read

Ikolojia (Uhusiano Wa Viumbe Na Mazingira) Ya Arabia

Sehemu muhimu ya Ikolojia ya peninsula ya Arabia ni maji. Kuwepo au kutokuwepo kwake kumeiunda historia yake kwa kiwango kikubwa. Wakazi walivutiwa na eneo la Makka huko Hijazi kwa kuwepo kwa chemchemi iliyogunduliwa na Hajra, mke wa Nabii Ibrahim (a.s.) mama yake Ismail (a.s.) na aliiita kwa jina la “Zamzam”.

Kwa kuhakikishiwa kupatikana kwa maji yake mazuri kwa misimu yote, waliujenga mji wa Makka kuizunguka hiyo chemchemi. Eneo la maji la jimbo hili linahusisha visima, mabubujiko na mibubujiko ya kasi. Eneo lote halina mito na vijito mbali na ule Hajat wenye urefu wa maili sitini ulioko Jamhuri ya Yemen. Lakini hata hiki sio kijito cha kudumu; kinakuwa kijito tu wakati mvua nyingi zinaponyesha kwenye bonde lake.

Kipengele kipya na chenye sehemu nyingi zenye umuhimu mkubwa katika siasa ya uchu- mi ni kuwepo kwa hazina kubwa ya mafuta katika peninsula ya Arabia. Mnamo 1900 peninsula yote ilikuwa na watu wachache, na ilikuwa kame, iliyokumbwa na umasikini na iliyotengwa.

Ilikuwa ni moja ya majimbo machache ulimwenguni takriban iliyokuwa haijaguswa na athari za Magharibi. Ndipo yalipokuja mafuta na kila kitu kikabadilika. Saudi Arabia ili- uza shehena yake ya kwanza mwaka 1923, na kisima chake cha kwanza cha mafuta kilichimbwa mwaka 1938. Ndani ya miaka michache, mapato ya mwaka kutokana na mafuta yalivuka dola milioni moja. Falme hiyo ilivuka kiwango cha dola bilioni moja mwaka 1970; dola bilioni 100 mwaka 1980.

Maisha ndani ya Saudi Arabia na katika ghuba ya Uajemi yalibadilishwa na athari za utajiri mpya mali za kustaajabisha, maendeleo ya haraka ya kiuchumi, kuwasili kwa wafanyakazi wa kigeni, ushawishi wa kimataifa pengine kimsingi zaidi kuliko maisha yamebadilika penginepo popote kwa wakati wowote katika uzoefu wa mwanadamu.

Utajiri wa mafuta unabadilisha Sura ya nchi katika sehemu nyingi za Saudi Arabia na nchi za Ki-sheikh za ghuba. Umefanya iwezekane kupata tekinologia ya kisasa ya kuvuta maji kutoka kwenye vina vikuu au kubadili maji ya bahari kwa kuyaondoa chumvi, na kuifanya ardhi kame kuwa ya kilimo kwa kutumia umwagiliaji. Kuigeuza ardhi kuwa ya kilimo pia kunabadilisha hali ya takwimu ya idadi ya watu, vifo na maradhi (demografia) ya peninsula hii. Makabila ya kuhamahama yanapata mizizi katika makazi ya kudumu popote upatikanaji wa maji unapokuwa wa hakika. Mbinu za kisasa zaidi zinatumika katika kujaribu kudhibiti mwondoko wa mchanga na kuondoa hali mbaya ya mazingira.

Myama maarufu sana huko Arabia alikuwa ni ngamia. Ngamia wa kiarabu ni yule wa aina ya nundu moja, mbali na yule wa Asia ya kati mwenye nundu mbili (Bactrian). Huyu mwenye nundu moja (Dromedary) ana kwato bapa, pana zenye wayo nene yenye vidole ambazo hazizami kwenye mchanga, na anaweza kusafiri masafa marefu jangwani. Maziwa ya ngamia yalifanya sehemu muhimu ya mlo wa Waarabu wa jangwani, na manyoya yake waliyatumia kutengenezea mahema yao. Ngamia, kwa hiyo, alikuwa na umuhimu wa lazima kwa uhai katika jangwa.

Lakini cha kushangaza na kustaajabisha, ngamia takriban ametoweka kutoka Saudi Arabia na nchi zote za Ki-sheikh za Ghuba ya Uajemi. William J. Polk anaandika kwenye kitabu chake, “Passing Brave” kilichochapishwa na Alfred A. Knopf, New York, mwaka 1973, hivi:

“Punde kabla ya kifo chake mwaka 1960, yule mchunguzi mkuu wa Kiingereza juu ya majangwa, St. John Philby, alibashiri kuwa ndani ya miaka thelathini, Arabia itakuwa haina ngamia. Alichekwa wakati huo, lakini leo inaonyesha ubashiri wake ungekuwa mkubwa mno.
Ngamia na mtegemezi wake, yule mhamajihamaji, takriban wametoweka kutoka Arabia. Hivyo enzi hiyo iliyoanza karibu miaka 3,000 iliyopita pamoja na ufugaji wa ngamia, inaisha. Ngamia amefanya jukumu muhimu katika kuibuka kwa ustaarabu.”

Magari makubwa ya dizeli, magari moshi na ndege za Jeti vimechukua nafasi ya ngamia na misafara yake imekuwa “haifai” katika Arabia.