read

Mlango Wa Tano

Uwalii Wa Ali (A.S.) Katika Qur’ani

Uchambuzi Fafanuzi:

Baada ya kuwa nimemaliza utafiti wa kwanza ambao ulinigharimu juhudi ya kifikra na ya kinafsi, na ulinifanya niishi maisha ya mapambano na nafsi yangu na mapambano mengine na wezangu na maustadhi wangu katika chuo kikuu, nilifikia kukinai kabisa kiasi cha kutotilia mashaka kuhusu jua na wala silitilii mashaka, na matokeo yake ilikuwa kama nilivyokwishafafanua, nayo ni wajibu wa kuwafuata Ahlul-Bayt (a.s.) na kuichukua dini kutoka kwao. Na huku kulikuwa ndio kukinai kwangu kwa mara ya kwanza kwa kiasi fulani cha wakati, hata hivyo nilikuwa sijaweza kuainisha msimamo na kuchagua madhehebu yangu japokuwa moyo wangu ulikuwa unanishinikiza nifuate madhehebu ya Shia, ingawaje marafiki zangu na ahali zangu na wezangu walikuwa wananiweka kwenye kundi la Shia na wengi miongoni mwao walikuwa wakiniita Shia na wengine wakiniita Khomeiniy!

Na mimi nilikuwa bado sijaainisha msimamo wangu. Nilikuwa sina shaka na nilipofikia, lakini nafsi yangu ile iamrishayo uovu ndio inayonikataza na kunipa wasiwasi: Vipi waiacha dini uliowakuta nayo baba zako?! Utafanya nini na jamii hii ambayo iko mbali na itikadi yako?! Wewe ni nani hata ufikie kwenye jambo hili?! Je wanavyuoni wakubwa wameghafilika na hilo?! Bali waislamu walio wengi pia?!

Na maelfu ya maswali ya kutilia shaka ambayo aghlabu yalikuwa yananishinda nguvu na kuninyamazisha! Na wakati mwingine yakitikisa akili yangu na dhamiri yangu, ni kama hivyo vuta nikuvute, na msongamano wa misuli na kuvunjika moyo wangu, hakuna kimbilio wala la kuliwazika nalo, wala rafiki wala mpenzi. Basi nilianza kuuliza na kutafuta vitabu ambavyo vimewapinga Shia labda vitaniokoa kutoka katika hali nilionayo na viniwekee ukweli wazi, pengine umejificha mbali na mimi. Na uwahabi ulinitosheleza jukumu la kuvikusanya, kwa kuwa imamu wa msikiti uliokuwa karibu yetu alikuwa ananiletea kila kitabu nimuombacho.

Na baada ya kuvichunguza, tatizo langu lilizidi na msongamano wa hali ya mambo ulinizidia na wala sikupata humo vitabuni utashi wangu, kwa sababu vilikuwa havina nilichokuwa nakitaka wala havikuwa na mjadala wa kimantiki, na yote yaliyomo humo ni, matusi, laana, shutuma, masingizio na uwongo. Ilinifanyia kizuizi kwa mara ya kwanza, lakini baada ya kuiondoa nafsi yangu mbali na taathira hizi za mtandao wa habari, ilinibainikia mbele yangu kuwa ni dhaifu mno kuliko utando wa buibui. Baada ya hapo niliazimia kuendelea na uchambuzi, japokuwa nilikinaishwa na kiwango nilichofikia katika uchambuzi wa mwanzo, lakini niliukabili ushawishi wa nafsi yangu na nikajiangazia ili kuona ukweli umedhihiri kwa mwanga kikamilifu. Hivyo chaguo langu liliangukia kuchambua dalili za uwalii ya Imam Ali (a.s.) na zinazoeleza wazi uimamu wake, na akilini mwangu mlikuwa na jumla ya dalili zinazofikisha kwenye lengo hili japokuwa zenyewe zinatosha kwa mwenye kuwa na akili iliyo safi na moyo ulio salama. Lakini nilitaka uwe uchambuzi tenganishi kati ya ima niwe Suni naamini ukhalifa wa Abu Bakr, Umar na Uthman au niwe Shia ninayeamini kuwa uimamu ni wa Ali (a.s.).

Na baada ya uchambuzi ilikuwa shitukizo! Kwa kuwa sikuweza, na mpaka hivi sasa sijaweza kukusanya, kudhibiti na kufuatilia dalili zote, sawa ziwe dalili za nukuu au za kiakili, ambazo zinasema wazi kabisa uimamu wa Amirul-Muuminin (a.s.). Baadhi ya dalili ni dhahiri na baadhi yake zinahitaji tangulizi ndefu ndefu.

Na ambalo nalisajili katika mlango huu ni dondoo ndogo, hiyo ni kwa ajili ya kuchunga muhtasari na kumpa shauku mchambuzi, na kulingana na itikadi yangu ni kwamba katika hizo zatosha baada ya kusherehesha na kufafanua. Na zifuatazo ni baadhi ya dalili hizo:

1. Kauli ya Mwenyezi Mungu:

إِنَّمَا وَلِيُّكُمُ اللَّهُ وَرَسُولُهُ وَالَّذِينَ آمَنُوا الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُمْ رَاكِعُونَ {55}

“Hakika kiongozi wenu hasa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walioamini ambao husimamisha swala na hutoa zaka na hali ya kuwa wamerukuu.” (Surat al-Maidah: 55).

Hoja Ya Dalili Katika Aya Hii:

Aya hii inakuwa wazi katika uwalii wa Amirul-Mu’minin na uimamu wake ikiwa itathibiti kuwa mradi wa kauli yake (s.w.t.): “ambao husimamisha swala na hutoa zaka na hali ya kuwa wamerukuu.” kuwa ni Imam Ali (a.s.). Na ikiwa itathibiti pia kuwa neno Walii maana yake ni anayefaa kutoa maamuzi.

Vyanzo Ambavyo Vimethibitisha Kuwa Aya Imeshuka Kwa Ajili Ya Ali (A.S.):

Dalili zimethibiti na riwaya zimefululiza kutoka pande mbili zote - Suni na Shia - kuwa Aya hii ilimteremkia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kumhusu Ali (a.s.) alipoitoa Zaka pete, yaani sadaka naye akiwa katika hali ya rukuu. Na habari hizi zimeelezwa na kundi la maswahaba miongoni mwao:

1. Abu Dharr al-Ghafaariy: Na kutoka kwake kundi la wanahadithi waliieleza riwaya hii, mfano:

• Abu Is’haqa Ahmad bin Ibrahim Tha’alabiy katika tafsir al-Kashfu Wal-bayan Ant-
Tafsiril-Qur’ani.

• Al-Hafidh al-Kabiir al-Hakim al-Haskaniy katika kitabu Shawahidut- Tanziil, Juz.1,
Uk.177. Chapa ya Beirut

• Sibt Ibnu Al-Jauziy katika kitabu Tadhkirah. Uk.18.

• Al-Hafidh Ibnu Hajar al-Asqalaniy katika Al-Kafu Al-Shafu Uk. 56. Na wengine miongoni
mwa wanahadithi na mahafidhi.

2. Al-Miqdad bin Al-Aswad: Na kutoka kwake ameiandika Al-Hafidh Al- Haskaaniy katika kitabu Shawahidut-Tanziil Juz.1, Uk. 171. Chapa ya Beirut, uhakiki wa Mahmudiy.

3. Abu Raafii Al-Qibtiy, huria wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w): Kutoka kwake wameandika kundi la waliokuwa mashuhuri mfano wa:

• Al- Hafidh Ibnu Mardawayhi katika kitabu al-Fadhailu.

• Jalalu Diin Suyutiy katika kitabu Durul-Manthur Juz.2, Uk. 293.

• Al-Muhadith al-Mutaqiy al-Hindiy katika kitabu Kanzul-Ummal Juz.1, Uk. 305…na
wengine.

4. Ammar bin Yaasir: Na riwaya zake zimeandikwa na:

• Al-Muhadithu al-Kabiir al-Tabraniy katika kitabu Muujamul-Ausat.

• Al-Hafidh Abu Bakar bin Mardawayhi katika kitabu Fadhail.

• Al-Hafidh al-Hakim al-Haskaaniy katika kitabu Shawahidut-Tanziil.

• Al-Hafidh bin Hajar al-Asqalaniy katika kitabu Al-Kafu Al-Shafu Uk. 56, kutoka kwa
Tabraniy na Ibnu Mardawayhi.

5. Amirul-Mu’minin Ali bin Abu Talib (a.s.): Na riwaya zake zimeandikwa na:

• Al-Haakim an-Nisaburiy, al-Hafidh Al-Kabiir katika kitabu Maarifatu Ulumil-Hadith Uk.
102. Chapa ya Misri 1937.

• Al-Faqiihu Ibnu Al-Maghaziliy as-Shaafiy katika kitabu al-Manaqib Uk. 311.

• Al-Hafidh al-Khawarizamiy katika al-Manaqib Uk.187.

• Al-Hafidh Ibnu Asaakir ad-Damashqiy katika kitabu Tarikhud-Damashq Juz. 2, Uk. 409.
Uhakiki wa al- Mahmudiy.

• Ibnu Kathir ad-Damashqiy katika kitabu al-Bidayat Wan-Nihayati Juz. 7, Uk. 357. Chapa
ya Beirut.

• Al-Hafidh bin Hajar al-Asqalaniy katika kitabu Al-Kafu Al-Shafu Fi Takhriiji Ahadithil-
Kaafi
, Uk. 56. Chapa ya Misr.

• Al-Muhadithu Mutaqiy al-Hindiy katika kitabu Kanzul-Ummal Juz.15, Uk. 146, katika
mlango wa fadhila za Ali (as).

6. Amru Ibnu Al-Aswi: Ameiandika toka kwake al-Hafidh Akhtab Khawarzami Al-Hafidh Abul-Muayid katika kitabu Al-Manaaqib Uk.129.

7. Abdullah bin Salaam: Ameiandika kutoka kwake Muhibudin Tabariy katika kitabu Dhakhairul-Uqba Uk.102, na katika Riyadhun-Nadhrah Juz. 2, Uk. 227.

8. Abdullah bin Abbas: Na wameiandika kutoka kwake:

• Ahmad bin Yahya al-Baladhuriy katika kitabu Ansabul-Ashrafu Juz. 2, Uk. 150. Chapa
ya Beirut. Uhakiki wa Mahmudiy.

• Al-Waahidiy katika kitabu Asbabun-Nuzul Uk. 192 chapa ya kwanza, mwaka 1389.
Uhakiki wa Sayyid Ahmad Swamad.

• Al-Haakimu al-Haskaaniy katika kitabu Shawahidut-Tanzil Juz.1, Uk. 18. Ibnu Al-
Maghaziliy as-Shaafiiy katika kitabu Al-Manaqib Uk. 314. Uhakiki wa Mahmudiy.

• Al-Haafidhu Ibn Hajar al-Asqalaniy katika kitabu Al-Kafu Al-Shafu Fi Takhriiji
Ahadithil-Kaafi. Chapa ya Misri. Jalalud-Din Suyutiy.

9. Jabir bin Abdullah al-Answariy: Na miongoni mwa walioiandika kutoka kwake ni al-Haakimu al-Haskaniy katika kitabu Shawahidut-Tanzil Juz.1, Uk.174.

10. Anas bin Malik – mtumishi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu - na ameiandika riwaya hiyo:

• Al-Hafidh al-Haskaaniy katika kitabu Shawahidut-Tanzil Juz.1, Uk.145.

• Al-Muhadith al-Kabiir al-Hamuwiy al-Juwayniy al-Khurasaniy katika kitabu
Faraidus-Samtiniy Juz.1, Uk.187.

Na tunachagua kutoka katika riwaya hizi nyingi ile aliyoieleza Abu Dharr al-Ghafaariy (r.a) katika riwaya ndefu aliyoiandika al-Haakim al-Haskaaniy kwa sanadi yake Uk. 177, Juz. 1. Chapa ya Beirut.

Amesema Abu Dharr al-Ghafaariy: “Enyi watu, anijuaye atakuwa amenijua hasa, na asiyenijua basi mimi ni Jundubu bin Janada al-Badriyu Abu Dharr al-Ghafaariy. Nilimsikia Nabii (s.a.w.w) kwa haya mawili vinginevyo yawe kiziwi, na nilimwona kwa haya mawili vinginevyo yapofoke, naye akisema: ‘Ali ni kiongozi wa watu wema na mwenye kuwauwa makafiri. Hupata nusra mwenye kumnusuru na hutelekezwa mwenye kumtelekeza.’ Ama mimi siku moja katika jumla ya siku niliswali na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) swala ya Dhuhuri, mwombaji aliomba msikitini, hakupewa kitu na yoyote. Yule mwombaji aliinua mkono wake kuelekeza mbinguni na akasema: ‘Ewe Allah shuhudia kuwa mimi nimeomba ndani ya msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na mtu hakunipa kitu.’ Na Ali (a.s.) alikuwa akirukuu, alifanya ishara kwa kidole chake cha mkono wa kulia na alikuwa amevaa pete, yule muombaji alikuja na kuichukua pete kutoka katika kidole hicho, na hiyo ilikuwa mbele ya macho ya Nabii (s.a.w.w). Pindi Nabii alipomaliza Swala yake, alinyanyua kichwa chake kuelekea mbinguni na akasema:

“Oh Mungu wangu kwa kweli ndugu yangu Musa alikuomba, akasema Mola wangu nikunjulie kifua changu na nirahisishiye mambo yangu, na niondolee fundo toka ulimini mwangu, ili wafahamu usemi wangu, na nijaaliye waziri – msaidizi – kutoka ahali wangu Harun ndugu yangu, kwa yeye kiimarishe kiuno changu, mshirikishe katika jambo langu.’ Ulimteremshia Qur’ani yenye kutamka: ‘Tutaimarisha kiuno chako kwa ndugu yako.’ Oh Mungu wangu, na mimi ni Muhammad Nabii wako na mwandani wako.

Oh Allah nikunjulie kifua changu, na nirahisishiye jambo langu, na nijaalie waziri kutoka ahali wangu Ali ndugu yangu, kwa yeye imarisha kiuno changu.’ Alisema: ‘Wallahi Mtume wa Mwenyezi Mungu hakukamilisha maneno, Jibril (a.s.) alishuka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na akasema: ‘Ewe Muhammad hongera ulilopewa kumhusu ndugu yako.’ Alisema (s.a.w.w): ‘Ewe Jibril ni nini?’ Jibril Akasema: ‘Mwenyezi Mungu ameamuru umma wako kumpenda mpaka siku ya Kiyama. Na amekuteremshia: “Hakika kiongozi wenu hasa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walioamini ambao husimamisha swala na hutoa zaka na hali ya kuwa wamerukuu.’”

Na riwaya hii imekuja kwa matamshi mengi tofauti, hapa tunafupisha kwa kutosheka na hii kwa kuwa inatosha kubainisha kusudio. Na hii ni miongoni mwa fadhila ambazo Amirul-Mu’minin hakushirikiana na yoyote, hatujamkuta yoyote katika historia amedai kutoa zaka akiwa katika rukuu. Na katika hili ni hoja tosha na dalili ya wazi kuwa Amirul- Mu’minin ndiye aliyelengwa wala si mwingine.

Na huenda baadhi ya watu wakajaribu kuitilia shaka Aya hii kunasibika kwake na Amirul-Mu’minin wakiwa na visingizio vya hoja tupu isiyo na maana yoyote. Hivyo utamuona Alusi anaitoa maana ya rukuu mbali na maana yake ya dhahiri, na anasema: “Makusudio ya rukuu ni unyenyekevu.” Hii ni taawili ya maana ya rukuu isiyokubalika, kwa kuwa hakuna ishara inayoondoa maana yake ya hakika na ya dhahiri katika Aya, nayo ni rukuu yenye harakati zake zilizozoeleka.

Hilo lilinitokea siku moja hali nikiwa najadiliana na kundi katika wezangu chuoni khususan kuihusu Aya hii, baada ya kuwathibitishia kuwa iliteremka kumhusu Amirul-Mu’minin Ali (a.s.), mmoja wao aliingiwa na mashaka akasema: “Ukiithibitisha kuteremka kwake kumhusu Ali basi itakuwa umemthibitishia dosari.”

Nikamuuliza vipi?

Akasema: ‘’Hilo lajulisha kuwa hakuwa na unyenyekevu katika Swala, kwani alimsikiaje muombaji na alimjibu vipi? Na yajulikana kuwa wachapa ibada na wachamungu huwa hawahisi kitu kuhusiana na waliowazunguka wakiwa katika hali ya kumuelekea Mwenyezi Mungu.”

Nikasema: ‘’Maneno yako sio sawa, kwa dalili ya Aya yenyewe. Kwa kuwa Swala ni ya Mwenyezi Mungu na unyenyekevu ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametupa habari ya kukubaliwa kwa Swala hii, bali kwa swala hiyo hiyo amethibitisha uimamu na wilaya ya mwenye Swala hiyo. Na mahali pa sifa ni wazi katika muktadha, hiyo ni sawa awe mtoa sadaka ni Ali (a.s.) au mtu mwingine hali iko sawa, kama utakuwa na shaka juu ya unyenyekevu wa Ali itakuwa bora shaka yako iwe juu ya Qur’ani. Na kwa kweli Aya hii iko katika hali ya uthabiti mno si kiasi cha kutiliwa shaka na wenye shaka. Aya iko na dalili ya wazi kabisa kuhusu wilaya ya Amirul-Mu’minin, ikiwa yajulikana kuwa kuithibitisha wilaya kwa Amirul-Mu’minin katika Qur’ani ni miongoni mwa mambo yaliyo wazi mno.”

Na nilipokuwa nawaambia maneno haya baadhi ya marafiki zangu, mmoja wao aliinua sauti na akasema: ‘’Tutajie Aya inayobainisha madai yako.’’

Nikasema: “Kabla ya hivyo tuone Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) amesema nini kumhusu Ali (a.s.). Bukhari ameeleza katika Sahih yake kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alimwambia Ali: “Wewe kwangu una daraja aliyokuwa nayo Haruna kwa Musa, isipokuwa tu hapana Nabii baada yangu.’’1 Kutokana na hali hiyo imedhihiri kuwa kila ambalo Harun alikuwa nalo analo Ali (a.s.), kwa hiyo yeye ana uimamu na ukhalifa na uwaziri na mengine ila unabii ambao Harun alikuwa nao.

Wote walipinga: ‘’Umetoa wapi hayo?!’’ Niliwaambia polepole nini nafasi ya Harun kwa Musa? Je Musa hakusema:

وَاجْعَلْ لِي وَزِيرًا مِنْ أَهْلِي {29}

هَارُونَ أَخِي {30}

اشْدُدْ بِهِ أَزْرِي {31}

وَأَشْرِكْهُ فِي أَمْرِي {32}

“Na uniwekee waziri katika jamaa zangu. Ndugu yangu Harun. Nitie nguvu kupitia yeye. Na umshirikishe katika kazi yangu.” (Surat- Twaha: 29-32)

Wakasema: ‘’Hatujasikia hilo labda Aya haipo katika njia hii…!” Hapo nilitambua chuki na utayarifu wa mjadala kutoka kwao. Nilisema hali nikiwa nimeshangazwa na mambo yao: “Kwa kweli jambo hili ni wazi halijakanushwa na yoyote.’’ Mmoja wao akasema: “Mzozo wa nini na Qur’ani hii mbele yako tutolee Aya ikiwa wewe ni mkweli!!” Hapo hali yangu ilitetereka kwa kuwa mimi nilikuwa nimesahau kabisa kabisa Sura gani juzuu gani, na punde hivi nilipata ushujaa nilisema nafsini mwangu: “Allahuma swali ala Muhammadin wa Aali Muhammad” Na nilifungua msahafu bila ya lengo, basi kwa mara ya kwanza jicho langu lilitua kwenye Aya hii:

قَالَ رَبِّ اشْرَحْ لِي صَدْرِي {25}

وَيَسِّرْ لِي أَمْرِي {26}

وَاحْلُلْ عُقْدَةً مِنْ لِسَانِي {27}

يَفْقَهُوا قَوْلِي {28}

وَاجْعَلْ لِي وَزِيرًا مِنْ أَهْلِي {29}

هَارُونَ أَخِي {30}

اشْدُدْ بِهِ أَزْرِي {31}

وَأَشْرِكْهُ فِي أَمْرِي {32}

“Akasema: Ee Mola wangu! Nipanulie kifua changu. Na unifanyie wepesi kazi yangu. Na ufungue fundo katika ulimi wangu. Wapate kufahamu kauli yangu. Na uniwekee waziri katika jamaa zangu. Ndugu yangu Harun. Nitie nguvu kupitia yeye. Na umshirikishe katika kazi yangu.” (Sura Twaha: 25 32)

Zingatio lilinibana na machozi yalinitiririka mashavuni mwangu, nilishindwa kuisoma Aya kwa kukithiri mshangao, niliwakabidhi msahafu ukiwa umefunguliwa na niliwaonyesha Aya, wote walishangazwa kwa mfadhaiko wa ghafla.

Aya: “Hakika Kiongozi Wenu Hasa…..” Ni Dalili Ya Uongozi Wa Amirul- Mu’minin:

Na baada ya kuthibiti katika utafiti wa kwanza kuwa Aya iliteremka kwa ajili ya Imam Ali (a.s.), hivyo maana yake inakuwa: “Hakika kiongozi wenu hasa ni Mwenyezi Mungu, Mtume wake na Ali bin Abu Talib.” Wala mtu yeyote hawezi kuingiwa na mashaka kuwa vipi Mwenyezi Mungu swt. alimsemesha mtu mmoja kwa nafsi ya wingi? Kwa kuwa hilo ni jambo linaloruhusiwa katika lugha ya Kiarabu, hivyo basi inakuwa nafsi ya wingi hapa ni ishara ya heshima, na ushuhuda juu ya hilo ni nyingi. Mfano wa kauli yake Taala “Ambao wakasema kwa kweli Mwenyezi Mungu ni fakiri na sisi ni matajiri. na msemaji alikuwa Hayyun bin Akhtab. Na ni kama kauli yake Taala: “Na miongoni mwao kuna ambao wanamuudhi Nabii na wanasema yeye ni udhunun Na Aya hii iliteremka kuhusu mtu mmoja miongoni mwa wanaafiki, ima kumhusu Julasu bin Sayuli au Nabtal bin al-Harth au Utaabu bin Qashiirah. Rejea Tafsirut-Tabariy Juz. 8 Uk. 198.

Na baada ya hivyo utafiti unabainisha maana ya neno walii lililotumika katika Aya husika. Shia wanashikilia kuwa walii katika Aya hii maana yake ni mwenye mamlaka ya kufanya jambo. Kwa hiyo utasema: Mwenye mamlaka juu ya mambo ya waislam au mwenye mamlaka ya mambo ya Sultan, ambaye mwenye haki ya kufanya mambo yao. Kwa ajili hiyo Shia wanasema: Ni wajibu kumfuata Amirul-Mu’minin (a.s.) kwa kuwa yeye ni mwenye haki ya kusimamia mambo ya waislam.
Na linalojulisha wajibu huo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekataza sisi kuwa na walii ambaye sio yeye (s.w.t.), na asiye kuwa Mtume wake na asiyekuwa walioamini ambao husimamisha swala na hutoa zaka na hali ya kuwa wamerukuu.

Hiyo ni kwa mujibu wa tamko la (innama) linalomaanisha: Mawalii wenu ni hawa tu. Yaani mawalii wenu ni hawa tu: Mwenyezi Mungu (s.w.t.), Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na ambao wanadumisha swala na wanatoa Zaka wakiwa rukuu. Hivyo basi lau ingekuwa makusudio ni uwalii wa upendo katika dini, haungekuwa mahususi kwa waliotajwa, kwa sababu upendo katika dini ni wa waumini wote. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema: Waumini wa kiume na waumini wa kike ni mawalii wao kwa wao.” kwa hiyo kuleta umahsusi kwajulisha kuwa aina ya uwalii huu ni tofauti na uwalii wa waumini wao kwa wao. Wala mradi wa “walioamini ambao husimamisha swala na hutoa zaka na hali ya kuwa wamerukuu” haujumuishi wote, yaani kwa kila aliye muumini, bali unakuwa mahsusi kwa Ali (a.s.), hiyo ni kwa dalili ya neno (Inna ma) ambalo lafidisha umahsusi, kwa hiyo inalitoa nje kundi la waumini.

Hiyo ni achia mbali Hadithi za hapo mwanzo zilizoeleza kuwa Aya inamhusu Ali bin Abu Talib (a.s.). Na kuwa sifa iliyokuja humo katika Aya (hutoa zaka na hali ya kuwa wamerukuu) haikuwa na uiano na yoyote na wala hakudai mtu yoyote asiyekuwa Amirul-Mu’minina (a.s.), kwa kuwa yeye ndiye aliyetoa zaka akiwa katika rukuu, kwa kuwa hali ya wenye kurukuu ni hali ya wenye kutoa zaka, na rukuu ni harakati mahsusi, hivyo kuiondoa rukuu mbali na maana yake hii ya kweli inakuwa ni aina ya tafsiri isiyokuwa na dalili, kwa kuwa katika Aya hakuna ishara inayoiondoa rukuu mbali na maana yake ya kweli. Kama ilivyo “hali ya kuwa wamerukuu” haijuzu kuiunga na maneno yaliyotangulia, kwa sababu swala imetangulia, na Swala ndanimwe mna rukuu, hivyo imekuwa kurudia kuitaja rukuu ni kukariri, kwa hiyo imebidi kuifanya iwe hali.

Na hii ni kuachia mbali ijmai ya umma kuwa Ali (a.s.) alitoa Zaka akiwa hali ya rukuu, hivyo Aya inakuwa mahsusi kwake. Al-Qawshajiy aliyesherehesha kitabu at-Tajriidu amenakili kutoka kwa wafasiri kuwa wao wameafikiana kuwa Aya iliteremka kumhusu Ali (a.s.), akiwa katika hali ya kutoa zaka pete, naye akiwa katika hali ya rukuu. Pia Ibnu Shahri Ashwab ameinakili katika kitabu al-Fadhwail, amesema katika maneno yake yaliyoelezwa: ‘’Umma umeafikiana kuwa Aya hii imeteremka kumhusu Amirul-Mu’minin (a.s.), na hadithi zinazotilia nguvu hilo zimefikia kiwango cha tawatur, kwani Sayyid Hashim al-Bahraniy amenakili katika kitabu chake Ghayatul-Marami kwa njia ya Ahlu Sunnah Hadithi ishirini na nne kuhusu kuteremka kwake kwa ajili ya Ali (a.s.) na kwa njia ya Shia Hadithi kumi na tisa.” Zingatia.

Hivyo ikiwa Aya imekuwa mahsusi kwa ajili ya Amirul-Mu’minin haitokuwa mradi wa walii ni uwalii ya sura ya jumla yaani kwa maana ya nusura na mahabba. Ni uwalii wa aina mahsusi, kwa hiyo inakuwa na maana ya anayefaa kufanya jambo fulani. Na Alama Mudhwaffar amesema kulihusu hilo: “Endapo itakubaliwa kuwa mradi wake ni msaidizi basi kuufunga usaidizi kwa Mwenyezi Mungu, Mtume wake na Ali halitokuwa sahihi, ila kwa kuizingatia moja ya pande mbili, ya kwanza:- Usaidizi wao kwa waumini ndani yake una kusimamia na kufanya mambo yao, hapo basi yarejea kwenye maana itakiwayo. Pili: Iwe usaidizi wa watu wengine kwa waumini kama si chochote kwa kuulinganisha na usaidizi wao, hapo basi pia latimia litakiwalo kwa kuwa ni katika mambo yanayolazimiana na usaidizi wao ulio kamili kwa waumini.”2

Kwa hilo imethibiti kuwa uwalii wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wa walioamini – Ali – ni uwalii aina moja, nayo ni uwalii wa haki ya kufanya. Na dalili juu ya hilo ni kutumika tamko moja katika ngazi zote, lau maana isingekuwa moja basi kungekuwa na mkanganyiko uliokusudiwa. Mwenyezi Mungu hawapotezi waja wake, kwa kuwa yeye lau angetaka maana nyingine ya uwalii wa waumini ingekuwa yafaa autenge pembeni uwalii huo wa waumini kwa kuutaja peke yake, ili kuondoa mkanganyiko, kama ilivyokuja katika Aya nyingine: “Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume” amekariri tamko utii. Kwa ajili hiyo Amirul-Mu’minin anastahiki kuwa Imamu wa wachamungu na walii wa waumini.

Aya Ya Tablighi Ni Tamko La Wazi Kuuhusu Uwalii:

Kauli yake (s.w.t.):

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنْزِلَ إِلَيْكَ مِنْ رَبِّكَ ۖ وَإِنْ لَمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ ۚ وَاللَّهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ ۗ إِنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ {67}

‘’Ewe Mtume! fikisha uliloteremshiwa kutoka kwa Mola wako, na kama hukufanya, basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri. (Surat-Maidah: 67).

Ilishuka Aya hii ili kubainisha ubora wa Amirul-Mu’minin (a.s.) huko Ghadiri Khum kama ambavyo ishara imetangulia katika hadithi ya Zayd bin Arqam iliyo katika Sahih Muslim.

Mwanzoni nilifikiri nitosheke na ishara tu ya tukio hili jinsi lilivyo wazi kwa mwenye kufuatilia vitabu vya Hadithi na historia, lakini mwandishi Msudani alinitibua, naye ni muhandisi As-Sadiq Al-Amiin. Yeye anakinza na kuwahujumu Shia katika gazeti la Sudan (Habari za Mwisho), imekuja mwanzo wa maneno yake:

“Kwa kweli tukio hili ambalo linaelezwa na vitabu vya Shia kuhusiana na Ghadir Khum ni kama hivi mwenendo wa wanavyuoni wa Shia kutajataja uzushi ambao wahesabiwa ndio msingi wa madhehebu ya Shia..”

Mimi sijui hali hii yatokana na kutoijua Hadihi na historia! Au kumchukia Imam Ali (a.s.) na kuzipinga fadhila zake, kwa kuwa tukio hili liko wazi hakuna kitabu cha historia kuhusu Uislam ambacho hakina habari hizi. Vipi imeghibu mbali na huyu mhandisi? Lililo wazi ni kuwa yeye hakujikalifisha nafsi yake, kufumba macho yake kisha achukuwe kitabu chochote kile cha Hadithi au historia miongoni mwa vitabu vya Ahlu Sunnah, halafu afungue kurasa zake na kama hatoikuta hapo itakuwa haki kwake ainasibishe na vitabu vya Shia au aiite uzushi.

Ghadir Katika Rejea Za Kiislam:

Hadithi ya Ghadir ni miongoni mwa Hadithi zenye wingi wa nyororo za wapokezi, hivyo wapokezi wake miongoni mwa maswahaba wamefikia mia moja na kumi. Na mwanachuoni Al-Amini amewahesabu wao pamoja na vitabu ambavyo vilivyoleta riwaya yake katika kitabu chake Al-Ghadir Jalada 1, Uk. 14-61. Mambo yatatuwia marefu endapo tutataja majina yao na vitabu vyao vilivyoandika Hadithi zao katika vitabu vya Ahlu Sunnah.

Wapokezi wake miongoni mwa Tabiina wamefikia themanini na nne kama ilivyokuja katika kitabu Al-Ghadir Uk. 62-72, wala wapokezi wa Hadithi ya Ghadir hawakusimama katika ukomo huu bali imenakiliwa mfululizo katika kila tabaka, na wamefikia jumla ya wapokezi 360 toka karne ya pili mpaka karne ya kumi na nne ya hijiriya.

Hii ikiwa mbali na maelfu ya vitabu vya kisunni ambavyo vimeitaja Hadith hii. Vipi itamuwia vyema mwandishi huyu baada ya hayo yote aseme kuwa huu ni uzushi wa kishia, hali ikiwa yajulikana kuwa riwaya ya Ghadir kwa njia ya Shia hazifiki nusu ya zilizokuja kwa njia ya Ahli Sunnah!? Lakini hili ni tatizo la insafu kwa wenye taaluma.

Wanaziachia kalamu zao bila ya utafiti au kufuatilia ili kupata uelewa. Basi hawa hapa wanavyuoni wa kisunni na waaminiwa wao miongoni mwa watu wa kale na waliokuja baada yao wanaeleza wazi usahihi wa Hadith ya Ghadir. Na miongoni mwao kwa mfano tu ni:

Ibnu Hajar al-Asqalaniy, aliyeifafanua Bukhari, anasema: “Ama Hadith: ‘Ambaye mimi ni walii wake basi Ali ni walii wake.’

Tirmidhiy na Nasaiy wameileta na ina njia nyingi sana, na amezidhibiti Ibnu Uqdatu katika kitabu pekee na sanad zake nyingi ni sahihi na hasan.”3

Na kitabu hiki alichoashiria Ibnu Hajar ni Kitabul-Wilayah Fii Twuruqi Hadithil-Ghadiir cha Abu Abbas Ahmad bin Muhammad bin Said Al-Hamdhaniy, mwanahadithi maarufu kwa jina la Ibnu Uqdatu, aliyefariki mwaka 333. Ibnu Al- Athiir amenukuu sana kutoka kwake katika kitabu chake Usudul-Ghabah, na pia Ibnu Hajar Al-Asqalaniy. Al-Asqalaniy amemtaja ndani ya kitabu Tahdhibut-Tahdhib Juz. 7, Uk. 337, baada ya kuitaja hadithi ya Ghadir akasema:

“Amekubali usahihi wake na kuchunguza njia zake Abu Abbas Ibnu Uqdatu. Akaiandika toka kwa sahaba sabini au na zaidi.” Na amemuishiria msanifu huyu katika kuthibitisha njia za Hadith ya Ghadiir Ibn Taymiyya kwa kauli yake: “Abu Abbas Ibn Uqdat ametunga kitabu kinachokusanya njia zake.”4

Ibnu Al-Maghaziliy As-Shafiiy: Baada ya kuitaja Hadithi ya uwalii kwa sanad yake anasema: “Hii ni hadithi sahihi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na wamieleza hadith ya Ghadir Khum kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) watu karibu mia miongoni mwao ni kumi - yaani kumi waliobashiriwa Janna – nayo ni Hadith iliyo thabiti sijui dosari yeyote kuihusu, Ali amekuwa pekee kwa fadhila hii hakuna yoyote anashirikiana naye.”5

Abu Jafar Muhammad bin Jarir bin Yazid At-Tabariy, mwandishi wa kitabu Tarikhut-Tabariy, ametunga kitabu maalumu, humo ameiweka Hadithi ya Ghadir, na amelitaja hilo mwandishi wa kitabu Al-Umda kwa kauli yake: “Mwanahistoria Ibnu Jarir Tabariy ameitaja habari ya siku ya Ghadir na njia zake katika njia sabini na tano, na ametunga kitabu maalumu ali- chokiita Kitabul-Wilayah ‘Kitabu cha Uwalii”6

Na imekuja katika ufafanuzi wa kitabu Tuhfatul-Alawiyah cha Muhammad bin Ismaiil Al-Amiir: “Amesema Al-Hafidh Ad-Dhahabiy katika Tadhkiratul-Hufadh anapotoa wasifu wa ambaye mimi ni kiongozi wake: ‘Muhammad bin Jarir ametunga kitabu kuhusiana na hilo.’ Dhahabiy ame- sema: Nilikiona na nilishangazwa na wingi wa njia zake.’’

Na kitabu cha Ibnu Jarir pia kimetaja kuwa Ibn Kathir katika historia yake amesema: “Nimekiona kitabu, humo zimekusanywa Hadithi za Ghadir Khum katika jalada mbili kubwa kubwa.”7

4) Al-Hafidh Abu Said Mas’ud bin Naasir bin Abu Zaid Sajastaniy, aliye- fariki mwaka 477 ameiandika Hadith ya Ghadir Khum katika kitabu Diraya Fii Hadithil-Wilayah katika Juzuu kumi na saba, amekusanya humo njia za Hadith ya Ghadir zilizoelezwa na Swahaba mia moja na ishirini.

Al-Amini amekwishawataja ndani ya kitabu Al-Ghadir wanavyuoni ishiri- ni na sita miongoni mwa wanavyuoni bora wa kisunni, ambao wametenga vitabu maalumu ili kuziandika riwaya za Hadith ya Ghadir, achia mbali vitabu ambavyo vimeitaja riwaya hii. Na tunahitimisha maneno yetu hapa kwa kutaja yale aliyoyasema Ibnu Kathir kutoka kwa Al-Juwainiy: “Yeye alikuwa anastaajabishwa na anasema: Nimeshuhudia kitabu huko Baghdad mkononi mwa mwandishi wa habari, ndani yake mkiwa na habari hizi, juu yake kimeandikwa: Jalada la ishirini na nane katika njia za: “Ambaye mimi ni walii wake basi Ali ni walii wake.” Na kinafuatiwa na Jalada la ishirini na tisa.”8

Vyanzo Vilivyothibitisha Kuteremka Kwa Aya Hii Kumhusu Ali (A.S.):

Ama kuhusu kuteremka Aya hii: ‘’Ewe Mtume! Fikisha uliloteremshiwa kutoka kwa Mola wako,” mahsusi kwa ajili ya Ali, hilo wamelisema wazi walio wengi miongoni mwao kwa mfano tu ni:

1) Suyutiy katika kitabu Durul-Manthur katika tafsiri ya Aya hii kutoka kwa Ibnu Abu Hatimi na
Ibnu Mardawayhi na Ibnu Asakir, kwa sanad zao kutoka kwa Abu Said, akasema: “Iliteremka
kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) siku ya Ghadir Khum kumhusu Ali.” Na pia
imenakiliwa kutoka kwa Ibnu Mardawayhi kwa kuiegemeza kwa Ibnu Mas’ud, kauli yake:
“Tulikuwa tukisoma wakati wa zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w): ‘Ewe Mtume
fikisha uliloteremshiwa kutoka kwa Mola wako kuwa Ali ni walii wa waumini, na ikiwa
hautofanya hautokuwa ume- fikisha ujumbe wake na Mwenyezi Mungu atakulinda mbali na
watu.”9

2) Ameeleza Al-Wahidiy ndani ya kitabu Asbabun-Nuzul kutoka kwa Abu Said akasema: “Iliteremka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) siku ya Ghadir Khum ikimhusu Ali.”10

3) Hafidh Abu Bakari Al-Farisiy, ameeleza ndani ya kitabu chake sehemu miongoni mwa Qur’ani iliyoteremka kumhusu Amirul-Mu’minin, kwa sanad itokayo kwa Ibnu Abbas kuwa Aya hii ilishuka huko Ghadir Khum ikimhusu Ali bin Abu Talib.

4) Hafidh Abu Nua’im Al-Asbahaniy, kwa sanadi yake kutoka kwa Aamashi, kutoka kwa Atiyyah amesema: “Iliteremka Aya hii kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) siku ya Ghadir Khum.”11

5) Hafidhu Ibnu Asakir As-Shafiiy, kwa sanad yake kutoka kwa Abu Said Al-Khudriy kuwa, hiyo iliteremka siku ya Ghadir Khum ikimhusu Ali bin Abu Talib.12

6) Badrud-Dini bun Al-Ainiy Al-Hanafiy, ametaja katika Umdatul-QariiyFii Sharhi Sahihil-
Bukhari
y akasema: “Amesema Abu Jafar

Muhammad bin Ali bin Al-Husein: Maana yake fikisha ulichoteremshiwa kutoka kwa Mola wako kuhusu fadhila ya Ali bin Abu Talib (r.a). Pindi ilipoteremka Aya hii aliushika mkono wa Ali na akasema: ‘Ambaye mimi ni walii wake basi Ali ni walii wake.”’

Tamko La Hotuba:

Na wengi kwa makumi kadhaa ya wengine mbali na hao wamethibitisha kuteremka Aya hii ikimhusu Ali bin Abu Talib. Na kutoka riwaya hizi mbalimbali tunachagua riwaya ya Al-Hafidh Abu Jafar Muhammad bin Jarir At-Tabariy. Ameiandika kwa sanad yake katika kitabu Al-Wilayah Fii Turuqi Ahadithil-Ghadir. Tamko lake ni kama ifuatavyo:

“Kutoka kwa Zayd bin Arqam, amesema: Alipofika Nabii (s.a.w.w) mahali paitwapo Ghadir Khum wakati wa kurudi kwake kutoka Hijja ya kuaga, na ilikuwa wakati karibu ya dhuhuri na joto ni kali, aliamuru mito inayotumi- ka pa kukalia mpanda farasi ikapangwa. Na Swalatu Jamia ilinadiwa. Tulikusanyika akahutubia hotuba fasaha, halafu akasema:

‘Kwa hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameniteremshia: ‘’Fikisha uliloteremshiwa kutoka kwa Mola wako, na kama hukufanya, basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu.’’

Hivyo basi Jibril ameniamuru kutoka kwa Mola wangu nisimame mahali hapa na nimjulishe kila mweupe na mweusi kuwa Ali bin Abu Talib ni ndugu yangu, wasii wangu, khalifa wangu na ni Imamu baada yangu. Nilimuomba Jibril aniombee msamaha kwa Mola wangu niache kulisema hili, kwa kuwa najua wachamungu ni wachache na wamekithiri wanaoni- udhi na wenye kunilaumu kwa sababu ya kukithiri kwangu kuwa na Ali na kumuelekea kwangu sana yeye, kiasi kwamba wameniita udhunu13

Allah (s.w.t.) akasema: “Na miongoni mwao wapo wale ambao wanamuudhi Nabii na wanasema yeye ni udhunu. Sema: Udhunu ni bora kwenu.”

‘Lau ningependa niwataje majina na niwaonyeshe ningefanya. Lakini mimi kwa kuwasitiri nimefanya heshima, hivyo Mwenyezi Mungu haridhii ila niufikishe. Oh ninyi watu juweni hivyo: Kwa hakika Mwenyezi Mungu amemfanya kwenu walii na Imam, na amefanya utiii kwake faradhi kwa kila mmoja. Hukumu yake ni yenye kupita na kauli yake ni jaizi, amelaaniwa mwenye kuwa kinyume naye, amerehemewa mwenye kumsadiki. Sikilizeni na mtii, kwa kweli Allah ni Mola wenu na Ali ni Imamu wenu. Halafu uimamu utakuwa katika kizazi chake kitokacho mgongoni mwake mpaka Siku ya Kiyama.

‘Hapana halali ila alilohalalisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wao, na hapana haramu isipokuwa aliloharamisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wao. Hapana elimu ila Mwenyezi Mungu ameipitisha kwake nami nimeinakili mpaka kwake, hivyo msipotee mbali naye wala msijivune mkamtweza, yeye ndiye ambaye anaongoza kwenye haki na anaifanyia kazi. Mwenyezi Mungu hatopokea toba ya yoyote atakayemkanusha wala hatomsamehe kabisa, Mwenyezi Mungu atafanya hivyo na atamuadhibu adhabu mbaya milele na milele.

‘Yeye ni mbora katika watu baada yangu, kwa kadiri ambayo riziki huteremshwa na kubakia viumbe. Mwenye kuwa kinyume na yeye ame- laaniwa. Kauli yangu ni kutoka kwa Jibril kutoka kwa Mwenyezi Mungu, nafsi ijiangaliye ilichotanguliza kwa ajili ya kesho. Ifahamuni Qur’ani iliyo muhkam (thabiti) wala msiifuate iliyo mutashabihu-(inayofanana), wala hatokufasirieni hilo ila yule ambaye mimi nimemshika mkono na kuuinua juu na kuwatambulisheni: Ambaye mimi ni walii wake hivyo basi huyu Ali ni walii wake. Na kumfanya yeye walii ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukuka, tambueni kuwa ameniteremshia mimi, nami nime- tekeleza, tambueni kuwa nimefikisha, tambueni kuwa nimesikilizisha, tambueni kuwa nimefafanua. Hautokuwa halali uamiri juu ya waumini baada yangu kwa yeyote asiyekuwa yeye.’

“Halafu alimnyanyua juu mpaka miguu yake ilifika usawa wa magoti ya Nabii (s.a.w.w) na akasema: ‘Oh ninyi watu! Huyu ni ndugu yangu na wasii wangu na mwenye kuelewa elimu yangu na ni khalifa wangu kwa mwenye kuniamini na juu ya kukifasiri kitabu cha Mola Wangu.”

Na katika riwaya nyingine: ‘’Oh Mungu Wangu! mpende atakayempenda na mfanyie uadui atakayemfanyia uadui na mlaani asiyemtambua na mghadhibikiye mwenye kuipinga haki yake. Ewe Allah! kwa hakika umeteremsha kwangu ukibainisha hilo kumhusu Ali:‘’Leo hii nimekukamilishieni dini yenu.” kwa uimamu wake, hivyo basi asiyemfuata yeye na atakayekuwa miongoni mwa kizazi changu kitokacho mgongoni mwake mpaka Siku ya Kiyama, hao amali zao zitakuwa zimeporomoka na watadumu motoni. Kwa kweli Ibilisi alimtoa Adam Peponi pamoja na kuwa yeye ni Swaf ’watullah kwa sababu ya husuda, hivyo basi msimhusudu, amali zenu zitaporomoka na nyayo zenu zitateleza. Kumhusu Ali sura ya “Naapa kwa Alasiri, kwa hakika mwanadamu yumo hasarani.” iliteremka.

‘’Enyi watu: “Aminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nuru ambayo ameiteremsha pamoja na yeye kabla hatujazifuta nyuso, na tuzirudishe nyuma yao au tuwalaani kama tulivyowalaani watu wa sabato.Nuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu iko kwangu na kwa Ali, halafu kwa kizazi kutokana na yeye mpaka kwa al-Qaimu al-Mahdiy.

Enyi watu, baada yangu watakuwepo maimamu wanaitia kwenye moto, na Siku ya Kiyama hawatonusuriwa, hakika Mwenyezi Mungu na mimi tunaepuka mbali nao, kwa hakika wao na wanusuru wao na wafuasi wao watakuwa kwenye tabaka la chini mno la moto.

Na wataufanya uimamu kuwa ufalme kwa kuupora, hapo basi mtamiminiwa, enyi viumbe, shaba ya moto na kutumiwa kijinga cha moto na wala hamtonusurika.’”

Hotuba hii haina haja ya maelezo na ufafanuzi, kwa hiyo ni juu ya mwenye akili azingatie. Dalili iko wazi ndani ya hotuba hii, ya wajibu wa kumfua- ta Imam Ali (a.s.), na ndani yake kuna kanusho kwa wanaosema kuwa eti makusudio ya uwalii ni mnusuru au mpenzi, kwa kuwa ishara za mahali na za kiusemi zinazuia hilo, kwa hiyo haiingii akilini kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alikuwa alizuie kundi lote hili wakati wa jua kali ili awaambiye: “Huyu Ali mpendeni na mumnusuru.”

Ni mwenye akili gani anaona maana hii? Na yeye kwa mtazamo huo atakuwa anamtuhumu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kuwa ni mtu wa mchezo usio na faida, kama ambavyo ishara za kiusemi zatilia nguvu hilo, hivyo kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w): “Hakika Ali bin Abu Talib ni ndugu yangu, wasii wangu, khalifa wangu na Imamu baada yangu.” Na kauli yake (s.a.w.w): “Kwa hakika Mwenyezi Mungu amemfanya kwenu walii na Imam, na amefanya utiii kwake ni faradhi kwa kila mmoja....”

Kwa hiyo suala la uwalii si jambo jepesi, Uislamu wote wasimama kwenye jambo hili. Je Uislamu sio kusalimu amri?! Ambaye hasalimu amri ya uongozi wa kiungu na kuutii katika amri zake zote, je ni haki kwetu tumuite mwislamu?! Bila shaka hapana. Vinginevyo katika hilo kutakuwa na mgongano. Kwani kuifuata miongozo iliopotoka na kusalimu amri kwenye miongozo iliyopotoka ni kuifanya Qur’ani katika jumla ya ushirikina. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema:

Wamewafanya makasisi wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Allah.” Wao hawakuwafanya sanamu bali walihalalisha kwa ajili yao aliloharamisha Mwenyezi Mungu na wameharamisha kwa ajili yao alilo- halalisha Mwenyezi Mungu na wakawafuata, na ni hivyo hivyo anayeuasi uongozi wa kiungu anahesabika kuwa ni mshirikina bila kizuizi.

Kwa hiyo mwenye kuizingatia Aya kwa jicho la uelewa na ufahamu atali- fichua hilo vyema kabisa. Hivyo kauli yake (s.w.t.): ‘’Ewe Mtume! Fikisha uliloteremshiwa kutoka kwa Mola Wako,” Kwa kweli Aya hii ni katika Surat Al-Maidah, nayo ni Sura ya mwisho ya Qur’ani kama ilivyokuja katika kitabu Mustadrakul-Haakim. Kama ambavyo Aya hii hii iliteremka huko Ghadir Khum kama ilivyotangulia. Na ilikuwa katika Hijja ya mwisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), hivyo yamaanisha kuwa Uislamu kwa maana ya dhahiri ulikuwa umefikishwa kama vile Swala, Zaka, Hijja na Jihadi…Hivi ni jambo gani hili la kiungu ambalo kutolifikisha kwake kwalingana na kutoufikisha ujumbe mzima?!

Hapana budi jambo hilo litakuwa ni kiini cha Uislamu na lengo lake, nalo ni kusalimu amri ya uongozi wa kiungu na kuzitii amri zake. Na ni wazi kuwa suala hili linafanya ipatikane hali ya kutowaridhisha maswahaba, walio wengi wanalikataa, na kwa sababu hiyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alimwambia Jibril katika moja ya riwaya zake ambayo maana yake ni: “Kwa kweli mimi nimepigana nao miaka ishirini na tatu ili wautambue unabii wangu, hivyo vipi watasalimu amri kwa uimamu wa Ali (a.s.) kwa mara moja.” Na hapo ndipo ukaja usemi wa Qur’ani: “Mwenyezi Mungu atakulinda na watu.” (Surat al-Maidah: 67)

Na baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alipofikisha jambo hili ambalo linalingana na risala yote, kauli yake Mwenyezi Mungu ilishuka:

نَزَّلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ مُصَدِّقًا لِمَا بَيْنَ يَدَيْهِ وَأَنْزَلَ التَّوْرَاةَ وَالْإِنْجِيلَ {3}

‘’Leo nimewakamilishieni dini yenu na kuwatimizieni neema yangu, na nimeridhia kwenu Uislamu uwe dini yenu. (Surat Aali Imran: 3)
Wanahadithi wengi wamebainisha uteremkaji wa Aya hii kwa ajili ya Ali, miongoni mwao ni Al-Amini ndani ya kitabu chake Al-Ghadir Juz. 1, uk. 230-237 ikiwa na vyanzo kumi na sita. Hivyo basi kukamilika kwa dini na kutimilizwa neema ni kwa uwalii wa Ali (a.s.).

Hivyo kuanzia hapa tunaweza kujua maana ya kila riwaya isemayo: “Kwa kweli kukubaliwa kwa amali kutoka kwa mja kunategemea kuwapenda Ahlul-Bayt (a.s.).” Kwa sababu wao ndio njia ambayo Mwenyezi Mungu ametuamuru kuifu- ata, amesema (s.w.t.): “Sema: Siwaombeni ujira wowote juu ya hili, ila mapenzi kwa karaba zangu.” Na mapenzi yao haimaanishi kuwapenda peke yake bali ni kuwafanya mawalii na kuwafuata na kuchukua mafunzo ya dini kutoka kwao.

Imekuja ndani ya Hadithi kutoka kwa Imam Ja’far bin Muhammad Swadiq (a.s.) amesema: ‘’Kwa kweli la kwanza atakaloulizwa mja atakaposimama mbele ya Allah (s.w.t.) ni: Swala za faradhi na kuhusu Zaka za wajibu na Saumu za wajibu na kuhusu Hijja za wajibu na kuhusu upendo wetu Ahlu Bayt. Akikiri upendo wetu halafu akifa nao ndipo Swala, Saumu zake, Zaka zake, Hija yake, vitakubaliwa, na kama hatokiri upendo wetu mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukuka basi Mwenyezi Mungu hatokubali kutoka kwake kitu katika amali zake.”14

Na kutoka kwa Ali (a.s.) alikuwa akisema: “Hapana kheri duniani isipokuwa kwa mmoja kati ya wawili, kwa mtu ambaye kila siku anazidisha hisani, na mtu ambaye anauwahi uovu wake kwa toba! Wapi ataipata toba? Wallahi lau atasujudu mpaka shingo ikatike Mwenyezi Mungu hatokubali kutoka kwake ila kwa uwalii wa Ahlul-Bayt.’’

Na kutoka kwa Anas bin Malik kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) amesema: ‘’Oh enyi watu …watajwapo Aali Ibrahim (a.s.) nyuso zenu zinakunjuka na watajwapo Aali Muhammad kana kwamba yawapofusha nyusoni mwao tembe ya komamanga?

Basi naapa kwa Ambaye amenituma kwa haki nikiwa Nabii, lau mmoja wenu aje Siku ya Kiyama akiwa na amali mfano wa mlima na wala asije na uwalii wa Ali bin Abu Talib (a.s.) basi Mwenyezi Mungu angemtupa motoni kifudifudi.”15 Na riwaya nyingine.

 • 1. Al-Bukhari, Kitabu cha fadhila. Na Sahih Muslim, Kitabu cha fadhila za sahaba.
 • 2. Dalailus-Swidqi, Juz. 2, Uk. 60.
 • 3. Fathul-Bariy Fii Sharhi Swahihil-Bukhariy, Juz.7, Uk. 61
 • 4. Minhajus-Sunah Juz. 4, Uk. 86.
 • 5. Manaqibu Amirul-Mu’minina Uk. 27-27.
 • 6. Al-Umdatu Uk. 55.
 • 7. Tarikh Ibn Kathiir, Juz. 11, Uk. 147.
 • 8. Al-Khulaswa Juz. 2, Uk. 298.
 • 9. Asbabun-Nuzuli.
 • 10. Asbabun-Nuzuli cha Al-Wahidiy Uk. 150.
 • 11. Al-Khasaisu, Uk. 29 – Sehemu ya Qur’ani iliyoteremka ikimuhusu Ali.
 • 12. Durrul-Manthur, Juz. 2, Uk. 298.
 • 13. Anayesikiliza kila analoambiwa.
 • 14. Biharul-Anwar Juz. 27 Uk.167.
 • 15. Biharul-Anwar Juz. 27 Uk.170.