read

Kabla Tu Ya Tangazo La Ujumbe Wake

Licha ya ukweli kwamba Arabia ilikuwa ni shimo la uovu na ngome ya ibada ya masamu na ushirikina, Muhammad mwenyewe hakuwa kamwe amechafuliwa na inda au dhambi yoyote, na kamwe hakuinama mbele ya sanamu lolote.

Hata kabla hajatangaza kwamba amekuja kusimamisha ufalme wa Mbingnii hapa duniani, tabia yake na mwenendo wake mwenyewe vilikuwa ni kiakisi (picha) cha Qur’an Tukufu. Hata wakosoaji wake hawakuweza kuonyesha tofauti kati ya tabia yake na maagizo ya Qur’an wakati wowote, kabla na baada ya Tangazo.

Baada ya Tangazo la ujumbe wake kama Mtume wa Mungu, aliziweka mila na desturi za kipagani chini ya amri ya kupigwa marufuku, lakini hakuna ushahidi kwamba kabla ya kufanya hivyo, yeye mwenyewe aliwahi kutenda jambo la kipagani, au hasa tendo lolote lenye kukinzana na Qur’an.

Inaonekana kwamba, Qur’an, kitabu cha Mungu kilikuwa kimegandamizwa kwenye moyo wa Muhammad tokea mwanzo, na pia inaonyesha kwamba “alihubiri” Uislamu hata kabla ya kubaathiwa, bali tu kupitia matendo yake na sio kwa maneno. Matendo yake yalikuwa fasaha sawa kama ilivyokuwa hotuba zake, na yaliutangazia ulimwengu ni vipi alivyokuwa mtu wa adabu.

Hata hivyo walikuwa ni wale mapagani waliomwita Amin (mwaminifu) na Sadiq (mkweli), na walikuwa ni watu haohao ambao, katika miaka ya baadae, walimsumbua, wakamuwinda, wakamfukuza, na kuweka na kutangaza malipo juu ya kupatikana kichwa chake.

Pamoja na kupotoka na ukorofi, kama mapagani wa Kiarabu walivyokuwa, bado walivutiwa na ukweli; hata ukiwa kwa adui. Bado kupendezewa kwao na ukweli wa Muhammad hakukuwazuia kutafuta kumuangamiza aliposhutumu ibada yao ya masanamu na ushirikina wao. Walishikwa na kiu juu ya damu yake tangu pale alipowaita kwenye Uislamu lakini hawakujiuliza kuhusu kuwa kwake mkweli. Juu ya hoja hii hapawezi kuwepo na ushahi- di wa kuaminika kabisa hasa zaidi ya wao.

Wenyeji wa Makka walipendezewa sio tu na uadilifu wa Muhammad, bali pia na maamuzi yake. Wakati mmoja, Maquraish walikuwa wanajenga upya Al-Kaaba, na katika ukuta mmoja wapo walikuwa waweke lile Jiwe Jeusi. Mtu alikuwa alilete lile Jiwe Jeusi kwenye eneo la ujenzi, alinyanyue kutoka ardhini, na aliweke katika sehemu yake juu ya ukuta huo. Ni nani alikuwa alifanye hili?

Kila ukoo uliidai heshima hiyo iwe juu yao wenyewe, lakini zile koo nyingine hazikuwa tayari kumkubalia yeyote katika jambo hili. Kutokubaliana huku kulisababisha maneno makali, na wakaidi wakatishia kuamua kwa upanga, ni nani angeweka lile Jiwe Jeusi mahali pake katika ule ukuta.

Wakati ule, mzee mmoja wa Kiarabu akaingilia kati, na akashauri kwamba badala ya kupigana na kuuana, wakuu wa koo zile wangepaswa wasubiri na kuona ni nani atakuwa mtu wa kwanza kuingia katika maeneo ya Al-Kaaba asubuhi itakayofuatia, na kisha kulikabidhi suala hilo kwake kulitolea hukumu.

Ulikuwa ni ushauri wa busara, na wale wakuu wakaukubali kwa busara. Asubuhi iliyofu- ata ule mlango wa Al-Kaaba ulipofunguliwa, walimuona Muhammad akiingia kupitia hapo. Wote walifurahi kwamba alikuwa ni yeye, na wakakubali wote kurufaisha mgogoro wao kwake, na kukubali uamuzi wake.

Muhammad aliagizia kipande cha nguo kiletwe, na kitandazwe pale chini. Kisha yeye akaliweka lile Jiwe juu yake, na akamwambia kila chifu kunyanyua moja ya pembe zake na kulibeba mpaka chini ya ule ukuta wa Al-Kaaba. Ilipokwisha fanywa hivyo, yeye mwenyewe alilinyanyua lile Jiwe na kuliweka kwenye nafasi yake.

Uamuzi wa Muhammad ulimridhisha kila mmoja. Kwa hekima zake, ameziokoa zile nyuso na ameepusha umwagaji wa damu. Tukio hili pia lilithibitisha kwamba nyakati za migogoro, Waarabu waliheshimu maoni yake. Alikuwa kiongozi wa watu mwenye kipaji.