wake, kama ambavyo yajulikana kutokana na muktadha wa Aya na kama riwaya zilivyobainisha, riwaya ambazo zinabainisha ushauri wa Mtume kwa swahaba zake vitani, kiasi kwamba suala la Shura limeambatanishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), sasa vipi ataweza kuwaamini juu ya jambo kubwa kuliko hilo nalo ni kuteua Khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).

Ikiwa hautomwamini mtu kushughulika na dinari mia moja mpaka umfanyie wasii na mwongozi, itakuwaje umwamini dinari elfu moja. Hili ni baya kumhusu binadamu mjuzi, nalo ni baya mno kumhusu Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume wake (s.a.w.w).

Halafu itaingiaje akilini Mwenyezi Mungu awakilishe jambo hili kwa umma ili umchague khalifa wake hali Mwenyezi Mungu na Mtume wake wameonya kuwa kutatokea mapinduzi mara tu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) atakapofariki. ‘’Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume aliyepitiwa na Mitume kabla yake. Basi je akifa au akiuliwa mtarudi nyuma kwa visigino vyenu........ (Surat al-Imran: 144).

Na endapo utachunguza Aya hizi itakuwia wazi kuwa wasemeshwao ni waislamu, kwa kuwa kugeuka kwa kafiri hakuna maana, na wala haiwezi kuchukuliwa kuwa yamaanisha kugeuka kwa Musailamatul-Kadhab kwa sababu kugeuka kwake kulitokea wakati Mtume (s.a.w.w) bado akiwa hai. Na akili itakubali vipi Mwenyezi Mungu na Mtume wake walitelekeze jambo hili bure kati ya waislamu hali wakiwa wanajuwa fitna itatokea kati yao bila ya kumwainisha mwangalizi na walii mwenye mamlaka ambaye kwake watarejea.

Na historia ni shahidi tosha juu ya hilo, kwa kuwa kukosekana kwa walii mwenye mamlaka ilikuwa ndio sababu ya fitna zilizotokea kati ya waislamu, upotovu ulienea kiasi kwamba waislamu walitawaliwa na watu mafasiki na mafasidi miongoni mwao, na wasiokuwa na haya wala tabia njema wala dini. Ili uzidi yakini rejesha mishale ya saa yako kupitia historia ya karne ya kumi na nne, na isimame kidogo zama za Bani Umayya na Bani Abbas ambao walijipandisha mamlaka juu na kukandamiza shingo za watu katika zama. Na ili uwatambue maamiri wao na mahakimu wao na jinsi walivyokuwa wanajionyesha waziwazi kwa kunywa pombe, na jinsi walivyokuwa wakicheza na mbwa na kima baada ya kuwa wamewavika nguo za hariri na dhahabu safi, na mengine miongoni mwa mambo ya fedheha za watawala, mambo ambayo kalamu inastahi kuyaandika.

Na hii yajulisha ubaya wa uchaguzi, na utasa wa nadharia hii kimsingi. Kwa sababu tunayemchagua leo huenda tutamlaumu kesho kisha hatuwezi kumuuzulu baada ya kumtawalisha. Waislamu walifanya kila juhudi kumuuzulu Uthman alibisha na alikuwa akisema: ‘’Siivui kanzu ambayo Mwenyezi Mungu amenivisha.’’
Na baada ya kuwa tumethibitisha kuwa dalili mbili hizi ambazo zimetumiwa na kundi la kwanza ziko mbali mno, kundi ambalo limeitegemea Shura kuwa ndio chanzo kisiasa cha kumchagua khalifa ili aongoze mambo ya waislamu baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na imetubainikia umbali wake na hadhi ya uongozi na ukhalifa, sasa turejee na tuyafumbie macho haya, na tufinye macho yetu na tufanye hatuyajui kiasi cha kuufikia mghafiliko, na tukubali kuwa hizi dalili mbili ni hoja katika maudhui ya ukhalifa na uongozi, je kujifanya hatujui na tumeghafilika na kusalimu amri kuna tibu uelewa wa nadharia hii ambayo inakabiliwa na utata wa kisheria katika kila kinachoambatana na muundo na utekelezaji wa madhumuni yake?

Kwa kweli dalili hizi mbili hazinyooshi kupindama wala kuziba pengo la mahitaji ya nadharia hii ya kina yenye ncha nyingi, kwa kuwa inahitaji kuwekewa mipaka na kufafanuliwa maana zake, kama ambavyo Nassu mbili hizi zilizoashiriwa zinakosa uzito wa Shura na vipimo vyake na jinsi ya kuvidhibiti, zaidi ya hapo ni kuwa yahitaji katika utekelezaji wake zana na njia za kutekelezea.

Na sisi hatukuti katika Hadith na riwaya zilizopokewa wala katika sera ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kuwa alileta dhana hii na kuulazimisha umma kuitekeleza. Lau ingekuwa amefanya hivyo tungemkuta Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ameyawekea mpaka maalumati yake yiliyo wazi au iwe amepata kufanya maandalizi ya kifikra na ya kiroho na kisiasa ili kuitumia dhana hii. Kwa uchache angekuwa ameandaa sampuli mbalimbali zenye kuwezesha kutawalia ukubwa wa majaribio na uongozi wake na kusimamia kufanya sharia na kuitekeleza, kama tulivokwisha tanguliza kuwa dalili hazizibi uwazi huu. Basi mwaenda wapi na mnaamuaje!

Pili: Shura Katika Matukio Ya Kivitendo Shura Na Saqifa Ya Bani Saidah:

Wanahistoria wamesema kuwa ukhalifa wa Abu Bakr ulikuwa kwa njia ya kumpendekeza katika ukumbi wa Saqifa ya Bani Saidah. Nayo kwa ukweli ndiyo sheria kimsingi ambayo Abu Bakr anajiimarisha nayo katika ukhalifa wake kwa waislamu. Kwa hiyo haiwezekani mwislamu alazimike na ukhalifa wake ila akijilazimisha na kuiamini Saqifa na kuizingatia kuwa ndio namna pekee ambayo kwayo huainishwa khalifa wa waislamu. Na kwa kuwa sisi katika utafiti wa hapo kabla tulithibitisha kubatilika kwa nadharia ya Shura kuwa ndio njia ya kumtawaza khalifa wa waislamu, tungependa hapa tulidhihirishe tukio la Saqifa, ambalo ni utekelezaji wa kimatendo wa nadharia ya Shura, ili tufichue umbali wa usafi wake, na kisha kutokana na utaratibu huo kupatikane kujiambatanisha nayo au kutojiambatanisha nayo.

Saqifa Katika Kitabu Tarikhut-Tabariy:

Tabariy amelitaja tukio hili kwa ufafanuzi katika Tarikh yake Jalada 2 iliyochapishwa na al-Istiqlal, Cairo mwaka 1358 A.H. sawa na mwaka 1939 A.D. Hapa tunanakili kutokana nayo muhtasari tu kwa kadiri ya haja, kutoka Uk. 455 – 460, kama ifuatavyo:

“Answari walikusanyika katika Saqifa ya Bani Saidah, waliacha jeneza la Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) wakiliandaa ahali zake kwa kumuosha. Ndani ya Saqifa - wakasema: Tumtawaze jambo hili baada ya Muhammad, Saad bin Ubadah. Walimleta nje Saad waliko wao akiwa mgonjwa. Naye – Saad - alimhimidi Mwenyezi Mungu na akamsifu, na alitaja kutangulia kwa Answar katika dini na fadhila zao katika Uislamu. Na kumwongezea kwao nguvu Nabii na swahaba wake, na vita vyao dhidi ya maadui zake, mpaka waarabu wakaimarika na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alitawafu akiwa radhi nao.

“Na akasema: ‘Lihodhini jambo hili mbali na watu wengine.’ Wote walimjibu kuwa umefanya rai muwafaka na umesema kauli sahihi, hatukiuki rai yako, tutakutawalisha jambo hili. Halafu walijibishana maneno wao kwa wao, wakasema: ‘Endapo muhajirina wa kikurayshi wakikataa wakisema: Sisi ni Muhajirina na Swahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) wa mwanzo, na sisi ni watu wa ukoo wake na wapenzi wake, basi imekuwaje mnatunyang’anya jambo hili baada yake?’ Kundi miongoni mwao likasema: ‘Basi sisi tutasema: Kwetu kuwe na Amiri na kwenu Amiri.’ Saad bin Ubadah akasema: ‘Huu ni unyonge wa kwanza.’

“Abu Bakr na Umar waliposikia suala la Answar, waliharakia kwenda huko Saqifa wakiwa na Abu Ubaidah bin al-Jarah na Usidu bin Hudhwairu na Uwaymu bin Saidah na Aswim bin Adiy atokanaye na kizazi cha Ajlani. Abu Bakr aliongea baada ya kumzuia Umar asiongee. Alimhimidi Mwenyezi Mungu na alimsifu halafu alitaja kutangulia kwa muhajiriina katika kumsadiki Mtume kabla ya waarabu wote, na akasema:

‘Wao ni wa kwanza waliomwabudu Mwenyezi Mungu ardhini na walimwamini Mtume, kwa hiyo wao ni wapenzi wake na jamaa zake na ni watu wenye haki zaidi wa jambo hili baada yake, wala yeyote hagombanii dhidi yao katika hilo ila ni dhalimu.’ Halafu alizitaja fadhila za Answar, na akasema: ‘Baada ya muhajirina wa mwanzo hana yoyote daraja mliyonayo kwetu, kwa hiyo sisi ndio maamiri na ninyi ni mawaziri. ‘

“Hapo Hubab bin al-Mundhir alisimama na akasema: ‘Enyi Answar shikilieni jambo lenu kwa kuwa watu wako kwenye kivuli chenu wala hatothubutu mwenye kuthubutu awe kinyume na ninyi, wala msitofautiane isijewaharibikia rai yenu na kupungukiwa jambo lenu. Na endapo hawa watakataa isipokuwa mliyoyasikia basi kwetu Amiri na kwao Amiri.’

“Umar akasema: ‘Hilo liko Mbali sana! Wawili hawawezi kuwa katika ala moja, wallahi waarabu hawatoridhia wawafanyeni muwe maamiri hali Nabii wao anatoka kwa asiyekuwa ninyi, lakini waarabu hawakatai kumtawalisha jambo lao ambaye unabii upo katika wao, na walii wa mambo yao kutokana na wao, na sisi tuna hoja na nguvu ya wazi kwa mwenye kuamini. Nani agombanie na sisi mamlaka ya Muhammad na uamiri wake, hali sisi ni wapenzi wake na jamaa zake!? Ila yule mfanya batili au mtenda dhambi au mwenye kujiingiza katika maangamizi.’

“Hapo al-Hubab bin al-Mundhir alisimama na akasema: ‘Enyi Maanswar shikilieni mikononi mwenu wala msisikilize usemi wa huyu na wenzake, vinginevyo watachukua hisa yenu ya jambo hili, na wakikataa mliyowaomba watoweni nje ya nchi hii na tawalieni juu yao mambo haya, kwa kuwa ninyi wallahi ni wenye haki zaidi ya jambo hili kuliko wao, kwa sababu kwa panga zenu ameifuata dini hii ambaye hakuwa anaifuata. Mimi ndio kigogo cha kurejewa na shina la kuogopwa. Au wallahi mkipenda tutalirejesha upya kama lilivyokuwa!’

“Umar akasema: ‘Hivyo basi Mwenyezi Mungu atakuua.’ Alisema: ‘Bali wewe atakuua.’ Abu Ubeidah akasema: ‘Enyi maanswar, kwa hakika ninyi mlikuwa wa awali kunusuru na kusaidia, kwa hiyo msiwe wa awali kubadilisha na kugeuza.’ Bashiru bin Saad al-Khazrajiy Abu Nuumani bin Bashir alisimama akasema: ‘Enyi Answar kwa hakika sisi wallahi japo tuwe wenye ubora katika jihadi dhidi ya washirikina, na wa mwanzo katika dini hii, hatukufanya hivyo ila kutaka ridhaa ya Mola wetu na kumtii Nabii wetu na kujitaabisha nafsi zetu, basi haitakikani tujitakie ushindi juu ya watu kwa hayo, wala kujitakia fahari ya dunia, kwa hakika Mwenyezi Mungu ni walii wa neema na ni Mbora. Wallahi, Mwenyezi Mungu asinione nikishindana nao kwa jambo hili kabisa, hivyo basi mcheni Mwenyezi Mungu wala msiwapinge wala kushindana nao.’

“Abu Bakr akasema: ‘Huyu hapa Umar, na huyu hapa Abu Ubeidah, mumtakaye kati ya hao wawili mfanyieni baia.’ Wakasema: ‘Wallahi hatuwezi kulitawaza jambo hili juu yako….....’

“Abdur Rahman bin Aufi alisimama kuongea na akasema: ‘Enyi Answar kwa kweli ninyi japokuwa muwe na ubora, kati yenu hayupo mtu mfano wa Abu Bakr, Umar na Ali.’ Mundhiru bin Arqam alisimama na akasema: ‘Hatuukatai ubora wa uliowasema, kwa kweli kati yao kuna mtu lau angedai jambo hili yoyote hangemshinda.’2

“Answar, au baadhi ya Answar wakasema: ‘Hatutamfanyia baia yeyote isipokuwa Ali.’

“Umar akasema: ‘Hivyo kelele zilizidi na sauti zilipanda kwa hiyo nilihofia kutofautiana nikasema: Nyosha mkono wako nikufanyiye baia.”
“Na walipokuwa wakienda ili wamfanyie baia, Bashiru bin Saad aliwatangulia na alimfanyia baia. Hubab bin Mundhir alinadi kumuita: ‘Ewe Bashiru bin Saad, umechukia chuki! Umemhusudu mtoto wa ammi yako asiupate uamiri?’ Alisema: ‘Hapana wallahi, lakini nimeona vibaya kushindania haki ya jamaa ambayo Mwenyezi Mungu ameijaalia kuwa ni yao.’

“Watu wa kabila la Aus walipoona alilofanya Bashiru bin Saad na wanaloitia makuraishi na wanalolitaka watu wa kabila la Khazraji, ambalo ni kumfanya Saad bin Ubada awe Amiir wao, waliambiana wao kwa wao, akiwemo Usaid bin Hudhwayru, naye alikuwa mmoja wa machifu: ‘Wallahi endapo mtawatawalisha juu yenu kabila la Khazraj mara moja hamtobakia na ubora kwao na wala hawatowafanyieni na nyinyi muwe na hisa pamoja nao abadan, hivyo basi simameni mfanyieni baia Abu Bakr.’ Ndipo walimwendea Abu Bakr na wakamfanyia baia. Saad bin Ubada aliharibikiwa na waliharibikiwa watu wa kabila la Khazraji na hatimaye kulikosa jambo ambalo kwalo walijikusanya...... Basi wakawa watu wanakuja kutoka pande zote wanamfanyia baia, na walikaribia kumkanyaga Saad bin Ubadah.

“Watu miongoni mwa watu wa Saad wakasema: ‘Jihadharini msimkanyage Saad.’ Umar akasema: ‘Muuweni! Mwenyezi Mungu amuuwe.’ Halafu alimsimamia kichwani na akasema: ‘Nilikusudia nikukanyage mpaka mwili wako uwe si wa kawaida.’ Qays bin Saad alizishika ndevu za Umar na akasema: ‘Wallahi lau ungemnyofoa unywele haungerejea….’ Abu Bakr akasema: ‘Polepole, ewe Umar! Upole hapa wafaa mno.’ Umar alimwacha. Saad akasema: ‘Ama wallahi lau ningekuwa na nguvu ambazo kwazo ningeweza kuinuka, basi ungesikia kutoka kwangu katika nchi na vichochoro vyake ngurumo ambayo ingekuzuia wewe na swahiba zako, na wallahi ningekukutanisha na kaumu ambao wewe kwao ni mfuasi na si kiongozi. Nibebeni kunitoa mahali hapa.’ Na walimbeba na kumwingiza nyumbani mwake…”

Tukio hili halihitajii ufafanuzi na tafsiri, kwani lenyewe binafsi linafichua jinsi Abu Bakr alivyotawalia ukhalifa…Na kuwa tukio hili liko mbali mno na kinachoitwa Shura. Kwa kuwa Shura haiendani na shaka kama hii ya mahali. Ambapo Saqifa ya Bani Saidah ilikuwa kondeni nje ya mji wa Madina, hali ilikuwa ndani ya msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ni mahali palikuwa panafaa zaidi kufanyika jambo hili. Kwa kuwa katika msikiti wa Mtume (s.a.w.w.) ni mahali pa kukusanyika waislamu na mahali pa kushauriana katika mambo ya dunia na dini.

Zaidi ya hapo ni ile shaka ya wakati, kwa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alikuwa angali amebaki kitandani, mwili wake uliotohara haujazikwa.3 Vipi nafsi zao hawa ziliwaruhusu wamtelekeze katika hali kama hii na waende kuzozania jambo la ukhalifa. Na wakubwa katika swahaba na watukufu wao wakawa wanashughulika mbali na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).

Je kuna mwenye akili timamu anaweza kuliita tendo kama hili kuwa ni Shura?! Na kwa kweli watu hawajaufanyia utafiti ukhalifa wa kiislamu ulio na uongofu ambao kwa njia yake umoja wa waislamu na kuwepo kwao kungehifadhika. Na maneno yao, yaani lugha zilizotumika wakati kila upande ulipojinadi kuwa ndio wenye haki zaidi ya kuwa khalifa wa Mtume (s.a.w.w), yanafichua jambo hili. Hebu izingatieni kauli ya Saad: “Lihodhini jambo hili mbali na watu wengine.” Walimjibu: “Rai yako ni muwafaka na kauli yako ni ya sawa, hatutakiuka rai yako.”

Na kauli ya Umar: “Nani agombanie na sisi mamlaka ya Muhammad na uamiri wake.” Na pia kauli ya al-Hubbab: “Lishikilieni mikononi mwenu wala msisikilize usemi wa huyu na swahiba zake wasije wakaenda na hisa yenu ya jambo hili.”

Kauli hizi zinafichua aina ya kaumu hii ya watu. Wao hawakutaka kitu kingine ila mamlaka na utawala.
Hiyo ni kuachia mbali maneno makali ambayo yalitokea baina ya maswahaba ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alitaabika nao miaka ishirini na tatu kuwapa malezi ya kiimani, kiroho na kimaada, mfano ni kauli ya Umar kumwambia Hubbab: “Basi Mwenyezi Mungu akuuwe.”

Na kauli ya Habbabu: “Bali akuuwe wewe tu.” Au kauli ya Umar kumwambia Saad: “Muuweni! Mwenyezi Mungu amuuwe.” Na usemi wake kumwambia Saad: “Nilikusudia nikukanyage mpaka mwili wako uwe si wa kawaida.” Au kauli ya Qays bin Saad kumwambia Umar hali amezishika ndevu zake: “Wallahi lau ungemnyofoa unyele haungerejea, na kinywani mwako mko wazi.”

Na mfano wa maneno kama haya mazito ambayo yanatokea mahali kama hapa pa uchaguzi, maneno nyeti kiwango cha kufikia kutishia kupiga na kuchochea kuuwa, kama yatajulisha chochote basi kitakuwa ni zile nafsi zilizojaa wingi wa chuki na zilizoshiba uadui na hali ya kutopendeleana kheri wenyewe kwa wenyewe. Hao ndio maswahaba vigogo! Hivyo itakuwaje sisi tukubaliane na ushauri wa mfano wa watu kama hawa endapo Shura itakuwa ni kitu sahihi?

Hebu sasa tazama maneno yao na hoja zao wao kwa wao, zenyewe ni hoja mbovu zilizo mbali na usahihi, kwa mfano Umar anatoa hoja kwa kusema: “Wallahi waarabu hawatoridhia wawafanyeni muwe maamiri hali Nabii wao anatoka kwa asiyekuwa ninyi, lakini waarabu hawakatai kumtawalisha jambo lao ambaye unabii upo katika wao, na walii wa mambo yao kutokana na wao.”

Ikiwa waarabu hawaridhiki na uamiri wa mtu aliye mbali na Mtume basi ni awla waridhike na uongozi wa mtu aliye karibu mno na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.), naye ni Ali bin Abu Talib (a.s.), na kwa ajili hiyo Jemedari wa waumini anasema: “Wametoa hoja kupitia mti na wameacha tunda.”4

Na ikiwa waarabu hawaridhiki na uamiri wa Ali (a.s.) bila shaka watakuwa hawaridhiki kabisa na uamiri wa mtu kutoka kabila la Taym. Na hii ikiwa ndio hoja yao basi Ali anayo hoja muafaka.

Abu Bakr al-Jawhiriy amesema kuhusiana na hoja ya Ali (a.s.): “Na Ali anasema: ‘Mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu na ndugu wa Mtume.’ walimpeleka mpaka kwa Abu Bakr, akaambiwa: Fanya baia. Akasema: ‘Mimi nina haki ya jambo hili kuliko ninyi, siwafanyieni baia na ninyi mwapaswa kunifanyia baia mimi. Mmelichukua jambo hili kutoka kwa Answar na mmeleta hoja dhidi yao kwa ukaribu wenu na Mtume wa Mwenyezi Mungu na waliwapeni uongozi na walikukabidhini uamiri. Na mimi ninaleta hoja dhidi yenu kama mlivyoileta hoja dhidi ya Answar.

Tufanyieni insafu ikiwa kweli mwamuogopa Mwenyezi Mungu nafsini mwenu, na tutambueni sisi kwenye jambo hili walichokitambua Answar kwa ajili yenu, kama sivyo basi rejeeni na dhulma hali mkiwa mnajua.’ Umar akasema: ‘Kwa hakika wewe si mwenye kuachwa ila tu mpaka ufanye baia.’ Ali alimwambia: ‘Kamua maziwa kwa ajili yake5 ewe Umar, una hisa yake, leo lifanyie mkazo jambo lake ili kesho akurudishie, wallahi siikubali kauli yako wala sikufuati.’6

“Walijaribu kwa njia kadhaa ili wampate Ali (a.s.). Siku moja walijaribu kumghuri Abbas wakasema: ‘Mpeni hisa iwe kwa ajili yake na kwa ajili ya kizazi chake baada yake yeye, kwa yeye mtakuwa mmeukata upande wa Ali bin Abu Talib na mtakuwa na hoja dhidi ya Ali endapo – Abbas – akielemea pamwe na ninyi”7

Na imekuja katika jibu la Abbas: “Ama uliyosema utalijaalia kwa ajili yangu, ikiwa (ukhalifa) ni haki ya waumini wewe hauna haki ya kutoa maamuzi katika hilo, na ikiwa ni yetu haturidhiki kuipata sehemu mbali na nyingine!

Zingatia kuwa ikiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ni mti, sisi ni matawi yake na ninyi ni miti ya jirani yake.”8 Na pindi mpango huu ulipokosa kufanikiwa waligeukia utaratibu wa kukirihisha.

Umar bin al-Khattab akasema: “Tulikuwa na habari Mwenyezi Mungu alipomfisha Nabii wake kuwa Ali, Zubair na walio pamwe na wawili hawa walikuwa kinyume na sisi, wakiwa nyumbani mwa Fatima.”9 Ndipo Abu Bakr alimtuma kwao Umar bin al-Khattab awafurushe kutoka nyumbani mwa Fatima, na alimwambia: “Endapo watakataa waue.”

Akaenda Umar bin al-Khattab na waliokuwa pamoja naye na kijinga cha moto ili aunguze nyumba pamoja na waliomo. Fatima aliwalaki na akasema: “Ewe mwana wa al-Khattab umekuja kuiunguza nyumba yetu?!” Alisema: “Ndio au muingie walimoingia umma.”10 Na katika kitabu Ansabul-Ashraf: “Fatima alikutana naye mlangoni na akasema: ‘Ewe mwana wa al-Khattab waja kuniunguza mlangoni kwangu?!’ Akasema: ‘Naam.”11

Na wanahistoria wametaja idadi ya watu ambao walikwenda kiadui kwenye nyumba ya Fatima ili kuiunguza:

1. Umar bin al-Khattab.
2. Khalid bin al-Walid
3. Abdur Rahman bin A’ufi
4. Thabit bin Qays bin Shammas
5. Ziyadu bin Labiid
6. Muhammad bin Muslim
7. Zayd bin Thabit
8. Salamah bin Salaamah bin Waghsh
9. Salamatu bin Aslam
10. Usidu bin Hudhwair

Al-Yaaqubiy amesema: “Walikuja wakiwa kikundi mpaka waliihujumu nyumba..........na upanga wake ulivunjika, yaani upanga wa Ali (a.s.) na waliingia nyumba hiyo.”12

Tabariy anasema: “Umar Bin al-Khattab alikwenda kwenye nyumba ya Ali ndani mukiwa na Talha na Zubair na wanaume kadhaa miongoni mwa muhajirina. Zubair alitoka akiwa ameshika upanga, na alijikwaa na upanga ulidondoka mkononi, walimrukia na kuuchukua.”

Na Fatima aliona walivyotendewa – yaani Ali na Zubair – alisimama kwenye mlango wa chumba na akasema: “Ewe Abu Bakr, haraka mno mmewashambulia Ahlul-Bayt wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Wallahi sintomsemesha Umar hadi nikutane na Mwenyezi Mungu.”13

Kwa ajili hii na kwa kumnyima Fatima mirathi yake na taabu nyingine, Fatima alichukia na alimkasirikia Abu Bakr, alimnunia wala hakumsemesha hadi alipotawafu, na aliishi baada ya Nabii miezi sita…! Na alipofishwa mumewe Ali (a.s.) alimzika usiku wala Abu Bakr hakuidhinishwa.14 Yaani hakuruhusiwa kuhudhuria jeneza la Bibi Fatima.

Na katika riwaya nyingine ni kuwa yeye – Fatima – alimwambia: “Wallahi nitaomba dhidi yako katika kila swala nitakayoiswali.”15

Kwa minajili hiyo Abu Bakr akasema katika ugonjwa wa umauti wake akasema: “Kwa kweli mimi sijutii kitu duniani isipokuwa vitatu nimevifanya, natamani nisingekuwa nimevifanya .......... Ama vitatu nilivyovifanya: Natamani kuwa mimi nisingefanya chochote kuikashifu nyumba ya Fatima japo wangekuwa wameifunga kwa ajili ya vita.”16

Na katika kitabu Tarikhul-Yaaqubiy: “Najuta bora nisingeipekua nyumba ya Fatima binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), na kuwaingiza watu japokuwa angekuwa ameifunga kwa ajili ya vita.”17

Kutokana na hali hiyo mshairi wa Mto Naili, Ibrahim, anasema: “Kauli yake kwa Ali, Umar aliisema, yenye heshima kwa aisikiae, kubwa kwa msemaji wake: Nitaunguza yako nyumba, siibakishi juu yako kama baia hautotoa, wewe na binti Mustafa ndanimwe. Hapana wakuropoka isipokuwa Abu Hafsa, mbele ya shujaa wa Kiadnani na mlinzi wao.”18

Mambo yaliendelea vibaya zaidi ya hivyo, walipomtishia Ali (a.s.) kumuua, kwa kweli walimtoa Ali kutoka nyumbani mwake kwa karaha na walikwenda naye kwa Abu Bakr na walimwambia: “Fanya baia.” Akasema: “Hakika mimi sitofanya …” Wakasema: “Kwa hiyo wallahi ambaye hapana Allah isipokuwa ni Yeye, tutakata shingo yako.” Akasema: “Kwa hiyo mtakuwa mnamuuwa mja wa Mwenyezi Mungu na ndugu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu.”19

Kwa njia kama hii ambayo ukhalifa ulianzia kwa ubabe na kuishia kwa kulazimisha kwa karaha na kutishia mtu kuuliwa, haiwezekani iwe ndio kigezo cha kusihi nadharia ya Shura. Na Abu Bakr alipotambua ubaya wa waliyotenda walikuja kuomba radhi kwa Fatima, lakini baada ya wakati kuwa umepita.

Fatima aliwaambia: “Mwaona endapo nitawahadithia Hadithi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu mtaitambua na kuifanyia kazi?” Wakasema: “Ndio!” Hivyo basi akasema: “Nakusihini kwa jina la Allah, hamkumsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu anasema (s.a.w.w.): ‘Kuridhika kwa Fatima ndio ridhaa yangu, kukasirika kwa Fatima ni kukasirika kwangu, hivyo mwenye kumpenda Fatima binti yangu amenipenda mimi na mwenye kumridhisha Fatima ameniridhisha mimi, na mwenye kumkasirisha Fatima amenikasirisha mimi!’’’

Wakasema: “Ndio tuliisikia kutoka Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).” Fatima (a.s.) akasema: “Kwa hakika mimi namfanya Mwenyezi Mungu na malaika wake mashahidi, kuwa ninyi mmenikasirisha wala hamkuniridhisha na nikikutana na Nabii (s.a.w.w.) kwa hakika nitamlalamikia kuhusu ninyi.” Na akasema naye akimkhatibu Abu Bakr: “Wallahi nitaomba kwa Mwenyezi Mungu dhidi yenu katika kila swala nitakayoiswali…”20

Kwa hiyo Abu Bakr hakustahiki ukhalifa wa waislamu kwa njia ya Shura, kwa kuwa Shura hii ni batili kinadharia, ukweli wa mambo Shura haikuwepo nje kiutendaji. Ikiwa tutalifumbia macho na kukubali kuwa Abu Bakr alitwaa madaraka ya ukhalifa kwa njia ya Shura, na kwamba Shura ndio njia pekee ya suala hilo, hivi ilikuwaje awe na haki ya kumsimika Umar khalifa baada yake?

Kwa mujibu huo Abu Bakr na ukhalifa wake anakuwa kwenye mambo mawili yaliyohadharishwa:

La kwanza: Iwe Shura ndiyo njia ambayo Mwenyezi Mungu ameiweka ili kumsimika khalifa, kwa hiyo Abu Bakr anakuwa mwasi wa amri ya Mwenyezi Mungu, kwa kule kwenda kinyume na amri hii, na kumsimika Umar

La pili: Shura iwe si jambo la kiungu, kwa hiyo unakuwa ukhalifa wa Abu Bakr si wa kisheria, kwa sababu ulikuja kwa njia ya Shura ambayo Mwenyezi Mungu hajaiamrisha.

Kwa mujibu huo unakuwa ukhalifa wa Umar na Uthman si wa kisheria, isipokuwa Imam Ali (a.s.), kwa kuwa umma wote umeafikiana kumfanyia baia awe khalifa baada ya kuuliwa Uthman, zaidi ya hapo ni kule kuwepo kwa tamko rasmi la ukhalifa na uimamu wake kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na toka kwa Mtume wake (s.a.w.w), na kama kutakuwa na Shura basi ni ya Ali (a.s.), kama ambavyo habari zimefululiza kuhusu hilo.

Na ili kukamilsha faida tunahitimisha utafiti huu kwa mjadala huu:

Aliulizwa Ali bin Maytham: Kwa nini Ali (a.s.) aliacha kupigana nao? Alisema: “Kama alivyoacha Harun kupigana na Samiriyyu hali ikiwa walimwabudu ndama.21 Alikuwa ni kama Harun aliposema: “Ewe mwana wa mama yangu! Hakika watu wamenidharau (Surat Aaraf: 150). Ni kama Nuh aliposema: “Kwa hakika nimeshindwa, kwa hiyo nisaidie.(Surat al-Qamar: 10). Na kama Lut aliposema: “Laiti ningelikuwa na nguvu kwenu, au nategemea kwenye nguzo zenye nguvu.” (Sura Hud:80). Na kama Musa na Harun, Musa aliposema “Mola wangu hakika mimi similiki ila nafsi yangu na ndugu yangu.’ (Surat al-Maidah: 25). “

Na maana hii ameichukua kutoka kauli ya Amiirul-muuminina aliyoisema pale ilipomfikia habari kuwa yeye hakushindana na wale wawili wa mwanzo, hapo basi akasema (a.s.):

“Mimi nina mfano wa kuuiga kutoka kwa manabii sita, wa kwanza wao ni Khalilu Rahman aliposema: “Na mimi nijitenga nanyi na mnayoyaabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu.” (Surat Maryam: 48). Mkisema kuwa: Yeye alijitenga nao bila ya kukirihishwa mtakuwa mmekufuru. Na mkisema kuwa: Yeye alijitenga mbali nao alipoona ya karaha, basi Wasii anao udhuru wa kufaa zaidi.

“Na kwa Nabii Lut (a.s.) aliposema: “Laiti ningelikuwa na nguvu kwenu, au nategemea kwenye nguzo zenye nguvu.” (Surat Hud: 80). Na mkisema kuwa: Lut alijitenga mbali nao bila ya kukirihishwa, mtakuwa mmekufuru. Na mkisema: Hakuwa na nguvu nao, kwa hiyo Wasii anao udhuru wa kufaa zaidi.

“Na kwa Yusuf aliposema: “Ewe Mola Wangu! Naipenda zaidi gereza kuliko haya wanayoniitia.” (Surat Yusuf: 33), endapo mtasema: Aliitaka jela bila ya chukizo limchukizalo Mwenyezi Mungu, mtakuwa mmekufuru. Na mkisema kuwa: Yeye aliitiwa kwenye jambo linalomchukiza Mwenyezi Mungu, basi Wasii anao udhuru wa kufaa zaidi.

“Na kwa Musa aliposema: “Basi nikakukimbieni nilipokuogopeni” (Surat Shuaraa: 21), endapo mkisema kuwa alikimbia bila ya hofu mmekufuru. Na kama mtasema: Aliwakimbia kwa sababu ya uovu waliomtakia, basi Wasii anao udhuru wa kufaa zaidi.

“Na kwa Harun alipomwambia nduguye: “Ewe mwana wa mama yangu! Hakika watu wamenidharau, na hata walikaribia kuniua” (Surat A’araf: 150), kama mtasema hawakumdhalilisha na kuwa tayari kumuua basi mtakuwa mmekufuru.
Na mkisema walimdhalilisha na walikuwa tayari kumuuwa na kwa ajili hiyo aliwanyamazia, basi Wasii anao udhuru wa kufaa zaidi.

“Na kwa Muhammad (s.a.w.w) alipokimbilia pangoni na kuniacha mimi kwenye tandiko lake na nilijitolea roho yangu kwa ajili ya Allah (s.w.t.).
Na mkisema kuwa: Alikimbia bila ya kuhofishwa na hofu yoyote waliyomfanyia mtakuwa mmekufuru. Na mkisema: Kwa kweli wao walimhofisha na hakuwa na njia ila kukimbilia pangoni, basi Wasii anao udhuru wa kufaa zaidi.” Hapo watu wakasema: “Umesema kweli ewe Amirul-Mu’minina.”22

TATU: Swahaba Na Aya Ya Kurudi Nyuma

وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهِ الرُّسُلُ ۚ أَفَإِنْ مَاتَ أَوْ قُتِلَ انْقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ ۚ وَمَنْ يَنْقَلِبْ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ فَلَنْ يَضُرَّ اللَّهَ شَيْئًا ۗ وَسَيَجْزِي اللَّهُ الشَّاكِرِينَ {144}

“Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume aliyepitiwa na Mitume kabla yake. Basi je akifa au akiuliwa mtarudi nyuma kwa visigino vyenu? Na atakayerudi nyuma kwa visigino vyake hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaoshukuru.’ (Surat al-Imran: 144).

Kwa kweli kiini cha Aya hii tukufu ni kuelezea kifo cha Mtume (s.a.w.w) na yatakayojiri baada yake, kama vile kugeukia kwenye ukafiri waliokuwa nao hapo kabla. Na kiini hiki kimekusanywa na matamko haya matatu: ‘’Na hakuwa Muhammad” “Basi je akifa au akiuliwa” “Mtarudi nyuma kwa visigino vyenu?” Ili kuingia kwenye undani wa Aya hii na kuiangazia mwanga wa ufafanuzi kiasi fulani, hapana budi kuuliza baadhi ya maswali yatakayoandaa kuleta fikra na kufanya jaribio la kuyajibu.

Kwa nini Muumba hakutosheka na kauli yake: ‘’Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume” na hapo hapo moja kwa moja amekuja na kauli yake: “Basi je akifa au akiuliwa” hali ikiwa muktadha wa Aya ungebaki umenyooka na uko sawa bila ya kifungu hicho, ila tu ametaja sifa ya risala humo, na kwa tamko la kutilia mkazo: Yeye ni Mtume, kabla yake wamepita Mitume?

Nini kinachotofautisha kati ya kifo cha kawaida na cha kuuliwa? Neno au inamaanisha tofauti kati ya kilichoungwa na kilichoungiwa. Basi nini tofauti kati ya vifo hivyo viwili?

Na kwa nini huku kukariri kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hali Yeye akiwa anajua fika kuwa Mtume Wake (s.a.w.w) atakufa kifo cha kawaida? Na nani wanaosemeshwa na kauli yake: “Mtarudi nyuma?” Na watarudi nyuma kugeukia kwenye nini?

Nini uhusiano wa kugeuka na kifo cha Mtume (s.a.w.)? Na mahali hapa ni pa msimamo, kwa nini ametumia tamko “Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaoshukuru,wala hakusema: “Wenye msimamo, au waislamu, au waumini?”

Kabla ya kujibu maswali haya hapana budi kutaja vitangulizi viwili muhimu:

Kwanza: Sababu ya kuteremka: Wanatafsiri wamesema kuwa sababu ya kuteremka kwa Aya hii ni kule kushindwa kulikowakumba waislamu kwenye vita ya Uhud. Kwa kuwa washirikina walivumisha habari kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ameuliwa vitani, kitu ambacho kilisababisha hali ya kuhisi kushindwa, kurudi nyuma, na baadhi ya waislamu kuingiwa na shaka. Mwenyezi Mungu aliiteremsha Aya hii akiwalaumu waislamu kwa hilo.

Pili: Nini la msingi kuzihusu Aya? Je la msingi kuzihusu Aya za Qur’ani ni kuwa zinafaa kwa kila zama isipokuwa ile yenye kutoka kwa dalili? Au kinyume chake?

Na makusudio yake ni kuwa lau Aya zingekuwa zinafaa katika kila zama, basi sisi tungeweza kuziingiza maana za Aya kwenye matumizi ya jumla mpaka zama isiyo ya sababu ya kuteremka kwake, na kama si hivyo basi kwa kweli sisi tunajiambatanisha na sababu ambayo Aya iliteremkia, na hivyo kuieneza mpaka zama isioteremkia ndiko kunakohitajia dalili.

Wanavyuoni wa kiislamu wameafikiana Sunni na Shia kuwa linalozingatiwa ni ueneaji wa maana ya tamko sio kuifanya sababu kuwa ndio mahsusi, kwa kuwa lau ingekuwa asili ni kutozipitisha kwa ueneaji maana ya Aya za Qur’ani katika kila zama, kuitendea kazi Qur’ani katika zama zijazo kungebatilika, au Aya nyingi tungeziacha kwenye kuruba zimeganda hazifai.

Na hilo haliendani na kiini cha Uislamu, mwenendo wake na mafunzo yake na uenevu wake. Hii ndio dalili ya kiakili, na inatiliwa nguvu na Aya nyingi za Qur’ani tukufu ambazo zinahimiza kuzingatia na kuitendea kazi Qur’ani tukufu na zinagombeza kufanya kinyume chake.

Ikiwa tutaruhusu rai ya pili basi kauli yake (s.w.t.): “Na Qur’ani isomwapo basi isikilizeni na nyamazeni ili mpate kurehemewa.” (Surat A’araf: 204) haingekuwa na maana. Kwa kuwa inaishiria kwenye Qur’ani yote wala haikuhusu sehemu ndogo mahsusi au baadhi yake, bali ni kila aya tujaribu kuifahamu na tunyamaze na tuyachukue mafunzo kutoka humo, kama ambavyo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametuamuru kuizingatia: “Je hawaizingatii Qur’ani au nyoyo zina kufuli.” (Surat Muhammad: 24) Na anakemea kuiamini sehemu tu ya Qur’ani na kutoamini sehemu yake nyingine: “Ambao wameifanya Qur’ani vipande vipande. (Surat Hijri: 91)

Na anasema (s.w.t.): “Na bila shaka tumewaeleza watu kwa namna nyingi katika Qur’ani hii kila mfano” (Surat Bani Isra’il: 89) Na amesema: “Na kwa hakika tumeifanya Qur’ani iwe nyepesi kufahamika, lakini je, yuko anayekumbuka?” (Sura Qamar: 17) Akasema tena: “Ni Kitabu kinachoelezwa Aya zake, Qur’ani yenye uwazi kwa watu wanaojua.” (Sura Fuswilat: 3) Na pia amesema: “Kwa hakika tumeifanya Qur’ani kuwa ya uwazi ili mfahamu.” (Sura Zukhruf). Hivyo Aya hizi zote zinatuhimiza kujiambatanisha na Qur’ani yote sio na baadhi yake tu.

Kwa hali yoyote, lau tutajiambatanisha na rai ya pili mwislamu yeyote hairidhii, na kwa mfano tu ni kuwa, kwa kweli aya tuikusudiayo ina dalili kiasi kwamba inathibiti kuwa Aya hii sio iliyozingirwa na wakati wa kuteremka kwake tu, bali inaendelea katika maisha yote ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na wa baada yake, na dalili kuhusu hilo zinakujia:

Kwa kweli habari zilizoenea kuihusu vita ya Uhud ni kuwa Mtume (s.a.w.w) ameuliwa, na Aya inazungumzia hali ile ya kuenea kwa habari au kutokea umauti wake: “Basi je akifa au akiuliwa.” Hivyo lau ingekuwa mahsusi kwa zama ilioshukia tu, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) angesema: “Basi je akiuliwa,” na labda kutajwa umauti ni dalili ya kuwa yaliyotokea katika vita ya Uhud ambayo ni kurudi nyuma na kugeuka basi mfano wake utajitokeza tena baada ya kufishwa Mtume (s.a.w.w).

Na faida ya kiutendaji ya utangulizi huu katika utafiti wetu ni kuwa sisi haitulazimu dalili nyingine katika kuieneza hukumu ya Aya ya kurudi nyuma na kugeuka zaidi ya hilo tukio ambalo Aya iliteremka, iwapo msingi wa kwanza utathibiti. Nao ndio haki kama ulivyoona.

Na kulingana na kauli ya pili, hapana budi kuwe na dalili mahsusi ili kuthibitisha kuwa Aya hii ni mahsusi kwa tukio ambalo kwa ajili yake Aya ya kurudi nyuma na kugeuka iliteremka, na kuwa yenyewe inaendelea kwa kadiri ya kuendelea kwa uhai wa Mtume (s.a.w.w) na baada yake, na ikiw kauli ya pili ni sahihi kwa mfano, dalili ya kutiririka Aya hii kwa kadiri ya kuendelea kwa maisha ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na baada yake ipo ndani ya mikunjo kunjo ya Aya yenyewe. Lakini ni Wapi na ni vipi?

Ama swali kuhusu wapi? Jibu ni kuwa: Katika kauli yake (s.w.t.): “Basi je akifa au akiuliwa.” Ama swali la kuwa: Ni vipi? Ni kuwa habari zilizoenezwa na kuvuma kuuzunguka mji wa Madina na ndani yake wakati wa vita vya Uhud ni kuuliwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), jambo ambalo lilisababisha hali ya kuritadi na kugeuka nyuma, hivyo lau Mwenyezi Mungu angetaka kuifanya Aya hii iwe mahsusi kwa vita vya Uhud tu angesema: “Basi je akiuliwa”, lakini kuingia kwake katika hali ya kifo cha kawaida pia: “Basi je akifa au akiuliwa” yatoa khabari kwa namna isio na kifuniko kuwa hali ile itajirudia pindi umauti wake wa kawaida utakapomtokea kweli. Na kule kukariri kulikotamkwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa neno au limaanishalo tofauti kati ya kilichoungwa na kilichoungiwa, kama wanavyoafikiana watu wa lugha, na yeye (s.w.t.) ni Mjuzi wa ghaibu na jinsi ya umauti wa kawaida wa Mtume wake (s.a.w.), si chochote ila ni utashi wake ili yaenee matukio mawili, tukio la kuenea uvumi wa kuuliwa kwake (s.a.w.w) katika vita vya Uhud na tukio la umauti wake (s.a.w.w).
Ama mwenye kuunasibisha kifo cha umauti wa kuuwawa na kitendo cha mwanadamu na umauti wa kawaida na kitendo cha Mola, na kuwa makusudio ya Mwenyezi Mungu kuutaja ufafanuzi huu ndani ya Aya ni tukio la Uhud tu, inamaanisha kuwa mtizamo umebadilika kutoka kitendo cha mwanadamu na kuwa kitendo cha Mwenyezi Mungu.

akini hilo Si barabara, kwani amesema (s.w.t.): “Hamkuwauwa lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewauwa.” Kwa hiyo inafaa kukiegemeza kitendo cha uuwaji Kwake (s.w.t.), zaidi ya hapo ni kuwa muktadha wa Aya na muundo wake hausaidii ufafanuzi huu. Kwa kuwa Allah (s.w.t.) anatilia shime kukemea na kukataza kugeuka, wala haangalii upande wa ufafanuzi kati ya kitendo cha mja na kitendo cha Mola.

Kwa kweli Mwenyezi Mungu amelitega jibu: “Mtarudi nyuma” nalo ni jibu la vitendo viwili vya sharti ambavyo ni “Basi je akifa au akiuliwa” na utegaji huu wajulisha kuwa mkazo wake upo katika hali ya kurudi nyuma, na huko kurudi nyuma kutakuja wakati wa umauti wake wa kawaida au wa kuuliwa kwake. Na kuiingiza herufi ya istifhamu kwenye sharti, hali ambayo yafidisha mkazo si kwa jambo lingine ila ni kwa ajili ya kupinga, kukaripia, na kuidhalilisha hali hii.

Na ni mbali mno Aya ifahamike kwa maana hii: “Endapo uvumi utaenea utakaposikika umauti wa Muhammad (s.a.w.w) kwa kitendo changu na nimejaalia kitendo changu kupitia makafiri kwa kule kumuuwa kwao kwa mikono yao, mtakuwa mmegeuka na kurudi nyuma.” Kwa kuwa mtazamo wa juu kwenye Aya hii ni kama kwenye Aya zote, hivyo maana kama hii inapunguza sana ile hali ya Mwenyezi Mungu kuwakemea, na ule mtazamo ambao ni kutofanya wepesi katika tukio kama hili, na pia inatawanya mkito wa Aya na kuifanya iwe na mihimili mingi, na hali hii ni kinyume na ubainifu wa yeyote mwenye hekima basi itakuwaje kwa Mwenye hekima kuliko wenye hekima wote.

Na linalotilia nguvu kuwa Aya tukufu haizingirwi na tukio hili ni yatakayokuja katika ufafanuzi wake ujao, ambayo ni katika yanayoondoa mkanganyiko wowote au shaka kuwa Aya hii haikuzingirwa na tukio lile moja tu, na kuwa ni yenye kuujumuisha wakati wa umauti wa Mtume (s.a.w.w) na baada yake.

Kisha, jua kuwa umauti una maana mbili: Ya jumla na makusudio yake ni kuichukuwa roho, Allah anasema: “Popote mtakapokuwa yatawafikia mauti, na ingawa muwe katika ngome zilizo na nguvu” (Surat an- Nisaa: 78). Na akasema: “Naye ndiye aliyekuhuisheni kisha akakufisheni, kisha atakufufueni, hakika mwanadamu ni mwenye kukufuru sana. (Surat Al-Hajj: 66).

Na una maana yake makhsusi iliyo mukabala na kuuwa, nayo ni ya mtu anayekufa mwenyewe kwa sababu ya kuharibikiwa na jengo lake la maisha. Na Aya yeyote itakayokuja na matamko mawili wakati mmoja, tamko la umauti wa kawaida na la kuuwawa, maana ikusudiwayo hapo itakuwa ni ile makhsusi. Na hilo linapata nguvu inapotumika neno au, ambalo lamaanisha utofauti kati ya sentensi iliyotangulia na inayofuata, na mfano wa hilo ni kauli ya Mwenyezi Mungu: “Na kama mkiuliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu au mkifa, basi msamaha na rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko vile wanavyokusanya.” (Surat Aali Imran: 157.). Na kauli yake: “Na kama mkifa au mkiuliwa, ni kwa Mwenyezi Mungu ndiko mtakakokusanywa.”(Surat Aali Imran: 158.). Na kauli yake: Wangekuwa kwetu wasingelikufa wala wasingeuliwa” (Surat Aali Imran: 156)

Kwa kuwa lau zingekuwa Aya hizi za umauti ziko katika maana yake ya sura ya jumla basi kungekuwa hakuna linalohalalisha kutumia tamko la kuuwa, kwa kuwa maana hiyo ya tamko kuuwa itakuwa imo ndanimwe, na hii ni kinyume na balagha, na hili ndio linaafikiana na mahali pa tofauti yetu.

Kwa mujibu huo inathibiti kuwa makusudio ya umauti katka Aya ya kugeuka ni maana makhsusi ambayo ni sehemu ya kifo. Hivyo kifo ima ni cha kawaida au ni cha kuuwawa.

Kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amejikita kuielezea sifa ya risala kumhusu Mtume Wake kuwa: Yeye ni Mtume wamepita kabla yake Mitume, hali ilikuwa inamtosha kauli yake: ‘’Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume” na aimalizie moja kwa moja na kauli yake: “Basi je akifa au akiuliwa”?

Na kwa mtazamo wa kwanza katika kujibu swali hili, kama walivyofanya baadhi ya wafasiri ni kuwa, Mwenyezi Mungu alitaka tu kuwatanabahisha waislamu ukweli nao ni kuwa Muhammad (s.a.w.w.) si wa kubaki milele, bali ni wa kupita na ni maiti mtarajiwa, hali yake ni hali ya mitume wengine ambao wamepita na wamekufa.

Maana hii ni dhahiri ila tu si maana pekee, kwa sababu lau makusudio yake yangekuwa kumthibitishia sifa ya umauti tu angesema: ‘’Na hakuwa Muhammad ila ni mwanadamu aliyepitiwa na wanadamu kabla yake” Ili kutilia nguvu tabia ya kibnadamu ya kufikia mwisho na kutobaki milele. Na kuna maana zenye umbali zaidi na za kina mno kuliko hii zimefanya itangulizwe sifa ya utume na itiliwe nguvu, nazo ni:

Kwanza: Kama ambavyo dini haikuwa imetegwa kwenye maisha ya mitume waliopita, pia haikutegwa kwenye maisha ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w), hivyo kama walivyokufa manabii waliotangulia na dini iliendelea baada yao, hivyo hivyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) atakapokufa au kuuwawa dini itaendelea baada yake.

Pili: Nayo ni ya kina sana na yenye kuhitaji mtazamo wenye umakini mno na yenye maana enezi zaidi nayo ni, kutilia nguvu uhakika wa uwiano wa mienendo kati ya umma mbalimbali baada ya umauti wa mitume yao, hivyo yaliyotokea katika umma zile yatatokea katika umma huu kama mfano uleule kiatu kwa kiatu, ukweli huu unatiliwa nguvu na Qur’ani na Sunna na hali halisi.

Ama kutoka kwenye Qur’ani ni hii kauli yake (s.w.t.):

تِلْكَ الرُّسُلُ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۘ مِنْهُمْ مَنْ كَلَّمَ اللَّهُ ۖ وَرَفَعَ بَعْضَهُمْ دَرَجَاتٍ ۚ وَآتَيْنَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ الْبَيِّنَاتِ وَأَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ ۗ وَلَوْ شَاءَ اللَّهُ مَا اقْتَتَلَ الَّذِينَ مِنْ بَعْدِهِمْ مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَاتُ وَلَٰكِنِ اخْتَلَفُوا فَمِنْهُمْ مَنْ آمَنَ وَمِنْهُمْ مَنْ كَفَرَ ۚ وَلَوْ شَاءَ اللَّهُ مَا اقْتَتَلُوا وَلَٰكِنَّ اللَّهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ {253}

“Hao Mitume tumewatukuza baadhi yao zaidi kuliko wengine. Katika wao wako ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na baadhi yao amewatukuza daraja nyingi. Na Isa mwana wa Mariam tukampa dalili zilizo wazi wazi, na tukamsaidia kwa roho takatifu. Na kama Mwenyezi Mungu angelipenda, wasingelipigana waliokuja nyuma yao, baada ya kuwafikia dalili zilizo wazi wazi, lakini walikhitilafiana. Wako miongoni mwao waliokufuru. Na kama Mwenyezi Mungu angelipenda, wasingelipigana lakini Mwenyezi Mungu hufanya anayoyataka.” (Surat Baqara: 253)

Hivyo neno yao larejea kwa Mitume, na lau angemkusudia Isa tu (a.s.) angesema: Baada yake. Wala haiwezi ikasemwa kuwa kwa neno hilo alimkusudia Isa (a.s.) kwa maana ya kumtukuza, kwa kuwa (kwa mujibu wa lugha ya kiarabu) mahali pa neno yao katika baada yao inatia dosari balagha na fasaha (ya kiarabu) ikiwa kwalo imekusudiwa kutukuza. Halafu kulingana na kauli ya kutokukusudiwa kutukuza sisi tunasema: Suala likija njia panda kati ya kulitumia tamko katika maana yake ya hakika au ya kinaya, sisi tutashikamana na maana ya asili, yaani kulitumia katika maana yake ya hakika.

Na hapa mahali petu tunapozungumzia ni kuwa matumizi ya neno yao kwa uhakika yarejea kwenye “Hao Mitume,” kati yao akiwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), kwa dalili ya kauli yake (s.w.t.) kabla ya Aya hii:

تِلْكَ آيَاتُ اللَّهِ نَتْلُوهَا عَلَيْكَ بِالْحَقِّ ۚ وَإِنَّكَ لَمِنَ الْمُرْسَلِينَ {252}

“Hizo ni Aya za Mwenyezi Mungu tunazokusomea kwa haki na kwa hakika wewe ni miongoni mwa Mitume.” (Surat Baqara: 252)

Halafu Muumba aliendeleza mtiririko wa usemi wake kwa kumwambia: “Hao Mitume tumewatukuza baadhi yao zaidi kuliko wengine.”

Kisha kwa kweli uwiano wa mienendo unajulishwa na riwaya nyingi zilizo mashuhuri na sahihi, waislamu wameafikiana kwazo. Mfano wa kauli yake (s.a.w.w): “Mtakuja kufuata mienendo ya waliokuwa kabla yenu…ndara kwa ndara kiasi kwamba hata kama wangeingia shimo la kenge mngeliingia.” Na kauli yake (s.a.w.w): “Msirejee kuwa makafiri baada yangu, baadhi yenu wakizipiga shingo za wengine.”

Na kama kauli yake: “Mayahudi wamefarakana na kufikia vikundi sabini na moja, na manaswara wamefarakana mpaka kufikia vikundi sabini na mbili na umma wangu utafarakana na kufikia vikundi sabini na tatu. Vikundi sabini na mbili motoni na kimoja kitaokoka.”

Bali hilo lajulishwa na Aya nyingi, kama kauli yake (s.w.t.): “Basi hawangoji ila mfano wa siku za watu waliopita kabla yao.” (Sura Yunus: 102) Na kama kauli yake (s.w.t.): Watu walikuwa kundi moja, basi Mwenyezi Mungu akawapelekea Manabii watoao habari njema na waonyao, na pamoja nao akateremsha Kitabu kwa haki, ili ahukumu baina ya watu katika yale waliyokhitilafiana. Wala hawakukhitilafiana katika hicho ila wale waliopewa baada ya kuwafikia dalili zilizo wazi, kwa sababu tu ya uasi kati yao. Hapo Mwenyezi Mungu akawaongoza walioamini kwa yale waliokhitilafiana katika haki kwa idhini Yake, na Mwenyezi Mungu humuongoza amtakaye kwenye njia iliyonyooka.” (Surat Al-Baqara: 213) Na kauli yake: ‘’Je watu wanadhani wataachwa waseme tumeamini, nao wasijaribiwe? Na bila shaka tuliwajaribu wale waliokuwa kabla yao, na kwa hakika Mwenyezi Mungu atawatambulisha wale waongo.” (Surat Ankabut: 2 3)

Kwa kweli dalili kubwa mno ya kuafikiana na mienendo ni tukio la maswahaba baada ya kutawafu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), kwa kuwa walikufurishana na kila mmoja alimfanya mwenzake kuwa ni fasiki na mpaka kufikia kuuwana wao kwa wao katika vita kali mno, kiasi kwamba waathirika wake ni zaidi ya waislamu mia moja elfu. Na hiki ni kigezo cha Aya: “Sivyo, hakika mwanadamu anaasi sana. Kwa kujiona ametosha.” (Surat Al-Alaq: 6-7)

Baada ya hivyo haiwezekani isemwe: Yawezekana vipi maswahaba wageuke hali ikiwa wao ndio waliojitolea muhanga mali zao na nafsi zao na waliwaua jamaa zao na walisimama pamwe na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) katika shida na raha na waliziona Aya zake na miujiza yake!!

Hujibiwa kuongezea yaliopita:

(a) Kwa kweli sentensi: “Mtarudi nyuma” wameelekezewa wao kwa dhati yao, kwa kuwa haikubaliki kiakili iwe wamekusudiwa makafiri au wanafiki hali wao kimsingi ni wenye kugeuka.

(b) Kwa hakika elimu haimuombei mwenye nayo anyooke. Wangapi wanajua kuwa haki iko ng’ambo ile lakini utashi wa nafsi ya mtu unamuamuru aelekee ng’ambo nyingine, naye huifuata. Bali kwa hakika aghlabu hali ya ukiukaji huja baada ya kuwa haki imejulikana. Allah anasema: “Na waliopewa kitabu hawakuhitilafiana ila baada ya elimu kuwajia, kwa sababu ya hasadi baina yao.” (Surat Aali Imran: 19). Na amesema: Wala hawakukhitilafiana katika hicho ila wale waliopewa baada ya kuwafikia dalili zilizo wazi, kwa sababu ya uasi kati yao” (Surat Al-Baqara: 213). Hivyo kila kitu ni wazi kwao, lakini wamekhtilafiana na wameuwana “Na kama Mwenyezi Mungu angelipenda, wasingelipigana waliokuja nyuma yao, baada ya kuwafikia dalili zilizo wazi wazi, lakini walikhitilafiana. (Surat Aali Imran: 253) Na amesema: ‘’Je umemuona yule aliyefanya tamaa yake kuwa Mungu wake, na Mwenyezi Mungu akampoteza licha ya elimu. (Sura Jathiya: 23)

Kwa kweli kujitolea muhanga na kuvumilia balaa hapo kabla hakumlindi mtu asipotee hapo baadaye. Kujitolea kwao muhanga na kuvumilia mabalaa sio kukubwa mno kuliko kujitolea muhanga na uvumilivu wa mabalaa ambako walimimniwa wana wa Israeli.
Firaun alipokuwa akiwakata miguu yao na mikono yao kwa tofauti walivuumilia, na aliwasulubu wakavumilia, aliwabakisha hai wanawake wao na watoto wao na kuwaua wanaume, walivumilia na walishikilia ulinganio wa Musa (a.s.) na waliona kwa namna ya wazi kabisa miuujiza ya Musa, na muujiza mkubwa mno ulikuwa kuatuka bahari pande mbili, kila upande mmoja ni sawa na mlima mkubwa sana.

Lakini Musa (a.s.) alipotengana nao tu wana wa Israil walimwabudia ndama. Hivyo hapo utaona kwamba tabia ya mwanadamu ni kukiuka anapohisi na kutambua kuwa anajitosha na kuhisi yuko katika amani:

كَلَّا إِنَّ الْإِنْسَانَ لَيَطْغَىٰ {6}

أَنْ رَآهُ اسْتَغْنَىٰ {7}

“Sivyo, hakika mwanadamu anaasi sana. Kwa kujiona ametosha.” (Surat Al-Alaq: 6 -7)

Mwanadamu japo apande daraja za imani namna gani akiwa si maasumu kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) uwezekano wa kugeuka na kukufuru upo. Na hakuna mfano mkubwa zaidi kuliko Balgham bin Baura:

وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ الَّذِي آتَيْنَاهُ آيَاتِنَا فَانْسَلَخَ مِنْهَا فَأَتْبَعَهُ الشَّيْطَانُ فَكَانَ مِنَ الْغَاوِينَ {175}

وَلَوْ شِئْنَا لَرَفَعْنَاهُ بِهَا وَلَٰكِنَّهُ أَخْلَدَ إِلَى الْأَرْضِ وَاتَّبَعَ هَوَاهُ ۚ فَمَثَلُهُ كَمَثَلِ الْكَلْبِ إِنْ تَحْمِلْ عَلَيْهِ يَلْهَثْ أَوْ تَتْرُكْهُ يَلْهَثْ ۚ ذَٰلِكَ مَثَلُ الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا ۚ فَاقْصُصِ الْقَصَصَ لَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ {176}

سَاءَ مَثَلًا الْقَوْمُ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَأَنْفُسَهُمْ كَانُوا يَظْلِمُونَ {177}

مَنْ يَهْدِ اللَّهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِي ۖ وَمَنْ يُضْلِلْ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ {178}

‘’Na wasomee habari za yule tuliyempa Aya zetu, kisha akajivuna nazo, na Shetani akamfuata na akawa miongoni mwa waliopotea. Na kama tungelitaka tungelimwinua kwazo hizo, lakini yeye akagandamana kwenye ardhi na kuyafuata matamanio yake. Basi hali yake ni kama hali ya mbwa, ukimpigia kelele anahema au ukimwacha anahema. Hivyo ndivyo hali ya watu waliozikadhibisha Aya zetu, basi simulia hadithi huenda watafikiri. Uovu ulioje wa mfano wa wanaozikidhibisha Aya zetu na wakajidhulumu nafsi zao. Mwenyezi Mungu atakayemuongoza basi yeye ndiye mwenye kuongoka na atakayempoteza basi hao ndio wenye khasara. (Surat A’araf: 175 - 178).

Je kuna Swahaba yeyote alifikia imani hii, kiasi chakuwa akibeba jina tukufu? Na alipotoka, basi hali itakuwaje kwa aliye daraja la chini yake?

Hapa swali ni: Kwenye jambo gani kugeuka na kurudi nyuma kulitimia? Bali kwa upande wetu tujiulize, kwenye jambo gani kwa kawaida mapinduzi hutimia?

Kwa kweli mbele yetu kuna chembechembe za mwanzo katika Aya, kupitia hizo tunaweza kufikia jibu kwa uchambuzi na kufikia natija:

Kwa hakika kugeuka kuna mafungamano ya moja kwa moja na kifo cha Mtume (s.a.w.w): “Basi je akifa au akiuliwa mtarudi nyuma kwa visigino vyenu?”

Kugeuka ni dalili ya kuwepo asili ambayo juu yake ugeukaji umeangukia, nayo ni asili maarufu kwa wenye kugeuka wote, na lau wageukaji wangekuwa hawaijui asili ile hawangeambiwa “Mtarudi nyuma kwa visigino vyenu?”

Na ambalo kwa ajili yake ugeukaji umefanyika, ndilo alikuwa amejiambatanisha nalo kwa muda mpaka ugeukaji ulipotokea.

Kwa hakika jambo hili lina mafungamano ya moja kwa moja na Allah (s.w.t.) na Mtume Wake (s.a.w.w), na ni dhidi yao wamegeuka.

Kwa kweli madhara ya ugeukaji huu yanawarejelea wageukaji duniani na akhera:

فَلَنْ يَضُرَّ اللَّهَ شَيْئًا ۗ{144}

“Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaoshukuru(Surat al-Imran: 144),

وَسَيَجْزِي اللَّهُ الشَّاكِرِينَ {144}

“Hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu” (Surat al-Imran: 144),

وَمَنْ يَشْكُرْ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ ۖ{12}

“Na atakayekushukuru basi kwa hakika atashukuru kwa ajili ya nafsi yake” (Surat Luqman: 12).

Halafu Mwenyezi Mungu amebainisha kuwa shukurani hii manufaa yake hurejeshwa kwa mja mwenyewe, pia hufahamika kutokana nayo kuwa kutoshukuru madhara yake yatarejea kwa mja mwenyewe.

Kwa hakika ugeukaji huu unaambatana na mienendo ya waliokuwa mwanzo, kwa hiyo kule walikogeukia wa mwanzo ndiko walikogeukia wa mwisho.

Mwenyezi Mungu hakusema atawalipa waumini na waislamu, bali amesema: “Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaoshukuru (Surat al-Imran: 144), jambo linalofahamisha kuwa wasiogeuka ni wachache mno, hiyo ni kulingana na usemi wake: “Na ni wachache wanaoshukuru katika waja wangu.” (Surat Sabaa: 13) na yatiliwa nguvu na kauli yake:

“Mtarudi nyuma” (Surat al-Imran: 144), ambayo yamaanisha jenasi na wingi, lau wageukaji wangekuwa wachache basi angesema: “Watarudi nyuma baadhi yenu” na haingekuwa sahihi kuwalaumu walio wengi.

Kwa hakika ugeukaji huu ni wa kweli na utatokea bila pingamizi, hilo ni kwa dalili ya jibu la sharti ambalo hufidisha kuthibiti pale tu sharti linapothibiti, na kule kutumia kitenzi cha wakati uliopita ambacho humaanisha kuthibiti bila kipingamizi.

Kwa kweli usemi ni khususan kwa waislamu na unawaelekea wao, wala hakuwakusudia makafiri kwa kuwa wao kimsingi wamekwishageuka tangu mwanzo, kama ambavyo hakuwakusudia wanafiki tu kwa kuwa hivyo ni kinyume na dhahiri ya Aya.

Lau angewakusudia kwa semesho tu angesema: “Mtadhihirisha ugeukaji wenu” bali dhati ya ugeukaji na kutokea kwake, itakuwa wakati wa kifo moja kwa moja.

Na ili kujua kiini cha ugeukaji huu wakati wa upembuzi na kutoa natija hapana budi kuchunga hizi chembechembe zote, na yatakiwa natija iafikiane nazo kiukamilifu, kama sivyo basi si zenyewe.

Kwa kweli Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alikuwa mtawala juu ya waislamu na baada ya kufa kwake ugeukaji ulitokea. Na ni zamu yetu tuulize:

Baada ya kufa mtawala kwa kawaida mageuzi hutokea katika nini? Ni maeneo gani ambayo Mtume (s.a.w.w) alikuwa anawakilisha amani halisi kwa ajili ya umma usihitilafiane, kiasi kwamba lau Mtume (s.a.w.w) hangekuwepo mzozo na tofauti hizi vingeibuka?

Na je Qur’ani imegusia hili? Je Qur’ani haikugusia kwa namna ya wazi jambo ambalo lilikuwa kubwa kwa watu ambalo walio wengi hawalikubali, na Mtume aliuhofia umma wake kuwafikishia jambo hili, lakini ilikuwa ni amri ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.):

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنْزِلَ إِلَيْكَ مِنْ رَبِّكَ ۖ وَإِنْ لَمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ ۚ وَاللَّهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ ۗ إِنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ {67}

“Ewe Mtume! fikisha uliloteremshiwa kutoka kwa Mola wako, na kama hukufanya, basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri. (Surat Maidah: 67).

Na kwa mtupo wa jicho la haraka na kwa muhtasari katika Aya tunagundua kuwa:

    1. 1 Kwa hakika jambo hili ambalo ni wajibu kulifanyia tabligh linalingana na kuifanyia tablighi Risala, na ikiwa hakulifikisha inakuwa kana kwamba hakuifikisha Risala yote kwa ujumla wake, kufuatia hali hiyo kulikana jambo hili ni kuikana Risala na kugeuka dhidi yake ni kugeuka dhidi ya Risala.

    2. 2 Kwa kweli jambo hili ni mahali pa chimbuko la tofauti kubwa kati ya watu, bali Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) alijihofia binafsi kuwahofu watu, ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimpa matumaini kuwa asihofu atakuwa katika amani: “Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu.” (Surat Maidah: 67).

    3. Jambo hili ni Risala kamili kwa kuwa ufahamu wa Aya ni kuwa akilifikisha jambo hili atakuwa ameifikisha Risala na ameikamilisha:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ{3}

‘’Leo nimewakamilishieni dini yenu na kuwatimizieni neema yangu, na nimeridhia kwenu Uislamu uwe dini yenu. (Surat Maida: 3)

Na hii yalingana na Aya inayozungumzia kugeuka na kurudi nyuma, ambayo inafahamisha kuwa ni kugeuka na kurudi nyuma dhidi ya dini hii yote.

    4. “Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. (Sura Maidah: 67) walio wengi miongoni mwa watu wanalichukia jambo hili ambalo Mtume aliamrishwa kulifikisha. Ni jambo gani hili ambalo anataka kulifikisha? Kwa kweli jambo hili kwanza laambatana na mgeuko, hiyo ni kwa kuwa:

Kwa sababu jambo hili linaambatana na Risala na kuligeuka ni kuigeuka Risala. Ndani ya jambo hili kuna alama za watu kugeuka kwa sababu ya kutoliridhia walio wengi.

Ilimbidi Mtume (s.a.w.w.) alifikishe kwa sababu ya kukaribia muda wa kufariki kwake: “Kwa hakika mimi niko mbioni kuitwa na itabidi nijibu” ili asiwaachie linalohalalisha kugeuka, na asimamishe hoja kamili dhidi yao, kwa kuwa kugeuka kwaambatana na kufariki kwa Mtume (s.a.w.w).

Kwa hakika jambo ambalo anataka kulifikisha ni kitu pekee ambacho yawezekana kukigeuka, kwa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alifikisha Risala yote na matawi yake mbalimbali, wala haikujitokeza katika mojawapo ya matawi yake kwa waislamu alama ya kutoiridhia isipokuwa jambo hili ambalo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alilihofia na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akamwahidi kumhifadhi ili watu wasimdhuru.

Kwa hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alikuwa katika jambo hili ni mfano wa amani halisi, akifa amani italegalega na watu watafanya kinyume chake.

Hivyo basi hakuna kitu kilichobaki ambacho kitakabiliwa na mageuzi ila ukhalifa ulioainishwa na Mwenyezi Mungu.

Ni Nani Ambaye Mtume Wa Allah (S.A.W.W.) Alitoa Habari Za Ukhalifa Wake?:

Habari zimefululiza na mamia ya rejea za waislamu zimenakili tukio la Ghadir na kuainishwa kwa Imamu Ali (a.s.) kuwa Khalifa wa waislamu kama yalivyotangulia maelezo yake.

Kutokana na hizi na habari nyinginezo miongoni mwa maelfu ya Hadithi inakuwa wazi kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alimwainisha Ali kuwa ndiye Khalifa na Imamu kwa viumbe, lakini jambo hili halikuwaridhisha baadhi ya waislamu, kwa hiyo hakutoweka Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) katika dunia hii ila walimgeuka na walimpora haki yake, na hawakubaki thabiti kwake kati yao ila wachache kama alivyosema (s.w.t.) mwishoni mwa Aya ya mageuzi:

وَسَيَجْزِي اللَّهُ الشَّاكِرِينَ {144}

“Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaoshukuru(Sura al- Imran: 144).

Hivyo kutokana na hayo inakuwa wazi kuwa:

Kwanza: Hao ni wachache, kwa dalili: (a) Tamko: Mtageuka, ambalo linamaanisha ueneaji na wingi. (b) “Na ni wachache wanaoshukuru katika waja wangu.”

Pili: Shukrani hii ni mkabala wa kufuru nayo ni kule kugeuka: “Miongoni mwao kuna aliyeamini na miongoni mwao kuna aliyekufuru” “Kwa hakika sisi tumemuongoza njia ima awe mwenye kushukuru au kukufuru.” Na njia hii ni maarufu kwa dalili: (a) Uongozi wake kwenye njia hii: “Kwa hakika sisi tumemuongoza njia.” (b) Kugeuka, kwa kuwa Aya iliyotangulia yasema:

Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaoshukuru, yaani ambao walifuata njia, kulingana na inavyoeleweka Aya hii. Na wasiokuwa wao ni makafiri kwa kuwa wao wameikengeuka njia. Njia hii wakati huo huo ni mahali pa balaa na neema. Balaa watu watapatwa nalo na neema kwa mwenye kuifuata, na kwa ambaye anashukuru ni neema.

Na kwa kawaida kugeuka ambako kunalingana na kufuru ni kugeuka dhidi ya neema, yaani kuikufuru. Na maadamu uwalii wa Ali ni neema: ‘’Leo nimewakamilishieni dini yenu na kuwatimizieni neema yangu” mageuzi yalitokea dhidi yake wala hawakusalimika na hilo ila wachache.

Linalotilia nguvu hilo ni Hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) aliposema: “Hali nikiwa nimesimama punde si punde kikundi kitapita, nitakapowatambua mtu mmoja atatoka kati yetu na wao na kusema: ‘Njooni.’ Nitasema: Wapi? Atasema: ‘Motoni wallahi.’ Nitasema: Wana nini? Atasema: ‘Kwa kweli wao wameritadi baada yako na kurudi kinyumenyume walikokuwa, sioni atakayeokoka miongoni mwao ila mfano wa ngamia wasio na mchunga.’”

Kwa hiyo Hadithi hii inatilia nguvu ambalo limejulishwa na Aya ya kugeuka, kuwa wachache watakuwa wenye kushukuru neema. Na akasema (s.a.w.w): “Sioni watakaookoka kati yao ila mfano wa ngamia wasio na mchunga.” Hivyo basi kama ambavyo ngamia waliokimbia kujitoa kwenye kundi huwa idadi yao ni ndogo, hali ni hiyo kwa Swahaba, wenye kuokoka miongoni mwao ni wachache mno.

Na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Mimi ni mtangulizi wenu kwenye Hodhi, mwenye kunipitia atakunywa na mwenye kunywa hatopatwa na kiu abadan. Kwa kweli nitajiwa na kaumu ya watu nawatambua na wananitambua, halafu patazuiliwa kati yangu na wao, hapo nitakuwa ninasema: Swahaba zangu! Patasemwa: Kwa kweli wewe huyajui waliyozusha baada yako! Nitakuwa ninasema: Wawe mbali wenye kubadilisha baada yangu.’’

Na kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alipomjibu Abu Bakr pindi Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa akitoa ushuhuda kwa mashahidi wenye imani na Pepo, akasema: “Amma wale, kwa kweli mimi nawatolea ushahidi.” Abu Bakr akasema: “Na sisi je ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Akasema (s.a.w.w): ‘’Ama ninyi sijui mtakayoyazusha baada yangu.’’ (Al-Muwatau, Jz. 1, uk. 307, Imam Malik. Na al-Maghazi ya Waaqid, uk. 310.)

 • 1. Ni mzunguko, sawa na kitandawili cha kuku na yai, yaani hapana kuku ila atokane na yai, na hapana yai ila litokane na kuku, hivyo mzunguko utaendelea bila ya mwisho, ndio maana inazingatiwa kuwa mzunguko ni batili.
 • 2. Anamkusudia Ali bin Abu Talib (a.s.).
 • 3. Pia ikumbukwe kuwa Umar bin al-Khattab alipopata habari ya kifo cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alirukwa na fahamu kwa huzuni, kama inavyodaiwa na masunni, na alifikia kudai eti Mtume (s.a.w.w) hajafa…
 • 4. Sharhu Nahjul-Balagha cha Ibn Abil-Hadid Jalada la 2. Uk. 2 .
 • 5. Yaani kwa ajili ya Abu Bakr, ili nawe baadaye upate hisa kutokana na utawala wake.
 • 6. Sharhu Nahjul-Balagha cha Ibn Abil-Hadid Jalada la 2, Uk. 2 – 5.
 • 7. Al-Imama was-Siyasa, cha Ibnu Qutaybah Juz.1, Uk. 14. Tarikhul-Yaqubi Juz.2, Uk. 1224 – 125.
 • 8. Tarikhul-Yaqubi Juz. 2, Uk. 124.
 • 9. Musnad Ahmad Juz.1, Uk. 55. Tabariy Juz. 2, Uk. 466. Ibnul-Athiyr Juz. 2, Uk.124. Ibnu Kathir Juz. 5, uk. 246.
 • 10. al-Iqdu Al-Farid cha Ibnu Abdi Rabih Juz. 3, Uk. 64. Na Abul-Fidai Juz.1, Uk. 156.
 • 11. Ansabul-Ashraf. Juz.1, Uk. 586. Kanzul-Ummal, Juz. 3, Uk. 140. Riyadhun- Nadhra Juz. 1, Uk. 167.
 • 12. Tarikhul-Yaqubi Juz. 2, Uk. 126.
 • 13. Sharhu Nahjul-Balagha cha Ibn Abil-Hadid Jalada la 1, Uk. 143. Juz. 2, Uk. 2-5.
 • 14. Bukhariy Juz. 5. Uk.177, Juz. 4.Uk.96.
 • 15. Al-Imama was-Siyasa, cha Ibnu Qutaybah Juz.1, Uk. 25.
 • 16. Tabariy Juz. 2, Uk. 619. Murujud-Dhahabi Juz.1, Uk. 414. Iqdul-Faridu Juz. 3, Uk. 69. Kanzul-Ummal Juz. 3, Uk.135. Imama was-Siyasa Juz. 1, Uk. 18. Na Tarikhud-Dhahabiy Juz. 1, Uk. 388.
 • 17. Tarikhul-Yaqubi Juz.2, Uk. 115.
 • 18. Diwanu ya Hafidh Ibrahim, chapa ya Misri.
 • 19. Al-Imama was-Siyasa, cha Ibnu Qutaybah Juz.1, Uk. 19.
 • 20. Al-Imama was-Siyasa, cha Ibnu Qutaybah Juz.1, Uk. 19.
 • 21. Yaani alitilia manani umma usifarakane hali ikiwa maadui wamezunguka wakingoja hali ya mambo, kama alivyotilia manani Harun Bani Israil wasi- farakane: “Kwa hakika mimi niliogopa usije kusema: Umewafarikisha wana wa Israel na hukungojea kauli yangu”. (Surat-Taha: 94.)
 • 22. Munadharatu Fil-Imamati. Al-Manaqib cha Ibn Shahri Ash’wan. Juz. 1, uk. 270.