read

Abu Bakr Kama Kiongozi Katika Swala

Wanahistoria wa Sunni wanadai kwamba wakati Muhammad Mustafa alipokuwa hawezi kuhudhuria kwenye Swala za jamaa kwa sababu ya maradhi yake, alimuamuru Abu Bakr kuongoza Swala za jamaa, na wanalitanguliza hili kama “ushahidi” kwamba alimtaka yeye Abu Bakr kuwa ndio mrithi wake. Kuna matoleo mbalimbali ya Hadith hii yaliyopo hadi sasa. Kwa mujibu wa mojawapo, Bilali alikuja kumuuliza Mtume (s.a.w.) kama ataongoza Swala, naye akasema: “La, mwambie Abu Bakr aongoze Swala.”

Kuna toleo la pili ambamo wakati wa Swala, Mtume (s.a.w.) alimuuliza mtu mmoja, Abdullah bin Zama’a alikokuwa Abu Bakr. Ibn Zama’a alitoka nje kwenda kumwita Abu Bakr lakini hakumpata. Bali alimpata Umar, na akamwambia aongoze Swala. Lakini pale Umar alipotamka takbir (Allah-u-Akbar), Mtume (s.a.w.) alimsikia, naye akasema: “Hapana! Hapana! Allah (s.w.t.) na waumini wanakataa hiyo. Mwambie Abu Bakr aongoze Swala hiyo.”

Kufuatana na Hadith ya tatu, Mtume (s.a.w.) aliwauliza wale waliokuwa karibu naye kama wakati wa Swala ulikuwa umekwishafika. Wakasema umefika, ndipo akawataka wamwambie Abu Bakr aongoze hiyo Swala ya jamaa. Lakini mkewe, Aisha, akasema kwamba baba yake alikuwa mtu mwenye huruma sana, na kama ataona nafasi yake (Mtume) pale Msikitini iko wazi, yeye (Abu Bakr) atalia sana, na hakuna atakayeweza kusikia sauti yake.
Lakini Mtume (s.a.w.) alisisitiza kwamba Abu Bakr asimame kama kiongozi wa Swala. Zipo Hadith nyingine pia kama hizi katika vitabu vya historia na maudhui yao zote ni kwamba Abu Bakr aliongoza jamaa katika Swala wakati wa siku za mwisho za Mtume (s.a.w.) duniani hapa.

Muhammad Ibn Ishaq

Ibn Shihab alisema, Abdullah ibn Abu Bakr bin Abdur Rahman bin al-Harith bin Hisham aliniambia kutoka kwa baba yake kutoka kwa Abdullah bin Zama’a bin al-Aswad bin al-Muttalib bin Asad kwamba wakati Mtume (s.a.w.) alipokuwa mgonjwa sana na mimi pamoja na idadi fulani ya Waislamu tulikuwa pamoja naye, Bilali alimwita kwa ajili ya Sala, na akatuambia kuwa tumuamuru mtu maarufu aongoze hiyo Swala. Hivyo nilitoka nje na hapo alikuwepo Umar na watu, Abu Bakr hakuwepo pale. Nilimwambia Umar asimame na kuongoza Swala, alifanya hivyo, na alipose- ma Allah-u-Akbar, Mtume (s.a.w.) akasikia sauti yake, kwani alikuwa na sauti yenye nguvu sana, na akauliza alikokuwa Abu Bakr, akisema mara mbili zaidi, “Allah (s.w.t.) na Waislamu wanakataa hiyo,”

Kwa hiyo nikatumwa kwa Abu Bakr na aliku- ja baada ya Umar amekwisha maliza Swala ile naye akaongoza.

Umar akaniuliza ni nini nilichokifanya hasa, akisema, “Pale uliponiambia niongoze Swala, nilidhani kwamba Mtume (s.a.w.) amekupa amri kwa jambo hilo; lakini kwa hilo nisingeweza kufanya hivyo.” Nilijibu kwamba hakunituma kufanya hivyo, bali pale nilipokuwa sikuweza kumpata Abu Bakr nilidhani kwamba yeye (Umar) alikuwa anastahili zaidi ya wale waliokuwepo kuongoza Swala.
(The Life of the Messenger of God)

Yaliyopita ni maelezo ya mwanzoni kabisa yaliyopo hadi sasa ya Hadith kwamba Abu Bakr aliongoza Swala. Msimulizi wake alikuwa ni Abdullah bin Zama’a. Yeye mwenyewe anasema kwamba Mtume (s.a.w.) alimtuma yeye kumwambia mtu maarufu ambayo ina maana mtu yoyote, aongoze Swala, na hakumtaja makhsusi Abu Bakr. Hata baadae, wakati Mtume (s.a.w.) alipomkataza Umar kuongoza Swala, hakumuamuru Abu Bakr kuchukua nafasi yake. Aliuliza tu alikokuwa Abu Bakr.

Abdullah bin Zama’a alidhani kwamba Umar alikuwa ndiye “mwenye kustahili zaidi” kuongoza Swala lakini Mtume wa Allah (s.a.w.) hakukubaliana naye.

Sir William Muir

Imesimuliwa kwamba katika tukio moja Abu Bakr alitokea kutokuwepo wakati adhana ya Swala ilipopigwa na Bilali, na kwamba Umar akiwa amepokea, kama alivyoamini kimakosa, amri ya Muhammad kuongoza katika nafasi yake, alisimama pale Msikitini, na katika sauti yake nzito akaanzisha Takbir, “Mungu ni Mkubwa!” kwa matayarisho ya Swala. Muhammad akisikia hili kwa bahati tu kutoka nyumbani kwake, alikemea kwa kutumia nguvu, “Hapana! Hapana! Allah (s.w.t.) na kundi zima la waumini wanakataza hilo! Si mwingine bali Abu Bakr! Asiongoze Swala mtu mwingine bali yeye tu.”
(The Life of Muhammad, London.1877)

Kama ilivyoelezwa hapo juu, kwa mujibu wa wanahistoria wa Sunni, lengo la Mtume (s.a.w.) katika kumuamuru Abu Bakr kuongoza Swala lilikuwa ni “kumtangaza” yeye kama mrithi wake.

Inawezekana kabisa kwamba Abu Bakr aliongoza Waislamu katika Swala katika wakati wa uhai wa Mtume (s.a.w.) mwenyewe. Ambacho, hata hivyo, kisichoelewaka ni kama ali- fanya hivyo kwa amri ya Mtume, au, angalau kwa idhini yake ya kimyakimya. Dai la kwamba Abu Bakr aliongoza Swala kwa amri ya Mtume (s.a.w.) linaleta maswali kwa sababu alikuwa afisa mdogo katika jeshi la Usamah, na Mtume (s.a.w.) alikuwa amemua- muru yeye kuondoka Madina na kupiga ripoti kwa Mkuu wake wa Kikosi huko Jurf ambavyo, inavyoonekana, kamwe hakufanya hivyo.

Hata kama ikichukuliwa kwamba Mtume (s.a.w.) alimuamuru Abu Bakr kusimama kama Imamu (kiongozi wa Swala), bado haieleweki kama ni vipi ilikuwa ni “kuidhinishwa” kwa ugombea wake wa urithi.

Hata hivyo, Abu Bakr mwenyewe, Umar bin al-Khattab, na Abu Ubaidah ibn al-Jarrah, wote watatu walikwisha tumika chini ya Amr bin Al-As katika vita vya Dhat es-Salasil, na waliswali Swala zao nyuma yake kwa majuma mengi tu. Amr bin Al-Aas aliliweka wazi kwao wote watatu kwamba yeye alikuwa ndiye bosi wao sio tu kati- ka jeshi bali pia kama kiongozi katika ibada za kidini.

Kama ilivyokwisha kuelezwa, Waislamu wa Sunni wanashikilia kwamba Mtume (s.a.w.) alimchagua Abu Bakr kuongoza Swala ya jamaa kabla tu ya kufa kwake kwa sababu alim- taka yeye awe ndiye khalifa wake.

Ibn Hajar Makki, mwanahistoria wa Sunni, anasema katika kitabu chake, Tathiir al-Janan (uk.40): “Abu Bakr aliwaongoza Waislamu katika Swala (kwa amri ya Mtume). Hii, kwa hiyo, ni ijma (makubaliano) ya wanazuoni wote kwamba ukhalifa wake ulikuwa kwa agizo la Mtume.”

Lakini Masunni haohao pia wanalichukulia wazo la kwamba kuwaongoza Waislamu wengine kwenye Swala hakutunukii heshima yoyote juu ya muongozaji mwenyewe, na kwamba sio lazima kwa mtu kuwa na “sifa stahilivu” kusimama kama Imamu (kiongozi wa Swala). Kwa kuhusiana na hili, wananukuu “Hadith” ifuatayo ya Mtume wa Uislamu (s.a.w.) iliyosimuliwa na Abu Hurayra: “Swala ni wajibu wa lazima juu yenu, na unaweza kuiswali nyuma ya mwislamu yoyote hata kama ni fasiq (hata kama anatenda madhambi makubwa).”

Kwa mujibu wa “Hadith” hii mtu fasiq (mtenda madhambi) anastahili vilevile kuwa Imam wa Swala kama mtakatifu; katika suala la kusimama kama Imam, mwenye dhambi na mtakatifu wanakuwa na usawa!

John Alden Williams

Na kuwasikiliza na kuwatii Maimam na Ma-Amirul-Mu’minin (ni lazima) – Yeyote yule aliyeupata Ukhalifa, ama awe mchaji au fisadi, ama watu walikubaliana naye na wanamfurahia au kama aliwashambulia kwa upanga mpaka akawa Khalifa na akaitwa “Amirul-Mu’minin.” Kwenda kwenye vita tukufu (jihad) kunafaa pamoja na mchaji au kamanda fisadi mpaka siku ya Qiyamah; mtu hamuachi yeye. Ugawaji wa ngawira za vita na kutoa adhabu zilizoagizwa na Sheria ni kwa Maimam. Haiwi kwa mtu yeyote kuwashutumu au kushindana nao. Kukabidhi pesa za Zaka kwao (kwa ajili ya ugawaji) inaruhusiwa na inafaa; yeyote anayewalipa wao atakuwa ametimiza wajibu wake iwe huyo Imam alikuwa mcha-mungu au fasiq. Swala ya mkusanyiko nyuma ya Imam na wale anaowaongoza ni halali na kamili; rakaa zote. Yeyote atakayezirudia ni mzushi, anayeitelekeza Hadith na kupinga Sunnah. Hakuna lazima kabisa katika Swala yake ya Ijumaa, kama haamini kuswali na Maimam, wawe wowote wale, wazuri au wabaya; iliyo Sunnah ni kuswali rakaa mbili nao na kulichukulia jambo hilo kuwa limekwisha. Katika hilo usiache shaka yoyote katika kifua chako.(Some Essential Hanbali Doctrines from a Credal Statement in Themes of Islamic Civilization, p.31, 1971)

Kwa mujibu wa fatwa ya Hanbali iliyonukuliwa hapo juu, yeyote na kila mtu anaweza kuwaongoza Waislamu katika Swala. Abu Hurayra na Abu Sufyan wanazo sifa zinazostahili sana kuweza kuwa viongozi wa Swala kama Abu Bakr.

Dhana hii iliundwa na vizazi vya baadae vya Waislamu. Mtu mmoja ambaye hakuishiriki pamoja nao, alikuwa ni Muhammad Mustafa, Mfasiri wa Ujumbe wa Mwisho wa Allah kwa wanadamu. Alimuona Umar bin al-Khattab kuwa “hana sifa zinazostahili” kuongoza Waislamu kwenye Swala, na akamkataza kufanya hivyo. Waislamu wa Shia wanaichukulia kama ilivyokuwa ni ya uongo, ile “Hadith” ambayo Abu Hurayra ameihusisha kwa Mtume wa Uislamu (s.a.w.) kwamba ni halali kuswali nyuma ya mtu yoyote, hata aliye fasiq. Wao wanasema kwamba Imam (kiongozi wa Swala) lazima awe:

Ni Mwislamu
Mwanaume
Mtu mzima
Mwenye akili timamu
Mkweli (Muadilifu)
Mjuzi

Mtu mwenye heshima nzuri, yaani, mtu anayefahamika kuwa na tabia nzuri.

Hadithi ya kwamba Abu Bakr aliwaongoza Waislamu katika Swala katika uhai wa Mtume, ama ni ya kweli au ya uongo.

Kama ni ya kweli, basi ina maana kwamba alitekeleza wajibu ambao kwa kulingana na Abu Hurayra na mafaqihi na wanachuoni wa Ki-Sunni, mtu yeyote na kila mtu mwingine alikuwa na sifa zinazostahili kufanya, na haikumfanya yeye kuwa “maalum” kwa namna yoyote ile;

kama ni ya uongo, basi ina maana kwamba hakuongoza mkutano wowote kabisa wa Sala wakati Mtume (s.a.w.) alipokuwa bado yu hai.

Lakini kama Hadith hii ni ya kweli, basi pia ina maana kwamba Swala yoyote inayoswaliwa nyuma ya Umar ibn al-Khattab, ni halali. Mtume (s.a.w.) alisema kwamba Allah (s.w.t.) Mwenyewe hakutaka Umar kusimama kama kiongozi wa Swala. Kung’ang’ania kwa Umar juu ya kuwaongoza Waislamu katika Swala, kabla au baada ya kifo cha Mtume, kusingeweza pengine kuzifanya Swala zile kuwa zisizokubalika zaidi kwa Allah (s.w.t.)!