Sehemu Ya Pili

1. Nguzo Za Maadili Ya Ukristo

Maadili ya Ukristo, kama mfumo mwingine wa kimaadili, yamejengwa kwenye nemsi moja au zaidi. Katika suala la Ukristo, nemsi kwa kawaida zimeidadishwa kuwa ni saba, kwa kuamini kwamba hizi saba, wakati zikiunganishwa na upande wao mwingine wa maovu, yaani, madhambi makubwa saba, zinaweza kueleza upeo wote wa tabia ya mwanadamu. Hizo saba zina zile nyemi nne za ‘asili,’ ambazo zilikuwa za kawaida kwa ulimwengu wa zamani wa kipagani, na nyemi tatu za wema wa ‘kiteolo- jia,’ ambazo zilikuwa kwa makhususi zinahusishwa katika Ukristo. Wema wa asili unaweza kupatikana kwa juhudi za mwanadamu, lakini zile za kiteolojia hupatikana kama zawadi maalumu kutoka kwa Mungu.1

Nyemi ya za asili ni: uangalifu, kadiri, ujasiri, na uadilifu. Orodha hii inasemekana huenda nyuma mpaka kwa Socrates na kwa uhakika wa kuonekana katika Pilato na Aristotle. Wanamaadili wa Kikristo kama vile Augustine na Thomas Aquinas wameiona orodha hii kuwa ni yenye maana. Kwenye hizi nne, Ukristo unaongeza nyemi zile tatu za imani za kiteolojia, matumaini, na upendo.2

Hizi tatu kwa asili ziliwasishwa na Mtume Paul, ambaye hakuzitofautisha tu hizi tatu kama nyemi makhususi za Ukristo, bali alichagua upendo kama ndio mkubwa wa hizi tatu: ‘Hivyo imani, matumaini na upendo hufuata hizi tatu; lakini kubwa ya hizi zote ni upendo.’
(1- Cor. 13:13)

Hivyo katika Ukristo upendo ukawa kiwango cha hukumu, na kama kuna mgogoro wa wajibat, kipaumbele lazima kitolewe kwenye upendo.3

Upendo ni muhimu mno kiasi kwamba safari yote ya kiroho au ya kimuujiza huonekana kama ya upendo. Akitoa mukhtasari wa kile alichosema katika kitabu chake kuhusu imani ya muujiza, William Johnson anaandika: [Imani ya muujiza] ni jawabu kwenye wito wa upendo; na kila hatua imenurishwa na kuongozwa na muwako hai, msisimko wa kibubusa, upendo ambao hauna kusita au kikwazo. Huu ni upendo ambao Paul anasema, ni bora kuliko zawadi yoyote ya kipaji, na hauna mipaka kwa hali yoyote. “Huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahamili yote… upendo kamwe
hauishi…” (1Cor. 13:7, 8.) 4

2. Upendo Kama Msingi Kwa Maadili Ya Ukristo

Matayo anatoa taarifa kwamba Yesu alisema, katika khutba aliyoitoa juu ya mlima, kwamba hakuja kuitengua sheria na manabii bali kuvitimiza:

“Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana amin, nawaambia, mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yatimie. Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Maana nawaambia ya kwamba, haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.” (Mat. 5:17-20) Katika Luka 16:17, tunasoma:

“Lakini ni vyepesi zaidi mbingu na nchi vitoweke, kuliko itanguke nukta moja ya torati.”
(Luk. 16:17)

Hivyo, wakati Yesu anachukuliwa kama mwalimu wa maadili, ni wazi kwamba alikuwa ni mrekebishaji wa mila ya Wayahudi zaidi kuliko mwanzishaji wa msngi mpya (wa sheria). Mila ya Wayahudi ina mwelekeo wa kuweka msisitizo mkubwa kulingana na waraka wa sheria; maelezo ya Yesu katika Injili humuelezea kama anayehubiri dhidi ya huu ‘usahihi wa waandishi na Mafarisayo,’ akitetea roho kuliko waraka wa sheria. Yesu alikuwa tayari kupuuza wajibu wa Sabato, kama ni lazima. Alisema: “Sabato iliwekwa kwa ajili ya mtu sio mtu kwa ajili ya Sabato.” (Mak. 2:27-28).

Halikadhalika Paulo angeweza kula chakula kwa vyovyote, iwe ilikuwa Kosher au la, inategemea iwapo katika hali iliyokubaliwa, huadilisha kwa ajili ya wengine (1: Cor; 19:23-26).

Kama nitakavyoeleza kwa urefu baadae, Yesu alileta moyo wa sheria, ambao kwayo ‘zinatengemea sheria zote na mitume’ (cf. Mt. 22:40) kama moja ya upendo kwa Mungu na kwa jirani yake mtu. Na kwa vile kwa uwazi alikuwa hapendekezi kwamba mafundisho ya zamani ya ‘mitume’ yatupwe, hakuona haja ya kuendeleza mfumo mpana wa kimaadili.

Kwani uadilifu wa Ukristo unabakia kuwa ni suala la ufunuo na uvumbuzi. Hivyo, Ukristo kwa hakika kamwe hauvunji dhana ya uadilifu wa kiyahudi kama suala la sheria ya Mungu ya kuvumbuliwa kwa kusoma na kutafsiri maneno ya Mungu kama yalivyofunuliwa katika maandiko. Katika njia hii, inaonekana kwamba hakuna mgongano kati ya nafasi ya Yesu katika Mt. 5:17-20 na Luk. 16:17 na msisitizo wa Injili nyingine na barua za Paulo juu ya moyo wa sheria.

Kwa hiyo, nafikiri msisitizo wa Yesu juu ya upendo wa Mungu na upendo wa mtu kwa jirani wake kama amri mbili kubwa si za kuchukuliwa kama kukatalia kwa sheria na haja ya kuwa mtiifu kwayo. Hakika, kitu alichokuwa anashauri Yesu ni kwamba watu wake lazima watekeleze mahi- taji yote ya sheria, lakini wakati huo huo lazima waelewe kwamba nukta yote ya hili na njia pekee ya kupata uchamungu ni kumpenda Mungu na upendo wa mtu kwa jirani wake. Kufuata sheria lazima kufanywe na moyo wote na sio juu juu au kama ada tu. Kama Mt. Francis de Sales alivyoshauri,5 baadhi wanaamini kwamba ukamilifu hupatikana katika maisha ya kimaadili; wengine wanaamini kwamba ukamilifu hupatikana katika sala; wengine katika kuziendea Sacramenti mara kwa mara; wengine katika kutoa sadaka.

Lakini, anasema, wanajidanganya wenyewe. Ukamilifu unapatikana katika kumpenda Mungu kwa moyo wote. Mtu anayempenda Mungu kamwe hafanyi kitu cho chote dhidi ya utashi Wake (Mungu) na kamwe haachi kufanya kitu ambacho humpendeza Yeye (Mungu). Hii ndio maana Mt. Augustini alisema: “Mpende Mungu na fanya utakavyo.” Kwa hiyo, hakuna mkinzano kati ya ukubwa wa upendo na utii kwenye sheria.

Ukristo umepokea amri kubwa za uadilifu wake kutoka kwenye Agano la Kale.6 Katika Mark. 12:28-31 tunakukuta kisa muhimu sana: “Na mmojawapo wa waandishi akafika, akawasikia wakisemezana naye akatambua ya kuwa amewajibu vema, akawauliza, Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza? Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israil, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” (Mrk. 12:28-31)

Kisa kama hicho hicho kinapatikana katika Mt. 22:34-40 na kuishia na msemo, ‘Juu ya amri hizi mbili sheria zote na mitume hutegemea.’ Katika Luk. 29:39-40 kisa hiki huishia na swali tofauti na jibu. Katika Luk. 10:25-28 inasema kwamba: “Na tazama, mwanasheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele? Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.”

Nikiwa nimeakisi juu ya dondoo hizi kutoka kwenye Injili na uhusiano wake na sehemu zinazofanana za Agano la Kale, tunaona kwamba Yesu, katika kujibu swali lilioulizwa na waandishi, alinukuu dondoo mbili tofauti kutoka kwenye maandiko ya Kiyahudi ambayo yalikuwa na uzoefu kwa wasikilizaji. Aliziweka pamoja kama pande mbili za sarafu ile ile. Alitaja amri ya upendo kwa jirani sanjari na amri ya upendo kwa Mungu kwenye kiwango cha juu sana na amri iliyo kubwa sana, amri ya kumpenda Mungu.7

Sehemu hizo mbili za Agano la Kale ni: “Sikiliza, Ewe Israili; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. (Kmb. Torati: 6:4-5)

“Usimchukie ndugu yako mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake. Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu; bali mpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi Bwana. (Wal. 19:17-18)

3. Upendo Na Dhana Husika

Baada ya kudokeza mukhtasari wa mjadala kuhusu Amri ya upendo, natu- fungue dhana za ‘upendo’ na visawe vyake. Kumekuwepo na fafanuzi tofauti zilizowasilishwa kwa ajili ya dhana ya ‘upendo.’ Kila kundi la wanafikira limesisitiza vipengele fulani vya dhana hii. Baadhi ni vya kifilosofia, kwa mfano, ufafanuzi wa upendo kama, ‘upendo wa kulingana au muungano na kile ambacho katika njia fulani hushikwa kama zenye hulka moja.8

Chervin katika kitabu: Church of love anasisitiza elementi tatu za upendo ambazo huonekana kukubalika kiujumla. Moja ni kwamba upendo ni tendo la kujitoa mwenyewe. Pendo sio tu kutoa kitu kwa mpendwa, huhitajia wewe kujitoa nafsi yako kwa mpendwa. Kwa mfano, kama kijana mwanamume anampa mke wake zawadi nyingi, lakini yeye mwenyewe akajitoa, mke atakuwa hana raha. Kipengele hiki cha upendo wa Mungu kwa ajili ya watu hujulikana kwa kuchukulia ukweli kwamba Amemtoa Mwanae wa pekee kwao.

Kwa maneno mengine, Amejitoa Mwenyewe kupitia kwa Mwanae. Juu ya kile ambacho Kanisa hufundisha kuhusu Mungu Baba, Katekisimo ya Kanisa la Uingereza inasema: “Kanisa linafundisha kwamba Mungu Baba aliniumba mimi na wanadamu wote, na kwamba katika upendo wake alimtuma Mwanae kupatanisha ulimwengu kupitia kwake.”9

Elementi ya pili ni kwamba upendo katu si wenye kutulia. Mpenzi hajitoi tu mwenyewe na kisha akapumzika. Badala yake, upendo huelekea kwenye urafiki wa karibu sana wa muungano ulio mkubwa na mkubwa mno. Imedokezwa kwamba “Kwa upendo mtu huachana na nafsi yake, kama ilivyokuwa, na kufanya makazi yake pamoja na mtu mpendwa.”10 Elementi ya tatu ni kwamba upendo unatengeneza. Upendo humfanya mpenzi kuishi katika njia ambayo humridhisha mpenziwe. Upendo wa mtu kwa Mungu humgeuza mtu kuwa muumini wa kweli.11

Mtu lazima aweke akilini kwamba kihistoria kumekuwa na mhamo katika Agano Jipya kutoka uelewaji wa upendo wa Kiyunani, ulioelezewa katika dhana ya Ki-Plato ya eros, kwenda kwenye uelewaji wa kibibilia wa upendo - agape. Ingawa upendo wa ashiki umekuwa mara kwa mara ukielewe- ka hasa kama matamanio ya kijinsia na hisia kali za mapenzi, mapokezi (classical) yake kidini na maana ya kifilosofia ilikuwa ni ‘upuuzaji wa nguvu za kiroho’12 au ‘hamu ya udhanifu ya kupata ubora wa juu wa kiroho na kielimu’ (Britannica, 1997).

Ukristo wa mwanzo ulichukulia eros (mungu wa upendo na matamanio ya kijinsia) kama muundo wa fahari kubwa ya ubinafsi na kujihami, kwa hiyo, Agano Jipya la Kigiriki halikutumia neno eros bali kwa kiasi mara chache sana neno ‘agape’. Agape lilitafsiriwa kwa Kilatini kama ‘caritas’ na hivyo likajitokeza kwenye Kiingeza kama ‘charity’ na baadye ‘upendo’. Katika Agano Jipya agape maana yake upendano kati ya Mungu na mtu. Neno kujuzu linakwenda mpaka kwenye upendo wa rafiki yake mtu tazama 1Yona 4:19-21: (“Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza. Mtu akisema,

Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; akisema, kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemuona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumuona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.”) Brett anaandika: “Upendo wa Ukristo ndio kitu unachonidai kiuhalisi kwa sababu wewe ni mtu mwingine kama mimi. Kuna elementi ya msingi wa usawa iliyojiingiza; ni lazima tuwapende jirani zetu kama sisi wenyewe.”13 (uk. 43)
Lazima ikumbukwe kwamba agape ilikuwa inatumika vile vile kwa maana ya ‘Sherehe za upendo’. Kipndi cha wakati wa karne ya kwanza AD, jumuiya za Kikristo zimejijenga kwenye vitengo vinavyojitegemea na walianza kujiona wenyewe kama Kanisa. Katika wakati huo walifanya aina mbli tofauti za ibada: ya kwanza, mikutano katika mtindo wa sinagogi ambao ulikuwa wazi kwa wadadasi na waumini na ilikuwa ina kusoma kutoka kwenye maandiko ya Wayahudi na ya pili, agape, au ‘sherehe za upendo’, kwa waumini tu. Ilikuwa ni chakula cha urafiki ambacho kwacho masikini walikaribishwa. Mtindo huu wa ibada ya pili, ilikuwa ni chakula cha jioni ambacho kwacho washiriki walishirikiana na wakati ambapo sherehe fupi, kukumbuka Chakula cha mwisho cha jioni, kufanya kumbu kumbu ya kusulubiwa msalabani.

Hii vile vile ilikuwa ni sherehe ya kutoa shukurani; jina la Kigiriki kwa ajili yake ni Eukaristi, ikiwa na maana ya ‘utoaji wa shukurani’. Chakula hiki cha wote taratibu kikawa hakiwezikani kwa vile jumuiya za Kikristo ziliongezeka na kuwa kubwa, na kwa hiyo Chakula cha Bwana kikawa kinafanyika kwenye hitimisho la sehemu ya umma ya ibada ya maandiko.

Dhana kama hiyo hiyo ni ‘charity’ (sadaka) (tarjuma ya neno la Kigiriki agape, vile vile lenye maana ya ‘Upendo’). Sadaka ni muundo wa hali ya juu sana wa upendo, upendano kati ya Mungu na mtu ambao hufanywa dhahiri katika upendo usio na choyo wa marafiki zake mtu. Katika teolojia na maadili ya Kikristo, sadaka ni kitu bora na cha hali ya juu sana kilichooneshwa katika maisha, mafundisho na kufa kwa Yesu Kristo.

Juu ya fikra ya Ukristo kuhusu sadaka, Mt. Augustine anaandika: “Sadaka ni wema ambao wakati tabia zetu ziko sawa sawa kikamilifu, hutuunganisha na Mungu kwani kwazo humpenda Yeye”. Kwa kutumia ufanunuzi huu na fafanuzi nyingine kama hizi kutoka kwenye simulizi za Kikristo, wanateolojia wa karne za kati (Karne za 15-17 AD.), hususan Mt. Thomas, ameiweka sadaka ndani ya nemsi za kiteolojia (sanjari na imani na matumaini) na akabainisha jukumu lake kama ‘msingi au chimbuko’ la vyote. Ingawa mabishano ya Mageuzo ya Kanisa (kati ya karne ya 16) yalishughulika zaidi na ufafanuzi wa imani kuliko matumaini au sadaka, wanamageuzi walitambulisha upekee wa agape ya Mungu kwa mtu kama upendo usio stahili. Kwa hiyo, walitaka kwamba sadaka, kama upendo kwa mtu, iwe imetegemezwa sio juu ya matamanio ya lengo lake, bali juu ya mbadiliko wa maudhui yake kupitia nguvu ya agape ya kimungu.

Neno la Mt. Augustine kwa tathimini ya uadilifu ambayo hushawishi tabia ni amor (upendo). Amor ni nguvu ya maadili ambayo humsukuma mtu kwenye kitendo. Bidhaa zote duni ni za kutumiwa kwa njia au msaada wa kwa ajili ya bidhaa za hali ya juu; ni za hali juu tu zenye ‘kufurahiwa’ kama hatima ya mwisho ambayo kwayo moyo umewekwa. Bidhaa za hali ya juu ambazo kwazo kufaulu pekee kwa mtu hufikia ukamilifu wake, kwa (maneno ya) Mt. Agustine ni, Mungu ambaye asili Yake ni agape. Itakuwa mshiriki katika agape ya kimungu, upendo wenyewe. Mungu atajitoa Mwenyewe kwa watu, na kwa kushirikisha upendo Wake, watu watapen- dana kama Anavyowapenda wao, wakichukuwa kutoka Kwake uwezo wa kujitoa wenyewe kwa wengine.

4. Upendo Wa Mungu

Ni wazi kutokana na kile tulichosema mpaka sasa kwamba katika Ukristo upendo umehusishwa kwa wote; Mungu na wanadamu. Hata hivyo, kuna tofauti muhimu kati ya upendo wa Mungu na wa mwanadamu. Tofauti moja ni kwamba huu wa kwanza ni halisi, miliki, ambapo wa mwisho ni kiarifu. Sababu kwa ajili ya hilo ni ukweli kwamba Mungu ni pendo, lakini wanadamu wanaweza tu kufanya upendo. Wanaweza kupendeka na wenye kupenda, lakini ni Mungu tu pekee ndio pendo. Ukweli huu unaelezewa kwa uwazi mara mbili katika dondoo ifuatayo:

“Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni pendo. Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu. Wapenzi, ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote.

Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu. Katika hili tunafahamu kuwa tunakaa ndani yake, naye ndani yetu, kwa kuwa ametushirikisha Roho wake. Na sisi tumeona na kushuhudia ya kuwa Baba amemtuma Mwana kuwa Mwokozi wa ulimwengu.

Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu. Nasi tumelifahamu pendo alilo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.” (I.Yoh; 4:8-16)

Imehojiwa14 kwamba kwa vile upendo ni lengo la msingi la kuingiliana Kwake na binadamu, pamoja na kujionesha Yeye Mwenyewe, na upendo usio na kipimo na nje ya mipaka ya ulinganishaji, upendo unaweza kuchukuliwa kama sifa mahususi zaidi ya kuwepo Kwake. Upendo ni asili Yake na kwa hiyo, ni jina sahihi kwa ajili Yake. 15

Mungu amewapenda wanadamu ‘kwa upendo usio kikomo’ (cf. Jer. 31:3). Mungu alikuwa wa kwanza kutupenda sisi. Tulikuwa hatupo bado, wala ulimwengu haujaumbwa bado, lakini tayari alikuwa ametupenda. Alitupenda wakati wote Yeye alikuwa Mungu na wakati wote Yeye Mwenyewe akiwa amejipenda.

Upendo wa Mungu kwa wanadamu umeoneshwa katika kuwepo kote na historia ya wanadamu: kama watu binafsi au kama jamii ya wanadamu. Upendo Wake umedhihirishwa katika uumbaji Wake wa wanadamu. Upendo Wake umedhihirishwa katika ulingano wa Agano la Sinai, katika uingiliaji Wake wote katika historia ya Israil, katika kuwepo Kwake wakati wote katikati ya watu Wake na katika kuendelea Kwake kuwakusanya tena na tena baada ya kuanguka kwao kabisa.

Mungu huwapenda wanadamu kiasi kwamba, sio tu kwamba Aliwapa vyote walivyo navyo, bali vile vile amefanyia kila kitu katika ulimwengu kwa faida yao.

Kama Mt. Augustino alivyodokeza, ‘kila kitu katika ardhi au juu ya ardhi huzungumza nasi na kutushawishi sisi kumpenda Yeye, kwa sababu vyote hutuhakikishia kwamba Mungu amevifanya kwa ajili ya upendo kwetu. Hili ndilo wazo lote kwa urahisi mtu anaweza kuelewa kutoka dondoo ifuatayo ya Zaburi katika Agano la Kale:

“Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na mwana wa Adamu hata umwangalie? Bado umemfanya mdogo kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima; umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umeviweka vitu vyote chini ya miguu yake. Kondoo, na Ng’mbe wote pia; Ndege wa angani na samaki wa baharini; Na kila kipitacho njia ya baharani.” (Zab.8:4-8)

Upendo wa Mungu kwa mtu hauna kikomo juu ya viumbe wote wazuri ambao Mungu amempa mtu. Kama nilivyotaja mapema, mtazamo wa Ukristo ni kwamba upendo wa Mungu katika ubora wake umejitokeza kati- ka kujitoa Mwenyewe kupitia kwa Mwanawe. Kwa mujibu wa Mt. Yohana, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanawe pekee…”
(cf. Yoh. 3:16)

Katika Ukristo, dhana ya upendo ya ubaba wa Mungu ni wa maana sana: Upendo wa Mungu kwa wanadamu unafananishwa na ule wa baba kwa watoto wake. Kwa mfano, katika Agano Jipya Mungu anatajwa kama, “Baba yetu uliye mbinguni…” (cf. Mt. 6:9) na kwa vile Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kuomba namna hii: “Baba yetu uliye mbimguni jina lako litukuzwe…” aya hii huchukuliwa kuwa sababu nzuri ya kufikiria kwamba Mungu anaweza kuwa na anapenda kuitwa ‘Baba.’16

Ni Baba aliye mbinguni ambaye “…Maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, na huwanyeshea mvua wenye haki na wasio na haki.” (cf. Mt. 5:45) Upendo wa Mungu wa ubaba hujidhihirisha wenyewe kwenye nadhari Yake kwa masikini (cf. Mt. 6:32), katika kuhusika Kwake kukubwa kwa mateka na wanaoonewa (cf. Luk. 4:18,19) na hata mkutano wake na wenye dhambi, imma wakiwa wanamtafuta au (cf. Luk. 15:4-7) au kwa imani akiwangojea ili aweze kusherehekea na kwa furaha akaribishe kurudi kwao (cf. Luk. 15:11-32)

Vile vile kuna mwelekeo katika fikra ya Ukristo kulinganisha upendo wa Mungu kwa wanadamu kibinafsi au kwa pamoja kwa ule wa bwana harusi na biharusi. Graham anahoji kwamba ulinganishi kama huo umethibitishwa kwa mujibu wa maandiko na vile vile kifilosofia. Anaamini kwamba hii ni karibu mno ya maafikiano ya kidunia. Anasema:

“Bwana wetu, ikiwa katika ardhi, uliridhia kudokeza Wewe Mwenyewe uhusiano kama huo na wazo hilo limekuwa sehemu ya kaida ya Katoliki. Mtu hanabudi kukumbuka ushawishi wa wimbo wa nyimbo za Solomon juu ya lugha ya kiroho kwa ajili ya uthibitisho wa hili.”17

Ni muhimu kutambua kwamba hata upendo wa viumbe kwa Mungu uko moja kwa moja katika deni la Mungu. Kama anavyosema Graham, “Mambo ya awali ya ndoa kubwa kati ya mbingu na ardhi, kama itakavy- oweza kutarajiwa, ni ya Mungu peke yake. Ni sehemu ya bwanaharusi kutoa maneno (ya posa) kwanza.18

Juu ya vipi mtu anaweza kutekeleza jukumu lake (pamoja na kumpenda Yeye) na kushinda ushawishi wa dhambi, katekesimo ya Romani Katoliki inaelezea: “Matayarisho ya mtu kwa ajili ya kupokea baraka tayari ni kazi ya baraka.” (na. 2001) Katekisimo iliyosahihishwa ya Kanisa la Uingereza inaandika: “Naweza kufanya mambo haya tu kwa msaada wa Mungu na kwa baraka zake. Kwa baraka za Mungu nina maana kwamba Mungu Mwenyewe hutenda ndani ya Yesu Kristo ili kusamehe, kutia moyo, na kuniimarisha kwa Roho Mtakatifu.” (Q. 26 & Q. 27).

Kwa ujumla, mtu anaweza kusema kwamba, tofauti na upendo wetu imma kwa Mungu au kwa wanadamu wenzetu, ambao ni jibu lisilo na hisia kwa mpendwa, upendo wa Mungu ni wenye kujenga na mashughuli. Kwa Mungu sio hali ya kwamba hutambua kitu fulani kinachopendwa kwa mtu mpendwa; bali hutoa sifa zinazofaa kwenye vitu na ‘hii kwa usahihi ndio upendo Wake kwao.’ Kama Mt. Thomas Aquinas alivyosema: “Upendo wa Mungu hushawishi na kutengeneza wema ambao uko katika vitu.” Kwa hiyo, Mungu hatupendi sisi kwa sababu ameona wema fulani kwetu; ni kwa sababu anatupenda ndio tukawa na wema.

Hivyo katika upendo wa Mungu tunaona ukamilifu na msingi bora usio na ubinafsi. Hakuna kitu pale kabla ya tendo Lake la upendo, hivyo hapati chochote kutoka kwa mpendwa, au kutoka kwenye pendo lenyewe. Mungu ana uhai wote na wema ndani yake, na kwa hiyo, hapati cho chote kwa kutupenda sisi. Haiwezekani kufikiria kwamba Anaweza kushiriki au kupata kutokona na kile ambacho tayari anacho.

Kwa kawaida swali hujitokeza; ni kwa nini Mungu aumbe ulimwengu. Kuna jibu la pamoja katika kaida ya Ukristo. Mungu aliumba mbingu na ardhi ‘kuonesha ukweli Wake Mwenyewe na wema na uzuri.’19
Tunaona katika kitabu cha Mifano kwamba, ‘Bwana amefanya vitu vyote kwa ajili Yake Mwenyewe.’ (Mif. Xvi, 4)20 Graham anaongeza kwamba ‘itakuwa sawa na dhambi ya mauti katika Mungu kutengeneza ulimwengu si kwa lengo lingine bali kusaidia wema mkamilifu ambao ni yeye.’21 Anahoji kwamba ni asili ya kile ambacho ni kizuri kuwasiliana chenyewe na wengine (Banum est diffusivum sui). Uzoefu vile vile huelezea kwamba, kwa kawaida watu wema ni wakarimu, wasio na ubinafsi na uwezo wa kuingia kwenye mawazo na hisia za watu waliomzunguka, ambapo watu wabaya ni wachoyo, wabinafsi na wanashindwa kuanzisha urafiki na wengine na kuwa na huruma nao.

5. Upendo Wa Mwanadamu Kwa Mungu

Upendo ni uhusiano wa pamoja kati ya Mungu na wanadamu, na hakika, ni kwa uhusiano huu kwamba Ametuumba sisi. Tunalipa fadhila za Mungu kwetu sisi, ambazo zimedhihiri zenyewe katika neema Zake zisizo na mpaka juu yetu, angalau kwa kumpenda Yeye.

Katika dondoo, iliyojaa umaizi, Mt. Bernard anaandika: “Je, Hapaswi kupendwa kwa kulipa, wakati tunafikiri nani amependwa, Amempenda nani, na kiasi gani Alipenda? Kwani ni nani Yeye kwamba apendwe? Yule yule Ambaye kila roho hushuhudia: “Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu; sina wema ila utokao kwako” (Zab. 16:2 vulg). Na je, sio upendo wake ambao ni fadhila ya ajabu ambayo “…hauta- futi mambo yake…?” (1Kor. 13:5). Lakini kwa nani umedhihirishwa upendo kama huo usioelezeka? Mtume (Paulo) anatuambia: “kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake…” (Rum. 5:10). Hivyo basi alikuwa ni Mungu ambaye alitupenda sisi, ametupenda bila kizuizi, na alitupenda sisi wakati tukiwa bado ni maadui. Na ni ukubwa uliokuaje wa upendo Wake huu? Mt. Yohana anajibu: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amuaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” (3:16)22

Clara Lubich, muasisi wa Facolare movement, anaandika kuhusu uwezo wa kiroho na ule wa marafiki zake: “Hadhi ambayo kwayo ametunyanyua, kwetu huonekana ni ya hali ya juu sana, na uwezekano wa kumpenda Yeye kwa kumlipa huonekana ni wa juu mno na usiostahiki kiasi kwamba tumezoea kurudia kusema: “Sio kwamba tunapaswa kusema: lazima tumpende Mungu, bali tuseme: Ee vile ambavyo tunaweza kukupenda, Bwana… vile ambavyo tunaweza kukupenda kwa moyo wetu huu mdogo”23

Upendo kwa Mungu hauna mpaka. Kama Mt. Bernard alivyosema: “Kipimo cha upendo Kwake ni upendo usiopimika.” Sababu yenyewe ni kwamba upendo wetu kwa Mungu, Ambaye wa milele na Asiyepimika, Ambaye ametupenda sisi mwanzo na bila masilahi yoyote binafsi, hauwezi kuwa na mpaka.

Naam hakika, upendo wa mwanadamu kwa Mungu una daraja tofauti. Kama tulivyoona mapema, katika dondoo mbali mbali za Bibilia, Yesu aliomba kumpenda Bwana Mungu wako “kwa moyo wako wote, na kwa nafsi yako yote, na kwa akili yako yote, na kwa nguvu zako zote.” Hili ni lengo la safari ya ki-Irifani. Upendo kwa Mungu waweza kushuhudia kufikia hatua ambayo huenea kwenye moyo wote wa mpendwa mpaka kufikia hali ambayo kwamba hajifikirii tena yeye mwenyewe au kitu kingine chochote zaidi ya Mungu.

Katika ukristo upendo kwa Mungu unaaminiwa kuwa wa wote, yaani, umetekelezwa na viumbe wote. Wakati anamuomba Mungu Mt. Augastino alionesha ukweli ule ule. Alisema: Ee Mungu, Ambaye hupendwa kwa kujua au bila kujua na kila kitu kilicho na uwezo wa kupenda.”
Akielezea nukta hiyo hiyo, Graham anahoji kwamba viumbe wote, pamoja na wanadamu, hutegemea kuwepo kwao juu ya Mungu, na kwa hiyo, lazima watambuliwe kama wampendao Mungu, wakinyoosha mikono yao kimya kuelekea Kwake katika shukurani kwa kitendo Chake uumbaji.”24

Kisha anaongeza kwamba kuna maana nyingine ya kumpenda Mungu, ambayo ni ya wanadamu pekee. Wanadamu wana uwezo wa kumpenda Mungu kwa kudhihirisha na kwa fahamu. Upendo huu kama ilivyo, huja baada ya ujuzi wa uainishaji wa Mungu. Tutaona katika sura ijayo kwamba kuna mtazamo mwingine ambao ni wa ma Irifani wa Kiislamu na mafilosofa ambao hukubali baadhi ya upendo wa fahamu ya Mungu katika viumbe wote, kama ilivyo, umetanguliwa na ujuzi wa uainishaji wa Mungu.

Kumpenda Mungu hakutuhitajii sisi kuacha vitu vyingine. Ni kweli kwamba ukaribu kwa Mungu katika maana hututaka sisi kujitoa kutoka kwa viumbe, wakiwemo hata sisi wenyewe, lakini hili ni kutafuta tu kwamba hakuna kinachoweza kusimama kama mshirika kwa Mungu, Mwenye kutegemewa rehema Yake. Kila kitu cha thamani kimehifadhiwa kwetu katika Mungu.

Kwa maneno mengine, “Hakuna kilicho kitukufu au cha taarifa nzuri ambacho hatimaye kitaachwa kwa ajili ya sadaka25 Katika ushuhuda wake anaelezea nukta hiyo hiyo kwa uzuri mno: “Lakini ninapenda nini, wakati ninapokupenda Wewe? Sio urembo wa miliki, sio ulinganifu maridhawa wa muda, wala ung’aavu wa mwanga, ufurshishao mno macho yetu, wala sauti tamu za nyimbo mbali mbali, wala harufu ya manukato ya maua, na lihamu, na viungo… hakuna katika hivi ninachokipenda, wakati ninapompenda Mungu wangu; na bado napenda aina ya nuru, na nyimbo, na manukato, na nyama, na kukumbatiana, wakati ninapompenda Mungu, nuru, sauti tamu, manukato, na nyama, mkumbatiano wa mtu wangu wa ndani: ambako hung’ara kwenye nafsi yangu, ni sehemu gani isiyoweza kudhibiti…Hiki ndicho nipendacho, wakati ninapompenda Mungu.”
(X, Vi, 8)

6. Upendo Wa Mwanadamu Kwa Mwanadamu Mwenziwe

Kama nilivyotaja mapema, upendo wa mtu kwa Mungu huendelea mpaka kwa jirani, kwa wanadamu wenziwe. Upendo huu ni wa wote pamoja na wenye dhambi, wasio Wakristo na maadui. Sasa ngoja tuchunguze kwa urefu zaidi upendo kwa wenye dhambi, wasio Wakristo na maadui.

Baadhi ya misemo ya Agano Jipya (1Yoh. 4:7- 5:4) huzungumza ulazima wa upendo kwa Wakristo wenziwe. Kwa hakika, utekelezaji wa upendo wa jirani ndani ya duru ya wanafunzi (wa Yesu) ulikuwa ni wa tabia ya wazi ya Kanisa la mwanzo. Usharika wa Ukrtisto, na zaidi ya yote, vyama vidogo vidogo na madhehebu, walidumu kwa karne nyingi kwa sababu ya ukweli kwamba ndani ya jumuiya zao upendo wa jirani ulikuzwa katika hali juu sana katika muundo wa usimamizi wa kiuchungaji, ustawi wa kijamii, na msaada katika hali zote za maisha.

Hata hivyo, upendo wa Ukristo haukuishilizwa kwenye tabaka yoyote au kundi la watu. Kinyume chake, kipengele jipya katika maadili ya Ukristo ilikuwa kwamba kilivuka vikwazo vyote vya kijamii na kidini na kumuona jirani katika hali ya mwanadamu anayeteseka sana. Upendo wa kijirani lazima utekelezwe bila ‘upendeleo’ (James 2:9). Katika tafsir ya Luka kisa mashuhuri ambacho kwayo amri ya upendo inaelezewa, mwanasheria anamuuliza Yesu: “Ni nani jirani yangu?” katika kujibu Yesu anaelezea kisa cha Msamaria Mwema. Katika kisa hiki jirani ni mgeni, mtu asiye tegemewa (kusema kweli ni, mtu aliyepuuzwa) ambaye hahusiki na jumuiya hiyo. (Luk. 10:29-37)

Juu ya upendo wa wote, Chiara Lubich anasema: “Ni upendo ambao hujua namna ya kumkaribisha jirani aliyepotea kuridi – iwapo huyu ni rafiki, kaka, dada, au mgeni – na humsamehe mtu huyu mara idadi zisizo na kikomo.

Ni upendo ambao husherehekea zaidi juu ya mwenye dhambi ambaye hutubia kuliko juu ya watu wema elfu moja.”26 Anaongeza kwamba upendo huu “Upendo huu hauna kipimo na hautapimwa.” Upendo huu “ni mwingi”, “wa wote” na “wenye nguvu”.

Amri ya wote ya Ukristo kwenye upendo imeelezewa kwa nguvu sana kati- ka haja yake ya mtu kuwapenda adui zake. Yesu mwenyewe anasema: “Mmesikia ya kwamba imenenwa, umpende jirani yako, na, umchukie adui yako; lakini mimi nawambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowadhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio na haki.” (Mt. 5:43-46) mahala pengine tunaona kwamba alisema: “Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wanawanea ninyi. Akupigae shavu la kushoto mgeuzie la pili, naye akunyang’anyaye joho yako, usimzuie na kanzu.” (Luk. 6:27-29)

Kwa hiyo, Mkristo wa kweli huwapenda maadui zake. Hakika, kama Clement alivyodokeza,27 kigezo cha ndani cha maendeleo ya mtu kiroho si chochote kuliko uwezo wa mtu kupenda maadui zake. Kisa kifuatacho huonesha umuhimu wa upendo (katika suala hili, upendo kwa maadui) na hali yake ya juu kwenye hofu na matumaini.

John Climcus katika kitabu chake, The ladder of Perfection anaandika: “Siku moja niliwaona watawa watatu wametukanwa na kudhalilishwa katika hali hiyo hiyo na wakati huo huo.

Wa kwanza alijisikia ameumizwa sana kiukatili; alihuzunika lakini aliweza kutokusema kitu chochote. Wa pili alifurahia mwenyewe lakini alisikitika kwa ajili ya yule mtu ambaye amemtusi. Wa tatu alifikiria tu maumivu aliyopata jirani yake, na akalia kwa shauku kubwa ya huruma. Wa kwanza alisukumwa na hofu; wa pili alishawishiwa kwa matumaini ya malipo; wa tatu alisukumwa na upendo.”28

Upendo wa mtu kwa jirani yake katika Ukristo una sifa za kufanana sana za asili, kama usawa, mwelekeo wa pamoja na ushirikiano wa asili.

Hii sifa ya usawa imeelezewa vizuri katika kile ambacho kimekwisha nukuliwa kutoka kwa Brett: “Upendo wa Ukristo ndio kitu unachoniwia kiuhalisi kwa sababu wewe ni mtu mwingine kama mimi.” Kwa sababu ya elementi hii ya msingi wa usawa, maadili ya Ukristo hayategemezi kaida zake juu ya jamii, kibailojia, kisaikolojia, kifiziolojia, kiakili, au tofauti za kielimu na daraja, lakini katika ujuzi na kuwaona wanadamu kama walioumbwa katika mfano wa Mungu.

Elementi mpya ya maadili ya Ukristo ni mwanzo wa maadili ya mtu binaf- si katika maadili ya ushirika, katika kuelewa urafiki wa Wakristo kama mwili wa Kristo. Muumin binafsi hajulikani kama mtu aliyejitenga ambaye ameasisi uhusiano mpya wa kiroho na wa kiuadilifu na Mungu, bali kama ‘jiwe linaloishi,’ kama chembe chembe inayoishi katika mwili wa Kristo ambamo kwawo nguvu za Ufalme wa Mungu tayari zinafanya kazi.

Mt. Petro aliandika kwa wakimbizi wa Kiyahudi waliotawanyika katika Pontus, Cappadocia, Asia na Bithynia: “Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yalio hai, mmejengwa mwe nyumba ya roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho zinazokubaliwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. (1 Pet. 2:4-5)

Na ni aina ya ushirika tunaouona katika kuelewa kwamba upendo wa Ukristo sio tu hisia za moyoni: lazima ufuatwe na matendo ya ukarimu na hatua za kumaliza mateso ya kundi lingine. Upendo sio tu kutakiana kheri au hisia za huruma. Upendo ni matendo, kutumia muda na gharama. Gilleman anasema: “Upendo wa Kristo hutwaa nafsi na mwili.
Fadhila yetu ya kiroho lazima ijipambe yenyewe katika matendo, katika kazi za ushirika za huruma (Mt. 25:35-45) na huduma za jamii (Mat. 4:32-37; 6:1).29

Kwa maneno mengine, Ukristo wa kiroho sio tu wa mtazamo wa ndani au mtazamo wa juu. Kama Brett anavyouelezea: “Lazima vile vile uwe wa mtazamo wa nje ukihusiana na jirani, kama ukitakiwa kuwa kamili.”30 Katika barua kwa makabila kumi na mbili yaliyotawanyika (Dispersion-Dispora), Mt. James aliandika:

“Ina faida gani, ndugu zangu, kama mtu anasema ana imani lakini haifanyi kazi, je, imani yake itamuokoa? Kama kaka au dada ni masikini na anakosa chakula cha kila siku, na mmoja wenu akasema kuwaambia ‘Nendeni kwa amani, kuweni wakunjufu na maridhawa,’ bila kuwapa kitu kinachohitajiwa na mwili, ina faida gani? Hivyo imani kwa yenyewe, kama haina kazi, imekufa.” (James 2:14 -17)

Kwa hiyo, upendo wa Ukristo lazima uelezewe katika hali zote za mwelekeo na matendo. Matendo lazima yawe chimbuko lake ni katika upendo, na upendo lazima uelezewe katika matendo. Uhalisi wa upendo wa Ukristo hutupeleka kwenye ubadilishanaji wa kipekee wa zawadi na mateso, ya nderemo na huzuni, ya kushindwa na ushindi; mtu binafsi ana uwezo kwa kujitolea mhanga na mateso, ili kuchangia kwenye maendeleo ya jumla. Miundo yote ya kikanisa, kisiasa na jumuiya za kijamii za Kikristo zimeasisiwa juu ya fikira hii ya msingi wa urafiki wa waumini, kama mwili wa Kristo.

Hivyo, katika Ukristo upendo una nafasi ya muhimu na jukumu zito katika teolojia na maadili. Mungu Mwenyewe ni pendo na ameumba ulimwengu kwa ajili ya upendo. Mungu ambaye ni pendo amemtuma Mwanawe kuwakomboa wanadamu na kuwalingania, akafanya ndani mfano Wake, ili kushiriki katka maisha Yake. Baba anaonesha upendo wa pekee kwa Mwana, akipitisha juu yake utukufu Wake, na Mwana anaonesha upendo wake kwa Baba kwa kutii amri Yake ili kuonesha upendo mkubwa kwa wanafunzi kwa Ufufuo wake.

Wanafunzi wanaonesha upendo wao kwa Mwana kwa kutii amri yake kupendana wenyewe kwa wenyewe, kujitoa mhanga kama Mwana mwenyewe. Kwa ujumla, jukumu la msingi la mtu ni kutekeleza upendo wa ukarimu, agape, na kuendeleza ufalme wa Mungu katika ardhi. Mtu lazima afanye kazi kwa ajili ya kuwepo daima kikamili- fu kwa Mungu katika ulimwengu alioufanya.

 • 1. Kwa mujibu wa mafundisho ya Ukiristo, nems za teolojia kwa asili hazitokani na mtu wa kawaida. Hutolewa
  na Mungu kupitia kwa Yesu na kasha kutekelezwa na muumin. Taz. Britannica 1997.
 • 2. Lazima ioneshwe kwamba St. Thomas katika Summa theologica anaongezea katika oradha ya nems, nems tatu za kiakili: Hekima, ujuzi na kipaji. Tazama vile vile Beirut, 1992, uk. 1992, uk. 9
 • 3. Vicent MacNamara (1989) hushikilia kwamba kumekuwa na mabadiliko katika teolojia ya kimaadili ya Katoliki juu ya hadhi ya upendo. Huamini kwamba upendo siku zote wakati uliopita haukuwa na upekee wa daraja hili; kulikuwa na wakati ambapo upendo (au hisani) ulikuwa ukichukuliwa kama moja ya mahitaji mengi ya uadilifu.
 • 4. Johnston, 197, uk. 135
 • 5. MacNamara, 1987, uk. 11.
 • 6. Mtu lazima aweke akilini kwamba, pamoja na ukweli kwamba maadili ya Ukristo chimbuko lake ni kwenye Angano la Kale na Yesu alikuwa kimsingi mtiifu kwa mila za Kiyahudi katika suala la upendo, hakuna msisitizo mwingi juu ya dhana ya upendo imma katika upande Mungu au upande wa mwanadamu katika Angano la Kale. Imedokezwa kwamba (T. Barrose, 1968, uk. 1043, 1044) Bibilia ya Kiyahudi hupendelea kutumia dhana zingine, kama vile mfungamano wa utii, uaminifu, upole na upendeleo wa nguvu ili kuelezea uhusiano wa Mungu na mtu. Kwa upande mwingine, uhusiano wa Wana wa Israil na Mungu (Yehova) huelezewa kwa dhana kama vile kuogopa, utumishi na mfungamano wa utii. Katika hali zote, ni mara chache tu upendo huongelewa. Upendo kwa mtu mwenzi kama jukumu la kidini hutokea mara tatu katika Bibilia yote ya Kiyahudi. Katika Angano Jipya upendo huwasilisha dhana kubwa kuhusu uhusianao wa Mungu na mtu. Dhana ya agano hutoa sehemu kwenye ile ya ubaba
 • 7. Paulo alishusha sheria zote na kuishia kwenye mtu kumpenda kijarani yake, "Yule ambaye humpenda jirani yake ameitekeleza sheria……. (Rum. 13:8-10)
  Kwani sheria yote imekamilishwa na neno moja…….(Wag.5:14)
 • 8. Johann, 1967, uk. 1039
 • 9. The revised catechism, 1996, Q. 9.
 • 10. Graham, 1939, 22
 • 11. Taz. Chervin,1973, 9. 10, 19, 62.
 • 12. Johann, 1967, uk. 1040.
 • 13. Brett, 1992, uk. 3.
 • 14. Cerini, 1992, uk. 9
 • 15. Barrosse (1967, uk. 1044) anafanya ulinganishi muhimu kati ya sehemu tofau- ti za N.T. yaani, Injili ya Matayo, Marko na Luka, na nyaraka za Paulo na maandiko ya Yohana. Nafikiri ulinganishi wake unaonesha kwamba kwa mfululi- zo msisitizo juu ya dhana ya upendo katika hizo sehemu tatu za N.T. huongezeka. Hufikia upeo wake katika maandiko ya Mt. Yohana ambaye kamwe hatumii neno lolote mbali na upendo kuelezea huruma za Mungu kwa mtu. Mateso ya Yesu Kristo - Kufufuka katika maandiko ya Mt. Paul huchukuliwa kudhihirisha upendo wa Yesu na wa Baba yake, ambapo katika maandiko ya Mt. Yohana huonesha kwamba Mungu ni pendo.
 • 16. Kwa mfano, tazama Cerini, 1992, uk. 21. Lubich anaandika: "Yesu, basi hivi ndivyo unavyoionesha! Hivi ndivyo unavyotangaza ukweli kwamba nina "Baba" (Ibid), imesimuliwa kutoka C. Lubich, Diary 1964/65 (New York, 1987), uk. 72&73.
 • 17. Graham, 1937, uk. 34
 • 18. Graham, 1937, 36.
 • 19. Graham, 1937, uk. 37.
 • 20. Hii ni kweli kwa mujibu wa tarjuma ya msemo uliotajwa na Graham. Tarjuma ya kisasa inaonekana kuwa ni "Bwana ametengeneza kila kitu kwa lengo lake.
 • 21. Graham, 1939, uk. 38
 • 22. Berdard, 1937, Sura ya 1.
 • 23. Lubich, May They All Be One, uk. 24. iliyodondolewa katika Cerini, uk. 38.
 • 24. Graham, 1939,uk. 16
 • 25. Graham, 1939, uk 60
 • 26. C. Lubich, Meditations (London, 1989), uk. 66, 67.
 • 27. O. Clement 1993, uk. 271.
 • 28. Imedondolewa katika Clement, 1993, uk. 271
 • 29. Gilleman 1967, uk. 1045.
 • 30. Brett, 1992, uk. 3.