read

Kifo Cha Muhammad Mustafa (S.A.W.) Na Umma Wake

Waislamu waliwajibika kwa Muhammad (s.a.w.) kwa kiapo cha namna mbili; kwanza katika wadhifa wake kama Mtume wa Allah (s.w.t.); na pili katika wadhifa wake kama Mtawala wa Arabia. Hakuna ambaye angeweza kuzuia uwajibikaji na utiifu kwake katika wadhifa wowote ule, na akabakia kuwa bado ni mwislamu.

Katika mwenendo wake kama Mtume wa Allah (s.w.t.) Muhammad (s.a.w.) amewapatia wokovu kutoka kwenye fedheha ya kuabudu masanamu, na alikuwa amewafundisha kumuabudu Mungu Mmoja; na katika mwenendo wake kama Mtawala wa Arabia, alikuwa amewaletea ukombozi kutokana na machafuko ya kisiasa na vita vya maangamizi.

Alikuwa amewapa sheria na taratibu. Alikuwa pia amewapa ukombozi kutokana na maadili ya vurugu, umasikini wa kiuchumi na utamaduni usiofaa. Alikuwa amewafanya kuwa matajiri na waliostaarabika, na alikuwa amewafanya kuwa taifa kubwa. Kwa kifupi, alikuwa ndio mfadhili wao mkubwa kabisa. Cha mwisho kabisa ambacho wangeweza kumfanyia kilikuwa ni kumpatia utii na upendo wao. Utii na upendo kwa Muhammad (s.a.w.) ulikuwa uwe ndio kigezo cha imani ya Waislamu katika kazi yake katika Uislamu!

Walikuwepo wale Waislamu, wengi wao wakitokana na watu wa kawaida, ambao walimpa Muhammad (s.a.w.) upendo wao na hakuna ambaye angeweza kukataa kwamba upendo wao ulikuwa ni halisi. Wakati alipofariki, walipatwa na majonzi; walivunjika mioyo, na kwao wao ule Msikiti, mji na dunia yote ilionekana iliyotelekezwa.

Lakini hisia za maswahaba wakubwa wa Muhammad (s.a.w.) kwenye kifo chake, zilikuwa tofauti. Wakati Muhammad (s.a.w.) alipofariki, maswahaba wake wakuu hawakushtushwa na kifo chake. Kama kifo chake kiliwahuzunisha, wao hawakuonyesha kuhuzunika kokote. Kitu kimoja ambacho hawakukifanya, kilikuwa ni kutokutoa rambirambi zao kwa ile familia iliyoondokewa. Hakuna hata mmoja miongoni mwao aliyekuja na kuwaambia: “Enyi watu wa Nyumba ya Muhammad, tunachangia pamoja nanyi huzuni yenu kwa kifo chake. Kifo chake ni pengo sio kwenu tu bali kwetu sisi sote.”

Katika wakati ambapo huruma inatarajiwa hata kutoka kwa wageni, kwa kweli, hata kwa maadui, haisadikiki lakini ni kweli kwamba Masahaba wa Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Allah (s.w.t.) waliinyima familia yake mwenyewe. Waliiacha familia yake kuomboleza kifo chake yenyewe.