Table of Contents

Mkakati Wa 24: Kuepuka Minong’ono Ya Shetani, Aliyelaaniwa

Abdullah, mtoto wa Sinan, anasemekana kwamba alisema:

“Nilimwelezea Imam as-Sadiq (a.s.) kuhusu mtu ambaye alisumbuliwa na waswas (minong’ono ya shetani) katika Wudhu wake na Swala yake, na kuongezea kwamba alikuwa ni mtu mwenye akili sana. Papo hapo Imam as-Sadiq (a.s.) akasema: ‘Ni akili gani aliyonayo, wakati anamtii shetani?’ Mimi nikasema: ‘Yeye anamtii vipi shetani?’ Imam akajibu: ‘Muulize yeye kuhusu chanzo chake naye atakwambia ni kazi ya shetani.’ (Al-Kulayni, Usul al-Kafi, I; Kitab al-Aql Wal-Jahl, Hadithi ya 10)

Katika al-Kafi, Kulayn (r.a.) anasimulia kutoka kwa Zurarah na Abu Basir kwamba wao walisema:
“Sisi tulimuuliza yeye – (yaani, al-Baqir au as-Sadiq (a.s.) kuhusu mtu ambaye alikuwa na mashaka ya mara kwa mara katika Swala yake, kwa kiasi ambacho hakuweza kujua ni kiasi gani amekwisha kuswali na kiasi gani alikuwa hajakiswali bado. Yeye alisema, ‘Anapaswa kurudia Swala yake.’

Sisi tukamwambia, ‘Hiyo inamtokea sana na kila anaporudia Swala yake mashaka pia hujitokeza tena.’ Imam akasema, ‘(Kwa hali hiyo) anapaswa kuyapuuza mashaka yake.’

Kisha Imam akaongezea: “Asimruhusu yule mwovu kuwa na mazoea ya kumwingia mawazoni na kwa kumshawishi yeye kuvunja Swala yake. Kwani shetani ni mwenye inda na anakuwa na mazoea kwa kile alichokizoea. Hivyo, pale ambapo mmoja wenu anakuwa hayatilii maanani mashaka yake na havunji Swala yake mara kwa mara, na hili likifanyika mara nyingi, mashaka hayatajitokeza tena kwake.’”

“Kisha tena Imam akaongeza, ‘Yule muovu anataka kutiiwa, na pale anapokosa kutiiwa basi hatarudi tena kwa yeyote kati yenu.’

Uhakikisho kutoka kwa Maimamu (a.s.) ni kwamba kama hamtamruhusu Shetani kuwaingilia kwenye nafsi zenu wakati wa Swala, basi hana uwezo wa kuwageuza mawazo yenu wakati wa swala. Yeye Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema, “Shetani anaweka pua yake, ambayo ni kama ile ya nguruwe juu ya moyo wa mwanadamu, na anamchochea yeye kugeuka na kuuelekea ulimwengu na kile ambacho Mwenyezi Mungu hakukifanya kuwa halali. Bali pale mtu atakapomkumbuka Allah (s.w.t.), Shetani huondoka kimya kimya na kwenda zake.’ (Majma’al-Bahrayn, uk. 305)

Zaidi ya hayo, kwa vile uhakika, kusadiki, utulivu, uimara, na uaminifu wa moyo vinasababishwa na mwongozo wa kimungu na ushauri wa malaika, unapaswa kumuomba Mwenyezi Mungu kutaka uongofu Wake na msaada wakati wa Swala.

Imam as-Sadiq (a.s.) amesema: “Mtu mmoja alikwenda kwa Mtume (s.a.w.w.) na akasema: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi nakulalamikia kuhusu minong’ono ya shetani ambayo inanisumbua sana wakati wa Swala kiasi kwamba sitambui ni kiasi gani cha Swala yangu ambacho nimekwisha kiswali.’ Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akamwambia:
“Pale unapoingia katika hali ya Swala, piga kwenye paja lako la kushoto kwa kidole cha mbele cha mkono wako wa kulia, kisha useme, ‘Kwa Jina la Allah, na kwa Allah, naweka mategemeo yangu kwa Mwenyezi Mungu, najilinda kwa Allah, Mwenye kusikia, Mwenye kujua, kutokana na shetani, aliyerujumiwa.’ Utakuwa umemshinda yeye (shetani) na kumfukuzilia mbali.”