read

Sehemu Ya Tatu: Shi'a Na Qur'an Tukufu

Shi'a wanaitakidi kuwa (Qur'an ni wahyi wa kimungu ulioteremshwa kutoka kwa Allah -swt- katika ulimi wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) kwa kubainisha kila kitu, nayo-Qur'an hiyo-ni muujiza wa milele ambao wanadamu wameshindwa kupambana nao katika balagha, fasaha na katika ukweli na maarifa ya hali ya juu, haiguswi na mabadiliko, mageuzi wala upotovu, na hii ambayo iko mikononi mwetu tunayoisoma ndiyo ile ile Qur'an iliyo teremshwa kwa Nabii (s.a.w.w.) na atakaye dai yasiyokuwa hayo basi ni mwongo au ni mwenye kukosea au amechanganyikiwa na wote -hao- hawako katika uongofu, hakika hayo ni maneno ya Allah-swt- ambayo hayapatwi na upotovu kwa hali yoyote).1

Na amesema Sheikhul Muhadith Muhammad Al-Qummi ambaye amepewa lakabu ya As-Swaduuq: " Itikadi yetu katika Qur'an ambayo ameiteremsha Allah (s.w.t.) kwa Nabii wake Muhammad (s.a.w.w.) ni ambayo iko baina ya majalada mawili na ambayo iko kwa watu na sio zaidi ya hayo na anayetunasibishia kuwa tunasema zaidi ya haya basi ni muongo”2

Na hayo yanatiliwa nguvu na aliyoyasema Al-Bahansawiy naye ni mmoja wa wanafikra wa Ikhwanul-Muslimin: "... hakika Shi'at al-Ja'afariyyah Al- Ithna-'Ashariyyah wanaona kuwa ni ukafiri kwa anayepotosha Qur'an ambayo 'Ummah umekubaliana tangu mwanzo wa Uislam. na kwamba msahafu uliopo baina ya Ahl as-Sunnah ndiyo ule ule uliopo katika misikiti na nyumba za Mashi'a." Na anaendelea katika kumjibu (Dhahir na Khatib) kwa kunukuu rai ya As-Sayyid Al-Khui ambaye ni mmoja wa maraaj'i wakubwa wa Kishi'a katika zama hizi*:

"Iliyo mashuhuri baina ya Waislamu ni kutokuwepo upotoshaji katika Qur'an na iliyopo mikononi mwetu ni Qur'an yote iliyoteremshwa kwa Mtume (s.a.w.w.)".3

Ama Sheikh Muhammad Al-Ghazali anasema katika Kitabu chake Difau anil-'Aqidati wash-shariah dhidu mata'inil-mustash'riqina "Nimesikia kutoka kwa hawa miongoni mwa ambaye anasema katika majlisi za hadhara: "Hakika Shi'a wana Qur'an nyingine ambayo ni zaidi na inapunguza Qur'an yetu iliyo maarufu."

Nikamwambia: "Iko wapi hii Qur'an? na kwa nini majini na wanadamu hawakuona nakala yake kwa muda wote huu mrefu? Huu uongo ni wa nini? Kwa nini kuwasingizia watu na (kuusingizia) wahyi."4

Ama Hadith ambazo sio Sahih ambazo baadhi wanaweza kuzitegemea ambazo zinaeleza kupotoshwa kwa Qur'an na ambazo zipo katika vitabu vya Hadith katika Shi'a, hakika ni dhaifu na hazikubaliwi na mfano wake ni nyingi katika vitabu Sahih vya Ahl as-Sunnah na tutaonyesha mifano ya hayo katika Sahih Bukhari, tunatanguliza Hadith walizozipokea kuhusu kusahau Mtume (s.a.w.w.) katika baadhi ya Ayah:-

Kutoka kwa baba yake kutoka kwa 'Aisha amesema: "Mtume wa Allah (s.a.w.w.) alimsikia mtu (mmoja) anasoma Surah usiku akasema: 'Allah (s.w.t.) amrehemu kwani amenikumbusha Ayah kadha wa kadha nilikuwa nimezisahau katika sura kadha wa kadha."5

Vile vile katika Sahih Bukhari ni kwamba, walipokuwa wanakusanya Qur'an hawakupata sehemu ya Surah al-Ahzab isipokuwa kwa Khuzaimah Al-Ansar na hii inapingana na ukweli unaosema kuwa Qur'an imepokewa kwa Tawaatur (na watu wengi sana) na wala sio kwa riwayah za ahad (mtu mmoja).

"Tulipokuwa tunanakili karatasi katika misahafu, niliikosa Ayah katika sura ya Ahzaab niliyokuwa namsikia Mtume wa Allah (s.a.w.w.) anaisoma (na ambayo) sikuikuta kwa yeyote isipokuwa kwa Khuzaimah Al-Ansariy, Khuzaima Al-Ansariy ambaye Mtume wa Allah (s.a.w.w.) amejaalia ushahidi wake kuwa ni sawa na ushahidi wa waumini wawili".6

Na katika riwayah nyingine kutoka kwa Zayd bin Thaabit alisema: "…Niliifuatilia Qur'an yote kutoka kwenye vipande vya nguo, mifupa, magome na kwa watu waliohifadhi hadi nikakuta Ayah mbili za sura ya Tawbah kwa Khuzaimah Al-Ansariy ambazo sikuzipata kwa yeyote mwengine"7

Na miongoni mwa Hadith ambazo zinasema wazi wazi kupotoshwa kwa Qur'an ni ambayo ameipokea Bukhari, vile vile katika Sahih yake katika Hadith kutoka kwa 'Umar Al-Khattab: Alitoka 'Umar bin Al-Khattab, nilipomwona anakuja nilimwambia Sa'idi bin Zaid bin Amr bin Naufail: "Hakika leo atasema maneno ambayo hajawahi kuyasema tangu akalie ukhalifa."

Akanipinga na akasema: "Ni kipi kimekufanya udhanie kuwa atasema ambayo hajawahi kuyasema kabla yake?" 'Umar alikaa juu ya mimbari, muadh-dhin alipomaliza, alisimama akamshukuru Allah (s.w.t.) kama inavyostahiki kisha akasema: "Ammaa ba'd, hakika mimi nitawaambia maneno nimejaaliwa kuyasema na sijui huenda kifo changu kiko karibu, atakayeyaelewa na kuyafahamu basi ayasimulie pale atakapoishia na ambaye anaogopa kutoyafahamu simruhusu anisingizie.

Hakika Allah (s.w.t.) alimtuma Muhammad (s.a.w.w.) kwa haki na akamteremshia Kitabu na miongoni mwa aliyo yateremsha Allah (s.w.t.) ni Ayah ya Rajm, tulisoma na tukaifahamu.

Mtume alifanya rajm na sisi tuliifanya baada yake, naogopa watu watakapopitiwa na muda mrefu atakuja sema msemaji wao Wallahi hatupati Ayah ya rajm katika Kitabu cha Allah (s.w.t.) basi wakapotea kwa kuacha faradhi aliyo iteremsha Allah (s.w.t.), na rajm katika Kitabu cha Allah (s.w.t.) ni haki kwa mwenye kuzini ambaye ameoa kwa wanaume na wanawake kama ushahidi ukithibiti au akiwa mja mzito au akikiri (mwenyewe)."8

Na katika Hadith nyingine: "'Umar anatamani kuongeza Ayah hiyo ambayo ameidai kuwa imeondolewa katika Kitabu cha Allah (s.w.t.) yeye binafsi. "'Umar amesema lau kama watu wasingesema 'Umar amezidisha katika Kitabu cha Allah (s.w.t.) basi ningeiandika Ayah ya rajm kwa mkono wangu, alikiri Maa'iz mara nne mbele ya Nabii (s.a.w.w.) kuwa amezini basi akaamuru apigwe mawe.9

Na Ayah iliyodaiwa ni kama ilivyo katika riwayah ya Ibn Majah: "As-shaikhu wa-sh- Shaikha Idha Zanayaa farjumuhumal-battah"10

Na ukweli katika kukaganyikiwa ni kwamba Ayah ya rajm ipo katika Tawrati ya Ahlul-kitab na wala sio katika Qur'an tukufu kama alivyo kanganyikiwa 'Umar ibn al-Khattab.

'Umar amesema: "Mtume aliletewa mwanamume na mwanamke wa kiyahudi wakiwa wamezini akawaambia (wale) wayahudi, Mtawafanyaje?" Wakasema: "(hawa) tunazipaka nyuso zao masizi na tunawafedhehesha", akasema: " Nileteeni Taurati na muisome kama nyinyi ni wakweli.”Walikuja wakamwambia mwanamme katika wanaowaridhia Aa'wari (aliyekuwa na makengeza) soma, akasoma hadi akaishia katika sehemu akaweka mkono wake juu ya sehemu hiyo. Akasema (s.a.w.w.): 'Nyanyua mkono wako', akanyanyua mkono wake basi ikadhihirika Ayah ya rajm. Akasema: “Ewe Muhammad hakika ni juu yake kurujumiwa, lakini sisi tunaficha baina yetu basi akaamuru warujumiwe, basi nilimwona akiwapiga mawe."11

Na kuchanganya kati ya Kitabu cha Allah (s.w.t.) na Taurati ambako 'Umar alitumbukia humo.

Mtume alimtanabahisha 'Umar alipomuona akiwa na karatasi ya Taurati mkononi mwake, Mtume alikasirika sana na akamwamuru 'Umar kutokuisoma na akasema: "Kama Mtume Musa (a.s.) angekuwepo angenifuata?"12

Pia imepokelewa kauli ya kutoka kwa 'Umar kuwa: "Kisha tulikuwa tunasoma katika Kitabu cha Allah (s.w.t.), msiwachukie baba zenu kwani ni ukafiri kwenu kuwachukia baba zenu au hakika ukafiri wenu ni kuwachukia baba zenu."13 (Yaani kuoa wake walio olewa na baba zenu). Na haifichikani kwa yeyote kuwa Ayah hii ni kama ile iliyotangulia haipatikani katika Kitabu cha Allah (s.w.t.).

Tunahamia kwa Sahaba Abdallah ibn Masu'ud ambaye imepokewa kutoka kwake kuwa alikuwa anasoma Ayah ya (Wallaili idha yaghsha...) kwa kuongeza wa dhakar wal-untha, kama ambavyo inajulikana vile vile kuwa Ayah hii iliyozidi haipo katika Kitabu cha Allah (s.w.t.).

Kisha akasema: "Namna gani Abdallah anasoma Wallaili idha yakh'sha, basi nikamsomea - Wallaili idha yakh'sha wannahaari idha tajallaa wadhakari wal-unthaa - akasema Wallahi alinisomea Mtume wa Allah (s.a.w.w.) kutoka katika kinywa chake hadi kwenye kinywa changu".14 Na hiyo bila shaka inapingana na yaliyo pokewa kwa Mtume wa Allah (s.a.w.w.) kwamba amesema katika Hadith mbili zifuatazo chini ambapo haingii akilini, Mtume (s.a.w.w.) kutuamrisha kujifunza Qur'an kwa mtu asiye na hifdhi nzuri.

Kutoka kwa Abdillahi ibn 'Umar amesema:"Huyo mtu sikuacha kuwa nampenda baada ya kumsikia Mtume wa Allah (s.a.w.w.) anasema: 'Jifunzeni Qur'an kwa watu wanne: kwa Abdillahi ibn Mas'ud …(akaanza kwaye)’15

Na amesema: "Hakika anaye pendeza kwangu sana miongoni mwenu ni mbora wenu wa tabia na akasema: Jifunzeni Qur'an kwa watu wanne: Abdallah bin Mas'ud, Salim mtumwa wa Abu Hudhaifah, Ubay bin Ka'ab na Ma'adhi bin Jabal."

Na Muslim amepokea katika Sahih yake kutoka kwa 'Aisha kwamba amesema: Ilikuwa katika yaliyo teremshwa katika Qur'an ('Ashara ridha'atim-ma'alumaatin) na Mtume amefariki ingali inasomwa katika Qur'an.16

Pia katika Muslim ni kwamba (Abu Musa Al-Ash'ari aliwatumia wasomaji wa Basra, na walikuwa wanaume mia tatu na akasema katika aliowaambia: hakika tulikuwa tunasoma Surah tuliyokuwa tunaifananisha kwa urefu na ukali na Surahal-Baraat, isipokuwa nimehifadhi baadhi yake "Lau kaana libni aadama waadiyaani min-malin labtaghaa waadiyan thaalithan, wa laa yamla'u jaufa-bni-aadama illa-t-turaab."17

Na katika Kitabu Al-Itiqan fi ulumil Qur'an cha Suyuti anataja baadhi ya riwayah kwamba Qur'an ina sura mia moja kumi na mbili tu au kwa kuongeza sura mbili Al-Hafd na Al-Khal'i...!18

Na Waislamu wote hawajui kitu kinachoitwa Suratul-hafdi wala Al-khal'i, na mengineyo yasiyo kuwa hayo mfano wa riwayah hizo dhaifu zilizopo kwa Ahl as-Sunnah na ambazo tunatosheka kwa kiasi tulichokinukuu.

Na baada ya hayo je, inajuzu kwa Shi'a kusema kuwa Qur'an ya Masunni imepungua au imezidi kwa kuwepo riwayah zinazosema hivyo katika vitabu vyao vya Hadith? Bila shaka laa! Kwa sababu kongamano la Ahl as-Sunnah ni kauli inayosema kutopotoshwa Qur'an.

Na maadamu hali ni hii, basi ni kwa nini tunaona tuhuma kali kutoka katika baadhi ya waandishi wa siku hizi katika kuwatuhumu Shi'a kwa kupotosha Qur'an kwa kupatikana tu baadhi ya riwayah dhaifu zinazosema hayo, ambazo hazikubaliwi kwao na kuna mifano ya riwayah nyingi katika vitabu sahihi vya Hadith vya Ahl as-Sunnah. Basi ambaye nyumba yake ni ya vioo asitupie mawe nyumba za wengine!

 • 1. Aqaidul Imamiyyah cha Muhammad Ridha Al-Mudhaffar uk. 41 chapa ya 3.
 • 2. I'tiqaadaatu-s-Swaduuq.
  *Amefariki mwaka 1992 AD. - 8/Safar/1413 AH.
 • 3. As-sunnatul Muftaraa 'alayhaa uk. 60.
 • 4. Difaa'un 'anil 'aqiydati wa-sh-shari'ati dhidda mataa'ini-l-mustash'riqiyna.
 • 5. Sahih Bukhari j. 6 uk. 508, Kitabu Fadhlil-Qur'an, Babu nis'yaanil-Qur'an.
 • 6. Sahih Bukhari j. 6 uk. 291, Kitabu-t-Tafsir, Babu - fa minhum man qadhaa nahbahu -.
 • 7. Sahih Bukhari j. 6 uk. 162, Kitabu-t-Tafsir, Babu - laqad jaa'akum rasuulun min anfusikum -.
 • 8. Sahih Bukhari j. 8 uk. 539, Kitabul Muhaaribina min Ahlil-kufri, Babu rajmil-hablaa mina-z-zinaa.
 • 9. Sahih Bukhari j. 9 uk. 212, Kitabul Ahkami, Babu-sh-shahaadati takuunu 'indal-haakim.
 • 10. Sunan Abi Daud
 • 11. Sahih Bukhari j..9 uk.476, Kitabu-t-Tawhid, Babu maa yajuuzu min tafsiyri-t-Tawraati.
 • 12. Haadhihi Naswihatiy ilaa kulli shi'iy cha Abi Bakari Al Jazaairiy uk.8.
 • 13. Sahih Bukhari j. 8 uk. 540, Kitabul Muhaaribina min Ahlil-kufri, Babu rajmil-hablaa mina-z-zinaa
 • 14. Sahih Bukhari j..5 uk. 63, Kitabu fadhailis-Sahaba, Babu manaaqibi 'Ammaar wa Hudhayfah.
 • 15. Sahih Bukhari j. 5 uk.70 -71, Kitabu fadhailis-Sahaba, Babu manaaqibi 'Abdillahi bin Mas'uud
 • 16. Sahih Muslim j.2 uk. 1075, Kitabu-r-radhaa', Babu-t-tahrim bikhamsi radha'aat, chapa ya Daru ih'yaai-t-turaathil-'arabiy.
 • 17. Sahih Muslim j. 2 uk.726, Kitabu-z-zakah, Babu lau anna libni Aadama waadiyayni labtaghaa thaalithan.
 • 18. Al-Ittiqaan fiy 'uluumil Qur'an cha Suyuuti.