read

Kubadilisha Makao Makuu kutoka Madina kwenda Kufa

Mnamo Rajab ya mwaka 36 h.a. (january 657) Ali aliamua kuhamisha makao makuu ya serikali yake kutoka Madina huko Hijazi kwenda al-Kufa huko Iraq. Wakati amani na utulivu vilipokuwa vimerudishwa hapo Basra, alimteua Abdallah ibn Abbas kama gavana wake mpya, na kisha akaondoka kuelekea Kufa ambayo ilikuwa kuanzia hapo, ndio makao makuu ya Uislam.

Mnamo mwezi 12 Rajab mwaka 36 H.A., Ali aliwasili katika milango ya Kufa. Waungwana mashuhuri wa mji huo wakatoka kuja kumlaki na kumpongeza kwa ushindi wake. Akiingia mjini hapo, Ali kwanza alikwenda kwenye Msikiti Mkuu, akaswali Swala ya shukrani kwa Allah swt. kwa ushindi huo, na kisha akatoa hotuba ambayo ndani yake aliwashukuru watu wa Kufa kwa kumuunga mkono kwao, na akawasifu kwa utendaji wao kwa kijasiri katika vita vya Basra.

Waungwana wa mji wa Basra walimuomba Ali akae kwenye kasri ya gavana lakini yeye hakukubali. Badala yake, akachagua nyumba ya hali ya kawaida kwa ajili ya makazi yake.

Wanahistoria wamejaribu kutafuta sababu za kwa nini Ali alibadilisha makao makuu kutoka Madina kwenda Kufa. Maprofesa Sayed Abdul Qadir na Muhammad Shuja-ud-Din wanaandika katika kitabu chao, The History of Islam, (historia ya Uislam, kilichochapishwa Lahore, Pakistan): “Miezi saba baada ya kuchukua madaraka ya serikali, Ali aliifanya Kufa kuwa makao makuu yake mapya. Zifuatazo zilikuwa ni baadhi ya sababu zilizochochea mabadiliko haya:

1. Vile vita vya Basra au vita vya Ngamia vilipiganwa na kushinda kwa msaada wa watu wa Kufa. Ali alifanya Kufa kuwa makao yake, kiasi fulani kwa kutambua utumishi wao huu.

2. Ali alikuwa na shauku ya kuiokoa Madina kutokana na maafa ya ugomvi wa wenyewe kwa wenyewe kama ule ulioishia kwa kuuawa kwa Uthman. Yeye hakupenda Madina kugeuka eneo la matukio ya machafuko ya kisiasa kwa wakati wowote, na alitaka kuuokoa mji wa Mtume kutokana na kuharibiwa au kunajisiwa katika vita vinavyowezekana hapo baadae.

3. Kufa ilikuwa kwenye nafasi ya katikati zaidi katika dola hiyo. Urahisi wa kiutawala
wa maeneo hayo makubwa na yanayosambaa ulihitajia mabadiliko haya.

4. Ilikuwa ni rahisi kwa Ali kufuatilia nyendo za Mu’awiyah kutoka Kufa kuliko kutoka Madina.”
(The History of Islam)

Kh. Muhammad Latif Ansari wa Pakistani, mwanahistoria wa siku hizi, ameonyesha katika kitabu chake, History of Islam, kwamba kama vile tu Abu Jahl na Abu Sufyan walivyohusika na kuhama kwa Muhammad kutoka Makka kwenda Madina, ndivyo mwanawe, Mu’awiyah, alivyohusika na kuhama kwa Ali kutoka Madina kwenda Kufa. Yeye anasema kwamba vita vya wenyewe kwa wenyewe vilikuwa vimekwishaanza lakini maeneo ya mapigano yalikuwa mbali sana kutoka Madina. Ali, kwa hiyo, alibadili makao hayo kwa sababu za mkakati, na hii inaunga mkono madai yake kwamba ilikuwa ni uasi wa Mu’awiyah, gavana wa Syria, uliohusika na uhamaji wake (Ali) kutoka Hijazi kwenda Iraq.

Kwa kweli, zilikuwepo sababu yakinifu na za udhanifu kwa nini Ali alibadilisha makao makuu. Baadhi ya hizo ni hizi:

(1). Wakati Ali aliposhika kiti cha ukhalifa, vituo muhimu vya mijini vya dola hiyo vilikuwa ni Damascus huko Syria, Makka na Madina huko Hijazi, na Basra na Kufa huko Iraq.

Damascus ilikuwa imeshikiliwa na Mu’awiyah, na ilikuwa, kwa hiyo, kitovu cha upinzani kwa Ali. Kati ya hiyo miji mingine minne, Makka, mwanzoni, ilikuwa mikononi mwa viongozi wa maasi – Aisha, Talha na Zubeir. Wakiwa Makka, walianzisha jeshi la watu wa kujitolea lenye wapiganaji 3,000. Waliondoka Makka pamoja na jeshi lao kuelekea Basra, na wakaukalia mji huo. Wengi wa wale watu wa Makka ambao hawakwenda Basra pamoja na jeshi hilo la waasi, walilipatia msaada wao wa nyenzo. Kwa sababu hiyo Ali akaiondoa Makka.

Madina ilikuwa na sifa ambayo sio nzuri hata kidogo. Kama ilivyoelezwa kabla, wakati Uthman alipouawa, Madina ilikuwa chini ya miguu ya waasi. Muhajirina na Ansari walitambua kwamba hapakuwa na mtu katika Dola ya Kiislam wa kuweza kuuokoa mji huo kutokana na kuporwa, watu kutokana na kuangamizwa, na serikali kutokana na kuanguka, isipokuwa Ali. Wao kwa hiyo, walimsihi kuchukua mamlaka ya serikali.

Ali aliwaambia Muhajirina na Ansari kwamba atalikubali pendekezo lao endapo watampa kiapo cha kutii amri zake mwote katika amani na katika vita. Walimpa kiapo chao cha kumtii yeye, na akalikubali pendekezo lao.

Lakini ni siku chache tu zilikuwa zimepita wakati uasi ulipoibua kichwa chake huko Makka dhidi ya mamlaka ya makao makuu. Ali aliingia Msikitini, na kuwataka Muhajirin na Ansari kusimama katika kuilinda serikali kuu. Jibu lao pekee lilikuwa ni ukimya.

Ali akawakumbusha kile kiapo ambacho walikuwa wamempa cha kumtii yeye na bado tu hawakuvutika. Kuwasihi kwake kote na makumbusho yote yalielekea kuan- gukia kwenye masikio ya uziwi.

Ilikuwa ni baada ya majuma mengi ya makumbusho na juhudi kubwa ndipo Ali akaweza kuorodhesha msaada wa watu mia saba waliojitolea hapo Madina. Hiki ndio kiasi Madina ilichoweza kumfanyia. Aliondoka Madina na watu hawa waliojitolea – na asirudi tena.

Basra, mji wa nne, ulikuwa umekubali mamlaka ya Ali, na yeye alikuwa amemteua Uthman ibn Hunaif Ansari kuwa gavana wake mpya. Lakini kabla ya Ali kuwasili Iraq, ule “utawala wa watu watatu” wa Aisha, Talha na Zubeir ulikuwa tayari umekwishaite- ka Basra. Uthman ibn Hunaif kwa shida tu aliweza kutoroka kutoka Basra akiwa hai.

Sasa “chaguo” la Ali lilipunguzwa na kuwa la mji mmoja tu – Kufa. Ali alimtuma Imam Hasan na Ammar ibn Yasir kwenda Kufa kumletea msaada wa kumuongezea yeye nguvu. Kufa ilituma wapiganaji 12,000 kwenda Basra, na walikuwa ni wapiganaji hawa ambao waliopigana katika vita vya Ngamia, na wakaushinda ule “utawala wa watu watatu” wa Aisha, Talha na Zubeir.

Makka, Madina na Basra zimemuacha Ali bila kufahamu fika kuhusu kile ambacho wangeweza kufanya katika dharura. Lakini raia wa Kufa walikuwa wamemtumia msaada katika wakati muhimu sana katika muda wake. Aliweza kuona wazi kwamba kama kuna vita na Mu’awiyah, alikuwa na jeshi la Kufa tu la kutegemea. Ilikuwa, kwa hiyo, ndio mantiki ya matukio yaliyoshawishi uamuzi wa Ali wa kuifanya Kufa makao makuu ya dola.

Watu wa Madina, inavyoonekana, walikuwa na vuguvugu la upendeleo wa matukio yanayotokea karibu yao. Wakati Ali alipotangaza kwamba atayahamisha makao makuu ya serikali kwenda Kufa, hakuna mtu miongoni mwao aliyelalamika dhidi ya uamuzi huu. Hawakuonyesha hisia kwa mabadiliko ya maana kubwa kama haya kana kwamba wasingejali kama mji wao unakuwa makao makuu ya Uislam au la!

(2). Madina ndio chimbuko la utamaduni na ustaarabu wa Kiislam. Mfano halisi wa maisha ya Kiislam uliweza kuonekana katika hali yake bora hapo Madina tu. Vita na mapambano ya kigeni vilikuwa vimeleta watu wa tamaduni nyingi tofauti katika milki ya Kiislam. Kama Madina ingekuwa pia ibakie kama makao makuu ya kisiasa na kiutawala ya dola hiyo, kama ilivyokuwa makao ya kiroho, basi watu wageni, na tamaduni zao ngeni na asili zisizo za Kiislam, wangeweza kuja kuishi ndani yake. Wenyewe wangeleta maadili, mila, tabia, desturi na ufuasi wa dini zao pamoja nao. Kwa kufanya hivyo, wangeweza ama kuumiliki ule utamaduni halisi wa Kiislam au wangeupunguza nguvu. Kwa vyovyote vile, Uislam halisi ungewekwa wazi nyakati zote kwenye athari za kigeni.

Joel Carmichael:

“Uislam uligongana na dhana kubwa sana za kiweledi za Kikristo, zilizojaa fikra za Greece na Roma. Mawazo ya Kikristo yaliingiza sio tu dhana nzima ya Kiyunani, bali pia na mawazo ya kawaida huko Uajemi na kwingineko katika Mashariki kongwe. Kwa sababu hiyo namna mbalimbali za mila na mawazo, ugumu muhumu wa mawazo na desturi, wote takriban ukiwa umekwisha meng’enywa (kurahisishwa) na Ukristo, ulipandikizwa kwa jumla kwenye ulimwengu mpya wa Kiislam.”
(The Shaping of the Arabs, New York, uk. 194, 1967)

Lakini Ali alihamisha kitovu cha kisiasa cha Kiislam kutoka Madina, na kwa hiyo akauokoa mtindo wa maisha wa Kiislam katika chimbuko lake hasa. Aliiokoa Makka na Madina kutokana na umililikiwaji wa kiutamaduni wa Wakristo, Wayahudi, Wagiriki, Warumi na Majusi. Alizidumisha sifa za miji hii miwili kama zilivyokuwa wakati wa Muhammad (s.a.w.w.), Mtume wa Allah swt., mwenyewe.

(3). Katika masuala mengi, makao makuu ya taifa pia yanakuwa makao makuu ya tabia mbaya, madhambi, uhali fu na maovu mengine. Babylon, Roma ya zamani na Byzantium (Istanbul), miji mikuu ya madola makubwa, ilikuwa pia sehemu za starehe za nyakati zao. Wanaume na wanawake wa mataifa yaliyotekwa wanatembelea miji hii mikubwa ya kifalme, na wanakuja pamoja na tabia zao mbaya. Ukuaji usiodhibitiwa, kujazana, na kutokujulikana kwa kutandawaa kwa vituo vya miji mikubwa huzaa maovu ya kila aina. Miji mikuu mingi ya kisasa inastahili kuchukua nafasi ya pili kwa Babylon na Roma kongwe.

Madina ilikuwa ndio kiini cha mafundisho ya Qur’an, na pia ilikuwa na kaburi la Muhammad, Mtume wa Allah swt., ndani yake. Muhammad alikuwa ndiye mfasiri wa Ujumbe wa Mwisho wa Allah swt. kwa wanadamu, na kazi yake ilikuwa ni kuwalika wanadamu kuishi maisha safi, ya kiungwana na sahihi. Uislamu ulikuwa ndio mjenzi wa tabia, uwezo wa hali ya juu, na hapakuwa na mfano bora wa maisha sahihi na yaliy- otakaswa kuliko maisha ya Mletaji wake. Kama Madina ingekuwa kama miji mikuu mingine ya kifalme ya hapo nyuma, basi mwaliko wa Uislamu kwa wanadamu waliobakia ungekuwa ni uvyosi (dhihaka). Ali ali uokoa utukufu wa Madina, na maadili ya kijamii ya ratiba ya kitabligh ya Kiislamu kwa kutenganisha vituo vya kiroho (au kidini) na vituo vya kisiasa vya dola.

Ali kwa kweli alikuwa ni mtu wa kiubashiri katika mawazo yake. Aliiokoa Madina kutokana na kugeuka kuwa mfano halisi wa Damascus au Baghdad au Cordova. Maonyesho makubwa ya ustaarabu yaliendelea kwa kasi sana huko Syria yakiendelezwa na kuzidishwa na himaya iliyokuwa ikipanuka kwa kasi. Utajiri wa zile nchi zilizotekwa ulimiminikia Damascus (na baadae, huko Baghdad na miji mingine). Pamoja na utajiri, kilikuja kiambatani chake – anasa – na tamaa ya tabaka linalotawala kutaka kukuza na kulea “sanaa.” Wasichana waimbaji na wachezaji walikuja kwenye vituo vya miji mikub- wa ya dola ya Waarabu kwa mmiminiko imara.
Wale wasomaji wanaotaka kuona mukhtasari wa tabia wa wakati wa ustawi wa himaya za Bani Umayya na Bani Abbas, wanaweza kufanya hivyo kwenye vitabu vingi sana, mion- goni mwavyo ni zile juzuu ishirini za Kitab al-Aghani cha Abul-Faraj Isfahani, au katika kitabu kingine kiitwacho The Ring of the Dove cha Imam Hazm wa Hispania, wote wakiwa vioo vya kuaminika vya nyakati zao.

A. J. Arberry:

“Dola hiyo iliendelea kuongezeka katika utajiri, jinsi biashara ilivyokwenda mbali zaidi; utajiri ulijikusanya mikononi mwa wale wachache walioushika, ambao walipenda utajiri ambao ungewashangaza wahenga wao wa Kibedui. Makasiri mazuri sana na yenye samani za kifahari – majumba yaliyopangwa yaliupamba mji mkuu Baghdad na vituo vya majimbo, Bokhara, Samarkand, Balkh, Shiraz, Damascus, Aleppo, Jerusalem, Cairo, Tripoli, Tunis, Fez, Palermo, Cordova. Maisha ya fahari na anasa (dolce vita) ya utawala wa makabaila mbaya unaopen- dezeshwa yanatoa taaswira kwa mng’aro kabisa, kama yalivyokuwa maisha huko Andalusia katika mkesha wa utekaji wa Uingereza wa Norman, katika The Ring of the Dove, kitabu cha muongozo chenye changamano sana juu ya mapenzi ya shujaa wa ukoo bora na mwanamke tajiri (aliyeolewa) kilichotungwa na mwanatheologia mashuhuri, Ibn Hazim. Wavulana watumwa na wasichana waimbaji, huduma zinazofanya maisha kuwa bora ambazo zilikuwa hazijulikani kwa Waarabu wa kale, ziliwapatia wanaume wa Kiislamu starehe mpya na washairi wakawapatia msamiati mpya. Mvinyo ulikatazwa kwa Waumini na katazo la wazi la Kitabu Kitukufu; lakini watawala wa Kiislamu walijiingiza kikamilifu, na mamanju wao walishindana kutukuza sifa za pombe (binti zabibu).
(Aspects of Islamic Civilization, uk. 15, 1967)

Ni lazima isidhaniwe, hata hivyo, kwamba ni ile miji ya mbali tu kama vile Cordova na Baghdad iliyochafuliwa na tabia mbaya za anasa na utajiri. Makka na Madina zenyewe hazikuwa salama kutokana na vivutio vyao.

Ella Marmura:

“Ushairi wa mada ya mapenzi ulipata ufafanuzi katika namna mbili tofauti. Moja ilikuwa ya kupendeza, yenye kufurahisha na ya kistaarabu, na hii ilimea katika miji ya Makka na Madina. Yote ilikuwa ni miji ya neema lakini iliyonyang’anywa mamlaka ya kisiasa. Wengi wa vijana makabaila wa Kiislamu ambao hawakuwa wameingizwa kwenye ofisi za umma, walifuja utajiri wao katika kutafuta starehe. Shule za uimbaji zilichipukia na kiasi cha ushairi wa hisia za mapenzi kilipangwa katika muziki. Kiongozi wa shule hii ya ushairi alikuwa ni Umar ibn Abi Rabiah (kafa mwaka 720), kabaila wa Makka. Namna ya pili ya ghazal – ushawishi wa ngono kwa wanawake ilistawi zaidi miongoni mwa Mabedui, ikielezea nguvu ya hisia na ikifafanua uchungu wote na kutokuwa na matumaini ya mapenzi ya kusikitisha.
(“Arabic Literature: a Living Heritage,” iliyochapishwa katika kitabu, Introduction to Islamic Civilization, kilichohaririwa na R. M. Savory, New York,1976)

Philip K. Hitti:

“Kusalimu amri kwa Makka kulimaanisha kukubali kwake Uislamu. Mmoja baada ya mmoja Makuraishi walihamia kwenye makao makuu mapya (Madina) kushiriki katika kuitangaza dini mpya na kuanza kazi mpya. Nafasi za juu kabisa ndani ya serikali na jeshi zilikuwa wazi kwa ajili yao. Makuraish wengi walishiriki katika mapambano ambayo katika kipindi cha imani halisi, hususan chini ya Umar ibn al-Khattab, yalisababisha kutekwa ile Ghuba yenye Rutuba, Uajemi na Misri. Baadae wengine walitumikia kama magavana wa majimbo katika milki iliyopatikana karibuni. Maisha hapo Makka kisha yakajengeka katika mikondo miwili tofauti, mmoja wa sham- rashamra na mwingine wa uchamungu.

Baada ya ushindi, ngawira, ushuru na kodi vilipata njia kwa wingi ndani ya mji; zikawa ni chanzo kipya cha mapato. Hii ilifidia sana hasara ya misafara ya biashara. Hijja, bila shaka, iliendelea; kwa kweli iliongezeka. Mwanzoni ikiwa kituo cha biashara, Makka sasa iligeuka kuwa kituo cha starehe. Watu wake waliopata utajiri hivi karibuni walileta wanawake maharimu wa Kiislamu, wacheza ngoma na waimbaji, wanaume kwa wanawake, na dhana mpya za ni nini kinachofanya maisha mazuri. Waliishi maisha ya kifahari katika majumba yenye mabustani na mazingira ambayo mfano wake, Makka haijawahi kamwe kuuona kabla ya hapo. (uk.21-22).
Wakati huohuo, maisha huko Madina, kama huko Makka, yalikuwa yanaendelea katika uelekeo tofauti, uelekeo wa hali ya kidunia. Hata hivyo, mtirirko wa dhahabu kutoka majimboni katika namna ya kodi ya kichwa na kodi ya ardhi ulimiminikia Madina kwanza. Kiwango kilichokuwa kinafurika kwenye hazina ya umma kilikuwa kikubwa mno.

Katika kutafuta kuungwa mkono na lile tabaka jipya la wanaotafuta starehe, Madina ilikuwa, juu ya mpinzani wake kwa upande wa kusini, na manufaa ya mwinuko mkubwa (kutoka usawa wa bahari), ugavi wa maji mzuri zaidi, na bustani zenye maeneo makubwa zaidi. Viongozi wastaafu wa serikali, watumishi wa serikali na jeshi, walileta watumwa na hawara zao, waimbaji wao, wachezaji na wanamuziki, waume kwa wanawake – na kuanzisha hali ya mazingira ambayo haijawahi kuonekana hapo kabla ndani ya Mji Mtukufu huo. (uk.55)” (Capital Cities of Arab Islam, 1973)

Hivyo ndivyo ilivyokuwa Madina hata baada ya hadhi yake ilipokuwa “imepunguzwa,” na ikawa imefanywa kuwa mji wa jimbo. Lakini ikiwa kama ingebakia kuwa makao makuu ya kisiasa na kibiashara ya dola hiyo ya Waislamu, ingekuwa, bila ya shaka, pia ndio makao makuu yao ya “burudani”, yakivuta sifa zote za Kibohemia za nyakati zao, katika kutafuta furaha za hisia.

(4). Qur’an Tukufu, Kitabu cha Allah swt., kilishushwa katika Kiarabu safi kabisa. Makka na Madina zilikuwa ndio chimbuko la Kiarabu cha Qur’an. Watu wanaozungumza lugha za kigeni na wanaoishi katika yale makao makuu ya wateka- ji wao, waliichafua lugha yao (lugha ya watekaji). Kama Madina ingebakia kuwa mji wa kifalme, kile Kiarabu cha Qur’an kingeweza, bila kuepukika, kupatwa na athari nyingi za kigeni. Maarifa ya Qur’an na ufafanuzi wake, na msamiati wake, hayakuweko katika mpango wowote katika karne ya kwanza ya Hijiria. Lakini ilikuwa ni muhimu kwa ajili ya kueleweka kwa Qur’an kwa kizazi cha wakati huo na vizazi vitavyofuata kwamba ile lugha ya Makka na Madina ibakie kama ilivyokuwa wakati wa Mtume (s.a.w.w.) ili kwamba maneno hayo ya Kiarabu yasije yakapata maana tofauti na zile zilizokuwa zikitumika katika wakati wake.

Lugha zote zinazoishi zinabadilika, na maneno yanabadilika maana zake. Kama kiumbehai chochote kinachoishi, maneno pia yanazali wa na vilevile yanakufa. Na kama kiumbehai kingine chochote kinachoishi, yanao uwezekano wa kuathiriwa na athari za kigeni na za kutoka nje. Mfano wake mzuri ni kule “kutohoa” Kiingereza cha kisasa. Kiarabu pia kingeweza “kutoholewa” lakini kiliokolewa kutokana na majaliwa haya na Ali ambaye alibadili muelekeo wa shughuli za wageni mbali na Madina. Yeye, kwa hiyo, ndiye mfadhili wa kwanza na mkuu sana wa lugha ya Kiarabu na sayansi za Qur’an.

(5). Watawala wa Bani Umayya wa Damascus waliishi kwa kuigiza wafalme wa Byzantium na Uajemi. Walikuwa wamejikusanyia wenyewe vifaa vyote vya anasa na ufuska ambavyo mamlaka yao yaliweza kuwatengenezea. Ule wepesi wa asili na usawa wa Uislamu vilikuwa vimetoweka kutoka Syria kama viliwahi kuwepo kamwe hapo mwanzoni. Ali, hata hivyo, alitaka kuwasilisha kwa ulimwengu mzima picha ileile ya Uislamu ambao Muhammad Mustafa aliiwasilisha kwa Waarabu huko Makkaa na Madina. Lakini ilikuwa ni picha ambayo majirani wa Syria na wengi wa Wasiryia wenyewe hawajawahi kuiona kamwe. Kwa kweli, katika miaka iliyofuatia, watawala wao walikuwa wawaonyeshe wao picha, sio ya Uislamu, bali picha dhidi ya Uislamu.

John Alden Williams:

“Wafalme wa Kiajemi wote, kutoka Ardashir mtoto wa Papak hadi Yazdagird, walijitenga binafsi na wajumbe wao kwa pazia. Safari moja nilimuuliza (yule mwanamuziki maarufu wa baraza) Ishaq ibn Ibrahim al-Mawsili: Je, wafalme wa Amawi walijionyesha kwa wajumbe wao na waimbaji?” Yeye akajibu, “Mu’awiyah na Marwan 1, Abd al-Malik, Walid 1, Suleiman, Hisham na Marwan II, walitenganishwa na wajumbe wao kwa pazia, hivyo kwamba hakuna mjumbe aliyeona kile alichokuwa akikifanya khalifa, kama alitekwa na muziki huo, au alitingisha mabega yake, au alicheza, au alitupa nguo zake, hivyo hakuna isipokuwa watumwa wake maalum ndio waliomuona. Na kwa makhalifa wa Amawi waliobakia, hawakuwa na aibu ya kucheza au kuvua nguo zao na kuonyesha nyuchi zao mbele ya wajumbe na waimbaji wao. Lakini kwa hilo, hakuna kati yao aliyekuwa kama Yazid ibn Abd al-Malik na Walid ibn Yazid kwa kutokuwa na haya na lugha chafu mbele ya wajumbe wao, na kuvua nguo zao, bila ya kujali walichokuwa wanakifanya.” (uk. 81) (Life at the Cali ph’s Court: kutoka kwenye Kitabu al-Taj, Cairo, 1914, uk. 5. Kisichokuwa na jina: kati ya 847 - 861 A.D. – Themes of Islamic Civilization, Berkeley, 1971)

Pale Ali alipofanya Kufa kuwa makao yake makuu, marafiki na maadui waliona kwa macho yao wenyewe ule Uislamu wa Muhammad (s.a.w.w.), Mtume wa Allah swt. Waliona kwamba mtawala halali wa Waislamu alifanya kazi kwa mikono yake mwenyewe katika mashamba na mabustani, na alijikimu yeye mwenyewe na familia yake kutokana na malipo aliyoyatokea jasho yeye mwenyewe. Waliona kwamba aliishi kwa mkate wa shairi mkavu lakini kila mtu mwingine katika milki yake alikuwa anakula vizuri. Waliona kwam- ba shati lake mwenyewe lilikuwa limefunikwa na viraka, raia zake walikuwa wakivaa vizuri. Waliona pia kwamba hakuwa na kasri la marumaru bali aliishi kwenye kibanda cha matope, na kwamba hapakuwa na askari wa zamu au doria mlangoni mwa nyamba yake, na kwamba alikuwa anafikiwa na kila mtu katika kila saa ya mchana au usiku.

(6). Kwa maslahi ya usalama wa Makka na Madina, Ali alitaka kuzifanya zisiwa maaru- fu kisiasa ili zisiweze kuvuta nadhari zisizohitajika. Mamlaka ya Mbinguni Duniani ambao Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) alikuwa ameuanzisha, ulikoma, baada ya kifo chake, kuwa wa “mbinguni,” na ulikuwa umegeuka kuwa serikali bandia ya Kigiriki au Kiajemi. Chini ya hali hiyo ya mabadiliko, hadhi na sifa ya utukufu ya miji hiyo pacha Makka na Madina zilikuwa siku zote katika hatari kubwa. Akizitabiri nyakati za mbele, Ali aliweka miji yote miwili nje ya mzunguko wa matukio ya kisiasa. Mwanawe mdogo, Husein, pia alikuwa na shauku hiyo hiyo ya kulinda utukufu wa mji wa babu yake. Yeye pia aliyaona mawingu ya mvua yakijikusanya kwenye upeo wa macho, na yeye pia aliondoka Makka, katika muda muafaka tu, kuondoa nadhari ya serikali mbali nayo.

Baada ya mauaji ya Karbala mnamo mwaka 680, ilikuwa ni ile miji mitukufu ya Kiislamu – Madina na Makka – iliyovuta akili ya Yazid, mtoto wa Mu’awiyah. Alimtuma jemedari wake, Muslim bin Aqaba, kwenda Madina pamoja na jeshi la Syria ambalo liliuwa raia 10,000 kwa ukatili. Waliokufa wali jumuisha masahaba wengi wa Mtume (s.a.w.w.). Madina ilitupwa kwenye ridhaa ya jeshi la wavamizi.

Msikiti Mkuu wa Mtume (s.a.w.w.) uligeuzwa kuwa zizi la wapanda farasi wa Syria. Wale wachache ambao walikuwa hawakuawa, iliwabidi wachukue kiapo cha utii kwa Yazid. Muslim bin Aqaba aliwaambia kwamba Yazid alikuwa ndio bwana wa maisha yao, na angeweza kuwauza kwenye utumwa, kama angetaka kufanya hivyo.

Alfred Guillaume:

“Kati ya kipindi kilichohusika na Sira na kuhaririwa kwa kitabu chenyewe inaji- tokeza ile misiba miwili ya Karbala, pale Husein na wafuasi wake walipouawa mnamo mwaka 61 H.A., na kule kutekwa nyara kwa Madina mnamo mwaka 63 H.A. wakati Ansari elfu kumi wakiwemo masahaba sio chini ya themanini wa Mtume walipouawa. (The Life of Muhammad, uk. xxvii, 1967)

Muslim bin Aqaba aliiacha Madina ikiungua taratibu na kuwa mabaki na kisha akaelekea Makka. Lakini alikufa kabla hajafika aendako, na uongozi wa vikosi vyake ukaenda kwa afisa mwingine wa Yazid, aitwaye Ibn Namir.

Huko Makka, Abdallah ibn Zubeir alikuwa amejitangaza mwenyewe kuwa khalifa. Ibn Namir aliushambulia mji huo kutoka kwenye vilima vinavyouzunguka na akaichoma Al-Kaaba. Lakini alikuwa hajaukamata mji huo bado wakati Yazid alipokufa huko Damascus. Mara baada ya hapo, ibn Namir akaacha kuuzingira na akaondoka kwenda Syria.

Lakini kile ambacho Makka na Abdallah ibn Zubeir walichokipata ilikuwa ni nafuu ya muda tu. Wakati Abdul Malik bin Marwan alipokuja kuwa khalifa, Makka kwa mara nyingine tena ikageuka uwanja wa vita. Jemedari wake, Hajjaj bin Yusuf aliizingira Makka, akaishambulia, na akabomoa sehemu ya Al-Kaaba. Abdallah bin Zubeir alichachamaa na kushikilia kwa miezi saba. Aliuawa katika maeneo ya Al-Kaaba, na mji ukasalimu amri kwa watekaji.

Philip K. Hitti:

“Katika mwaka 683 jeshi la Syria lilitumwa na Yazid dhidi ya mdai ukhalifa, Abdallah bin Zubeir. Muasi huyo alitafuta kimbilio kwenye ardhi isiyodhuriwa ya nyumba tukufu lakini hatahivyo alishambuliwa na Al-Kaaba ikashika moto. Lile Jiwe Jeusi lilikatika vipande vitatu.

Nyumba ya Allah, kwa maneno ya mwanahistoria mashuhuri, al-Tabari, “ilionekana kama kifua kilichochanika cha mwanamke mwenye huzuni.” (Capital Cities of Islam, 1973)

Ali alitafuta, kwa kubadilisha makao makuu, kuziokoa Makka na Madina kutokana na maangamizi ambayo yaliikumba licha ya juhudi zake za kinyume chake. Lakini basi ni nani mwingine katika ulimwengu wote wa Waislamu aliyeshiriki katika kuhusika kwake yeye na wanawe katika heshima na usalama wa miji hii miwili?

Pale Husein ibn Ali alipohisi kwamba hatari inaisogelea miji hiyo, yeye aliondoka haraka sana, na watu wote wa familia yake, kuelekea Iraq, ambako alijua, alikuwa na makutano na kifo. Lakini Abdallah bin Zubeir hakusita katika kukaribisha unajisi na uharibifu kwenye miji hiyo, na mauaji ya halaiki juu ya wakazi wake.

Ulimwengu wa Kiislamu bado unapaswa kukubali deni lake la shukurani kwa Ali kwa busara zake, busara zake na ubinadamu. Alivilinda vyanzo vya Uislamu katika uhai wake, na Alichukua hatua kwa ajili ya ulinzi wavyo baada ya kufa kwake. Hakuna njia nyingine yoyote ambayo angeweza kuiokoa Hijazi kutokana na kupatwa na mivurugiko hiyo, ghasia na kiwewe vilivyosababishwa na siasa na vita, isipokuwa kwa kuhamisha makao makuu kutoka Madina kwenda Kufa.

Wakati Ali alipobadilisha makao ya dola hiyo, Mu’awiyah alidhani kwamba alikuwa, hatimaye, amemkamata Ali akifanya jambo ambalo linaweza kuhojiwa, na alimwandikia kwamba yeye Ali alikuwa “ameutelekeza” mji wa Mtume – kitendo ambacho ni cha “kulaumika” sana kiasi kwamba hakiwezi kusameheka.

Miaka minne tu baadae, Mu’awiyah mwenyewe akawa ndiye mtawala wa juu kabisa wa dola ya Waislamu, na hapakuwa na mtu yoyote anayeweza kumuuliza juu ya kitendo chake chochote. Ikiwa kama alikuwa na mapenzi sana na mji wa Mtume kama alivyojifanya kuonyesha katika barua yake kwa Ali, angeweza kuufanya kuwa makao yake makuu. Lakini hakufanya hivyo wala hata mmoja kati wa warithi wake, wala hawakufanya hivyo makhalifa wa utawala wa Bani Abbasi.