read

Demokrasia Na Waislamu

Waislamu wa kisasa wanaamini na kudai kwamba serikali katika Uislamu ni ya kidemokrasia katika mwenendo. Serikali inayoendeshwa na Waislamu inaweza kuwa ya kidemokrasia katika mwenendo lakini serikali ya Kiislam sio ya kidemokrasia.

Hadi mwisho wa Vita vya Dunia vya Kwanza, Waislamu waliishi kila mahali chini ya utawala wa wafalme na masultani. Waliwaita wafalme na masultani wao Dhwillullah (kivuli cha Allah), na walifurahia sana kuishi kwenye kivuli hicho (kana kwamba Allah ana kivuli), ijapokuwa, ukiondoa wachache tu, wafalme na masultani hao walikuwa ndio madhalimu wakubwa, madikteta na wenye mabavu wabaya zaidi wa watawala. Walitumia madaraka kamili juu ya wananchi wao, na waliweza kumuua yoyote yule aliyewakasirisha.

Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, madaraka ya wafalme na masultani yalianza kufifia. Katika utambuzi unaobadilika wa karne ya ishirini, wafalme na masultani hao wakawa “wa kizamani,” na Waislamu wakafanya ugunduzi kwamba demokrasia ilikuwa ni ya Kiislam.

Wakaanza kuimba sifa za demokrasia, na wengi wao wakawa “wafuasi” wake. “Kubadilika” kwao kuingia kwenye demokrasia kuna maana kwamba katika zile karne kumi na nne za historia yake, Uislamu ulikuwa “sio wa kidemokrasia,” na ni muda tu baada ya 1919 tangu pale ulipokuwa “wa kidemokrasia.”

Wale Waislamu wanaodai kwamba demokrasia ni Uislamu, wanasema kwamba, baada ya kifo cha Mtume wa Allah (s.w.t.) maswahaba zake walianzisha ile al-Khilafat ar-Rashida (Ukhalifa ulioongoka), na ulikuwa ndio mfano bora wa serikali ya kidemokrasia.

Al-Khalifat ar-Rashida ilidumu kwa miaka thelathini tu. Baada ya ile miaka thelathini, ile demokrasia ya Kiislam ilibadiliwa na ufalme wa kidikteta. Ule mfumo wa serikali ulioitwa “demokrasia ya Kiislam” ulikomea hapo. Demokrasia ya Kiislam ikadhihirika kuwa ni bidhaa inayoharibika haraka sana. Ilidumu, takriban, chini ya miaka thelathini – wala sio hata kwa kizazi kizima!

Demokrasia ya Kiislam ilikufa bila kudaiwa (kimyakimya), bila kuombolezwa na bila kuimbwa. Ni nani aliyeiuwa? Je, ni wapagani? Ni waabudu masanamu? Wanafiki? Wachawi? Wayahudi? Au Wakristo? Hapana. Ni Waislamu wenyewe ndio walioiuwa. Na walikuwa ni Waislamu gani hao walioiuwa demokrasia ya Kiislam? Hawakuwa wale Waislamu wa karne za baadae.

Walitokana wote na kizazi (generation) cha wakati wa Muhammad Mustafa (s.a.w.) mwenyewe, na wote walikuwa ni “maswahaba” zake. Kama programu ya Uislamu inaingiza uanzishwaji wa demokrasia kama muundo mzuri wa serikali kwa ajili ya Waislamu, basi itakuwa hali gani kwa wale wahujumu walioiharibu katika utoto wake? Demokrasia ya Kiislam ilianzishwa na maswahaba wa Mtume (s.a.w.) lakini wale watu waliyoiharibu, walikuwa pia ni maswahaba zake.

Wakati kundi moja la maswahaba, likiongozwa na Abu Bakr na Umar, lilianzisha desturi ya demokrasia ya Kiislam (kama inavyodaiwa na Waislamu wa Sunni), kundi jingine la maswahaba, likiongozwa na Mu’awiyah ibn Abu Sufyan na Amr bin Al-Aas, liliivunja.

Kundi la tatu la maswahaba, likiongozwa na Abdullah ibn Umar bin al-Khattab na Abu Hurayra, lilishuhudia mapambano kati ya demokrasia ya Kiislam na wachimbia kaburi (walioiua) wake.

Walikuwa watazamaji wakimya wa mapambano ya kifo cha demokrasia ya Kiislam. Pale kulipokuwa hakuna shaka iliyobaki kwamba Mu’awiyah ndiye “mshindi,” wao, wakiwa wameyaona mambo kama yalivyokuwa na wayakinifu, walitangaza kwamba walikuwa pamoja naye – pamoja na Mu’awiyah – muangamizaji wa demokrasia ya Kiislam!

Faris Glubb:

“Serikali ya Kiislam ilikuwa imebomolewa kabisa katika sehemu kuu ya Ulimwengu wa Kiislam kwa kutwaliwa kwa madaraka na Mu’awiyah mwaka wa 40 Hijiria. Mu’awiyah alivunja Ufalme wa Allah ulioanzishwa na Mtume na akaubadilisha na ufalme wa kidunia. Alibadili ukhalifa wa haki na wa kidemokrasia kwa ufalme wa kidhalimu wa kurithiana……..

(Makala yenye kichwa cha habari “The islamic Ideal of Ethical Government,” iliyochapishwa kwenye Muslim News International, London, Machi 1963)

Abu Bakr, Umar, Mu’awiyah, Amr bin Al-Aas, Abdullah bin Umar bin al-Khattab, na Abu Hurayra, wote walikuwa maswahaba wa Mtume wa Uislamu. Abu Bakr na Umar walianzisha demokrasia ya Kiislam; na Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas wakaivunja. Je, ina maana kwamba wajenzi na wavunjaji – makundi yote – yako sawa, na demokrasia na ufalme wa kidikteta vyote ni vya “Kiislam?”

Tunaweza kisimamisha hukumu, kwa muda huu, juu ya demokrasia ya “Kiislam” lakini mafaqihi na wanazuoni wa Sunni wa wakati huu hawako tayari kuongeza kwamba heshima ufalme kama pia kuwa ni “Kiislam.” Kulingana na wao, hakuna kitu kama ufalme wa Kiislam.

Wanakubaliana kwa pamoja katika kuutangaza ufalme kuwa “sio Kiislam.”

G.H. Jansen:

“Hali halisi ya kisiasa ya dola ya Kiislam au taratibu kwa kawaida ni ya manufaa makubwa. Alipojishughulisha na kazi ya utendaji ya kuandaa katiba mpya kwa ajili ya Pakistani ambayo ‘itakuwa katika ulingano na mafundisho na historia ya Uislamu,’ (Rais) Ayub Khan aliwataka wataalam wake kuchunguza historia ya Kiislam na katiba za nchi nyingine za Kiislam.

Mambo mawili yalijitokeza wazi kutoka kwenye uchunguzi huu: Hapakuwa na nafasi ya ufalme katika Uislamu, na urithi hauwezi kuwa katika msingi wa kurithiana kiukoo. Umma wote kwa jumla lazima uwe na haki ya kuchagua kiongozi wao na haki ya kumuondoa. (Hii ina maana kwamba falme zote za Kiislam, na kujisingizia kwao kwa kidini, zilikuwa sio za Kiislam kabisa). Katika misingi hii miwili kwa kweli yapo makubaliano miongoni mwa waboreshaji wetu wa kisiasa, lakini katika kila hali nyingine ya sera ya Kiislam zipo tofauti za maana na za msisitizo. (Militant Islam, New York)

Ikhwaan al-Muslimiin (Udugu wa Kiislam) wa Misri, imezishutumu tawala zote za kijeshi (udikteta) vile vile kama sio za Kiislam.

G.H. Jansen:

“Hawa Ikhwaan al-Muslimin wametilia mkazo kwamba hakuna serikali iliyoanzishiwa kwa nguvu inayoweza kukubalika, kwa sababu mashauriano (shura’a) ni lazima kulingana na Sura ya 42 Aya ya 35 ya Qur’an. Kwa hiyo tawala za kijeshi zilizotokana na mapinduzi sio za Kiislam.” (Militant Islam, New York)

Ni makubaliano kwa hiyo, ya wanazuoni wa Sunni wa Pakistani na wasemaji wa Sunni wa Ikhwaan al-Muslimin wa Misri, kwamba ufalme na tawala za kijeshi zote sio za Kiislam.

Lakini ni makubaliano ya siku za baadaye. Mafaqihi na wanazuoni wa Sunni wa nyakati za zamani wasingeidhinisha wazo hili. Makubaliano yao yalikuwa tofauti kabisa na haya. Walitetea uwezo wa juu kabisa wa ukatili, kama ilivyoonyeshwa kabla.

Na hivi huu msemo “sio Kiislam” sio tasifida (neno la staha badala ya lenyewe) ya “upagani”? kama ndivyo, na ikiwa kwa mujibu wa mafaqihi wa Sunni wa Pakistani, ufalme ni taasisi ya kipagani, basi ni nini fatwa yao juu ya hao wafalme wenyewe. Wanaweza wafalme kuendesha serikali isiyo ya Kiislam, na bado wakawa ni Waislamu wa kweli? Na ni ipi fatwa yao juu ya yule mtu ambaye kwanza alijitwalia ile Khilafa ar-Rashida katika mapinduzi, na kisha akaibadilisha na kuwa ufalme, yaani, Mu’awiyah bin Abu Sufyan? Alikuwa akijigamba mara kwa mara kwamba yeye alikuwa ndiye wa kwanza wa wafalme wa Waarabu.

Maoni ya mafaqihi wa Sunni wa Pakistani na yale maoni ya Ikhwaan al-Muslimin kule Misri juu ya mwenendo wa ufalme na tawala za kijeshi, yanafanana na ya Muhammad Asad, mwanachuoni wa kisasa, wa Sunni wa Ulaya. Anaandika katika kitabu chake, State and Government in Islam (1980):

“………. Na tuwe wazi katika akili zetu juu ya jambo moja angalau: haijakuwepo kamwe dola ya kweli ya Kiislam baada ya wakati wa Mtume na ukhalifa wa Madina ulioongozwa na warithi wa mara tu wa Mtume, wale Khulafau Rashidiin wanne, Abu Bakr, Umar, Uthman na Ali.”

Kwa mujibu wa maamuzi hayo yaliyopita, Dola ya Kiislam ilikoma kuwa ya Kiislam mara tu Mu’awiyah alipoitwaa.

Lakini Mu’awiyah alifika mbali zaidi ya kuibadilisha ile Khilafa ar-Rashida kuwa isiyo ya Kiislam, yaani, ufalme wa kipagani. Aliupitisha ufalme kama “urithi” wake kwa umma wa Waislamu. Umma wa Waislamu kwa hiyo, umetawaliwa kwa karne zote hizi, na wafalme, na unatawaliwa na wao hata leo hii katika miaka ya 1990 – katika nchi kama Saudi Arabia, Jordan na Morocco.

Lakini, hata hivyo, Mu’awiyah huyu huyu, kwa Waislamu wa Sunni, bado ni “sahaba na mwandishi” wa Mtume (s.a.w.), na, ooh! ndio, “Mwenyezi Mungu amuwiye radhi” (kwa kubadili ukhalifa wa Kiislam kuwa ufalme wa kipagani).

Labda ni zoezi la kuvutia kuwaza kama wanazuoni wa Sunni wanaweza kuyaona makosa katika hoja zao wenyewe, na hitilafu za wazi katika makubaliano yao wenyewe. Kama wanaweza, basi itapendeza kuona jinsi watakavyozirazinisha (kuzitazama kimamtiki)

Waislamu wengi wanaangalia nyuma kwa shauku sana kwenye zama zile za miaka thelathini ya ile Khulafa ur-Rashidun (makhalifa walioongoka) kama “zama za ustawi” za Uislamu. Kwa kweli, hazikuwa za ustawi hivyo kama wanavyoziona wao, au, vizuri zaidi, zilikuwa za ustawi kwa wale Waislamu ambao walilimbikiza viwango vikubwa vya dha- habu juu yao katika ile miaka ya “ustawi”.

Walikuwapo wanne tu wa hawa makhalifa “waongofu”. Watatu kati yao walikutana na vifo vya kikatili, wawili katikati ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mmoja wao, yaani, Abu Bakr, ambaye hakuuawa, na ambaye alikufa kifo cha kawaida, alikuwa khalifa kwa miaka miwili tu.

G.H. Jansen:

“Hata hivyo chanzo kingine cha mfano wa kisheria ni zile sunna za Khalifa al- Rashidun, wale ‘makhalifa waongofu,’ wale watawala wanne waliomfuatia Muhammad.
Walikuwa ni Abu Bakr, Umar, Uthman na Ali, na vipindi vyao vinne vilidumu kuanzia 632 hadi 661 A.D. Huu muda mfupi wa miaka ishirini na tisa unazingatiwa, kupitia kwenye ukungu unaovunga kwa makusudi, wa wakati, kama ‘zama za ustawi’ wa Uislamu.

Kwa nini zifikiriwe hivyo kunajadilika, kwani ufupi wake ulikuwa kwa sababu ya hao makhalifa wanne, wawili waliuawa na mmoja alikatwa na maadui zake, nyumbani kwake, wakati alipokuwa anasoma Qur’an. Migawanyiko yote ambayo ilikera Uislamu na ulimwengu wa Kiarabu tangu hapo, ilizaliwa wakati wa zile zama za ‘ustawi’.

Zilikuwa kwa hakika ni zama za kupendeza, kipindi ambapo Waislamu Waarabu waliteka sehemu yote kubwa inayopanuka kuanzia Tripolitania upande wa Magharibi mpaka kwenye mipaka ya India upande wa Mashariki. Kwa hiyo, zile ‘sunnah’ za kile hawa watawala wanne adhimu lakini wenye mikosi walichokisema na kukifanya ziliongezwa kwenye mkusanyiko unaokua wa sheria za Kiislam.
(Militant Islam, New York)

Wanahistoria wawili wa kisasa wa Pakistani, Profesa Sayyed Abdul Qadir na Profesa Muhammad Shuja-ud-Diin, wamemnukuu Abul Kalam Azad katika kitabu chao, History of Islam (Lahore, Pakistan) katika mlango wenye kichwa “The Meaning of Khilafat” – Maana ya Ukhilafat – kama ifuatavyo:

“Inapaswa kuwepo serikali kwa ajili ya uongozi, ustawi na furaha ya mwanadamu ambayo itauokoa ulimwengu kutoka kwenye ukatili, udhalimu ukandamizwaji na unyonyaji; na ambayo itarudisha amani na usalama kwa wote ili iwezekane kutangaza Sheria ya Allah (s.w.t.) juu ya ardhi hii, kwa sababu hiyo kuigeuza iwe pepo.”

Ilikuwepo serikali kama hiyo – ile iliyoanzishwa na Muhammad, Mtume wa Allah (s.w.t.) (rehema na amani juu yake na kizazi chake), pale Madina – ambayo ilikuwa inaigeuza dunia hii kuwa pepo kwa kutangaza Sheria ya Allah (s.w.t.) juu yake. Lakini muda wa serikali hiyo ulikatishwa na kifo chake (s.a.w.).

Baada ya kifo chake, watu wapya walitwaa mamlaka ya serikali yake. Lakini malengo yao, sera na programu zao hazikuwa ni sawa na zake, na wao, kwa hiyo, walibadili mwenendo wa serikali yake.

Serikali ya Muhammad (s.a.w.) ilikuwa ndio Ufalme wa Mbinguni juu ya Ardhi, lakini baada ya kifo chake, iligeuka kuwa serikali ya “Ki-Aristotle”.