read

Hijra Mbili Za Waislamu Kwenda Abyssinia (A.D.D 615-616)

Muhammad Mustafa (rehma na amani juu yake na Ahlul-Bait wake), alishirikiana katika huzuni zote na madhara ya wafuasi wake walioteswa kwa kuamini kwamba “Mungu ni Mmoja”, lakini hakuwa na njia ya kuwalinda. Pale vurugu za washirikina dhidi ya Waislamu zilipokuwa hazionyeshi dalili yoyote ya kutoshadidi, aliwashauri waondoke Makka na kutafuta hifadhi huko Abyssinia (Ethiopia) ambayo wakati huo ikitawaliwa na mfalme wa Kikristo, anayefahamika sana kuwa ni mtu muadilifu na mcha-Mungu.

Kwa kuitikia ushauri huu, kikundi cha Waislamu, chenye wanaume kumi na mmoja na wanawake wanne, kiliondoka Makka na kwenda Abyssinia. Kikundi hicho kilimhusisha Uthman bin Affan, khalifa wa baadae wa Waislamu; mke wake, Ruqayya; na Zubayr bin al-Awwam, binamu yake Mtume. Mtukufu Mtume (s.a.w.) alimteua Uthman bin Mazun, mmoja wa maswahaba wake wakuu, kama kiongozi wa kikundi hiki.

Ibn Ishaq:

“Wakati Mtume (s.a.w.) alipoyaona madhara ya maswahaba wake na kwamba ingawa ameweza kuyaepuka kutokana na kusimama na Allah (s.w.t.) na ami yake, Abu Talib, hakuweza kuwalinda, aliwaambia: ‘Kama mngekwenda Abyssinia (ingekuwa bora kwenu), kwani huyo mfalme (huko) hatavumilia dhulma na ni nchi ya kirafiki, mpaka wakati huo ambapo Allah (s.w.t.) atakapowatoeni kwenye dhiki yenu.’ Hapo maswahaba wake wakaenda Abyssinia, wakiogopa kuasi na kukimbilia kwa Allah (s.w.t.) pamoja na dini yao. Hii ilikuwa Hijra ya kwanza katika Uislamu. (The Life of the Messenger of God)

Hijra ya kwanza ilifanyika katika mwaka wa tano wa tangazo la Uislamu – 615. A.D.

Mfalme wa Abyssinia aliwakaribisha wakimbizi hao wa Kiislam kutoka Makka kwenye falme yake. Aliwapatia hifadhi, na walifurahia amani, usalama na uhuru wa kuabudu chini ya himaya yake. Kama mwaka mmoja baadae, Waislamu hao huko Abyssinia walisikia minong’ono kwamba Maquraishi huko Makka wameupokea Uislamu. Kama ilikuwa kweli basi hakukuwa na sababu ya wao kuishi uhamishoni. Walikuwa na hamu ya nyumbani, na waliamua kurudi Makka.

Lakini walipowasili Makka, waligundua kwamba sio tu kwamba ile minong’ono waliyoisikia ilikuwa ya uongo, bali pia kwamba Maquraishi wameongeza mateso ya Waislamu.

Wao, kwa hiyo, wakaondoka Makka kwa mara nyingine. Waislamu wengine wengi pia walifuatana nao. Kundi hili jipya lilikuwa na wanaume 83 na wanawake 18. Muhammad Mustafa akamteua binamu yake wa kwanza, Jafar ibn Abi Talib, kaka yake mkubwa Ali, kama kiongozi wa kikundi hiki.

Hajra hii ya pili ya Waislamu kwenda Abyssinia, ilitokea katika mwaka wa sita wa kutangazwa Uslamu, unawafikiana na mwaka wa 616. A.D.

Hijra hii ya Waislamu kwenda Abyssinia, na kupokewa kwao katika baraza la kirafiki la nchi ile, kuliwaogofya Maquraishi. Waliichukulia hofu ile kwamba Waislamu wanaweza kuongezeka nguvu, au kupata washirika wapya, na kisha, siku yoyote, wanaweza kurudi Makka kushindana nao. Ili kubadili mwelekeo wa tishio hili linalowezekana, kama walivyoliona, waliamua kutuma ujumbe kwenye baraza la mfalme wa Abyssinia kumshawishi kuwahamishia (kwa kuwakabidhi) Waislamu hao Makka.

Wakimbizi hao wa Kiislamu ambao walitarajia kuachwa katika amani, walishangazwa na kuwasili, katika mji mkuu wa Abyssinia, kwa ujumbe kutoka Makka, ukiongozwa na Amr bin Al-Aas. Amr alileta zawadi nono kwa ajili ya mfalme na watumishi wake ili kujipendekeza kwao.

Pale mfalme alipokutana na wajumbe wa Maquraishi, Amr alisema kwamba Waislamu wale walioko Abyssinia hawakuwa wakimbizi kutokana na mateso bali walikuwa watoro wa haki na sheria, na akamuomba kuwahamishia Makka. Mfalme, hata hivyo, akataka kusikia upande wa pili wa Hadith pia kabla ya kutoa uamuzi, na akamwita Jafar ibn Abi Talib kwenye baraza kujibu mashtaka yale dhidi ya Waislamu.

Jafar alitoa utetezi kabambe kabisa. Ufuatao ni mukhtasari wa hotuba yake ndani ya baraza la Abyssinia katika kujibu maswali yaliyotolewa na yule mfalme wa Kikristo.

“Ewe Mfalme! Tulikuwa tu watu wajinga na tuliishi kama wanyama wa porini. Wale wenye nguvu kati yetu waliishi kwa kuwinda wanyonge. Hatukutii sheria yoyote na hatukukubali mamlaka yoyote mbali na ile nguvu ya kinyama. Tuliabudu masanamu yaliyotengenezwa kwa mawe au magogo ya miti, na hatukujua chochote cha heshima ya utu. Na kisha Allah (s.w.t.) kwa Rehma Zake, akatutumia Mtume Wake ambaye alikuwa mwenyewe ni mmoja wetu. Tulijua juu ya ukweli wake na uaminifu wake. Tabia yake ilikuwa nzuri sana, na alikuwa wa ukoobora sana wa Waarabu.

Alituita sisi kwenye ibada ya Mungu Mmoja, na akatukataza kuabudu masanamu. Alitusihi tuseme kweli, na kuwatetea wanyonge, maskini, watu wa chini, wajane na mayatima. Alituamuru tuwaheshimu wanawake, na kutowakashifu kamwe. Tulimtii na kufuata mafundisho yake. Watu wengi katika nchi yetu ni washirikina bado, na walichukia kusilimu kwetu kwenye hiyo dini mpya ambayo inaitwa Uislam. Walianza kututesa sisi na ilikuwa ili kuepukana na mateso kutoka kwao kwamba tulitafuta na kupata hifadhi katika himaya yako.”
Wakati Jafar alipomaliza hotuba yake, mfalme alimuomba asome baadhi ya Aya zili- zoshushwa kwa Mtume wa Waislamu. Jafar akasoma Aya chache kutoka kwenye Surat Maryam, Sura ya 19 ya Qur’an Tukufu.

Mfalme aliposikia Aya hizi, alisema kwamba asili yake Aya hizo, ilikuwa ni sawasawa na ile ya Injili. Ndipo basi akatamka kwamba ameridhika na ukweli wake, na akaongeza, kwenye huzuni kubwa ya Amr bin Al-Aas, kwamba Waislamu wale wako huru kuishi kwenye himaya yake kwa kiasi cha muda wowote wautakao.

Lakini Amr bin Al-Aas alijishauri mwenyewe juu ya mkakati mpya, ambao, aliamini, ungeshambulia vile vigezo dhidi ya Jafar. Siku iliyofuata, kwa hiyo, alirudi kwenye baraza hilo na alimwambia mfalme kuwa yeye mfalme alipaswa kupuuza madai ya ulinzi wake kwa Waislamu hao kwa sababu waliikana jinsiasili tukufu ya Kristo, na wao wakadai kwamba alikuwa ni binadamu kama watu wengine.

Alipoulizwa na mfalme juu ya suala hili, Jafar alisema: “Ufahamu wetu juu ya Yesu ni kama ule wa Allah (s.w.t.) na Mtume Wake (s.a.w.), yaani, Yesu ni mja wa Allah (s.w.t.) Mtume Wake, Roho Wake, na Amri Yake iliyotolewa kwa Maryam, yule bikra maasuma.”

Mfalme akasema: “Yesu yu kama vile tu ulivyomuelezea alivyo, na si kingine zaidi ya hayo.” Kisha akizungumza na wale Waislamu, akasema: “Nendeni majumbani kwenu na mkaishi kwa amani. Sitawatoa kamwe kwa maadui zenu.” Alikataa kuwahamisha wale Waislamu, akarudisha zile zawadi ambazo Amr bin Al-Aas alizileta, na akaufukuza ule ujumbe wake.

Washington Irving

“Miongoni mwa wale waliokimbilia Abyssinia, alikuwemo Jafar, mtoto wa Abi Talib, ambaye ni nduguye Ali, hivyo ni binamu wa Muhammad. Alikuwa ni mtu wa ufasaha wenye mvuto na umbo la kupendeza mno. Alisimama na kujitokeza mbele ya mfalme wa Abyssinia, na akazifasili imani za Kiislamu kwa ghera na uwezo.

Mfalme ambaye alikuwa Mkristo wa Nestoria, aliziona imani hizi zenye kufanana sana kwa namna nyingi na zile za madhehebu yake na zenye kupingana sana na zile za ibada nzito ya masanamu ya Maquraishi, kwamba mbali sana na kuwakabidhi wale wakimbizi, aliwachukua zaidi mahsusi kwenye upendeleo na ulinzi, na kuzirudisha kwa Amr bin Al-Aas na Abdullah, zile zawadi walizozileta, na kuwatoa kutoka kwenye baraza lake. (Life of Mohammed)

Waislamu walikaa miaka mingi huko Abyssinia na waliishi kwa amani. Miaka kumi na tatu baadae katika mwaka wa 7 A.H. (A.D. 628) – walirejea, sio kwenda Makka bali Madina. Kuwasili kwao kulifuatana na kutekwa kwa Khaibar na Waislamu.

Jafar ibn Abi Talib alikuwa ndio kiongozi wa Waislamu wote waliokuwa wamehamia Abyssinia katika mwaka wa 615 na 616. Anaonekana kama ndio alikuwa mtu pekee wa ukoo wa Bani Hashim kuondoka kwenda Abyssinia pamoja na wale wakimbizi wengine.

Watu wengine wote wa Bani Hashim walibakia Makka.

Montegomery Watt:

“Mbali na watu wawili wa pekee Waislamu wote wa mwanzo waliobakia Makka (na hawakwenda Abyssinia) walitokana na kikundi cha koo tano, kikiongozwa na ukoo wa Muhammad wa Bani Hashim. Kikundi hiki kinaelekea kuwa ni namna ya Umoja wa Waadilifu ulioundwa upya. Kwa hiyo ndio kiini cha upinzani kwa wale wafanya biashara wakubwa pamoja na tabia yao ya ukirikimba.”
(Muhammad, Prophet and Statesman, 1961)