read

Aya Ya Hijaab

Kwanza, hebu ngoja tuzisome Aya za Qur'ani Tukufu zinazohusu jambo hili. Ziko Aya tatu katika Sura ya An-Nur.

(1-2) Aya mbili za kwanza ni hizi:

"Waambie waaminio wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, hili ni takaso kwao; bila shaka Mwenyezi Mungu Anazo habari za yale wanayoyafanya.

"Na waambie waaminio wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe "Ziinat" (mapambo) yao “Ma Dhwahara Minha” (Isipokuwa yale yanayodhihirika katika hayo); na waangushe “Khumur” (shungi) zao mpaka “Juyuub” (vifuani) mwao, na wasionyeshe “Ziinat” (mapambo) yao ila kwa waume wao, au baba zao, au baba wa waume zao, au wana wao, au wana wa waume wao, au umbu zao, au wana wa maumbu wao, au wana wa dada zao, au wanawake wao, au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au watu wafikao mara kwa mara wasio watamanifu katika wanaume, au watoto ambao hawajajua siri za wanawake; wala wasipige miguu yao ili yajulikane wanayoyaficha katika mapambo yao; na tubieni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi waaminio, ili mpate kufaulu. (Qur'ani, 24:30-31).

Maelezo ya Maneno Muhimu:

(i) Ziinat:

Ziinat: Ni kile mwanadamu akitumiacho kujipambia kama vile mapambo, nguo na vitu kama hivyo.

(ii) Khumur:

Kwa 'Khumur' zao, yaani kwa shungi zao, wingi wa ‘khimar' ambalo maana yake ni ushungi; unaitwa hivyo maana unafunika kichwa.

(iii) Juyuub:

Wingi wa Jaib; yaani mfuko wa shingo. Kabla ya kuteremshwa Aya hii, wanawake wa Kiarabu hawakuwa na kawaida ya kufunika shingo zao na kwa kawaida mishipi ya shingo ilikuwa chini (walijitwalia mtindo wa karne ya ishirini… "). Hivyo waliamrishwa kufunika shingo zao kwa shungi zao.

(iv) Mahram:

Orodha ya ndugu ambao mwanamke anaruhusiwa kuwaonyesha Ziinat (mapambo) zake inatolewa katika Aya hii. Ndugu hawa wanaitwa "Mahram". Maana ya Mahram na wale ndugu (wa kuzaliwa, kulea au wa ndoa) ambao ndoa kati yao na mtu huyo imekatazwa daima. Hivyo, baba wa mumewe au mkwe ni "Mahram”; lakini dada wa mkeo si Mahram, maana unaweza kumuoa baada ya kufariki mkeo (au baada ya kumtaliki mkeo).

Neno "baba zao" hujumlisha ami (baba mdogo au baba mkubwa) na amu (mjomba).

(v) Illa Ma Dhwahara Minha:

"Isipokuwa yale yaliyodhihirika katika hayo". ltaelezwa baadaye.

Aya nyingine katika Sura hiyo hiyo inamsamehe mwanamke mzee sana kuvaa ushungi.

"Na Al-Qawaaid (wanawake wazee) ambao hawatumaini kuolewa, basi si vibaya kwao “Yadhwa’ana” (kufunua) nguo zao (za kujifunika usoni) bila kuonyesha mapambo; na kama wakichelea ni bora kwao; na Mwenyezi Mungu ni Asikiaye, Ajuaye. (Qur’ani, 24:60).

Maelezo ya Maneno Muhimu:

(vi) Al-Qawaaid: Ni wale wanawake waliokwisha pita umri wa kuingia katika hedhi (damu ya mwezi) na nifas (damu ya uzazi) na si wenye tamaa za ndoa kwa sababu ya uzee wao.

(vii) Yadhwa’ana: Neno hili halina maana ya kuvua vazi (kama vile shati n.k.) kutoka mwilini. Lina maana ya kulaza upande nguo ya nje (kama vile ushungi au blanketi). Hadithi moja inaelezea kuwa “Ataulaza upande Mharuma (Shali au kashida) au nguo ya kujifunikia kwa nje).”

Tofauti hii hudhaniwa kuwa ndio sheria yenyewe kwa ujumla. Wanawake wazee wanaweza kulaza upande shungi zao au "Burqa” inaonyesha kuwa wengine hawaruhusiwi kulaza upande shungi zao. Na hata hao wanawake wazee wameombwa kutolaza upande shungi zao kwa maana ni bora kwao na (pengine kutoa mfano mzuri kwa kizazi kidogo).

Na ziko Aya Nne katika Sura ya Al-Ahzab:

Mbili katika hizo ni hizi:

Enyi wake wa Nabii, ninyi si kama yeyote katika wanawake mkimcha (Mungu), basi msiwe laini katika usemi ili asitamani mtu mwenye ugonjwa moyoni mwake, na semeni kauli njema. Na kaeni majumbani mwenu, wala msionyeshe mapambo sawa na maonyesho ya ujinga wa zamani; … (Qur'ani, 33:32-33).

Maelezo ya Maneno Muhimu:

(viii) Wake wa Nabii: Aya hii inazungumza na wake wa Nabii lakini wanawake wote wa Kiislamu wamejumlishwa ndani yake; kama vile aya nyingi sana zinazozungumza na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) zina maana ya kuzungumza na Ummah mzima. Kwa mfano iko aya isemayo:

"Ewe Nabii! mtakapotoa talaka kwa wanawake; basi toeni talaka katika wakati wa eda zao..." (Qur'ani, 65:1).

Ni imani ikubaliwayo kabisa kuwa sheria za Qur'ani ni kwa Ummah wote ila pale panapoeleza wazi wazi kuwa si kwa watu wengine.

(ix) Ninyi si kama ye yote katika wanawake:

Wanawake wa Kiislamu si kama wanawake wa kikafiri. Hivyo ni lazima watunze cheo chao.

(x) Sawa na Maonyesho ya Ujinga wa Zamani:

"Kukaa majumbani mwenu” ni heshima ya Uislamu; na kujionyesha ni alama ya biashara ya zama za Ujinga na Kufuru.

(5) Aya ya tatu yao ni hii:

“…..Nanyi mnapowaomba (wakeze Nabii Muhammad s.a.w.w.) basi waombeni nyuma ya pazia; hayo ni safi kabisa kwa mioyo yenu na kwa mioyo yao... (Qur'ani, 33:53).

Maelezo ya Maneno Muhimu:

(xi) Aya hii vile vile inazungumza na wakeze Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Inaonyesha wazo la Hijaab kwa mwanamke wa Kiislamu, kuwa ni lazima abakie nyumbani mwake; na wanaume Ghair Mahram wake wazungumze naye inapokuwa lazima tu; na inapobidi kuzungumza naye, wazungumze naye nyuma ya pazia linalowafanya wasionane.

Ilipoteremshwa Aya hiyo hapo juu, Sahaba mmoja alimuuliza Mtume (s.a.w.w.) kama iliwabidi Waislamu kujificha wasionwe na binti zao, mama zao, na maumbu wao pia. Hapo ndipo ilipofunuliwa aya hii ifuatayo:

(6) Aya yenyewe:

"Si dhambi juu yao (wanawake) katika (kuonana na) baba zao, wala watoto wao, wala umbu zao, wala wana wa dada zao, wala wanawake wao, wala wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume; Mwogopeni Mwenyezi Mungu (enyi wanawake); bila shaka Mwenyezi Mungu ni Shahidi juu ya kila kitu (Qur’ani, 33:55).

Hivyo, swali aliloliuliza yule Sahaba likawa limejibiwa.

(7) Aya ya mwisho katika Sura hii ni hii:

"Ewe Nabii, waambie wake zako na mabinti zako na wake wa waaminio wateremshe juu yao "Jilbaab" (shungi) zao; ili wajulikane wazi wazi na wasiudhiwe; na Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mrehemevu. (Qur'ani, 33:59).

Maelezo ya Maneno Muhimu:

(xii) Jalabib: Neno "Jalabib" ni wingi wa neno "Jilbaab".

Jilbaab ni joho kubwa kuliko ushungi na fupi kuliko Mharuma (shari au kashida) ambalo mwanamke hulivaa kichwani na kumfunika mpaka kifuani...

Na inasemekana kuwa "Jilbab" ni blanketi na aina zote za mavazi zifunikazo mwili kama vile mharuma n.k. Na maana yake ni kuwa, ni lazima wateremshe mitandio juu ya miili yao ili izifunike nyuso zao na mabega yao.

Aya hizi zinawaongoza wanawake kama ifuatavyo:

(a) Ni lazima wakae majumbani mwao.

(b) Wasiseme kwa maneno laini wanaposema na watu Ghair-Mahram wao.

(c) Ni lazima liwepo pazia mlangoni.

(d) Wasionyeshe "Ziinat" zao ila kwa wale Mahram wao.

(e) Kama ikiwabidi kutoka nje ya majumba yao (kwa sababu ya haki) waifunike miili yao kwa mitandio.

Kutokana na Aya hizi zote, inaonyesha kuwa ziko hatua mbili za Hijaab (a) Hijaab ya Macho na (b) Hijaab ya nguo.

Hijaab Ya Macho

Wanaume walioamini wateremshe macho yao chini, na wanawake walioamini ni lazima wateremshe macho yao chini. Hakuna aruhusiwaye kumtazama mtu asiye wa umbile lake (la kiume au la kike), ila tu awapo Mahram wake.

Kwa kuwa mwanaume ameamriwa kujitahidi kutafata mahitaji ya maisha, hakuambiwa kuficha mwili wake (ila kwa kiwango fulani tu). Vivyo amelazimishwa kuteremsha macho yake chini na kutowatazama wanawake wasio mahram wake.

Ziko hadithi nyingi sana zisemazo:

"Tazamo (la jicho) ni mshale wenye sumu utokanaona mshale wa Shetani".

"Hakika kutazama kunakotokana na Shetani".

"Jihadharini na kutazama".

Ye yote yule ayajazaye macho yake kwa (kutazama vitu) Haram, (yaani watu wasio Mahram) Mwenyezi Mungu atayajaza macho yake kwa Moto ila tu anapotubia na akarudi (kwenye Uchamungu.

Hadithi nyingi sana zaeleza kuwa tazamo jingine baada ya tazamo la kwanza ni mshale wa Shetani na ni Haramu".

Hijaab Ya Nguo

Tunaweza kulijadili jambo hili chini ya vichwa vya habari vifuatavyo:

1. Kiwango Cha Kujifunika:

Vazi hilo ni lazima liufunike mwili mzima wa mwanamke, ila zile sehemu zilizosamehewa. Kufuatana na hadithi sahihi za vitabu vya Kishia na Kisunni, “mwili mzima wa mwanamke ni Awrah”.

Kwa mfano katika hadithi hii ifuatayo tunaambiwa:

“Hakika wao (wanawake) ni ‘awrah’.

Mwanamke ni ‘awrah’.

Nini maana ya neno "awrah"?

“Via vya uzazi vinaitwa "awrah" kwa sababu ni aibu kuvitazama; na kila kitu ambacho mtu hukificha (kwa sababu ya fahari au aibu) kinaitwa "Awrah"; na wanawake ni “Awrah”.

Kufuatana na maelezo ya kitabu kiitwacho "Al-Urwatul Wuthqaa" kilichoandikwa na Sayyid Kadhim Yazdi, chenye maelezo chini ya kurasa yenye majina ya Mujtahid wote waliohai, kuna aina mbili za mitandio:

(1) Kwanza: ni ule mtandio ulio Wajibu wakati wote:

Huu ni: Kuficha Awratain (sehemu za siri, nyuma na mbele) kutoka machoni pa watu wote, wanaume na wanawake, Mahram, na Ghair-Mahram, walio balehe na wasio balehe.

Tofauti: Mume na mke wanaweza kutazamana. Vile vile mtoto mdogo sana amesamehewa kuifuata amri hii.

Kwa vile ni Haramu kuzifunua sehemu hizi za mwili mbele ya mtu ye yote yule, basi ni Haramu kuzitazama.

Ni wajibu kwa Mwanamke kujifunika mwili mzima (ila uso na mikono yake hadi kwenye vifundo vya viganja jambo ambalo tutalieleza baadaye) kutoka machoni pa watu wote ila mumewe na Mahram wake.

Uso na mikono:

(i) Kiasi upo uwezekano wa mtu fulani kumtazama kwa ashki, basi itakuwa wajibu kufunika uso na mikono pia.

(ii) Kama hakuna uwezekano huo, basi itakuwa ‘Ahwat’ (ni bora) kuzifunika sehemu hizo kwa mujibu wa Fatwa ya Sayyid Mahmuud Husaini Shahrudi, Sayyid Abul Qasim Khui, Sayyid Muhammad Kadhim Shariatmadari, Sayyid Muhammad Redha Gulpaygani na sayyid Hadi Milani.

(iii) Ni haramu kutazama kwa ashki mwili, uso au mkono wa mume au mke, awe Mahram au Ghair- Mahram (Ila kwa mume na mkewe).

(2) Aina ya Pili ya Mtandio inahusu Sala:

(i) Mwanaume ni lazima afunike Awratain zake hata kama hapana mtu wa kumtazama. Na ni Ahwat kuifunika sehemu ya mwili iliyo baina ya kitovu na magoti.

(ii) Mwanamke ni lazima afunike mwili wake mzima pamoja na nywele na masikio ila uso (tangu paji la uso hadi kidevu, kwa urefu ni sehemu yote ya uso yenye upana wa tangu dole gumba hadi kidole cha katikati) mikono (tangu vifundo vya kiganja hadi ncha za vidole) na miguu mpaka penye vifundoni. Ni wajib kufunika sehemu ya ‘zile sehemu zilizosamehewa’ katika amri hii “Min Babil Maqaddamah”.

(iii) Si lazima kwake kufunika mapambo yake wakati wa sala au sehemu za uso zilizokwatuliwa.

(iv) Kama yuko mtu anayeutazama au atakayeweza kuutazama kwa ashki uso wake, mikono yake au miguu yake wakati wa Sala, basi itamuwajibikia kuzifunika sehemu hizi vile vile, si kwa sababu ya Sala, bali kwa sababu ya Sheria nzima iliyotajwa kabla kwa ujumla.

2. Uso Na Mikono

Katika aya ya kwanza imeelezwa kuwa wanawake wasidhihirishe ‘Ziinat' (mapambo) zao ila "Ma Dhwahara Minha" (yale yaliyodhihirika katika hayo)”.

Kuna kutoafikiana kuhusu maana ya haya mapambo yaliyosamehewa kufichwa.

Kipo kikundi (katika Madhehebu za Kisunni na Kishia) kisemacho kuwa maana ya kifungu cha maneno kisemacho “Ma dhwahara Minha" ni uso na mikono, sehemu ambazo kufuatana na maoni yao, mwanamke anaruhusiwa kutozifunika. Ili kuikubali tafsiri hii, ni lazima mtu ajiendeleze maana ya neno “Ziinat” kujumlisha "uzuri wa kimaumbile”.

Kikundi kingine kinasema kuwa kifungu hiki "Ma Dhwahara Minha" kina maana ya yale matukio ambapo sehemu yoyote ya mwili wa mwanamke au pambo linaonekana kwa ajili ya sababu zisizozuilika kama vile kuvuma kwa upepo, au nguo za nje zenyewe.

Tukiachilia mbali hadithi za Masunni, ziko Hadithi nne katika vitabu vya Kishia ambazo wazi wazi au kiundani ndani zinaiunga mkono tafsiri ya kwanza.

Hadithi ya kwanza imesimuliwa na Bwana Mardak bin Abid ambaye alisikia kwa mtu fulani aliyemsikia Imamu Ja’afar Sadiq (a.s.) akisema kuwa haya mapambo yanayoweza kuachwa wazi ni: uso, mikono na miguu (chini ya vifundo).

Hadithi ya pili imesimuliwa na Bwana Qasim bin Urwah aliyeisikia kutoka kwa Imamu Ja’afar Sadiq (a.s.) aliyesema kuwa ina maana ya wanja na pete (ikiwa na maana ya macho na mikono).

Hadithi ya tatu imesimuliwa na Bwana Sadan bin Muslim aliyemsikia Imamu Ja’afar Sadiq (a.s.) akisema kuwa mapambo haya yawezayo kuachwa wazi ni pete na bangili (ikiwa na maana ya mkono tu).

Sasa yule mtu katika hadithi ya kwanza, Bwana Qasim bin Urwah katika hadithi ya pili na Bwana Sadan bin Muslim katika hadithi ya tatu ni watu wasiofahamika kabisa. Hakuna ajuaye mabwana hawa ni nani, ni kiasi gani twaweza kuyategemea maneno yao.

Hadithi ya nne imesimuliwa na Bwana Amr bin Shimr aliyeisikia kutoka kwa Bwana Jabir bin Ansar, kuwa Bwana Jabir alisema kuwa alikwenda pamoja na Mtume (s.a.w.w.) nyumbani kwa Fatima (a.s.) na akamuona (Bibi Fatima) amepauka. (Yaani Bibi Fatima a.s.) hakuufunika uso wake n.k.

Huyu Amr bin Shimr alikuwa muongo mkubwa na wanavyuoni wa Kisunni na Kishia wanasema kwa pamoja kuwa alikuwa na desturi ya kubuni hadithi na kuzihusisha na Mabwana Jabir, Jufi na wengineo.

Zaidi ya hapo hadithi hii inakwenda kinyume na hadithi zikubaliwazo zithibitishazo kuwa Bibi Fatima (a.s.) alikuwa akijifunika kabla ya kumruhusu Sahaba mmoja kipofu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuingia nyumbani mwake, na kuwa hakupenda jeneza lake kuwekwa katika ubao usiofunikwa (kama ilivyokuwa kawaida ya zama hizo) kwa sababu watu watajua urefu wake.

(Hivyo oni lililo sahihi ni lile la kikundi cha pili, lisemalo kuwa maana ya maneno “Dhwahara Minha” ni yale matukio tu ambapo kiungo cha mwili au pambo hufunuka kwa ajili ya sababu zisizozuilika).

Hata hivyo, ni tofauti za kimaandishi tu. Tukija kimatendo Wanavyuoni wote (kwa pamoja) wanasema kuwa kama ipo hatari ya watu kumtazama mwanamke usoni kwa nia mbaya, basi ni wajibu wake mwanamke huyo kuufunika uso wake. Na kufuatana na wasemavyo wengine, ni "Ahwat”.

Sasa ni juu yenu kuamua kati ya Mwenyezi Mungu na ninyi wenyewe kama ipo hatari hiyo katika hii jamii iliyopata mwanga.

3. Uzito

Hiyo nguo ni lazima iwe nzito vya kutosha ili isiweze kuionyesha rangi ya ngozi ya mwili au umbile la mwili.

Ni lazima tuwakumbushe wanawake wetu kuwa shabaha ya Hijaab si kuvaa nguo “yo yote” bali ni kuficha mwili. Nguo zionyeshazo au zilizo nyembamba zinazoonesha rangi ya ngozi ya mwili au umbo la mwili si Halali.

Kama vile Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alivyosema: "Katika zama za mwisho watakuwepo wanawake (Kasiyatin Ariyatin) watakaovaa nguo lakini wakabakia uchi. Kwa hakika hao wamelaaniwa.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) siku moja alimuona bibi arusi aliyevaa nguo nyembamba na akasema: "Si mwanamke aiaminiye Sura ya An-Nur yule avaaye nguo ya aina hii".

4. Kupwaya

Nguo hiyo isibane kiasi cha kuonyesha umbile la mwili wa mwanamke.

5. Nguo Ya Juu Ipasikavyo Kuwa:

(a) Shabaha ya kuvaa nguo hii ya juu ni kuficha "Ziinat". Hii inaonyesha kuwa hii nguo ya juu yenyewe isiwe ya aina inayoweza kuwavutia watazamaji kwa upande wa nguo za ndani za mwanamke. "Ziinat" haziwezi kufichwa na nguo zifanyazo watu waelekeze macho yao kwa mvaaji. Ni aina hii ya nguo iliyokatazwa na aye hii ya Qur'ani:

“…Wala msionyeshe mapambo sawa na maonyesho ya ujinga wa zamani.....” (Qur'ani 33:33).

(b) Wanawake wasivae nguo ambazo kwa ujumla zinafahamika kuwa kwa kawaida huvaliwa na wanaume. Mtukufu (s.a.w.w.) amewalaani wanaume wafanyao mambo kama wanawake na wanawake wafanyao mambo kama wanaume.

(c) Isiwe nguo ya sifa, fahari na upuzi. Kuvaa nguo zakupendeza sana ili kujionyesha hali ya mtu, nguo chafu sana, au nguo zilizokunjana kunjana ovyo ili kuonyesha jinsi mtu asivyojijali, au mtu kuzikataa kanuni za jamii hairuhusiwi. Kujionyesha na fahari ni mambo yasiyofaa katika Uislamu na hayapendwi na Akhlaq za Kiislamu. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema: "Ye yote yule avaaye nguo ya sifa katika ulimwengu huu Mwenyezi Mungu atamvisha nguo ya aibu katika Siku ya Kiama, ambayo imewashwa moto.