read

Abu Bakr, Khalifa Wa Kwanza Wa Waislamu

Abu Bakr alikuwa ni mwana wa Abu Qahafa, na aliishi kama mfanyabiashara hapo Makka. Yeye alisilimu baada ya Khadija, Ali ibn Abi Talib, na Zayd bin Haritha.

Inasemekana kwamba Abu Bakr alitoa mali nyingi katika kumsaidia Muhammad (s.a.w.) kuliko mtu mwingine yeyote. Hapo Makka, aliwaacha huru watumwa wengi lakini hakuna ushahidi kwamba alitoa msaada wowote kwa Muhammad (s.a.w.). Muhammad, kwa kweli, hakutaka msaada wowote kutoka kwa Abu Bakr au kutoka kwa mtu yoyote yule, bali wakati mmoja hapo Makka, ukoo wake, Bani Hashim, ulikuwa katika hali ya kuzingirwa kwa miaka mitatu, na ulikuwa katika dhiki kubwa.

Hakuna ushahidi wowote kwamba Abu Bakr alifanya jaribio lolote la kuiondoa hiyo dhiki ya ukoo huo uliokuwa umezingirwa lakini upo ushahidi kwamba baadhi ya makafiri waliwaletea mahitaji muhimu, na walifanya hivyo kwa hatari kubwa mno juu maisha yao wenyewe.

Wakati Muhammad (s.a.w.) alipokuwa tayari kuhama kutoka Makka kwenda Yathrib, Abu Bakr alimpa ngamia. Lakini Muhammad alikataa kumpanda ngamia huyo bila kumlipia gharama yake. Kwanza alilipa gharama ya ngamia kwa Abu Bakr, kisha ndipo akampanda. Abu Bakr aliandamana na Muhammad (s.a.w.) katika safari hiyo, na alikuwa naye mle pangoni.

Binti ya Abu Bakr, Aisha, aliolewa na Muhammad (s.a.w.) na alikuwa mmoja wa wake zake wengi hapo Madina.

Dr. Montgomery Watt anaandika katika makala yake juu ya Abu Bakr katika Encyclopedia Britannica, juz. 1, uk. 54 (1973) kama ifuatavyo:

“Kabla ya Hijira (kuhama kwa Muhammad kutoka Makka kwenda Madina, A.D.622), yeye (Abu Bakr) alionekana wazi kama mtu wa pili kwa Muhammad kwa uchumba wa Muhammad kwa binti yake Aisha na kwa Abu Bakr kuwa sahaba wa Muhammad kwenye ile safari ya kwenda Madina.”

Kwa mujibu wa makala hii, hizi basi ndio zilikuwa sifa mbili muhimu za Abu Bakr za kuwa wa “pili” kwa Muhammad, yaani, (1) binti yake aliolewa na Muhammad, na (2) alisafiri pamoja na Muhammad kutoka Makka kwenda Madina!

Hivi wakuu wa nchi na viongozi wa mataifa wanachaguliwa kwa misingi ya sifa kama hizi? Kama ndivyo wanavyochaguliwa, basi Abu Bakr alikuwa na washindani sio chini ya kumi na sita kwenye kiti cha Arabia.

Kulikuwa na takriban wanaume kumi na sita ambao mabinti zao waliolewa na Muhammad (s.a.w.w.) kwa nyakati tofauti; mmoja wao alikuwa ni Abu Sufyan mwenyewe, na wawili wao walikuwa Mayahudi.

Hoja ya pili katika makala hii haina “nguvu” zaidi kuliko ile ya kwanza. Kulingana na hoja hii, Abu Bakr alikuja kuwa mkuu wa dola ya Madina kwa sababu wakati mmoja alisafiri pamoja na Muhammad kutoka mji mmoja kwenda mwingine – zoezi la ajabu la kikweli katika “mantiki ya kisayansi.”

Hapo Makka, Mtume (s.a.w.) alimfanya Abu Bakr kuwa “ndugu” wa Umar ibn al-Khattab; huko Madina, alimfanya “ndugu” wa Kharja bin Zayd.

Katika kuzingirwa kwa Khaybar, Abu Bakr alipewa bendera, na aliongoza vikosi kwenda kuiteka hiyo ngome lakini bila mafanikio.

Katika msafara wa Dhat es-Salasil, Muhammad Mustafa (s.a.w.) alimtuma Abu Bakr pamoja na wapiganaji wa kawaidi wengine 200 chini ya ukamanda wa Abu Ubaidah bin al-Jarrah kwenda kuongezea nguvu vikosi vya Amr bin Al-Aas. Huyu Amr alichukua uongozi wa vikosi vyote. Abu Bakr kwa hiyo, alitumikia mabwana wawili katika msafara mmoja – kwanza Abu Ubaidah na kisha Amr bin Al-Aas.

Vilikuwepo vita na misafara mingi ya Uislamu lakini hakuna ushahidi kwamba Abu Bakr alijipatia sifa kamwe katika mojawapo ya hizo. Katika msafara wa Syria, Mtume wa Allah alimweka Abu Bakr chini ya uongozi wa Usamah bin Zayd bin Haritha.

Mtume (s.a.w.) hakuwahi kumteua Abu Bakr kwenye nafasi yoyote ya madaraka na mam- laka, kiraia au kijeshi. Safari moja alimtuma Makka kama kiongozi wa kikundi cha mahujaji kwenda kuendesha ibada za Hijja. Lakini baada ya kuondoka kwa Abu Bakr, Mtume (s.a.w.) alimtuma Ali ibn Abi Talib kutangaza huko Makka, ile Sura ya tisa ya Qur’an Tukufu (Surat al-Bara’ah au at-Tauba), ujumbe mpya ulioshuka kutoka Mbingnii. Abu Bakr hakuruhusiwa kuisoma. Ali ndiye aliyeisoma.

Sifa nyingine pekee ya Abu Bakr ilikuwa kwamba kabla tu ya kifo cha Mtume (s.a.w.), yeye aliongoza Swala ya jamaa.

Montgomery Watt:

“Tokea 622 hadi 632 yeye (Abu Bakr) alikuwa mshauri mkuu wa Muhammad, lakini hakuwa na shughuli maarufu ya umma isipokuwa kwamba alisimamia msafara wa mahujaji kwenda Makka mwaka 631, na aliongoza Swala za jamaa huko Madina wakati wa maradhi ya mwisho ya Muhammad.
(Encyclopedia Britanicca, Juz, 1. uk.54, 1973)

Baadhi ya waandishi wanadai kwamba Abu Bakr alitokana na “familia ya kwanza ya Kiislamu.” Labda, ina maana kwamba watu wote wa familia walisilimu kabla ya watu wote wa familia yoyote nyingine kusilimu. Lakini kama mtoto na baba wa mtu ni watu wa familia yake, basi dai lake haliwezi kuwa chochote ila la uongo. Mtoto wa Abu Bakr, Abdur Rahman, alipigana dhidi ya Mtume wa Uislamu katika vita vya Badr.

Inasemekana kwamba aliposhambulia Waislamu, Abu Bakr mwenyewe alitaka kumshambulia katika pambano la watu wawili tu, lakini hakuruhusiwa kufanya hivyo na Mtume (s.a.w.).

Baba yake Abu Bakr, Abu Qahafa, aliishi Makka. Hakusilimu mpaka Makka iliposalimu amri kwa Mtume (s.a.w.) mnamo A.D. 630. Abu Bakr mwenyewe anasemekana kwamba alimleta mbele ya Mtume, na ilikuwa ni hapo tena ambapo alisilimu. Familia ambayo watu wake wote walikuwa wamesilimu kabla ya familia nyingine yoyote, ilikuwani familia ya Yasir. Yasir, mke wake, na mtoto wao, Ammar, wote watatu walisilimu kwa wakati mmoja, na walikuwa miongoni mwa Waislamu wa mwanzoni.

Wakati Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.w) alipofariki, Abu Bakr (na Umar) hawakuhudhuria mazishi yake. Walikwenda kwanza kwenye ukumbi wa Saqifah, na kisha kwenye Msikiti Mkuu, kupata na kuhesabu kura zao. Wakati huohuo, Muhammad (s.a.w.) alikuwa amekwisha kuzikwa.

Wakati Abu Bakr alipochukua madaraka ya serikali, hakuwaruhusu Waislamu kuadhimisha kipindi cha maombolezo kwenye kifo cha Mtume wao. Hapakuwa na wala mazishi ya kitaifa kwa ajili ya Muhammad Mustafa (s.a.w.), Mtume wa Mwisho na Mkuu, wa Allah (s.w.t.) Duniani; wala hakukuwa na maombolezo rasmi au yasiyo rasmi juu ya kuondoka kwake. Ilionekana kana kwamba kifo chake na mazishi yake yalikuwa ni mambo yasiyo na muhimu kabisa katika mioyo ya maswahaba zake mwenyewe.