read

Kutangazwa Kwa Surat Bara’ah (At-Taubah)

Wakati msimu wa hijja ya mwaka wa 9 H.A. ulipowadia, Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) alikuwa na idadi kubwa ya kazi zilizombana ambazo zilihitaji uangalizi wake wa haraka kiasi kwamba alikuwa hawezi kuondoka Madina. Yeye, kwa hiyo, alimtuma Abu Bakr kwenda Makka kama kiongozi wa kundi la mahujaji mia tatu kwenda kuongoza ibada za Hijja.

Lilikuwa ni jukumu la uongozi halisi, mbele ya watu, la kwanza kabisa la Abu Bakr. Abu Bakr na mahujaji hao waliondoka Madina. Siku moja baada ya kuondoka kwao. Mtume (s.a.w.) alipokea kutoka Mbingnii wahy mpya uitwao Bara’a (At-Taubah) – Sura ya tisa ya Qur’an, na aliamriwa kwa dhati kabisa kuitangaza huko Makka ama yeye mwenyewe binafsi au kutoa mamlaka ya kufanya hivyo kwa mtu kutoka kwenye familia yake mwenyewe, lakini sio kwa mtu mwingine yeyote.

Kulingana na amri hii ya Mbingnii, Muhammad Mustafa alimwita binamu yake, Ali ibn Abi Talib, akampa kipando chake apande, na akamuamuru kupeleka ule wahy mpya Makka, na kuutangaza huko katika mkusanyiko wa mahujaji – Waislamu na mapagani.

Muhammad ibn Ishaq

Wakati At-Taubah iliposhuka kwa Mtume (s.a.w.) baada ya kuwa alikwishamtuma Abu Bakr kusimamia hijja, mtu mmoja alionyesha nia kwamba angeipeleka kwa Abu Bakr. Lakini akasema: “Hakuna mtu atakayeitangaza kutoka kwangu bali mtu wa nyumba yangu mwenyewe.” Ndipo akamwita Ali na akasema: “Chukua sehemu hii kutoka mwanzo wa At-Taubah, na uitangaze kwa watu siku ya kafara wakati watakapokusanyika huko Mina.” (The Life of the Messenger of God)

Washington Irving

Muhammad alimtuma Abu Bakr kama mkuu wa mahujaji kwenda Makka, yeye mwenyewe akiwa ameshikwa sana na shughuli za jamii na za nyumbani kiasi cha kumfanya asiweze kukosekana Madina.

Sio muda mrefu sana baadae Muhammad akamwita mkwe wake na Sahaba mtiifu, Ali, na akimpandisha juu ya ngamia mwepesi sana kati ya ngamia wake, alimhimiza kufanya haraka kwa kasi yote kwenda Makka, huko akatangaze mbele ya umati wa mahujaji waliokusanyika kutoka sehemu zote, Sura muhimu ya Qur’an, aliyoipokea hivi punde kutoka mbingnii.

Ali alitekeleza kazi yake kwa moyo na usahihi wake uliozoeleka. Aliufikia huo mji mtukufu kileleni mwa tamasha hilo kubwa la kidini. Alisimama mbele ya umati mkubwa uliokusanyika kwenye kilima cha Al-Akaba, na akajitangaza yeye mwenyewe kama mjumbe kutoka kwa Mtume, akiwa amebeba wahy muhimu.

Kisha yeye akasoma ile Sura ambayo yeye alikuwa mbebaji, ambayo ndani yake ile dini ya upanga (sic) ilitangazwa katika ugumu wake wote.

Wakati Abu Bakr na Ali waliporudi Madina, huyu Abu Bakr alionyesha mshangao na kutoridhika kwake kwamba hakufanywa kuwa mtangazaji wa wahy muhimu kama huo, kama ulivyoonyesha kuunganishwa na kazi yake ya awali, lakini alitulizwa kwa uhakikisho kwamba wahy mpya wote lazima utangazwe na Mtume (s.a.w.) mwenyewe, au na mtu kutoka kwenye familia yake wa karibu. (The Life of Muhammad)

Sir William Muir

Kuelekea mwishoni mwa hijja, katika sikukuu ya kuchinja (kafara), pale mahali pa kutupia mawe karibu na Mina, Ali aliusomea kwa sauti ule umati mkubwa uliokusanyika karibu yake katika ile njia nyembamba, ile amri ya mbingnii.

Alipokuwa amemaliza kusoma kifungu hiki, Ali aliendelea: “Nimeamriwa kuwatangazieni kwamba hakuna asiyeamini atakayeingia peponi. Hakuna muabudu sanamu atakayefanya hijja baada ya mwaka huu; na hakuna mtu yoyote atakayefanya mzunguko wa Nyumba Tukufu akiwa uchi.

Yeyote yule aliye na mkataba na Mtume, utaheshimiwa mpaka ukomo wake. Miezi minne imeruhusiwa kwa kila kabila kurudi kwenye nchi zao kwa usalama. Baada ya hapo wajibu wa Mtume (s.a.w.) unakoma.”

Mkusanyiko mkubwa wa mahujaji ulisikiliza kwa utulivu mpaka Ali alipomaliza. Kisha wakatawanyika na kuondoka kila mtu kwenda nyumbani kwake, kutangaza kwa makabila yote ya peninsula nzima hii amri kali ambayo wameisikia kutoka kwenye midomo ya Ali. (The Life of Muhammad, London, 1877)

Muhammad Husein Haykal

Baada ya (Ali) kumaliza kisomo chake cha Qur’an, aliendelea kwa maneno yake mwenyewe: “Enyi watu, hakuna asiyeamini atakayeingia Peponi; hakuna mshirikina atakayefanya hijja baada ya mwaka huu; na hakuna mtu aliyeko uchi atakayeruhusiwa kuizunguka Al-Kaaba. Yeyote aliyeingia mkataba na Mtume wa Allah – rehema na amani ziwe juu yake – atatimiziwa mkataba wake mpaka kipindi chake kitakapokwisha.” Ali alitangaza haya maagizo manne kwa wale watu na kisha akampa kila mtu miezi minne ya amani ya kawaida na msamaha ambayo ndani yake mtu yoyote anaweza kurudi nyumbani kwa usalama. Kuanzi wakati ule na kuendelea, hakuna muabudu sanamu aliyefanya hijja na hakuna mtu aliye uchi aliyefanya mizunguko ya Al-Kaaba. Kuanzia siku ile na kuendelea, Dola ya Kiislam ilianzishwa.
(The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Ali ibn Abi Talib “alizisoma tena zile Aya za Allah (s.w.t.)” huko Mina, akimuwakilisha Mtume wa Allah (s.a.w.). Hii lazima iwekwe akilini na msomaji kwamba “kusoma Aya za Allah (s.w.t.)” ni kitendo chenye madaraka makubwa. Ni kitendo, kwa kweli, muhimu sana kiasi kwamba Allah (s.w.t.) Mwenyewe alikitwaa. Tunasoma katika Qur’an:

تِلْكَ آيَاتُ اللَّهِ نَتْلُوهَا عَلَيْكَ بِالْحَقِّ ۚ وَإِنَّكَ لَمِنَ الْمُرْسَلِينَ {252}

Hizi ni Aya za Allah. Tunakusomeeni kwa haki, Hakika wewe ni miongoni mwa Mitume.
(Sura ya 2; Aya ya 252)

تِلْكَ آيَاتُ اللَّهِ نَتْلُوهَا عَلَيْكَ بِالْحَقِّ ۗ وَمَا اللَّهُ يُرِيدُ ظُلْمًا لِلْعَالَمِينَ {108}

Hizi ni Aya za Allah. Tunakusomea kwa haki; Na Allah hapendi kuwadhulumu walimwengu.
(Sura ya 3; Aya ya 108)

Kulingana na Aya hizi, Allah (s.w.t.) Mwenyewe Alizisoma Aya Zake kwa Muhammad, Mtume Wake, na baadae (mara alipokwisha kuzisikia) akazisoma kwa wanadamu wote. Kusoma Aya za Allah (s.w.t.) kulikuwa ni moja kati ya kazi zake muhimu. Umuhimu wa kazi hii unaakisiwa na Aya zifuatazo za Qur’an Tukufu:

رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولًا مِنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ ۚ إِنَّكَ أَنْتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ {129}

Ewe Mola wapelekee miongoni mwao Mtume, anayetokana nao wenyewe. Atakayewasomea Aya Zako na awafundishe Kitabu na Hekima na awatakase; hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima. (Sura ya 2; Aya ya 129)

كَمَا أَرْسَلْنَا فِيكُمْ رَسُولًا مِنْكُمْ يَتْلُو عَلَيْكُمْ آيَاتِنَا وَيُزَكِّيكُمْ وَيُعَلِّمُكُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُعَلِّمُكُمْ مَا لَمْ تَكُونُوا تَعْلَمُونَ {151}

Kama tulivyotuma Mtume kwenu, anayetokana na ninyi, anayekusomeeni Aya Zetu na kukutakaseni, na kukufudisheni Kitabu na Hekima, na kukufundisheni yale mliyokuwa hamyajui. (Sura ya 2; Aya ya 151)

لَقَدْ مَنَّ اللَّهُ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ إِذْ بَعَثَ فِيهِمْ رَسُولًا مِنْ أَنْفُسِهِمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِنْ كَانُوا مِنْ قَبْلُ لَفِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {164}

Hakika Allah aliwafanyia wema mkubwa Waumini, pale alipowapelekea Mtume aliyetoka miongoni mwao wenyewe, Aliyewasomea Aya Zake na kuwatakasa, na kuwafundisha Kitabu na Hekima, ambapo kabla ya hapo walikuwa katika upotovu uliowazi. (Sura ya 3; Aya ya 164)

هُوَ الَّذِي بَعَثَ فِي الْأُمِّيِّينَ رَسُولًا مِنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِنْ كَانُوا مِنْ قَبْلُ لَفِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {2}

Yeye ndiye aliyempeleka kwa watu wasiojua kusoma, Mtume anayetoka miongoni mwao, awasomee Aya Zake na awatakase, na awafundishe Kitabu na hekima, ingawa kabla ya hapo, alikuwa katika upotovu ulio dhahiri. (Sura ya 62; Aya ya 2)

Kulingana na Aya hizi, Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) alikuwa na kazi za kufanya zifuatazo:

1. Kusomea watu Aya za Allah (s.w.t.);

2. Kuwafundisha maandiko na hekima;

3. Kuwatakasa;

4. Kuwafundisha katika elimu mpya.

Ya kwanza kutajwa katika kazi za utume ni, “kusoma Aya za Allah (s.w.t.)” Ni muhimu sana kwamba inachukua utangulizi juu ya kazi nyingine zote za Mtume.

Kusoma Aya za Allah (s.w.t.) kumetajwa pia pekee pekee katika Qur’an katika Aya zifuatazo:

كَذَٰلِكَ أَرْسَلْنَاكَ فِي أُمَّةٍ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهَا أُمَمٌ لِتَتْلُوَ عَلَيْهِمُ الَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَهُمْ يَكْفُرُونَ بِالرَّحْمَٰنِ ۚ {30}

Hivyo tumekutuma kwenye umati ambao wamekwisha kupita kabla yao umati zingine, ili uwasomee haya tunayokufunulia kwa njia ya wahy… (Sura ya 13; Aya ya 30)

إِنَّمَا أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ رَبَّ هَٰذِهِ الْبَلْدَةِ الَّذِي حَرَّمَهَا وَلَهُ كُلُّ شَيْءٍ ۖ وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُسْلِمِينَ {91}

وَأَنْ أَتْلُوَ الْقُرْآنَ ۖ فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ ضَلَّ فَقُلْ إِنَّمَا أَنَا مِنَ الْمُنْذِرِينَ {92}

Ama mimi nimeamrishwa nimuabudu Allah, Mlezi wa mji huu, -na niisome Qur’an: na mwenye kuongoka, basi ameongoka kwa faida ya nafsi yake mwenyewe, na mwenye kupotea, basi sema: “Hakika mimi ni miongoni mwa waonyaji.” (Sura ya 27; Aya ya 91 – 92)

قَدْ أَنْزَلَ اللَّهُ إِلَيْكُمْ ذِكْرًا {10}

الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۚ {11}

...Hakika Allah amekuteremshieni ukumbusho, Mtume, anayekusomeeni Aya za Allah zinazobainisha, Ili kuwatoa walioamini na wakatenda mema kutoka kwenye Giza, na kuwapeleka kwenye Nuru… (Sura ya 65; Aya ya 10-11)

Pia kuna onyo lifuatalo katika Qur’an Tukufu:

نَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ اللَّهِ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ ۗ وَاللَّهُ عَزِيزٌ ذُو انْتِقَامٍ {4}

…Hakika wale waliozikanusha Aya za Allah, watakuwa na adhabu kali (katika Akhera). Na Allah ni Mwenye Nguvu na Mwenye kulipiza kisasi. (Sura ya 3; Aya ya 4)

Ilikuwa ni kazi hii – Kusoma Aya za Allah (s.w.t.) – ambayo Ali ibn Abi Talib alitakiwa aitekeleze.

Kama ilivyoelezwa hapo juu, katika Dhil-Hija ya mwaka wa 9 H.A., Muhammad, Mtume wa Allah (s.w.t.), alikuwa na shughuli sana hivyo kutoweza kwenda Makka kutekeleza Hija, na kutangaza ile Surah ya Bara’a iliyoshuka karibuni. Kwa hiyo, kwa amri dhahiri ya Allah (s.w.t.), ilimbidi achague mtu mwingine wa kutekeleza kazi hii. Mtu aliyechaguliwa alikuwa ni Ali ibn Abi Talib.

Mnamo mwaka wa 8 H.A. (A.D. 630) wakati wa kutekwa Makka, Ali na bwana wake, Muhammad Mustafa waliitakasa Nyumba ya Allah (s.w.t.) (Al-Kaaba) kutokana na masanamu ya Waarabu. Ali aliyavunja masanamu yale vipande vipande, na akavitupa vipande hivyo nje ya Al-Kaaba.

Mnamo mwaka wa 9 H.A. (A.D.631), aliitakasa Al-Kaaba kutokana na waabudu masanamu wenyewe kwa kuwatangazia kwamba hawataruhusiwa tena kamwe kuingia katika maeneo yake matukufu.

Msimu wa hija wa mwaka wa 9 H.A, ulikuwa ndio mkusanyiko wa mwisho wa waabudu masanamu wa Arabia katika maeneo ya Al-Kaaba au hapo Makka.

Allah (s.w.t.) alimchagua Ali ibn Abi Talib kuirudisha Nyumba Yake (Al-Kaaba) kwenye hali yake ya utakaso wake wa asili, na akatuma Agizo maalum kwa Muhammad Mustafa, Mtume Wake, kufanya kusudi Lake lieleweke kwake (Ali). Ali, mtumwa wa Allah (s.w.t.) aliirudisha ile Nyumba Tukufu na Iliyobarikiwa kwenye hali ileile ambayo Mtume Ibrahim na Ismail (A.S) waliyoiacha nayo karne nyingi nyuma.

Katika kutangaza hapo Mina katika mwaka wa 9 H.A., ile Sera ya Dola ya serikali ya Kiislam, Ali alikuwa ndiye “Chombo” cha Allah (s.w.t.), kama vile katika mwaka wa 7 H.A., alivyokuwa “Mkono” wa Allah (s.w.t.) ambao uliiteka Khaybar kwa ajili ya Uislamu, na akaweka msingi wa Ufalme wa Mbinguni juu ya Ardhi. Kisa cha ushukaji na utangazaji wa Sura ya Bara’a (Sura ya 9 ya Qur’an Tukufu), kinadhihirisha kwamba:

1. Ali ibn Abi Talib ni mtu wa familia ya Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) aliyebarikiwa.

2. Kazi za Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) zinaweza kufanywa, katika kutokuwepo kwake, na Ali tu, na sio na mtu mwingine yoyote.

3. Mwakilishi au mshikamakamu wa Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) anaweza kuchaguliwa na Allah (s.w.t.) Mwenyewe au na Mtume Wake, lakini sio na umma wa Kiislam.

4. Ali ndiye mtu mwenye sifa stahilifu zaidi za kumuwakilisha Mtume wa Allah (s.a.w.) na hakuna mtu mwingine mwenye sifa bora zaidi kuliko yeye.

5. Kazi muhimu zaidi ya Mkuu wa Dola ya Kiislamu ni kutangaza Amri za Allah (s.w.t.) katika dunia hii. Ingawa Abu Bakr alikuwapo mahali hapo huko Makka, hakuruhusiwa kutangaza Amri za Allah (s.w.t.); bali Ali ibn Abi Talib ndiye aliyezitangaza.

Marmaduke Pickthall

Ingawa Makka ilikuwa imekwishatekwa na watu wake sasa walikuwa ni Waislamu, ile amri rasmi ya hija ilikuwa imebadilishwa; wapagani wa Kiarabu wakiifanya kati- ka namna yao na Waislamu kwa namna yao.

Ilikuwa ni baada tu ya msafara wa mahujaji ulipokuwa umeondoka Al-Madina katika mwaka wa tisa wa Hijiria, wakati Uislamu ulikuwa umetawala huko Arabia ya Kaskazini, ambapo lile Tangazo la Tauba, kama linavyoitwa, lilipoteremshwa.

Mtume (s.a.w.) alituma nakala yake kwa Abu Bakr, kiongozi wa hija, pamoja na maagizo kwamba Ali alikuwa ndiye alisome Tangazo hilo kwenye mkusanyiko wa watu uliokuwako huko Makka. Madhumuni yake yalikuwa kwamba baada ya mwaka ule Waislamu tu, ndio wafanye hija, nafasi zikiwa zimetolewa tu kwa waabudu masanamu kama wale ambao walikuwa na mkataba na Waislamu na hawajawahi kuvunja mkataba wao wala hawajawahi kumsaidia yeyote aliyekuwa dhidi yao (Waislamu). Hao walikuwa watumie fursa ya mkataba wao kwa muda ule, lakini mkataba wao utakapokwisha watakuwa kama waabudu-masanamu wengine. Tangazo lile linaweka mwisho wa uabudu masanamu katika Arabia. (Introduction to the Translation of Holy Qur’an, Lahore, Pakistan, 1975)
Yalikuwa ni mapenzi yake Allah (s.w.t.) kwamba mja Wake mpendwa, Ali ibn Abi Talib, aweze, kwa kusoma Tangazo Lake, kukomesha uabudu masanamu katika Arabia daima.

Msafara Wa Mwisho

Baada ya kutekwa kwa Makka makabila mengi ya kipagani yalikuja kuwa Waislamu kwa hiari, ambapo kuna mengine ambayo yaliingia Uislamu wakati Mtume (s.a.w.) alipotuma mubaligh wake kwao kuwaelekeza kwenye kanuni na matendo ya dini. Mmoja wa mubaligh wake alikuwa ni Ali ibn Abi Talib. Bwana wake alimtuma kwenda Yemen katika mwaka wa 10 H.A. kuyaalika makabila ya Yemen kwenye Uislamu.

Ingawa ule msafara wa mwisho ambao Mtume (s.a.w.) aliuandaa ulikuwa ni ule ambao ulikuwa utumwe kwenda kwenye mpaka na Syria chini ya uongozi wa Usama bin Zayd bin Haritha, haukuondoka kamwe Madina katika wakati wa uhai wake. Kwa hiyo, ule msafara wa Ramadhani ya mwaka wa 10 H.A. ambao aliutuma Yemen chini ya uongozi wa Ali, ulikuwa ndio wa mwisho ambao hasa uliondoka Madina alipokuwa bado yuko hai.

Ali aliwasili Yemen pamoja na wapanda farasi wake katikati ya kipupwe, na aliwalingania watu wa kabila la Madhhaj kuukubali Uislamu, lakini walimjibu kwa mfululizo wa mishale na mawe ambapo na yeye aliviashiria vikosi vyake vifanye mashambulizi. Waliwashambulia wale watu wa kabila na kuwashinda lakini hawakuwafukuza kwa sababu ujumbe wa Ali ulikuwa wa amani na sio wa vita. Amri zake kwa vikosi vyake zilikuwa ni kupigana tu katika kujihami wenyewe.

Madhhaj waliomba amani ambayo Ali bila kusita aliwapatia, na akatoa mwaliko wake upya kwao kuukubali Uislamu. Safari hii wao na pia kabila la Hamdan waliitikia mwito wake, na wakasilimu. Ujumbe wa Ali ulifanikiwa. Yemen yote wakawa Waislamu kwa kupitia juhudi zake. Alitekeleza ujumbe wake, kama kawaida, kwa ustadi mzuri sana na kujiamini, na akadhihirisha kwamba alikuwa ndiye mubaligh wa Uislamu kwa uwezo halisi.

M. Shibli

Kikundi chenye nguvu sana na chenye uwezo huko Yemen kilikuwa kiliundwa na jamaa wa kabila la Hamdan. Mwishoni mwa mwaka wa 8 H.A., Mtume (s.a.w.) alimtuma Khalid bin Walid kuwalingania kwenye Uislamu. Khalid alikaa miezi sita miongoni mwao akihubiri Uislamu lakini hakuweza kupata wafuasi wapya wowote, na ujumbe wake ulishindwa. Alikuwa ni jenerali na mtekaji lakini sio mhubiri na mubaligh. Mwishowe Mtume (s.a.w.) alimwita arudi Madina, na badala yake, akamtuma Ali ibn Abi Talib.

Ali aliwakusanya watu wa kabila la Hamdan katika bonde, akasoma mbele yao ule ujumbe wa Mtume wa Allah (s.a.w.) na akawafikishia Uislamu. Safari hii waliitika – kwa kuukubali Uislamu. Kabila zima, wote wakawa Waislamu.

Ali alituma taarifa juu ya matokeo ya ujumbe wake kwa Mtume (s.a.w.) huko Madina. Wakati Mtume (s.a.w.) alipoisoma taarifa hiyo, alimshukuru Allah (s.w.t.) kwa Rehema Zake, na akinyanyua macho yake kuelekea juu Mbinguni, akaomba baraka juu ya kabila la Hamdan. Hili alilifanya mara mbili.
(Sira-tun-Nabi, Juz.11, (Toleo la 10) 1974, Chapa ya Ma’arif Printing Press, Azamgarh,India).

Katika miaka kumi ya mwisho ya maisha yake, Mtume (s.a.w.) wa Uislamu aliandaa misafara themanini ambayo iliondoka Madina kwa shughuli mbalimbali - mingine ya kivita na mingine ya amani. Msafara wa Ali kwenda Yemen ni wa manufaa maalum kwa sababu ulikuwa ni wa mwisho wa yote. Hakuna msafara mwingine ulioondoka Madina katika uhai wa Mtume.

Mwaka wa 10 H.A. (631A.D.) unaitwa ‘Mwaka wa Wajumbe’. Makabila mengi ya Kiarabu yalituma wajumbe huko Madina kwa kuukubali Uislamu, na kumpa Muhammad Mustafa kiapo chao cha utii kama mtawala wao wa kidunia.

Katika mwaka wa kwanza wa Hijiria (A.D. 622) Madina ilikuwa na hadhi ya Serikali ya Jiji lakini kwa miaka kumi ilikuwa imechipuka kuwa makao makuu ya Serikali ya “Taifa”. Peninsula yote ilikuwa imekubali mamlaka yake ya kiroho na kidunia.
Muhammad Mustafa, (Rehema Allah (s.w.t.) ziwe juu yake na juu ya kizazi chake), alikuwa amesi- mamisha amani ya ndani katika nchi nzima, na alikuwa amechukua hatua zenye nguvu kulinda maslahi ya “Kitaifa” ya umma wa Kiislamu. Hakukuwa na tishio kwenye usalama wa Dola ya Kiislamu kutokana na uvamizi wowote wa nje.

Wayahudi na Wakristo walilkuwa wanalipa kodi au ushuru (Jizya). Walikuwa wanafaidika na haki zote za uraia wa Dola ya Kiislamu, na walikuwa wakifaidi uhuru kamili wa kidi- ni. Waarabu, wengi wao sasa wakiwa wamesilimu na kuwa Waislamu, walikuwa katika mkesha wa ufufukaji wa “Kitaifa” wenye nguvu. Kulikuwa na chache tu ya neema zisizo na idadi ambazo Uislamu ulizileta kwenye peninsula ya Arabia.