Kitabu kilichoko mikononi mwako, ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza, kwa jina la Concentration In Prayer (Umakini katika Swala) kilichoandikwa na Jameel Kermalli, Daktari mwanasaikolojia.

Kitabu hiki kinafundisha namna ya mtu kuwa makini katika Swala yake. Kilichomsukuma mwandishi huyu kuandika kijitabu hiki, ni ukweli kwamba sisi kama binadamu hatuko huru kutokana na mawazo ya aina aina ambayo humjia mtu hata wakati akiwa katika Swala, wakati mwingine mawazo huwa makali sana kiasi cha kumbatilishia mtu Swala yake. Ni tatizo kubwa sana ambalo wengi wetu tunalo. Kwa hakika hali hii hutokea kwa kuchezewa na shetani aliyelaaniwa.