Table of Contents

Mkakati Wa 22: Kukumbuka Kifo

Wanavyuoni wakubwa wamekushauri wewe kujishughulisha na kujikumbusha mwenyewe juu ya kifo kama njia ya kumuogopa Allah (s.w.t.) na kudumisha uangalifu katika Swala zako za kila siku na mawasiliano na Allah (s.w.t.). Dhana ni kuendeleza uchamungu na hofu ndani yako na kuidhihirishia nafsi yako umuhimu wa Swala.

Allah (s.w.t.) anasema katika Hadith al-Qudsi: “Ninamstaajabia yule mtu ambaye ana uhakika wa kifo na bado anacheka (bila ya sababu yoyote)!

“Ewe Mwana wa Adam (a.s.)! Kila siku maisha yako yanapungua lakini bado huelewi? Kila siku ninakushushia neema Zangu lakini huna shukurani Kwangu juu ya (neema) hizo. Wewe hutosheki na riziki Yangu ndogo wala huridhiki na iliyo nyingi.”

Utaweza tu kuogopa kifo kama unayajua yatakayokutokea wewe baada ya kifo. Kwa hakika, Maimam Ma’asum (a.s.) wamekushauri wewe wakati wote kufikiria na hofia kifo na kwamba kifo ni silaha nzito kwa muumini mchaji kumshinda Shetani na majeshi yake dhaifu. Kwa hakika: “Kumbukumbu ya mara kwa mara juu ya kifo hupunguza matamanio ya mtu.”(Imam Ali (a.s.)

Tofauti na imani za baadhi ya watu kwamba kukumbuka kifo na Siku ya Kiyama kunamfanya mtu apuuze mambo ya kidunia na mapato ya mali, imani yetu sisi ni kwamba kukumbuka kifo kunatukinga sisi kutokana na uzembe na vurugu. Yeyote yule ambaye ni mwangalifu kuhusu utendaji wake, mkubwa au mdogo, hatafanya tendo lolote ovu. Inavyoonekana, hii ni mojawapo ya njia zinazofaa kuchunguza kwa makini tabia yako na kuendesha maisha mazuri na ya heshima.

Kwa njia hii, utaweza kuwa na sababu nzito na yenye maana ya kutokupoteza umakinifu wako wakati unapowasiliana na Mwenyezi Mungu (s.w.t.).

Imam as-Sadiq (a.s.) anasema yafuatayo kuhusu athari za kukumbuka kifo na Siku ya Kiyama:

“Kukumbuka kifo kunazima tamaa zisizo na mpaka. Kunang’oa ule msingi hasa wa uzembe na utepetevu. Kwa kukumbusha ahadi ya Allah (s.w.t.), kunaimarisha moyo wa mwanadamu. Kunalainisha ule ugumu wa kiakili wa mwanadamu.

Kunabomoa mabango ya tamaa zisizo na mipaka na uhalifu. Kunazima maovu ya uroho na kuifanya dunia kuwa dhaifu machoni mwa mtu.”
Allamah Taba Tabai (r.a.) ananukuu Hadithi ndefu ifuatayo katika Tafsir al-Mizan: Hakika! Pale mwana wa Adam anapofikia siku yake ya mwisho katika dunia hii, na ya kwanza katika ile ijayo, mali yake, watoto na matendo yake humjia mbele yake. Anaigeukia mali yake na kusema, ‘Wallahi! nilikuwa mwenye uchu juu yako na mlafi. Ni nini ulichonacho kwa ajili yangu?’ Kisha anawageukia watoto wake na kusema, ‘Wallahi! Kwa hakika nilikuwa mpenzi wenu na nilikuwa mlinzi wenu. Ni nini mlichonacho kama akiba kwa ajili yangu?’ Wao watasema, ‘Sisi tutakupeleka kaburini kwako na tutakuzika ndani yake.’

Kisha atayageukia matendo yake na kusema, ‘Wallahi! Nilikuwa sijishughulishi nanyi na mlikuwa ni wenye maudhi kwangu. Ni nini mlichonacho kwa ajili yangu?’ Kwa hiyo yatasema, ‘Mimi ndiye mwenzio ndani ya kaburi lako na vilevile katika Siku ya Mkusanyiko nitakapofikishwa pamoja nawe mbele ya Mola wako.’

Baada ya kifo chake, kama ni mpenzi wa Allah (s.w.t.), yeye anajiwa na mgeni, mwenye kunukia manukato zaidi ya watu wote, mwenye haiba nzuri sana aliyevaa mavazi yaliyopambwa sana, naye atamwambia, ‘Furahia kwa viburudisho kutoka kwa Allah (s.w.t.) na maua kutoka kwenye Bustani ya Neema. Umeshukia mashukio mema.’ Baada ya hapo yeye atasema, ‘Wewe ni nani?’ Ndipo mgeni huyo atakapojibu, ‘Mimi ni matendo yako mema. Ondokana na dunia na uende zako Peponi.’ Na hapo anamtambua yule anayeuosha mwili wake na kwa bidii sana anamuomba mbebaji wake kumharakishia kaburini kwake.

Kisha wakati anapoingia kaburini kwake, malaika wawili wanamjia yeye nao ni wenye kusaili ndani ya kaburi, wakiwa na nywele zilizotengenezwa kwa madaha, wakiandika juu ya ardhi kwa meno yao, sauti zao kama radi inayonguruma na macho yao kama kimulimuli cha radi kinachochiriza.

Wao wanamuuliza; ‘Ni nani Mola wako? Na ni nani Mtume wako? Na ni ipi Dini yako?’ Na yeye anasema, ‘Allah (s.w.t.) ndiye Mola wangu, Muhammad (s.a.w.w.) ndiye Mtume wangu na Uislamu ndio Dini yangu.’ Wao watatamka kwa mshangao wa furaha, ‘Mwenyezi Mungu akuidhinishe katika kile unachokitaka na unachofurahi nacho.’ Na hii ndio maana ya Maneno ya Allah (s.w.t.):

يُثَبِّتُ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ{27}

“Mwenyezi Mungu huwaimarisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Akhera. ..” (14: 27)

Wanalifanya kaburi lake kuwa lenye nafasi kubwa kwa ajili yake kwa umbali wa kiasi macho yake yanavyoweza kuona na wanamfungulia lango la Peponi na kusema, ‘Lala kwa furaha, usingizi wa harusi anayependeza.’

Na ni Neno la Allah (s.w.t.):

أَصْحَابُ الْجَنَّةِ يَوْمَئِذٍ خَيْرٌ مُسْتَقَرًّا وَأَحْسَنُ مَقِيلًا {24}

“Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makazi mema na mahala penye starehe njema” (25: 24)

Na kama ni adui wa Mola wake, basi anamjia mgeni, mbaya wa sura kati ya viumbe wote wa Allah (s.w.t.), katika mavazi na harufu mbaya sana. Na atamwambia yeye, ‘Karibu kwenye starehe ya maji yanayochemka na kuungua kwenye moto wa Jahannam.’ Na yeye (huyo maiti) ndipo anamtambua yule anayemuosha mwili wake na kwa bidii sana anamuomba mbeba jeneza amrudisha nyuma.

Na akishazikwa ndani ya kaburi lake, wakaguzi wanamjia na kumuondoa sanda kutoka mwilini mwake. Kisha wanamuuliza, ‘Ni nani Mola wako? Ni ipi Dini yako? Na ni nani Mtume wako?’ Na yeye anasema, ‘Mimi sijui!’ Kwa hiyo nao wanamwambia, ‘Hukua unajua, wala hukuwa kwenye njia iliyonyooka.’ Halafu wanampiga na rungu la chuma, kipigo ambacho kinamtisha kila kiumbe wa Allah (s.w.t.) isipokuwa majini na watu.
Baada ya hapo wanamfungulia mlango wa Jahannam na kumwambia. ‘Lala katika hali mbaya.’ Hivyo anabanwa katika nafasi nyembamba kama mpini katika kichwa cha mshale, mpaka ubongo wake unatoka nje kupitia kati ya kucha na nyama za vidole. Na Allah (s.w.t.) anamfungulia majoka ya duniani na nge wake na wadudu ambao wanaendelea kumuuma mpaka Allah (s.w.t.) atakapomfufua kutoka kaburini mwake, na atatamani sana kufika kwa Saa hiyo, kwa sababu ya matatizo anayojikuta nayo ndani yake yeye mwenyewe.

Inapendekezwa kwamba mwenye kuabudu afikirie juu ya kifo kabla ya kila swala. Anapaswa ajione kana kwamba saa ya kifo imewadia, na kwamba swala hiyo ni swala yake ya mwisho kwa Mola wake na ni dakika chache za mwisho za kuomba maghfira na kupata Huruma Tukufu. Kama Imam Ali (a.s.) anavyosema:

“Sali Swala yako ya wajibu kwa wakati wake, kama mtu anayeswali swala yake ya muago, na ana wasiwasi kwamba baada ya hii hatapata tena fursa ya kuswali tena. Kama mtu anagundua kwamba kuna mtu pembeni yake anaiangalia swala yake, yeye anakuwa mwangalifu zaidi katika kutekeleza swala yake. Jihadhari! Wewe umesimama mbele ya Anayekuona bali wewe humuoni Yeye!

‘Hata hivyo, jambo muhimu kuhusu suala hili ni kujihisi kuwa mwenye haja – hali ambayo sisi tunaihisi kwa uchache sana. Mioyo yetu haiamini kwamba chanzo cha furaha katika Akhera, na njia ya maisha yanayodumu kirefu, ni Swala.

Tunaichukulia swala kama mzigo wa ziada katika maisha yetu. Tunadhani kwamba ni utezwaji na ushurutishwaji. Kukipenda kitu ni kutambua matokeo yake. Tunayaelewa matokeo yake na moyo unayaamini, na kwa hiyo, hatuhitaji ushauri wowote au maonyo katika kuyapata.

‘Lakini kama tunaamini juu ya kuwepo maisha ya Akhera na kujihisi kwamba tunayahitaji maisha hayo, na kuiona ibada, hasa Swala, kuwa ni msingi wa kuishi huko, na ni chanzo cha furaha katika dunia hiyo, sisi, bila shaka, tutajaribu kufanya juhudi zetu zote kuyapata maisha hayo, na hatutahisi ugumu au uchovu ndani yetu; ama hasa, tutaharakisha kuyapata kwa shauku kamili na uchu mkubwa, na kuhimili kila magumu na kupitia hali zote juu ya lengo hilo.’
(Imam al-Khumeini – Nidhamu za Swala)