read

Kugombea Madaraka – 3 Saqifah Banu Sa’ida

Bukhari amemnukuu Umar bin al-Khattab akisema: “Wakati yeye (Mtume (s.a.w.) alipofariki, Maansari walitupinga sisi. Walijikusanya ndani ya Saqifah Banu Sa’ida. Ali, Zubayr na marafiki zao pia walitupinga.”

Ni nini hicho ambacho Umar na marafiki zake walichokuwa wakikifanya, na ambacho Maansari walikipinga?

Wakati Mtume (s.a.w.) alipofariki, Maansari, siku zote wakiwa wepesi kuhisi mikondo ya kichinichini ya kisiasa, na wenye hofu na tamaa na dhamira za Muhajirina, walijikusanya katika ukumbi nje ya Madina unaoitwa Saqifah, na walimwambia Saad ibn Ubada, kiongozi wao, kile walichokijua juu ya mipango ya Muhajirina. Saad alikuwa mgonjwa na akamwambia mwanae, Qays, kwamba yeye alikuwa hakujihisi kuwa na nguvu za kutosha kuhutubia huo mkutano, na kwamba atamweleza alichotaka kukisema, na yeye Qays akakirudie kwa waliohudhuria. Saad akaongea na mwanae, naye akafikisha maana yake kwa Ansari.

Hotuba Ya Saad

“Enyi kundi la Ansari! Mnao umuhimu katika Uislamu ambao hakuna mtu anayeweza kuukataa, na hili peke yake linakufanyeni ninyi kuwa kitu maalum katika Arabia yote. Mtume wa Allah (s.a.w) alihubiri Uislamu miongoni mwa watu wake mwenyewe kwa miaka 13 na ni wachache wao tu walioukubali ujumbe wake. Walikuwa wanyonge sana kiasi kwamba walikuwa hawana uwezo wa kumlinda yeye au kutetea Uislamu. Allah (s.w.t.) katika baraka Zake alipendelea kuweka heshima ya kumlinda Muhammad (s.a.w.) juu yenu. Alikuchagueni ninyi mbali na watu wengine kutoa hifadhi kwa Mtume Wake na Waislamu wengine kutoka Makka. Aliridhia kuuimarisha Uislamu kupitia kwenu ili kwamba mpigane na maadui wa dini Yake.

Mmemlinda Mtume Wake kutokana na maadui zake mpaka ujumbe wa Uislamu ukaenea katika Arabia yote. Kupitia panga zenu ameiteka Arabia kwa ajili ya Uislamu, na ilikuwa ni kwa kupitia panga zenu kwamba wapagani wote walishindwa. Kisha wakati ukafika ambapo Mtume wa Allah (s.a.w) aliiaga dunia hii; alikuwa radhi juu yenu alipokuwa akienda mbele za Mola wake. Kwa hiyo, baada ya kifo chake, ni haki yenu kuitawala Arabia.”

Ansari walionyesha makubaliano ya pamoja na Saad, na wakaongeza kwamba kwa maoni yao, hapakuwepo na mtu aliyestahili zaidi yake kuwa mtawala wa Waislamu wote.

Ilikuwa ni wakati huu ambapo Abu Bakr, Umar na Abu Ubaidah ibn al-Jarrah, waliwasili ndani ya Saqifah. Pale Ansari walipowaona, mmoja wao – Thabit bin Qays – akasimama na kuwaambia kama ifuatavyo:

“Sisi ni waja wa Mungu, na ni wanusuru wa Mtume Wake (s.a.w.). Na ninyi, wakimbizi kutoka Makka, ni watu wachache tu. Lakini tunajua kwamba mnataka kuiteka Dola ya Madina, na mnataka kutuondoa sisi humo.” (Tabari na Ibn Athir)

Hii ni kauli yenye kufichua. Ina maana kwamba Muhajirina walikuwa wanapanga mipango ya kupora mamlaka, na ule mkusanyiko wa Ansari mle Saqifah ulikuwa ni jibu tu la mwanzo wa jambo lao.

Wakati Thabit bin Qays alipofanya ufichuzi huu, hakuna hata mmoja kati ya Muhajirina hawa watatu aliyempinga. Umar anasema kwamba pale Thabit bin Qays alipokaa chini, yeye alisimama na kuongea kitu kinachofaa. “Nilikuwa nimeandaa hotuba nzuri sana nikitarajia tu jambo kama hili,” alisema.
(Tarikh-ul- Khulafa).

Huku ni kukubali kwa Umar mwenyewe kwamba alikuwa amefanya maandalizi yaliyochanganuliwa kabla kukabiliana na dharura yoyote ile. Lakini Abu Bakr alimzuia, na yeye mwenyewe akasimama kuwahutubia Ansari.
Alisema: “Hakuna shaka kwamba Allah (s.w.t.) alimtuma Muhammad (s.a.w.) na Imani ya kweli na nuru ya dini Yake. Yeye (Muhammad) kwa hiyo, aliwaita watu kwenye dini ya Allah (s.w.t.) Tulikuwa wa kwanza kuitikia wito wake. Tulikuwa wa kwanza kuukubali Uislamu. Yeyote aliyesilimu baada yetu sisi, alifuata kutangulia kwetu. Zaidi ya hayo, sisi tuna uhusiano na Mtume wa Allah (s.a.w.w), na sisi ndio wenye sharafu kubwa zaidi ya Waarabu wote kwa damu na nchi. Hakuna kabila lisilotambua mamlaka ya Maquraishi, na nyie, Maansari, ndio mliotoa hifadhi na mliosaidia. Nyinyi ni ndugu zetu katika imani. Tunawapenda na kuwathamini ninyi kuliko watu wengine.

Lakini viongozi lazima wawe wanatoka kwa Maquraishi. Sisi tutakuwa ndio watawala na nyie mtakuwa mawaziri. Msione wivu juu yetu. Mmetusaidia sisi huko nyuma, na sasa hampaswi kuwa wa kwanza kutupinga sisi. Ninawaombeni mtoe viapo vyenu vya utii kwa mmoja wa hawa watu wawili, Umar au Abu Ubaidah. Nimewateua wote wawili kwa sababu hii; wote wanastahili heshima hii, na wote wana sifa zinazafaa kwa cheo cha Amir.”

Muhammad Husein Haikal:

“Umar na Abu Bakr walikuja kwenye uwanja wa Saqifah. Wakifuatiwa na idadi ya Muhajirina, walikalia viti vyao katika mkutano huo. Mara, mzungumzaji akasimama na kuwahutubia Ansari kama ifuatavyo: “Sifa zote na shukrani ni zake Allah (s.w.t.) Sisi ni Ansari, yaani Wasaidizi wa Allah (s.w.t.) na sisi ni jeshi la Uislamu. Ninyi, Muhajirina, ni watu wachache tu katika jeshi hilo. Hata hivyo, mnajaribu kutunyang’anya sisi haki yetu ya uongozi.”

Kwa kweli, kwa Ansari, lilikuwa ni lalamiko la siku nyingi, hata katika wakati wa uhai wa Mtume (s.a.w.). Sasa pale Umar alipolisikia tena, alichukia sana, na alikuwa tayari kulikomesha kwa upanga kama ikibidi kuwa lazima. Lakini Abu Bakr alimzuia na akamuomba kuwa muungwana. Yeye kisha akawageukia Ansari na akasema: “Enyi Ansari! Tunayo jadi na kizazi kitukufu sana. Sisi ndio tunaoheshimiwa sana na kutukuzwa mno na vilevile ndio tulio wengi sana katika kundi lolote ndani ya Arabia. Zaidi ya hayo, sisi ndio ndugu wa damu wa karibu sana wa Mtume (s.a.w.). Qur’an yenyewe imetoa upendeleo kwetu sisi. Kwani ni Allah (s.w.t.) Mwenyewe – Yeye ashukuriwe na atukuzwe – Ambaye amesema, Wa kwanza kabisa walikuwa ni Muhajirina, kisha Ansari, na kisha wale waliowafuata haya makundi mawili katika wema na uadilifu. Sisi ndio wa kwanza kuhama kwa ajili ya Allah (s.w.t.) na ninyi ni Ansari, yaani, Wenye kunusuru.

Hata hivyo, ninyi ni ndugu zetu katika imani, wen- zetu katika vita, na wanusuru wetu dhidi ya maadui. Yote mazuri mliyodai juu yenu ni ya kweli, kwani ninyi ndio wabora zaidi wa wanadamu. Lakini Waarabu hawataukubali uongozi wa kabila lolote isipokuwa la Quraishi. Kwa hiyo, sisi tutakuwa ndio viongozi, na nyie mtakuwa mawaziri wetu.” Kufikia hapa Ansari mmoja akasimama na akasema: “Kila uamuzi utategemea juu yetu sisi. Na uamuzi wetu sisi ni kwamba mnaweza kuwa na kiongozi wenu; sisi tutakuwa na wa kwetu.” Lakini Abu Bakr akasema kwamba kiongozi wa Waislamu lazima atokane na Quraish, na mawaziri kutokana na Ansari. Kufikia hapa aliishika mikono ya Umar na Abu Ubaidah na akasema: “Yeyote kati ya hawa watu wawili anazo sifa za kuwa kiongozi wa Waislamu. Chagueni mmoja kati yao.”
(The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Lakini Umar alisimama na akasema kwa kupinga: “Ewe Abu Bakr, sio sahihi kwa mtu yey- ote kupewa nafasi ya kwanza juu yako wewe kwa sababu wewe ndio mbora wetu sisi sote.Wewe ulikuwa ‘sahaba wa kwenye pango,’ na wewe ndiye ‘wa pili katika wawili.’ Na kuna yeyote aliyesahau kwamba Mtume (s.a.w.) alikuamuru kuongoza Swala wakati alipokuwa mgonjwa? Kwa hiyo, wewe ndiye mtu anayestahili zaidi kuwa mrithi wake.”

Ansari mwingine alisimama kuwajibu Abu Bakr na Umar, na akasema: “Tunatambua kutangulia kwenu katika Uislamu na sifa zenu nyingine, na tunawapenda pia. Lakini tunao wasiwasi kwamba baada yako, watu wengine wataitwaa serikali, na hawatakuwa wema na waadilifu kwetu. Kwa hiyo, tunashauri kwamba wawepo watawala wawili, mmoja Muhajir na mwingine Ansari (huu ulikuwa ufichuaji mbaya wa kwanza upande wa Ansari wa udhaifu wao wenyewe). Kama huyo Muhajir akifariki, nafasi yake ichukuliwe na Muhajir, na kama huyo Ansari akifariki, nafasi yake ichukuliwe na Ansari mwingine. Kama mkiukubali mpango huu, tutakupeni kiapo chetu cha utii. Huu ndio utaratibu mzuri ambao unaweza kufanywa kwa sababu kama Quraishi anakuwa ndio kiongozi pekee wa dola, Ansari wataishi kwa hofu, na kama Ansari anakuwa Khalifa, Maquraishi wangeishi kwa hofu.”

Abu Bakr akazungumza kujibu hivi: “Allah (s.w.t.) alimtuma Muhammad (s.a.w.) na Kitabu Chake kwa wanadamu. Wakati huo kila mmoja alikuwa akiabudu masanamu. Muhammad alipowaambia wayabomoe masana- mu hayo, wao walilichukia hilo. Hawakutaka kuyatelekeza. Kwa hiyo, Allah (s.w.t.) akawachagua Muhajirina kushuhudia Utume wa Muhammad (s.a.w.). Waarabu waliobakia waliwatukana na kuwatesa Muhajirin, lakini walikuwa imara katika msaada wao kwake. Walikuwa wa kwanza kumuabudu Allah (s.w.t.) na walikuwa wa kwanza kumtii Mtume Wake. Wana uhusiano naye, na wao ni ndugu zake. Kwa hiyo, wao peke yao wanastahili kuwa warithi wake, na hakuna mtu atakayewapinga katika hili isipokuwa madhalimu.

Nanyi, Enyi Ansari! Ni watu ambao ubora wenu haukanushiki. Hakuna mtu anayeweza kuishinda nafasi yenu ya juu katika Uislamu. Allah (s.w.t.) aliwafanyeni ninyi kuwa wanusuru wa dini Yake na Mtume Wake. Na ilikuwa ni kuelekea kwenu ambako alihamia. Kwa hiyo, cheo chenu katika Uislamu ni cha juu kabisa baada ya Muhajirin. Tunakupendeni na kukutukuzeni ninyi. Lakini inastahili tu kwamba viongozi watoke kwa Muhajirin na mawaziri kutoka kwa Ansari. Chochote tukachokifanya, tutakifanya kwa kushauriana nanyi.”

Mzungumzaji aliyefuatia alikuwa ni Hubab ibn al-Mundhir wa Madina. Alisema: “Enyi kundi la Ansari! Watu hawa (Muhajirin) wapo chini ya ulinzi wenu. Hawana mamlaka yoyote ya kuwapinga ninyi. Macho ya Waarabu wote yanakutazameni ninyi, na mnao utanguliaji ule ule katika Uislamu kama walionao. Wallah wao (Muhajirin) kamwe hawakuthubutu kumuabudu Allah (s.w.t.) hadharani mpaka mlipowapa hifadhi katika mji wenu. Hakuna mahali ambapo Swala iliswaliwa wazi-wazi isipokuwa kwenye mji wenu. Waabudu masanamu na washirikina hawakushind- wa ila kwa panga zenu. Kwa hiyo, uongozi ni haki yenu na wala sio yao. Lakini kama hawatakubaliana na hili, basi pawepo na viongozi wawili, mmoja kutoka kila kimoja kati ya vikundi hivi viwili.”

Umar alijibu hotuba ya Hubab ibn al-Mundhir kwa kusema:“Haiwezekani kwamba pawepo na wafalme wawili katika falme moja. Waarabu hawataukubali utawala wa mtu yeyote ambaye si wa kabila la Quraishi kwa vile Mtume wa Allah (s.w.t.) mwenyewe alikuwa mtu wa kabila hilo. Khalifa wa Waislamu kwa hiyo, lazima awe ni mtu wa kabila lile lile kama Mtume mwenyewe. Ule ukweli kwamba yeye alikuwa ni Quraish unakamilisha kabisa hoja yote. Sisi ni Maquraishi, na hakuna mtu yeyote atakayeweza kubishana nasi katika wajibu wetu wa uongozi.”

Hubab ibn al-Mundhir akasema tena: “Enyi Ansari! Msimsikilize mtu huyu na wenzie. Ukhalifa ni haki yenu. Uchukueni. Kama hawakubaliani na haki hii, wafukuzeni ndani ya mji wenu. Kisha mnachagua kiongozi kutoka miongoni mwenu wenyewe. Kile mlichokipata kwa panga zenu, msikitoe hicho kwa watu hawa, na kama mtu yoyote ananipinga mimi hivi sasa, nitamnyamazisha kwa upanga wangu.”

Abu Ubaidah ibn al-Jarrah ndipo akasimama, na akasema: “Enyi kundi la Ansari! Mlikuwa wa kwanza kumsaidia Mtume wa Allah, na kutoa hifadhi kwa dini yake. Je, mtakuwa ninyi wa kwanza sasa kusababisha msambaratiko katika dini ile?”

Mzungumzaji aliyefuatia alikuwa ni Ansari mwingine, ambaye ni Bashir bin Saad. Alijua kwamba Ansari walikuwa wamedhamiria kumchagua Saad ibn Ubada kama kiongozi wa umma wa Kiislam. Alikuwa na chuki na Saad na hakupenda kumuona yeye akiwa mtawala wa Arabia.

Kwa hiyo, alichokisema ndani ya Saqifah kilichochewa, sio na mapenzi na Abu Bakr au wale Muhajirin bali na chuki yake juu ya Saad. Alisema:

“Enyi kundi la Ansari! Bila shaka tuna kipaumbele katika Uislamu, na katika vita vya Kiislam. Lakini kwa vile ni hivyo, tusilazimike kuwa wabinafsi. Nia yetu iwe tu ni kutafuta radhi za Allah (s.w.t.) na kumtii Mtume Wake (s.a.w.). Huduma zetu kwa Uislamu zilikuwa ni kwa ajili ya Allah (s.w.t.) na sio kwa ajili ya manufaa ya dunia, na Yeye atakulipeni kwa ajili hiyo.

Kwa hiyo, tusijaribu kuwekeza juu ya huduma hizo sasa. Mtume wa Allah (s.a.w) alitokana na kabila la Quraishi; kwa hiyo, ni haki kwamba warithi wake wawe pia wanatokana na kabila hilohilo. Wanastahili kuwa warithi wake. Ukhalifa ni haki yao na sio yetu, na tusiwapinge katika jambo hili. Kwa hiyo, muogopeni Allah (s.w.t.) na msijaribu kuchukua kisichokuwa chenu.”
Hotuba hii ya Bashir bin Saad ilimtia hamasa Abu Bakr ya kusimama mara nyingine tena na kusema: “Kama nilivyosema kabla, viongozi wawe wanatokana na Quraishi. Kwa hiyo, Enyi Ansari! msisababishe mgawanyiko miongoni mwa Waislamu. Ni ushauri wangu kwenu kwamba mtoe kiapo cha utii kwa mmoja kati ya watu wawili hawa walioko hapa, Umar na Abu Ubaidah bin al-Jarrah. Wote wawili ni Maquraishi wanaostahili.”

Lakini Umar akamwingilia kati akisema, “Inawezekanaje kwamba mtu mwingine yeyote apokee kiapo cha utii wakati wewe upo miongoni mwetu. Wewe ndiye mtu mzima zaidi katika Quraishi, na umetumia muda mwingi zaidi pamoja na Mtume (s.a.w.) kuliko yeyote kati yetu.

Kwa hiyo, mtu yeyote asijiweke mwenyewe mbele yako. Nyoosha mkono wako ili nikupe kiapo changu cha utii.” Umar aliushika mkono wa Abu Bakr, na akauweka mkono wake juu yake kama ishara ya kiapo. Alikuwa, kwa kitendo hiki, amemthibitisha Abu Bakr kama khalifa. Abu Ubaidah bin al-Jarrah na Bashir bin Saad Ansari pia wakatokea mbele, wakaweka mikono yao juu ya mkono wa Abu Bakr, kiapo chao kwake.

Bashir bin Saad Ansari alikuwa akionyesha shauku sana katika kutoa kiapo cha utii kwa Abu Bakr. Hubab ibn al-Mundhir aliyekuwa anamtazama, akasema kwa sauti kubwa:

“Ewe Bashir! Wewe ni msaliti kwa watu wako mwenyewe. Tunajua ni kwa nini uliru- ka mbele kuchukua kiapo cha utii kwa Abu Bakr. Wewe unamchukia Saad ibn Ubadah, wewe haini mnyonge. Ni jinsi gani unavyochukia kumuona yeye akiwa Amir wa Waislamu.”

Ilikuwa ni katika wakati huu wa maamuzi ya hatma ambapo wengi wa watu wa makabila ya Kibedui ambao waliishi kati ya Madina na Makka walijitokeza uwanjani. Walikuwa na uadui na Ansari, na walikuwa wameingia hapo mjini waliposikia habari za kifo cha Mtume wa Allah (s.a.w.w) Walipong’amua kile kinachopikwa pale Madina, walijitawanya karibu na Saqifah.

Kutokeza kwao kwa ghafla kuliongeza nguvu nyingi sana kwenye hamasa ya Abu Bakr na Umar; na kwa wakati huo huo, kulitia mawimbi juu ya uhakika wa Ansari. Watu hawa wa makabila walikuwa wote wana silaha. Kwa kutokea kwao, nguvu ya ushawishi katika ule mjadala mrefu kati ya Muhajirin na Ansari, ikaenda kwa Muhajirin.

G .E . Von Grunebaum:

“Katika kipindi cha vurugu Ansari hatimae walishawishika kutong’ang’ania juu ya urithi kwenda kwa mmoja wa watu wao wenyewe wala juu ya watawala wawili wa Sahaba na Msaidizi, na kwa kiasi fulani chini ya shinikizo kutoka kwa Mabedui ambao walikuwa wanamiminika kuingia ndani ya mji huo, walikubali kufanya heshi- ma kwa Abu Bakr.” (Classical Islam – A History 600 – 1258)

Umar alisema baadae kwamba mpaka walipotokea wale watu wa makabila, alikuwa na mashaka makubwa kuhusu matokeo ya ule mjadala na Ansari.

Kutokea kwao katika muda muafaka, na matumizi yao ya shinikizo juu ya Ansari, kulihakikisha makubaliano ya hawa Ansari katika kufika kwa Abu Bakr kwenye kiti.

Hila ya Bashir ilishinda. Aliihujumu ile nia ya – kupigana ya Ansari. Malalamiko ya Saad ibn Ubada na Hubab ibn al-Mundhir hayakuwa na mafanikio yoyote.

Wakati Umar, Abu Ubaidah na Bashir walipotoa kiapo cha utii kwa Abu Bakr, wengine wote walifuata kama kondoo.

Ansari walikuwa wameshindwa mapambano!

Ufumbuzi wa mafanikio ya Abu Bakr katika kuchaguliwa khalifa hapo Saqifah ulikuwa ni ule uadui wa pamoja wa yale makabila mawili ya Madina ya Aus na Khazraj. Yote yalikuwa yamepigana “Vita vya Miaka Mia Moja” vya wenyewe kwa wenyewe, na walikuwa wamesimamisha uhasama wao kwa sababu tu ya kuchoka kwao kimwili.

G .E . Von Grunebaum:

“Hawa Aus na Khazraj walikuwa hali ya kuendelea katika vita vya msituni dhidi yao kwa vizazi na vizazi. Ugomvi wao ulifikia kwenye kilele cha kumwaga damu mnamo mwaka 617 katika “Vita vya Bu’ath,” ambavyo baada yake wahusika wakuu walichoka sana kiasi kwamba ilififia mpaka kwenye mapatano ya kusimamisha vita, yaki- ingiliwa tu na vitendo vya kisasi vya mara kwa mara.
(Classical Islam – A History 600 – 1258)

Vita vya mwisho vikubwa kati ya Aus na Khazraj vilikuwa vimepiganwa miaka minne tu kabla ya kutokea kwa Mtume (s.a.w.) hapo Madina kama Mpatanishi. Mara tu wote walipomkubali yeye kama kiongozi wao, walikubaliana pia kuridhia kwenye maamuzi yake katika migogoro yao yote, na walifanya makubaliano ya kusitisha mapambano kwenye vita vyao visivyokwisha. Lakini mara tu yule Mpatanishi na hakimu alipokufa, chuki zao za zamani, hofu na wasiwasi viliwaka moto tena. Pale viongozi wa Aus walipoona kwamba Khazraj walikuwa wamemtoa Saad ibn Ubada – Mkhazraji – kama mgombea wa ukhalifa, walifikiria kwamba kama atachaguliwa kuwa khalifa, basi wao – Aus – watashushwa mpaka kwenye hadhi ya utwana kwa wakati wote. Maslahi yao, waliona, yatalindwa vema kama kiongozi wa umma angekuwa ni Muhajir kutoka Makka badala ya Khazraj wa Madina.

Wao kwa hiyo, wakaharakisha kumhakikishia Abu Bakr kwamba walikuwa watiifu kwake kabla Khazraj hawajaweza kumtangaza Saad ibn Ubadah kama mkuu mpya wa Madina. Ilikuwa kwa hiyo ni Aus wa Madina ambao walikuwa hasa wamesaidia katika kupatikana kwa mafanikio ya Abu Bakr katika kuchag- uliwa kwake kama khalifa. Vipengele vingine, kama vile usaliti wa Bashir bin Saad, mwenyewe akiwa Khazraj, kwa kabila lake mwenyewe, la Khazraj; na uingiliaji wa watu wa kabila la Kibedui katika wakati mgumu, pia vilichangia mafanikio ya Abu Bakr.

Maxime Rodinson:

“Watu wa Madina, hususan wale wa kabila la Khazraj, walihisi kwamba Wahamiaji wa Kiquraishi ambao walikuwa wamekuja pamoja na Muhammad (s.a.w.) ambao walikuwa siku zote wakiwaonea wivu, sasa watajaribu kudai uongozi juu yao wenyewe. Mtume (s.a.w.) alikuwa amekufa. Hapakuwa na sababu tena ya kuendelea kuwatii hawa wageni. Waliitisha mkutano katika ukumbi wa moja kati ya koo zao - Banu Sa’ida, kuzungumzia njia bora ya kulinda maslahi yao. Walichoshauri kufanya kilikuwa ni kuchagua mmoja wa watu wao maarufu, Sa’d ibn Ubadah, kama Kiongozi mpya wa Madina.

Abi Bakr alikuwa katika nyumba ya Muhammad (s.a.w.), alidokezwa juu ya hili na akakimbilia kwenye sehemu hiyo pamoja na wanasiasa wenzie, Umar na Abu Ubaidah. Waliungana humo njiani na kiongozi mwingine wa kabila jingine la Madina, la Aus, mahasimu wa Khazraj. Jambo la mwisho kabisa walilotaka lilikuwa ni kuona madaraka yakiwa kwenye mikono ya Khazraj. Mitaani humo msisimko ulikuwa unaenea kwa watu wa makabila mengine ya Madina, ambao walikuwa hawana tamaa ya kushika nafasi ya ukibaraka katika mchezo wowote wa madaraka ambao ulikuwa karibu uanze.

Usiku ulipoingia, kila mtu alikuwa amesahau ule mwili (wa Mtume (s.a.w.)) uliokuwa bado umelala katika kibanda kidogo cha Aishah (ingawa – la kibanda - si sahihi).

Majadiliano yaliyoendelea kwa mwanga wa tochi na taa za mafuta, yalikuwa marefu, makali na yenye rabsha. Mtu mmoja wa Madina alishauri kwamba wangechaguliwa viongozi wawili, mmoja Quraishi na mmoja wa Madina. Watu wengi walitambua kwamba hiyo itakuwa ni njia ya kukaribisha ugomvi na balaa juu ya jamii. Kila mmoja alikuwa anapiga kelele kwa wakati mmoja; wangeweza hata kufikia kupigana.” (Muhammad, tafsiri ya Ann Carter, 1971)

Walifikia kupigana. Saad ibn Ubadah alimkamata Umar kwenye ndevu zake. Umar ali- tishia kumuua yeye kama angeng’oa unywele mmoja toka kwenye ndevu zake. Umar akamwambia Hubab ibn al-Mundhir: “Allah akuuwe wewe,” naye huyu akamwambia: “Allah akuuwe wewe.”

Hubab ibn al-Mundhir alifanya juhudi kubwa kuokoa hali hiyo. Alipojaribu kuwazuia Ansari kutoa kiapo cha utii kwa Abu Bakr, kundi moja likamvamia, likampokonya upan- ga wake, na likamsogeza pembeni.

Walikuwa ni Mabedui wanaowaunga mkono Muhajirin. Hubab alikosa upanga wake lakini bado alizipiga nyuso za wakazi wa Madina ambao walikuwa wakitoa kiapo cha utii kwa Abu Bakr. Aliwalaani na kusema: “Enyi Ansari! Naweza kuona kwa macho yangu mwenyewe kwamba watoto wenu wanaomba chakula kwenye milango ya nyumba za hawa watu wa Makka lakini badala ya kupata chakula wanapigwa kwenye meno na watu hawa, na wanafukuzwa.”

Abu Bakr akamuuliza Hubab: “Unawazia hofu kama hizo kutoka kwangu mimi?” Akasema: “La. Sio kutoka kwako bali kutoka kwa wale watakaokuja baada yako.” Akijaribu kumhakikishia, Abu Bakr akasema: “Kama hilo likitokea, mnaweza wakati wote kukana kiapo chenu kwa makhalifa wenu.” Yeye kwa uchungu akajibu kwa ukali sana: “Itakuwa tumekwisha kuchelewa sana wakati huo, na haitasaidia chochote.”

Ulikuwa ni mkutano huu wa fujo, wa kiajabu ajabu na usio na mpangilio, wa ndani ya ukumbi wa Saqifah ambao ulimchagua Abu Bakr kama khalifa. Ansari hawakuridhika sana na kuchaguliwa kwake. Wao kwa hali yoyote ile, hawakuteua mtu anayestahiki-sana. Umar kwa ustadi sana aliliweka kando suala la sifa-stahilifu, na kamwe hakuliruhusu liibuke ndani ya mjadala huo. Suala la sifa za mgombea lilifunikwa chini ya wingu la ufasaha wa kukwepa kwepa.

Saad ibn Ubadah, kiongozi wa Khazraj, na “mshindi wa pili” ndani ya Saqifah ambamo mbinu-zote-zinakubaliwa na huru kwa watu wote, alikuwa mmoja wa wale watu ambao walikataa kula kiapo cha utii kwa Abu Bakr. Alimwambia Abu Bakr: “Ewe Abu Bakr! Kama nisingekuwa kwenye hali hii ya kutokujiweza kwa sababu ya maradhi yanayonid- hoofisha, ningekurudisheni Makka wewe na marafiki zako, kwa ndugu zenu wenyewe.” Saad kisha akawaomba marafiki zake wamtoe nje ya Saqifah. Kwa muda fulani Abu Bakr hakumuingilia yeye, na kisha siku moja akamtumia ujumbe akimtaka aje kutoa kiapo cha utii. Saad akakataa. Umar akamshinikiza Abu Bakr achukue kiapo chake kwa nguvu.

Lakini Bashir bin Saad Ansari akaingilia kati kwa kusema: “Saad akiwa amekwisha kataa, kamwe hatokupeni kiapo chake cha utii. Kama mkimlazimisha yeye, inaweza kusababisha umwagaji wa damu, na watu wa Khazraj wote watasimama pamoja naye dhidi yako. Kwa maoni yangu mimi, haitakuwa busara kulazimisha jambo hili. Yeye, hata hivyo, ni mtu mmoja tu, na akiachwa alivyo, hawezi kufanya madhara yoyote kwa namna yoyote ile.”

Wale watu wote waliokuwepo kwenye lile baraza la khalifa, waliyaunga mkono maoni ya Bashir, na Saad aliachwa kwa amani. Alipona maradhi yake, na miaka mitatu baadae, aka- hama kwenda Syria.

Maandishi ya hotuba zilizotolewa pale Saqifah, na maelezo juu ya matukio yaliyotokea pale, yamechukuliwa kutoka kwenye vitabu vifuatavyo:

1. Tarikh – Tabari
2. Tarikh al-Kamil – Ibn Athir
3. Kitab-al-Imama was-Siyasa – Ibn Qutayba Dinwari
4. Siraat-ul-Halabiyya – Halaby