read

Jografia Ya Arabuni

Ni makubaliano ya wanahistoria kuanza historia ya eneo kwa jografia yake. Wanafanya hivyo kwanza kwa sababu tamthiliya ya historia inaonyeshwa kwenye “uwanja” wa pazia lake la ki-jografia; na halafu tena kwa sababu ya kipengele kinachojulikana katika siasa za kijografia kama “utambuaji wa jografia”. Imesemekana kwamba sio desturi nyingi nyingine zinaungana kuunda athari ambazo zikitendekea kupitia vizazi vinavyofuatana, hutengeneza tabia ya watu na dola, na tabia huchukua sehemu muhimu katika kuunda historia yao.
Peninsula (rasi) ya Arabia ndio chanzo cha Uislamu. Uislamu “umezaliwa” ndani yake humo, na “ukakua” ndani yake, na ulikuwa tayari “umekomaa” ulipotoka ndani yake.

Ilikuwa katika miji ya Kiarabu ya Makka na Madina ambamo utambulisho wa Uislamu fasaha ulikuzwa, na Uislamu kwa kweli “ulitengemaa.” Ufahamu wa jografia ya Arabia, kwa hiyo ni muhimu sana kwa ajili ya kuelewa mkondo wa historia yake.

Ufuatao ni mukhtasari wa jografia ya peninsula ya Arabia: Arabia, kama eneo lolote jingine, ina namna ya mandhari inayonyoosha na kuwabadili wale wanaoishi ndani yake na wanaopita humo. Ni ardhi kavu, nzito isiyokalika, na iko au ilikuwa, mpaka kupatikana kwa mafuta, ni kikwazo cha kudumu cha uhai kwa umahiri wa mwanadamu.

Uhai wake humo ulitegemea uwezo wake wa kukubaliana nayo.

Kinyume na fikra za watu wengi, Arabia sio kwamba yote ni nyika ya mchanga. Ina sehe- mu kubwa tofauti katika umbo juu ya usawa wake wa ardhi, sehemu zake muhimu zikiwa ni mchanga wenye joto kali, milima yenye rangi ya urujuari, mabonde membamba yaliyo katikati, vilele vyake vya ajabu vinavyochoma kwenye anga ya shaba, mawe yenye kupukutika, nyanda ngumu, maumbile ya kushtusha ya miamba ya kijiometria na yenye umbo la pia, vichuguu vya mchanga vinavyohamahama daima na chemchemi na mazingira ya maziwa, vijito na bustani.

Ingawa karibu sehemu kubwa ya usawa wa ardhi ya jangwani ni wazi na kame, Arabia ina sehemu nyingi ambazo zinaonekana vizuri kwenye mwanga wa picha. Zina mandhari nzuri za ajabu zenye mahadhi nzuri, zenye kutawala mawazo zenye kupumbaza na kuhadaa – uzuri wa mchanga laini, ambao kama mawimbi ya bahari, daima uko unatembea. Uzuri huu unafifia haraka zaidi kuliko uzuri wa nakshi za mti usio na maua na wenye manyoya kwenye ukungu, na hata zaidi ya theluji iliyodondoka mara. Mawimbi ya mchanga yamerefuka kufikia upeo wa macho na zaidi, katika dunia ya ukimya na utupu. Jua linaweka mabaka yenye mwanga mkali juu ya mchanga, na upepo unafanya michoro ya kisanii ndani yake na kuifuta punde kidogo baadae. Hivyo upepo wakati wote unaumba, unaharibu na kuumba tena mandhari.

Na mandhari haya, katika tash’bihi zake zisizo na ukomo yamezaliwa kutia nuru na kutoonekana katika hewa ya jangwani, na kuyeyuka bila kutambuliwa, Sura ya nchi inakuwa ikibadilika na kupata daima Sura mpya nyingi za ajabu, na inakuwa ikisogea bila kutabirika toka sehemu moja kwenda nyingine. Mchanga unaweza kurundikwa kuwa chuguu kubwa linaloweza kufikia zaidi ya mita 150 juu ya msingi wa mwamba. Kutegemea mwelekeo na nguvu ya upepo, vichuguu hivyo huchukua namna nyingi za maumbo kama mwezi muandamo wa sherehe au migongo mirefu iliyosambamba au mkusanyiko mkubwa wa milima kama piramidi ambayo inaweza kuitwa milima ya mchanga.

Ikiwa kama jangwa hilo linazo Sura nyingi, pia inazo hali nyingi, na nyingi zao hazitabiriki. Kitambo kimoja inaweza kuwa ya udanganyifu unaofaa na utulivu lakini kitambo kidogo tu kinachofuatia, inaweza kuwa na ghasia mbaya, rahisi kubadilika, yenye kuogofya na kutoaminika kama bahari iliyochafuka. Misafara mizima ya watu ngamia na farasi, inase- mekana kupotea ndani yake, imemezwa, kama kwamba na michanga katili yenye njaa.

Katika dhoruba ya mchanga ambayo inaweza kudumu kwa masiku kidogo, jua mwezi, nyota, kontua za Sura ya nchi na peo za macho vimefutiliwa mbali, na safu za mchanga zenye hasira zinazunguka ovyo ovyo, na kutoa vivuli vya kisanii (surreal) juu ya usawa wa jangwa linaloghadhibika. Katika kiangazi, jua la wima linatoa tufani ya joto ambayo huchoma ardhi kama iliyochomwa na mwenge wa moto, jangwa linakuwa lenye mgawanyiko wa element mbili – joto na mchanga. Wakati mwingine wimbi la vumbi linafuatiwa na manyunyu yenye baridi na upepo yanayoonyesha “pinde mbili” za mvua – upinde mkubwa ukiwa na mdogo zaidi kati yake. Hivyo kitisho na uzuri vyote vinapatana kwenye mzunguko wa maisha ya jangwani.

Lakini kuanzia upande mmoja hadi mwingine na daima, hilo jangwa linabakia kutengwa, kimya, baya, lisilostaarabika la kutisha na kuogofya; na linabakia limefunikwa katika hofu yake kuu na upweke. Baadhi ya watu wanaamini kwamba hili jangwa lenye mkanganyiko lina “muujiza” wake ambao kwa kina sana huwagusa watu. Ni kwa kuegemea kwenye pazia hili kwamba, Mwarabu – mtoto wa jangwa - alifikia kilele cha maisha yake.
Arabia ndio peninsula (rasi) kubwa duniani lakini Waarabu wenyewe wanaiita Jazirat-ul- Arab (kisiwa cha Arabia), ambayo kwa namna nyingine ndicho. Ikipakana upande wa Mashariki na Ghuba ya Uajemi, Kusini na bahari ya Arabia, na upande wa kaskazini na “bahari kuu ya mchanga” ya jangwa la Syria.

Kiumbo, Arabia ni ya pembe nne yenye eneo la maili mraba milioni 1.2. Pwani ya Bahari nyekundu kutoka Ghuba ya Aghaba upande wa kaskazini mpaka Bab-el-Mendeb upande wa Kusini, ina urefu wa maili 1,200; na kutoka Bab-el-Mendeb upande wa Magharibi hadi Ras-el-Hadd upande wa Mashariki ni karibu urefu huohuo.

Kwa Sura, Arabia ni uwanda wa juu, mkubwa unaonyanyuka taratibu kutoka Mashariki kwenda Magharibi.

Mbali na Yemem na mabonde yaliyotawanyika katika safu za milima ya Magharibi nchi yote ni ya mchanga na mawe, na kavu na iliyochakaa.

Ifuatayo ni migawanyiko ya Kisiasa ya peninsula ya Arabia (1992)

1. Falme ya Saudia.
2. Jamhuri ya Yemen
3. Usultani wa Oman
4. Umoja wa Falme za Kiarabu
5. Qatar
6. Bahrain
7. Kuwait.

Yafuatayo ni maelezo mafupi ya kila moja ya maeneo haya saba ya kisiasa:

1. Falme Ya Saudia

Hii Falme ya Saudia inachukua maili za mraba 850,000 za peninsula ya Arabia. Idadi ya watu wake inakisiwa kuwa milioni kumi, na mji wake mkuu ni Riyadh. Majimbo yake ya “Pwani” ni Hijaz na Asir kwenye bahari ya Red Sea. Uwanda mfinyu wa Pwani ya Tihama unakwenda sambamba na bahari nyekundu (Red Sea).

Miji pacha ya Makka na Madina iko mwenye jimbo la Hijaz. Hijaz kwa hiyo, ndio nchi takatifu ya Uislamu. Hesabu ya watu wa Hijaz inakadiriwa kuwa milioni mbili, na eneo lake ni maili mraba 135,000. Miji mikuu na miji ya kawaida ya Hijazi ni Jeddah, bandari ya Makka, na sehemu kuu ya kibiashara ya nchi hiyo; Yanbu, Bandari ya Madina; Ta-if, kituo cha mlimani kilichoko Kusini Mashariki ya Makka, na mji mkuu wa kiangazi wa falme hiyo; Khaybar, Tabuk na Tayma. Huu “Mpango kabambe” wa Uislamu ulikamilishiwa Hijaz, na historia ya kuzaliwa na kukua kwake kumefungamana bila kutengeka na jimbo hili kunakolifanya kitovu cha ulimwengu wa Kiislamu.

Asir ndio ukanda wenye rutuba kiasi wa nyanda za Pwani na milima upande wa Kusini Magharibi, Kaskazini mwa Yemen, wenye vilele vinavyonyanyuka kufikia futi 10,000, na mvua za kutosha kufanya kilimo cha matuta ya mkingamo. Kile kituo maarufu cha mlimani cha Abha na makazi muhimu ya kilimo ya Jizan yako Asir. Jizan ndio bandari ya Asir.

Najd ni nyanda za juu za katikati ya Arabia yenye muinuko wa wastani wa futi 3,000. Hali inayotawala ya topografia (mandhari) yake ni ule mfumo wa milima uitwao Tuwayq. Riyadh, mji mkuu wa falme hii, upo Najd. Chemchemi za Buraydah na Hayil ziko sehemu ya Kaskazini ya Najd.

Al-Hasa au jimbo la Mashariki liko kwenye Ghuba ya Uajemi. Mafuta yote na gesi ya falme hii zipatikana katika jimbo hili. Linazo pia zile chemchemi maarufu za Hofuf na Qatif. Vituo vya kibiashara vinavyoongoza jimboni humu ni Al-Khobar na mji wa bandari wa Dammam. Miji mingine maarufu ni Dhahran na Ras Tanura.

Ruba’-al-Khali (upande wa wazi) ulioko Kusini ndio bonge kubwa la mchanga duniani linaloendelea, na linachukuwa eneo la maili mraba 250,000. Kwa Waarabu linajulikana tu kama “Ar-Ramal” (michanga).
Kwa jumla ni jangwa lisilo na uhai, na ni moja kati ya sehemu ambazo ni pweke mno na kame za dunia. An-Nufud kaskazini mwa peninsula hii ndio jangwa kuu la pili katika Arabia. Lina eneo la maili mraba 30,000.

2. Jamhuri Ya Yemen

Jamhuri ya Yemen iko Kusini na Kusini Magharibi ya peninsula ya Arabia, na idadi ya watu ya milioni kumi na moja na eneo la maili mraba 190,000. Ndio eneo pekee la peninsula hii linalopata mvua za monsuni, na kuifanya sehemu yenye rutba sana na yenye watu wengi. Mlima mrefu sana wa Arabia, an-Nabi Shu’aib, uko Yemen na unafikia urefu wa futi 12,350. Sana’a ndio makao makuu na mji mkubwa zaidi katika nchi hii. Upo katika muinuko wa futi 7200, na unafahamika kwa hali yake ya hewa ya kiafya nzuri. Aden ndio mji mkuu wa kibiashara. Al-Mocha, Al-Huhaydah, Ta’izz na Mukalla ni miji mingine mikuu. Sayun na Shibam ni miji ambayo ni maarufu kwa magorofa yake marefu.

3. Falme Ya Oman

Falme ya Oman inachukua pembe ya Kusini Mashariki ya peninsula ya Arabia na ina majimbo ya Oman na Dhafar. Ina idadi ya watu milioni moja na eneo la maili mraba 90,000. Muscat ndio makao makuu na Matrak ndio mji mkubwa zaidi.

4. Umoja Wa Famle Za Kiarabu (Imarati)

Jamhuri ya Falme za kiarabu inaudwa na nchi saba: Abu Dhabi, Dubai, Ajman, Sharjah, Fujaira, Ras-el-Khaimah, na Ummul-Qawain. Zina jumla ya maili mraba 32,000 na idadi ya watu 500,000. Makao makuu ya umoja huo ni Abu Dhabi ambayo pia ndio kubwa zaidi na mji maarufu zaidi wa falme hizo.

5. Dola Ya Qatar

Qatar ina eneo la maili mraba 4,250 na idadi ya watu 200,000. Makao makuu yake ni Doha. Qatar ina idadi ndogo zaidi ya watu katika dola yote ya Kiarabu.

6. Dola Ya Bahrain

Bahrain ni mkusanyiko wa visiwa 30, vyenye eneo la maili mraba 240 kwa jumla, na idadi ya watu 300,000. Manama, mji mkuu wa dola hii, upo kwenye kisiwa cha Bahrain, na Muharraq ndio mji mkuu wa pili katika mkusanyiko huu wa visiwa.

7. Dola Ya Kuwait

Kuwait ina maili mraba 6,200 kwa eneo na inayo idadi ya watu milioni 1.5. mji wa Kuwait ndio makao makuu.

Hali Ya Nchi

Ingawa Tropik ya Kansa inapita katikati ya peninsula ya Arabia, nchi hiyo sio ya joto jingi. Kiangazi chake ni kirefu na chenye joto jingi, chenye halijoto linalopanda hadi kufikia nyuzi joto130 Farenhaiti katika sehemu nyingi. Vipupwe vyake ni vifupi na vyenye baridi. Mvua ni haba, zenye wastani wa inchi nne kwa mwaka. Pembe yake ya Kusini-Magharibi; hatahivyo, hupata mvua kubwa kiasi, kwa kadiri ya inchi ishirini.

Uotaji Wa Mimea

Uotaji mimea kwa jumla umetawanyika sana kutokana na kukosekana mvua na kwa sababu ya kuwepo chumvi nyingi kwenye udongo. Miti halisi ni adimu sana na vichaka ni vya kawaida. Mimea yote imebidi ijitohoe yenyewe ili kukubaliana na hali ya kuwepo jangwa.

Mtende huota kila penye maji. Ndio mti maarufu unaopandwa sana katika peninsula yote. Matunda ya tende ndio zao kuu la Waarabu wengi, na mti wake unatoa mbao yenye thamani na mazao mengineyo. Miti aina ya Tamarisk na Acacia pia inapatikana katika sehemu nyingi za nchi hii.

Nafaka

Nafaka kuu za Arabia ni ngano, shairi, mahindi na ulezi. Kahawa inalimwa Yemen; na pamba kwa viwango tofauti huko Yemen na Oman. Matunda ya maembe yamelimwa kwa mafanikio katika Oasisi za jimbo la Al-Hasa la Saudi Arabia, na minazi inakua huko Oman. Misitu kama iliyopo Saudi Arabia, ni vikundi vichache vya miti ya mirende (junipers) katika nyanda za juu za Yemen.