read

Kuhusu Mwandishi, Sayyed Ali Asghar Razwy (1925-1996)

Marehemu Seyyid Ali Asghar Razwy anakumbukwa sana kama mwanachuoni wa Kiislamu mwenye maneno mazuri, ambaye haiba yake njema na moyo wa uchangamfu vililmpendezesha kwa wote waliokuwa na bahati nzuri ya kukutana naye. Wakati wote wale waliozungumza naye waliondoka wakiwa wameathirika sana kifikra, wakiwa wamejifunza kitu kutoka kwa mtaalamu huyu mwenye mvuto.

Seyyid Ali Asghar alizaliwa huko Simla, India mnamo mwaka 1925. Baba yake, Agha Seyyid Muhammad Shah alikuwa amehamia hapo zamani kutoka Baluchistan. Agha Seyyid Muhammad Shah alikuwa, yeye mwenyewe ni Aalim, aliyepata elimu yake huko Najaf na Qum, na alikuwa ndiye mwakilishi wa Marehemu Ayatullah Seyyid Abul Hassan Al-Isfahani (R.A.).

Seyyid Ali Asghar Razwy alijiunga katika utumishi wa serikali ya India mara baada ya kuhitimu Shahada ya B.A. Hons kutoka Chuo Kikuu cha Kashmir. Baadaye alishiriki kikamilifu katika vuguvugu la kuunda Pakistani na mwishowe akahamia Pakistani ambako alijiunga na Idara ya mambo ya nje.

Mnamo mwaka 1950, alikwenda Washington D.C. kama mjumbe wa ujumbe wa Kibalozi wa Pakistani. Mnamo mwaka 1954, alihamishiwa Kabul na mwaka mmoja baadaye Seyyid Ali Asghar akahamia Canada na halafu Marekani mnamo mwaka 1960 ambako alifanya kazi na shirika moja la kibiashara.

Akiwa mfanyakazi wa huduma za kijamii, alijiunga na The Muslim World League na kwa miaka mingi akawa ni chimbuko la uongozi kwa iliyokuwa jumuiya changa ya Kishia katika Marekani ya Kaskazini. Anayo sifa ya kipekee ya kuwa mzungumzaji wa kwanza, katika Marekani ya Kaskazini, kuhutubia jamaa ya waumini kwa Kiingereza.

Miongoni mwa kazi zake za maandishi za awali ni wasifu – The Biograpy of Seyyidati Khadijatul-Kubra na Salman Farsi. Seyyid Ali Asghar pia aliandika idadi ya vijitabu na majarida ya kidini juu ya mada mbalimbali.

Muswada huu wenye sifa daima, A Restatement of The History of Islam and Muslims ulikubaliwa kuchapishwa (kama kitabu) na Mulla Asgharali M. M. Jaffer, aliyekuwa Raisi wa The World Federation mnamo Julai, mwaka 1996.

Kwa kuchapishwa kwa kitabu hiki, ambacho Marehemu alikifanyia kazi kwa kipindi cha miongo ya miaka, miezi minane tu baada ya kifo chake cha kuhuzunisha, mnamo Septemba, 15, mwaka 1996 kwenye hospitali ya Calvalry huko New York, yeye ameacha urithi wa kudumu wa maarifa na elimu yake na hivyo kujihakikishia mwenyewe thawab-l’jari – thawabu zenye kuendelea.

Wasomaji wanaombwa kusoma Surat al-Fatiha kwa ajili ya kumbukumbu yake.