Sehemu Ya Tatu

1. Upendo Wa Mungu Kama Sababu Kubwa Kwa Ajili Ya Uumbaji

Dhana ya upendo ni moja ya dhana muhimu katika filosofia ya Kiislamu, teolojia, irifaniyah na maadili; hakika katika baadhi ya vipengele, ina nafasi muhimu na jukumu zito. Kwa mfano, katika kufafanua mtazamo wa Kiislamu wa uhusiano kati ya Mungu na ulimwengu wote kwa ujumla, na hususan kati ya Mungu na wanadamu, upendo una nafasi muhimu zaidi.

Katika sura hii, jukumu langu kubwa ni kuelezea nafasi ya upendo katika maadili ya Kiislamu, lakini kabla ya hilo nitafafanua juu ya dhana ya upen- do katika mtazamo wa ulimwengu wote wa Kiislamu.

Mapema katika kalam (teolojia ya Kiislamu) mdahalo mkali ulianzishwa juu ya madhumuni ya uumbaji wa Mungu na matendo. Baadhi ya wanate- olojia wanafikiria kwamba uhusishaji wa sababu au madhumuni kwenye vitendo Vyake hutufikisha kwenye dhana kwamba Mungu ana haja na viumbe wake na Aliwaumba kukidhi baadhi ya haja, kama vile mwanadamu ambaye anasema, kufanya kazi ili kupata pesa, au mafunzo ili kujifundisha.

Hata hivyo mtazamo wenye kuongoza, hususan miongoni mwa wale ambao wamekuwa na mwelekeo zaidi wa kimantiki, siku zote wamekuwa na mwelekeo kwamba Mungu ni Mwenye hekima (hakim), hivyo chochote anachofanya ni kwa ajili ya madhumuni fulani haswa ambayo yamechunguzwa kabla na kwa uangalifu. Imeelezewa katika Qur’ani kwamba: “Je, mnafikiria kwamba tumekuumbeni bure…?” (23:115)

Ama kwa hakika, ni wazi kwamba Mungu Mwenyewe hapati chochote kutoka kwa viumbe Wake, wala kwenye kitendo Chake cha uumbaji. Hii sio kwa sababu tu kwamba Yeye yuko huru kikamilifu kutokana na haja ya aina yoyote, bali vile vile kwa sababu kimantiki haiwezekani kwamba athari iliyopangwa itakuwa na aina yoyote ya ushawishi (kuhusu kuishi) juu ya sababu yake.

Chochote itakachokuwanacho athari hiyo, kimepatikana kutoka kwenye sababu. Na itakuwa ni mzunguko kuifikiria vinginevyo. Mungu hakuumba ulimwengu ili kujipatia manufaa fulani Mwenyewe, bali kutoa manufaa. Shairi mashuhuri la Kifursi linasema: “Sikuumba ulimwengu kupata manufaa fulani, Nimeumba ulimwengu kuwaonyesha watu ukarimu Wangu.”

Kuna simulizi mashuhuri ya kimungu (Hadith quds) ambayo inaweza kupatikana katika vitabu vyote vilivyoandikwa kuhusu lengo la uumbaji katika Uislamu. Kwa mujibu wa hadith hii, Mwenyezi Mungu Anasema: “Nilikuwa hazina iliyofichwa; nilipenda kujulikana. Kwa hiyo niliumba ulimwengu ili kwamba niweze kujulikana.”1 Neno la asili la Kiarabu kwa neno ‘upendo’ limetokana na neno hubb, ambalo lina maana ya kutaka au kupenda.

Hubb ni dhana ya jumla ambayo yaweza kutumika kwenye vitu vya kawai- da, kama vile kupendelea aina fulani ya chakula, ambayo kwa Kiingereza/Kiswahili inaweza kutafsiriwa kama ‘kupenda’. Au inaweza kumaanisha vitu muhimu zaidi katika uhai wa mtu, kama vile hamu kali sana ya mtu au matazamio, kwa kiasi kwamba mtu anaweza hata kuwa tayari kuangamizwa kwa ajili ya kumridhisha mpenzi au kupata matazamio yake.

Hubb katika hali hiyo inaweza kutafsiriwa kama ‘upendo’. Kuna istilahi nyingine katika utamaduni wa Kiislamu ambayo wakati mwingine inatumika katika Kiarabu na kwa kawaida zaidi katika Kifursi kumaanisha upendo mkali, ishq. Vile vile kuna wudd urafiki mkubwa mno na yule mpendwa.

Hivyo, swali linakuja: Kwa nini Mungu kapenda kujulikana? Kwa hakika, Mungu hana tamaa ya fahari. Madhumuni ya kupenda Kwake ajulikane yanafahamika kwa kuchukulia kwamba Mungu Ni Mwenye Busara, Mwenye Huruma, na Mwenye kudra. Aliumba ulimwengu, na hususan wanadamu, ili kuwapa upeo wa huruma na ukamilifu ambao wana uwezo wa kuupokea.

Ama kwa hakika, ukamilifu wa aina yoyote ya kiumbe huamuliwa kwa daraja ya kurandana kwake au ukaribu kwa Mungu, na vipen- gele muhimu zaidi katika hili ni upendo kwa Mungu, na kabla ya hapo, kumjua Mungu, kwa vile hakuwezi kuwa na upendo bila ya kujua kina- chopendwa.

2. Upendo Wa Mungu Kwa Ajili Yake Mwenyewe

Kwa vile sababu ya kupenda kitu si nyingine bali ile ya ule utambuzi wa mpenzi, wa uzuri na ukamilifu, au kiujumla zaidi, uchangamfu wa mpendwa, upendo mkubwa sana uwezekanao kwa hakika ni upendo wa Mungu kwa Yeye Mwenyewe. Mungu ni mzuri zaidi na mkamilifu zaidi, na utam- buzi wake Yeye Mwenyewe vile vile ni utambuzi ulio bora, hivyo upendo Wake kwa Yeye Mwenyewe na furaha ni vitu vizito mno. Avicenna anaandika:

“Yule aliyepo kwa lazima (wajib al-wujud) ambaye ana ukamilifu wa juu zaidi, mbora na mwangavu na anayejitam- bua Yeye Mwenyewe kama hivyo pamoja na utambuzi mkamilifu…Yeye Mwenyewe ni mpendaji mkubwa mno na mwenye kupendwa mkubwa mno na anayo furaha kubwa mno…”2
Mahali pengine anasema: “Kitu ambacho kina furaha kubwa mno kuhusiana na kitu fulani ni kile cha Kwanza (al-Awwal) kuhusu Yeye Mwenyewe, kwa vile anao ufahamu mkubwa mno na anao ukamilifu mkubwa mno.”3

Sadrud-din al-Shirazi, ajulikanaye kama Mulla Sadr na muasisi wa shule ya al-Hikmah al-Muta’aliyah, anazungumzia nukta hiyo hiyo:

“Upendo unasababishwa na kile kinachopatikana au kitakachopatikana kutoka kwa mpendwa. Wema wa hali ya juu na kuwepo na mhemuko zaidi ndio kustahiki zaidi kwa ajili ya kupendwa na upendo mkubwa mno kwa ajili ya wema. Sasa kiumbe ambacho ni huru kutokana na uwezekano na dharura, kwa ajili ya msingi wake, kina daraja ya msingi ya kupenda. Kwa hiyo, upendo kwa ajili Yake Yeye Mwenyewe ni upendo kamili zaidi na wenye utii zaidi.”4

Aliongeza kwamba, kwa vile Mwenyezi Mungu ni halisi (sio mchanganyiko wa vitu) na sifa za Mwenyezi Mungu sio nyongeza (au kubahatisha) kwenye asili Yake katika kuwepo (fikra ambayo inakubaliwa zaidi na mafilosofa wa Kiislamu na wanateolojia wengi na hujulikana kama umoja wa asili Yake na sifa Zake), upendo Wake ni sawa sawa na asili Yake. Katika njia hii, mtu anaweza kusema kwa kuthibisha kwamba Yeye ni pendo kama ambavyo Yeye ni ujuzi na uhai.

3. Upendo Wa Mungu Kwa Ajili Ya Viumbe

Upendo wa Mungu kwa ulimwengu kwa ujumla, na hususan kwa wanadamu kwa pamoja unaaminiwa na kusisitizwa na Waislamu wote. Hakika, moja ya majina ya Mwenyezi Mungu ni al-Wadud, ‘Mwenye kupenda.’

Hii ni kwa nyongeza kwenye yale majina ambayo huhusisha upendo Wake kwa vimbe, kama vile al-Rahman na al-Rahim, yenye maana ya Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu. Kila surah ya Qur’ani, isipokuwa sura ya 9, (ambayo huanza na Aya kuhusu kuwaonya makafiri) huanza kwa msemo: “Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu”.

Hata hivyo bado idadi ya kurudiwa rudi- wa kwa msemo huu katika Qur’ani ni sawa na idadi ya surah, yaani 114, kwa vile katika surah ya 27 msemo huu umtokea mara mbili. Inafaa kuta- jwa kwamba ingawa moja ya vitu vilivyohusishwa kwa Mwenyezi Mungu katika Uislamu ni ghadhabu (ghadhad), utekelezaji wake ni wa ukomo zaidi ukilinganisha na Huruma Yake na upendo kwa viumbe Wake. Hakika, ghadhabu Yake ni kwa wale tu ambao kwa makusudi hukufuru au hutenda vitendo viovu. Hii ni fikra ambayo Waislamu wote wanakubaliana nayo, na inaelezewa kwa uwazi katika vyanzo vingi. Hapa ningependa kutaja kauli moja yenye nguvu. Katika dua mashuhuri ya Jushan al-Kabir, Mwenyezi Mungu hutajwa kama ‘Ambaye huruma imeitangulia (kwa kipaumbele) ghadhabu Yake’.

Kama tutakavyoona baadae, ghadhabu au hasira vile vile iko nje ya upen- do na huruma Yake. Kama upendo au huruma Yake isingekuwepo asingejali kabisa. Ni kama baba anayemkasirikia mwanawe wakati anapofanya makosa. Ni kwa sababu anajali na wasi wasi kwa ajili ya mtoto wake na kwa familia yake yote, kwa sababu anamtaka mtoto wake kurekebisha tabia yake na kuweka mfano kwa watoto wengine wasiige vitendo hivyo vya makosa.

Mwenyezi Mungu ana daraja tofauti za upendo kwa ajili ya viumbe Wake. Moja ni upendo Wake wa jumla na ulionea ambao hujumuisha viumbe wote. Kama kungelikuwa hakuna upendo kama huo kusingekuwepo na kiumbe yoyote. Upendo huu hujumuisha hata watenda maovu, kwa vile nao vile vile wanadhihirisha au kuwasilisha hatua fulani za wema katika asili yao na hiki ndicho kipengele cha uhai wao ambacho kinapendwa na Mungu, ingawa kinaweza kushindwa na kipengele cha kishetani cha tabia zao na kwa hiyo hatimaye wanaweza kuchukiwa.
Daraja kubwa ya upendo wa Mungu ni upendo Wake kwa waumini wa kweli, wale ambao wanaamini katika Yeye na kufanya matendo mema. Hao ndio watu ‘Anaowapenda na ambao humpenda Yeye’ (5:54). Katika Qur’ani, tunaona kwamba Mungu anawapenda ‘watendao haki’ (5:42; 8:60; 9:49), ‘wale ambao hujitakasa wenyewe’ (9:108), ‘wachamungu’ (3:76; 9:4 & 7), ‘wale ambao hufanya wema (kwa wengine)’ (5:13 & 93; 3:134 & 148; 2:195), ‘wale ambao humuamini (Yeye)’ (4:35), ‘wavumilivu’ (3:146) na ‘wale ambao hutubia sana na kujitakasa wenyewe’ (2:222).

Inafaa kutajwa kwamba katika Qur’ani katika masuala mengi hasira ya Mungu inaelezewa, sio kwa kuangalia katika kuchukia Kwake, bali kiasi kwa misemo ya kuzunguka, kama vile, ‘Mwenyezi Mungu hampendi kila muovu afanyaye dhambi’ (2:276), ‘Mwenyezi Mungu hawapendi waovu’ (3:57 & 140), ‘hakika Mwenyezi Mungu hampendi menye fahari, ajivunaye’ (4:36) na ‘hakika Mwenyezi Mungu hampendi yule ambaye ni muovu, mwenye dhambi’ (4:107).

4. Upendo Wa Mungu Kwa Ukamilifu Wa Wanadamu

Kwa mujibu wa Uislamu, daraja la juu zaidi la upendo wa Mungu kwa kiumbe yeyote ni upendo Wake kwa wanadamu wakamilifu kama vile mitume. Mtume Muhammad ana sehemu maalumu kuhusiana na hili. Moja ya vyeo vyake maarufu mno ni Habib Ullah, ambacho kina maana ya mpendwa wa Mungu. Katika moja ya semi mashuhuri za ki-Mungu, Mungu anamhutubia Mtume: “Lau isingekuwa wewe, nisingeumba ulimwengu.” Kama ambavyo S.H. Nasr na wengine wengi walivyoonesha, “Mawalii wa Kiislamu kwa karne nyingi wameona katika upendo wa Mungu kwa Mtume na upendo wake (Mtume) kwa Mungu sampuli kifani ya upendo wote kati ya mtu na Muumba wake. 5

5. Upendo Wa Mwanadamu

Kufanana kwa kile tulichoona mwanzo katika suala la upendo wa Mungu, upendo wa mwanadamu kwa Mungu, kwa viumbe Wake, kwa matendo mema, na kwa kila moja hutekeleza jukumu zito katika mtazamo wa Kiislamu, wa kiulimwengu, hususan katika teolojia, irifani na maadili. Hakika, upendo kwa ajili ya ukweli uliounganishwa katika dini hujenga imani. Ingawa imani, kwa wanateolejia Waislamu, imeegemezwa juu ya ujuzi wa ukweli wa kidini, haipunguziki kwenye ujuzi huo. Kunaweza kuwa na watu ambao wana ujuzi mambo ya kidini, lakini ambao bado hawajitumi kwenye imani yoyote. Dini na kuamini huja tu wakati mtu kwa hiyari yake anajituma mwenyewe ukubalifu wa kanuni za imani na akawa hakatai kuzifuata. Katika maneno mengine, upendo unakuwepo tu pale wakati mtu anapopenda imani za dini na sio tu wakati mtu anapokuja kuzijua. Qur’ani inasema:

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنْفُسُهُمْ {14}

"Na wakazikanusha (ishara za Mungu au miujiza), na hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo…"(27: 14)

Sampuli kifani ya wale ambao wanajua vizuri sana lakini wakakataa kutekeleza kile walichokwishajua ni Iblis, yule shetani mkubwa. Kwa mujibu wa vyanzo vya Kiislamu, Iblis hufanya chochote afanyacho kwa kiburi na ubinafsi, sio kwa ajili ya ujinga.

Hivyo, mtu anakuwa muaminifu na muumini wakati tu anapokuwa na heshima na upendo kwa ajili ya ukweli fulani. Tunasoma katika hadithi mashuhuri kwamba Mtume Muhammad aliwauliza masahaba wake kuhusu 'kishikizi imara cha imani'. Walipendekeza vitu tofauti kama Swala na Hijja. Wakati waliposhindwa kutoa jibu sahihi, Mtume akasema:

"Kishikizi imara cha imani ni kupenda kwa ajili ya Mungu na kuchukia kwa ajili ya Mungu, kuwa marafiki na marafiki wa Mungu na kuwakataa maadui Zake.6

Wazo kama hilo hilo limesisitizwa na Maimamu wa Nyumba ya Mtume. Kwa mfano, Fudhayl ibn Yasar, mfuasi wao, alimuuliza Imamu Sadiq iwapo upendo na chuki chimbuko lake ni imani. Imamu akajibu: "Je, imani ni kitu chochote mbali ya upendo na chuki?"7 Hadithi kama hiyo inasimuliwa kutoka kwa Imamu Baqir. Inasimuliwa vile vile kwamba Imamu Baqir alisema: "Imani ni upendo na upendo ni imani." 8

Uchunguzi wa jumla wa Qur'ani na hadithi unaonesha kwamba katika mtazamo wa Kiislamu, upendo, imma katika muundo wake Kimungu au katika muundo wa kibinadamu, ni wa vitu vya thamani na tunu tu kwa kiasi kwamba ni vya thamani na tunu. Matokeo ni kwanza, kwamba daraja za upendo ambazo vitu tofauti hustahiki au hupokea hutofautiana kutokana na ubora wao, na pili, kwamba kila kitu ambacho kiko katika mgongano na vile vitu vyenye thamani na tunu au huzuia utambuzi wao, lazima kichukiwe.

Kwa mfano, kama haki ni yenye kupendwa, dhulma lazima ichukiwe; au kama mtu ambaye husema ukweli ni mwenye kupendwa, mtu ambaye huongopa lazima achukiwe. Kama mambo yalivyo, kuhusu vipengele vingine vya tabia zao na vitendo vyao, hali inaweza kuwa tofauti. Mtu mmoja anaweza akapendwa au kusifiwa kwa kitu fulani na wakati huo huo anaweza kuchukiwa au kulaumiwa kwa kitu kingine.

Kinyume na baadhi ya imani nyingine, kipengele kimoja cha upendo kati- ka Uislamu ni kwamba, kwa kawaida huchukuliwa sanjari pamoja na "chuki (ya maovu) kwa ajili ya Mungu." Mtu lazima apende kwa ajili ya Mungu, na kuchukia kwa ajili ya Mungu. Kuna tabia miongoni mwa baadhi ya watu kufikiri kwamba haitakikani kuwepo kwa chuki kabisa. Watu hawa hufikiria kwamba ubora na wema wa tabia na kuwa 'mkunjufu' hutegemea kuwa na urafiki na kila mtu.

Kwa hakika Uislamu hupendekeza kwa Waislamu kupenda watu na kuwa na msimamo wa kutegemea mema na huruma na uhusiano mnyofu pamoja nao, hata kama hawaamini katika Uislamu na katika Mungu. Hata hivyo sio yamkini kwa mtu ambaye ana kanuni katika maisha yake na ametoa maisha yake kufanikisha maadili matakatifu kutojali matendo maovu na uonevu wa watu waovu na kufanya urafiki na kila mtu. Hakika mtu kama huyo atapata maadui fulani. Siku zote kuna watu wazuri na wabaya katika jamii. Kuna watu wenye haki na madhalimu. Wema na ubaya ni mihimili miwili inayopingana. Kuvutiwa kwenye wema hakuwezekani bila kujitoa kutoka kwenye ubaya.

Wakti wanadamu wawili wanavutiana na wanataka kuwa marafiki, lazima tuangalie sababu kwa ajili ya hilo. Sababu si chochote bali ni mlandano na mfanano. Mpaka kuwe na mlandano baina ya watu hawa wawili, vinginevyo hawawezi kuvutiana na kuelekea kwenye urafiki wa pamoja. Rumi katika Mathnawi yake anataja visa viwili vizuri ambavyo huonesha ukweli huu.

Kisa kimoja ni kwamba, siku moja tabibu mwenye busara sana na mashuhuri aliwaomba wanafunzi wake wampe dawa fulani kwa ajili yake mwenyewe. Wanafunzi wake walisituka. Wakasema: "Ewe Bwana! Dawa hii ni kwa ajili ya matibabu ya vichaa, lakini wewe ni mtu mwenye busara mno ambaye tunakujua." Bwana akajibu: 'Wakati nikiwa njiani nikija hapa, nilikutana na mtu mwendawazimu. Wakati aliponiona alitabasamu. Sasa nina wasiwasi huenda ameona mfanano fulani baina yangu na yeye; vinginevyo asingefaidi vile kuniangalia."

Kisa kingine kinahusiana na mtu mwingine mwenye busara ambaye aliona aina fulani ya ndege kama kunguru amekuwa na urafiki na korongo. Walitulia pamo- ja na kuruka pamoja! Mtu yule mwenye busara hakuweza kuelewa ni kwa namna gani ndege wawili wa jamii mbili tofauti ambao pia hawana mfanano katika umbo au katika rangi wanaweza kuwa marafiki. Alikwenda karibu na kugundua kwamba wote wawili wana mguu mmoja tu.

Yule mtu mwenye busara akasema:
"Niliona urafiki baina ya kunguru na korongo.
Mshangao ulinipata, nilichunguza hali zao
Kuona ni nini dalili ya kufanana kwao ninazo weza kuziona.
Hivyo nilitambaa, na, ajabu ilyoje!
Niliona kwamba wote wawili ni vilema."

Katika Uislamu, kumekuwa na msisitizo mkubwa juu ya ulazima wa kuendeleza undugu na urafiki pamoja na watu wa imani na wenye nia njema, na wakati huo huo kupigana dhidi ya waovu. Kama mambo yalivyo, katika Uislamu upendo ni kwa wote, na Mtume wa Uislamu hakutumwa ila, "…kuwa rehema kwa wanadamu wote" (Qur'an 21:107).

Kwa hiyo, hata kupigana dhidi ya wale ambao hufanya maovu na dhulma ni lazima kuwe ni kwa ajili ya upendo. Ni tendo la upendo sahihi kwa ujumla na hata tuseme kumuua mtu kama Hitler, kupigana dhidi yake, kumuadhibu na ikiwa lazima kumuangamiza. Vinginevyo, atafanya uhalifu zaidi na atajishusha hadhi zaidi na zaidi na atapata adhabu kali zaidi katika ulimwengu huu na ulimwengu ujao.

Kuna kisa kizuri mno kwamba siku mmoja mtawala muonevu alimtaka mtu mchamungu kuomba kwa ajili yake. Katika kumjibu, yule mtu mchamungu alimuomba Mungu asimuache kuishi zaidi ya hapo. Yule mtawala muonevu alisituka na akasema: "Nilikuomba kuniombea mimi na sio dhidi yangu!"

Yule mchamungu akajibu: "Hivyo ndivyo nilivyofanya haswa. Ni bora zaidi kwako wewe na kwa hakika kwa ajili ya watu halikadhalika, kwamba uhai wako uwe mfupi. Utakuwa huna nafasi ya kuongeza kwenye uhalifu wako na watu watapata nafasi zaidi ya kupumzika."

Upendo wa mantiki na akili ni ule ambao unahusisha mazuri na masilahi ya binadamu na sio idadi ndogo ya watu. Mtu anaweza kufanya mambo mengi kuleta mema kwa watu au kundi ambalo huleta uovu kwa jamii au wanadamu kwa ujumla. Kwa mfano, kama hakimu akimuachia mhalifu mwenye hatia huenda amefanya kitu kizuri kwa mtu yule, lakini madhara makubwa yatakuwa yameletwa kwenye jamii na kwenye uadilifu wa haki. Mtu hatakikani aachilie upenzi wake ufiche ukweli. Kama mtoto wetu mpendwa anahitaji sindano au upasuaji haitakiwi tuuruhusu upendo wetu na mapenzi yetu yazuie kufanyika hilo.

Kwa mujibu wa Uislamu, upendo lazima uelimishwe. Upendo mtakatifu ni upendo ambao ni halisi na wenye kumaizi mno. Imekuwa ni wazo la kawaida katika mafundisho ya kimaadili ya wahubiri wakubwa wa Kiislamu na mabwana wa Kisufi kwamba mtu asiuachilie upendo wake kwa ajili ya kitu fulani au mtu fulani, umfanye apuuze ukweli wote.

Sababu ya msisitizo huu ni kwamba upendo kwa kawaida una tabia ya kumfanya mpenzi 'kipofu na kiziwi'. Kama unampenda mtu haielekei kabisa kwamba utakuwa na mtazamo wa kiupendeleo, isipokuwa kama pendo hilo limeelekezwa na akili. Hii ndio maana hata Waislamu Masufi wanajaribu wasizidiwe na upendo. Sirajud-Din anaandika:

"Sufi hana hiyari bali kuwa muangalifu, makini na mwenye kumaizi, kuweka kila kitu katika sehemu yake sahihi, na kukipa kila kitu haki yake… ni kwa sababu ya mtazamo huu kwamba Usufi ni njia ya elimu zaidi kuliko njia ya upendo. Kwani kwa hilo unaelekea kukataa upendeleo ambao mtazamo wa upendo kwa lazima huufumbia macho na hata pengine kuunga mkono."9

6. Upendo Wa Mwanadamu Kwa Mungu

Kwa mujibu wa Uislamu, kiwango cha chini cha mategemeo kutoka kwa waumini ni kwamba Mungu lazima awe na sehemu ya kwanza kabisa kati- ka nyoyo zao, kwa maana kwamba hakuna pendo lingine litakalopita upendo wa mtu kwa Mungu; Mungu lazima awe lengo la juu sana na mbele zaidi la upendo. Qur’a inasema:

قُلْ إِنْ كَانَ آبَاؤُكُمْ وَأَبْنَاؤُكُمْ وَإِخْوَانُكُمْ وَأَزْوَاجُكُمْ وَعَشِيرَتُكُمْ وَأَمْوَالٌ اقْتَرَفْتُمُوهَا وَتِجَارَةٌ تَخْشَوْنَ كَسَادَهَا وَمَسَاكِنُ تَرْضَوْنَهَا أَحَبَّ إِلَيْكُمْ مِنَ اللَّهِ وَرَسُولِهِ وَجِهَادٍ فِي سَبِيلِهِ فَتَرَبَّصُوا حَتَّىٰ يَأْتِيَ اللَّهُ بِأَمْرِهِ ۗ وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ {24}

“Sema: Ikiwa baba zenu, na wana wenu, na ndugu zenu, na wake zenu, na jamaa zenu, na mali mliyoyachuma, na biashara mnazoogo- pea kuharibika, na majumba mnayoyapenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na jihadi katika njia Yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri Yake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.” (9:24)

Aya hii inaonesha kwa uwazi kabisa kwamba upendo kwa Mungu lazima uwe juu kuliko chochote kile ambacho mtu anaweza kukipenda katika maisha. Ukubwa huu hujionesha wenyewe wakati upendo kwa Mungu na kwa dini Yake vikigongana na upendo kwa vitu binafsi. Katika hali hii, muumini lazima awe na uwezo wa kutoa mhanga vitu vyake binafsi avipendavyo kwa ajili ya Mungu.

Kwa mfano, kama Mungu akitutaka kutoa maisha yetu kwa ajili ya kulinda maisha ya watu wasio na hatia au usalama wa nchi yetu au vitu kama hivyo, hatupaswi kuacha mapenzi yetu ya maisha ya raha au kuwa na familia na kadhalika na kadhalika kutuzuia sisi kufanya jihadi katika njia Yake.

Kwa hiyo, muumini sio mtu anayempenda tu Mungu. Muumini ni mtu ambaye upendo kwa Mungu ni wa juu sana na anao upendo imara kabisa. Qur’ani inasema:

وَمِنَ النَّاسِ مَنْ يَتَّخِذُ مِنْ دُونِ اللَّهِ أَنْدَادًا يُحِبُّونَهُمْ كَحُبِّ اللَّهِ ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَشَدُّ حُبًّا لِلَّهِ ۗ وَلَوْ يَرَى الَّذِينَ ظَلَمُوا إِذْ يَرَوْنَ الْعَذَابَ أَنَّ الْقُوَّةَ لِلَّهِ جَمِيعًا وَأَنَّ اللَّهَ شَدِيدُ الْعَذَابِ {165}

“Na katika watu wapo wanaochukuwa waungu wasio kuwa Mwenyezi Mungu. Wanawapenda kama kumpenda Mwenyezi Mungu. Lakini walioamini wanampenda Mwenyezi Mungu zaidi sana…” (2:165)

Kwa nini mtu ampende Mungu? Kwa mujibu wa Uislamu, sababu moja ya kumpenda Mungu ni katika ukweli kwamba Mungu ni Mwenye thamani mno, mkamilifi mno, na mzuri mno kiasi kwamba mtu hawezi kamwe kutambua, na, kwa hiyo, kwa sababu asili ya mtu hutamani uzuri na ukamilifu, humpenda Mungu.

Wanachuoni wengi wa Kiislamu, hususan wana-irfani (mystics), wamese- ma kwamba kila mtu huhisi katika moyo wake upendo mkubwa kwa Mungu bila ya lazima ya kuwa na habari nao. Wanahoji kwamba hata wasioamini, ambao hufukuzia tu malengo ya kiulimwengu au ya anasa, hupenda na kumuabudu Mungu katika kile wanachokichukulia kama mwisho mzuri. Kwa mfano, wale wanaotaka kuwa na nguvu (za kiutawala) hupenda kuwa na mamlaka ya juu sana. Kuwa Meya, au hata Rais hakutawaridhisha wao.

Hata kama wangekuwa wanamiliki ulimwengu mzima, watafikiria kuhusu kumiliki sayari nyingine. Hakuna katika ulimwengu kitakachotuliza roho zao. Mara tu watu wanapopata matlaba yao, wanatambua kwamba hayatoshelezi na hutaka wapate zaidi. Wana- irfani wa Kiislamu, kama vile Ibn Arabi, akisukumwa na Qur’ani, huami- ni kwamba sababu iliyopo nyuma ya jambo hili ni kwamba kila mtu kwa kweli anataka mwisho mzuri, yaani, Mungu. Qur’ani inasema:

يَا أَيُّهَا الْإِنْسَانُ إِنَّكَ كَادِحٌ إِلَىٰ رَبِّكَ كَدْحًا فَمُلَاقِيهِ {6}

“Ewe mtu! Hakika wewe unajikusuru kwa juhudi kumwendea Mola wako, basi utamkuta.” (84:6)

Hata hivyo, ukweli ni kwamba watu wengi wanafanya makosa katika kutambua ni kipi kilicho kizuri zaidi. Baadhi wanaweza kuchukulia pesa kama kitu kilicho kizuri zaidi au kwa maneno mengine, kama mungu wao. Wengine wanaweza kuchukulia nguvu za kisiasa kama mungu wao. Qur’an inasema:

أَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَٰهَهُ هَوَاهُ أَفَأَنْتَ تَكُونُ عَلَيْهِ وَكِيلًا {43}

“Je! Umemuona aliyeyafanya matamanio yake kuwa ndio mungu wake? Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake?” (25:43; 45:23)

Kama ikitokea kwamba wamefikia kile walichokipanga kama ukamilifu wao, hulka yao ya upendo kwa Mungu, uzuri wa hali ya juu, itabakia bila majibu na hivyo wataona huzuni na uvunjikaji moyo. Ibn Arabi anasema: “Hakuna kingine mbali na Mungu ambacho kimewahi kupendwa.

Mungu ndiye ambaye amejidhihirisha Mwenyewe ndani ya cho- chote kile ambacho hupendwa katika macho ya wale ambao hupenda. Hakuna kiumbe chochote isipokuwa hupenda.

Hivyo, ulimwengu wote hupenda na hupendwa, na yote haya hurejea nyuma mpaka Kwake kama ambavyo hakuna ambacho kilikuwa kinaabudiwa kingine kuliko Yeye, kwa vile chochote kile mja (wa Mungu) alichokuwa daima akiabudu, amekuwa hivyo kwa sababu ya dhana potofu ya Mungu ndani yake; vinginevyo kamwe kisingeweza kuwa kinaabudiwa.

Mungu, Mtukufu mno, anasema (katika Qur’ani): “Na Mola wako ameamuru usiabudu yoyote isipokuwa Yeye.” (17:23). Hili halikadhalika ni suala la upendo. Hakuna mtu ambaye amewahi kupenda chochote kingine kuliko Muumba wake. Hata hivyo, Yeye, Mtukufu mno, amejificha kwao chini ya pendo kwa ajili ya Zainab, Su’ad, Hindi, Layla, dunia (ulimwengu huu), pesa, nafasi ya kijamii na vitu vyote vinavyopendwa katika ulimwengu”.10

Ibn Arabi anaongeza kwamba: Wanairfani hawajawahi kusikia shairi lolote au sifa au kitu kama hicho bali kuhusu Yeye (na walimuona Yeye) nje ya mipaka ya mapazia.

Sababu nyingine ya kumpenda Mungu ni kulipa fadhila za upendo na baraka Zake. Kuna utajiri mkubwa wa fasihi katika vyanzo vya Kiislamu juu ya vipengele mbali mbali na vidhihirisho vya upendo wa Mungu na neema kwa wanadamu wote, ukichanganya, kwa busara, pamoja na watendao maovu na wale wasioamini katika Yeye.

Wanadamu humpenda yeyote yule awafanyiae wema, na hufurahia upendeleo na ukarimu kama huo na kujiona wenye kuwajibika kuwa wenye shukurani. Mtume alisema: “Mpende Mungu kwa sababu amefanya wema kwako na amekuteremshia neema juu yako.”11

Kwa mujibu wa hadith za Kiislamu, Mungu aliwaambia wote; Musa na Daudi: “Nipende Mimi na nifanye Mimi nipendeke kwa watu Wangu.”12 Kisha katika kujibu swali lao la kwa vipi watamfanya Yeye apendeke kwa watu, Mungu akasema: “Wakumbusheni kuhusu neema na ukarimu wangu, kwani hawakumbuki neema Zangu bila hisia ya shukurani”13

Katika du’a ya kiirfani, ijulikanayo kama Mnong’ono wa mwenye kushukuru, Imamu Sajjad anasema: “Ewe Mola wangu mtiririko wa fadhila Zako zisizokatika kumenichanganya nisiweze kukushukuru Wewe!

Wingi wa neema Zako umeniacha mimi bila uwezo wa kuzihesabu sifa Zako!

Mfuatano wa matendo Yako ya upole umenipotosha kutokana na kukutaja Wewe katika kukuhimidi!

Mwendelezo wa kasi ya manufaa Yako umenizuia kueneza habari za neema Zako za uungwana!”

Kisha akaongeza:-

Ee Mola wangu, shukrani zangu zimekuwa ndogo mbele ya ukubwa wa fadhila Zako, na shukurani zangu na uenezaji wa habari umenywea kando ya ukarimu Wako kwangu!

Neema Zako zimenifunika na majoho ya nuru ya imani, na upole wa wema Wako umeweka juu yangu pazia za nguvu! Upelo Wako umenifunga na vibano visivyoweza kuondolewa na kunipamba na mikufu ya shingo ambayo haivunjiki!

Fadhila Zako ni nyingi, ulimi wangu ni dhaifu mno kuweza kuzihesabu!

Neema Zako ni nyingi, ujuzi wangu unashindwa kuzifahamu, bila ya kuzungumzia kumalika kwao!

Hivyo vipi nitapata kushukuru?14

Muumini ambaye ameanza safari yake ya kiroho kuelekea kwa Mungu, kwanza hufikia kwenye kutambua baraka za Mungu juu yake, katika ukweli kwamba Mungu humpa riziki nyingi na msaada ambao humuwezesha kutenda. Akiwa ameendelea na safari yake huku akiwa amesheheni mtazamo wa kiirfani wa ulimwengu, atatambua kwamba hakika kila kitu kizuri hutoka kwa Mungu Mwenyewe.

Tunasomaa katika Qur’ani:

مَا أَصَابَكَ مِنْ حَسَنَةٍ فَمِنَ اللَّهِ ۖ وَمَا أَصَابَكَ مِنْ سَيِّئَةٍ فَمِنْ نَفْسِكَ ۚ {79}

Wema wowote uliokufikia (Ewe mwanadamu), umetoka kwa Mwenyezi Mungu, na ubaya wowote uliokufikia, unatoka kwako mwenyewe.” (4:79)

Hakuna haja ya kufikiria vinginevyo. Sababu ya kulazimisha mateso ya kidhalimu inaweza kuwa moja ya sababu zifuatazo au mchanganyiko wa zote:

Ukosefu wa uwezo: Mtu ambaye huwaonea wengine anaweza kufanya hivyo kwa sababu anataka kupata kitu kutokana na uonevu huo, au kwa sababu hawezi kujizuia kufanya kitu chenye madhara kwa wengine.

Ukosefu wa elimu: Mtu anaweza kuwa na nia njema ya ukarimu, lakini kwa sababu ya ukosefu wa taarifa au kufanya maamuzi yenye makosa anaweza kufanya kitu ambacho humuumiza mtendewa.

Chuki na nia mbaya: Mtu anaweza kuwa na uwezo wa kufanya matendo mazuri na vilevile anaweza kujua jinsi ya kuyafanya, lakini anashindwa kufanya hivyo, kwa sababu sio mpole vya kutosha kufanya hivyo, au hata vibaya zaidi, kwa sababu anamchukia mtendewa na anataka kukidhi hasira na ghadhabu kwa kusababisha maumivu juu ya mtendewa.

Wanafikra wa Kiislamu wanahoji kwamba, kamwe Mungu hafanyi kitu chochote cha uovu au cha madhara kwa waja Wake, kwa vile hakuna katika sababu lizotajwa hapo juu za kuwa hivyo: Yeye ni Mwenye nguvu zote, Mwenye ujuzi wote na Mwingi wa Huruma.

Hivyo, picha ya Mungu katika Uislamu ni picha ya Yule Ambaye ni pendo, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu na Mwingi wa Ukarimu, Yule ambaye huwapenda viumbe wake zaidi kuliko vile ambavyo wangempen- da Yeye au wao wenyewe, Yule ambaye hasira na ghadhabu zake ni kutokana na upendo na hutanguliwa na upendo. Inaonekana hakuna tofau- ti miongoni mwa Waislamu katika kuamini Mungu ambaye ni pendo, ingawa wanaweza kutofautiana katika kiasi cha msisitizo ambao wanauweka juu ya kipengele hiki cha mtazamo wa ulimwengu wa Kiislamu ukitofautisha na wengine. Kwa ujumla, inaweza ikasemwa kwamba wanairfani wa Kiislamu na Masufi wanahusika zaidi na kipengele hiki cha Uislamu kuliko mafilosofa wa Kiislamu, na kwa upande mwingine mafilosafa wanahusika zaidi kuliko wanateolejia.

Lakini, kama ilivyotajwa kabla, hakuna kutokuelewana katika kumuona Mungu kama Yule ambaye ni pendo, Mwenye Kurehemu na Mwingi wa Ukarimu. Tunasoma katika Qur’ani kwamba katika kujibu dua ya Nabii Musa kwa ajili ya maisha mazuri katika ulimwengu huu na ulimwengu ujao, Mungu alisema:

لَ عَذَابِي أُصِيبُ بِهِ مَنْ أَشَاءُ ۖ وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ ۚ {156}

“… (Ama kwa) Adhabu yangu nitamfikishia nimtakaye, na rehema yangu imeenea kila kitu…” (7:156)

Tunakuta katika Qur’ani kwamba kundi la Malaika ambao hubeba Arshi ya Mungu wakiomba:

وَيَسْتَغْفِرُونَ لِلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَحْمَةً وَعِلْمًا فَاغْفِرْ لِلَّذِينَ تَابُوا وَاتَّبَعُوا سَبِيلَكَ وَقِهِمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ {7}

“…Ewe Mola wetu! Umekienea kila kitu kwa rehema na elimu, kwa hiyo, basi wasamehe waliotubu na wakaifuata njia yako na waepushe na adhabu ya Jahannam.” (40:7)

Ingawa pendo la Mungu sio holela na linaweza kutofautiana kutoka maudhui moja kwenda nyingine, kutokana na ubora wao, Huwapenda viumbe wote. Upendo wake kwa wafanyao makosa na wale ambao wamegeuza migongo yao Kwake ni mkumbwa mno kiasi kwamba huvuka kabisa mategemeo yao. Msisitizo juu ya kipengele hiki cha upendo wa Mungu kina sehemu kubwa ya fasihi ya Kiislamu, ikiwemo Aya za Qur’ani, Ahadith na mashairi. Kwa mfano, tunasoma katika Qur’ani:

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنْفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِنْ رَحْمَةِ اللَّهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ {53}

“Sema: Enyi waja wangu! Mliojidhulumu wenyewe, msikate tamaa katika rehema za Mwenyezi Mungu, bila shaka Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote, hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe Mwenye kurehemu.” (39:53)

Wazo la kutubia ni moja kati ya dhana za msingi katika suala hili. Katika Aya nyingi za Qur’ani, Mungu anazungumzia uwezekano wa kutubia siku zote na kurejea Kwake, kwani Yeye ni Mwingi wa kusamehe. Anasema:

فَمَنْ تَابَ مِنْ بَعْدِ ظُلْمِهِ وَأَصْلَحَ فَإِنَّ اللَّهَ يَتُوبُ عَلَيْهِ ۗ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ {39}

“Lakini mwenye kutubia baada ya dhulma yake, na akatenda wema, basi Mwenyezi Mungu atapokea toba yake, hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” (5:39)

Qur’ani vilevile hurejea kwenye ukweli kwamba Mungu hawasamehi tu wale ambao wanatafuta msamaha, bali vile vile Anaweza kubadilisha matendo yao mabaya kwenye kuwa matendo mema. Kwa wale ambao hutubia na kuamini na kufanya matendo mema, Qur’ani inasema: “…Basi hao ndio ambao Mwenyezi Mungu atawabadilishia maovu yao kuwa mema, na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” (25:70)

Inavutia kwamba katika Qur’ani, Mungu hawasilishwi tu kama Mwenye kukubali toba ya kweli ya waja wake na kuwasamehe wakati wakimgeukia Yeye. Hakika, ni Mungu Mwenyewe ambaye kwanza huwahudumia waja Wake ambao wamevunja, kwa njia moja au nyingine, uhusiano wao wa utumwa na Mungu, lakini bado wana upendo juu ya wema na ukweli katika nyoyo zao (yaani, nyoyo zao hazikupigwa muhuri).

Mungu huwasamehe waja kama hao na kisha wanatubia na kurejea Kwake, na kisha Mungu hugeukia kwao na kuwasamehe. Kwa hiyo, kama anavyoelezea S.H. Tabatabai mwandishi wa Al-Mizan kwenye tafsri ya Qur’ani katika juzuu ya 20, kila toba moja na istighfara ya mja mkosaji hufuatiwa na misamaha miwili ya Mungu: msamaha wa kwanza humpa mtu huyo uwezo kwa ajili ya toba ya hiyari na masamaha wa pili ni msamaha Wake (Mungu) baada ya mtu kutubia. Ukweli kwa uwazi umedokezwa na Qur’ani:

وَظَنُّوا أَنْ لَا مَلْجَأَ مِنَ اللَّهِ إِلَّا إِلَيْهِ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ لِيَتُوبُوا ۚ إِنَّ اللَّهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ {118}

“…Wakadhani kuwa hakuna pa kumkimbilia Mwenyezi Mungu ila kuelekea Kwake, kisha akawaelekea ili wapate kutubu, hakika Mwenyezi Mungu ndiye apokeaye toba, Mwenye kurehemu.” (9:118)

Kwa mujibu wa wanairfani wa Kiislamu, ujuzi wa mtu juu ya Mungu kama aliye mbora sana na mkamilifu na chanzo cha vitu vyote vizuri, na upendo wa mtu kwa Mungu Ambaye ni Pendo na Rehema, huwa imara sana na hivyo kukizunguka kile chote kitakachokaa moyoni mwa mtu. Wakati huo huo, ujuzi wa udhaifu wa mtu na kasoro mbele za Mungu huwa na nguvu sana na wa kina sana kiasi kwamba mtu atahisi hali ya utupu na kutokuwepo kitu.

Kama ambavyo mtu huyo anapoteza ubinafsi na kuwa mkarimu, atatambuliwa kwa kila aina ya uzuri. Kutoka kwenye hali ya kutokuwa na kitu, mtu hufikia daraja ya ‘hali ya kuwa na kila kitu’. Hatahisi ukomo au kizuizi. Katika hadithi mashuhuri, tunasoma kwamba “Utumwa kwa Mungu ni kiini, ambacho asili yake ni utawala”. (Shomali, 1996, uk. 32). Mtumwa halisi wa Mungu ambaye utashi wake umelingana kwenye utashi Wake ana uwezo wa kufanya matendo yasiyo ya kawaida.

Sheikh Mahmud Shabistari katika kitabu chake Sa’adat-Nameh ana maele- zo mazuri sana ya kile anachokichukulia kuwa ni hatua tofauti za safari ya kiroho kuelekea kwa Mungu. Anasema:

“Utumishi na ibada ya Mungu
ni imla ya Mwingi wa Huruma
kwa kila kiumbe: mtu na jinni sawa sawa.
Na bado amri yake humbana ajieleze
Mteule mno zaidi, kama Mungu alivyosema:
“Sikuumba majinni na watu
ila wapate kuniabudu.” (Qur’ani 51:56)

Kupitia ibada mtu huletwa kwenye sala (maombi);
Kutoka kwenye sala mpaka kwenye fikra za kiirifani, na kisha kutoka kwenye fikra
Moto wa irifani hulipuka, mpaka aone
ukweli kwa jicho lndani la tafakari.
Hikima kama hiyo huja kutoka kwenye upendo usio na uchoyo [au upole]: Ya mwisho ni matunda yake, ya kwanza ni tawi.

Hatimaye huja upendo ambao huondosha vinginevyo vyote:
Upendo hutangua maana zote za ‘mbili’;
Upendo hufanya zote kitu kimoja,
Mpaka hakuna ‘changu’
Wala ‘chako’
Kubakia.”15

Suhrawardi katika The Reality of love anafafanua mtazamo wake juu ya safari ya kiroho. Anaamini kwamba safari hii na hali zake na vituo vyake hutokeza kwenye wema (husn), upendo (mihr) na huzuni yenye tafakari (huzn). Anahusisha wema kwenye ujuzi wa Mungu na upendo kwenye ujuzi wa nafsi. Huzuni ni matokeo ya ujuzi wa kile kilichokuwa hakipo na kisha kikawepo.

Suhrawardi anaamini kwamba ujuzi wa nafsi huongoza kwenye uvumbuzi kwamba nafsi ni ya kimungu na hili husababisha katika kumpenda Mungu na kuwa na uzoefu wa kiirifani. Kwa hakika ni wazo la ki-Qur’ani ambalo linasisitizwa kwa uwazi na kwa wingi sana na Sunnah kwamba kuna ulazima wa uhusiano kati ya mtu kujua nafsi yake na kumjua Mola wake. Kwa mfano, Mtume Muhammad alisema: “Yeyote yule ambaye anaijua nafsi yake amemjua Mola wake.”16

Suhrawardi anaamini kwamba huzuni inasababishwa na kutafakari juu ya utaratibu ambao huonesha utenganisho wa mtu na uondakaji wake kutoka kwenye makazi yake ya asili.17

Kwa mujibu wa Uislamu, upendo kwa Mungu ni mashughuli sana na hudhihirika wenyewe kwenye vipengele vyote vya maisha ya mtu. Hutengeneza upendo wa mtu na chuki. Vile vile hutengeneza tabia ya mtu pamoja na watu wengine na nafsi ya mtu mwenyewe. Katika hadithi mashuhuri ya nawafil (ibada za suna) tunasoma: “Hakuna kinachomfanya Mja wangu kuwa karibu na Mimi kulinganisha na utekelezaji wa matendo ya wajib, wajibat.

Mja wangu daima hukaribia karibu na Mimi kwa nawafil mpaka nimpende. Wakati ninapompenda, basi nitakuwa masikio yake ambayo husikilizia, macho yake ambayo kwayo huonea, ulimi wake ambao kwawo huzungumzia, na mikono ambayo kwayo hushikia: kama akiniita Mimi, nitamjibu, na kama akiniomba Mimi, nitampa.”18

Mpenzi muaminifu hana uwezo wa kumuasi mtu mpendwa au kukataa matakwa yake. Imamu Ja’far al-Sadiq alisema: “Je, unamuasi Mungu na kujifanya unampenda? Hii ni ajabu. Kama ungekuwa mkweli ungelimtii Yeye, kwani mpendwa ni mnyenyekevu mbele ya mtu anayempenda.”19

Tunasoma katika Qur’ani: “Enyi mlioamini! Atakayeiacha dini yake miongoni mwenu, basi hivi karibuni Mwenyezi Mungu ataleta watu (ambao) atawapenda, nao watampenda, wanyenyekevu kwa Waislamu, wenye nguvu juu ya makafiri, wanapigania Jihad katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawaogopi lawama za wenye kulaumu.......” (5: 54)

Historia ya Uislamu imejaa kumbukumbu za wale ambao wameshirikisha upendo halisi na uliokithiri juu ya Mungu na dini Yake. Mmoja wa wale ambaye amejitoa nafsi yake kwa moyo wote kwenye Uislsmu alikuwa ni Bilal Al-Habashi, mtumwa mweusi.

Makafiri wa Makka walimtesa wakimtaka ataje majina ya masanamu yao na kuelezea imani yake kwao na kuukufuru Uislamu. Walimtesa katika jua linalochoma kwa kumlaza kwenye mawe yenye kuunguza na kuweka mawe mazito juu ya kifua chake. Abu Bakar sahaba tajiri wa Mtume, alikuwa anapita wakati aliposikia kilio cha Bilal. Alikwenda karibu na kumshauri afiche imani yake, lakini Bilal hakuwa tayari kufanya hivyo, kwa vile upendo daima ulikuwa wenye vuguvugu na wa hatari. Akielezea tukio hili, Rumi anasema:

Bilal alikuwa anautoa mwili wake kwenye miba:
Bwana wake alikuwa akimchapa viboko kwa njia ya kusahihisha,
[Akisema] “Kwanini wewe unampenda Ahmad [jina lingine la Mtume]?
Mtumwa muovu, asiyeamini katika dini yangu!”

Alikuwa akimpiga katika jua kali na miba
[Ambapo] alilia kwa kujigamba “Mmoja!”
Mpaka Siddiq [Abu Bakar] alipokuwa anapita karibu na sehemu hiyo,
Kile kilio cha “Mmoja” kiliyafikia masikio yake,
Baadae alimuona katika faragha na akamuonya:

“Ficha imani yako,
Yeye [Mungu] anajua siri [zote] zilizojificha: ifiche shauku yako.”
Yeye [Bilal] akasema: “Najuta mbele yako wewe, Ewe mwana wa Mfalme.”
Kulikua na kujuta kwingi kwa namna hii,
[Mpaka] hatimaye akaacha kujuta,
Na akatangaza na kujitoa mwili wake kwenye taabu [majonzi],
[Akilia]: “Ewe Muhammad! Ewe adui wa nadhiri na majuto!
Ee wewe ambaye umejazwa kwenye mwili na mishipa yangu yote!
Vipi kutakuwa na nafasi ndani yake ya kwa ajili ya majuto?
Kuanzia sasa nitaondosha majuto kutoka kwenye moyo huu.
Vipi nitajutia juu ya maisha ya milele?”

Upendo ndio mtulizaji wa yote, na nimetulizwa kwa upendo:
Kwa upofu wa upendo nimefanywa mnga’avu kama jua.

Ee upepo mkali, mbele Yako Wewe mimi ni bua:
Vipi nitajua wapi nitaangukia?
Iwapo mimi ni Bilal au mwezi mwandamo,
Nakimbia na kufuata mwendo wa jua Lako.
Mwezi una nini cha kufanya na unene au wembamba?
Hukimbia kwenye visigino vya jua, kama kivuli.

Wapenzi wameangukia kwenye mvo mkali:
Wameweka nyoyo zao kwenye amri ya upendo.
[Wako] kama kijaa kinachozunguka zunguka
mchana na usiku na kuomboleza kusikokwisha.20

Upendo Wa Mwanadamu Kwa Wanadamu Wenzake

Muumini ambaye anampenda Mungu anategemewa kuwapenda watu Wake na kuwa na huruma kwao. Mtume alisema: “Enyi waja wa Mungu, na iwe kupenda kwenu na kuchukia kwenu kuwe ni kwa ajili ya Mungu, kwa sababu hakuna awezaye kupata wilayah (uongozi) ya Mungu bila hilo, na hakuna atakaye pata mwonjo wa imani bila hilo, ingawa swala zake na saumu zake ziwe nyingi kwa idadi.”21

Kama kupenda kwa mtu na kuchukia kwake ni kwa ajili ya Mungu tu, itakuwa vigumu kwake kutowapenda watu Wake. Juu ya haja ya upendo kwa watu, tunaona kwamba Qur’ani inawasifia wale watu wa nyumba ya Mtume ambao walifunga siku tatu na kutoa kila siku chakula chao kidogo amacho walikuwa nacho nyumbani siku ya kwenza kwa masikini, siku ya pili kwa yatima siku ya tatu kwa mfungwa: “Na huwalisha chakula masikini na yatima na mfungwa hali ya kuwa wanakipenda. (Husema) Tunakulisheni kwa ajili ya radhi ya Mwenyezi Mungu tu, hatutaki kwenu malipo wala shukurani.” (76: 8-9)

Kuna hadithi maarufu sana iliyosimuliwa katika vyanzo tofauti kwamba Mtume alisema: “Watu wote ni wa familia ya Mungu, hivyo watu wapenzi sana kwake ni wale ambao hunufaisha familia Yake zaidi.”22 Kwa mujibu wa hadithi, na sawa na kile kilichotajwa katika Agano jipya (Mt; 25:31-46) Siku ya Hukumu Mungu atawauliza baadhi ya watu kwa nini hawakumtembelea wakati alipokuwa mgonjwa, kwa nini hawakumpa maji wakati alipokuwa ana kiu. Watu wale watauliza: Hii imewezekana vipi kutokea ambapo Wewe ni Mola wa ulimwengu?

Kisha Mungu atawajibu: Fulani wa fulani alikuwa mgonjwa hukumtembelea na fulani wa fulani alikuwa na njaa na hukumlisha na fulani wa Fulani alikuwa na kiu na hukumpa maji ya kunywa. Je, hukujua kwamba kama ungefanya hivyo ungenikuta pamoja naye?23

Hivyo katika Uislamu upendo una jukumu muhimu sana katika maadili imani irifani (mafundisho ya kumfikia mungu kwa tafkira), teolojia na hata filosofia. Kuleta taswira ya Kiislamu ya ulimwengu pamoja na hadithi ya uumbwaji wa ulimwengu na binadamu na kisha utendeaji wa Mungu kwa binadamu mtu siku zote ana hitaji kuomba kwa Mungu dhana ya upendo. Mungu mwenyewe ni pendo na ameumba ulimwengu kwa upendo. Huwatendea wanadamu kwa upendo.
Imani vilevile huanza na upendo, upendo ulioshinda kabisa kwa ukweli fulani, na unatakiwa kustawishwa kwa lishe ya pendo hili mpaka kiwango cha kufikia kwamba upendo wa mtu kwa Mungu hujaza moyo wote wa mtu na ukaelekeza vipengele vyote vya maisha.

Upendo kwa Mungu unaweza kuongezeka tu wakati tunapopunguza ubinafsi wetu na kama mwishowe tunaweza kuondokana na ubinafsi tutakuwa watu wakamilifu ambao utashi na ridhaa zao zitakuwa ni utashi na radhi za Mungu.

Upendo kwa Mungu na uhuru kutokana na ubinafsi unaweza kupatikana kwanza kwa kujitolea mhanga na kuachana na matamanio yetu kwa ajili ya Mungu na watu Wake na kisha kwa kutokuwa na matamanio zaidi ya yale ambayo Mungu anayatamani na hakuna utashi zaidi kuliko wa kwake. Basi, hakika, hakutakuwa na muhanga na hakuna maumivu. Hukumu za uadilifu ni mwongozo kwenye njia hii ya upendo, ikiangazwa kuelekezwa kwa mafundisho ya wasomi na mitume.

Hitimisho

Dini zote mbili Ukristo na Uislamu huona upendo kuwa ni dhana kubwa ya imani zao. Katika ukristo upendo ni nemsi kubwa sana (1Kor. 13:13) na amri ya upendo ni amri ya kwanza iliyo kubwa sana (Mark. 12:28-31 Mat.22:34-40, Luk. 20:25-28). Kati Uislamu ‘upendo ndio kishikio madhubuti cha imani’24 upendo ni imani. 25

Katika dini zote upendo umehusishwa kwa Mungu na halikadhalika kwa wanadamu. Hata hivyo upendo wa Mungu ni tofauti na upendo wa mwanadamu. Upendo wa Mungu ni halisi, ni milki kwa vile Mungu Mwenyewe ni upendo.26 Katika suala la binadamu, upendo ni kiarifu, kitu cha bahati kisichotegemewa kwao na chenye kuweza kuondolewa kutoka kwenye asili yao.

Upendo wa Mungu ni wa daima dumu. Hutupenda kwa pendo la daima na kudumu. Ameumba ulimwengu na mwanadamu kwa upendo. Mungu anawapenda wanadamu mno sana kiasi kwamba ameumba kila kitu katika ardhi kwa ajili yao. (Katika Ukirsto kwa mfano, Zab. 8:4-8; Katika Uislamu Qur. 2: 29 & 45:13) Katika Ukristo upendo wa Mungu kwa mara nyingi huonekana katika muundo wa uzazi. Vile vile wakati mwingine hufananishwa na upendo wa bwana harusi kwa bi harusi wake. Katika Uislamu zahania zaidi na mwelekeo wa ruiya kwa Mungu na upendo wake hutwaliwa. Upendo wa Mungu kwa mtu ni mkubwa zaidi kuliko ule wa mama au wa baba kwa mwanawe.

Kamwe Mungu haitwi baba au bwana harusi. Katika Uislamu kitu cha karibu nijuacho kwa kielezo cha ubaba na umama, na sio kile cha bwana harusi au biharusi ni kile ambacho kinaweza kuonekana katika hadithi, (na sio katika Qur’ani) kwamba watu huchukuliwa kama ‘yaal’ Wake. Neno hili linaweza kutafsiriwa kama familia, lakini maana yake halisi ni kikundi cha watu ambacho mtu huchukua utunzaji wake na kwake yeye huwajibika kwa matumizi yao ya maisha. Kwa njia hii, hujumuisha wazazi wa mtu au hata wageni, kama vile yatima ambao mtu amechukuwa jukumu la kuwalipia matumizi yao Kwa hiyo Mungu hawasilishwi kama baba na watu hawawasilishwi kama watoto wake - au hata familia yake. Naam, hakika Mungu anapenda watu wote na huwaruzuku watu wote na hata wasiokuwa wanadamu kwa njia ya riziki zao.

Upendo wa Mungu una sifa ya ukamilifu na isiyo na ubinafsi na Hapati chochote kutokana na upendo wenyewe au kutoka kwa mpendwa. Mungu ameumba ulimwengu kuonesha mbele ukweli wake mwenyewe na uzuri wake.27 Amewaumba watu “ili ajulikane.” 28
Katika Uislamu na Ukristo upendo kwa Mungu ni kwa wote, na hutekelezwa na viumbe wote. Kwa mfano, Mt. Augustino anasema “Ee Mungu! Ambaye hupendwa kwa kujua au bila kujua na kila kiumbe kili- cho na uwezo wa kupenda.” Ibn Arabi anasema: “Hakuna chochote kama Mungu ambacho kiliwahi kupendwa.”

Katika simulizi zote hizo hapo juu upendo wa mwanadamu kwa Mungu huenea mpaka kwa wanadamu wenzake. Kwa kawaida wale ambao huaminiwa kuwa karibu na Mungu hustahiki upendo zaidi. Katika Ukristo baadhi ya semi muhimu za Agano jipya (1Yoh.4:7-5:4) hufichua haja ya mtu kumpenda mkristo mwenziwe. Upendo kwa jirani huendelea mpaka kwa watu wa nje hakikadhalika. Hujumuisha hata mpaka maadui. Yesu anasema: “Bali nawaambieni, wapende maadui zako na waombee wale ambao wanakutesa ….” (Mt.5, 43-45).

Katika Uislamu sifa mashuhuri ya ki-Qura!n ya Mtume Muhammad ni “Rehema kwa walimwengu wote” Rahmatu lil’AalimiIn. Katika vita vya Uhud, wakati wengi wa masahaba wake, pamoja na ami yake Hamza, walipouliwa kishahidi na makafir wa kabila lake mwenyewe, na yeye alijeruhiwa na meno yake kuvunjika, Mtume alisema:

“Ewe Mola wangu! Waongoe watu wangu, Hakika hawajui” Hivyo badala ya kuwalaani aliwaombea. Mtume Muhammad alitangaza kwamba ujumbe wake ni “wakukamilisha tabia njema” Orodha ya tabia njema hujumuisha: kuwatembelea wale ambao hawakutembelei wewe, kutoa na kuwapa msaada wale ambao hawatoi au kukupa wewe msaada, kuwa muadilifu na mkarimu kwa wale ambao hawakuchunga haki zako. Hiki ni kitu bora zaidi kuliko kulipa tu fadhila za mtu kwa mtu mwenywe.

Hata hivyo dhana ya upendo katika Uislamu imesokotana na ile ya chuki. Upendo kwa Mungu na kwa wale wema lazima uandamane na chuki kwa mwovu (shetani). Katika Uislamu imani haiwi kamili mpaka hisia na mapenzi ya mtu yote yawe yanaelekezwa na upendo kwa Mungu. Mtu wa imani hawezi kuchukia kitu au yule ambaye Mungu anampenda, kama vile ambavyo hawezi kuwapenda maadui Zake. Mungu hampendi ‘muovu yeyote asiye na shukurani’ (Qur’ani 9;109), ‘madhalimu’ (Qur’ani 3:57 & 11:40), wenye kiburi, wajivunao (Qur’ani 4:36) ‘aliye haini’ (Qur’ani 4:106).

Kwa njia hii, Uislamu unatofautisha kati ya kumpenda mtu na kupenda vitendo au tabia zake. Unaweza kumpenda mtu na bado ukachukia vitendo au tabia zake. Wakati mwingine upendo wako kwake huhitaji wewe kum- saidia na kumshauri na wakati mwingine hukuhitajia wewe kumzuia na ikiwa lazima kupigana naye. Hiki ndiyo kitu pekee ambacho mzazi wa kweli au rafiki mwenye upendo na mapenzi anachoweza kufanya kuhu- siana na mhalifu na muuwaji.

Hivyo kimsingi inaonekana kutokuwepo kwa kutokueleana kati ya Ukristo na Uislamu juu ya dhana ya upendo, ingawa kihistoria wakristo na Waislamu huenda walisisitiza vipengele tofauti au huenda waliutekeleza kwa namna tofauti. Ukweli unaofanana kama huo unaweza vilevile kuonekana miongoni mwa madhehebu tofauti za dini mmoja.

 • 1. Km. Majilesi, 1983, juzuu ya 87, uk. 344.
 • 2. Avicenna, 1956, uk. 369.
 • 3. Avicenna, 1375 A.H., Juz. 3, uk.359.
 • 4. Al-Shirazi, 1378 A.H., Juz. 2, uk. 274
 • 5. Nasr, 1989,p.321
 • 6. Al-kulayni, 1397 A.H. Kitab al- Imam wal-Kufr, “Bab al- Hubb fi Allh wal- Bughd fi Allah”, no 6,p.126
 • 7. Ibid., no.5,p.125
 • 8. Al-Majlisi, 1983, Kitab al- Iman wal -kufr, “Bab al- Hubb fi allah wal Bughd fi Allah wal Bughd fi allah”,
  Ixvi, p.238.
 • 9. Siraj ed-Din, 1989,p.234
 • 10. Ibn Arabi,1994,Vol.2.,p.326
 • 11. al-Daylami, 1370 A.H., p.226
 • 12. al-Majlisi, 1983, Vol.8,p.351 & Vol.14,p.38; (my translation)
 • 13. Ibid.
 • 14. Chittick, 1987,pp.242 & 243
 • 15. Cited from Lewisohn, 1995, pp.231 & 232
 • 16. For a discussion on self-knowledge (ma’rifat al-nafs), See Shomali, 1996
 • 17. For a discussion on his view in this regard see Razavi, 1997, especially p. 680
 • 18. al-Kulayni, 1397 A.H., ‘Vol. 4.’ p.54
 • 19. Cited from Mutahhari, 1985, Ch.6
 • 20. Mathnawi, Book 1, translated by Nicholson.
 • 21. Majlesi, 1983, Vol. 27,
 • 22. e.g. Hemyari,1417 A.H., p. 56
 • 23. Kwa mfano tazama: al-Hilli, 1982, p.374.
 • 24. e.g. al-Kulayni, 1397 A.H.,p.126
 • 25. Ibid.’p.125
 • 26. In Christianity, e.g. 1 John 4:8-16; In Islam, it is an established idea among Muslim philosophers and many theologians regarding all Divine attributes: Go is love as He Is knowledge e.g. al-Shirazi, 1378 A.H., Vol. 2,p.274.
 • 27. Graham, 1939,p.37
 • 28. e.g. Majlesi, 1983, Vol.87,p.344