read

Kugombea Madaraka 4

Wakati Abu Bakr alipokubaliwa kuwa khalifa pale saqifah, yeye, Umar bin al-Khattab na Abu Ubaidah bin al-Jarrah walirudi kwenye Msikiti wa Mtume (s.a.w.). Ndani ya Msikiti mlikuwa na watu wengi, miongoni mwao, watu wa ukoo wa Bani Umayya; Saad bin Abi Waqqas; Abdur Rahman bin Auf; na baadhi ya Muhajirina wengine.

Alipowaona wamekutana faragha kwenye kundi moja. Umar alisema kwa sauti: “Abu Bakr amechaguliwa kuwa khalifa wa Waislamu. Sasa nyie wote hapa mpeni kiapo cha utii. Ansari, Abu Ubaidah na mimi tayari tumekwisha fanya hivyo.”

Bani Umayya waliokuwepo mle ndani ya Msikiti walikuwa wa kwanza kuitika mwito wa Umar, na kuchukua kiapo cha utii kwa Abu Bakr. Saad ibn Abi Waqqas, Abdur Rahman bin Auf na wengineo waliwafuatia hao, na wakachukua kiapo cha utii kwa Abu Bakr.
Takriban “mamwinyi” wote walichukua kiapo cha utii kwa Abu Bakr siku ya Jumatatu. Wale “watu wa kawaida” hawakujua kuhusu kuchaguliwa kwa Abu Bakr bado. Walikuja pale Msikitini siku ya Jumanne. Kutwa nzima walikuwa wakija na kuingia na kutoka nje ya Msikiti, na Abu Bakr alikuwa akishughulika kupokea viapo vyao vya utii kwake. Ilikuwa tu siku ya Jumatano ambapo hatimae alikuwa huru kushughulikia mambo mengine.

Wakati huohuo, muda wote wa kinyang’anyiro kikali cha madaraka ndani ya Saqifah, na baadae, Ali ibn Abi Talib na watu Bani Hashim, walikuwa wakishughulikia mazishi ya Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.). Pale Mtume alipokuwa amekwishafanyiwa mazishi, Ali na Bani Hashim walirudi majumbani kwao.

Watu wengi hapo Madina walikuwa wamekwisha kuchukua kiapo cha utii kwa Abu Bakr lakini walikuwepo wengine ambao walikuwa bado. Muhimu sana miongoni mwao wote alikuwa ni Ali ibn Abi Talib, kiongozi mpya wa ukoo wa Bani Hashim. Khalifa mpya na washauri wake waliamini kwamba ilikuwa ni muhimu sana kwamba Ali achukue kiapo cha utii sawa na watu wengine.

Wao, kwa hiyo, walituma aitwe kutoka nyumbani kwake lakini alikataa kuja. Kukataa kwake kulimkasirisha Umar. Mapema kidogo, alikuwa mtu mwenye kuathiri uteuzi, lakini sasa amekuwa Mtendaji Mkuu wa serikali mpya ya Saqifah.

Yeye, kwa hiyo, alikwenda pamoja na wasindikizaji wenye silaha kutekeleza amri za serikali, na akatishia kuichoma nyumba ya binti ya Muhammad Mtume wa Allah (s.a.w.), kama Ali asingekuja kwenye baraza kuchukua kiapo cha utii kwa Abu Bakr. Mtu mmoja alikumbusha kwamba nyumba ile ilikuwa ni mali ya binti ya Mtume (s.a.w.), hivyo Umar angewezaje kuichoma. Lakini Umar akasema haidhuru kama nyumba hiyo ilikuwa ni ya mtoto wa Mtume (s.a.w.). Kilichokuwa na umuhimu hasa, alisisitiza, ni kiapo cha utii ambacho Ali alipaswa akichukue.

Edward Gibbon:

“Bani Hashim peke yao walikataa kiapo cha utii (kwa Abu Bakr); na kiongozi wao (Ali), katika nyumba yake mwenyewe, alidumisha zaidi ya miezi sita (ingawa sio kweli), kimya kizito na cha upweke, bila ya kupatiliza vitisho vya Umar, ambaye alijaribu kuyachoma kwa moto makazi ya binti ya Mtume (s.a.w.).” (The Decline and Fall of the Roman Empire)

Hata mtu kama Shibli, mwandishi wa wasifu wa Umar, na mmoja wa washabiki wake wakubwa sana, amelazimika kukubali kwamba “Umar alikuwa mtu mwenye hasira mbaya sana, na haishangazi kabisa kama alifanya jaribio la kuchoma moto nyumba ya binti ya Mtume (s.a.w.).” - (Al-Faruuq)

Uzuri ulioje, utamu ulioje, na ujasiri ulioje wa Umar kujaribu kuchoma nyumba ya Fatima Zahra!

Siku tatu baada ya kifo cha Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Mwisho wa Allah (s.a.w.w) kwa wanadamu, Umar alifika mlangoni mwa nyumba ya Fatima Zahra. Kundi lingine la wachomaji moto mali wa maksudi lilikuwa pamoja naye, na alidai kiapo cha utii cha Ali kwa Abu Bakr.

Uonyeshaji huu wa “ushujaa” lazima utakuwa “umemfurahisha” sana Allah (s.w.t.) hasa, pale mtu anapokumbuka kwamba mbali na Ali na Fatima, walikuwemo pia ndani ya nyum- ba yao, watoto wao wadogo wanne – wajukuu wa Muhammad Mustafa (s.a.w.). Walipishana kwa umri kutoka miaka miwili hadi nane. Watoto hao lazima watakuwa “wal- isisimka” kusikia sauti ya Umar. Kwao wao, lazima alikuwa kama mfano wa “Santa Claus,” (Baba Chrismas) - Santa Claus huyo wa jangwani, akiwa amesimama mlangoni mwa nyumba yao akiwa na “zawadi” ya moto kwa ajili yao. “Zawadi” yake, huenda atakuwa amewaeleza, ilikuwa na nguvu ya kubadili zile kuta za kijivu zisizovutia za nyum- ba yao ndogo kuwa ndimi za moto zinazoruka na kualika alika zenye rangi nyingi.

Kipi tena angewafanyia hao ili “kuwaliwaza” na “kuwafariji” baada ya kifo cha babu yao, Muhammad (s.a.w.), ambaye alikuwa akiwapenda sana? Hivi wamekwishawahi kamwe kuona kioja cha “fataki” yenye kumeremeta kupita kiasi kama hicho anachoweza kuwaonyesha punde hivi tu kama baba yao, Ali ibn Abi Talib, hakuchukua kiapo cha utii kwa Abu Bakr?

Kwa wakati huu, Zubayr ibn al-Awam alikuwa pia pamoja na Ali. Mke wake alikuwa mmoja wa mabinti wa Abu Bakr lakini mama yake yeye alikuwa ni Safiyah bint Abdul Muttalib, shangazi yake Muhammad (s.a.w.) na Ali. Yeye, kwa hiyo, alidai kwamba na yeye pia alikuwa mtu wa ukoo wa Bani Hashim.

Umar alimuamuru kuchukua kiapo cha utii kwa Abu Bakr. Lakini alikataa na kutishia kutumia upanga wake kama atasumbuliwa sana. Umar aliwakemea vibaraka wake wanyakue upanga wake. Walifanikiwa katika kumzidi nguvu. Alinyang’anywa silaha, na akapelekwa kwenye baraza la baba-mkwe wake. Ilikuwa ni katika hali hii kwamba alitoa kiapo chake cha utii kwake.

Umar alijaribu kupata nguvu kwa vitisho, kufoka – kwa kiburi, na udanganyifu. Zamani, mtu alikuwa anaweza kutaja udanganyifu wake lakini sasa ilikuwa haiwezekani kufanya hivyo. Pamoja na Zubayr kumalizwa hivyo, Umar aligeuzia mazingatio yake kwa Ali, na alipelekwa kule kwenye baraza. Humo ndani ya baraza, Umar alirudia dai lake la kiapo lakini Ali akasema:

“Mimi ni mtumwa wa Allah (s.w.t.) na ni ndugu yake Muhammad, Mtume Wake. Mtumwa wa Allah (s.w.t.) hawezi kuwa mtumwa wa mtu mwingine yeyote. Kama mmefanikiwa katika kuiteka serikali ya Muhammad (s.a.w.) kwa sababu ninyi, kama ulivyosema, ninyi mpo karibu zaidi kwake kuliko Ansari, basi mimi ni mdogo wake, na ni nani miongoni mwenu ambaye anaweza kudai kuwa karibu naye zaidi kuliko mimi? Waislamu wote wanapaswa kunipa mimi viapo vyao, na sio mtu mwingine yeyote.

Mnainyang’anya familia ya marehemu bwana wenu haki yao. Mliwashawishi Ansari kwa hoja kwamba Mtume wa Allah (s.a.w.w) alikuwa ni mmoja wenu, na hakuwa mmoja wao, na waliuachia ukhalifa kwenu. Sasa naitumia hoja hiyo hiyo – hoja yenu – ambayo mliitumia dhidi ya Ansari. Sisi ndio warithi wa Mtume wa Allah (s.a.w.w) katika uhai wake na baada ya kifo chake. Kama mnauamini ujumbe wake, na kama mmeukubali Uislamu kwa uaminifu, basi msizichukue kwa nguvu haki zetu.”

Umar alimjibu hivi: “Wewe ni mtumwa wa Allah (s.w.t.) lakini sio ndugu yake Mtume Wake (s.a.w.). Kwa hali yoyote, itakubidi utoe kiapo cha utii kwa Abu Bakr, na hatutakuachia hapa mpaka umefanya hivyo.”

Ali akasema: “Ewe Umar! Kama unatetea suala la Abu Bakr kwa shauku kubwa namna hiyo, hilo linaeleweka. Leo unamfanya mfalme ili kwamba kesho akufanye wewe kuwa mfalme. Mimi sitafanya kile unachonitaka nifanye, na sitampa kiapo changu.”

Abu Ubaidah ibn al-Jarrah alikuwa mwanachama wa “kundi la watu watatu” (troika), na kwa hiyo, alikuwa wakili mkali wa serikali ya Saqifah. Yeye pia alifanya jaribio la kumshawishi Ali kuitambua ile serikali mpya, na kuchukua kiapo cha utii kwa kiongozi wake. Alisema:

“Ewe binamu ya Mtume (s.a.w.)! wewe ni mdogo kuliko watu hawa. Wao ni wakubwa sana kuliko wewe na wanao uzoefu mkubwa kuliko ulionao wewe. Inakubidi uchukue kiapo cha utii kwa Abu Bakr sasa hivi, na kisha, siku isiyo na jina, zamu yako inaweza kuja pia. Unastahili kuwa kiongozi wa Waislamu kwa sababu ya utan- guliaji wako kwenye Uislamu, ushujaa wako, ujuzi wako, elimu yako, na utumishi wako kwenye Uislamu. Na kisha wewe ni mkwe wa Mtume wetu.”

Ali alimjibu kama ifuatavyo: “Enyi Muhajirin! Msiyatoe madaraka na mamlaka ya Mtume wa Allah (s.a.w.w) nje ya nyumba yake kwenda kwenye majumba yenu. Wallahi, urithi wa Muhammad (s.a.w.) ni haki yetu sisi. Yeye mwenyewe alitoa tamko hili, na sio mara moja bali mara nyingi tu. Hivi yupo mtu kati yenu ambaye ana ujuzi mzuri na uelewa wa Qur’an kuliko nilionao mimi? Yupo yeyote miongoni mwenu ambaye anayo elimu nzuri ya vitendo na Hadith za Mtume wa Allah (s.a.w.w) kuliko niliyonayo mimi? Yupo yeyote kati yenu ambaye anaweza kuiendesha serikali yake vyema kuliko mimi niwezavyo? Kama yupo, mtajeni, na mimi nitamstahi yeye. Lakini hayupo. Ni mimi tu niwezaye kutoa amani ya kweli, ustawi na haki ya kweli kwa Waislamu wote. Kwa hiyo msiangukie kwenye vishawishi vyenu, na msiweke tamaa na mapenzi yenu wenyewe mbele ya amri za Allah (s.w.t.) na Mtume Wake (s.a.w.). Na kama mkifanya hivyo, mtapotoka kwenye Haki, na mtaangukia kwenye Upotovu.”

Bashir bin Saad, yule yule aliyekuwa Ansari wa kwanza kuchukua kiapo cha utii kwa Abu Bakr ndani ya Saqifah, alikatisha hotuba ya Ali, na akasema: “Ewe Ali! Kama ungetuambia hayo kabla, sisi tusingekuwa tumempa kiapo cha utii mtu yeyote badala yako wewe.”
Ali akamwambia: “Wewe ulikuwa huyajui yote haya? Unachojaribu kushauri ni kwamba kama vile wote nyie mlivyomtelekeza Mtume wa Allah (s.a.w.w) mara tu alipofariki, mimi pia ningemtelekeza, na mimi pia ningeingia Saqifah kugombea ukhalifa pamoja nanyi? Hili nisingeweza kulifanya. Kufanya hivyo kusingestahili kabisa kwangu mimi. Nisingeweza kumtoroka Mtume wa Allah (s.a.w) katika kufa kwake kama nisivyomtoroka wakati wa uhai wake.”

Baada ya maelezo haya, Ali alitoka kwenye baraza ya Abu Bakr iliyokuwa imeendeshwa kwenye Msikiti wa Mtume (s.a.w.). Hizo ndizo zilikuwa mbinu za kuchaguliwa kwa Abu Bakr kama khalifa wa Waislamu – mfululizo wa ufaraguzi wa kuwa tayari kufanya lolote, na mara nyingi wenye misukosuko.

Wakati wa kuchukua viapo kwa faragha ndani ya Saqifah, na vile vya hadhara ndani ya Msikiti wa Mtume (s.a.w.), kulipokamilika, Abu Bakr, khalifa mpya, akatoa hotuba yake ya uzinduzi. Baada ya kumshukuru Allah (s.w.t.) na kumtukuza, alisema:

“Enyi Waislamu! wale kati yenu waliokuwa wakimwabudu Muhammad, basi nawajue kwamba amekufa; lakini wale kati yenu waliokuwa wakimwabudu Allah (s.w.t.) nawajue kwamba Yeye yuko Hai, na hatakufa kamwe.

Enyi Waislamu! Ingawa mmenichagua mimi kama kiongozi wenu, mimi sio mbora sana miongoni mwenu.

Kama mtu mwingine angechukua dhima ya mzigo huu ambao mmenitwisha mimi, ingekuwa bora sana kwangu. Kama mnanitegemea niwatawale kama vile tu Mtume wa Allah (s.a.w) alivyofanya, basi lazima niwaambie kwamba hiyo haiwezekani. Mtume (s.a.w.) alipokea Wahy kutoka Mbingnii, na alikuwa asiyetekosea (maasum) ambapo mimi ni mtu wa kawaida tu. Mimi sio bora kuliko ninyi.

Kwa hiyo, kama mkiniona ninakwenda katika njia iliyonyooka, nifuateni; lakini kama mnaniona nikiikengeuka, nishutumuni. Kama nikifanya sawa, niungeni mkono; kama nikifanya makosa, nisahihisheni. Nitiini mimi pale tu nitakapokuwa ninamtii Allah (s.w.t.) na Mtume Wake (s.a.w.). Lakini kama mkiniona ninawakiuka wao, nanyi pia mniepuke.

Mnayo Qur’an pamoja nanyi, na imekamilika. Mtume wa Allah (s.a.w) amekuonyesheni kwa maagizo na kwa mifano pia namna ya kujiweka nyie wenyewe katika maisha haya. Mwenye nguvu zaidi miongoni mwenu ni yule anayemuogopa Allah (s.w.t.) Mdhaifu sana miongoni mwenu mbele ya macho yangu ni yule mwenye-dhambi. Taifa linaloacha jihadi, linapoteza hadhi yake. Salini Swala zenu kwa wakati makhsusi, na msizikose. Allah (s.w.t.) awe na huruma juu yenu, na Akusameheni ninyi wote.”

Hotuba ya khalifa mpya ilikuwa ni ya maelezo ya malalamiko-binafsi kweli, porojo lisilo na dhamira maalum, isiyotia moyo au umaizi. Kauli ya mwanzo, hata hivyo, ilikuwa na maana. Aliwaambia Waarabu kwamba kama walikuwa wakimuabudu Muhammad (s.a.w.), amekufa! Hivi kuna Waarabu wowote waliomuabudu Muhammad? Kwa miaka 23, Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Allah (s.a.w) aliyebarikiwa, alikuwa akilifundisha somo la Tauhid (Mungu mmoja) liingie kwenye vichwa vya Waarabu. Ikiwa baada ya juhudi kubwa namna hiyo, walianza kumuabudu yeye badala ya kumuabudu Allah (s.w.t.) basi kazi yake yote kama Mtume, lazima iamuliwe kwamba ilishindwa kabisa.

Lakini ujumbe wa Muhammad (s.a.w.) haukuwa kazi bure. Waislamu walimuabudu Allah (s.w.t.) na hawakumuabudu Muhammad. Wao, kwa hakika, walirudia mara nyingi kwa siku kwamba Muhammad alikuwa ni mtumwa wa Allah (s.w.t.) na Abu Bakr alilijua hili. Hivyo ni kwa nini aliona umuhimu kuwaambia kwamba kama walikuwa wakimuabudu Muhammad, amekufa?

Kauli ya Abu Bakr ilikuwa ni hila ya ujanja. Muhammad (s.a.w.) ndio kwanza amefariki, na ilikuwa ni kawaida kwa Waislamu kuwa na huruma kwa watu wa familia yake kwa kuondokewa kwao kukubwa. Lakini Abu Bakr alikuwa na hofu na huruma hii. Aliiona ni ya hatari kwa usalama wake binafsi juu ya ufalme. Kipindi cha maombolezo rasmi kingeweza kuwa cha hatari pia kwake. Yeye, kwa hiyo, alilinganisha maombolezo juu ya kifo cha Muhammad (s.a.w.) na “kumuabudu” Muhammad (s.a.w.), na ni nini kinachoweza kuwa cha kulaumika katika Uislamu kama “kumuabudu” Muhammad – mwanadamu – badala ya kumuabudu Allah (s.w.t.)!

Abu Bakr, kwa njia hii, aligeuza azma ya umma wa Kiislamu mbali na huruma yoyote ambayo ungeweza kuihisi kwa familia inayohuzunika ya Muhammad (s.a.w.).

Waarabu hawakuabudu kitu chochote vizuri zaidi kuliko vipande vya mawe au miti; Muhammad (s.a.w.) aliwafanya wawe wanaomuabudu Allah (s.w.t.) – Muumba mmoja na Mola wa Ulimwengu. Waarabu walikuwa ni wachunga kondoo au maharamia; Muhammad (s.a.w.) akawafanya wafalme na washindi. Waarabu walikuwa washenzi na wajinga; Muhammad (s.a.w) akawafanya taifa lililostaarabika zaidi duniani.

Alikuwa ni mfadhili mkubwa sio tu kwa Waarabu wa wakati wake mwenyewe bali kwa wanadamu wote kwa wakati wote. Mtu kama huyo alipofariki, Waarabu, Waislamu, ambao walikuwa wafaidikaji wa kazi yake kwao, walipaswa kupondwa na huzuni. Lakini cha kushangaza, kushtusha na kisichopingika, hawakuwa hivyo! Ingawa walikuwa wamepoteza baraka kubwa sana ambayo Allah (s.w.t.) alishusha kwao – kupitia Mpendwa Wake Mwenyewe, Muhammad hawakuonyesha hisia zozote za hasara hata kidogo.

Haikujitokeza kwa umma wa Kiislamu kwamba Muhammad (s.a.w.) alikuwa ni mwon- gozaji wake, na kiongozi wake sio tu katika maisha bali hata katika kifo, alipaswa kupata mazishi ya kitaifa, na palipaswa kuwa na kipindi cha maombolezo rasmi kwa ajili yake.

Umma wa Kiislamu ni dhahiri uliona kwamba kuomboleza kwa ajili ya kifo cha Muhammad (s.a.w.), na kumfanyia mazishi, zilikuwa ni kazi ambazo ni vema kuachiwa kwa watu wa familia yake mwenyewe. Watu wa familia yake waliomboleza kwa ajili yake, na walimfanyia mazishi.