read

Kifo Cha Malik Ibn Ashtar Na Kupokonywa Kwa Misri

Gavana wa Ali huko Misri alikuwa ni Muhammad bin Abu bakr. Mnamo mwaka 658 (38 H.A.) Mu’awiyah alimtuma Amr bin Al-Aas pamoja na jeshi la wapiganaji 6,000 kuiteka Misri kwa ajili yake. Muhammad alimuomba Ali kumtumia msaada wa kuihami Misri. Ali alitambua kwamba mtu pekee atakayeweza kuiokoa Misri kutoka kwenye makucha ya Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas, alikuwa ni Malik bin Ashtar. Yeye, kwa hiyo, alimtuma Malik kama gavana mpya wa Misri, na akamwita Muhammad ibn Abu Bakr kurudi Kufa.

Lakini Malik wala Muhammad hawakuweza kamwe kuvifikia vituo vyao. Malik aliondoka Kufa kwenda kuchukua madaraka ya Misri. Lakini mashushushu wa Mu’awiyah, wakiwa wamejifanya kama wamiliki wa nyumba za kulala wageni kijijini, walikuwa wakisubiri kumpokea yeye kwenye mpaka. Walimtilia sumu kwenye kinywaji chake, na akafa kutokana na athari zake (Abul Fida). Malik alikuwa ni mshindani asiyeshindika wa Mu’awiyah.

Yule shushushu aliyekuwa amemtilia Malik sumu, mara moja akatoa taarifa ya “mafanikio” yake kwa Mu’awiyah, na yeye Mu’awiyah hakuweza kuamini bahati yake nzuri. Katika kilele cha furaha, alisema kwa mshangao: “Leo Ali amepoteza mkono wake wa pili.” Kwa kumuua Ammar bin Yasir katika vita vya Siffin, Mu’awiyah alikuwa ameukata mkono mmoja wa Ali; na sasa kwa kumuua Malik, amekata mkono wake mwingine pia. Baada ya kifo cha Malik, Ali alikuwa amepoteza mikono yote miwili. Mu’awiyah alikuwa ameukata mkono wa Ali kwa msaada wa silaha yake ya siri lakini yenye nguvu sana – sumu! Sumu “iliwayeyusha” washindani wa Mu’awiyah wasioshindika, na kumuondolea yeye hofu kudumu.

Francesco Gabrieli:

“Katika miaka ile Amr bin Al-Aas iliiteka upya Misri kwa ajili ya Bani Umayya, akimuengua kwa njia ya sumu, Malik al-Ashtar ambaye Ali alikuwa amemtuma kwenda huko kama gavana.
(The Arabs, A Compact History, uk. 69, 1963)

Kwa Ali, kifo cha Malik kilikuwa ni pigo lenye kuyumbisha. Kama angekuwepo kamwe mtu mmoja katika Arabia ambaye alikuwa ni jeshi la mtu mmoja, alikuwa ni Malik. Kuwepo kwake kulichochea kujiamini katika jeshi lake mwenyewe, na jina lake lilitia hofu katika mioyo ya maadui. Waarabu hawakutoa kwamwe mshika upanga mwenye kuogopesha zaidi yake. Kwa kutumia ujasiri na uwezo, alijisogeza mwenyewe mpaka kwenye upeo wa ubingwa. Ni moja ya misiba katika historia ya Waislamu kwamba kazi yake ilikatwa ghafla katika ujana wa maisha yake. Alikuwa jasiri, shupavu, mwenye akili, muungwana na muumini.

Walikuwepo watu wengi, ambao mpaka kifo cha Ammar ibn Yasir, walikuwa hawajajiamulia kama wapigane au wasipigane upande wa Ali. Ilikuwa ni baada tu ya kutimia kwa utabiri wa Mtume wa Allah swt. kwamba Ammar atakuja kuuawa na watu waovu, ambapo waliporidhika kwamba haki na kweli iko upande wa Ali. Lakini Maliki hakuwa kamwe na matatizo kama hayo. Yeye alijua Ali na Ukweli walikuwa hawatenganishiki, na alikuwa thabiti kabisa katika utii na uungaji mkono kwake.

Wanahistoria wengine wamesingizia kwamba Malik alikuwa mmoja wa wale watu waliokuwa wamehusika katika kifo cha Uthman. Ni kweli kwamba Malik alikuja Madina kutokea Kufa pamoja ujumbe wa watu lakini hakuwa amekuja kumuua Uthman. Alikuja kumuomba tu Uthman kumuondoa gavana muovu na asiye na maadili. Yeye alikuwa ndiye mtu wa fahari kabisa ndani ya Arabia, na kitu kimoja ambacho asingeweza kukifanya ni kuua mzee wa miaka 84. Malik, kwa hakika, wala hakuingia kwenye kasiri la Uthman kwa wakati wowote ule. Kama angekuwa ameingia, Naila (mkewe Uthman) angezitoa habari hizi wakati Ali alipokuwa anawahoji mashahidi wa uhalifu huo; na Marwan angetangaza habari hizo za kuingia huko kwa dunia nzima. Lakini hakufanya hivyo kamwe.

Dai la kwamba Malik alikuwa mmoja wa wauaji wa Uthman, lilibuniwa na Mu’awiyah. Alikuwa anatoa mawazo mapya nyakati zote. Katika vita vya Siffin, pale alipomwona Malik akiwaendea kwa nguvu walinzi wake, aliguta kwa woga na hofu: “Ooh niokoeni kutokana na Malik; yeye ndiye aliyemuua Uthman.”

Mu’awiyah alijua kabisa kwamba Malik hakumuua Uthman lakini alijua pia kwamba wale watu wa Syria walimpenda sana Uthman na wangemvamia muuaji wa Uthman kama majini, endapo wangempata. Kwa kumwita Malik muuaji wa Uthman, alitumaini kwamba angewazindua watu wa Syria kufanya juhudi kubwa mno kuzuia mashambulizi yake, na hivyo kuokoa maisha yake mwenyewe. Wanahistoria wa Damascus wenye kujipendekeza walikichukua kilio hicho kutoka kwa Mu’awiyah, na tangu hapo, uongo huo umekuwa ukipita kutoka kizazi hadi kizazi.

Ni moja ya kejeli za historia ya Waislamu kwamba ingawa Aisha, Talha na Zubeir waliwa- chochea wazi wazi watu kumuua Uthman, hawakuwa wametuhumiwa kamwe katika baraza lake. Na ni nini kilichomzuia Mu’awiyah mwenyewe kwenda Madina kuokoa maisha yake Uthman? Hakuna! Lakini hakufanya hivyo kamwe. Alizuia msaada wake kwa makusudi, na kumuacha Uthman afe. Lakini baada ya kifo chake, alifanya ushirikiano, kwa kubadilishana na Misri, na Amr bin Al-Aas, ili “kutafuta kulipiza kisasi kwa kifo cha Uthman.” Kama ilivyoelezwa kabla, Amr alikuwa mmoja wa maadui wasiosuluhishika kabisa wa Uthman, na huenda alikuwa ndiye muuaji hasa!

Mpangilio wa mambo ulibadilika baada ya kifo cha Uthman. Kwanza Aisha, Talha na Zubeir, na kisha Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas walisimama kama wahusika wakuu wa Uthman kutafuta kulipiza kisasi kwa ajili ya damu yake. Shauku zozote mbalimbali na mara nyingi za utusitusi za wale wanaume na wanawake waliozunguka maiti ya Uthman, ni dhahiri kwamba usalama wake haukuwa hofu yao walau hata kidogo. Huu ni ukweli ambao hauwezi kukanushika lakini pia ni ukwali ambao wanahistoria wa Sunni hawapendi kuufichua. Inafariji zaidi sana na ni rahisi sana kwao kudai kwamba Muhammad ibn Abu Bakr au Malik ibn Ashtar walihusika katika mauaji ya Uthman kuliko kukubali kwamba Aisha, Talha, Zubeir, Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas, wote walishiriki katika msiba huu wa kutisha wa kifo cha khalifa huyu mzee.

Malik ibn Ashtar alifariki wakati Ali akiwa anamhitaji sana, na hapakuwa na mtu ambaye angeweza kuchukua nafasi yake. Mshituko wa Ali, wa kifo cha marafiki kama Ammar ibn Yasir na Malik ibn Ashtar, ulikuwa wa kuumiza sana lakini alihimilishwa na Imani yake. Aliuona kila mshituko mpya, kila huzuni mpya, na kila msiba mpya, mtihani juu ya imani yake, na ilibakia imara. Imani yake katika rehema za Muumba wake ilikuwa kubwa mno kuliko kitu chochote ambacho kingeweza kumfika, na hakukubali kukata tamaa hata kidogo.

Malik alikuwa ni mtu wa namna ya kipekee kweli kweli. Alikuwa mjuzi wa vita kikamilifu, aliyejitoa, mwenye kuheshimika, na mwenye uhodari kwa kiwango cha juu kabisa na mwenye kujiamini. Alikuwa ni mfalme miongoni mwa watu. Mtu mashuhuri zaidi kuliko yeye katika upekee wake wa ujasiri na wa dhahiri, na wepesi na ufuatiliaji wa adui unaojulikana sana, hauonekani popote katika historia ya Arabuni.

Propaganda imefanya majina wa watu wengine kujulikana zaidi kuliko yeye lakini bado anabakia kutolinganishika. Alikuwa ndiye ‘Asiye Kifani’ wa Uislamu.
Huenda haiwezekani kumpa Malik ibn Ashtar heshima iliyokubwa zaidi kuliko ile aliyopewa na bwana wake mwenyewe, Ali Ibn Abi Talib. Katika vita vya Layla-tul-Harir, Ali aliweka mikono yake juu ya mabega ya Malik, na akasema: “Umenitumikia mimi kwa heshima na utii ule ule ambao mimi nilimtumikia bwana wangu, Muhammad, Mtume wa Allah aliyebarikiwa.”

Kupokonywa Misr

Amr bin Al-Aas aliingia Misri bila upinzani wowote, na pindi alipokabiliana na Muhammad ibn Abu Bakr, alimshinda kwa urahisi sana. Muhammad alikuwa hana jeshi, na alijaribu kupigana akiwa na wapiganaji wachache tu. Watu wa Syria walimkamata, na wakamtesa mpaka akafa. Amr akaikalia Misri, na ikawa sehemu ya milki za Mu’awiyah.

Ali alimpenda Muhammad ibn Abu Bakr kama mwanawe mwenyewe. Kifo chake kilikuwa ni mshituko mwingine mbaya mno uliombidi kustahimilia. Aliswali kwa ajili yake na akamuombea rehema na baraka za Allah juu ya nafsi yake tukufu.

Mnamo mwaka wa 659 Mu’awiyah aliongeza vita vyake vya kero dhidi ya Ali, na akatuma vikosi kwenda Jazirah na Hijazi kutishia watu, na kuwavunja hamasa zao. Sera yake mwanzoni ilikuwa ni kuwatia cheche za hofu na kuacha moto ufanye yaliyobakia lakini manahodha wake mara wakaigeuza kuwa taswira yenye kubadilika ya vurugu na kifo. Huko Jazirah, Nu’man bin Bashir aliishambulia Ainat-Tamar akiwa na watu 2,000; Sufyan bin Auf aliishambulia Anbar na Madaen akiwa na wapiganaji 6,000; Abdallah bin Masadah Fizari aliishambulia Tima pamoja na kundi la maharamia 1,700; na Zahhak bin Qays na wafuasi wake wakauangamiza mji wa Waqsa. Waliwaua wale wanaume wote, wanawake na watoto ambao waliwashuku kuwa na urafiki kwa Ali, na wakaipora hazina ya umma popote walipoiona.

Dr. Hamid-ud-Din:

“Kule kuipata Misri kuliimarisha mikono ya Mu’awiyah kupita kiasi. Kisha yeye akatuma vikosi vya jeshi lake ndani ya Hijazi, Jazirah na Iraq. Walipita wakipora, kueneza hofu na kuua. Mu’awiyah alishambulia kingo za Tigris yeye mwenyewe binafsi, na akaitwaa hazina ya umma huko Jazirah.”
(History of Islam, Lahore, Pakistan, uk. 204, 1971)

Mu’awiyah na majenerali wake walikuwa wametwaa sera ya kufanya vita vya mara kwa mara dhidi ya mrithi wa Mtume wa Uislamu na kiongozi wa Waislamu wote. Kwao wao, vita vya mara kwa mara vilimaanisha vita visivyo vya kawaida; vitendo vichache vya kawaida vya kijeshi, na hofu isiyo na kikomo. Waliitumbukiza Dar-ul-Islam kwenye kiwewe ambacho haijaweza kutokana nacho kamwe.

Katika mwaka 660, Mu’awiyah alimtuma Bisr bin Artat pamoja na wapiganaji 3000 kwenda Hijazi na Yemen katika ghasia za uporaji, kubomoa, kuunguza na kuua. Huko Yemen, Bisr aliuwa kwa mikono yake mwenyewe, vichanga mapacha wa Ubaidullah ibn Abbas ambaye alikuwa gavana wa jimbo hilo. Wakati aliporudi Syria, akiwa amevimbiwa damu isiyo na hatia, makumi ya maelfu ya Waislamu yalikuwa yameuawa.

Mmoja wa magavana wa Ali katika wilaya ya mpakani, alikuwa ni Kumayl ibn Ziyad. Aliomba ruksa ya bwana wake ya kuivamia Syria. Uvamizi kama huo ndani ya Syria, yeye alisema, utamlazimisha Mu’awiyah kusimamisha mashambulizi yake ndani ya Hijazi na Iraq.

Lakini maombi yake yalipata majibu bainifu kutoka kwa Ali ambaye alimuandikia hivi: “Sikutegemea kabisa wewe kupendekeza kwamba tushambulie miji na vijiji vya Syria. Ni kweli kwamba watu wa Syria ni maadui zetu lakini pia wao ni binadamu, na zaidi ya hayo, wao ni Waislamu.

Kama tutatuma vikosi vya mashambulizi ndani ya Syria, inawezekana kabisa kwamba waathirika wa vitendo vyetu vya hatua za kuadhibu hawatakuwa wale Wasyria majambazi ambao wanasumbua mipaka yetu bali ni makundi ya raia wa Syria – watu ambao sio wapiganaji.

Hivi itakuwa ni sawa na haki, kwa hiyo, kuwapora na kuwaua kwa makosa ambayo wao hawakuyatenda? La hasha. Hawatapata adhabu kwa makosa ya viongozi wao.
Kitu cha maana kwetu sisi kufanya, kwa hiyo, ni kuimarisha ulinzi wetu wenyewe dhidi ya adui, na kumfukuza kabla hajaweza kufanya madhara yoyote kwa watu wetu.”

Ile mantiki inayotawala ya “taswira” ya kulipiza hofu kwa hofu haikumvutia Ali; yeye aliiona kimsingi ni yenye kupotosha.

Ingawa Ali aliwafukuza wale wavamizi kutoka kwenye milki zake, sheria na amani ilikuwa imevunjika. Wasyria walianza kuusumbua ule mpaka kwa marudio yanayoongezeka. Bisr bin Artat aliishinda ile ngome ndogo inayolinda ule mji wa mkakati wa Anbar na akaukalia. Kisha yeye akawaua kwa upanga makundi yote kama ilivyokuwa kawaida yake yeye.

Ali aliwaita watu wa Iraq kusimama katika kulinda makazi yao dhidi ya Wasyria lakini akawaona si wenye kuonyesha hisia. Wakati wa kipupwe walisema kulikuwa na baridi sana kuweza kwenda kwenye mapambano, na wakati wa kiangazi walisema kulikuwa kuna joto sana. Viongozi wengi wa Iraqi walikuwa bado wanamfanyia kazi Mu’awiyah kwa malipo ya zawadi na ahadi zake, na walieneza chuki katika nchi. Mu’awiyah pia alifanya bidii ya kudhoofisha utii kwa Ali wa jeshi la Iraqi. Kwake yeye, mgogoro haukuishia kwenye utendaji wa majeshi, bali uliendelezwa nyuma ya mpaka na mawakala na mashabiki wake, kwa uchochezi na hujuma, na kwa propaganda na kutia kasumba.

Kwa vile kulikuwa hakuna hatua za adhabu dhidi yao, wale majambazi wa Syria walitiwa moyo wa kujipenyeza ndani na ndani zaidi ya Iraq.

Ali alifanya majaribio mengi ya kuwatoa Wairaqi kwenye ulegevu na unyong’onyevu wao lakini walijifanya kana kwamba yale mashambulizi ya Wasyria yalikuwa hayawaumizi wao. Tabia yao ya kutojitokeza ilimkera sana yeye kiasi kwamba aliwaambia kwamba kama hawatatii maagizo yake, na kuchukua silaha ili kulinda mipaka yao, atawaacha hapo Kufa, na pamoja na wafuasi wachache aliokuwa nao bado, atakwenda kujaribu kumsi- mamisha adui, bila ya kujali matokeo.

Tishio hili lilionekana kufanya kazi. Wairaqi ghafla wakatambua kwamba kama Ali atawaacha, watakuwa wamebakia bila kiongozi. Wao, kwa hiyo, wakamhakikishia yeye kwamba watamtii – katika amani na katika vita. Ali mara moja akaanza kazi ya kuliandaa upya jeshi, na kuhamasisha vikosi vipya. Alimuita Abdallah ibn Abbas kutoka Basra, na akawaamuru viongozi wengine na vikosi vyao kukusanyika katika kambi ya Nukhayla karibu ya Kufa.

Ali alijitosa kazini kufidia muda ambao ulikuwa tayari umepotea kutokana na uchelewaji wa mwanzoni wa Wairaqi katika kutii maagizo yake. Lakini huu mkurupuko mpya wa nguvu uliwashitua maadui zake, na wakatumbukia kwenye njama ya kumuwahi kumvurugia mipango yake mapema.

Ali alikuwa amekamilisha matayarisho yake kwa ajili ya kuivamia Syria lakini pale alipokuwa anatoa maelekezo ya mwisho katika mpango wake wa ugavi wa usafirishaji wa watu na mizigo vitani, akauawa katika Msikiti Mkuu wa Kufa wakati wa mawio ya Ramadhani 19 ya mwaka wa 40 H.A. (27 Januari, 661).