read

Kifo Cha Muhammad (S.A.W.), Mtume Wa Allah (S.W.T.)

MALENGO YA MAISHA YA MUHAMMAD MUSTAFA (s.a.w.), kama Mtume wa Mwisho wa Allah (s.w.t.) katika dunia hii yalikuwa:

• Kuangamiza ibada ya masanamu na ushirikina;

• Kutangaza rasmi Tauhidi ya Muumba;

• Kufikisha Ujumbe wa Muumba kwa wanadamu;

• Kukamilisha mfumo wa dini na sheria;

• Kutakasa nafsi za wanaume na wanawake;

• Kukomesha dhulma, uovu na ujinga;

• Kuanzisha mfumo wa amani pamoja na haki;

• Kuunda chombo katika namna ya hali ya kisiasa kwa ajili ya utambuzi wa malengo hayo yote
yaliyopita, na chombo ambacho kitadumisha mwendo wa kazi yake.

Ndani ya ile miaka 23 ya kazi yake kama Mtume wa Allah, Muhammad (s.a.w.) alikuwa amefanikisha malengo yote Haya, na kisha ilianza kuonekana kama ilivyo kwa wanadamu wengine wote, yeye pia ilimbidui aondoke kwenye dunia hii. Kama ilivyoelezwa hapo kabla, alipokea taarifa hii kwa mara ya kwanza pale Suratun-Nasr (msaada), Sura ya 110 ya Qur’an Tukufu, iliyonukuliwa mapema katika kitabu hiki, iliposhushwa kwake.

Muhammad Mustafa alitumia maisha yake yote katika Swala na ucha-mungu lakini baada ya kuteremshwa kwa Nasr kuzama kwake katika kumuabudu Muumba wake kukawa kukubwa zaidi kuliko hapo kabla, katika kujiandaa kukutana Naye.

Mtume (s.a.w.) mwenyewe alidokeza, angalau katika matukio haya mawili kwamba kifo chake hakikuwa mbali sana naye:

1. Katika hotuba yake ya Hija ya Muago pale Arafat siku ya Ijumaa, mwezi 9 Dhil-Hajj, mwaka wa 10 H.A., alisema: “Labda, hii ndio Hija yangu ya mwisho.” Katika kumalizia hotuba yake, aliuliza swali kwa mahujaji, yaani, “Mtakapoulizwa na Mola wenu kuhusu kazi yangu, majibu yenu yatakuwa yapi?” Mahujaji wakajibu kwa sauti moja: “Ulifikisha ujumbe wa Allah (s.w.t.) kwetu, na ulitimiza wajibu wako.” Alipolisikia jibu hili, alitazama kuelekea Mbinguni, na akasema: “Ewe Allah! kuwa shahidi kwamba nimetekeleza wajibu wangu.”

2. Wakati wa “kutawazwa” kwa Ali ibn Abi Talib pale Ghadir-Khumm, mnamo mwezi 18 Dhil-Hajj, 10 H.A., Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Allah (s.a.w.w) alizungumzia tena kifo chake kilichokuwa kinakaribia kwa kusema: “Mimi pia ni mwanadamu, na ninaweza kuitwa mbele ya Mola wangu wakati wowote.”

Makumi ya maelfu ya Waislamu waliyasikia matangazo haya ya Mtume wao (s.a.w.), na wote walijua kwamba hatakuwa nao kwa muda mrefu zaidi. Yeye mwenyewe alijua kwam- ba alikuwa amekamilisha kazi yake ambayo Mola wake alimkabidhi, na alikuwa, kwa hiyo, na shauku ya kukutana Naye.

Mtume (s.a.w.) alitumia nyakati zake za kila usiku pamoja na wake zake mbalimbali kwa zamu. Mnamo mwezi 19 Safar ya mwaka wa 11 H.A., ilikuwa ni zamu yake kulala kwenye chumba cha Aisha. Usiku, alitembelea viwanja vya makaburi vya Baqii akiwa pamoja na mtumishi wake, Abu Muwayhiba, ambaye baadae alisimulia kwamba:

“Mtume (s.a.w.) alisimama katikati ya makaburi na akayahutubia kwa maneno yafuatayo: ‘Amani iwe juu yenu ninyi mlioko kwenye makaburi haya. Mumebarikiwa katika hali yenu ya sasa ambamo mmejitokeza kutokea kwenye hali ambamo watu wanaishi katika dunia. Mashambulizi ya kuangamiza yanashuka moja baada ya jingine kama mawimbi ya giza, kila moja baya zaidi ya yale yaliyotangulia.’”

Muhammad Husein Haykal anasema kwamba yale maradhi “makali” ya Mtume (s.a.w.) yalianza asubuhi iliyofuatia ule usiku ambao alitembelea uwanja wa makaburi, yaani, mnamo mwezi 20 Safar. Yeye anaendelea kusema:

Ilikuwa ni hapo kwamba watu waliingiwa na wasiwasi na lile jeshi la Usamah halikuondoka. Kweli, ile Hadith ya Abu Muwayhibah inatiliwa shaka na wanahistoria wengi ambao wanaamini kwamba maradhi ya Muhammad (s.a.w.) yasingeweza kuwa ndio sababu pekee ambayo ilizuia hilo jeshi kutoondoka kwenda al-Sham, kwamba sababu nyingine ilikuwa ni kule kutoridhika kwa wengi, pamoja na idadi ya Muhajirina wakubwa na Ansari, kuhusiana na uongozi wa jeshi hilo. (The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Tukio lifuatalo linaelekea kuwa limetokea asubuhi ya mwezi 20 ya Safar:

Sir William Muir

Usiku mmoja Mtume (s.a.w.) alitembelea kwenye viwanja vya makaburi nje ya viunga vya mji. Huko alichukua muda mrefu akiwa amezama katika tafakari na kuwaombea marehemu. Wakati wa asubuhi, akipita kwenye mlango wa Aisha, ambaye alikuwa anaugua kutokana na maumivu makali ya kichwa, alimsikia akilalamika (kupiga kite): kichwa changu! oh, kichwa changu! Akaingi ndani na akasema: “Hapana, Aisha, kwa hakika mimi ndio ningekuwa na haja ya kulia - kichwa changu kichwa changu!” Kisha kwa mwelekeo wa upole: “Lakini usingependa wewe kuchukuliwa wakati nikiwa bado hai; ili niweze kukuswalia wewe, na kukusetiri wewe, Aisha, katika sanda yako, hivyo nikupeleke wewe kaburini?”

“Hilo litokee kwa mwingine,” alimaka Aisha, “na sio kwangu mimi!” kimzaha akaongeza: “Ah, hilo ndilo unalolitaka wewe! Hakika, naweza kukuota wewe, baada ya kwisha kunifanyia yote haya na kunizika mimi, unarudi moja kwa moja nyumbani kwangu, na kutumia jioni hiyo hiyo kwa kucheza mahali pangu na mke mwingine!”

Mtume (s.a.w.) akatabasamu kwa mzaha wa Aisha, lakini maradhi yalizidi kumsonga kwa nguvu kuweza kutoa jibu katika mwelekeo huo huo. (The Life of Muhammad, London, 1877)

Betty Kelen

Yeye (Mtume) aliomba usiku kucha (kwenye makaburi ya Baqii) na akarudi nyumbani kwake, akiingia kwenye nyumba ya Aisha, ambaye alikuwa anaumwa na kich- wa, na alipomuona Mtume (s.a.w.) alikunja uso wake na akasema, “Oh! kichwa changu!”

“Hapana, Aisha,” alisema Mtume (s.a.w.), “ni oh! kichwa changu mimi!” Akaketi chini kwa nguvu, kichwa chake kikimgonga, maumivu yakibana viungo vyake muhimu, sasa akasema: “Hivi inakuhuzunisha kujifikiria wewe mwenyewe kufa kabla yangu, ili kwamba niweze kukusetiri kwenye sanda na kukuzika wewe?”

Alikuwa anaonekana kama mgonjwa wa kufa, lakini Aisha, ambaye aliamini kwam- ba alikuwa kwa hali yoyote ile amefika mwisho wa njia yake ya ndoa za kidiplomasia, alimpa jibu la kisirani: “Hapana. Kwa sababu naweza pia kufikiria kuja kwako wewe moja kwa moja kutoka makaburini kusherehekea usiku wa harusi.” (Muhammad, The Messenger of God)

Muhammad Husein Haykal

Asubuhi iliyofuata, Muhammad (s.a.w.) alimkuta Aisha, mke wake, akilalamikia maumivu ya kichwa, na akiwa ameshikilia kichwa chake kati ya mikono miwili, huku akiugulia, “oh! kichwa changu!” Yeye mwenyewe akiwa na maumvu ya kichwa, Muhammad (s.a.w.) alijibu, “Lakini hasa, Ewe Aisha, ni kichwa changu mimi!”
Hata hivyo, maumivu hayakuwa makali sana kiasi cha kumlaza kitandani, kumzuia kazi zake za kila siku, au kumzuia yeye kuongea na wake zake na hata kutaniana nao. Aisha alivyoendelea kulalamika kuhusu kichwa chake, Muhammad (s.a.w.) alimwambia: “Haitakuwa vibaya hata hivyo, Ewe Aisha, kama ingekuwa ufe kabla yangu mimi. Kwani nitaweza hapo kukuswalia na kuhudhuria mazishi yako.” Lakini hili liliamsha tu harara za Aisha mwenye ujana, ambaye alijibu: “Wacha hayo yawe majaaliwa mema ya mtu mwingine na sio mimi. Kama hilo litanitokea mimi, utakuwa una wake zako wengine utakaokuwa pamoja nao.”
(The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Mtume (s.a.w.) hakutoa jibu lolote kwa dhihaka ya Aisha, na akaegemea kwenye ukuta. Pale maumivu yalipopungua, alinyanyuka na akawatembelea wake zake wengine kama alivyokuwa akifanya siku zote. Siku ya mwezi 24 Safar, alikuwa kwenye nyumba ya mke wake, Maimuna, alipopata shambulizi la ghafla la maumivu makali ya kichwa na homa.

Inasemekana kwamba aliwaita wake zake wote na akawaomba wamhudumie kwenye chumba cha Aisha. Walikubali kufanya hivyo.

Mtume (s.a.w.) alikuwa amechoka sana kiasi cha kushindwa kutembea mwenyewe. Kwa hiyo, Ali alimsaidia kwa upande mmoja, na Abbas, ami yake, upande mwingine, na walimsindikiza kutoka kwenye chumba cha Maimuna kwenda kwenye chumba cha Aisha. Alikaa kwenye chumba cha Aisha mpaka kifo chake siku chache baadae.

Lakini licha ya homa na udhaifu wake, Mtume (s.a.w.) alikwenda Msikitini kila mara alipoweza, na akawaongoza Waislamu kwenye Swala. Siku ya mwezi 26 Safar, anase- mekana kujisikia vizuri kidogo, na alikwenda Msikitini akisaidiwa na Ali na Abbas. Aliongoza Swala ya zuhr, na baada ya Swala, akaongea na mkusanyiko wa waumini.

Hii ilikuwa ndio hotuba ya mwisho ya Mtume wa Uislamu, na ndani yake alitoa dokezo moja zaidi lililifichikana la kifo chake kilichokuwa kinakaribia. Wanahistoria wa Sunni wanasema kwamba Abu Bakr ambaye alikuwepo katika hadhara hiyo, alielewa kile Mtume (s.a.w.) alichokisema, na akaanza kulia kwani alikuwa na moyo wa huruma sana. Mtume (s.a.w.) alimwona akilia na akajaribu kumliwaza, na kisha akigeukia ule mkusanyiko, akasema:

“Namshukuru sana Abu Bakr zaidi kuliko mtu mwingine yoyote kwa msaada wake wa hali na mali, na kwa usuhuba wake. Kama katika umma huu, ingekuwa kamwe nichague mtu kama rafiki, ningeweza kumchagua yeye. Lakini sio lazima kwa sababu udugu wa Kiislamu ni kifungu imara zaidi kuliko kingine, na kinatutosha sisi sote. Na kumbukeni kwamba milango yote inayofungukia Msikitini, lazima ifungwe isipokuwa mlango wa nyumba ya Abu Bakr.”

Mtume (s.a.w.) aliwaonya Waislamu wasije wakarudia kwenye kuabudu masanamu, na kukumbuka kwamba wao walikuwa wenye kumuabudu Mungu Mmoja, na akaongeza: “Kitu kimoja ambacho kamwe msije mkakifanya, ni kuabudu kaburi langu. Yale mataifa ya siku zilizopita ambayo yaliabudu makaburi ya mitume yao, walipatwa na ghadhabu ya Mola, na waliangamizwa. Jihadharini, msije mkawafuata wao.”

Mapema siku hiyo ilitolewa taarifa kwa Mtume (s.a.w.) kwamba Ma-Ansari walikuwa na huzuni kubwa sana kwa sababu ya maradhi yake. Ulikuwa, kwahiyo wakati muafaka wa kuwaambia Muhajirina kuhusu Ma-Ansari na huduma yao kubwa kwa Uislamu.

Akasema: “Msije mkasahau hata mara moja kile walichokufanyieni Ansari. Wamekupeni makazi na hifadhi. Walichangia nyumba zao na mkate wao pamoja nanyi. Ingawa hawakuwa matajiri, walitanguliza mahitaji yenu mbele kuliko yao. Wao ni ‘wakfia’ wangu kwenu.

Watu wengine wataongezeka kwa idadi lakini wao watapungua tu. Yote yaliyokuwa wajibu kwa Ansari, wameyatimiza kwa uaminifu kabisa, na sasa ni zamu yenu kutimiza wajibu wenu kwao.”

Ansari pia walikuwepo mle ndani ya Msikiti, na walikuwa wakijaribu kuzuia vilio vyao vya kikweukweu. Akiongea nao, Mtume (s.a.w.) akasema: “Enyi Ansari! Baada ya kifo changu mtakabiliwa na huzuni nyingi na matatizo.”
Wakamuuliza: “Ewe Mtume wa Allah! una ushauri gani kwetu? Itatupasa tufanyeje zitakapofika hizo nyakati ngumu?”

Yeye akasema: “Msiache ustahimilivu wenu, na wekeni imani zenu kwa Allah (s.w.t.) wakati wote.”

Ule msafara wa kijeshi wa kwenda Syria bado ulikuwa umesimama. Mtume (s.a.w.) aliwashutumu maswahaba zake kwa kutojali maadili kwao katika kupiga ripoti kikazi kwa jenerali wao, na akawaamuru kwa mara nyingine kuondoka hapo mjini papo hapo. Alikatisha kuongea kwa muda kidogo, na kisha akaomba laana ya Allah (s.w.t.) juu ya watu wale wote watakaodharau amri yake ya kwenda Syria.

Hotuba yake ikaisha. Mtume (s.a.w.) alishuka kwenye mimbari na kurudi chumbani kwake. Alijihisi kuzimia kutokana na ile juhudi ya kuongea, na hakwenda pale Msikitini tena. Ilikuwa ndio mara ya mwisho kuonekana hadharani.

Sehemu ya kwanza ya hotuba yake ambayo inahusiana na Abu Bakr, inaelekea ni ya uongo, na inaonekana kuwa imeongezwa. Kama ilivyokwisha kuonyeshwa, Abu Bakr alikuwa chini ya amri ya kujiunga na jeshi la Usamah lakini inawezekana kwamba Mtume (s.a.w.) alipuuza kushindwa kwake kuripoti kikazi. Mtume (s.a.w.) anaweza pia kuwa alitambua mchango wake wa mali kwa Uislamu. Aliwakomboa watumwa wengi huko Makka, na alitoa mali yake yote kuandaa msafara wa Tabuk.

Hadithi ya kwamba Mtume (s.a.w.) aliamuru milango yote iliyokuwa ndani ya Msikiti ifungwe isipokuwa mlango wa chumba cha Abu Bakr, ni Hadith ya kubuni ya dhahiri pia. Abu Bakr aliishi katika kitongoji cha Madina kilichokuwa kikiitwa Sunh. Hakuwa akiishi hapo mjini, na hakuwa na chumba ambacho mlango wake ulifungukia Msikitini.

Mtume (s.a.w.) pia alisema katika hotuba yake kwamba kama ingekuwa amchague mtu yoyote kuwa rafiki, angemchagua Abu Bakr.

Kama hotuba hii vile ilivyosimuliwa, ni sahihi, basi ina maana kwamba Mtume (s.a.w.) alitangaza hadharani kwamba hakutaka kumfanya Abu Bakr kuwa rafiki. Kama kauli yake itafafanuliwa, itasomeka hivi: “Kama ingekuwa nichague rafiki, ningemchagua Abu Bakr. Lakini sitamchagua. Sisi wote ni wahusika wa udugu wa Kiislam wa ulimwengu mzima, na hilo linatutosha sisi sote.”

Hata hivyo, kulikuwepo na nini cha kumzuia Muhammad Mustafa kumchagua Abu Bakr kama rafiki? Hakuna! Malaika Mkuu Jibril hakuja kutoka mbinguni kumwambia asimchague Abu Bakr kama rafiki, wala hakuwepo yeyote duniani hapa aliyetishia kumfanyia madhara yoyote kama angemchagua yeye (Abu Bakr) kuwa rafiki.

Kwa vile huku kulikuwa ni kuonekana kwa mara ya mwisho hadharani kwa Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Allah (s.a.w.w) na kwa vile, kwa mujibu ya madai ya Sunni, alimpenda sana Abu Bakr, alipaswa kuitumia nafasi hii, sio tu kwa kumtangaza yeye kama rafiki bali pia na kumtangaza yeye kama khalifa (mrithi) wake. Kama angefanya hivyo, angeweza mtu yoyote kumpinga? Lakini kwa sababu moja au nyingi za ajabu, hakufanya hili wala lile. (Muhammad hakumchagua Abu Bakr kama rafiki wala hakumfanya yeye kuwa mrithi wake). “Mapenzi” yake kwa Abu Bakr yalipaswa kupata maelezo, lakini hayakupata; “kukosekana” kwa ajabu sana kwa upande wake katika wakati muhimu kabisa.

Tarehe 27 ya Safar, Mtume (s.a.w.) alijihisi mnyonge sana kuweza kusimama na kuswali. Wanahistoria wa Sunni wanasema kwamba ilikuwa ni kuanzia tarehe hii kwamba alimuamuru Abu Bakr kuongoza Waislamu katika Sala. Yeye mwenyewe, wanasema, alibakia amekaa na akafanya vitendo vya Swala.

Bukhari, mkusanyaji wa Hadithi (maneno ya Mtume), anasimulia tukio lifuatalo Katika Sahih yake: “Mnamo mwezi 28 Safar, Abbas ibn Abdul Muttalib alikuja kumuona Ali, na akase ma: ‘Wallahi, Muhammad karibuni atakufa. Ninaweza kulijua hilo kutokana na kuonekana kwa nyuso za watoto wa Abdul Muttalib wanapotaka kufa. Mimi, kwa hiyo, nashauri kwamba uzungumze naye na umuulize yeye kuhusu suala la urithi (ushikamakamu) wake.’ Lakini Ali akasema: ‘Hapana. Sio katika hali aliyonayo sasa hivi. Mimi sipendi kulileta suala hilo.”

Wanahistoria wa Kishia wanaikataa kabisa “Hadith” hii. Wao wanasema kwamba Mtume (s.a.w.) alikuwa ametangaza, sio mara moja, bali mara nyingi tu kwamba Ali alikuwa ndiye mrithi wake na mtawala wa Waislamu wote.

Kama Waarabu hawakuwa wamkubali kama bwana wao hata baada ya matangazo mengi, tangazo moja zaidi lingekuwa vigumu kuweza kufanya mabadiliko. Mtume, kwa kweli, alifanya jaribio la kuandika wosia wake pale alipoitisha kalamu, karatasi na wino lakini alikutana na dharau. Na Ali hakutaka mtu yoyote aonyeshe “moyo wake wa kujasiri” kwa kukemea kwamba Mtume wa Allah (s.a.w.w) alikuwa “akiropoka.” Kusikia hiyo kauli ya tusi kungeweza tu kuharakisha kifo cha bwana wake kutokana na mshituko.

Kama Hadith hii ni ya kweli, inaelekeza tu kwenye upendo wa Ali kwa bwana wake, na kupenda kusaidia kwake kumkinga kutokana na kila mshituko.

Waislamu wa Kishia pia wanasema kwamba Abbas mwenyewe angeweza kulichukua suala hilo la kujadili na Mtume (s.a.w.) ambaye alikuwa ni mpwa wake. Mtume (s.a.w.) alikuwa mchangamfu, na mwenye kuweza kufikiwa hata na wageni. Kulikuweko na nini, kwa hiyo, kwa Abbas, cha kuwa na mashaka nacho?

Masahaba waliweza kuona kwamba Mtume (s.a.w.) hatapona kutokana na homa yake na maumivu ya kichwa. Mara alipokuwa amezuiliwa kwenye kitanda cha mauti yake, wengi wao walijihisi kwamba walikuwa “salama” kama wangeacha kumtii yeye. Kwa hiyo, lolote alilofanya katika kuwashinikiza wao katika kwenda Syria, wao hawakwenda, na msafara wa Usamah kamwe haukutimizwa – katika uhai wake!

Wakati wa mchana, Muhammad Mustafa alimwita Ali, na akamwambia: “Kwangu mimi ni mwisho wa safari. Nitakapokufa, wewe uoshe mwili wangu, uuvishe sanda, na uushushe kaburini. Ninadaiwa pesa na watu fulani na fulani, miongoni mwao Myahudi mmoja alinipa mkopo wa kutayarishia jeshi la Usamah. Lipa madeni haya kwao wote pamoja na huyo Myahudi.” Kisha akaivua pete aliyokuwa amevaa, akampa Ali, na akamuomba aivae ambapo aliivaa. Na pia alimpa yeye (Ali) upanga wake, mkuki, deraya na silaha nyinginezo.

Jumatatu, Rabi al-Awwal 1, 11 H.A.

Jumatatu, mwezi 1 Rabi al-Awwal ya 11Hijiria ilikuwa ndio siku ya mwisho ya Muhammad ibn Abdullah (s.a.w.), Mtume wa Allah (s.w.t.) katika dunia hii. Kulikuwa na nyakati ambapo alijisikia nafuu kidogo lakini wakati mwingine, alikuwa dhahiri kwenye maumivu makali. Aisha, mke wake, anasimulia ifuatavyo:

“Jinsi siku ilivyosogea kuelekea mchana, Fatima Zahra, binti yake Mtume wa Allah (s.a.w.w) alikuja kumuona Mtume. Alimkaribisha na kumwambia akae kandoni mwake. Kisha akamwambia kitu ambacho sikuweza kusikia lakini alianza kulia. Alipoyaona machozi ya binti yake, alimwambia kitu kingine ambacho pia sikuweza kusikia lakini yeye alianza kutabasamu. Yeye alifanana sana na baba yake katika mwenendo, tabia na Sura.”

Muda baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.), Aisha alimuuliza Fatima ni kitu gani ambacho baba yake alimwambia yeye ambacho kwanza kilimfanya alie na kisha kikamfanya atabasamu.

Fatima akasema: “Kwanza baba yangu aliniambia kwamba alikuwa anakaribia kufa. Nilipolisikia hili, nilianza kulia. Kisha akanijulisha kwamba mimi ndio nitakayekuwa wa kwanza kabisa kukutana naye huko mbinguni, nalo pia, ni hivi karibuni tu. Nilipolisikia hili, nilifurahi sana, na nikatabasamu.”

Washington Irving

Mtoto pekee wa Muhammad aliyekuwa amebakia, Fatima, mke wa Ali, alikuja sasa kumuona yeye Muhammad. Aisha alizoea kusema kwamba hajawahi kumuona mtu yoyote anayefanana na Mtume (s.a.w.) zaidi katika uzuri wa moyo kama huyu binti yake. Alimshuhulikia siku zote kwa upendo wa heshima. Alipokuja kwake, alizoea kusimama, kumfuata, kumshika mkono na kuubusu, na humkalisha kwenye sehemu yake mwenyewe Mtume.

Kukutana kwao katika safari hii kunasimuliwa hivyo na Aisha, katika Hadith zilizohifadhiwa na Abulfida.

“Karibu mwanangu,” alisema Mtume, na akamfanya akae karibu naye. Kisha akanong’ona kitu fulani katika sikio lake, ambacho kwacho alilia. Katika kutambua huzuni yake, alinong’ona kitu kingine zaidi, na sura yake ikan’gara kwa furaha.

“Hii ina maana gani?” nilimuuliza Fatima. “Mtume (s.a.w.) anakuheshimu wewe kwa dalili ya mategemeo ambayo hajayaonyesha juu ya yeyote kati ya wake zake.” “Siwezi kutoa siri ya Mtume wa Allah (s.a.w.w)” alijibu Fatima. Hata hivyo, baada ya kifo chake, alisema kwamba kwanza alimtangazia kifo chake kilichokuwa kinakaribia; lakini alipomwona yeye analia alimtuliza kwa kumhakikishia kwamba angemfuata baada ya muda mfupi na kuwa Malkia wa peponi.” (The Life of Muhammad)

Kuelekea mchana ule Mtume (s.a.w.) alikuwa na hali ya kutotulia. Aliulowesha uso wake mara kwa mara kwa maji baridi kutoka kwenye gudulia lililokuwa karibu yake. Alipomuona katika maumivu kama hayo, Fatima alilia: “Oh mateso ya baba yangu!” Mtume (s.a.w.) alijaribu tena kumliwaza, na akasema: “Baada ya siku hii ya leo, baba yako hatakuwepo kwenye mateso tena.” Na akaongeza: “Wakati nikifa, sema, “Sisi wote ni wa Allah na Kwake ndio marejeo yetu.”

Sasa, kupumua kwake kukawa sio kwa kawaida, na alisikika akinong’ona kitu. Ibn Saad anasema katika Tabaqaat yake kwamba Mtume (s.a.w.) alikuwa akisema: “Ninachokitafuta sasa ni kuwa pamoja na Allah (s.w.t.)” Haya yalikuwa ndio maneno yake ya mwisho.

Muhammad (s.a.w.) alisikika akiyarudia maneno haya mara tatu, na kisha akanyamaza kimya – daima! Muhammad, Mtume wa Mwisho wa Allah (s.a.w.w) kwenye dunia hii, akafariki.

Aisha anasema: “Niliweka mto chini ya kichwa chake, na nikafunika kichwa chake na shuka. Kisha nikasimama pamoja na wanawake wengine, na wote tukaanza kulia, tukipiga vifua na vichwa vyetu, na kujipiga makofi kwenye nyuso zetu.”

Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Allah (s.w.t.) alifariki siku ya Jumatatu ya kwanza ya Rabi al-Awwal ya mwaka wa kumi na moja Hijiria wakati wa mchana. Alikuwa ameishi kwa miaka 63 iliyopungua siku nane tu.

Wanahistoria wa Ki-Sunni wanasema kwamba Mtume (s.a.w.) alifariki, sio kwenye tarehe mosi bali mnamo tarehe 12 Rabi al-Awwal. Waislamu wa Shia wanasema kwamba alifariki, sio kwenye mwezi mosi ya Rabi al-Awwal bali siku moja mapema zaidi, yaani mwezi 28 Safar.

Makubaliano ya wanahistoria wa kisasa wa Magharibi, ni kwamba, Mtume (s.a.w.) alifariki mnamo tarehe 8 Juni, 632. Tarehe nane ya Juni, kwa bahati, pia ndio siku ya kuzaliwa kwake.

Mazishi Ya Mtume (S.A.W.)

Mwili wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) ulioshwa siku ya Jumanne. Ni watu sita tu waliokuwapo kwenye huduma hii ya mazishi. Nao walikuwa ni:

• Ali ibn Abi Talib

• Abbas ibn Abdul Muttalib

• Fadhl ibn Abbas

• Qathm ibn Abbas

• Usamah ibn Zayd bin Haritha

• Aus bin Khuli Ansari

Usamah, mkuu wa jeshi la kwenda Syria, alikuwa yuko Jurf, akiwa bado anawangojea maswahaba.

Baadhi yao walimpelekea habari kwamba Mtume (s.a.w.) alikuwa anafariki, na kwamba angepaswa arudi Madina. Alirudi, na muda kidogo baadae, bwana wake akafariki.

Ali aliuosha mwili wa Mtume (s.a.w.) wakati Usamah akiwa anammwagia maji. Wakati mwili ulipokwaisha kuoshwa, Ali aliufunika na sanda, na akauswalia.
Kisha yeye akatoka nje, na akawaambia Waislamu waliokuwa ndani ya Msikiti, waende chumbani na kuswali Swala ya maiti. Bani Hashim walikuwa wa kwanza kumswalia, na kisha Muhajirina na Ansari wakatekeleza wajibu huu.

Hapo Madina, palikuwa na wachimba-kaburi wawili. Walikuwa ni Abu Ubaida bin al- Jarrah na Abu Talha Zayd bin Sahl. Waliitwa wote lakini ni huyu wa mwisho tu ndiye aliyepatikana. Alikuja na akalichimba kaburi. Ali aliingia mle kaburini ili kulisawazisha vizuri. Kisha akaunyanyua mwili kutoka pale chini, na akauteremsha taratibu ndani ya kaburi, akisaidiwa na ami yake na binamu zake. Kaburi kisha likafunikwa kwa udongo, na Ali akanyunyizia maji juu yake.

Wakati Ali na watu wengine wa Bani Hashim walipokuwa wanashuhulika na mazishi ya Mtume wa Uislamu (s.a.w.), Abu Bakr, Umar, Abu Ubaidah bin al-Jarrah, na wengineo, walikuwa wanashughulika huko Saqifah wakicheza bahati na sibu ya madai ya ukhalifa. Abu Bakr, ilivyotokea, alikuwa ndiye mgombea aliyeshinda.

Alipokuwa amepokea viapo vya utii vya Ansari hapo Saqifah, yeye na marafiki zake walirudi kwenye Msikiti wa Mtume (s.a.w.w.). Ndipo akapanda kwenye minmbari ya Mtume (s.a.w.) kupokea viapo kama hivyo kutoka kwa watu wengine.

Siku ya Jumatatu jioni, na kutwa nzima ya Jumanne, watu walikuwa wanakuja Msikitini kuchukua kiapo cha utii kwake. Kuchukua kiapo kulikwisha baadae sana usiku wa Jumanne, na ilikuwa ni Jumatano tu ambapo huyu khalifa mpya alipopata muda wa kugeuzia mawazo yake kwa bwana wake aliyekwisha fariki, na kufanya Swala ya maiti kaburini pake.

Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Allah (s.a.w.) kiongozi wa Waislamu wote, na Rehma kuu ya wanadamu, hakupata mazishi ya kitaifa. Kiasi kidogo tu cha watu – ndugu zake wa karibu – walimfanyia mazishi. Wengi wa wale waliodai kwamba walikuwa ni maswahaba na rafiki zake, walimtelekeza wakati wa saa yake ya kufa. Kutokuwepo kwao kwenye mazishi yake kulikuwa ndio kuvurugika kukubwa kabisa kwa mipango kwenye mazishi yake.

Ibn Saad anasema katika Tabaqaat yake kwamba Ali ibn Abi Talib aliyalipa madeni yote ya Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Uislamu. Alimtuma mpiga-mbiu mjini kote Madina, na wakati wa msimu wa Hijja, alituma mpiga-mbiu huko Makka, kutangaza kwamba yeye Ali angelipa madeni yote ya Muhammad (s.a.w.), na kwamba yeyote ambaye alikuwa na madai, aende kwake kulipwa. Aliwalipa wadai bila ya kuwauliza maswali yoyote na bila ya kutaka uthibitisho kwamba Muhammad (s.a.w.) alikuwa anadaiwa na wao kitu cho- chote, na hili alikuwa akilifanya mpaka mwisho wa siku zake.