read

Umuhimu Wa Hijaabu

Ili kuona jinsi Hijaab ilivyopewa umuhimu katika Sheria za Kiislamu, inatosha kutazama jinsi Sheria na amri nyinginezo zinavyorekebishwa na kubadiliwa ili kuihifadhi sheria ya Hijaab:

(1) Kusali msikitini ni bora kuliko kusali nyumbani. Thawabu huongezeka kwa kadri jamaa iongezekavyo.

Lakini kwa wanawake ni kinyume na hivi. Kuna thawabu nyingi kuswali nyumbani kuliko kuswalia msikitini, na ni thawabu zaidi kuswali katika chumba cha ndani zaidi kuliko kuswali katika baraza au ukumbi.

(2) Sala ya Jamaa: Mojawapo ya misingi ya Sala ya Jamaa ni kuwa pasiwepo “Hayil (kizuizi) kati ya Imamu na Maamuma na kati ya maamuma mmoja na mwingine.

Lakini amri hii si kwa wanawake. Kama wakitaka kuswali kwa Jamaa, ni lazima wasali nyuma ya “Hayil”.

(3) Adhana na Iqamah: Kuadhini na Kukimu vimetiliwa mkazo sana kabla ya sala tano za faradhi. Lakini wanawake wamesamehewa kuadhini na kukimu. Kama wakitaka kufanya hivyo wanaweza kufanya iwapo hapana mtu asiye Mahram wao awezaye kuzisikia sauti zao. Au sivyo itakuwa Haram kwao kufanya hivyo (Ingawa wanaweza kufanya hivyo kwa kunong’ona).

(4) Ni wajibu kwa wanaume kusoma Alhamdu na Sura katika rakaa mbili za mwanzo za sala ya Alfajiri, Magharibi na Isha kwa sauti.

Wanawake wanatakiwa waswali zote kwa kunong’ona.

(5) Sala ya Ijumaa ni Wajibu Aini anapokuwepo Imamu au Naibu wake aliyemteua, na ni Wajibu Aini au Wajib Takhyiri wakati wa Ghaibat kufuatana na Fatwa na Ulama wengi.

Lakini Mwanamke amesamehewa wajibu huu.

(6) Ghusl-i-Mayyit: Ni lazima mwoshaji awe Mwislamu, lakini kama mwanamke Mwislamu atakufa na wako Wanaume Waislamu wasio Mahram wake na Wanawake wa Kikristo, basi ni Iazima yule mwanamke wa kikristo aombwe aoge kisha amuoshe yule maiti wa kike wa Kiislamu.

Mwanachuoni mwingine Muhaqqiq Hilli hakubaliani na maoni haya. Yeye anasema kuwa Ghusl-i-Mayyit ni Ibada na inahitaji kutia Nia na Nia ya Kafir si sahihi. Hivyo badala ya kuwaruhusu Waislamu wa Kiume kumuosha, anasema kuwa ni lazima huyo maiti azikwe bila Ghusl.

(7) Kuna thawabu kubwa kuchukua Jeneza la maiti wa Kiislamu na kutembea katika msafara wa maziko.Wanawake wamesamehewa kushiriki katika shughuli hizi.

(8) Katika Ihram, mwanamke haruhusiwi kufunika uso wake, lakini kama alivyoandika Bwana Muhaqqiq Thani Karki, sheria hii inahusiana na Ihram wala haihusiani na kuwaona watu walio Mahram wake.

Ayatullah Abul Qasim Khui ameandika kuwa mwanamke apendapo kujificha kutokana na watu wasio Mahram wake katika Ihram, anaweza kuvutia chini pembe ye Ihram yake katika uso wake na kidevu chake; lakini ni Ahwat kuwa aweke mkono wake au kitu kingine; chochote badala ya kuiweka nguo hiyo usoni mwake.

(9) Jihad, kupigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni Ibada ipendwayo zaidi.

Wanawake hawaruhusiwi kushiriki katika Ibada hii.

Hivyo tunaona kuwa kila Sheria ya kawaida inapopingana na Sheria ya Hijaab, si hijaab itoayo njia. Kila mara ni ile inayopingana na Hijaab ambayo hutolewa mhanga kwa ajili ya amri ya Hijaab.