read

Kutawazwa Kwa Ali Ibn Abi Talib Kama Mtawala Wa Baadae Wa Waislamu, Na Kama Kiongozi Wa Umma Wa Kiislam

Hija ya mwisho ilikuwa imekwisha, na Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) na lile kundi kubwa la wafuasi wake, walikuwa sasa wako tayari kurudi majumbani kwao. Alitoa ishara na ile misafara ya mahujaji ikaanza kuondoka Makka.

Katika kipande kifupi upande wa kaskazini ya Makka, kuna bonde linaloitwa Khumm, na huko Khumm kulikuwa na kisima au bwawa la maji (Ghadiir). Khumm ipo katika maku- tano ya njia nyingi. Wakati Mtume (s.a.w.) alipowasili katika ujirani wa Ghadiir, alipokea ujumbe mpya – wahy unaofuata kutoka Mbinguni:

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنْزِلَ إِلَيْكَ مِنْ رَبِّكَ ۖ وَإِنْ لَمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ ۚ وَاللَّهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ ۗ إِنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ {67}

Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako. Na kama hutafanya hivyo, basi utakuwa kama hujafikisha ujumbe Wake wowote. Na Allah atakulinda na watu. Hakika Allah hawaongoi watu makafiri. (Sura ya 5; Aya ya 67)

Agizo la Mbinguni lilikuwa mara chache, kama ilikuwa, ni yenye kuamrisha hivyo, kama ilivyo kwenye Aya hii, na ilihusishwa, dhahiri kabisa, kwenye jambo lenye umuhimu sana ambalo Mtume (s.a.w.) ilimbidi ajieleze mwenyewe – hapo hapo.

Yeye, kwa hiyo, aliamu- ru mwenyewe msafara wake usimame, na aliirudisha misafara yote ambayo ilikuwa imek- wenda ama mbele au imekwenda pande zingine tofauti tofauti. Yeye mwenyewe alisubiri mpaka msafara wa mwisho ambao ulikuwa umeondoka Makka, pia umewasili jirani na kisiwa cha Khumm.

Mahujaji walikuwa wakagawanyike hapo Khumm kwenye misafara yao tofauti na walikuwa wakatawanyike, kila mmoja akielekea aendako. Mtume (s.a.w.) alikuwa na tangazo muhimu sana la kutangaza kabla ya kutawanyika kwa mahujaji, na alikuwa na shauku sana kwamba idadi kubwa kabisa ya Waislamu walisikie kutoka kwake.

“Mimbari” ilitengenezwa kwa haraka bila vifaa maalum kwa matandiko ya ngamia, na Mtume (s.a.w.) akapanda juu yake ili kwamba kila mtu kwenye ule mkusanyiko mkubwa aweze kumuona yeye kwa macho yake mwenyewe. Binamu yake, Ali, alikuwa amesimama karibu yake.

Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) alikuwa sasa yuko tayari kutoa lile tangazo la kihistoria katika kutimiza lile agizo tukufu lililonukuliwa hapo juu. Alimshukuru Allah (s.w.t.) kwa ile Neema kubwa ya Uislamu, na kwa Rehema Zake na Wema Wake, na kisha akauliza swali hili kwa Waislamu:

“Je, ninayo haki au sina haki kubwa zaidi juu ya nafsi zenu kuliko ninyi wenyewe mliyonayo juu yake?”

Waislamu wakajibu kwa sauti moja: “Mtume wa Allah anayo haki kubwa juu ya nafsi zetu kuliko sisi wenyewe tuliyonayo juu yake (hiyo nafsi).” “Kama hivyo ndivyo,” alisema, “basi ninao ujumbe muhimu sana wa kufikisha kwenu,” na akauelewesha ujumbe huo kama ifuatavyo:

“Enyi Waislamu! Mimi ni binadamu kama ninyi, na ninaweza kuitwa hivi karibuni mbele ya Mola wangu. Urithi wangu wa thamani sana kwenu ni Kitabu cha Allah (s.w.t.) na watu wa Nyumbani kwangu, kama nilivyowaambieni kabla. Sasa sikilizeni hili kwa makini kwamba mimi ni Bwana (Maula) wenu ninyi wote – wa Waumini wote.
Wale wanaume na wanawake wote wanaonikubali mimi kama Bwana wao, ninawataka wamkubali (hapa aliushika mkono wa Ali na akaunyanyua juu zaidi ya kichwa chake) Ali pia kama Bwana (Maula) wao. Ali ni Bwana wa wale wanaume na wanawake wote ambao mimi na Bwana wao.”

Alipokwisha kuutoa ujumbe huu, Muhammad Mustafa alinyanyua mikono yake kuelekea juu mbinguni, na akasema: “Ewe Allah sw! Kuwa Rafiki wa yule ambaye ni rafiki wa Ali, na kuwa ni Adui wa yule ambaye ni adui yake. Msaidie yule anayemsaidia Ali, na umtelekeze yule anayemtelekeza yeye Ali.”

Uliopita ni mukhtasari wa yale ambayo Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) aliyoyasema hapo Khumm. Maneno halisi na muktadha wa hotuba yake yamehifadhiwa katika kile kitabu maarufu Taudih-ed-Dala’il kilichoandikwa na profesa mkubwa wa Kisunni, Allamah Shahab-ud-Diin Ahmed. Ufuatao ni ufupisho wa hotuba hiyo kama ilivyoandik- wa katika Taudih-ed-Dalai’l:

Ninatoa sifa na shukurani kwa Allah (s.w.t.) kwa neema Zake zote. Nashuhudia kwamba hapana Mola ila Allah (s.w.t.) na Yeye ni Mmoja, Mwenye Nguvu zote, Mkamilifu. Wote tunamtegemea Yeye. Yeye hana mke, hana mtoto, hana washirika. Mimi ni mmoja wa waja Wake lakini Yeye amenichagua mimi kama Mtume Wake kwa ajili ya uongofu kwa wanadamu. Enyi watu! muogopeni Yeye katika nyakati zote na kamwe msimuasi Yeye. Msipigane ila kwa ajili ya Uislamu, na kumbukeni kwam- ba elimu ya Allah (s.w.t.) imekizunguka kila kitu.

Enyi Waislamu! tahadharini kwamba wakati nitakapokuwa nimeondoka, watatokea watu ambao watahusisha Hadith za uongo kwangu mimi na watakuwepo watu wengine watakaoziamini hizo.

Lakini ninaomba ulinzi wa Allah (s.w.t.) kwamba nisi- je kamwe kusema kitu chochote bali Ukweli na kuwaiteni kwenye lolote ila kile Yeye alichoteremsha kwangu. Wale wanaovuka mipaka katika jambo hili, watapata adhabu.

Kufikia hapa sahaba mmoja, Ibada ibn Samit, alisimama na akauliza: “Ewe Mtume wa Allah (s.w.t.)! wakati huo utakapofika, ni nani tutakaye muangalia kwa ajili ya mwongozo?”

Mtume wa Allah (s.w.t.) alijibu kama ifuatavyo:

“Muwafuate na kuwatii ‘Watu wa Nyumba yangu’ (Ahlul-Bait).” Wao ndio warithi wa elimu yangu ya kinabii na utume. Watawaokoeni kutokana na upotovu, na watawaongozeni kwenye uongofu. Watawalinganieni kwenye Kitabu (Qur’an Tukufu) na Sunnah yangu. Wafuateni hao kwa sababu hawana shaka kamwe juu ya jambo lolote. Imani yao juu ya Allah (s.w.t.) haiyumbi. Wao ndio wale walioongozwa sawasawa; wao ndio wale Maimamu, na ni wao peke yao wanaoweza kuwaokoeni kutokana na ukafiri, uasi na uzushi.

Allah (s.w.t.) amekuamuruni kuwapenda Ahlul-Bait wangu. Utii kwao umefanywa ni lazima juu yenu (Qur’an Tukufu: Sura ya 42; Aya ya 23). Wao ndio wale walio- takaswa (Qur’an Tukufu Sura ya 33; Aya ya 33). Ndio wale waliopewa uadilifu na ubora ambao hakuna mtu mwingine yoyote aliyenao. Wao ndio Wateule wa Allah (s.w.t.) Mwenyewe.

Sasa nimeamriwa na Allah (s.w.t.) kutoa tangazo hili: Hapa aliushika mkono wa Ali, akaunyanyua juu kabisa, na akasema: “Fahamuni ninyi wote, yeyote yule ambaye mimi ni Maula (Bwana) wake, Ali ni Maula (Bwana) wake. Ewe Allah! Kuwa Rafiki wa yule ambaye ni rafiki wa Ali, na kuwa Adui kwa yule ambaye ni adui wa Ali. Ewe Allah! Msaidie yule anayemsaidia Ali, na mtelekeze yule anayemtelekeza Ali.”

Hotuba ilikwisha. Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.w.t.) alikuwa kiutaratibu na kirasmi amekwisha kumtangaza Ali ibn Abi Talib kuwa Mkuu wa Waislamu wote, na amemteua kama kiongozi wa Dola na Serikali ya Kiislamu.

Mara tu baada ya kutolewa tangazo hili, Aya nyingine, Aya ya mwisho ya Qur’an Tukufu, iliteremshwa kwa Muhammad. Inasomeka kama ifuatavyo:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ {3}

Leo hii nimekukamilishieni dini yenu, na Nimekutimizieni Neema Yangu, na Nimekuchagulieni Uislamu kuwa dini yenu. (Sura ya 5; Aya ya 3)

Ilikuwa ni siku ya 18 ya mwezi wa 12 wa mwaka wa 10 wa kalenda ya Kiislam (Machi 21, 632) wakati Aya ya mwisho ya Ufunuo ilipoteremshwa duniani hapa. Wahy ulikuwa umeanza mwaka 610 A.D., katika pango la Hira huko Makka, na ulifikishwa mwisho mwaka 632 A.D., katika bonde la Khumm kwa tangazo kwamba Ali ibn Abi Talib atakuwa ndiye Mtekelezaji Mkuu, baada ya Muhammad mwenyewe, wa Serikali ya Madina na Dola ya Kiislamu.

Ibn Hajar Asqalani anaandika katika Isaba kwamba baada ya kutoa tangazo hili, Mtume wa Allah (s.a.w.) aliweka kilemba juu ya kichwa cha Ali ibn Abi Talib, na hivyo kukamilisha kutawazwa kwake.

Masahaba wote walimpongeza Ali katika tukio hili tukufu wakati Mtume wa Allah (s.a.w.) mwenyewe alipomtawaza yeye na kumtangaza kama mshikamakamu na mrithi wake. Miongoni mwa wale ambao walimpongeza walikuwa Umar bin al-Khattab na wake za Mtume.

Hasan bin Thabit Ansari alikuwa ndiye mshairi wa baraza la Mtume, na alitungia mashairi matukio yote muhimu. Kutawazwa kwa Ali kulikuwa ni moja kati ya matukio ya kihistoria sana ambayo yalikitia changamoto kipawa chake cha ushairi. Alitunga wimbo wa sifa ambao aliutoa kwa heshima ya Ali.

Ifuatayo ni tarjuma ya haraka haraka ya beti zake:

Katika siku ya Ghadir Khumm, Mtume (s.a.w.) na Waislamu aliwaita, na nilimsikia wakati yeye aliposema: “Ni nani Mola wenu, na ni nani Bwana wenu?” Wote wakasema: “Allah (s.w.t.) ndiye Mola wetu, na wewe ndiye Bwana wetu, na hakuna yeyote kati yetu anayeweza kukukaidi wewe.”

Hivyo alimuomba Ali asimame. Wakati Ali aliposimama, aliushika mkono wake, na akasema:
“Nakuchagua wewe kama kiongozi baada yangu. Kwa hiyo, yeyote yule ambaye Bwana wake ni mimi,
Ali ni Bwana wake pia. Kwa hiyo, nyote nyie muwe marafiki zake wa kweli na wafuasi wake.”

Mtume (s.a.w.) kisha akaomba, akisema: “Ewe Allah! kuwa Rafiki kwa wale ambao ni marafiki wa Ali; na kuwa Adui wa wale ambao ni maadui zake.”

Mshairi mwingine ambaye alitunga mashairi katika tukio la kutawazwa kwa Ali, alikuwa ni Qays ibn Ubada Ansari. Alisema:

Wakati maadui walipoasi dhidi yetu, nilisema kwamba Mpaji wetu, Allah (s.w.t.) anatutosha sisi, na Ndiye Mlinzi bora tunayeweza kuwa naye.

Ali ni Bwana wetu na ni bwana wa waumini wote. Hili linathibitishwa na Qur’an Tukufu na ni hivyo tangu ile siku Mtume wa Allah (s.a.w.) aliposema: “Yeyote yule ambaye Bwana wake ni mimi, Ali ni Bwana wake pia” Hili kwa hakika lilikuwa ni tukio la kufahamika sana.

Chochote kile Mtume wa Allah (s.a.w.) alichokisema siku ile, ni mwisho; ndio neno la mwisho, na hakuna kabisa nafasi ya hoja yoyote ndani yake.

Kwa mshangao na kutosadikika, hata mtu kama Amr bin Al-Aas “alitiwa moyo” kutoa shairi kwa heshima ya Ali hapo Ghadir Khumm. Ifuatayo ni mistari miwili ya utunzi wake:

Pigo la upanga wa Ali ni kama kile kiapo cha utii ambacho kila mmoja alikichukua ile siku ya Ghadir, na ambacho kilimfanya kila mtu kusalimu amri mwenyewe mbele ya mamlaka yake (mapya).

Kama hizo Aya mbili za Qur’an zinazohusu kutawazwa kwa Ali, zitasomwa katika utaratibu wa mpango wake, na katika fuo lake la kihistoria, maana zao zitakuwa wazi.

Nitazinukuu mara nyingine tena katika uchambuzi mfupi; na kwa wepesi wa rejea, nitaziita Aya ya kwanza na ya pili.

1. Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako. Na kama hutafanya hivyo, basi utakuwa kama hujafikisha ujumbe Wake wowote. Na Allah atakulinda na watu. Hakika Allah hawaongoi makafiri.

2. Leo hii Nimekukamilishieni dini yenu na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuchagulieni Uislamu kuwa dini yenu.

Kutawazwa kwa Ali kulitokea ndani ya mfumo wa Aya hizi mbili za Qur’an. Kutawazwa kwake kulikuwa ni jambo lenye mkazo kiasi kwamba Muhammad Mustafa, Mpokezi wa Wahy, aliamriwa, katika Aya ya kwanza, kusimamisha chochote alichokuwa anakifanya, na ashuhulishwe kwanza na hilo. Yeye, kwa hiyo, aliwaamuru mahujaji wote wakusanyike katika bonde la Khumm, na akawaambia kwamba Ali atawatawala wao kama mrithi wake katika Ufalme wa Mbinguni katika Ardhi.

Mara tu Mtume (s.a.w.) alipokwisha kufanya hivyo, kisha hii Aya ya pili ilishushwa kama ishara ya idhini ya Mbinguni ya kitendo chake. Kutangazwa kwa Ali kama mrithi wake kulikuwa ndio ukamilisho na kilele cha kazi ya maisha ya Muhammad. Kwa tangazo hili, kazi yake kama Mtume wa Allah (s.a.w.) ilikamilika. Alikuwa amemtangaza Ali kuwa mrithi wake kwenye matukio mengi wakati uliopita lakini pale Ghadir-Khumm, alimtawaza rasmi kama Kiongozi wa Umma wa Kiislamu wa baadae.

Kati ya Aya hizi mbili za Qur’an–moja yenye nguvu sana katika kudai kitendo na ile nyingine ikiwa dhahiri mno katika kuthibitisha kwake usimikwaji wa Ali kama mrithi wa Mtume (s.a.w.) – na kauli ya Mtume: “Ali ni Bwana wa wale wanaume na wanawake wote ambao mimi ni Bwana wao,” kuna uwiano wa kimantiki na wa dhahiri.

Walaghai wengine wamejadili bila msingi hili neno Maula kama lilivyotumiwa na Mtume (s.a.w.) wakati aliposema: “Ali ni maula wa wale wanaume na wanawake ambao mimi ni maula wao. Wanakubali kwamba kauli hiyo ni halisi lakini wanalitafsiri neno maula sio kama “Bwana” bali ni kama “rafiki.” Lakini hii haikuwa ndio dhimiri ya Mtume (s.a.w.) mwenyewe. Hivi aliirudisha ile misafara yote na kuwaamuru wakusanyike katika lile bonde la Khum lisilo na kivuli kwa ajili tu ya kuwaambia kwamba Ali ni rafiki yao? Je, ilichukuliwa na maswahaba wakati ule kwamba Ali hakuwa rafiki yao, na Mtume (s.a.w.) ikambidi awahakikishie wao kwamba yeye (Ali) kwa kweli alikuwa ni rafiki yao?

Wale watu wanaolitafsiri hili neno maula kama “rafiki,” labda wanasahau kwamba Mtume (s.a.w.) alilitumia kwa kujihusisha yeye mwenyewe kabla hajalitumia kumhusu Ali, na hili linaweza kuruhusu tu tafsiri moja sahihi, ndio kusema, kama Muhammad, Mtume, ndiye Bwana wa Waislamu wote, Ali pia ni Bwana wao.

Walaghai hao pia wanasahau kwamba kabla ya kumtangaza Ali kama mrithi wake na mkuu wa Waislamu wote, Mtume (s.a.w.) alikwisha kuwauliza swali lifuatalo:

“Ninayo au sinayo haki kubwa zaidi juu ya nafsi zenu kuliko mliyonayo ninyi wenyewe juu yenu?”

Jibu la Waislamu kwa swali hili lilikuwa ni “ndio” isiyo na kifani. Swali hili lilikuwa ni la utangulizi wa tangazo la Mtume (s.a.w.) kwamba Ali alikuwa ndiye mrithi wake. Hilo swali na hilo tangazo vilikuwa ni sehemu ya muktadha huo huo, na kama vikisomwa pamoja, havitaacha shaka yoyote akilini mwa msomaji kwamba hili neno maula maana yake ni “Bwana” na sio “rafiki.”

Wengi wa wafasiri wa Ki-Sunni wamekubali kwamba ile amri ya Allah (s.w.t.) kwa Mtume Wake katika ile Aya ya kwanza inafungamana hasa na tangazo kwamba Ali ndiye Mkuu wa Waislamu wote. Baadhi ya wafasiri hawa ni:

Wahidi katika Asbab-un-Nuzuula Suyuti katika Tafsir Durr al-Manthur Ibn Kathir
Imam Ahmad bin Hanbal
Abu Ishaq Nishapuri
Ghazali katika Sirrul-Alamiin
Tabari katika Tarikh-ar-Rusul wal-Muluuk
Sheikh Abdul Haq Muhaddith wa Delhi, India
Hapa ni lazima pia ielezwe kwamba kabla ya kushushwa kwa Aya hiyo ya kwanza (5:67), amri zote zinazohusika na Shari’ah (mfumo wa kanuni na taratibu za dini ya Kiislam), kama vile Sala za kila siku, Funga, Zaka, Hajj (kwenda Hija Makka), na Jihad – kwa hakika zile sheria zote kwa maisha ya mtu binafsi, kijamii, kiuchumi na kisiasa za Waislamu, zilikuwa tayari zimekwisha kutolewa kwa Muhammad. Alikuwa amekwisha zifikisha, na Waislamu walikuwa wakizifanyia kazi, na zimekuwa sehemu muhimu za maisha yao. Alikuwa amekwisha kutambulisha na kutekeleza kila sheria.

Kitu pekee ambacho Mtume (s.a.w.) alikuwa bado hajakifanya hadi kufikia wakati huo, kilikuwa ni kumtambulisha rasmi kwa umma wake, mrithi wake mwenyewe. Umma huo ulikuwa unayo haki ya kujua ni nani atakayekuwa mtawala wake baada ya kifo chake (yeye Mtume). Hiki ndicho alichokifanya wakati alipoamriwa “kufikisha ujumbe.” Hii amri ya Allah (s.w.t.) ilikuwa na nguvu sana, na Mtume (s.a.w.) hakuweza kuahirisha utekelezaji wake kwa muda mwingine.

Lakini mara tu baada ya Mtume (s.a.w.) kutekeleza ile amri ya mbingnii, kwa uwazi kamili na kwa uamuzi wa mwisho kabisa, ile Aya ya pili (5:3) iliteremshwa, na iliweka muhuri wa uthibitisho juu ya kitendo chake.

Kwa usimikwaji rasmi wa Ali ibn Abi Talib kama mrithi wa Muhammad na kama kiongozi wa Waislamu wote, imeandikwa katika Aya za mwisho zilizoteremshwa kwenye Kitabu cha Allah (s.w.t.).

Aya ya mwisho ya Kitabu cha Allah (s.w.t.) ilishushwa na iliandikwa mnamo Machi 21, 632, kama ilivyoelezwa kabla, na mlango wa Wahy ukafungwa milele. Siku themanini baadae, yaani, mnamo Juni 8, 632, Muhammad Mustafa aliagana na umma wake, na akaenda mbele ya Mola wake. Hakuna kumbukumbu kwamba aliupa umma wake amri mpya zozote au makatazo (Awamir au Nahawi), ya mafundisho au ya vitendo, katika muda wa hizi siku 80. Uislamu ulitangazwa kuwa umekamilika na kutimia mara tu baada ya Mtume Wake kumteua Ali ibn Abi Talib kuwa mrithi wake.

Allah (s.w.t.) awazidishie waja Wake, Muhammad na Ali, na watu wa familia zao, Fadhila Zake, na Neema na Baraka Zake.

Muhammad Mustafa angeweza sasa kuangalia nyuma kwa kuridhika juu ya kazi yake, na angeweza kuangalia mbele kwenye wakati ujao kwa matumaini mapya, kwa kujiamini na furaha. Kwa kumuweka Ali kama mrithi wake, aliuona uendeleaji wa ile kazi ambayo kwayo alitumika bila kujizuia kwa miaka 23, na ambayo ilikuwa imejaa vitisho na hatari nyingi. Kazi yake imehitaji mihanga isiyo na idadi kwa upande wake. Sasa ilionekana kwake kwamba zile suluba zake zote na ile mihanga mwishowe imezaa matunda, kwa vile alijua kwamba Ali atakiendesha chombo cha Uislamu kule kiendako kwa ustadi uleule kama yeye mwenyewe alivyofanya.

Muhammad hakumchagua Ali kuwa mrithi wake kwa sababu tu kwamba alikuwa binamu yake, mkwewe, na sahaba wake mpendwa; wala hakumchagua kwa sababu ya sifa binafsi zake yeye Ali. Muhammad alikuwa na kidogo sana cha kufanya na uchaguzi wake. Mpangilio wa muda wa kushuka kwa Aya hizi mbili za mwisho za Qur’an Tukufu (5:67 na 5:3), na matukio yaliyopita wakati wa muda baina ya wahy hizi mbili, na uwiano wao, vinamuongoza mfuatiliaji kwenye hatima moja tu, yaani, uchaguzi wa Ali kama mrithi wa Mtume (s.a.w.) wa Uislamu, ulifanyika Mbinguni. Allah (s.w.t.) Mwenyewe aliyemchagua Ali.

Allah (s.w.t.) asingeweza kuchagua wa tatu au wa pili. Angeweza kuchagua tu yule msafi sana, mbora, wa kipekee kabisa, kama alivyokuwa Ali. Ali alikuwa ndio alama na kielelezo dhahiri cha Ukweli wa Uislamu, na alikuwa ndiye shahidi wa kwanza wa Ukweli wa Mtume (s.a.w.) wa Uislamu. Allah (s.w.t.) awabariki wao wote na familia zao.

Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) alitumia kila nafasi kutaka uangalifu wa Waislamu kwenye daraja tukufu ya Ali. Katika moja ya Hadithi zake mashuhuri (kauli, simulizi), alisema kwamba uhusiano wake na Ali ulikuwa ni sawa na ule wa watangulizi wake wa kinabii – Musa na Harun – pamoja na tofauti tu kwamba Ali hakuwa ni Mtume.

Hadithi hii ilisimuliwa na Saad bin Abi Waqqas, na imeandikwa na Imam Muslim katika Sahihi yake kama ifuatavyo:

Amir bin Sa’d bin Abi Waqqas amesimulia kutoka kwa baba yake kwamba Mtume wa Allah (s.w.t.) (amani iwe juu yake) akimwambia Ali alisema: “Unayo daraja ileile katika uhusiano na mimi kama Harun aliyokuwa nayo kwa Musa lakini pamoja (na tofauti hii ya wazi) kwamba hakuna nabii baada yangu.” Sa’d akasema:

“Nilikuwa na hamu kubwa ya kuisikia moja kwa moja kutoka kwa Sa’d, hivyo nilikutana naye na nikamweleza kile ambacho Amir (mwanae) alikuwa amenisimulia, ndipo akasema: “Ndio, niliisikia.” Mimi nikasema: “Uliisikia wewe mwenyewe?” Hapo akaweka vidole vyake juu ya masikio yake na akasema: “Ndio, na kama sivyo, basi masikio yangu yote nayazibe kabisa.”

Sa’d bin Abi Waqqas amesimulia kwamba Mtume wa Allah (s.w.t.) (amani iwe juu yake) alimuacha Ali ibn Abi Talib nyuma yake alipokuwa anakwenda Tabuk, ambapo yeye (Ali) alisema: “Ewe Mtume wa Allah, unaniacha mimi hapa pamoja na wanawake na watoto?” Hapo Mtume (s.a.w.) akasema: “Huridhiki wewe kuwa kwangu mimi kama alivyokuwa Harun kwa Musa bali kwa tofauti kwamba hakutakuwa na nabii baada yangu mimi?”

Hadithi hii imesimuliwa kutoka kwa Shu’ba kwa sanadi ileile ya wapokezi. Amir bin Sa’d bin Abi Waqqas amesimulia kutoka kwa baba yake kwamba Mu’awiyyah bin Abu Sufyan alimteua Sa’d kama gavana na akasema: “Ni nini kinachokuzuia kumtukana Abu Turab (Ali)?” Akasema: “Ni kwa sababu ya mambo matatu ambayo nilimsikia Mtume wa Allah (s.w.t.) akiyasema juu yake ambayo kwayo sintamtukana yeye, na kama ingekuwa nipate hata moja tu ya yale mambo matatu, lingekuwa na thamani sana kwangu kuliko ngamia wekundu. Nilimsikia Mtume wa Allah (s.w.t.) akisema kuhusu Ali pale alipomuacha yeye (huko Madina) wakati alipokuwa anakwenda kwenye msafara (Tabuk).

Ali alimwambia: “Ewe Mtume wa Allah (s.w.t.) hivi unaniacha mimi hapa na wanawake na watoto.?” Hapo Mtume wa Allah (s.w.t.) akamwambia: ‘Hivi huridhiki wewe kuwa kwangu mimi kama Haroun alivyokuwa kwa Musa bali pamoja na tofauti kwamba hakuna utume baada yangu?’ Na mimi pia nilimsikia akisema ile Siku ya Khaibar: ‘Nitampa bendera hii mtu ambaye anampenda Allah (s.w.t.) na Mtume Wake, na ambaye Allah (s.w.t.) na Mtume Wake wanampendwa.’ Yeye (msimuliaji) akasema: Tulikuwa tunaisubiri kwa hamu sana wakati yeye (Mtume) aliposema: ‘Mwiteni Ali.’ Alikuja na macho yake yalikuwa yanawasha. Alimuweka mate kwenye macho yake na akampa ile bendera, na Allah (s.w.t.) akampa ushindi..

Safari ya tatu ilikuwa ni wakati Aya ifuatayo iliposhuka:
“…Tuwaite watoto wetu na watoto wenu…”

Mtume wa Allah (s.a.w.) alimwita Ali, Fatima, Hasan na Husein na akasema:
“…Ewe Allah! Hawa ndio watu wa familia yangu…”

Hadithi ya Mtume (s.a.w.) ambamo amesema kwamba Ali alikuwa kwake kama Harun alivyokuwa kwa Musa, inakubaliana na Aya za Qur’an Tukufu zifuatazo:

(Musa aliomba):
“Ewe Mola wangu! Nikunjulie kifua changu;
Niwepesishie kazi yangu;
Na uniondolee vifundo kwenye ulimi wangu; Wapate kuyaelewa maneno yangu;
Na unipe waziri katika familia yangu; Harun, ndugu yangu,
Kwake yeye uniongezee nguvu zangu, Na umshirikishe katika kazi yangu:
Ili tukutukuze sana;
Na tukukumbuke sana; Hakika Wewe unatuona sisi.”

(Allah (s.w.t.)) Akasema:

قَالَ قَدْ أُوتِيتَ سُؤْلَكَ يَا مُوسَىٰ {36}

وَلَقَدْ مَنَنَّا عَلَيْكَ مَرَّةً أُخْرَىٰ {37}

“Hakika umekubaliwa maombi yako, Ewe Musa!” Na hakika tulikwisha kukufanyia hisani juu yako mara nyingine kabla. (Sura ya 20; Aya ya 36 hadi 37)
Nabii Musa (a.s.) alimuomba Allah (s.w.t.) ampatie Waziri kutoka kwenye familia yake mwenyewe. Hakutaka waziri kutoka miongoni mwa maswahaba na marafiki zake. Aliomba kwamba Harun, ndugu yake, awe ndiye Waziri wake, na angekuwa ni chanzo cha nguvu kwake.

Allah (s.w.t.) alijibu du’a ya Mtume Wake Musa, akampa ndugu yake, Harun, kama waziri wake, na akamfanya kuwa chanzo cha nguvu kwake.

Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Mwisho wa Allah, pia alichagua waziri wake kutoka kwenye familia yake mwenyewe. Chaguo lake lilikuwa ni Ali, ndugu yake. Ali aliongeza nguvu zake, na alishiriki kwenye kazi yake pamoja naye, kama vile ambavyo aliahidi kufanya, miaka mingi iliyopita, katika karamu ya Dhu’l-‘Ashiira huko Makka katika mkusanyiko wa wazee wa koo za Bani Hashim na Bani Muttalib.

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ وَجَعَلْنَا مَعَهُ أَخَاهُ هَارُونَ وَزِيرًا {35}

(Kabla ya hapa) Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamweka pamoja naye, nduguye Haroun, kuwa waziri. (Sura ya 25; Aya ya 35)

Allah (s.w.t.) Mwenyewe alimchagua Harun kuwa Waziri. Haukuwa umma (watu) wake Musa ambao walimchagulia Waziri wake.

وَوَاعَدْنَا مُوسَىٰ ثَلَاثِينَ لَيْلَةً وَأَتْمَمْنَاهَا بِعَشْرٍ فَتَمَّ مِيقَاتُ رَبِّهِ أَرْبَعِينَ لَيْلَةً ۚ وَقَالَ مُوسَىٰ لِأَخِيهِ هَارُونَ اخْلُفْنِي فِي قَوْمِي وَأَصْلِحْ وَلَا تَتَّبِعْ سَبِيلَ الْمُفْسِدِينَ {142}

Tulimuahidi Musa masiku thelathini, na tukayatimiza kwa kumi zaidi: Hivyo ikatimia ahadi ya Mola wake, masiku arobaini. Na Musa akamwambia ndugu yake Harun (kabla ya kuondoka): Shika mahala pangu miongoni mwa watu wangu; ufanye haki na wala usifuate njia ya waharibifu. (Sura ya 7; Aya ya 142)

Musa alimweka ndugu yake, Harun, kwenye madaraka juu ya umma (watu) wake, na hakuuacha (huo umma) bila ya kiongozi ingawa alikuwa anaondoka kwa siku arobaini tu.

Muhammad Mustafa (rehma na amani ziwe juu yake na kizazi chake) hakukengeuka kwenye mwenendo huu wa manabii na mitume wa Allah (s.w.t.) Yeye pia hakuwaacha Waislamu bila ya kiongozi, na alimchagua ndugu yake, Ali, kama kiongozi na mtawala wao baada yake.

Musa aliomba:

قَالَ رَبِّ اغْفِرْ لِي وَلِأَخِي وَأَدْخِلْنَا فِي رَحْمَتِكَ ۖ وَأَنْتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ {151}

“Ewe Mola wangu! Nisamehe mimi na ndugu yangu! Na utuingize katika Rehema Yako! Kwani Wewe ni Mwenye kurehemu kuliko wote wenye kurehemu. (Sura ya 7; Aya ya 151)

Musa hakujiombea yeye peke yake tu; alimuombea ndugu yake Harun pia. Muhammad Mustafa pia aliombea wote, yeye mwenyewe na ndugu yake, Ali. Aliomba rehema za Allah (s.w.t.) juu yao wote na familia zao.

وَلَقَدْ مَنَنَّا عَلَىٰ مُوسَىٰ وَهَارُونَ {114}

سَلَامٌ عَلَىٰ مُوسَىٰ وَهَارُونَ {120}

إِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ {121}

إِنَّهُمَا مِنْ عِبَادِنَا الْمُؤْمِنِينَ {122}

Na kwa hakika tuliwafanyia hisani Musa na Harun. Amani iwe juu ya Musa na Haroun. Hakika hivyo ndivyo tunavyowalipa walio wema. Hakika wawili hao ni katika waja walioamini.
(Sura ya 37; Aya ya 114, 120, 121, 122)

Allah (s.w.t.) aliweka Rehema Zake juu ya Musa na Harun, na aliweka Rehema Zake juu ya Muhammad na Ali, waja Wake walioamini. Wote wanne walitenda haki, na Allah (s.w.t.) akawalipa wao, na akashusha amani na salamu kwao.
Ingawa Harun alichaguliwa ki-mungu kuwa mrithi na msikamakamu wa Musa, alikufa katika uhai wake (Musa), hivyo kusababisha kuchaguliwa kwa kiongozi mpya. Kiongozi mpya alikuwa ni Yush’a bin Nun (Joshua). Kama Harun, yeye pia, aliteuliwa ki-mungu kuwa mshikamakamu wa Musa, na umma haukuwa na lolote la kufanya katika kuchaguli- wa kwake.

Baada ya kifo cha Musa, mshikamakamu wake, Yush’a bin Nun, aliwaongoza Bani-Israil kwenye ushindi.

Vigezo vya hekima katika suala la kuchagua na kuweka kiongozi wa umma wa Kiislam, baada ya kifo cha Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.w.t.) vinaweza kuonekana wazi katika Aya za Qur’an zilizonukuliwa hapo juu. Ali alikuwa ndiye chaguo la Mbinguni. Chote alichokuwa afanye Muhammad, ni kule kutoa lile tangazo rasmi kwamba Ali atakuwa ndio kiongozi wa Waislamu baada ya kifo chake yeye mwenyewe. Ilikuwa ni kutoa Tangazo hili ambako aliwaamuru Waislamu kukusanyika kwenye bonde la Khumm.

Mwislamu wa kisasa anaweza kuchukulia kwamba hili Tangazo la kihistoria lililotolewa na Mtume, lazima lingefuatiliwa na sherehe ya kimataifa miongoni mwa Waislamu. Inaonekana kuwa ni ajabu kusema kwamba haikuwa hivyo. Walikuwepo Waislamu waliokuwa na furaha lakini walikuwepo wengine wengi ambao hawakufurahia. Hawa wengine waliwazia mategemeo mengine, na walijali tamaa nyingine, na mategemeo na tamaa zao havikubadilisha mwelekeo wa tangazo la Mtume (s.a.w.) pale Ghadir-Khumm. Tangazo lake, la wazi kabisa na lisilo na mashaka, ilivuruga matumaini na tamaa zao.

Lakini hawakuvunjika moyo. Walitunga jambo jingine. Walianza kunon’gona kwenye masikio ya Waarabu kwamba uteuzi wa Ali kama Mkuu wa Waislamu wote kulikuwa ni kitendo kilichochochewa na tamaa ya Mtume (s.a.w.) ya kuhodhi mamlaka ya kisiasa katika familia yake mwenyewe – katika ukoo wa Bani Hashim - na kuwaondoa wengine wote, na kwamba haikuwa na uhusiano wowote na Wahy. Walitegemea kwamba ikiwa “hoja” yao itawavutia Waarabu, basi watakuwa na uwezo wa kuwaingiza kwenye kugombania madaraka ambamo wao wenyewe wanaweza wakawa wa juu. Tokea muda huo, Kwa hiyo, walianza kufanya kazi ya kujipangia mkakati mpya wa kupambana na hali hiyo mpya.

Walikuwa ni akina nani watu hawa? Hawakuainishwa kwa majina yao lakini kuwepo kwao na uwezo wao katika fitna vinaonekana katika ile Aya ya kwanza (5:67). Mtume, ni dhahiri, alikuwa anasita kuchukua hatua, akiwa anajua upinzani mkubwa wa Waarabu wengi kwenye kuchaguliwa kwa Ali kama kiongozi wa baadae wa Dola ya Kiislam. Lakini alihakikishiwa kwamba Allah (s.w.t.) atamlinda kutokana nao hao; kwamba akushinde kusitasita kwake, na autangaze ushika-makamu wa Ali ibn Abi Talib.

Kupinga lile Tangazo la kihistoria pale Ghadir-Khumm kulikuwa ni kumpinga mwenyewe. Upinzani juu yake, mpaka wakati wa Tangazo lile, hata hivyo, ulikuwa umejificha na kuto- jionyesha; lakini muda si mrefu ulikuwa utokeze kichwa chake cha husuda katika wakati wa uhai wake yeye mwenyewe. Suala hili limeshughulikiwa katika Sura ya 39.

Kule kuteuliwa, na Muhammad Mustafa, pale Ghadir-Khumm, kwa Ali ibn Abi Talib kama mrithi wake, kumesimuliwa na maswahaba wake wafuatao:

Khuzayma bin Thabit
Sahl bin Sa’ad
Adiy bin Hatim
Aqba bin Aamir
Abu Ayyub Ansari
Abul-Haithum bin Taihan
Abdullah bin Thabit
Abu Ya’la Ansari
Nu’man bin Ajlan Ansari
Thabit bin Wadee’a Ansari
Abu Fadhala Ansari
Abdur Rahman bin Abd Rabb
Junaida bin Janada
Zayd bin Arqam
Zayd bin Sherheel
Jabir bin Abdullah
Abdullah bin Abbas
Abu Said al-Khudri
Abu Dharr al-Ghiffari
Salman el-Farsi
Jubayr bin Mutim
Hudhayfa bin Yaman
Hudhayfa bin Usayd

Miongoni mwa wanahistoria ambao wameandika matukio ya Ghadir-Khumm ni Athiir-ud-Diin ndani ya kitabu chake Usudul-Ghaba; Halabi katika kitabu chake Siira-tul-Halabiyya; na Ibn Hajar katika kitabu chake al-Sawa’iq-al-Muhriqa.

Wapokezi wa Hadith waliotaja matukio ya Ghadir-Khumm ni akina Muslim, Nasai, Tirmidhi, Ibn Majah; Ahmad Hanbal na Hakim.