Table of Contents

Mkakati Wa 10: Amana

Inasemekana kwamba Amir-ul-Mu’minin, Ali (a.s.) alikuwa akijikunyata na kutetemeka pale ulipofika wakati wa Swala. Alipoulizwa wakati mmoja kuhusu hali hii isiyokuwa ya kawaida, yeye alisema:

“Wakati umefika, wa ile amana ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu aliitoa kuzipa mbingu, ardhi na milima, lakini vikakataa kuibeba na vikawa na woga nayo.
(Mustadrak al-Wasa’il; Kitabu cha Swala, Mlango wa 2, Hadithi ya14)

Hii ni kwa marejeo ya moja kwa moja kwenye Aya ya Qur’an tukufu ifuatayo:

إِنَّا عَرَضْنَا الْأَمَانَةَ عَلَى السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالْجِبَالِ فَأَبَيْنَ أَنْ يَحْمِلْنَهَا وَأَشْفَقْنَ مِنْهَا وَحَمَلَهَا الْإِنْسَانُ ۖ إِنَّهُ كَانَ ظَلُومًا جَهُولًا {72}

“Kwa hakika sisi tulizitolea amana mbingu na ardhi na milima, lakini zikakataa kuichukua na zikaiogopa, lakini mwanadamu akaichukua.Bila shaka yeye ni dhalimu mkubwa na mjinga sana. (33: 72)
Wakati wowote Ma’sum (a.s.) walipokuwa wakisimama mbele za Allah (s.w.t.) katika Swala, viungo vyao vilitetemeka, na kwa sababu ya hofu kubwa, hata idadi ya upumuaji wao iliweza kuhesabika. Walikuwa wakihangaika kana kwamba wameumwa na nyoka na Swala ilikuwa inaswaliwa kama vile hakutakuwa na fursa nyingine kamwe ya kuswali Swala nyingine.

Muhammad, mtoto wa Ya’qub, akimnukuu Imam as-Sadiq (a.s.) katika Furu’al-Kafi, juzuu ya 3, uk. wa 300, Hadithi ya 4 anasema:

‘Baba yangu alikuwa akisema, wakati Ali, mtoto wa al-Husein (a.s.) alipokuwa akisimama kwa ajili ya Swala, alionekana kama shina la mti, ambalo halina kitakacholitingisha labda upepo unaweza kulitingisha.’

Katika kitabu al-‘Illa, Aban ibn Taghlib, akimnukuu Muhammad, mtoto wa Ali ibn al-Husein anasema:
“Nilimwambia Imam as-Sadiq (a.s.): ‘Mimi niligundua kwamba wakati Ali, mtoto wa al-Husein (a.s.) aliposimama kwa ajili ya Swala, rangi yake ilibadilika.’ Yeye akaniambia: ‘Wallahi, Ali ibn al- Husein alijua kwamba alikuwa amesimama mbele ya nani.”(Wasa’il al-Shi’ah; juz. 4, uk. 685, mlango wa 2, Hadithi ya 4)

Hiki ni kigezo bora sana kwetu sisi kutoka kwa Ma’sumin (a.s.) ambao kila neno lao na kitendo chao vyote vilikuwa ni kwa mujibu wa radhi za Mwenyezi Mungu. Kwa hakika ni jambo la kujifaharisha sana kuweza kujiaminisha mwenyewe kwamba Swala utakayoswali itakuwa ni ya mwisho na kwamba unaweza usipate tena nafasi ya kuswali Swala nyingine. Tabia hii inaweza kudumishwa tu kwa watu wachamungu, na uchamungu na hofu juu ya Allah (s.w.t.) ni sifa mbili ambazo unapaswa kutafuta kuwa nazo.

Katika kitabu kiitwacho Uddatud-Da’i, imeandikwa kwamba: ‘Malalamiko ya uombaji wa Nabii Ibrahim (a.s.) yalikuwa yakisikika umbali wa maili moja, kiasi kwamba Mwenyezi Mungu alimsifu kwa kusema: ‘Ibrahim alikuwa mpole, mwenye kuomba na mwenye kutubu.’

Wakati alipokuwa akiswali, sauti ya mchemko kama ile ya bwela ilisikika ikitokea kifuani mwake. Sauti kama hiyo pia ilisikika kutoka kwenye kifua cha Mtume wetu (s.a.w.w.). Fatima (a.s.) alikuwa akitweta katika Swala kwa sababu ya hofu yake juu ya Allah (s.w.t.).
(Mustadrak al-Wasa’il, Mlango wa 2, Hadithi ya 15)