read

Ali Na Mifano Bora Ya Uhuru Na Fursa

Ikiwa kama katika umma wa Muhammad, Mtume wa Uislamu, Ali alikuwa ndiye mjumbe mkuu wa amani, alikwa, bila shaka, pia ndiye mlinzi mkuu ndani yake wa uhuru na fursa za mtu binafsi.

Katika uchaguzi wa kiongozi wa Waislamu, Ali alifunikwa mara tatu lakini kwa kinyume kikubwa sana, ilikuwa ni kwake ambako waliiona fursa, kwa mara ya kwanza na ya mwisho katika historia yao, ya kuchagua kwa uhuru kiongozi wao wenyewe, na wakamchagua. Katika kumchagua Ali, walikuwa bila kujua wakimchagua mdhamini wa uhuru wao wenyewe.

Kama ilivyoelezwa kabla, pale Muhajirin na Ansari hapo Madina waliposisitiza kwamba Ali achukue mamlaka ya serikali, na alikubali kufanya hivyo, alitangaza kwamba hakuna mtu hata mmoja aliyekuwa chini ya pingamizi lolote au chini ya shinikizo lolote la kuchukua kiapo cha utii kwake. Kwa hiyo, wale watu wote waliochukua kiapo cha utii kwake, walifanya hivyo kwa hiari.

Lakini walikuwepo watu wengi hapo Madina ambao sio tu walizuia kiapo chao cha utii kwa Ali bali pia walianza kuondoka Madina. Ali hakufanya jaribio la kuwazuia. Alipofahamishwa kuhusu kuondoka kwao, yeye alisema; katika utawala wake, kila mtu alikuwa huru kuishi Madina au kuondoka, na kwamba yeye hatamlazimisha mtu yeyote kuishi au kuondoka. Maadui zake walitaka kuondoka Madina naye akawaruhusu kuondo- ka, na hakuwauliza maswali yoyote.

Wengi wa masahaba wa Mtume waliokuwepo Madina, walikuwa wametoa kiapo cha utii kwa Ali. Miongoni mwao alikuwa ni Talha na Zubeir. Walikuwa wametegemea kwamba Ali angewafanya kuwa magavana wa Kufa na Basra.

Lakini Ali aliteua watu wengine kwa ajili ya nafasi hizo mbili na kwa sababu hiyo wao wakaondoka Madina na makusudio ya kuvunja kiapo chao cha utii. Ali aliwaachia waende zao.

Sera hii ya “kutoingilia mambo” inapingana vikali na sera ya Umar ibn al-Khattab, khalifa wa pili, ambaye aliwazuia wale masahaba wakuu wa Mtume, hususan Muhajirin, kuandamana na majeshi yake kwenda Uajemi au Syria au Misri, na kwa huzuni yao kubwa, aliwaamuru wao kubakia Madina.

Alifanya hivyo kwa kudhania, kwa sababu ya hofu yake kwamba watatumia umaarufu na hadhi zao walizokuwa nazo kama masahaba wa Mtume, kama wangeruhusiwa kuingia kwenye yale majimbo mapya yaliyotekwa. Masahaba hao, mpaka hapo, walikuwa hawajafanya kitu chochote kutumia umaarufu wao. Lakini Umar alikisia kwamba wangefanya, na kwa misingi ya kukisia huku, akawazuia uhuru wao wa kutembea.

Ali hakumzuia Talha na Zubeir hapo Madina kwa misingi ya kukisia kwake kwamba walikuwa na uhaini mioyoni mwao dhidi ya dola hiyo, ambao wote walikuwa nao.

Miezi michache baadaye, Aisha, Talha na Zubeir, walisimama katika maasi dhidi ya Ali, na wakaenda Basra. Lakini Ali bado hakutumia mbinu yoyote ya “kutumia nguvu” kuwafanya wakubaliane. Ilimbidi akabiliane na changamoto yao lakini alipendelea kufanya hivyo bila ya kutumia madaraka yake ya dola.
Kwanza kabisa, Ali alikuwa hakumwandikisha jeshini mtu yoyote. Yeye alikwenda kwenye Msikiti Mkubwa wa Madina, na akawaeleza Waislamu juu ya uasi wa Aisha, Talha na Zubeir.

Aliwasihi wamuunge mkono katika kudumisha amani katika Dar-ul-Islam, na katika kulinda umoja wa dola. Aliwakumbusha pia kwamba wao walimpa kiapo chao cha kumtii yeye katika amani na katika vita. Lakini hapakuwa na majibu. Alirudia kuwasihi kwake katika siku ya pili na tatu na ya nne.

Baada ya siku nyingi, ni watu mia saba tu walioitikia maombi ya Ali, na ilikuwa ni pamoja na jeshi hili dogo ambapo aliondoka Madina. Hakuna wakati ambapo alijaribu kumlazimisha mtu yeyote kwenye jeshi lake. Watu wote wale waliopigana upande wake, walikuwa wa kujitolea.

Pili, Ali alitoa msamaha kwa raia wa Basra ingawa walistahili adhabu kwa ajili ya uhaini. Yeye, kwa kweli, hakuwafanya angalau kuwa wafungwa pale waliposhindwa kwenye vita. Yeye kwa hiyo aliwaruhusu marafiki na maadui zake vile vile kufurahia neema za uhuru.

Kukataa kwa Ali kuwazuia pale Madina wale watu ambao hawakumpa kiapo chao cha utii, ruhusa yake kwa Talha na Zubeir kuondoka Madina, na msamaha wake kwa wale waasi wa Basra, ni ushahidi fasaha wa kukusudia kwake kutetea maadili bora ya uhuru na fursa.

Ali alithibitisha kwamba, katika Ufalme wa Mbinguni juu ya Ardhi, uhuru na fursa havikuwa ni maadili madogo na yasiyo na uhakika za kuthaminiwa na Waislamu bali vilikuwa haki yao, na kwamba hawakuwa waishi kama wafungwa kwa maana yoyote ya istilahi hiyo. Uhuru uliopunguzwa ni kinyume na heshima ya uraia wa Ufalme wa Mbinguni. Kila ambaye aliingizwa kwenye Ufalme wa Mbinguni, alikuwa amekombole- wa; alipata kuwa huru na alibakia kuwa huru.

Wakati Ali alipochukua mamlaka ya serikali, umma wa Waislamu ulikuwa katika hali isiyokuwa ya kawaida. Tabaka lake la watawala lilikuwa limefikia hali ya utajiri wa kupindukia na kiburi cha mwisho kabisa cha madaraka. Alitambua kwamba ile hali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ya dola ilihitaji uundwaji upya wa serikali na jamii. Lakini jaribio lake la kuunda upya serikali na jamii lilikasirikiwa na matajiri na wenye nguvu, na kukasirika kwao kulifumuka katika vita vya Basra na Siffin, kama ilivyoonyeshwa hapo kabla.

Kundi la tatu lililotangaza upinzani kwenye sera ya marekebisho ya Ali, lilitokana na Khariji. Wao walitaka kufanikisha malengo yao kwa kupitia mapinduzi ya vurugu na mageuzi ya nguvu. Waliliweka wazi kwamba hawatamruhusu Ali kurudisha ufanisi, umoja na nguvu kwenye serikali kwa njia ya amani na utaratibu.

Makhariji hao waliutukana uhuru amabao Ali aliutoa kwa Waislamu. Hawakushutumu tu sera zake bali pia waliitilia shaka imani yake yenyewe. Lakini yeye hakujaribu kuwazuia.

Alizivumilia shutuma zao zisizo na kiasi na zenye kuchoma sana alimuradi hazikuvuruga amani, na hazikuhatarisha usalama wa Waislamu wengine.

Ali aliacha kosa la maoni livumilike ikiwa akili iliachwa huru kupigana nalo. Lakini Makhariji waliitumia kila fursa ya uhuru wao, na wakaanza kueneza vurugu uvunjaji wa sheria na vitisho katika ardhi. Ilikuwa ni pale tu walipovuka vitisho vya kuwauwa raia wema, wenye kufuata sheria, na hasa wakawaua wengi wao, ambapo Ali akalazimika kwenda kinyume nao kuzuia uovu wao.

Mji wa Kufa, makao makuu ya Ali, ulikuwa wazi kwa Makhariji na maadui zake wengine. Walifaidi uhuru kiasi kile kile walichofaidi marafiki zake. Waliishi hapo Kufa, au waliin- gia na kutoka walivyotaka. Ali kamwe hakumuweka hata mmoja wao kwenye uchunguzi.

Raia wote wa Dola ya Kiislamu – wanaume, wanawake na watoto – walilipwa mishahara yao kutoka kwenye Hazina ya Umma. Makhariji walichukua mafungu yao kama raia wengine.

Ali na maafisa wake kamwe hawakufanya kamwe jaribio la kuwafanya wawe wachangamfu, watiifu na wenye kushawishika kirahisi kwa kupitia shinikizo la kiuchumi. Walibakia kuwa maadui wagumu wa dola na jamii walioahidi kuangamiza vyote, dola na jamii. Hatimae mmoja wao akaumuua yeye.

Hata baada ya yote haya, hata katika nyakati za giza kabisa, Ali hakuruhusu kamwe utajiri wa kinyume ufutilie mbali maadili ya uhutru na fursa kutoka kwenye moyo wa umma wa Muhammad. Uhuru na fursa vilibakia kwake yeye ni vya kulindwa kwa madhara yoyote, visivyoweza kuharibika, thabiti, kama imani yake binafsi katika ushindi mkubwa na usiopingika wa Haki na Ukweli.

Labda hakuna kitu ambacho ni rahisi sana kama kutukuza sana sifa za uhuru na fursa laki- ni Ali ndiye mtawala mweledi pekee katika ulimwengu mzima ambaye alitoa heshima zake kwavyo (uhuru na fursa), sio katika ufasaha wa kutamka, bali katika vitendo vya dhahiri. Hakuna mtawala katika historia ya ulimwengu aliyewahi kutoa uhuru zaidi kwa raia zake – marafiki na maadui halikadhalika – kuliko Ali! Uhuru aliotoa kwa raia zake kwanza ulimgharimu ushindi katika vita vya Siffin, na kiksha ukamgharimu maisha yake mwenyewe. Lakini inaonekana kwamba katika maoni yake, uhuru wao ulikuwa ni kitu cha thamani sana, na hakuonea wivu ile bei aliyolazimika kulipa ili kuuhifadhi.

Utawala wa Ali ulikuwa ni mfumo mpya wa kidini kwa jamii ya mwanadamu, na matu- maini mapya kwa wanadamu. Hakuna tena kamwe, katika historia, Waislamu na wasiokuwa Waislamu walipoweza kufaidi uhuru na fursa kama hiyo waliyofaidi wakati wa ukhalifa wa Ali ibn Abi Talib!

Ali Na Urithi Wake

Ali alikuwa na dharau juu ya utajiri na ufahari; yeye alikuwa na heshima juu ya mtu binafsi; na allikuwa na imani katika uwezo wa hali ya juu wa akili kama ikiachwa huru bila ya vikwazo vya kiasili na upendeleo. Yeye alikuwa ni adui wa upendeleo, na alipigana dhidi yake maisha yake yote.

Kama mlezi wa kweli wa Uislamu, Ali alikazia macho kwenye maslahi ya Uislamu tu. Kama ilibidi atoe mhanga maisha yake ili kulinda maslahi ya Uislamu, alifanya hivyo kwa furaha kabisa. Katika usiku wa Hijira ya bwana wake, Muhammad (s.a.w.w.), kutoka Makka kwenda Madina, yeye alilala kwenye hatari. Tokea siku ile, maisha yake yaliteng- wa kwa huduma kwa Muhammad na ulinzi wa Uislamu.

Katika kumchunguza Ali na amali zake, sehemu tatu kuu zinaonekana wazi. Ya kwanza ni tabia yake, ambayo takriban inakubalika kilimwengu kwamba ndio bora zaidi. Kwa nafsi yake na katika wadhifa wake alisimama nyuma ya mifano bora na kanuni ambazo zimewekwa wazi ndani ya Qur’an. Rekodi ya ukhalifa wake inaonyesha kwamba mifano yake bora na kanuni zake ni changamoto kwa kila kizazi cha Waislamu: usawa kwa watu wote, uhuru, usiokiukwa hata katika nyakati za vita na hali ya tahadhari ya “kitaifa”; maendeleo ya binadamu yenye amani, kupitia fursa binafsi na msaada wa taasisi za serikali. Yeye, kwa hiyo, aliwakilisha ushindi mkubwa kabisa wa tabia na itikadi.

Ya pili ni mafanikio ya Ali kama kiongozi wa kijeshi. Alikuwa ni jemadari mwenye kipaji ambaye utu wake ulimshangaza kila mmoja. Aliwaongoza Waislamu kwenye vita kwa umahiri mzuri sana, ujuzi, uvumilivu na utulivu. Yeye peke yake ndiye aliyefanikiwa, kati ya watawala wote, katika kuchanganya kanuni za maisha na falsafa ya Uislamu pamoja na mkakatiki na mbinu za kisiasa na vita.

Ya tatu ni kile kiasi ambacho athari za mwenendo na maadili ya Ali zimechangia katika ustawi na umaarufu wa Waislamu. Aliwafundisha kwamba njia za kufanikishia malengo zilikuwa ni tukufu sana kama malengo yenyewe, na kwamba njia hizo kama malengo yenyewe, zilikuwa zisiwe na mashaka yoyote. Yeye dhahiri kabisa alijishughulisha na mambo ya msingi kabisa.

Jamii ya Kiislamu iliyokamilifu ni ile ambamo watu na watawala wao wanatii sheria ya Allah swt. Madhumuni ya Ali kwa hiyo, yalikuwa ni kuusimika umma katika safu za wale watu ambao wanaitii sheria hiyo. Kwa kufanya hivyo, alipanua upeo wa maadili ya jamii ya Kiislamu, na akaimarisha misingi yake.

Ali aliwasilisha kwa umma wa Waislamu mlingano uleule wa tabia kama bwana na kiongozi wake, Muhammad, alivyokuwa amefanya kabla yake; na wote wawili walionyesha uwezo ule ule na moyo ule ule wa uvumilivu wa kuweza kukabilana kwa mafanikio na mitihani mikali sana na changamoto ambazo kwazo ushindi na maafa, kwa kulandana, viliwakabili wao. Moyo wa kutoa kafara kwa ajili ya wajibu na utaratibu, ni urithi wa manabii wote wa Allah swt. Moyo huo huo ndio “urithi” wa Ali ibn Abi Talib kwa umma wa Muhammad Mustafa. Rehma na amani ya Allah juu yao na familia zao.