Neno La Mchapishaji

Kitabu kilichoko mikononi mwako, ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza, kwa jina la: “Love in Christianity and Islam.” Sisi tumekiita: “Upendo katika Ukirsto na Uislamu.”

Kitabu hiki, “Upendo katika Ukristo na Uislamu” ni matokea ya utafiti wa kielimu uliofanyika na Mwanachuoni wa Kiislamu, Bi. Mahnaz Heydarpoor.

Bi. Mahnaz Heydarpoor ni mke wa mwanachuoni mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Dr. Mohamed Shomali. Bi. Mahnaz ni mhitimu wa chuo Kikuu mashuhuri cha Qum, Iran. Alikwenda Uingereza kuungana na Mumewe ambaye alikwenda huko kwa ajili ya masomo. Kwa vile na yeye ni msomi aliona asikae bure bali aitumie fursa hiyo kufanya utafiti wa upendo katika Ukiristo na Uislamu, ili kuona dini hizi kubwa mbili zinazungumzia nini kuhusu nukta hiyo na mchango wao katika maadili na uadilifu.

Ili kufanikiwa katika utafiti wake alifanya mazungumzo ya mara kwa mara na Wakristo, kuishi nao katika vyuo vyao vya kidini na kuhudhuria mikutano yao. Matokeo ya shughuli hiyo yote ni kitabu hiki ulichonacho mikononi mwako.

Tumekiona kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote. Kutokana na ukweli huu, Taasisi yetu ya ‘Al-Itrah Foundation’ imeona ikitoe kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili, kwa madhumuni yake yale yale ya kuwahudumia

Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili. Tunamshukuru ndugu yetu, Dr. M. S. Kanju kwa kukubali jukumu hili la kukifanyia tarjuma kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.

Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam.