read

Jeshi La Usamah

Zayd bin Haritha alikuwa ni mtumwa aliyeachwa huru na rafiki wa Muhammad Mustafa. Aliuawa katika vita vya Muutah mnamo A.D.629 ambavyo aliongoza Waislamu dhidi ya Warumi. Waislamu walishindwa katika vita hivyo, na walikimbilia Hijazi.

Mtume (s.a.w.) wa Uislamu alitaka kufutilia mbali ile kumbukumbu ya kushindwa kule lakini alikuwa akisubiria muda unaofaa kwa kufanya hivyo. Tangu wakati ule Mtume, rehema na amani juu yake na Ahlul-Bait wake, alipohamia Yathrib (Madina) mnamo mwaka 622, alifanya kazi kwa bidii sana. Alikuwa amebeba mzigo wa majukumu ambayo hata shirika la mashirika ya watu lingeona kwamba ni mazito zaidi mno.

Tangu ile Hijja ya Muago mnamo Machi 632, alifanya kazi takriban bila kupumzika. Kazi ngumu mfululizo na ugumu maishani mwote vilichukua hesabu yake, na akaugua. Maradhi haya yalikuwa yawe ya kufisha. Ingawa alijisikia udhaifu hata kabla maradhi hayajaanza, hakuuruhusu udhaifu huo kuingilia kati kazi zake kama Mtume wa Allah (s.a.w.). na kama kiongozi mkuu wa Waislamu.

Ule “wakati unaofaa” uliosubiriwa kwa muda mrefu unaelekea kuwa umewadia mwishoni. Mtume (s.a.w.) aliandaa na kuanzisha jeshi jipya kufanya uvamizi wa mpaka wa Syria. Hadhi ya Uislamu ilikuwa imevunjwa katika vita vya Muutah, na wakati ulikuwa umefika wa kuirudisha upya. Kuongoza jeshi hilo, Mtume (s.a.w.) alimchagua Usamah, kijana wa miaka 18, mtoto wa Zayd bin Haritha, shahidi wa Muutah. Wote baba na mwana walikuwa vipenzi wakubwa wa Mtume. Lakini hakuwafanya kuwa majenerali kwa ajili ya upen- deleo; aliwafanya majenerali kwa sababu walifuzu kwa uwezo wao wa kusimamia watu wengine, na kuwaongoza kwenye vita.

Mnamo mwezi 18 Safar ya mwaka 11 A.H., Muhammad Mustafa aliweka bendera ya Uislamu mikononi mwa Usamah, akamweleza kwa kifupi malengo ya pambano hilo, na akampa maelekezo juu ya jinsi atakavyoliendesha. Kisha ndipo akawaamuru maswahaba wake wote, isipokuwa Ali na watu wengine wa Bani Hashim, kupiga ripoti kikazi kwa Usamah, na kuwajibika chini yake. Masahaba hawa walijumuisha watu wazima, watu matajiri sana, na watu wenye nguvu sana wa Maquraishi kama vile Abu Bakr, Umar, Abdur Rahman bin Auf, Abu Ubaida ibn al-Jarrah, Sa’ad bin Waqqas, Talha, Zubayr, Khalid bin Walid, na wengine wengi. Mtume (s.a.w.) alimuamuru Usamah kuondoka haraka mbele ya maswahaba hao na jeshi kuelekea kwenye kituo chake.

Sir William Muir

Katika siku ya Jumatano iliyofuata, Muhammad alishikwa na maumivu ya kichwa makali na homa; lakini yalipita. Asubuhi iliyofuata alijikuta amepona kabisa kuweza kufunga kwa mkono wake mwenyewe kwenye mlingoti wa bendera, ile bendera kwa ajili ya jeshi. Aliikabidhi kwa Usamah pamoja na maneno haya: ‘Pigana chini ya bendera hii kwa jina la Allah (s.w.t.) na kwa njia Yake. Hivyo utawashinda na kuwaua wale watu ambao hawamuamini Allah (s.w.t.)’ Kisha kambi ikawekwa hapo Jurf; na kundi lote la wapiganaji, bila ya kumuondoa hata Abu Bakr na Umar, waliitwa kujiunga nayo. (The Life of Muhammad, London, 1877)

Muhammad Husein Haykal

Waislamu hawakukaa kwa muda mrefu hapo Madina kufuatia kurudi kwao kutoka kwenye Hija ya Muago huko Makka. Mtume (s.a.w.) aliamuru mara moja ukusanyaji wa jeshi kubwa na akaliamrisha kwenda al-Sham. Alituma pamoja na jeshi hilo idadi ya wazee wa Kiislam, wale Muhajirina wa mwanzo, miongoni mwao ambamo Abu Bakr na Umar walikuwemo. Alitoa uongozi wa jeshi hilo kwa Usamah ibn Ziyad ibn Haritha, (The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Mtume (s.a.w.) alilitaka jeshi hilo kuondoka Madina mara moja. Lakini ni ajabu kwamba jeshi hilo halikuonyesha shauku ya kumuitika yeye.

Badala ya utii, Mtume (s.a.w.) alikutana na upinzani – kutoka kwa baadhi ya maswahaba wake! Tokea wakati huo na kuendelea, Mtume (s.a.w.) ilimbidi apambane na matatizo mawili; moja lilikuwa ni kuvuka katika maradhi yake na jingine ni kushinda ule upinzani wa jeshi lake. Zile siku chache za mwisho za maisha yake hapa duniani zilitawaliwa na pambano hili lenye nchambili.

Wale watu wakubwa wa Ki-Quraishi walichukia sana kule kunyanyuliwa kwa mvulana wa miaka 18 juu yao wote, na kwamba pia, mtoto, sio wa nasaba bora ya Quraishi, bali wa mtu aliyekuwa mtumwa kabla! Kwa hiyo, badala ya kuripoti kwake kikazi, wengi miongoni mwao wakaanza kutoroka na kuchelewesha muda kwa makusudi.

Wengine miongoni mwao walikuwa hawakuridhika kabisa na uchaguzi wa Usamah kama jenerali wao kiasi kwamba walionyesha waziwazi kutoridhika kwao.

R.V.C. Bodley

...Wakongwe hawakulipenda lile wazo la kuwashambulia wale Warumi ambao walikuwa bado wanaogofya na mvulana, ambaye alikuwa na uzoefu mdogo wa kivita, kama kiongozi wao. Muhammad alikuwa, hata hivyo, hashitushwi na malalamiko hayo. Alikuwa anaanzisha kigezo, kilichotazamwa tangu hapo miongoni mwa Waislamu, kwamba umri na hadhi katika jamii hakusababishi kufanya majenerali wazuri. Alikuwa akijenga ndani yao ujumbe wa demokrasia ambao walikuwa waupeleke duniani kote. Bila ya kujadili ule uteuzi alimuita Usamah Msikitini na kumk- abidhi bendera ya Uislamu pamoja na kumnasihi namna ya kuiletea heshima. (The Messenger, New York. 1946)

Kuteuliwa kwa Usamah kama jenerali hakukuwa, hata hivyo, ndio sababu pekee ya kwa nini baadhi ya maswahaba hawakupenda kwenda Syria.

Kulikuwa na baadhi ya sababu nyingine pia za kwa nini waliamini ilikuwa ni muhimu sana kwao kubakia Madina, bila kutilia maanani amri za Mtume wa Allah (s.a.w.) Usamah alimuuliza Mtume (s.a.w.) kama haingekuwa bora kuahirisha ule uvamizi wa Syria mpaka atakapopona homa yake. Lakini Mtume (s.a.w.) alisema: “La. Nakutaka wewe uondoke muda huu huu.”

Usamah alikwenda kwenye kambi yake huko Jurf lakini wachache wa maswahaba walikuja kuripoti kwa ajili ya kazi. Walijua kwamba ugonjwa wa Mtume (s.a.w.) umeleta “wasi-wasi” juu ya Umma (jamii), na waliona kwamba ni “hatari” kuondoka Madina kwa wakati kama huu ingawa waliona ni “salama” kudharau amri zake. Waliweka ile kanuni ya dhahabu ya “Usalama Kwanza” mbele ya amri za Mtume wa Allah (s.a.w.)

Mtume (s.a.w.) alikuwa na homa na maumivu makali ya kichwa lakini alimudu kwenda Msikitini, na kuhutubia ule mkusanyiko pale ambao ulijumuisha wengi wa waliochelewa nyuma, hivi:

“Enyi Waarabu! Mmekuwa wanyonge kwa sababu nimemteua Usamah kama jenerali wenu, na mnaleta maswali kama anazo sifa za kuwaongozeni ninyi kwenye vita. Ninajua ninyi ni watu wale wale mlioleta swali hili hili kuhusu baba yake. Wallahi, Usamah ana sifa za kuwa jenerali wenu kama vile baba yake alivyokuwa na sifa za kuwa jenerali. Sasa tiini amri zake na muende.”

Betty Kelen

Mara baada ya ile Hijja ya Muago, pamoja na nia yake kuongezeka kasi zaidi kuelekea kaskazini kana kwamba katika kumfikisha mwisho, Muhammad aliandaa jeshi jipya la kupigana ugenini kwenda Syria, akimuweka mtoto wa Zayd, Usamah, kuliongoza – dhidi ya ushauri wa baadhi ya majenerali wake, kwa vile Usamah alikuwa na miaka ishirini tu. Muhammad aliwaambia kwa ukali, ‘Mnamkemea yeye kama mlivyomkemea baba yake, lakini yeye anastahili zaidi uongozi kama baba yake alivyokuwa.’

Hakutaka tena kupoteza muda kutetea utendaji wake. Aliiweka bendera yake kwenye mikono ya Usamah na akamtuma kwenda kwenye uwanja wa kukusanyikia, lakini mabishano yale yaliendelea kumchoma moyo hata hivyo. (Muhammad, Messenger of God)

Wakati wowote Mtume (s.a.w.) alipopata nafuu kidogo kutokana na homa na kichwa chake, aliwauliza wale waliokuwepo kama jeshi la Usamah limeondoka kwenda Syria. Aliendelea kuwahimiza, ‘Pelekeni jeshi la Usamah mara moja.’

Wapiganaji wa kawaida wa jeshi hilo waliitika amri za Mtume, na wakapiga ripoti kikazi kwa mkuu wa kikosi huko Jurf lakini wengi wa maswahaba wakubwa hawakufanya hivyo. Wengine miongoni mwao walisita humo mjini; wengine, chini ya msukumo wa Mtume (s.a.w.) kwa muda wote, walikwenda Jurf lakini wakarudi. Walibaki wakisafiri kati ya kambi na mjini. Wengine wao walikuja mjini kuchukua vitu ambavyo vilikuwa vinakosekana kwenye zana, na wengine walitaka kusikia habari. Bado wengine walirudi “kujulia hali ya afya ya Mtume.” Walikuwepo pia wale maswahaba ambao hawakwenda Jurf kabisa. Walibakia pale mjini kwa sababu ya “mapenzi” yao kwa Mtume (s.a.w.) kwa vile walikuwa hawakuwa na ule “moyo” wa kumuacha yeye katika wakati ambapo anaumwa vibaya sana.

Lakini haya malalamiko ya “mapenzi” na “wasiwasi” kwa ajili ya ustawi wake hayakumpendeza Mtume (s.a.w.) mwenyewe. Kigezo cha kuthibitisha mapenzi yao kwake kilikuwa ni utii wao kwenye amri zake. Aliwaamuru kuondoka kwenda Syria lakini hawakwenda. Walimuasi yeye wakati wa siku zake za mwisho wa maisha yake.

Betty Kelen

Maradhi yake Mtume (s.a.w.) yalizidi, lakini alijaribu kuyatupilia mbali kwa ajili ya Usama, kwani vile habari za ugonjwa wa Muhammad zilivyoenea kote, huyu kijana alikuwa akipata muda mgumu kukusanya vikosi vyake. Watu wengine waliokuwa wamejiunga naye, walikuwa wakirejea Madina, na kwa uhakika hakuna waliokuwa wanabakia. (Muhammad, Messenger of God)

Mwishowe, lisilopingika likatokea. Muhammad, Mtume (s.a.w.) wa mwisho wa Allah (s.a.w.) katika dunia hii, akafa. Juhudi yake ya kuwatoa maswahaba zake nje ya Madina, zikafika mwisho, pamoja na muonekano wa “ushindi” kwa maswahaba. Hawakupiga ripoti kikazi kwa Usamah na jeshi halikwenda kwenye pambano – wakati wa maisha yake!

Kwa Waislamu, kila amri ya Muhammad ni amri ya Allah (s.w.t.) Mwenyewe kwa sababu yeye ndiye Mfasiri wa amri hizo, wa Mapenzi na Makusudio ya Allah (s.w.t.) Uasi kwa Muhammad ni uasi kwa Allah (s.w.t.) Mwenyewe. Kwa hiyo, wale watu waliomuasi yeye (Muhammad) walipata ghadhabu za Allah (s.w.t.)

Vita vya Muutah vilipiganwa mnamo mwaka 629 A.D., na kuishia kwenye kushindwa kwa Waislamu. Mtume (s.a.w.) alitaka kufuta lile doa la kushindwa. Lakini haikuwa mpaka miaka mitatu baadae – mnamo mwaka 632 A.D. – ambapo alimuamuru Usamah kuvamia mpaka wa Syria katika ufidiaji wa yale maafa ya Muutah.

Upangiliaji wa muda wa msafara wa Usamah unazua msongamano wa maswali. Kwa nini Mtume (s.a.w.) asitume msafara wake wa kuadhibu huko Syria katika muda wowote wakati ile miaka mitatu ya kati? Kwa nini alichagua muda kabla tu ya kifo chake mwenyewe kuutuma msafara huo? Kwa nini, ghafla tu, ilikuja kuwa muhimu sana juu yake kuwatuma maswahaba wake na wapiganaji nje ya Madina?

Kama ilivyoonyeshwa kabla, baada ya ile Hijja ya Muago, afya ya Mtume (s.a.w.) ilianza kuonyesha dalili za mfadhaiko. Miezi miwili baadae, hali yake ilizidi kuwa mbaya zaidi, na siku kadhaa baadae, akafa.
Pia, kama ilivyoonyeshwa kabla, Mtume (s.a.w.) aliwaambia Waislamu katika zaidi ya tukio moja kwamba hakuwa na muda mrefu zaidi wa kuishi katika dunia hii. Tabari, yule mwanahistoria, amemnukuu Abdullah ibn Abbas akisema: (kama miezi miwili baada ya ile Hija ya Muago) “Mtume wa Allah (s.w.t.) alituambia kwamba huenda angekufa ndani ya muda wa mwezi mmoja.” (Ta’rikh Tabari, juz.2, uk. 435).

Pia imesimuliwa kwamba usiku mmoja Mtume (s.a.w.) alikwenda kwenye uwanja wa makaburi ya Al-Baqi, akifuatana na mtu wa nyumbani. Baada ya kuwaombea wafu, alimwambia huyo mwenzie: “Wao (wale wafu) wako kwenye hali nzuri kuliko wale ambao wako hai. Hivi punde maovu mapya mengi sana yatatokea, na kila moja litakuwa lenye kuogofya na kutisha sana kuliko lile lililolitangulia.”

Kwa upande mmoja Mtume wa Allah (s.a.w.) alikuwa akitabiri kifo chake mwenyewe, na alikuwa pia akitabiri kutokea kwa maovu mapya na kuzuka kwa vurugu mpya; na kwa upande mwingine akiwashawishi Masahaba zake kuondoka Madina na kwenda Syria!

Kuzingatia kukaribia kwa kifo chake yeye mwenyewe, ni lipi la muhimu sana kwa Mtume (s.a.w.) kufanya: kutafuta kulipiza kisasi kwa ajili ya kifo cha rafiki yake ambaye aliuawa miaka mitatu iliyopita kwenye mpaka wa mbali au kulinda Nchi ya Madina na umma wa Kiislam kutokana na hatari ambazo, alisema, zilikuwa zijitokeze karibuni?

Jibu la wazi kwa swali hili ni kwamba kama kisasi cha kifo cha Zayd kingeweza kusubiri kwa miaka mitatu, kingeweza kusubiri zaidi kidogo, na kwamba usalama wa Nchi na ule wa umma, ulikuwa ni wa muhimu zaidi sana kuliko kitu chochote kingine. Kwa hiyo, Mtume (s.a.w.) alipashwa kulipanga jeshi hilo ndani ya, na kuizunguka Madina, badala ya kulituma nje ya nchi.

Lakini inaonekana kwamba Mtume (s.a.w.) mwenyewe hakuweza kukubaliana na tathmi- ni hiyo. Hakukiona chochote chenye umuhimu zaidi kuliko kutuma maswahaba zake kwenda Syria nje ya Arabia yenyewe. Alipogundua kwamba wanapuuza amri zake, akawalaani.

Shahristani, yule mwanahistoria, ameandika katika kitabu chake, Kitab al- Milal wan-Nihal (uk.8): “Mtume wa Allah (s.a.w.) alisema: ‘Jeshi la Usama lazima lion- doke mara moja. Allah (s.w.t.) awalaani wale watu ambao hawaendi pamoja naye.’”

Ilikuwa ni mara yake ya kwanza katika uhai wake ambapo Muhammad Mustafa, Mtume (s.a.w.) wa Rehma na aliye Rehma kwa ulimwengu wote, alipomlaani mtu yoyote. Kabla ya hili, alikuwa hajawahi kamwe kumlaani mtu yoyote – sio hata wale maadui zake wenye msimamo mkali kabisa kama Abu Jahl na Abu Sufyan. Hakuwalaani watu wa Taif pale walipompiga mawe na kumfukuza nje ya mji wao. Pia, huko nyuma, kama mtu yeyote alikuwa hawezi kwenda vitani, hakumlazimisha kwenda, na alimwacha abakie nyumbani. Lakini katika suala la jeshi la Usamah, hakutaka kusikia sababu zozote au visingizio kutoka kwa mtu yeyote kwa kushindwa kwake kwenda na jeshi hilo. Amri yake kwa maswa- haba zake ilikuwa ni isiyobadilika, isiyoyumba na yenye mkazo.

Katika dakika za mwisho za maisha yake, mtu hupenda kwamba ndugu zake wote na marafiki wawe karibu naye. Anapenda na kutegemea kwamba baada ya kifo chake, watashiriki katika mazishi yake; watamuombea, na watailiwaza familia yake. Lakini kinyume na kanuni zote za mwenendo huu katika wakati kama huu, Muhammad Mustafa alikuwa akifanya kila aliloliweza kuwaondoa maswahaba na marafiki zake kutoka Madina. Hakumtaka yeyote kati yao kubaki pamoja naye.

Waislamu wa Sunni wanadai kwamba Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Uislamu, hakuchagua mrithi wake mwenyewe, na aliliacha suala la kuchagua kiongozi wa Umma kwa maswahaba zake. Kama wako sahihi katika madai yao, basi ile amri ya Mtume (s.a.w.) kwa maswahaba kuondoka Madina na kwenda Syria, kunaleta tatizo lenye ugumu sana kwao.

Ni dhahiri kwamba Mtume (s.a.w.) alikuwa afariki. Yeye mwenyewe amesema hivyo mara kwa mara. Muda ulikuwa umewadia, kwa hiyo, kwa maswahaba zake kukusanya vichwa vyao pamoja na kutafuta sehemu mpya ya mamlaka. Lakini Mtume (s.a.w.) alikuwa ana- sisitiza kwamba waende mamia ya maili mbali na yeye – na kutoka Madina.

Kama aliwataka wao kuchagua au kuteua mrithi wake kupitia “ushauri wao wa makubaliano,” angeweza yeye kuwaamuru wao kuondoka Madina? Tena, yeye mwenyewe aliuonya umma kwamba ulikuwa unatishiwa na hatari mpya kubwa kubwa. Asingeweza kwa hiyo, kuwataka maswahaba zake kubakia Madina, na kuukinga umma kutokana na hatari hizo kubwa? Hata hivyo, ni nani angeukinga umma wa Muhammad kutokana na hatari hizo kama sio maswahaba zake wenyewe?

Kwa vile Mtume (s.a.w.) alijua kwamba atakufa, asingetayarisha kamwe na kuandaa jeshi la Usamah. Badala yake, angependekeza kwa maswahaba zake kwamba wanapashwa kutengeneza mkakati, kwa ushauri wa makubaliano, kuzuia yale maovu mapya na hatari ambazo tayari zimetishia kwenye upeo wa macho ya Madina.

Lakini Muhammad Mustafa hakufanya hivi. Yeye, kwa kweli, alifanya kinyume chake tu. Aliwaamuru maswahaba zake kutoka nje ya Madina, na kamwe hajawahi kuwa na mkato kwao hivyo kama alivyokuwa safari hii. Je, inaweza kuwa na maana kwamba walikuwa ni maswahaba wenyewe ambao aliwaona kama watunzi wa maovu na hatari mpya zinazo- tishia umma wake?

Kwa kweli, usalama na wokovu wa Waislamu ulilala kwenye utii wao usio na kuuliza kwenye amri za Mtume (s.a.w.) wao. Pale walipomuasi yeye, waliufungua mlango wa maovu yote, vurugu na hatari.

Katika mazingira yalimotokea matukio ya wakati huo, inaonekana kwamba Muhammad Mustafa alikuwa na sababu muhimu sana za kuchelewesha jeshi la Usamah mpaka dakika za mwisho. Alikwisha kutangaza wazi, kwa usahihi kabisa na kwa kurudia rudia kwamba Ali ibn Abi Talib atakujakuwa mrithi wake. Lakini alikuwa pia anatambua kuwepo kwa hisia za kichinichini za upinzani wa maswahaba zake kwa Ali.

Mtume (s.a.w.) pia alijua kwamba kile kikundi kilichokuwa kinampinga Ali, kilikuwa na nguvu sana na chenye hadhari sana.

Kwa hiyo, aliwaza kwamba kama wakati wa kifo chake, watu wa kikundi hiki kinachozungumziwa, watakuwa nje ya Madina, yeye (Ali) atamrithi bila ya kadhia yoyote. Lengo hasa la Mtume, katika kuandaa jeshi la Usamah, kwa hiyo, lilikuwa ni kuwatuma wale watu mbali kutoka Madina, ambao wangempa Ali changamoto katika kupanda kwake kwenye kiti cha ukhalifa. Alitegemea kwamba katika kutokuwepo kwa maswahaba hapo Madina, Ali angekipanda kiti, na watakaporudi, wangemkuta yeye imara kabisa katika usimamizi wa serikali.

Jeshi la Usamah, kwa hiyo, lilikuwa ni utangulizi wa kuhamisha madaraka kutoka kwa Muhammad kwenda kwa mrithi wake, Ali ibn Abi Talib.

Lakini maswahaba hawakuwa waondoke Madina. Kule kubakia Madina, walimpinga Mtume (s.a.w.) mwenyewe, na pia walizipuuza laana zake. Walijua kwamba kama Ali mara atakapopanda kwenye hicho kiti, basi wao (maswahaba) watakuwa wamefungiwa nje ya “makasri ya madaraka” daima dumu, na walikuwa, kwa sababu hii, wazuie kupanda kwa Ali kwenye kiti hicho kwa gharama zote. Hawakuwa na nia ya kufungiwa nje ya “makasri ya madaraka”

Mambo yafuatayo yawekwe akilini na msomaji kwa ajili ya kutathmini upya kwa tukio kwenye mfululizo wa matukio ya jeshi la Usamah:

1. Vita vya Muutah vilipiganwa mnamo A.D.629. Wakati wa kiangazi cha mwaka A.D.632, mpaka wa Syria ulikuwa tulivu na shwari, na hapakuwa na tishio lolote, la kweli au la kuhisiwa, la uvamizi wa Madina kutokea kaskazini. Kwa kweli, hakukuwa hata na tetesi la shambulizi juu ya Madina au Hijazi kutoka kwa yeyote yule. Na bado, Muhammad Mustafa alikuwa akionyesha shauku kubwa ya kupeleka jeshi lake huko Syria.

2. Jeshi la Usamah liliandaliwa, inavyoonekana, ili kurudisha hamasa ya Waislamu baada ya kushindwa kwao katika vita vya Muutah, na kuwaadhibu wale watu waliomuua baba yake, Zayd bin Haritha. Mtume (s.a.w.) alimtwisha Usamah kazi ya kulipiza kisasi kutoka kwa wauaji wa baba yake. Sasa Ja’afar bin Abi Talib, Shahidi mwenye Mbawa (at-Tair) wa Uislamu, na kaka mkubwa wa Ali, naye pia aliuawa kwenye vita hivyo hivyo. Lakini Mtume (s.a.w.) hakumtuma Ali au mtu mwingine yoyote wa ukoo wa Bani Hashim pamoja na jeshi hilo. Aliwabakisha wao wote pamo- ja naye hapo Madina.
3. Mbali na maradhi yake makali, Mtume (s.a.w.) alikuwa akilihimiza jeshi hilo kwenda Syria. Yeye kwa hasira aliutupilia mbali ule wasiwasi uliotangazwa wa baadhi ya Masahaba zake juu ya hali yake, na akawaamuru kwenda pamoja na Usamah mara moja.

4. Usamah bin Zayd bin Haritha alikuwa ndio mkuu wa jeshi wa wale maswahaba wa Mtume (s.a.w.) ambao walikuwa wazee wa kutosha kuwa babu zake kama vile Abu Bakr, Umar, Uthman, Abu Ubaidah bin al-Jarrah, Abdur Rahman bin Auf, na wengine wengi. Mtume (s.a.w.) kwa hiyo alikuwa akiikazia kanuni, kabla tu ya kifo chake, kwamba Waislamu wasiwe wa kumfikiria mtu kustahili uongozi kwa sababu tu alikuwa mtu mzima.

5. Kama mtu mwenye sifa zinazostahili anakuwepo wa kuwa kiongozi, basi mtu asiye na sifa hizo asimuondoe mahali pake. Masahaba walitoa vipingamizi kwenye uongozi wa Usamah juu ya msingi huu. Mtume (s.a.w.) alikubali kwamba yule tu mwenye sifa zinazostahili ndiye anayepaswa kupewa madaraka makubwa. Lakini alisisitiza kwam- ba Usamah alikuwa anastahili zaidi kuliko wale watu wote walioamriwa kuwa chini yake, licha ya ujana wake mdogo.

6. Waislamu wa Sunni wanasema kwamba Mtume (s.a.w.) “alishauriana” na maswahaba zake, na hili liliifanya serikali yake kuwa ya “kidemokrasia.” Ni kweli kwamba “alishauriana” nao mara chache katika masuala madogo lakini yeye mwenyewe alifanya maamuzi bila kuwahusisha wao.
Pale Hudaybiyah, Umar bin al-Khattab aliongoza upinzani kwake alipokuwa akijadili masharti ya amani pamoja na wapagani. Alipuuza upinzani wake, akaendelea na kusaini mkataba nao. Baadae, mafaqihi wa Sunni walieleza kwamba Mtume (s.a.w.) alipuuza upingaji wa Umar kwa sababu alikuwa (yeye Mtume) akitenda chini ya amri ya Mbinguni. Wako sahihi. Lakini kuteuliwa kwa Usamah kama mkuu wa jeshi hakukuwa na uhusiano wowote na amri za Mbinguni na Mtume (s.a.w.) alikuwa huru kutangua amri zake wakati anapokabiliwa na upinzani kutoka kwa maswahaba. Bali alikataa hata kuzungumza nao juu ya suala hilo seuze “kutaka ushauri” wao juu ya suala hilo.

7. Amri za Mtume (s.a.w.) kwa maswahaba zake kuwa jeshini chini ya Usamah, na kuon- doka Madina kwenda Syria, zilikuwa wazi sana. Lakini hawakuondoka Madina, na akafa. Wao, kwa hiyo, waliijua dhamiri yao ambayo ilikuwa ni kuwepo kimwili hasa pale Madina wakati wa kifo chake.

8. Masahaba wale wa Mtume (s.a.w.) ambao aliwaamuru kupiga ripoti kikazi kwa Usamah – mkuu wao – walikuwa wakimdharau wakati alikuwa bado yu hai. Ikiwa waliweza kutojali amri zake na matakwa yake katika uhai wake, wanaweza kama kawaida, kutojali amri na matakwa yake katika suala la mrithi wake baada ya kifo chake. Waliweka tamaa na maslahi yao binafsi mbele ya amri na matakwa ya Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) aliyebarikiwa.