read

Hisia Za Familia Na Za Masahaba Wa Muhammad Mustafa (S.A.W.) Juu Ya Kifo Chake

WATU WA FAMILIA YA MUHAMMAD MUSTAFA (s.a.w.) walikuwa wamesongwa na wimbi kubwa la huzuni kwa kifo chake. Binti yake, Fatima Zahrah, alikuwa ndiye “Nuru ya macho yake.” Lakini sasa macho yale yalikuwa yamefumbwa daima; yasingeweza kumsalimia yeye na watoto wake tena. Wala asingeweza kusikia kutoka midomoni mwake ile sauti ya upendo na upole ikimkaribisha nyumbani; walinyamazishwa daima. Kwake yeye alikuwa ni baba, ni “mama,” Malaika mlezi, na Rehma ya Allah (s.w.t.) juu ya ardhi. Kwake yeye, alikuwa ndio kitovu cha uhai wenyewe.

Kwa Muhammad (s.a.w.), binti yake, Fatima, na familia yake, walikuwa ndio mfano halisi wa mapenzi yake yote, upendo wake, shangwe zake na furaha zake. Alimradi wakati alipokuwa hai, alimtendea kwa heshima kubwa mno, na alimuonyesha tofauti ambayo inastahili tu kwa Malkia. Lakini kwake yeye, alikuwa ni zaidi kabisa kuliko malkia.

Kati ya watu wote aliowajua yeye Mtume (s.a.w.) yeye (Fatima) alikuwa wa kwanza na wa mbele kabisa katika moyo wake.

Sasa Fatima alikuwa na haja moja tu – kukutana na baba yake huko mbinguni. Aliitambua haja hii mapema – majuma kumi tu baada ya kifo chake. Kifo chake (Fatima) kilimuacha mume wake na watoto wake kuvumilia sio moja bali huzuni mbili.

Hasan na Husein (a.s) walikuwa ni wajukuu wa Muhammad Mustafa (s.a.w.). Walikuwa ni vipenzi vyake. Walikaa mapajani mwake wakati alipokuwa yuko Msikitini au nyumbani, na walipanda mabegani mwake alipokuwa akitembea nje. Mapaja yake yalikuwa ndio “pepo” yao, na mabega yake yalikuwa ndio “vipando” vyao. Sasa ile “pepo” na “vipando” vilikuwa vimewapotea daima.

Macho yao, yakiwa na utando wa machozi, yalimsaka bila mafanikio, babu yao mpendwa kila mahali. Mimbari yake na baraza ya Msikiti wake vilikuwa sasa viko tupu, na kuta zake nzio zenyewe zilionekana kuwa katika maombolezo. Msikiti wake ulikuwa kama koa ambamo lulu yake imekwisha toka. Vilio vya maomboleza na malalamiko ya watoto hawa wadogo wawili vilirudi kutoka kwenye kuta za Msikiti wake katika mwangwi wenye majonzi.

Watoto wote wawili waliingiliwa na hisia ngeni, zisizoeleweka na za wasiwasi, na walishikwa na hofu zisizo yakini na zisizotajika. Walikuwa ni wadogo sana kuweza kupam- banua hisia hizi au kuelewa hofu hizi; lakini hata hivyo walihisi hiyo hisia mpya ya kukosa usalama ambayo iliwasumbua wao wote. Kwa mara ya kwanza katika miaka michache waliyoishi, waliwindwa na hali isiyo na usalama. Babu yao alikuwa, kwao wao, ni dalili na ishara ya usalama, na sasa alikuwa ameondoka.

Kwa Ali, kifo cha Muhammad (s.a.w.) kilikuwa ni msiba mkubwa katika maisha. Dunia yake ilikuwa imemzunguka Muhammad (s.a.w.) tangu alipozaliwa. Muhammad (s.a.w.w) alikuwa ndio kitovu na mzingo wa dunia yake. Kutoka kwenye dunia ile, Muhammad alikuwa ametoweka, na sasa Ali hakujua namna atakavyoishughulikia. Alijihisi kama ame- funguliwa kutoka kwenye minyororo yake, na maisha ghafla yalionekana kupoteza sababu yake ya kuwepo, kwa ajili yake yeye.

Ali alikuwa ndio roho ya Uislamu. Tabia yake ilikuwa adhimu sana na haiba yake ilikuwa haiwezi kulinganishikika. Lakini alikuwa ametegemea juu ya Muhammad (s.a.w.) awe kama kichocheo cha roho na haiba yake kukua. Alikuwa na kila sifa ya uwezekano ambao ulimfanya yeye kuwa wa muhimu sana kwa Uislamu lakini zimechukua ustadi wa ajabu wa Muhammad (s.a.w.) kuzifanya zijulikane.

Na sasa wakati akiwa na umri wa miaka 32, wakati akiwa kwenye ujana wa maisha yake, wakati akiwa kwenye ufanisi wa nguvu zake, na wakati akiwa angeweza kutoa zaidi kwa Uislamu na kwa dunia yote, zaidi kuliko alivyokwishatoa, Muhammad (s.a.w.) akafariki. Kifo cha Muhammad (s.a.w.) kilikuwa ni kipingamizi kwa Ali ambacho hakuweza kukomboka kutokana nacho kwa maisha yake yote yaliyobakia.

Hisia za Fatima Zahrah, Hasan, Husein na Ali (a.s), kwa kifo cha Muhammad (s.a.w.) zilikuwa za kawaida na za kutibika. Wote watano waliunda jamii ya familia, iliyounganishwa katika mapenzi yao, na utii wao kwa Allah (s.w.t.), Muhammad (s.a.w.) alikuwa ndio “mhimili” wa jamii hii ndogo.

Kwa kifo chake, “jamii” hii ilivunjika, ikiwaacha watu wengine wa familia hiyo wakiwa wamekanganyikiwa kabisa. Labda hawakujua kwa wakati ule, ingawa walikuwa waje kujua punde tu, kwamba kifo cha Muhammad (s.a.w.) kimeashiria tu mlolongo mzima wa mishtuko na huzuni mpya kwao.

Tokea hapo na kuendelea, walikuwa wawe kwenye hali ya “kuzingirwa” na huzuni. Kila siku mpya ilikuwa ilete mshituko mpya, na huzuni mpya. Lakini kwa kupitia msukosuko huu wa majanga na misiba, imani yao katika rehema za Allah (s.w.t.) na katika ushindi bora wa haki na ukweli, ulibakia imara kama jiwe, na ya kudumu. Matumaini yao ya kupata radhi za Allah (s.w.t.) yalizidi kuongezeka nguvu zaidi daima kwa kila wimbi jipya la mshituko na huzuni.

Ili kuhimili mshituko wa kifo cha Muhammad (s.a.w.), watu wa familia yake walitafuta na kupata msaada kutoka kwenye kile Chanzo Kimoja ambacho hakishindwi kamwe – Rehma za Allah (s.w.t.) zisizo na mipaka.