read

Orodha Ya Wapokezi Wa Uongo Wa Saba’100

Mzushi Wake Ni Seif Bin ‘Amru At-Tamimiy Aliyefariki Mwaka Wa 170 Hijriyyah. Wapokezi Wake:-

JINA MWAKA ALIOFIA
Tabari 310 Hijriyyah
Ibn-Asaakir 571 Hijriyyah
Adh-Dhahabi 748 Hijriyyah
Ibnul-Athir 630 Hijriyyah
Abul-Fidai 733 Hijriyyah
Abi Bakar 741 Hijriyyah
Fan Fulton Nikison
Ibn-Kathir 774 Hijriyyah
Ibn-Khaldun 808 Hijriyyah
Ghiyathu-d-din 940 Hijriyyah
Mir Akhawandi 903 Hijriyyah
Ibn Badaran 1346 Hijriyyah
Rashid Ridhaa 1356 Hijriyyah
Sa’ad Afghani
Farid Wajidi
Ahmad Amini

Saba: Vita Vya Siffin Na Uasi Wa Mu’awiyah Bin Abi Sufian.

Baada ya kutimia nusura kwa Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) katika vita vya Jamal, Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na jeshi lake aliondoka kwenda kuondoa upinzani ambao aliuongoza Mu’awiyah bin Abi Sufian huko Sham, na majeshi mawili yalikutana katika mto Furat. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) alijaribu kusuluhisha jambo hili kwa njia ya mazungumzo, isipokuwa majibu ya Mu’awiyah bin Abi Sufian kwa ujumbe ambao Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) aliutuma kwake yalikuwa: “Ondokeni kwangu mimi sina njia nyingine isipokuwa vita tu.”1

Hivi ndivyo yalivyokutana majeshi mawili. Na zilipo dhihiri ishara za ushindi kwa jeshi la Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na kundi ovu likakaribia kushindwa, waliandaa hila (`hadaa ya misahafu`), kwani walinyanyua misahafu juu ya ncha za mikuki na panga. Hila hiyo ya udanganyifu ikabadilisha msimamo wa jumla kwa wengi, pamoja na kwamba Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) alijitahidi kufichua hadaa ya kunyanyua misahafu kwamba huo ni udanganyifu wa kupoteza ushindi ambao umekaribia kwa jeshi la Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), isipokuwa wale waliotaka vita visimamishwe hawakukubali wito wake wa mara kwa mara, na wakamlazimisha kukubali suluhu pamoja na kuwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) alipinga sana, na pia akapinga kuchaguliwa Abu Musa Al-Ash’ari kuwa mjumbe anayewakilisha jeshi lake katika suluhu, kwa sababu ya udhaifu wake na wepesi wa rai yake pale alipowaambia: “Sikubali mumchague Abu Musa kuwa hakimu kwa sababu yeye ni dhaifu kwa ‘Amr na hila zake.”2

Na hasa baada ya kumwondoa ugavana wa Kufah, ni katika yanayomfanya aone kuwa uaminifu wake kwake ni dhaifu, pamoja na hayo kundi katika jeshi la Imam lilimng’ang’ania Abu Musa tu.

Na kuonyesha kuwepo hila na njama ni utangulizi wa lengo la kunyanyua misahafu, na kutumia utukufu wa Qur’an kwa waumini dhaifu sambamba na hilo, ni pamoja na kuwepo kundi lililomuunga mkono Mu’awiyah bin Abi Sufian lilijipenyeza katika jeshi la Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na wakaeneza nguvu zao katika safu ya jeshi la Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), mpaka wakamlazimisha suluhu na uteuzi wa mjumbe wake, katika suluhu baadaye ambapo ilifanya matokeo yawe kama alivyo sema Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) kwa maslahi ya Mu’awiyah bin Abi Sufian ambapo mambo yalianza kumnyookea kidogo kidogo, baada ya kufanya uasi wake mkubwa ambapo alitoka katika utii wa Amirul-Muuminina na Khalifa wa Waislamu ambaye ni wajib kumtii, kwa uasi wake na tamaa ya utajiri wa kidunia ambao ni ndoto yake ya muda mrefu.

Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) alitoa habari za uovu wa Mu’awiyah bin Abi Sufian, alimwambia ‘Ammar: “Litakuuwa kundi ovu” na yalitokea aliyoyasema Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) alipokufa shahidi ‘Ammar akiwa anapigana chini ya uongozi wa Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) huko Siffin. Amesema: “Tulikuwa tunasomba matofali na ‘Ammar alikuwa anasomba matofali mawili mawili, Mtume (s.a.w.w.) akapitia karibu yake na akagusa vumbi kichwani kwake na akasema: “Namhurumia ‘Ammar litamuuwa kundi ovu, ‘Ammar anawalingania kwa Allah (s.w.t.) na wao wanamwita kwenda kwenye moto.”3

Na katika Mustadrak Sahihain kwa sanad ya Khalid Al-’Arabi amesema: “Niliingia mimi na Abu Said Al-Khudhri kwa Hudhaifah tukasema: “Ewe Abu ‘Abdillah! Tusimulie uliyoyasikia kutoka kwa Mtume wa Allah (s.a.w.w.) miongoni mwa fitina”.

Hudhaifah akasema: “Mtume wa Allah (s.a.w.w.) amesema: “Zungukeni pamoja na Kitabu cha Allah (s.w.t.).” Tukasema watu wakihitalifiana tutakuwa pamoja na nani? Akasema angalieni kundi ambalo lina mtoto wa Sumayyah, liandameni kwani yeye anazunguka pamoja na Kitabu cha Allah (s.w.t.), nimemsikia Mtume wa Allah (s.a.w.w.) anamwambia ‘Ammar: ‘Ewe Abul-Yaqidhan! Hutokufa mpaka likuue kundi lililo potoka njia.”4

Na uovu wa Mu’awiyah bin Abi Sufian ulikuwa ni jambo lenye kutarajiwa kutokea, kwa sababu ya kuchukua ugavana wa Sham tangu wakati wa ‘Umar na akapata mali, jaha na majumba ya fahari aliyo yajenga.

Na akajijenga wakati wa ‘Uthman, haikuwa rahisi kuyaacha na alikuwa na yakini kuwa Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) kama hatomuuzulu basi atamnyang’anya yote aliyo yamiliki kutoka katika hazina ya Waislamu, na atamfanya awe sawa na watu wengine miongoni mwa Waislamu.

Na kisa chake pamoja na Abudhar wakati wa ‘Uthman kinaonyesha tunayoyasema kupenda kwake dunia na ufujaji wake katika mali za dola kwa ujumla, na upinzani wa Abudhar kwa Mu’awiyah bin Abi Sufian ulisababisha aamuru kufukuzwa Abudhar kwenda Rabadhah baada ya kuwa alimwita arejee Madina.

“Kutoka kwa Wahhab amesema: “Nilimkuta Abudhar Rabadhah nikamwambia:”Ni kipi kilichokuleta katika ardhi hii?” Akasema: “Tulikuwa Sham, basi nikasoma Ayah: ‘Na wale ambao wanalimbikiza dhahabu na fedha na wala hawazitoi katika njia ya Allah (s.w.t.), basi wabashirie adhabu iumizayo.’ Mu’awiyah bin Abi Sufian akasema hii haikuteremka kwetu, hii haikuteremka isipokuwa kwa Ahlul-Kitab, akasema; na nikasema: Hakika imeshuka kwetu na kwao.”5

Na Abudhar aliadhibiwa kwa kufukuzwa pamoja na kwamba kuna ushahidi wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) juu ya ukweli wake aliposema: “Haikumfunika mbingu wala hakutembea ardhini (mtu) mkweli wa kauli kuliko Abudhar.”6

Na tabia ya Mu’awiyah bin Abi Sufian katika ugavana na utawala inadhihirika wazi katika kauli ya baba yake Abu Sufian kwa ‘Uthman baada ya kupewa Bai’a: “Enyi Bani Umayyah udakeni kama mnavyodaka mpira, (naapa) kwa ambaye Abu Sufian anaapa kwake sikuacha kuwa nalitamani liwe kwenu na mlirithishe kwa watoto wenu.”7 Na katika mapokezi mengine kuna ziada: “Huko Akherah hakuna Jannat (pepo) wala Jahannam (moto).”8 Na hii inathibitisha ni aina gani ya Uislamu ulioingia katika nyoyo zao hali wao wanauchukia.

“Abu Sufian amesema: “Wallahi sikuacha kuwa dhalili hali ya kuwa na yakini kuwa jambo lake litadhihiri, hadi Allah (s.w.t.) akauingiza moyo wangu katika Uislamu na mimi ni mwenye kuchukia.”9

Na miongoni mwa kauli za Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) kwa Mu’awiyah bin Abi Sufian ni ambayo ameipokea Muslim katika Sahih yake. Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) siku moja alimtuma ‘Abbas kwenda kwa Mu’awiyah bin Abi Sufian ili aje amwandikie Ibn ‘Abbas akamkuta anakula, Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) alimrejesha tena kwenda kumwita akamkuta anakula hadi mara ya tatu, Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) akasema Allah (s.w.t.) asilishibishe tumbo lake”.10 Pia katika Sahih Muslim, amesema Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.); “Amma Mu’awiyah bin Abi Sufian ni fakiri hana mali yoyote.”11

Na katika Musnad Ahmad, amesema Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) kwa Mu’awiyah bin Abi Sufian na ‘Amr bin ‘Aas: “Ewe Allah (s.w.t.) watie katika fitina kuwatia na waingize motoni kuwaingiza.”12

Na zipo Hadith nyingi zisizokuwa hizo miongoni mwa Hadith zinazo bainisha ukweli wa Mu’awiyah bin Abi Sufian huyu ambaye amehitimisha vitendo vyake katika dunia hii kwa kumtawalisha mwanae Yazid mlevi, fasiki kuwa khalifa wa Waislaam baada yake.

Nane-Kufa Shahid Kwa Al-Imam ‘Ali Ibn Abi Talib (A.S.)

Vita vya mwisho alivyopigana Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) ni vita vya Nahrawan ambapo alipigana dhidi ya kundi lililo lazimisha suluhu Siffin, lakini likajuta baada ya siku chache, hivyo likatengua ahadi yao na wakatoka katika Bai’a ya Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na ambalo baadaye likajulikana kwa jina la Khawarji au Al-Maariqina (waasi). Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) aliwashinda na akawa anajiandaa kurudia mapambano na wapinzani wa Sham baada ya suluhu kushindwa walipokutana wajumbe wawili, lakini Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) akawa ameuliwa shahidi na

‘Abdurahman bin Muljim naye ni mmoja wa Makhawariji ambaye alimpiga Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) kwa dharuba ya upanga huku akiwa katika sala ya Al-fajiri katika msikiti wa Kufah asubuhi ya kuamkia siku ya kumi na tisa katika Mwezi mtukufu wa Ramadhan Mwaka wa 40 Hijriyyah baada ya kuongoza kwa muda wa miaka mitano.

Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) alibakia siku tatu akiumwa kutokana na pigo, ambapo alimwita mtoto wake Al Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) mjukuu wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) kuja kushika majukumu yake ya Uimamu katika kuongoza ‘Ummah baada yake.

Al Imam Hasan Ibn ‘Ali Ibn Abi Talib (A.S.) Na Suluhu Ya Mu’awiyah Bin Abi Sufian

Baada ya Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) kufa shahid, Al Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) alipanda Mimbar na watu wa Kufah walinyanyuka na kumbay’i Khalifa wa Nabii na Imam wa Ummah. Lakini hilo halikudumu isipokuwa kwa muda wa miezi sita ambapo habari za Kufah Shahid Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) zilifika Sham, na Mu’awiyah bin Abi Sufian aliondoka na jeshi kubwa kuelekea Kufah kwenda kuchukua hatamu za uongozi wa Waislamu na kumlazimisha Al Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) kufanya suluhu. Imam Hassan hakuwa na njia nyingine isipokuwa kukubali. Na hapa baadhi ya watu wanatia shaka juu ya suluhu ya Al-Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), wakati ambapo ndugu yake Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) alichagua njia ya vita na kupigana.

Hakika Al-Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) hakufanya mkataba wa suluhu pamoja na Mu’awiyah bin Abi Sufian bali amelazimishwa. Kulikuwa na mgawanyiko katika jeshi lake na hali ya Iraq kwa ndani haikuwa ni muafaka kwa vita, na ufalme wa Roma ulikuwa unangojea fursa ya kuupiga Uislam, na ulikuwa umejiandaa kwa jeshi kubwa tayari kuwapiga vita Waislamu.

Na kama vingetokea vita baina ya Mu’awiyah bin Abi Sufian na Al-Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), basi ushindi ungekuwa ni wa ufalme wa Roma na sio kwa Al Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) wala kwa Mu’awiyah bin Abi Sufian.

Na hivyo kukubali kwa Al Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) kumeondoa hatari kubwa iliyokuwa ikitishia Uislamu. Kwa ujumla hali iliyo kuwepo wakati wa Al-Imam Hassan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), sio hali iliyo kuwepo wakati wa Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), ambaye baadaye alichagua njia ya Thawrah na vita ambavyo ndugu yake Al-Imam Hassan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) alivitayarisha kwa udadisi wake kwa kudhihirisha ukweli wa wafalme wa Bani Umayyah katika wakati wake.

Ama misingi ya makubaliano ya suluhu ilikuwa kama ifuatavyo:-

1. Al-Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) asalimishe utawala na hatamu za uongozi kwa Mu’awiyah bin Abi Sufian kwa sharti, Mu’awiyah bin Abi Sufian ahukumu kulingana na misingi ya Qur’an na Sunnah za Mtume wa Allah (s.a.w.w.).

2. Baada ya kufa Mu’awiyah bin Abi Sufian Ukhalifa utakuwa ni haki ya Al-Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na kama akifariki basi Ukhalifa utakuwa kwa Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.)

3. Shutuma zote na uovu dhidi ya Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) uzuiwe, iwe ni kwenye Mimbar au popote (Mu’awiyah bin Abi Sufian alikuwa ana amuru makhatibu katika wilaya zote kumtukana Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), Hassan na Ibn ‘Abbas, katika kila hutuba ya Ijumaa na Iddi, na Mu’awiyah bin Abi Sufian hakutekeleza ahadi yake hii wala nyinginezo ambazo zilikubaliwa).

4. Kutoa kiasi cha dirham milioni tano zilizopo katika hazina ya Kufah ziwe chini ya usimamizi wa Al-Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na ni wajibu kwa Mu’awiyah bin Abi Sufian kutuma kwa kila mwaka dirham milioni moja za pato kwa Al-Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) ili azigawe kwa familia za wale ambao walikufa shahid katika vita mbili, Jamal na Siffin, katika upande wa Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.).

4. Mu’awiyah bin Abi Sufian anaahidi kuwaacha watu wote wa aina yeyote kutokana na kusumbuliwa na anaahidi vile vile kuwa atatekeleza misingi ya suluhu hii kwa umakini na anaifanya dini iwe ni shahidi juu yake.

Tisa: Kufa Shahid Kwa Al-Imam Hasan Ibn ‘Ali Ibn Abi Talib (A.S.)

Mu’awiyah bin Abi Sufian alimshawishi (Ju’udatu binti Al-Ash’ath bin Qais) mke wa Al-Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) ambaye alikuwa ni wa ukoo wa familia zinazo wapinga Ahlul-Bayt (a.s.), kwa kumtumia dirham laki moja akamwahidi kuwa atamwozesha kwa mtoto wake Yazid kama atampa sumu Al-Imam Hasan bin Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.). Mke mwovu alidanganyika na ahadi za uongo za Mu’awiyah bin Abi Sufian na akampa Imam sumu, na hiyo ilikuwa Mwaka wa 50 Hijriyyah. Mu’awiyah bin Abi Sufian alifurahi sana alipojua kufa shahid kwa Al-Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) kwa kuwa alikuwa anaona kuwa ni kipingamizi kikubwa katika matakwa yake na hasa katika kuimarisha utawala katika familia ya Mu’awiyah bin Abi Sufian kimekwisha kuondoka.

Kumi: Thawrah (Mapambano) Ya Karbala Na Kufa Shahid Kwa Al Imam Hussein Ibn ‘Ali Ibn Abi Talib (A.S.)

Al-Imam Hussein bin ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) ni Imam wa tatu wa Ahlul- Bayt (a.s.), na tukio muhimu katika historia lilikuwa ni kujitoa muhanga na kufa kwake shahid pamoja na watoto wake Ahlul-Bayt (a.s.) na wafuasi wake pale Karbala. Katika tukio lililotingisha akili na fikira na kuandikwa katika kurasa za historia na litaendelea kuthibiti na kubaki daima.

Hakika sababu zilizowazi za Thawrah ya Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), ni upotovu ambao ulidhihiri wakati huo katika watawala wa Bani Umayyah na ukandamizaji wao kwa watu.

Mu’awiyah bin Abi Sufian kwa muda wa miaka ishirini alikuwa anaimarisha kumtawalisha mwanae mwovu Yazid na kumpa nguvu ili kumfanya kuwa Amirul-Muuminina na Khalifa wa Mtume wa Allah (s.a.w.w.) kwa Waislamu, na kwa hivyo akakhalifu ahadi zake kwa Al- Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na kutengua ahadi zote alizomwahidi Allah (s.w.t.).

Yazid kwa mtazamo wa makundi yote ya Kiislam, alikuwa anakunywa pombe wazi wazi na anakunywa hata makapi na kukesha, na kuimba mashairi ya kipuuzi tunataja baadhi yake:- “Muziki wa didan umenishughulisha kutosikia adhana, na mwanamke kikongwe asiyejiweza amekuwa ni badala ya hurulain”.

Hakuna ajabu katika hili kwani Yazid bin Mu’awiyah bin Abi Sufian amelelewa na yaya wa Kikristo, na alikuwa ni kijana mjinga mwovu, tegemezi, mfujaji, hana haya, asiyeona mbali na asiye na maarifa kama walivyosema wanahistoria.

Baada ya kufariki Al-Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) katika Mwaka wa 50 Hijriyyah, Mashi’a wa Iraq walijaribu kujikomboa na walimwandikia Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) wakitaka amuuzulu Mu’awiyah bin Abi Sufian katika uongozi wa Waislamu. Lakini Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) akawaambia katika jibu lake kuwa ana ahadi na makubaliano na Mu’awiyah bin Abi Sufian hawezi kuyavunja.

Baada ya kufa Mu’awiyah bin Abi Sufian Mwaka wa 60 Hijriyyah, Yazid alichukua utawala, basi utawala wake ukawa ni mwanzo wa upuuzi na madhambi. Katika hali hii Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) aliona sio kwamba wakati ni mwafaka tu, bali ni wajibu kufanya harakati na Thawrah kwa ajili ya kuunusuru Uislamu na misingi ya dini, na sio kwa ajili ya kuchukua Ukhalifa na utawala ambao ndiyo ulikuwa matamanio ya Bani Umayyah, ambapo walipania mno katika kuupata na hasa baada ya watu wa Iraq kukataa kumnusuru Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na hofu yao kwa Bani Umayyah.

Na anabainisha wazi Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) katika moja ya hotuba zake alipokuwa karibu na Karbala kuhusu sababu ya Thawrah yake, kwa kusema:

“Enyi watu atakayemwona kiongozi mwovu anahalalisha aliyoharamisha Allah (s.w.t.) baada ya kumwahidi, anakhalifu Sunnah za Nabii wake, na anahukumu baina ya waja wa Allah (s.w.t.) kwa ufisadi na ujeuri; na asimpinge kwa ulimi wake na vitendo vyake; basi ni haki kwa Allah (s.w.t.) kumtupa Jahannam.” Vile vile amesema: “Enyi watu, na hakika wao wamemtii Shetani na wamemwasi Allah (s.w.t.) na wamefanya ufisadi katika ardhi, wamevunja Sunnah na wamefuja hazina ya mali ya Waislamu, na wamehalalisha aliyoyaharamisha Allah (s.w.t.), na wakaharamisha aliyoyahalalisha Allah (s.w.t.), na mimi nina haki zaidi kumpinga kuliko watu wengine.” Akakusanya wafuasi wake na Ahlul Bayt wake waliokuwa pamoja naye na akawaeleza wazi kukataa na kusitasita kwa watu wa Kufah, kisha akawaambia: “Wafuasi wetu wametufedhehesha hivyo anayependa kuondoka basi na aondoke na wala hatakuwa na dhima yetu.”

Pamoja na hivyo Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) alibaki na msimamo wake na azma ile ile aliyotoka nayo Makkah na hakuwa na yeyote isipokuwa wafuasi, ndugu, watoto na watoto wa Ami zake, na idadi yao haizidi sabini na nane na hapo alitamka tamko lake lenye kudumu; “Kama dini ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) haiwezi kusimama isipokuwa kwa kuuliwa kwangu, basi enyi mapanga niuweni.”

Na alikutana na jeshi la Yazid bin Mu’awiyah bin Abi Sufian, ambalo idadi yake ilikuwa ni elfu thelathini na mbili, chini ya uongozi wa Hur bin Yazid Ar-Riyaahi. Kwa kawaida kulikuwa na uwezekano mkubwa wa jeshi la Banu Umayyah kuuwa kundi hili lenye idadi ndogo, na hiyo ni kweli. Katika siku hiyo yalitokea mauaji hayo kwa Ahlul-Bayt (a.s.) na kudhulumiwa kwao kunasikitisha, kana kwamba Yazid bin Mu’awiyah bin Abi Sufian alikuwa analipa malipo ambayo Mtume wa Allah (s.a.w.w.) alimuomba: “Sema siwaombi juu yake malipo isipokuwa kuwapenda jamaa zangu”.

Tarekh imesimulia matukio na mauaji ambayo ni vigumu mno kwa mtu yeyote kuyaelezea. Kati ya hayo ni ya mtoto mchanga, naye ni ‘Abadallah bin Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), ambaye Imam Hussein alimbeba kwenda kumwombea maji baada ya wao kuweka kizuizi baina ya watu wa kambi ya Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), na mto Furati na kiu ikawabana sana. Alimbeba kwenda kumwombea maji na ili kuzitikisa dhamiri zao na kuathiri hisia zao za kibinadamu, hawakumjibu isipokuwa kwa kumlenga mshale mtoto mchanga na wakamwua, na mashahidi katika wafuasi wa Hussein na Ahlul-Bayt (a.s.) waliendelea kuuawa mmoja baada ya mwingine. Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) alikuwa ni wa mwisho kufa shahid katika vita hivyo vibaya.

Hawakutosheka kwa kumuuwa Bwana wa vijana wa watu wa Jannat (pepo) bali walikata kichwa chake na wakakitenganisha na mwili wake, kichwa cha Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na vichwa vya wafuasi wake vilichukuliwa na kuwa zawadi, wauaji walivigawa na wakavinyanyua huku wakielekea kwa Yazid bin Mu’awiyah bin Abi Sufian huko Sham ambaye, baadhi ya Waislamu wamempa sifa ya Amirul-Muuminin basi hakuna nguvu wala hila isipokuwa kutoka kwa Allah (s.w.t.)...!

Hakika matukio, mambo na misimamo ambayo tumeieleza na ambayo wameafikiana wapokezi wote wa Kiislamu Sunni na Shi’a, yanabainisha wazi malengo matukufu na ambayo kwa ajili yake Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) alifanya Thawrah, pamoja na hayo, ingawa ufisadi, uasherati na upotovu, na uovu ulioenea ambao ni wajibu kuuondoa kwa mkono, ulimi na kuchukia kwa moyo kumepatikana, wanaokosoa Thawrah hii tukufu kwa sababu ya kutumbukia kwao katika propaganda wa upotoshaji wa Bani Umayyah ambao umejaribu kupotosha historia, na vile vile kwa sababu ya kutumbukia kwao katika ta’asub (ushabiki) mbaya za kimadhehebu.

Hivyo zikadhihiri hukumu zenye kutia kasoro na kauli zenye kutuhumu juu ya Thawrah ya ambaye Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) amesema juu yake kwa mapokezi ya Waislamu wote, kwamba yeye ni Bwana wa vijana wa watu wa Jannat; kwa mfano kauli ya Ibn Taymiyyah: “Hakika Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) kwa Thawrah yake amekwisha toka katika utii wa kiongozi wa Waislamu na kwamba vile vile amechochea fitina katika ‘Ummah wa Kiislamu!!” Na kama tutamwuliza huyu juu ya kutoka Mu’awiyah bin Abi Sufian katika utii wa Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) jibu lake lingekuwa hiyo ni fitina iliyotokea baina yao na wala wao hawana dhambi katika hilo.

Na hili si lingine isipokuwa ni hali miongoni mwa hali za kujaribu kupotosha na udanganyifu ambao uko wazi katika historia ya Kiislamu, vinginevyo itatafsiriwaje hali ya baadhi ya Waislamu ya kujifanya kutojua mauaji haya ya kihistoria, ambayo humo wameuliwa watoto wa Mtume wa Allah (s.a.w.w.) katika hali mbaya kabisa ya mauaji na adhabu?

Sio hayo tu, bali watawala wengine wa Bani Umayyah walifuata mwendo wa Mu’awiyah bin Abi Sufian na mtoto wake Yazid; watawala wengine katika kuzima harakati za wapinzani wa utawala wao, na hasa Ahlul-Bayt (a.s.) wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), walihahikisha kwamba, daima wanakandamizwa, wanafukuzwa, wanaadhibiwa na kuuliwa.

Na udhalimu wao ulikuwa kwa Ahlul-Bayt (a.s.) na wasiokuwa Ahlul-Bayt (a.s.), walikuwa ni shabaha katika kila nyanja ambazo kuna dhana ya kuleta ushindani katika utawala wao wa kidunia na ufalme wa Kisra.
Historia imeandika kwa mfano - tukio la mauaji ambalo alichinjwa ‘Abadallah bin Zubeir, na akachunwa katika eneo takatifu la Makkah ambalo hata makafiri walikuwa wanalitukuza na kuliheshimu, wala hawakuhalalisha kumwagwa humo damu ya mnyama tukiachilia mbali ya binadamu. Al-Ka’abah Tukufu haikumsaidia kitu chochote Ibn Zubeir ambapo aligandamana na pazia yake kwa watawala wa Bani Umayyah.

Vipi nyumba ya Allah (s.w.t.) itakuwa na utukufu kwao na wao ndio ambao waliipiga Al-Ka’abah Tukufu kwa manjanikh (makombeo ya moto), wakati wa utawala wa Abdul-Malik bin Marwan ambaye alitoa mamlaka katika mkono wa mwovu wake Hajjaj ya kuuwa, anauwa na kuchinja watu bila ya haki, na ambao Hassan Al-Basri amesema juu yao: “Kama ‘Abdul-Malik asingekuwa na kosa isipokuwa Hajjaj basi lingemtosha”. Na amesema ‘Umar Abdul-Aziz: “Kama kila ‘Ummah ungekuja na mwovu wao na sisi tukaja na Hajjaj basi tungewashinda”, tukiachilia mbali kisa mashuhuri cha ‘Abdul-Malik cha kuchana Kitabu cha Allah (s.w.t.).

Je, vitendo hivi vinamfanya mwenye kuvitenda kuwa Mwislamu? Tukiachilia mbali kumuuwa kwake Khalifa wa Waislamu na Amirul- Muuminin?

Hapana shaka kwamba sisi leo tuna haja ya kuangalia historia ya Kiisalmu, na kudadisi katika mengi ya matukio na kuchunguza kwa yale yaliyopo miongoni mwa uhusiano mkubwa na maisha yetu ya kila siku na yawe ndiyo hukumu yetu katika kundi hili au lile, mbali na dhuluma au makosa kwa sababu ya matukio hayo Waislamu wamegawanyika madhehebu na makundi yenye kuzozana, kila moja linadai kuwa ndilo kundi lenye kunusurika na sio kwa yeyote kusubiri wahyi kutoka mbinguni umteremkie na kumwambia jina la kundi hili lenye kunusurika.

Na Allah (s.w.t.) ametujaalia akili ili tutofautishe ovu na jema na akatukataza kuiga kwa upofu na akatutanabahisha: “Bali aliwajia kwa haki na wengi wao ni wenye kuchukia haki.” Na akatuhadharisha kuchukua kutoka kwa kila mtu, “kama akikujieni fasiki kwa habari basi chunguzeni msije mkawadhuru watu kwa ujinga na mkaja juta kwa mliyoyafanya.”

Shura Baina Ya Misingi Na Utekelezaji

Baadhi ya wenye kukhalifu wanajaribu kupinga Ayah za Uimamu wa Ahlul Bayt (a.s) kwa madai kuwa Uimamu wa Waislamu umefanywa kuwa Shura na wametoa ushahidi wa Ayah mbili kutoka katika Kitabu cha Allah (s.w.t.). Ya kwanza ni:

وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ{38}

“Na jambo lao ni Shura baina yao.” (Asy Syuura 42:38)

Ayah hii haionyeshi Shura katika mambo yote ya Waislamu, hiyo ni kwa sababu kushauriana hakusihi katika jambo ambalo kuna Ayah ya Allah (s.w.t.) na kauli ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.):

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَنْ يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَنْ يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُبِينًا {36}

“Haikuwa kwa Muumini mwanamme wala Muumini mwanamke anapohukumu Allah (s.w.t.) na Mtume wake wawe na hiari katika jambo lao na atakae muasi Allah (s.w.t.) na Mtume wake basi amepotea upotevu ulio wazi.” (Al-Azhaab 33:36)

Vinginevyo, je inajuzu kushauriana katika idadi ya raka’a za sala kwa mfano, au mengineyo katika hukumu ambazo kumeteremka Ayah, na tumebainisha yaliyo pokewa kutoka kwa Mtume wa Allah (s.a.w.w.) miongoni mwa hadith za Uimamu, hivyo haibaki nafasi ya kushauriana. Ama Ayah ya pili ambayo ni:

وَاسْتَغْفِرْ لَهُمْ وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ ۖ{159}

Washauri katika jambo” (Ali-Imran 3:159)

Bali anamwambia: “ukiazimia mtegemee Allah (s.w.t.).” Na fanya kulingana na unavyoona na inadhihiri kuwa nafasi ya kushauriana inayo pendekezwa ni katika vita, na utapata mfano katika ushauriano huu katika sehemu ya nne ya kitabu hiki wakati Mtume lipowashauri Masahaba wake katika vita vya Badr. Na kama tutajaalia uwa hukumu ya Khalifa wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) ni Shura hakika tutajiuliza. Hii Shura ni ya namna gani?

Na ni ipi njia ya kuitekeleza? Na namna gani makhalifa walitekeleza Shura hii? Na nini hukumu ya khalifa ambaye anafikia katika utawala hali amekwishavunja misingi ya Shura?

Na namna gani makhalifa walitekeleza Shura hii kisha tuangalie namna gani kila mmoja katika makhalifa wa mwanzo alivyofika katika utawala.

1. Ukhalifa Wa Abubakr Ibn Abu Quhafa

Hakika njia ambayo ilitimia katika kumtawalisha Abubakr na kupewa Bai’a, amekwisha ieleza ‘Umar ibn Al-Khattab - kama ilivyotangulia - ilikuwa ghafla, lakini Allah (s.w.t.) ameepusha shari yake. Na tumeona kutukanana kwa Muhajirin na Ansar juu ya Ukhalifa, na Ansar walitoa hoja ya kustahiki kwao ukhalifa, tukizingatia asili na nafasi yao katika uongozi wa Madina na kunusuru kwao kukubwa katika Uislamu, na hoja za Muhajirin zilikuwa kwamba wao wanastahiki zaidi, na Abubakr alipendekeza uongozi uwe wa Muhajirin na wasaidizi wawe ni Ansar. Ansar wakamjibu kutokana na mapendekezo yake kuwa kila kundi katika makundi mawili yawe na kiongozi kwa kauli yao: “Kwetu kuwe na kiongozi na kwenu kuwe na kiongozi.”

Na tumeona namna gani ‘Umar aliokoa msimamo huu kwa kuuchukua kwa nguvu na kumpa Abubakr bay’a. Wakati ambapo Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) pamoja na jamaa wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) hawakuwepo, hivyo Ahlul- Bayt (a.s.) wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) hawakupata fursa katika kuchagua au hata kutoa maoni, iko wapi Shura katika hayo yote?

2. Zama Za ‘Umar

Njia ambayo amefikia ‘Umar katika utawala ni kutokana na wosia aliyo ulioandikwa na Abubakr akiwa katika maradhi yake ya mwisho mbele ya ‘Uthman bin ‘‘Affan tu! Na ‘Umar akachukua wosia huo na kutoa ushahidi kwa watu na akachukua Bai’a kwao kwa sababu hiyo. Je, iko wapi Shura katika hili?

3. Zama Za ‘Uthman Bin ‘‘Affan

Njia ambayo amefikia ‘Uthman bin ‘‘Affan katika utawala, ilitegemea kikao cha Shura na ‘Umar bin Al-Khattab peke yake aliteua wajumbe wake sita, na akajaalia rai ya mwisho mikononi mwa Abdur-Rahman bin ‘Auf katika hali ya kugawanyika wajumbe sita sehemu mbili kama ilivyotokea. Shura iko wapi hapo?

4. Zama Za Mu’awiyah Bin Abi Sufian

Njia ambayo Mu’awiyah bin Abi Sufian alifikia katika utawala, ilikuwa ni kwa kunyanyua upanga dhidi ya Khalifa wa Waislamu na Imam wao aliyepewa Bai’a na wao, baada ya watu kumkimbilia na kumbay’i baada ya kuuliwa ‘Uthman bin ‘Affan kisha, baada ya kumlazimisha Al-Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) kufanya suluhu.

5. Zama Za Yazid Bin Mu’awiyah Bin Abi Sufian.

Njia ambayo Yazid bin Mu’awiyah bin Abi Sufian amefikia katika utawala ilikuwa ni wosia kutoka kwa baba yake, ambaye alileta njia mpya katika ukhalifa na kuufanya kuwa ni wa kurithiana. Shura iko wapi hapa?

Na Yazid bin Mu’awiyah bin Abi Sufian alizatiti utawala wake kwa kumwua Al-Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), na watoto wengine wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) pale Karbala. Vivyo hivyo ndivyo watawala wengine wa Waislamu walifikia katika utawala tangu siku hiyo hadi leo hii.

Hivyo njia ambayo ilitumika kuwatawalisha makhalifa katika maelezo tuliyoyataja tunailinganisha na njia ambayo inatumiwa kuwateua watawala wa dola za kimagharibi katika njia ambayo inaitwa Demokrasia.

Basi ni ipi kati ya njia mbili hizi ambayo ni bora kwa mtazamo wa akili sahihi ambayo imeepukana na ta’asub ya dini na madhehebu?

Jamhuri ya Waislamu katika Ahl as-Sunnah wamekataa Hadith zilizopokelewa kutoka kwa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) kuteua Maimamu wa Ahlul-Bayt (a.s.) kuwa ni Makhalifa wake katika ‘Ummah wa Kiislamu, hivyo wakapinga Hadith katika hilo na wakawapinga wale wanaoziitakidi kwa kusema kwamba jambo hili ni Shura, wakati ambapo Shura haikuwa na athari yoyote katika kutawalisha makhalifa ambao wanawakubali. Wamepinga Hadith za Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) kuhusu ukhalifa na wakaukubali kutoka kwa asiyekuwa Mtume, na hawakuweka sharti la Shura katika nassi (pokezi) nyingine zisizokuwa hizo bali wamekubali uteuzi wa waliye mchagua.

Wamehukumu uhalali wa Yazid bin Mu’awiyah bin Abi Sufian, ingawa kulikuwa na Thawrah ya Bwana wa mashahidi, na wakahukumu uhalali wa Mu’awiyah bin Abi Sufian ingawa alimuasi Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na akatoka katika utii wake.

Hakika kosa la wazi ambalo Jamhuri ya Waislamu wanatumbukia kwalo, ni kuchukua Hadith za Nabii katika madhehebu ambayo wanayaamini - yaani wengi wao wanakataa Hadith kwa sababu tu ina khalifu madhehebu yao hata kama Hadith hii imetoka katika vitabu vyao ambavyo wanaamini usahihi wake - pamoja na kwamba hukumu ya akili inawajibisha kuchukua madhehebu kutoka katika nassi na wala si kinyume.

Mwisho Wa Utafiti Wa Uimamu

Tumebainisha katika yaliyotangulia Hadith za Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) katika Uimamu ambao unapatikana katika Maimamu wa Ahlul-Bayt (a.s.) wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), na ambao ni maalumu kwa Maimamu kumi na wawili (a.s.), ambao wa kwanza ni Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.). Na tukaweka wazi baadhi ya (mambo) yasiyo eleweka vizuri katika Hadith hizo miongoni mwa dalili, na tukatengua shaka zinazoizunguka. Kisha tukabainisha jinsi Jamhuri ya Masahaba walivyo amiliana na Hadith hizo, kisha Jamhuri ya Waislamu ikaufuata mwendo wao huo hadi leo hii.

Hakika mafhumu ya Uimamu ndiyo ambayo yamewafarakisha Waislamu punde tu baada ya kufariki kwa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), isipokuwa Mashi’a ndio wamejulikana kwa kuchukua kwao Sunnah hizi kutoka katika njia ya Ahlul-Bayt (a.s.) na Maimamu wao kumi na wawili; ambapo Ahl as-Sunnah wanachukua Sunnah za Nabii kutoka kwa sahaba yeyote. Aidha wameongezea katika Sunnah ya Nabii, Sunnah ya Makhalifa wawili Abubakr na ‘Umar (na utaona katika sehemu zinazofuatia mengi miongoni mwa ushahidi juu ya ukweli huu).

Na tumebainisha namna gani Jamhuri ya Masahaba walivyofanya ijtihad kati ya Waislamu waliotangulia (na waliosifika zaidi kwa hilo miongoni mwao ni Abubakr, ‘Umar, ‘Aisha na Mu’awiyah bin Abi Sufian); mbele ya Hadith za Mtume kuhusu Uimamu. Jambo ambalo limewaweka mbali Maimamu wa Ahlul Bayt (a.s.) katika uongozi wa mambo ya ‘Ummah wa Kiislamu, na hasa baada ya kufa shahidi Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na wakawa ni wenye kupokonywa haki.

Moja kwa moja wamekuwa ni kundi la upinzani ambao hawaoni uhalali wa watawala ambao wameshika uongozi wa Waislamu bila ya haki. Basi wafuasi wa Ahlul Bayt (a.s.) wakawa ni kundi lenye kuchukiwa na watawala wa Waislamu; na hasa Bani ‘Umayyah na Bani ‘Abbas.

Na mgawanyiko wa Waislamu ulikuwa ni makundi mawili yaliyo dhihiri baada ya matukio mawili ya Vita vya Jamal na Siffin, na kufa shahidi kwa Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.). Baada ya kuwa kundi la Ahlul Bayt (a.s.) ni lenye kufichikana katika zama za Makhalifa watatu wa mwanzo kufuatana na siasa ya hekima aliyoifuata Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), kila kundi likawa linadhihirisha dalili na ushahidi walio nao katika haki ya madai yao na kundi lao.

Wakati ambapo wafuasi wa Mu’awiyah bin Abi Sufian, Yazid bin Mu’awiyah bin Abi Sufian na watawala wengine wa Bani ‘Umayyah walikosa hoja na ushahidi wa kupinga Hadith zenye nguvu za Uimamu wa Ahlul-Bayt (a.s.), mmoja wao ambaye ni Seif bin ‘Umar At-Tamimiy ambaye amejulikana kwa uongo na uzindiki kwa maulamaa wa Hadith walio tangulia, akazua kwa msaada wa mabwana zake ambao kwayo amejengea Ushi’a kwa huyu mtu wa bandia; na tumebainisha ubatili wa njama hii ya uongo wa ‘Abdillah bin Saba,’ na hata kama ikadhaniwa kuwa alikuwepo kweli, basi hakika yeye siye ambaye alitangaza uwasii wa Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na kumfanya kuwa Khalifa, bali ni Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) kutokana na Hadith tulizozieleza katika sehemu ya kwanza.

 • 1. Fusuulul-muhimmah cha Ibnu Swabbaagh Al-maalikiy uk. 83, chapa ya Dar al-adh’waa’.
 • 2. Tadhkiratul-khawaas cha Sibtwi Ibn Al-Jawziy uk. 79.
 • 3. Sahih Bukhari j. 4 uk. 52, Kitabul-Jihad, Babu mas’hil-ghubaari ‘ani-r-ra’si fiy sabiylillah.
 • 4. Mustadrak Sahihain j.2 uk. 148, chapa ya Dar al-kitaabil-arabiy.
 • 5. Sahih Bukhari j. 6 uk. 146, Kitabu Tafsir, Babu qawlihi - wal-ladhiyna yaknizuna-dh-dhahaba -.
 • 6. Sahih Tirmidhi j.13 uk. 210, Manaaqibu Abiy dharri (r.a.) na Musnad Ahmad j.2 uk.175.
 • 7. Tarekh Tabari.
 • 8. Tarekh Tabari.
 • 9. Sahih Bukhari j. 4 uk. 122, Kitabul-Jihaad.
 • 10. Sahih Muslim j. 5 uk. 462, Kitabul-birri wa-s-swadaqah wal-adab, Babu man la’anahu-n-Nabiy.
 • 11. Sahih Muslim j. 3 uk. 293, Kitabu-t-Talaaq, Babul-mutwallaqatu laa nafaqata laha.
 • 12. Musnad Ahmad j. 4 uk. 421, Ahmad hakutaja majina yao bali amesema”fulani na Fulani”. Majina yao utayakuta katika Tarekh Tabari.