read

Ali (A.S.) Kama Mjumbe Wa Amani

Ali kama msaidizi mkuu wa Uislamu na mlinzi na ngao ya Muhammad (s.a.w.w.), ni maudhui pana na ngumu. Bali Ali kama Mjumbe wa Amani ni maudhui pana vivyo hivyo na ngumu vivyo hivyo. Ni watu wachache, kama walikuwepo, waliopenda amani zaidi ya, au waliochukia vita kuliko Ali.

Wanafunzi wa historia wanajua kwamba maombi kwa ajili ya amani, haki na uadilifu, yanafanywa tu na wale watu ambao ni wanyonge na ambao wako katika hali ya kujihami. Hakuna sababu kwa wale wenye nguvu na wenye shari kutoa maombi kwa ajili ya amani.

Alexander the Great, Julius Ceaser, Genghis Khan, Tamerlane na watekaji wengine wakuu katika historia hawakufanya maombi yoyote kwa ajili ya amani kwa yale mataifa waliyoyashinda. Ikiwa Louis XIV na Napoleon waliwasihi kamwe maadui zao juu ya amani, ilikuwa ni pale tu majeshi yao yalipoanza kurudishwa nyuma. Katika nyakati zetu, haikuwa ni Hitler aliyekuwa akiomba amani kwa mtu yoyote; yalikuwa ni yale mataifa aliyokuwa ameyateka yaliyokuwa yakiomba amani kwa ajili ya ubinadamu. Kama kuna mpangilio wowote katika historia ambao ni wenye msimamo, ni ule wa kwamba wenye nguvu, waliolewa madaraka, wanapuuza kabisa; na wanyonge wanatafuta au wanajaribu kutafuta kimbilio kwenye maadili muhimu na misingi ya kimaadili.

Katika kanuni hii ya kawaida na ya kilimwengu, ipo hata hivyo, tofauti moja, nayo hiyo ni kwa Ali ibn Abi Talib. Hata pale alipokuwa na nguvu na maadui zake walipokuwa wanyonge, aliomba kutoka kwao amani kwa ajili ya ubinadamu, na aliwaomba wao kujiepusha na umwagaji damu. Hata pale alipokuwa mshindi, aliwatendea maadui zake aliowashinda kana kwamba wao watamuunga mkono kwa kuacha vita. Kama adui alilemewa, na alitaka kuokoa maisha yake, alichopaswa kufanya kilikuwa ni kumuomba tu Ali kuokoa maisha yake, na yeye Ali aliyaokoa maisha ya adui huyo.

Na alifanya hivyo bila ya kutanguliza masharti yoyote. Maadui zake walilijua hili kupitia uzoefu wa siku nyingi, na waliitumia kila fursa ya utambuzi huu. Wengi miongoni mwa watu walikwepa adhabu ya kifo kwa njia hii, kwa ajili ya uhaini na uasi.

Kama ilivyoonyeshwa kabla, Ali kwa desturi alikuwa na msimamo katika kutetea kanuni. Kwa desturi hii, ilimbidi alipe gharama kubwa sana. Lakini je, kulikuwa na njia nyingine? Kwake yeye kulikuwa hakuna. Kama angekuwa, kwa wakati wowote ule, katika kipindi chake, amepingana na kanuni, basi asingekuwa na tofauti na watawala wengine.

Hao watawala na viongozi wengine wanatoa heshima za waziwazi kwenye mifano na utaratibu wao binafsi lakini katika utekelezaji wanaonyesha mapenzi yao tu kwenye siasa ya hali na mali; kwenye falsafa ya siasa bila maadili; na wanaweka maslahi yao binafsi mbele ya kitu kingine chochote.

Kama Ali angepuuza kanuni kwa ajili ya sera, basi serikali yake ingekoma kuwa ni Mamlaka ya Mbinguni juu ya Ardhi. Hili hakuweza kuliruhusu. Yeye alikuwa ameuhuisha Mamlaka ya Mbinguni juu ya Ardhi ambao ulianzishwa kwanza na Muhammad (s.a.w.w.). Wote hawa walitambua kwamba “Mamlaka” hayo yalikuwa ni muundo nyeti na wenye kuweza kuvunjika, na kwamba ulikuwa unatishiwa kutoka pande zote na nguvu zenye uadui – zote, za dhahiri na za siri. Walijua pia kwamba kama wangepingana na kanuni, basi “Mamlaka” hayo yangeanguka kutokea humo. Kufanya hivyo, kwa hiyo, kulikuwa hakuwaziki kwao wao. Wao hawakupingana na kanuni, na kama ilibidi walipe gharama kubwa kwa ajili ya kuitetea, walilipa kwa furaha kabisa.
Ali alikuwa anashughulikia baa la maadili linaloletwa na vita. Yeye aliamini kwamba vita na maandalizi ya vita, vilikuwa haviendani na afya na ustawi wa jamii ya wanadamu. Kuvishinda vita (kwa maana ya kuvizuia), kwa hiyo, kulikuwa ndio mshughuliko wake mkubwa.

Kwake Ali, hakukuwa na jema lolote katika vita. Yeye bila kuyumba alizitumia na kuzitil- ia nguvu amri za Qur’an kwenye siasa na vita. Kama angeweza kupata ushindi kwa njia yenye utata, alipendelea kusamehe ushindi bali hakutafuta kimbilio kwenye udanganyifu. Taratibu zake mwenyewe na utu wake vilikuwa, kwake yeye, vina umuhimu mkubwa zaidi kuliko ushindi katika vita.

Kama ilivyokwisha kuonyeshwa mapema kwenye mlango uliotangulia huko nyuma, katika nyakati za Mtume, kila wakati Ali alipokutana na adui katika pambano, alimpa mambo matatu ya kuchagua.

Haya yalikuwa:

1. Kubali Uislamu; au,
2. Usipigane dhidi ya Muhammad ambaye ni Mtume wa Allah, na ujitoe katika vita hivi;
3. Kama machaguo hayo mawili ya awali hayakubaliki kwako, basi wewe kuwa wa kwanza kunishambulia mimi.

Wakati wa ukhalifa wake yeye mwenyewe, Ali alilazimika kupigana dhidi ya wale Waislamu ambao walisimama katika uasi dhidi ya serikali kuu. Aliwaomba wamalize migogoro kupitia majadiliano badala ya kupigana.

Kupigana, kwake yeye kulikuwa ndio chaguo la mwisho, na lenye kuchukiza sana. Lakini kama mtu yoyote alimpinga yeye, basi huyo mpinzani ilibidi awe wa kwanza kumshambulia yeye Ali. Yeye kamwe hakuwa wa kwanza kumshambulia adui yake. Alisisitiza kupigana pambano la kujihami tu.

Katika mapambano ya Mtume, kabla ya mapigano ya jumla ya vikosi, mabingwa wa kila upande walipigana wawili wawili kama vile wale wapiganaji wa kimaonyesho wa Kirumi. Katika vita vya Uhud, bingwa kutoka kwenye jeshi la Makka alitoka kwenye safu zao na kuwapa changamoto Waislamu. Ali alitoka kwenda kupambana naye. Muda kidogo baadae, Ali alikuwa amemshinda mpinzani wake, na alikuwa ameweka goti lake kifuani mwake ili kumpa pigo la kifo. Katika muda huo, kama kitendo chake cha mwisho cha ujasiri, yule bingwa aliyeanguka akamtemea Ali mate.

Kingekuwa ni kitendo cha kawaida kabisa na cha kibinadamu kwa upande wa Ali kuutumbukiza upanga wake kwenye moyo wa mkosaji wake, ambaye, sasa akiwa ameshindwa, amevunja kanuni za desturi ya uungwana wa kipagani – kosa lisilosameheka katika Arabia.

Lakini Ali alifanya kinyume chake kabisa. Alinyanyuka kutoka kwenye kifua cha adui yake, akauweka upanga wake kwenye ala yake, na akarudi kwenye safu zake mwenyewe.

Majeshi yote yalikuwa yakiangalia mfululizo wa matukio haya, na wote walishangaa laki- ni hakuna aliyeshangazwa zaidi kuliko yule adui ambaye alikuwa ameshindwa wakati uleule, na hakuweza kuamini kwamba alikuwa salama. Ni nini ilikuwa maana ya kitendo hiki cha ajabu, alijiuliza kwa mshangao; hivi Ali hatamuua kwa ufidhuli wake huu?

Yule shujaa wa Makka alinyanyuka pale chini, alimkimbilia Ali, na akamuuliza ni kwa nini hakumuua yeye. Ali akasema: “Kitendo chako cha kijinga kilinifanya mimi nikasirike. Sasa kama ingekuwa nikuue wewe, ningeridhika dhidi ya dhara binafsi. Lakini mimi sitafuti kuridhika dhidi ya madhara binafsi. Sipendi kumuua mtu yeyote kwa sababu binafsi yoyote ile.”

Yule pagani alipoyasikia majibu ya Ali, mshangao wake ukawa mkubwa zaidi kuliko mwanzo. Lakini alielewa kwamba Ali alikuwa anapigana kwa ajili ya mfano bora. Jibu la Ali lilitimiza kile ambacho upanga wake haukukitimiza; lilivunja kule kutoamini kwa adui yake, na yule adui akasilimu.

Tendo hili moja lilielezea falsafa ya Ali ya maisha. Alidhihirisha wazi kwamba chuki yake, kama vile tu upendo wake, ilikuwa haiathiriwi na hisia.

Hakuchukia au kupenda kwa ajili yake binafsi; alichukia au kupenda kwa ajili ya Allah swt. tu. Kama alipigana, ilikuwa ni kwa kutaka radhi za Allah tu; na kama alifanya amani, ilikuwa pia kwa kutafuta radhi za Allah swt. Sababu yake kamili ilikuwa ni kupata radhi za Allah swt.

Kama Ali alidharau kuua kwa sababu ya kanuni yake, alidharau pia kuua kwa sababu ya ubinadamu wake. Ilikuwa ni kwa ubinadamu wake kwamba mtu hatari na mdanganyifu kama Amr bin Al-Aas alikuwa na deni la uhai wake katika vita vya Siffin. Abbas Mahmud

Al-Akkad wa Misri anaandika katika kitabu chake, ‘Abqariyyat Imam Ali (Cairo,1970): Ushujaa na uadilifu wa Ali havikumruhusu kutumia fursa ya hali ambamo alimkuta adui yake katika hali ngumu na bila msaada. (Katika vita vya Siffin) Amr bin Al-Aas ghafla alitambua katika pambano kwamba alikuwa akikabilana na Ali, na akaanguka chini kuangukia uso wake. Mtu mwingine yoyote angeweza kumuua, na hivyo kuondosha chanzo cha matatizo ya kila wakati lakini Ali aligeuza uso wake pembeni kwa kukirihika, na hakujishughulisha naye.

Katika vita vya Siffin, Ali mara nyingi alipigana kwa kujigeuza (ili asitambulike). Yeye kwa hiyo alikuwa amejigeuza wakati Amr bin Al-Aas alipokabiliana naye lakini muda kidogo baadae akamtambua. Katika kumtambua, yeye hakupoteza fahamu za akili yake. Aliangukia uso wake na akafunua matako yake, akijua fika jinsi ambavyo Ali angeipokea hila hii. (Ali alikuwa anatabirika!)

Ali alirudi nyuma kutoka kwenye kioja hiki cha kinyaa. Afisa mdogo katika jeshi lake Ali akaguta: “Huyu ni Amr bin Al-Aas. Usimwache akatoroka. Muue huyo.” Lakini Ali aliepu- ka kumuua Amr bin Al-Aas kwa vile alivyokuwa amelala katika hali ile ya kinyonge.

Vita vya mwisho ambavyo Ali ilibidi apigane, vilikuwa ni vita vya Nahrwan, vilivyopigan- wa mwaka wa 658. Katika vita vile, mpiganaji wa kikharij alijikuta akiwa chini ya ncha ya upanga wa Ali. Akitegemea kukatwa katika vipande viwili, alinywea kwa hofu, na upanga wake na ngao vikamdondoka kutoka mikononi mwake. Lakini kwa wakati ule, alishangazwa kumuona Ali akirudisha mkono wake, kugeuza hatamu za farasi wake kutoka alikokuwa yeye, na kupambana na mtu mwingine kabisa.

Bila kuamini macho yake mwenyewe, alikemea: “Ewe Ali! Hivi ndio hutaniua mimi?” Ali akamjibu “Hapana.” Yule Kharij akauliza, “kwa nini? itamaanisha adui mmoja kupungua kwa ajili yako.”

Kisha mahojiano yafuatayo yakatokea baina yao:

Ali: Siwezi kukuua wewe sasa hivi kwa sababu umepoteza upanga wako na ngao yako, na huna chochote cha kuweza kujilinda nacho.

Khariji: Ninafahamu, na hiki ndio kile nilichokisikia tu kwamba wewe humuui adui asiyekuwa na silaha. Lakini nimesikia pia jambo jingine, na ningeta- ka kujua kama ni kweli.

Ali: Ni nini hicho ulichokisikia na ambacho unataka kukithibitisha sasa hivi?

Khariji: Nimesikia kwamba hukatai ombi hata la adui kama sio la kupita kiasi.
Kama hili ni kweli, basi ningekuomba unipe upanga wako sasa kwa vile nimepoteza wa kwangu.

Ombi hilo halikuwa la busara sana, hasa ukichukulia wakati wake na mahali pake lakini Ali hakusita.

Alikamata makali ya upanga, na akampa yule adui yake kwenye mpini. Adui huyo akauchukua, akajihakikishia yeye mwenyewe kwamba Ali alikuwa hana upanga, na akauliza:

Khariji: Sasa hivi huna silaha Ali. Hebu niambie ni nani atakayekuokoa kutokana nami sasa?

Ali: Allah. Allah ataniokoa mimi. Imani yangu iko Kwake, na wala sio kwenye huo upanga au ngao.

Jibu la Ali lilimshangaza yule Khariji asiyekata tamaa kwa mara nyingine tena, lakini pia lilimshinda, na akasema kwa mshangao:
“Umenishinda, Ewe mtu wa ajabu! Kuanzia sasa hivi, mimi nitakuwa mtumishi wako. Nitapigana upande wako dhidi ya maadui zako, na nitawaua hao.”

Pendekezo la Khariji huyu lilipaswa kumfurahisha Ali, naye alipaswa kumkaribisha yeye kwenye safu zake mwenyewe, lakini akasema: “Usipigane kwa ajili yangu wala dhidi yangu. Pigana tu kwa ajili ya Haki na Ukweli. Kama unaamini kwamba Haki na Ukweli viko upande wangu, basi kwa hali yoyote ile, pigana upande wangu.”

Mkono wa Ali ulikuwa ndio silaha yenye nguvu zaidi sana katika ghala la Uislamu. Katika kila tukio, ulifungua lango la ushindi ambapo kila mkono mwingineo ulishindwa kufanya hivyo.

Mkono wake pia ulikuwa “ufunguo” wa amani, na amani haiwezi kupata mtetezi mkubwa zaidi kuliko yeye mahali popote. Lakini kama ilivyoelezwa hapo juu, yeye alikuwa mtetezi wa amani kutoka kwenye nafasi ya nguvu, na sio kutoka moja ya unyonge. Kazi yake ilikuwa ni umbile la amani yenyewe.

Ali alikuwa hajengi ufalme. Yeye kwa hiyo, hakushughulika kama mjenga ufalme. Mjenga ufalme lazima awe mchokozi, mvamizi. Yeye lazima azishinde nchi nyingine na anapaswa aangushe falme zingine ambazo katika mabaki yake atajenga ufalme wa kwake mwenyewe. Ali hakuwa na malengo kama hayo. Kwa hiyo, yeye hakuvamia nchi yoyote. Nia yake yeye ilikuwa ni kurudisha kasi ya kazi ambayo bwana wake, Muhammad, Mtume wa Allah swt. alikuwa ameianzisha. Hili alifanikiwa kulifanya katika ile miaka michache ya ukhalifa wake.

Ali aliishi maisha halisi kabisa katika maana sahihi ya istilahi yenyewe. Vazi lake lilitengenezwa kutokana na kitambaa duni kabisa lenye viraka chungu nzima juu yake. Chakula chake kilikuwa ni magamba makavu ya mkate wa shairi uliyochacha ambayo ilimbidi ayaloweke kwenye maji ili yaweze kulika.

Mara chache, yeye alikula tende kiasi. Alikuwa akijinyima sana chakula, na mara kwa mara akiwaambia Waarabu wasile sana, na hasa, wasile sana nyama. (“Enyi Waarabu! Msiyafanye matumbo yenu kuwa makaburi ya wanyama.”)

Hapo Madina, Ali aliyafanya maisha yake kama ya kibarua. Wakati alipokuwa mtawala wa Waislamu, mtindo wake wa maisha haukubadilika. Bado aliishi kama kibarua. Aliwatawala Waislamu kwa “ushirikiano” wa kazi. Kwa namna fulani, serikali yake ilikuwa ndio “Serikali ya Leba” (ya wafanyakazi) ya kwanza katika historia, na pia ndio ya mwisho, kwani hakuwa mfanyakazi wa kukaa kwenye “kiti chenye mikono” bali kwa hakika alifanya kazi kwenye mashamba na mabustani kwa ajili ya ufanisi.

Ali mara kwa mara alitoa heshima kubwa kwenye mazungumzo yake na kibarua, mfanyakazi na fundi stadi. Walikuwa ni “marafiki wa Allah,” na je, mtu angefanya vizuri zaidi kuliko kuwalea hao – marafiki wa Allah? Yeye aliwalea, na alivutiwa nao kisilika.

Kinyume chake, na inaweza kuonekana ni ajabu, yeye hakuweza kamwe, katika wakati wowote wa maisha yake, kufanya urafiki na matajiri. Kutokea mwanzo, ulikuwepo mfarakano usiofumbulika kati yake na wao. Alikuwa mbali sana na “makabaila” na “wakwasi,” na “mabepari” wa siku zile kama pembe moja ya dunia ilivyo kutoka kwenye nyingine. Ali alikuwa akijihisi vibaya sana juu yao.

Ali alitoa heshima kwa kazi za mikono kwa mfano wake yeye mwenyewe. Alitengeneza nguo zake binafsi na viatu vyake yeye mwenyewe, alikamua mbuzi wake mwenyewe, alichota maji kutoka kwenye visima, na kutwisha na kuwatua mizigo ngamia wa misafara. Wakati alipokuwa Madina, alipata riziki yake kama mtunza bustani wa mkulima wa kiyahudi. Aliyanywesha mashamba yake. Alikifanya kibarua kuwa na heshima, na vibarua kujivunia kuitwa hivyo. Falme yake ilikuwa ni nchi ya ukarimu wa kijamii na “pepo ya vibarua” ya uhakika kiasi ambacho dunia haijawahi kuona kabla au baada.

Ingawa ile miaka minne ya utawala wa Ali ilitingishwa na maasi na vita vya wenyewe kwa wenyewe, hapakuwa na hata mtu mmoja katika milki zake aliyepatwa na njaa kwamwe. Sio kwamba hapakuwa na njaa tu bali pia hapakuwa na kupanda kwa gharama za maisha. Kila mmoja alikuwa na chakula kingi na matumizi ya kumtosha.

Huko Kufa, mayatima, wajane, vikongwe, na wagonjwa wote hawakuwa na wasiwasi juu ya chakula na makazi; Ali aliwaondolea matatizo yao yote. Katika majimbo, magavana wake walikuwa wawalishe masikini na wenye njaa kabla hawajaweza kujilisha wao wenyewe.

Kwa mayatima, Ali alionyesha mapenzi na upendo mwingi sana mpaka ikasemekana kwamba alikuwa anawadekeza. Alizikusanya lawalawa zote, asali na mapochopocho mengine aliyoweza kupata, na akawalisha kwayo hawa. Ali alikuwa mmoja wa wahisani, wanahuruma wakubwa walioishi kamwe. Hapo Kufa, alikuwa ametoa makazi kwa mkoma mmoja katika sehemu nje ya mji. Alimtembelea kila siku, akamuosha na kumfunga vidon- da vyake, akamlisha kwa mikono yake mwenyewe kwa vile alikuwa hana mikono, akam- laza kitandani, na kisha akarudi mjini.

Ali hakuwa mpiganaji-mwema tu wa Uislamu, na mjumbe wake wa amani; alikuwa pia ndiye mlezi wa kwanza wa elimu katika umma wa Waislamu. Mahmoud Said al-Tantawi wa Misri anaandika katika kitabu chake cha Masahaba Kumi wa Muhammad, kilichochapishwa Cairo katika mwaka 1976:

“Ali alisimama katika kilele cha utukufu katika matawi yote ya elimu. Alikuwa ndiye mtu mwenye elimu zaidi kabisa katika sheria za Kiislamu. Alikuwa ndiye bingwa mkubwa kabisa katika elimu ya Qur’an. Alikuwa na uelewa sahihi zaidi wa malengo, na ufahamu kamili zaidi wa maana ya Qur’an kuliko mtu mwingine yeyote. Alidumisha usafi wa Kiarabu kama lugha, na akaweka sheria zake za kisarufi (nahau). Alikuwa ndiye fasaha zaidi wa waongeaji wote, na alipozungumza aligusa kila moyo kwa kiasi ambacho hakuna kitu kingine katu kilichoweza kufanya hivyo. Watu waliosikia hotuba zake, mara nyingi walilia kama watoto wadogo.

Ustadi huu ungekuwa sio wa kawaida kabisa kama ungepatikana kwa mtu mwingine yeyote. Lakini sio wa ajabu kwa Ali kwa sababu alipaswa kuwa kama hivi. Hata hivyo, alikuwa ni Mtume wa Allah swt. mwenyewe aliyemkuza, na akamuelimisha yeye. Ali alikuwa wa kipekee kwa maana ya kwamba alikunywa sana elimu ya Mtume kwenye chanzo asili chenyewe. Hiki ni kitu ambacho hakuna mtu mwingine yeyote aliyekifanya isipokuwa yeye.” (Ten Companions of Muhammad, uk. 150, 157, na 162)

Wanazuoni wote katika taratibu za tassawuff (usufi wa Kiislamu) wanafuatilia misingi ya mafundisho yao kwenye falsafa ya Ali. Yeye ndiye mtawala mkuu anayetambulika katika nyanja ya usufi. Madhumuni ya falsafa yake ni mapenzi yenye nguvu juu ya Allah swt., na mapenzi juu ya viumbe Vyake vyote.

Waadhi za Ali, hotuba, barua, maagizo, semi za ucheshi na methali za busara kwa ufupisho makini kabisa zilikisanifu Nahjul-Balagha (Somo la Hekima Fasaha), kuunda chemchemi ya falsafa ya Kiislamu, na nyumba ya hazina ya elimu za Qur’an. Zinamuelimisha msomaji katika namna nyingi mbalimbali za masomo kama vile Upweke wa Allah, utambuzi na mapenzi juu ya Allah; uhai na kifo; mbingu na ardhi; uumbaji na maangamizo ya mwisho; uadilifu binafsi na wa jamii; hiari na majaaliwa; serikali na kazi zake; maadili, mantiki na falsafa ya Qur’an; ufafanuzi wa Qur’an; historia na mantiki yake; sheria na hukumu; uhu- siano wa mtu na Allah na jamii; uhusiano kati ya sheria tukufu na zile zinazotumika; jamii bora; hekima na busara; msingi wa maadili wa dola; asili ya sheria halisi na mamlaka; haki na wajibu; na ujumbe wa Muhammad kama Mtume wa Mwisho wa Allah kwa wanadamu, sunnah na Hadith zake.

Ali aliandika na kuzungumza kwa uzuri na ufahamu ulio kamilifu, na aliweka mkazo maalum juu ya usahihi. Ujumbe mwingi wa kiitikadi ulikoleza kabisa matini na tamathali za semi za Nahjul-Balagha. Tirmidhi na Tabrani, wakusanyaji wa Hadith, wamemnukuu Muhammad, Mtume wa Allah swt. kwamba alisema: “Mimi ni Jiji la Elimu, na Ali ni Lango lake.” Kama mfuasi wa kwanza wa Muhammad (s.a.w.w.), Ali alitoa michango adhimu sana kwenye nyanja ya fikra pamoja na michango adhimu sawa na hiyo kwenye uwanja wa vitendo.

Huduma za kijeshi za Ali kwa Uislamu zinaelekea kufunika mafanikio yake kitaaluma. Zinahodhi mazingatio ya mwanafunzi wa historia, na hivyo ile picha ya jumla inaelekea kutoka “nje ya mtazamo.” Kwa kweli, yeye alikuwa ndiye mwanzilishi wa udhibiti wa taaluma na mamlaka ya kielimu ya Waislamu. Hakuna khalifa kamwe ambaye alitoa mpango wa mfululizo nyaraka, maagizo, barua, waadhi na hotuba; na hakuna khalifa ambaye alijishughulisha mwenyewe kwenye uwanja mpana wa masuala, kama alivyofanya yeye. Maandishi yake, maagizo na hotuba juu ya ufafanuzi wa Qur’an ndio mategemeo ya kitaaluma ya Uislamu. Yeye alikuwa ni mfano kamili wa vipaji vingi.
Jurji Zaydan, mwanahistoria Mlebanoni-Mmisri, anaandika katika kitabu chake Collected Works, juz. I, uk. 550 kwamba wakati Amr bin Al-Aas alipovamia Misri, gavana wa Misri alitumia barua ile barua ambayo Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah swt aliyokuwa amemuandikia yeye gavana, miaka michache ya nyuma, akimualika kwenye Uislamu. Amr aliipokea barua hiyo, na ilikuwa na muhuri wa Mtume (s.a.w.w.).

Mwanahistoria huyu anaendelea kusema: “Yeye Amr aliutambua ule muhuri wa Mtume. Kisha akauangalia ule mwandiko, na ulikuwa ni mwandiko wa Imam Ali ibn Abi Talib. Ali alikuwa ndiye mtu wa kwanza ambaye alianzisha sanaa ya uandishi katika (uenezaji wa) Uislamu. Alikuwa ndiye mwandishi wa Mtume. Walikuwepo waandishi wengine pia, na Amr bin Al-Aas alikuwa mmoja wao. Pale aliporidhika kwamba ilikuwa ni barua ya Mtume, yeye aliibusu., akaiweka juu ya kichwa chake, na kisha akaisoma kama ifuatavyo ..”

Ali alikuwa, kwa hiyo, ndiye mwasisi ambaye “alihamasisha” sanaa ya maandishi katika huduma ya Uislamu. Abbas Mahmud Al-Akkad wa Misri, anasema katika kitabu chake, Abqariyyat Al-Imam Ali (Cairo, 1970): “Ilibakia juu yake Ali kutoa mwongozo katika mafundisho ya Tawhiid (Upweke wa Allah swt.), katika haki za Kiislamu, katika sheria, katika fasihi ya Kiarabu (nahau), na katika ustadi wa uandishi wa Kiarabu. Tutakuwa sahihi kama tukiita kazi yake kuwa ndio msingi wa elimu za Kiislamu za zama zote. Au, vizuri zaidi, kama tukimwita yeye Ensaiklopidia ya Elimu yote ya Kiislamu katika karne ya kwanza ya Uislamu.”

Wakati wa ukhalifa wake mwenyewe, Ali alilazimika kushughulika na mlolongo wa maasi, lakini kila alipopata vipindi vya nadra vya amani, alitumia fursa bora kabisa ya hivyo kuelewesha maadili ya Kiislamu kwenye umma wa Muhammad Mustafa.

Makundi ya wanaotafuta elimu walikusanyika huko Kufa kusikiliza mawaidha ya Ali. Baada ya kila waadhi, alikaribisha maswali kutoka kwao. Mara kwa mara alikuwa akiwaambia: “Enyi Waislamu! Niulizeni swali lolote kuhusu jambo lolote mtakalokuwa nalo vichwani mwenu, na fanyeni hivyo sasa hivi. Kumbukeni kwamba sitakuwa nanyi milele.”

Ali alihimiza uhuru wa maswali na mijadala ya wazi juu ya masuala yote ya kidini, kima- fundisho, kisheria, kisiasa, kisaikologia na kisAyansi, na aliwahimiza Waislamu kuufanya Msikiti kuwa “baraza” kwa ajili ya kutoa mawazo yao kwa uhuru.

Ali alikuwa na imani nzito juu ya heshima na thamani ya mtu binafsi, na haki yake ya uhuru wa kuamua katika ushawishi wake wa kidini, na katika desturi zake za kisiasa, kiuchumi na kijamii. Alikuwa na imani katika uwezo na kipaji cha mtu kutimiza majaaliwa yake kama mwakilishi wa Allah swt. katika dunia hii.

Akiwahutubia watu katika moja ya tenzi zake maalum, alisema: “Mnafikiria kwamba ninyi ni mwili mdogo (binadamu); bado ile dunia kubwa (ulimwengu) imefichwa ndani yenu.”

Ali alikaribia kuwa “mtu wa enzi.” Yeye alikuwa ni walii, mwanazuoni, mfanyakazi, mshairi, mpiganaji, mshindi, hakimu, mwanafalsafa, mhisani, faqihi, msemaji fasaha, mtawala na mwanasiasa mweledi lakini juu ya mambo yote, alikuwa ndio wazo kuu la uzuri na ubora, la wale wanaume na wanawake wanaompenda Allah swt. Kitovu cha tabia yake kilikuwa ni mapenzi juu ya Allah swt. Alikuwa “amepumbazwa” na mapenzi juu ya Allah swt. Waadhi zake na hotuba zimejaa msisimko wa mapenzi haya. Ndani ya mojawapo, yeye alisema:

“Furaha yangu kubwa inanijia wakati ninapokuwa na subira juu ya Muumba wangu. Furaha hii ni kubwa sana kiasi kwamba siwezi kufikiria malipo mengine yoyote ambayo yanaweza kupita haya. Hayo ndio malipo yake yenyewe makubwa.”

Katika hotuba nyingine yeye alisema: “Mimi simuabudu Allah swt. kwa kuchochewa na shauku yangu ya kuingia Peponi kwa sababu hiyo ni ibada ya yule mtu anayefanya kazi kwa ajili ya mshahara wake.

Mimi simuabudu Allah swt. kwa kuchochewa na hofu yangu ya kutupwa ndani ya jahannam kwa sababu hiyo ni ibada ya mtumwa. Mimi ninamuabudu Allah kwa sababu ya mapenzi yangu juu Yake, na kwa utambuzi kwamba Yeye peke yake ndiye mwenye kustahiki ibada na utii ninaompa Yeye.”

Katika barua ambayo Ali alimwandikia rafiki yake, alisema: “Kama yale mapazia yote yanayomficha Allah ili tusimuone yangenyanyuliwa kutoka machoni mwetu, na kama ingekuwa nijikute mimi mwenyewe mbele Yake bila ya lolote kati ya mapazia hayo, imani yangu juu ya kuwepo Kwake ingebakia vilevile hasa, kama ilivyo sasa hivi.”

Ali alikuwa akifahamu kwa ukunjuvu zaidi juu ya wema na neema za Alllah zisizokuwa na kikomo. Moja ya dua zake alizokuwa akizipendelea sana ilikuwa: “Ninaomba hifadhi ya nguvu za Mwenyezi Mungu, na ninaomba mazingira ya neema na baraka Zake zisizo na mpaka, na ninakualikeni kuomba pamoja nami ili kwamba Yeye atupe sisi hiari na uwezo wa kusalimisha matakwa yetu kwenye matakwa Yake, na atuwezeshe sisi kutenda vyema kwa heshima mbele Yake, na mbele ya viumbe Vyake vyote.”

Chanzo cha vifungu vilivyonukuliwa hapo juu, sio akili au ubunifu wa Ali bali ni mapen- zi yake makunjufu kwa Allah swt!