read

Utangulizi

Neno “Hijaab” ni neno la Kiarabu lenye maana ya kisetiri, pazia, buibui, mtandio, au ushungi. Neno hili limetumika katika Qur'ani Tukufu kwa maana ya kuwatenga wanawake kutokana na wanaume wanaoweza kuoana nao, lakini hawakuoana nao (wanaume walio Ghair-Mahram wao).

Hivyo, kwa wanawake wa Kiislamu, kutochanganyika na wanaume wageni na kuvaa buibui au ushungi watokapo nje ya nyumba zao, ni amri ya Mwenyezi Mungu, wala si lolote lile miongoni mwa yale wanayoyafikiria wajinga au yale wanayoyasema maadui wa Uislamu; kama tutakavyoona katika hotuba hii.

Hotuba hii ilitolewa katika Semina ya nane ya "Golden Crescent Group" iliyofanyika mjini Lushoto mnamo tarehe 22/10/1977.

Kiini cha Uislamu ni "Kujitoa kabisa ili kutimiza Penzi la Mwenyezi Mungu", kuzifanya fikara na mwelekeo wa mtu kuwa wenye kuzitii Amri za Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu Anasema:

Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri, wawe na hiari katika shauri lao; Na mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotevu ulio wazi." (Qur’ani, 33:36).

Hivyo basi, kama utauliza ni kwa nini Hijaab ni wajibu, jibu pekee liwezalo kutolewa ni, kwa sababu Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wameamua hivyo. Na ni lazima huo uwe mwisho wa hoja zote kwa kadiri mwanamume aliyeamini na mwanamke aliyeamini wahusikavyo.

Katika zama hizi, Hijaabu imelinganishwa na kutoendelea kwa jamii na inafikiriwa kuwa ni ishara ya kifungo cha wanawake. Wahubiri wengi wanafikiria kuwa ni bora kutolizungumzia jambo hili katika majlisi zao. Lakini Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Inapotokea Bid’ah na mwanachuoni asikiseme kile akijuacho (dhidi ya Bid’ah hiyo), basi (mwanachuoni huyo) hulaaniwa na Mwenyezi Mungu, malaika na wanadamu.”

Islamu ni dini thabiti ambayo ndani yake sheria zote na taratibu zote vimerekebishwa vizuri na kama mtu anataka kugeuza sehemu fulani, utaratibu wote utaharibika. Ni lazima uukubali muundo mzima kama ulivyo. Huwezi kuchagua la kuchukua na la kuacha kutoka katika muundo huu.

Uislamu unaamini kuwatenganisha wanaume na wanawake.
Umewapa wanaume na wanawake madaraka tofauti kabisa, kutegemeana na uwezo wao wa kimaumbilee Mwanaume anawajibika kutafuta mahitaji ya maisha kwa ajili yake na jamii yake. Mwanamke amepewa madaraka ya kusimamia mambo ya nyumbani, na kulea watoto chini ya misingi ya Kislamu.

Watetezi wa uhuru wa wanawake huudhihaki mgawanyo huu wa kazi, wakidai kuwa malezi mazuri ya watoto ni kazi duni yenye kuwashusha cheo wanawake. Hawatambui kuwa mpango wao mpya wa kijamii, unaowanyima watoto malezi na uangalizi wa wazazi ndio sababu kubwa ya kuongezeka kwa makosa ya watoto, jambo ambalo baadaye huipasua pasua jamii.

Hijaab, kama tuijuavyo, haikuwepo Uarabuni kabla ya Uislamu. Ilianzishwa na Mtume (s.a.w.w.) mjini Madina baada ya kuteremshwa amri maalum za Qur’ani Tukufu, miaka mingi kabla ya kusilimu kwa watu wasio Waarabu.

Ummul-Mu’uminiin, Bibi Aisha alikuwa kila mara akiwasifu wanawake wa Kiansar (wa Madina) kwa maneno haya "Baraka za Mwenyezi Mungu ziwashukie wanawake wa Kiansar. Mara baada ya kuteremshwa Aya za Sura ya An-Nur waliacha kutoka nje (ya nyumba zao) kama walivyokuwa wakifanya kabla ya hapo. Walianza kuvifunika vichwa vyao kwa nguo nyeusi, kana kwamba kunguru alitua vichwani mwao."

Hadithi nyingine yenye maana hii hii imepokewa kutoka kwa Ummul-Mu’uminiin, Bibi Ummu Salma.

Hivyo basi, jitihada za baadhi ya Makafiri waliojifanya kuwa ni wajuzi sana wa Uislamu ya kuonyesha kuwa Hijaab iliuingia Uislamu Waarabu walipoziteka nchi jirani, hazina maana hata kidogo. Haya ni mojawapo ya misingi ya sheria za Kiislamu. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: "Kuwa na haya ndio Uislamu."