read

Hamza Aukubali Uislamu – A.D. 615

Muhammad, Mtume wa Allah (s.w.t.) ingawa yuko salama chini ya ulinzi wa ami yake, Abu Talib, hakusalimika na bughudha za washirikina. Wakati wowote walipopata mwanya wa kumuudhi, hawakuupoteza.
Wakati mmoja Abu Jahal alimkuta akiwa peke yake, na akatumia lugha ya kishenzi na ya kuchukiza sana juu yake Muhammad. Jioni hiyo hiyo wakati ami yake, Hamza ibn Abdul Muttalib alivyorudi nyumbani kutoka safari ya mawin- doni, mtumwa wake wa kike alimuelezea kile kisa cha fedhuli isiyo na sababu ya Abu Jahal kwa Muhammad na ustahimilifu wa Muhammad, ambao yeye alikuwa shahidi.

Hamza alikuwa mpiganaji, mwindaji na mwanamichezo, na alikuwa hana habari sana na mambo ya kila siku ya mjini hapo. Lakini tabia ya Abu Jahal kwa mpwa wake ilimpandisha sana hasira kiasi kwamba alichukua upinde wake, na akaingia kwenye mkutano wa Maquraish ambamo yeye Abu Jahal alikuwemo akiwachambulia wenzie matukio ya siku ile.

Hamza akampiga kichwani mwake na upinde wake, na kumsababishia atokwe na damu, na akasema: “Na mimi pia nimekuwa Mwislamu.”

Huu ulikuwa ni mtihani kwa Abu Jahal lakini aliona kwamba kimya kilikuwa ni sehemu bora ya ujasiri, na hakugombana na Hamza, pia akawazuia rafiki zake ambao walitaka kusimama kumtetea.

Betty Kelen:

“Ami yake Muhammad, Hamza, mtu wa umri wake mwenyewe, alisifika kuwa mwenye nguvu sana na uwezo kati ya Maquraish, shujaa wao katika vita na michezo. Alitumia muda wake mwingi kwa kuwinda vilimani. Siku moja alipokuwa anarudi kutoka kwenye msako na uta wake ukinin’ginia kwenye bega lake, mtumwa wake wa kike alimweleza jinsi Abu Jahal alivyomrundikia matusi mpwa wake.

Hamza alijikuta mwisho kabisa wa uvumilivu wote. Alimpenda Muhammad, ingawa alikuwa hamuelewi (japo kwa makosa, sio kweli). Alikimbilia Msikitini, ambako alimuona Abu Jahal akiwa amekaa miongoni mwa marafiki zake. Akanyanyua uta wake mzito na akampiga nao pigo kubwa sana kichwani mwake. “Utamtukana tena nitakapojiunga na dini yake?” alipiga kelele, akinyoosha misuli yake mikubwa mbele ya Maquraish. Hamza akawa Mwislamu, na hili lilitia nguvu kwenye imani hiyo. Baadhi ya Maquraish walikuwa waangalifu zaidi juu ya kumwita Muhammad mshairi.(Muhammad, the Messenger of God, 1975)

Hamza akawa mwislamu mchamungu na shujaa wa Uislamu. Alikuwa ndiye askari- mwenza wa mpwawe mwingine, Ali, na ilikuwa ni wao wote waliowauwa wengi wa viongozi wa Maquraish katika vita vya Badr, vilivyokuwa vipiganwe miaka michache baadae.

Katika vita vya Uhud, Hamza alimuua mshika-bendera wa pili wa wapagani, na pale waliposhambulia mstari wa Waislamu, alijItosa kati yao. Alikuwa akipasua njia yake kupitia kwenye safu zao pale alipopigwa na mkuki uliotupwa na Wahshi, mtumwa wa kihabeshi.

Wahshi alipangwa kwa ajili ya kazi hii hasa, na Hindu, mke wa Abu Sufyan na mama yake Muawiya; na muabudu sanamu mwingine wa Makka. Hamza alianguka chini na akafa mara moja.

Baada ya kusambaratika kwa Waislamu siku ile, Hindu na wanawake wengine makatili kutoka Makka, walikatakata viungo vya miili ya Waislamu waliouawa. Alipasua tumbo la Hamza, akalin’goa ini lake, na akalitafuna. Alimkata pia pua yake, masikio, mikono na miguu, akavitunga kama “mkufu,” na kuingia Makka ameuvaa kama tuzo la vita.

Muhammad Mustafa alisikitishwa sana na kifo na kukatwakatwa kwa mwili wa muumini hodari wa Uislamu kama Hamza. Alitoa majina ya “Simba wa Mungu”, na “Kiongozi wa Mashahidi” juu yake. Hamza aliukubali Uislamu katika mwaka wa tano wa kutangazwa Uislamu.

Kusilimu Kwa Umar – A.D. 616

Tukio maarufu la mwaka wa sita wa Tangazo la Uislamu lilikuwa ni kusilimu kwa Umar bin Khatab, khalifa wa baadae wa Waislamu. Alikuwa mmoja wa maadui wakali sana wa Uislamu na Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) na alikuwa mtesaji mkubwa wa Waislamu. Yule mwanahistoria wa kisasa wa Kimisri, Amin Dawidar, anasema kwamba chuki ya Umar kwa Uislamu, na uhasama wake kwa Muhammad, vilifanana tu na chuki na uhasama kwavyo wa ami (mjomba) wake wa upande wa kikeni, Abu Jahl.
Inasemekana kwamba siku moja kwa maudhi tu, Umar alikusudia kumuua Muhammad, na hivyo kuuzima mwale wenyewe wa Uislamu. Aliondoka nyumbani kwake akiwa na nia hii.

Kama ilivyokwisha elezwa, Waislamu kwa wakati huu (siku za mwisho za mwaka wa sita) walikuwa bado wanajikusanya katika nyumba ya Arqam bin Abi Arqam kuswali Swala zao za jamaa. Walikuwa wanaanza kujikusanya wakati mmoja wao, akitazama nje ya dirisha, akamwona Umar akija kuelekea nyumbani hapo na upanga uliochomolewa.

Katika hali ya wasiwasi kiasi, aliwaambia wale watu wengine wa jamaa ile kile alichokiona. Labda, na wao pia walikuwa na wasiwasi. Lakini Hamza, ambaye pia alikuwemo ndani ya nyumba hiyo ya Arqam, aliwatuliza, na akasema kwamba kama Umar alikuwa anakuja na nia nzuri, basi ilikuwa ni sawa sawa; lakini kama sivyo, basi yeye Hamza atamchoma kwa upanga wake Umar mwenyewe. Lakini ilitokea kwamba Umar alikuja kwa nia ya kusilimu, na akafanya hivyo.

Hadithi inaelezwa kwamba Umar alikuwa anakwenda kuelekea Dar-ul-Arqam kwa nia ya kumuua Muhammad wakati mpita njia alipomsimamisha, na kumjulisha yeye kwamba dada yake mwenyewe na mumewe wamekuwa Waislamu, na akamshauri kuiweka nyumba yake mwenyewe sawa kabla ya kuanza mpango mwingine wowote mkubwa wa kubuniwa tu.

Muhammad Husein Haykal:

“Umar alikwenda pale (Dar-ul-Arqam) – kwenye nyumba ya Arqam, akiwa amekusudia kumuua Muhammad na hivyo kuwaondolea Maquraish mzigo, na kusimamisha upya heshima ya ile miungu ambayo Muhammad aliipinga. Akiwa njiani kuelekea Makka alikutana na Nu’aym ibn Abdullah. Baada ya kujua nia ya Umar, Nu’aym akasema, “Wallahi umejidanganya mwenyewe, ewe Umar! Unadhani Bani Abd Manaf watakuacha utembee ukiwa hai pindi utakapokuwa umemuua mtoto wao Muhammad? Kwa nini usirudi nyumbani kwako mwenyewe na angalau ukakuweka sawa?” (The Life of Muhammad)

Umar alikasirika kusikia kwamba dada yake na mumewe wamekuwa Waislamu. Mara moja akabadili njia kutoka ile ya kwenda kwenye nyumba ya Arqam na kuchukua ya kwenda nyumbani kwa dada yake kuchunguza madai yale. Kwa majibu ya maswali yake, dada yake alimpa jibu makinifu lakini la ukwepaji.

Ibn Ishaq:

“Umar alifika kwenye mlango (wa nyumba ya dada yake) wakati Khabbab (sahaba wa Mtume) alikuwa akisoma chini ya uongozi wake ile Sura ya Taha na pia “Jua litakapokunjwa” (81:1). Washirikina walikuwa wakikiita kisomo hiki “takataka”. Umar alipoingia, dada yake aliona kwamba alikusudia madhara na akaficha zile karatasi ambazo walikuwa wakisoma. Khabbab akatorokea ndani ya nyumba. Umar akauliza ni upuuzi gani aliokuwa akisikia, ambapo dada yake akamjibu kwamba yalikuwa ni mazungumzo tu kati yao…” (The Life of the Messenger of God)

Umar alihamaki kwa kile alichoamini kuwa ni uongo, na akampiga dada yake usoni. Pigo hilo lilisababisha mdomo wake kutokwa na damu. Alikuwa ampige tena lakini kule kuona damu kulimfanya asite. Ghafla alionekana kupunguza ukali, na kisha kwa sauti iliyobadiika akamuomba amuonyeshe kile alichokuwa akisoma. Alimhisi amebadilika lakini akasema: “Wewe ni muabudu masanamu mchafu, na siwezi kukuruhusu kugusa Neno la Allah (s.w.t.)”

Umar mara moja aliondoka zake, akaoga, akarudi nyumbani kwa dada yake, akasoma yale maandishi ya Qur’an, na kisha akaenda kwenye nyumba ya Arqam ambako alisilimu rasmi.

Sir William Muir anasema kwamba kusilimu kwa Umar kulitokea mwishoni mwa mwaka wa sita wa ujumbe wa Mtume. Anaongezea tanbihi ifuatayo chini ya kurasa: “Kusilimu kwa Umar kulitokea ndani ya Dhil-Hajj, mwezi wa mwisho wa mwaka. Waumini wanasemekana sasa kufikia kwa jumla watu 40 wanaume na wanawake; au kwa hesabu zingine, wanaume 45 na wanawake kumi na moja.
(The Life of Muhammad, 1877, uk. 95)

Umar alikuwa na miaka kama 35 wakati aliposilimu.

Muhammad Husein Haykal:

“Kwa wakati ule, (aliposilimu) Umar ibn al Khattab alikuwa mtu mzima wa miaka thelathini na tano kwa umri.” (The Life of Muhammad)

Waislamu wengi wanadai kwamba kwa kusilimu kwa Umar, Uislamu ulipata nguvu mpya, na Waislamu walikuwa sasa wametiwa moyo kuwapinga wapagani. Waliweza sasa, kulingana na madai haya, kutoka nje ya sehemu zao za kujifichia, na kuswali waziwazi kwenye maeneo ya Al-Kaaba, ama hasa, alikuwa ni Umar mwenyewe aliyewatoa kwenye sehemu zao za kujifichia, na hawakuwa sasa wakimuogopa Abu Jahl au mtu mwingine yeyote.

Muhammad Husein Haykal:

“Waislamu waliorudi kutoka Abyssinia walifanya hivyo kwa sababu mbili. Kwanza, Umar ibn al Khattab alisilimu mara tu baada ya Hajira yao.

Pamoja naye, alileta kwenye kambi ya Waislamu ukakamavu , dhamiri, na msimamo ule ule wa kikabila ambao alikuwa akipiga nao Waislamu kabla. Hakuficha kamwe kusilimu kwake wala kamwe hakuwakwepa wale wapinzani wa Kiquraishi. Badala yake, alitangaza kusilimu kwake hadharani na aliwapinga Maquraishi wazi wazi.

Hakuridhika na kujificha kwa Waislamu wenyewe, mienendo yao ya siri kutoka upande mmoja wa Makka hadi mwingine, na kusimamisha kwao Swala kwenye umbali wenye usalama kutokana na mashambulizi yoyote ya Maquraishi. Umar alianza kupigana na Maquraishi mara tu alipoingia kwenye imani ya Uislamu, daima akishinikiza njia yake karibu na Al-Kaaba, na akasimamisha Swala yake pale pamoja na Waislamu wowote walioamua kujiunga naye.” (The Life of Muhammad)

Lakini madai haya ya ajabu yanapata nguvu ndogo katika ushahidi. Na kama ushahidi huo una maana yoyote, unaelekea kupingana na madai yenyewe.

Madai mengine ni ya ubadhilifu sana. Kwa mfano, yule mwanahistoria wa Kimisri, Amin Dawidar, anasema ndani ya kitabu chake, Pictures From the Life of the Messenger of God kwamba kusilimu kwa Umar kulikuwa ni pigo la kifo kwa Maquraishi.

Kilichotokea hasa ni kwamba kusilimu kwa Umar kulioana na wimbi jipya na ambalo halijawahi kutokea, la hofu kuu lililotojikeza juu ya Waislamu. Ambapo kabla ya kusilimu kwake ni Waislamu wale tu walioathirika na mateso ambao hawakuwa na wakuwalinda, sasa hakuna mwislamu, sio hata Muhammad Mustafa mwenyewe, aliyekuwa salama kutokana na nia mbaya za washirikina.

Muhammad Husyn Haykal:

“Huko uhamishoni kwao (nchini Abyssinia) walisikia kwamba kwa kusilimu Umar Maquraishi wamesimamisha mateso yao juu Muhammad na wafuasi wake. Kwa mujibu wa Hadith moja baadhi yao walirudi Makka, kwa mujibu wa nyingine, walirudi wote. Walipofika Makka waligundua kwamba Maquraishi wamerudia mateso ya Waislamu kwa chuki zaidi na nguvu mpya. Kwa kushindwa kuhimili, baadhi yao walirudi Abyssinia wakati wengine waliingia Makka chini ya ulinzi wa kiza cha usiku na wakajificha kabisa.” (The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Lakini hii haikuwa ndio basi. Mengine mengi yalikuwa bado yatokee. Sasa Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) hakuweza walau kuishi Makka.

Kwa kweli, zaidi kidogo ya wiki ilikuwa imepita tangu kusilimu kwa Umar, wakati Muhammad na watu wote wa familia na ukoo wake, walikuwa waondoke Makka, na waende uhamishoni.

Kwa hiyo, ile dhana kwamba kusilimu kwa Umar kuliwafanya Waislamu kuacha tahadhari zao na mkao wa kiulinzi, na kutowaogopa makafiri, moja kwa moja hailingani na mambo.

S. Margoliouth:

“…hatuna kumbukumbu yoyote ya tukio lolote ambalo juu yake Umar alionyesha ujasiri mkubwa wa kuonekana, ingawa mifano mingi inapatikana juu ya ukatili wake na hamu ya kuua; katika vita vya Hunain alikimbia, na kwenye tukio jingine aliokole- wa maisha yake kwa utu wema wa adui.”
(Muhammad and the Rise of Islam, 1931)

Profesa Margoliouth amefanya marejeo kwenye lile tukio ambapo adui mwenye utu mwema alinusuru maisha ya Umar. Atakuwa lazima anarejea ile vita ya Handaki au kule kuzingirwa kwa Madina (627 A.D). Katika vita vile, Ali ibn Abi Talib alimuua yule jemadari wa Makka, Amr ibn Abd Wudd, ambapo maaskariwenza wake walikimbia kwa haraka kuvuka lile Handaki. Walipokuwa wakikimbia, Umar alijaribu kumpita mmoja wao. Shujaa huyu aliyekuwa akirudi nyuma, alikwisha wahi kusikia kwamba Ali kamwe alikuwa hamuandami adui anayekimbia.

Yeye, kwa hiyo, alitambua kwamba yoyote huyo anayemfukuzia basi, hawezi kuwa ni Ali. Kwa upekuzi tu, aliibia kutazama nyuma na akagundua kwamba alikuwa ni Umar aliyekuwa akimjia kwa vitisho. Alipomuona Umar, mara moja aligeuza hatamu za farasi wake kumkabili, na hili lilimfanya Umar asimame. Shujaa huyu aliyemjua Umar, akamwambia: “Kama mama yangu asingenifanya niapie kwamba kamwe sitamuua Quraishi, ungekuwa maiti sasa hivi. Mshukuru yeye (mama), na usisahau kwamba nimeyasalimisha maisha yako.”

Ifahamike kwamba Hamza alisilimu mwaka mmoja kabla Umar hajawa mwislamu, na ameadhimisha kusilimu kwake kwa kumshambulia Abu Jahl, ami (mjomba) wa kikeni wa Umar, kwa upinde wake. Mtu hawezi kumtegemea Umar kuigiza mfano wa Hamza kwa kumshambulia ami yake mwenyewe, lakini hakuna kumbukumbu yoyote kwamba alishambulia muabudu sanamu mwingine yoyote kwa kuonyesha fidhuli kwa Mtume wa Allah (s.a.w.).

Zaidi ya hayo, pale Hamza alipokubali Uislamu na akaitoa damu pua ya Abu Jahl, Umar mwenyewe alikuwa muabudu sanamu.

Ilikuwa ni wajibu wake, kwa jina la “mshikamano wa kikabila,” kushindana na Hamza, na kulinda heshima ya kaka wa mama yake. Hata hivyo, kwa mujibu wa madai mengi yaliyosambaa, alikuwa ndiye mtu shupavu sana, anayetisha sana, mwenye hasira kali, na mkaidi sana hapo Makka. Na ni nani isipokuwa Umar angeweza kuthubutu kumtia changamoto Hamza? Lakini changamoto hiyo haikutokea kamwe.