read

Kususiwa Kiuchumi Na Kijamii Kwa Bani Hashim

Mwaka wa sita wa Tangazo ulikuwa unakaribia. Wapagani walikuwa tayari wamemaliza miaka mitatu kupiga kampeni dhidi ya Uislamu. Wamezalisha uchungu mwingi na uhasama dhidi ya Waislamu katika miaka hii mitatu, lakini walikuwa na kidogo sana, kama kilikuwapo chochote, cha kuonyesha kwa ajili ya juhudi zao. Walitumia kila silaha dhidi ya Waislamu kuanzia vivutio mpaka ushawishi, hadi matusi mpaka kebehi, na dhihaka mpaka vitisho vya kutumia nguvu na utumiaji hasa wa nguvu zenyewe, lakini bila mafanikio. Ile nguvu ya imani ya Waislamu iliwakanganya.

Kutofaulu kwao kwa mara kwa mara kuliwalazimu Maquraish kutathimini upya ile hali ana kwa ana, Muhammad na Uislamu, na baadhi yao walijaribu kuliangalia tatizo lao kwa namna nyingine mpya. Katika kutafuta kwao ufumbuzi wa tatizo hili linalichusha, alianza taratibu kuwapambanukia juu yao kwamba adui yao hakuwa kile kikundi cha wale Waislamu wasio na mizizi na waliokumbwa na umasikini walioko pale Makka. Adui wa kweli – adui wa waabudu masanamu na washirikina – walimtambua alikuwa ni Abu Talib! Hata hivyo alikuwa ni Abu Talib aliyekuwa akimlinda Muhammad na Uislamu kwa uaminifu na msimamo thabiti. Waislamu, kwa upande mwingine, hawakuwa na uwezo wa kumlinda Muhammad. Kwa kweli, walikuwa wao wenyewe katika haja kubwa ya ulinzi.

Mafanikio haya katika “kumtambua adui” yalikuwa na uzito wa udhihirisho kwa viongozi wa Maquraishi katika harakati zao dhidi ya Uislamu, na yamewawezesha kupanga mkakati mpya.

Abd-al-Rahman ‘Azzam:

“Mwishowe, ule utawala wa wachache wa pale Makka uliamua kwa wasiwasi mkub- wa kuchukua hatua dhidi ya Abu Talib. Kwa mawazo yao, yeye ndiye aliyekuwa mlinzi hasa wa kufuru hii, ingawa bado alikuwa ni mtetezi wa kuheshimika wa mila za Makka na hajasilimu kwenye dini ya Muhammad (si -japo sio kweli). Walikubaliana kumpelekea masharti ya mwisho…(The Eternal Message of Muhammad, London, 1964)

Huko nyuma, Maquraish walikwishawahi kufanya majaribio ya “kumtenga” Muhammad kutoka kwenye ukoo wake, na walitegemea kwamba wangeweza ama kumchombeza au kumhadaa Abu Talib katika kutotilia maanani msaada wake na ulinzi kwa mpwa wake na Uislamu. Kama wangemtenganisha Muhammad na ukoo wake, walitumaini, wangeweza kutatua hilo tatizo gumu na sumbuvu kwa njia rahisi ya “kumfilisi” yeye.

Lakini Abu Talib hakuwaacha Maquraishi “kumtenga” Muhammad. Sio tu yeye mwenyewe aliyekuwa akimlinda mpwa wake, alikusanya pia ukoo wote wa Bani Hashim nyuma yake. Huu ukoo wa Bani Hashim ulikuwa imara katika msaada wake kwa Muhammad, na wakuu wa Maquraish walijikuta wanyonge mbele yake.

Baada ya mashauriano marefu na mjadala, Maquraishi walikubali kwamba “ukaidi” wa Bani Hashim ulihitaji hatua madhubuti, na waliamua kumtenga na kumfukuza sio tu Muhammad bali walinzi wake wote pia, yaani, ule ukoo wa Bani Hashim wote.

Ilitarajiwa kwamba jaribio lolote la kuwafukuza Bani Hashim lingepelekea kwenye kingamizo la vikundi hapo Makka. Kila mmoja hapo Makka angekuwa ajitangaze mwenyewe kuwapendelea au kuwapinga Bani Hashim. Lakini mara ikaja kuwa dhahiri kwamba katika mkabala huu, Bani Hashim watakuta Arabia yote imejipanga dhidi yao.

Muhammad Husein Haykal:

“Ni kama haiwezekani kwa sisi kufikiria nguvu na kiasi cha jitihada ambazo Maquraishi walitumia katika mapambano dhidi ya Muhammad, au uvumilivu wake katika miaka mingi mirefu ya mapambano hayo.

Maquraishi walimtishia Muhammad na jamaa zake, hususan ami zake. walimdhihaki yeye na ujumbe wake, na walimtusi yeye vilevile na wafuasi wake. Waliwaagiza washairi wake kumtukana yeye kwa uhodari wao makini sana na kuelekeza utani wao mkali dhidi ya mahubiri yake. Walimpa madhara na maumivu kwenye nafsi yake na kwenye nafsi za wafuasi wake.

Walimuahidi hongo za pesa, za hadhi ya kifalme na mamlaka, za vyote vile vinavy- omridhisha mtu aliye mgumu kabisa wa kuridhisha miongoni mwa watu. Hawakuwafukuza tu na kuwatawanya wafuasi wake kutoka kwenye nchi yao wenyewe, bali waliwadhuru katika uchuuzi na biashara zao wakati ikiwafukarisha. Ilimtahadharisha yeye na wafuasi wake kwamba vita pamoja na masaibu yake inge- waangukia juu yao. Mambo yote yaliposhindikana, walianza msusio juu yao uliopangwa kuwaua kwa njaa.”
(The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Siku chache kabla ya mwanzo wa mwaka wa 7, wakuu wa koo mbali mbali za Quraishi walikutana katika kikao kizito cha faragha ndani ya “baraza la mji” la Makka, na pale, kwa makubaliano, walirasimu na kutia sahihi waraka unaotamka kwamba ila tu, kama huo ukoo wa Bani Hashim utamkabidhi Muhammad kwao, utafanyiwa mgomo wa kiuchumi na kijamii. Wakajiapiza wenyewe kutonunua chochote, wala kuuza chochote, kwa watu wa ukoo wa Bani Hashim, na waliweka marufuku kuoana kati yao na wao.

Mkataba huu ulipelekwa kwenye makabila mengine kwa ajili ya kuidhinishwa. Walipokwishaidhinisha, ukatundikwa kwa taadhima kwenye ukuta wa Al-Kaaba. Kuidhinishwa kwa mkataba huo kulikuwa ni kitendo cha uchokozi!

Abu Talib aliweza kuona dhahiri kwamba mfumo wa wasiwasi ulikuwa unaelekea kwa Bani Hashim. Hali ya Makka imekuwa ya mlipuko kiasi kwamba ukoo wa Bani Hashim ulijikuta kwenye hatari kubwa. Abu Talib alitambua kwamba haitakuwa busara kuishi katika mji, wakati wowote adui anaweza kuzichoma moto nyumba zao.
Kwa maslahi ya usalama wa ukoo huo, yeye, kwa hiyo, akaamua kuondoka Makka, na kutafuta usalama wa ukoo huo katika bonde karibu ya Makka ambalo baadae lilikuja kujulikana kama Sh’ib Abu Talib. Bonde hilo lilikuwa na namna ya ulinzi wa asili, na lilikuwa kwa hali yoyote lenye usalama wa kuishi kuliko kuishi kwenye nyumba zao mjini hapo ambazo zilikuwa sio sala- ma kwa mashambulizi.

Katika siku ya kwanza ya mwaka wa 7 wa Tangazo la Uislamu, kwa hiyo, zile koo mbili za Bani Hashim na Bani al-Muttalib ziliondoka Makka na zikachukua makao kwenye bonde. Koo hizo zilikuwa katika hali ya kuzingirwa (karantini). Ilikuwa iwe karantini ndefu!

Muhammad Husein Haykal:

“Ule mkataba ambao koo za Quraishi ziliuingia wa kumgomea Muhammad na kuwazingira Waislamu uliendelea kutekelezwa kwa miaka mitatu mfululizo.”(The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Marmaduke Pickthall:

“Kwa miaka mitatu, Mtume (s.a.w.) alikuwa amefungiwa pamoja na jamaa zake wote katika ngome yao ambayo ilikuwa katika moja ya mabonde linalokwenda hadi Makka.”
(Introduction to the Translation of Holly Qur’an,1975)

Hadithi ya karantini ya Bani Hashim ni mlango wa kusisimua katika utenzi wa Kiislam, na umesimuliwa na kila mwanahistoria wa somo hilo, miongoni mwao:

Sir William Muir:

“…Maquraishi walifanya muungano dhidi ya Bani Hashim – kwamba hawatawaoa wanawake zao, wala kuwaoza wanawake kwao; kwamba hawatauza chochote kwao, wala kununua kitu chochote kutoka kwao; na kwamba kuhusiana nao kwa aina yoyote ile kukome.

Amri ya kupigwa marufuku huko iliwekwa kwa maandishi kwa uangalifu, na yakafungwa kwa mihuri mitatu. Pale wote walipojifunga wenyewe kwenye mkataba huo, kumbukumbu hiyo ikatundikwa kwenye ukuta wa Al-Kaaba, na hivyo kibali cha kidini kikatolewa kwenye mahitaji yake.

Bani Hashim hawakuweza kuhimili mwelekeo wa maoni ya umma ambayo yamepata nguvu kali hivyo dhidi yao, na yenye wasiwasi kwamba yanaweza kuwa ni utangulizi tu wa mashambulizi ya wazi, au wa mapigo ya gizani ambayo bado ni mabaya zaidi, walijitenga kwenye nafasi ya mji iliyojitenga inayojulikana kama Sh’ib Abi Talib. Imeundwa na moja ya mabonde mikatiko ya milima, ambamo yale mawe yanayochomoza ya Abu Qubais yamelemea kwenye viunga vya Mashariki ya Makka. Iliingiliwa kwenye upande wa mji kwa njia ya chini yenye lango, kwa njia hiyo ngamia alipita kwa taabu. Kwenye pande nyingine zote ilitengwa na mji kwa majabali na majengo.

Katika usiku wa kwanza wa mwezi wa kwanza wa mwaka wa saba wa ujumbe wa Muhammad, hawa Bani Hashim, pamoja na Mtume (s.a.w.) na familia yake, walijitenga kwenye kambi ya Abu Talib; na pamoja nao kilifuata pia kizazi cha Al-Muttalib, ndugu yake Hashim. Amri ya utenganisho ilitumiliwa kwa ukali kabisa. Hawa Bani Hashim mara wakajikuta wamekatwa kwenye njia yao ya kupatia nafaka na mahitaji yao mengine ya maisha; na uhaba mkubwa ukajitokeza kwa sababu hiyo

… akiba hiyo ya Bani Hashim isiyotosheleza iliyojalizwa tena kwa majaribio ya nadra na ya siri, iliwaweka kwenye upungufu na dhiki. Raia waliweza kusikia uliaji wa watoto wanaoteseka kwa njaa ndani ya bonde hilo … miongoni mwa ndugu wa kundi hili lililotengwa, walipatikana waliojaribu, mbali na vitisho vya Maquraishi, kupitisha mara kwa mara mahitaji kwa hila wakati wa usiku, kwenye kambi ya Abu Talib. Hakim, mjukuu wa Khuwalid, alikuwa, japo jaribio lenyewe wakati mwingine lilikuwa hatari, akibeba mahitaji kumpelekea shangazi yake Khadija. (The Life of Muhammad, London, 1877)

Mwanzoni mwa karantini hiyo, Ali alikuwa na umri wa miaka 16, na alibebeshwa kazi ngumu na ya hatari ya kuwapatia chakula ukoo mzima.
Alitekeleza kazi hii kwa kuhatarisha sana maisha yake na alileta maji na nafaka wakati wowote alipopata chochote kile. Kwa mfuko mmoja wa ngozi ya mbuzi wa maji, ilimbidi alipie kipande kimoja cha dhahabu, na alijiona mwenye bahati kama alifanikiwa kuufikisha kule kwenye bonde. Juhudi zake, hata hivyo, zilileta nafuu ya kiasi tu kwenye kabila hilo lililozingirwa.

Abu Talib mwenyewe hakuwa akilala usiku. Kwake yeye usalama wa kimwili wa mpwa wake ulipewa umuhimu wa kwanza kuliko kitu kingine chochote. Wakati Muhammad ali- poshikwa na usingizi, Abu Talib alimuamsha na kumwambia alale katika kitanda cha mmojawapo kati ya wanawe wanne, na alimuamuru mwanae kulala kwenye kitanda cha Muhammad. Baadae kidogo, atamuamsha mpwa wake tena, na kumwambia aende kwenye kitanda cha mwanae mwingine.

Aliutumia usiku wote katika kumhamisha Muhammad kutoka kwenye kitanda kimoja na kumuweka kwenye kingine. Hakudanganyika juu ya maadui zake; walikuwa wang’ang’anifu, wadanganyifu, mafisadi na wasiosamehe. Yeye, kwa hiyo, hakuwatweza. Kama mmoja wao angenyemelea ndani ya bonde hilo kwa nia ya kumuua Muhammad, yumkini kabisa, angemuua mmoja wa watoto wa Abu Talib. Yeye Abu Talib na mkewe daima walikuwa tayari kuwatoa mhanga watoto wao kwa ajili ya Muhammad.

Kulikuwa na nyakati ambapo Ali, licha ya ujasiri na uwezo wake mkubwa, alishindwa kupata mahitaji yoyote, na watoto (na watu wazima pia) waliishi kwa njaa. Lakini kuishi kwa njaa na kiu kulikuwa ni kawaida ndani ya bonde hilo. Wakati maji yakiwepo, akina mama walichemsha majani makavu ndani yake ili kuwaliwaza watoto wao wanaolia. Kilio cha watoto wenye njaa kiliweza kusikika nje ya bonde hilo, na Abu Jahl na Bani Umayya walikipokea kwa kicheko cha dhihaka. Walichekelea “ushindi” wao wa kuwafanya watoto wa Bani Hashim kulilia maji na chakula.

Zawadi ya thamani sana kwa hizi koo zilizotengwa katika miaka hii mitatu, ilikuwa ni maji. Maji yalikuwa ni zawadi ya maisha, na koo mbili hizi ziliyapokea kutoka kwa Khadija. Yeye alimpa Ali vile vipande vya dhahabu ambavyo alinunulia maji. Masikitiko yake juu ya wale waliomzunguka yalijionyesha kwa njia nyingi. Aliswali na kuomba rehma za Allah (s.w.t.) juu ya waliotengwa. Swala ilikuwa ndio “mkakati” wake wa kushughulikia shida. Ilikuwa, alivyouona, ni mkakati rahisi lakini wenye nguvu.

Mara chache, wale marafiki wachache ambao Bani Hashim walikuwa nao huko Makka, walijaribu kuingiza chakula kwa magendo ndani ya bonde hilo, lakini kama hao mapagani walikikamata, walikichukua.

Mmoja wa marafiki wa Bani Hashim aliyekuwako Makka alikuwa ni Hisham ibn Amr al-Aamiri. Aliwaletea chakula na maji kila mara kiasi alivyoweza. Muda aliouchagua wa kupeleka hayo mahitaji kwenye bonde hilo, ulikuwa ni masaa machache kabla ya kucha; lakini hatimae Maquraishi walimkamata, na walitishia kumuua kama angeng’ang’nia kuleta ngamia wake waliosheheni bondeni hapo kwa ajili ya Bani Hashim. Rafiki mwingine wa siri wa Bani Hashim alikuwa ni Hakim ibn Hizam, mpwawe Khadija. Yeye na mtumwa wake walibeba chakula na maji kumpelekea Khadija ambayo mara moja aliyatoa kwa watoto.

Abul Bukhtari alikuwa mmoja wa marafiki wa Hakim. Yeye pia alileta mahitaji ya lazima kwa Bani Hashim.

Usiku mmoja yeye na Hakim walikuwa wamepanda ngamia kwenda huko kwenye bonde wakati waliposhitukizwa na Abu Jahl. Aliwaambia kwamba atawanyang’anya zile bidhaa na ngamia. Mwanzoni, Abul Bukhtari akajaribu kuelewana naye kwa maneno lakini hakutaka kusikiliza kitu chochote. Alizuia ile njia ya kwendea kwenye bonde na akakataa kuwapisha wapite.

Abul Bukhtari alijaribu kulazimisha kumpita Abu Jahl, na hili lilisababisha ugomvi mkali wa ngumi kati yao. Mizozo kama hii ilizuka mara kwa mara karibu na bonde hilo lakini wale marafiki wachache ambao ukoo wa Bani Hashim waliokuwa nao hapo mjini, hawakuvunjika moyo, na walifanya kila kitu walichoweza kuwaletea msaada.

Hisham bin Amr al-Aamiri, Hakim bin Hizam, na Abul Bukhtari, hawakuwa Waislamu lakini hawakutaka kuona mtoto yeyote au hata mtumwa wa Bani Hashim akifa kwa njaa, na wakahatarisha maisha yao wenyewe mara kwa mara katika kuleta chakula na maji kwenye Sh’ib Abu Talib. Walikuwa vilevile wakifurahia kulipia madeni ya huduma za msaada kama hizo kwa miaka mitatu, na chote walichokitafuta kama malipo yao kilikuwa ni usalama wa zile koo zilizotengwa.
Haina budi ionyeshwe hapa kwamba ile chuki na hasira ya Bani Umayya ya Quraishi ilielekezwa sio dhidi ya Waislamu bali dhidi ya ukoo wa Bani Hashim. Nia yao ilikuwa ni kuuangamiza Uislamu. Lakini hawangeweza kuangamiza Uislamu bila ya kumuua Muhammad. Walifanya idadi kubwa ya majaribio ya kumuua lakini walishindwa kwa sababu hawakuweza kumfikia. Alikuwa salama na shwari katika “ngome” ambayo Abu Talib na Bani Hashim wameijenga kwa ajili yake.

Bani Umayya waliwalenga kwa usawa kabisa Bani Hashim kama wahusika wa kushindwa kwao kote na kukatishwa tamaa katika vita vyao juu ya Uislamu, na kamwe hawakuipu- uza ili kuwashinda katika mapambano yao marefu na magumu dhidi yake.

Na kwa Waislamu ambao hawakutokana na ukoo wa Bani Hashim, walikuwepo wengi, na wote walikuweko Makka. Hawakwenda Sh’ib Abu Talib pamoja na Bani Hashim. Wengine miongoni mwao wanasemekana walikuwa matajiri, wenye uwezo na mashuhuri, na wote walidai kwamba walikuwa wakimpenda Mtume wao; lakini cha kushangaza, hakuna hata mmoja wao aliyekuja kumuona sembuse kumletea msaada wowote, wakati wa miaka mitatu ya karantini.

Walifurahia starehe na usalama wa majumbani mwao hapo mjini kwa miaka mitatu wakati Mtume wao, Muhammad Mustafa, akiishi kwenye ncha ya upanga, akizungukwa na maadui wenye kiu na damu yake, na katika hali ya wasiwasi kamili akiwa hajui kamwe ni matata gani mchana au usiku unaokuja utamletea yeye na kwa ukoo wake.

Karantini hii ya Bani Hashim iliondolewa miaka mitatu baadae, mwaka wa A.D. 619, na ukoo huo ukarudi mjini. Miaka kumi imepita tangu Muhammad, rehma na amani ziwe juu yake na Ahlul-Bait wake, alipotangaza kwa mara ya kwanza ujumbe wake.

Mgomo wa Maquraishi umeshindwa kuzaa matokeo yaliyotarajiwa. Watu wa Bani Hashim walikuwa majasiri, na murua wao ulikuwa juu. Ilikuwa haiwaziki kwao vilevile, hapo mwishoni mwa karantini, kama ilivyokuwa hapo mwanzoni, kumtoa Muhammad, mpendwa wao, kwa maadui wake.

Bani Hashim na Bani Al-Muttalib walirejea majumbani kwao huko Makka baada ya miaka mitatu. Muda wote wa miaka hii mitatu, utajiri wote wa Khadija na Abu Talib ulikwisha. Walikuwa waanze, kama ilivyokuwa, mwanzo mpya katika maisha, kwa kuweka matofali yao kwenye nafasi zao – moja moja.

Kama wakuu wa Maquraishi waliiondoa karantini, haikuwa kwa sababu kulikuwa na “mabadiliko ya moyo” yoyote kwa upande wao. Waliiacha karantini hiyo kwa sababu kulikuwa na nguvu nyingine zilizokuwa zikifanya kazi dhidi yake. Yafuatayo ni maelezo yaliyotolewa katika chanzo cha mapema sana kinachopatikana hadi leo,Wasifu wa Mtukufu Mtume wa Uislamu’ cha Muhammad ibn Ishaq, cha matukio yaliyofikia kilele katika kurudi Makka kwa koo za Bani Hashim na Bani al-Muttalib kutoka Sh’ib Abu Talib, baada ya miaka mitatu.

Kutanguka Kwa Mgomo

“Bani Hashim na Bani al-Muttalib walikuwa katika bonde (maficho ya mlimani) la Sh’ib kwa vile Maquraishi waliweka ahadi ya kuwatenganisha. Kisha baadhi ya watu wa kabila la Quraishi lenyewe walichukua hatua za kuutangua mgomo huo dhidi yao. Hakuna aliyehangaika sana na hili kuliko Hisham ibn Amr … kwa sababu ya kwamba alikuwa mtoto wa ndugu ya Nadla bin Hashim bin Abd Manafi kwa mama yake na alihusiana kwa karibu sana na Bani Hashim. Aliheshimiwa sana na watu wake.

Nimesikia kwamba wakati koo hizi mbili zilipokuwa kwenye bonde lao, alikuwa akipeleka ngamia aliyesheheni chakula usiku na kisha, alipokuwa amemfikisha kwenye mlango wa njia, alimuondolea hatamu yake, akampiga kwa kishindo ubavu- ni, na akamfanya akimbie ndani ya uchochoro wa njia inayoelekea kwao. Atafanya vivyo hivyo safari nyingine, akiwaletea nguo.

Akaenda kwa Zubayr bin Abu Umayya bin Al-Mughira ambaye mama yake alikuwa ni Atika binti ya Abdul Muttalib na akasema: ‘Unaridhika kula chakula na maji na kuvaa nguo wakati ukijua hali ya ami zako wa kikeni? Hawawezi kununua au kuuza au kuchanganya damu. Wallahi kama wangekuwa ami za Abu’l-Hakam bin Hisham (Abu Jahl), na ukamtaka afanye alivyokutaka wewe ufanye, asingelikubali hilo kamwe.’

Yeye (Zubayr) akasema, ‘Unanishangaza wewe Hisham, mimi nitafanya nini? Nipo mtu mmoja tu. Wallahi, kama ningekuwa na mtu mwingine wa kuniunga mkono mimi, ningeutangua mapema sana.’ Akasema, ‘Nimepata mtu – mimi mwenyewe.’ ‘Tafuta mwingine,’ akasema. Hivyo Hisham akaenda kwa Al-Mutim bin Adiy na akasema, ‘unaridhika kwamba koo mbili za Bani Abd Manafi ziangamie huku ukiona ukiwaafiki kuwafuata Maquraishi? Utaona kwamba hivi karibuni watakufanyia vivyo hivyo na wewe.’ Mutim akatoa jibu kama lile la Zibayr na akataka mtu wa nne.

Hivyo Hisham akaenda kwa Abu’l Bukhtari bin Hisham ambaye alitaka mtu wa tano, na kisha kwa Zama’a bin Al-Aswad bin Al-Muttalib, ambaye aliomba mtu wa sita, na akamkumbusha udugu na wajibu wao. Aliuliza endapo wengine walikuwa tayari kushirikiana kwenye kazi hii.

Akampa majina ya wale wengine. Wakakubaliana wote kukutana usiku karibu na Hujun, juu ya Makka, na walipokutana, walijifunga kulichukulia swala la ile hati hadi wamepata utanguzi wake.

Siku iliyofuata, wakati watu walipokusanyika pamoja, Zubayr alivaa joho, akazunguka Al-Kaaba mara saba; kisha akaja mbele na kusema: ‘Enyi watu wa Makka, hivi sisi tule na kujivisha wenyewe wakati Banu Hashim wanaangamia, wakiwa hawawezi kununua wala kuuza? Wallahi sintapumzika hadi pale hati hii ya mgomo muovu itakapopasuliwa!

Abu Jahal akapaza sauti: ‘Unajidanganya. Haitapasuliwa.’

Zama’a akasema: “Wewe ni muongo mkubwa; hatukuipenda hati hii hata pale mwanzo iliporasimiwa na kutiwa saini.”Abu’l Bukhtari akasema, ‘Zama’a anasema kweli. Hatukuridhika na hati hii ilipokuwa inaandikwa, na haturidhiki nayo sasa hivi.’

Al-Mutim akaongeza: “Wote mnasema kweli, na yeyote anayesema vinginevyo, huyo ni muongo. Tunamuomba Allah ashuhudie kwamba tunajitoa kwenye wazo zima na kile kilichoandikwa kwenye hati hiyo.” Hisham akaongea kwa maana hiyo hiyo, na akawaunga mkono marafiki zake.

Kisha Al-Mutim akaiendea ile hati na kuichana vipande vipande. Aligundua kwamba wadudu walikwisha itafuna isipokuwa yale maneno, “Kwa Jina lako Ewe Allah (s.w.t.)” Hii ni kanuni iliyozoeleka ya Maquraishi ya kuanzia maandishi yao. Mwandishi wa hati hii alikuwa ni Mansur bin Ikrima.”

Mutim ibn Adiy akachana ile hati ya fedheha ya Maquraishi katika vipande vipande. Vile vipande vikapeperushwa na upepo, na hakuna sazo lililoachwa. Ni kitendo kilichohitaji msimamo na ujasiri – msimamo kwamba Bani Hashim walikuwa waathirika wa udhalimu, ukatili na majuto, wasio na hatia; na ujasiri kuwakaidi Maquraishi. Kitendo chake imara kilikuwa ni ishara kwamba ile karantini ya Bani Hashim imekwisha, na kwamba watu wake sasa wanaweza kurejea mjini.

Mutim mwenyewe na wapiganaji vijana wa ukoo wake walikwenda kwa vipando vyao wakiwa katika mavazi kamili ya kivita, kwenye bonde hilo na kumsindikiza Muhammad Mustafa na watu wote wa koo mbili za Bani Hashim na Bani al-Muttalib, kurudi Makka na majumbani kwao.

Dr. Muhammad Hamidullah anaandika kwenye ukurasa wa 10 wa kitabu chake, Introduction to Uislamu, kilichochapishwa na International Islamuic Federation of Student Organizations, Salimiah, Kuwait (1977):

Baada ya miaka mitatu, watu wanne au watano wasiokuwa Waislamu, wenye ubinaadamu zaidi kuliko wote waliobakia na wanaotokana na koo tofauti, walitangaza bayana shutuma zao za ule mgomo wa kiuonevu.

Dr. Hamidullah amedhania kwamba kushindwa kwa mgomo huu ni matokeo ya ubinadamu wa “watu wanne au watano wasiokuwa Waislamu.” Walikuwa, anasema, ‘wenye ubinadamu zaidi kuliko wengine waliobaki.’ Ana haki. Lakini walikuwa na ubinadamu zaidi hata ya waleWaislamu waliokuwa wakiishi Makka?

Kwa mshangao, cha ajabu, jibu la swali hili lenye kughasi ni la kukubali. Hata hivyo, mbali na hawa mashujaa watano – wasiokuwa Waislamu, wote – ubinadamu haukumsukuma mtu mwingine yeyote hapo Makka – asiyekuwa mwislamu au mwislamu – kuwakaidi Maquraishi na kutenda katika ulinzi wa Bani Hashim. Kuna swali jingine moja, yaani, kwa nini Zubayr alijiona yuko yeye peke yake?
Wakati Hisham alipolijulisha kwa mara ya kwanza hili suala la kutangua huu Mkataba wa washirikina wa kuwagomea hawa Bani Hashim, kwa rafiki yake Zubayr, na akamsuta kwa kutokuwa na hisia juu ya mateso ya Bani Hashim, na kwa kushindwa kwake kushughulika kuyamaliza mateso yale, Zubayr akasema, “Unanishangaza ewe Hisham, mimi nifanye nini? Mimi ni mtu mmoja pekee. Wallahi, kama ningekuwa na mtu mwingine wa kuniunga mkono, ningeutangua mapema tu.”

Jibu la Zubayr ni la fumbo. Kwa nini alijiona yuko peke yake? Kwa nini asijaribu kuorodhesha uungaji mkono wa Waislamu ambao walikuwa wengi hapo Makka? Kwa mujibu wa wanahistoria, baadhi ya Waislamu hapo Makka walikuwa ni watu wenye hadhi na wenye mali, na walikuwa na ushawishi wa kutosha kwa washirikina. Lakini kwa sababu za kisirisiri, haikuwajia ama kwa Zubayr mwenyewe au kwa rafiki yake yoyote, kuwakusanya Waislamu hawa kwenye kundi moja – “timu” – ambalo lilimaliza huu mgomo kwa Bani Hashim.

Zubayr na rafiki zake walifanikiwa katika juhudi zao za kuwarudisha Bani Hashim hapo mjini. Lakini kwa kitendo chao hiki, wamedhihirisha kwamba wale Waislamu ambao walikuwa wanaishi Makka, hawakuwa “wenye lazima” kwa Muhammad au kwa Uislamu.

Ni mojawapo ya ukweli mkubwa kabisa unaofanana na uongo katika historia ya Uislamu kwamba ule mkono uliofikia na kuchana vipande vipande, ule mkataba wa washirikina wa kuutenga na kuuhamisha ule ukoo wa Bani Hashim, ulitokana, sio kwa “mu’min” bali kwa “asiyeamini” Mutim ibn Adiy! Sio Mutim wala yeyote kati ya marafiki zake wanne, yaani, Hisham ibn Amr, Zubayr ibn Abu Umayya, Abu’l Bukhtari ibn Hisham, na Zama’a ibn Al-Aswad, aliyekuwa mwislamu. Lakini wote watano walikuwa mashujaa wenye maadili, na hawakuridhia katika dhulma iliyokuwa ikifanywa kwa Bani Hashim. Hawakutulia mpaka waliporejesha haki ndani ya Makka.

Kusema kweli, hawa mashujaa watano hawakuwa Waislamu. Lakini wao na wao wenyewe tu walikuwa na ujasiri na busara ya kutetea kanuni ambayo ni ya Kiislam, yaani, ile Kanuni ya Haki. Walitetea haki, na kitendo chao cha kishujaa, kiliwaletea sifa njema ya kudumu katika kisa kirefu cha historia ya Uislamu.

Waislamu, kwa upande mwingine, sio tu hawakushughulika; hawakuupinga walau, ule ubeuzi na uonevu wa Maquraishi katika kuwafukuza Bani Hashim kutoka Makka. Walidumisha, kwa miaka mitatu, upweke wenye hadhari na ukimya usioaminika. Matendo yao, inavyoonekana, yalitawaliwa na busara. Kwa hiyo, yote yale waliyofanya, ilikuwa ni kupitisha muda, na kuangalia mwelekeo wa matukio, kama watazamaji wasiojali.