read

Kutekwa Kwa Makka

Maquraishi walishindwa kutumia ushindi wao wenyewe juu ya Waislamu katika vita vya Uhud, lakini hawa Waislamu waliposhindwa katika vita vya Muutah na Wakristo, walijaribu kutumia ule ushindi wa Wakristo, na kurudisha ile hali ya kabla ya Hudaybiyya kati- ka Arabia. Kushindwa kwa Waislamu kule Muutah kulichukua nafasi kubwa katika matukio yaliyotangulia kuanguka kwa Makka mnamo mwaka 630.

Muhammad Husein Haykal

Tunaweza kukumbuka kwamba mara tu Khalid na lile jeshi waliporudi Madina bila ya uthibitisho wa ushindi (katika vita vya Muutah), waliitwa wakimbizi. Askari wengi na makamanda walijihisi kuabika sana kiasi kwamba walikaa majumbani ili wasionekane na kudhalilishwa hadharani. Vile vita vya Muutah viliwapa Maquraishi ile picha kwamba Waislamu na nguvu zao sasa wameangamizwa na kwamba, hadhi yao na hofu ambavyo hapo kabla waliviingiza kwa wengine vyote vimetoweka. Hii iliwafanya Maquraishi kuegemea kwa nguvu sana kwenye hali zilivyokuwepo kabla ya Mkataba wa Hudaybiyya. Walidhani sasa wangeweza kuanzisha vita ambavyo dhidi yake Waislamu walikuwa hawawezi kujihami wenyewe, bila kuzungumzia juu ya kujibu mashambulizi au kulipiza kisasi. (The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Kulingana na makubaliano ya ule Mkataba wa Hudaybiyya, yale makabila ya Waarabu yalikuwa huru kuingia kwenye mahusiano ya mkataba ama na Waislamu au hao Maquraishi. Kwa kuchukua fursa ya mapatano haya, lile kabila la Banu Khuza’a waliandika mkataba wa urafiki na Mtume wa Uislamu, na kabila lingine – Banu Bakr – wakawa washirika wa Maquraishi.

Uhasama ulidumu baina ya haya makabila mawili tangu nyakati za kabla ya Uislamu lakini sasa yote yalipaswa yafuate masharti ya ule Mkataba wa Hudaybiyya, na kuepuka kushambuliana.

Lakini miezi kumi na nane baada ya huo Mkataba wa Hudaybiyya kutiwa saini, kundi la wapiganaji la Banu Bakr ghafla likawashambulia Banu Khuza’a majumbani mwao wakati wa usiku. Wakati wa shambulio hili unatolewa kama ni mwishoni mwa Rajab ya mwaka wa 8 A.H. (Novemba 629). Banu Khuza’a hawakufanya chochote kuchochea shambulio hili.

Walichukua hifadhi katika maeneo ya Al-Kaaba lakini maadui zao waliwafuatilia hata hapo, na wakawaua baadhi yao. Wengine waliokoa maisha yao kwa kutafuta ulinzi wa Budail bin Waraka na rafiki yake, Rafa’a, katika nyumba zao, hapo Makka.

Muhammad Husein Haykal

Ule Mkataba wa Hudaybiyya uliandika kwamba mtu yoyote asiye wa Makka akitaka kujiunga na kambi ya Muhammad au ile ya Maquraishi anaweza kufanya hivyo bila ya kipingamizi. Kwa msingi wa kipengele hiki, lile kabila la Khuza’a lilijiunga na safu ya Muhammad, na lile la Banu Bakr likajiunga na Maquraishi. Kati ya Banu Khuza’a na Banu Bakr idadi ya migogoro ya zamani ambayo ilikuwa haijasuluhishwa ilibidi isimamishwe kwa sababu ya mipango mipya.

Pamoja na Maquraishi kuamini kwamba (baada ya vita vya Muutah) uwezo wa Waislamu umevunjika, Banu al Dil, ukoo mmoja wa Banu Bakr, walidhani kwamba muda umefika wa kilipiza kisasi chao dhidi ya Khuza’a. (The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Banu Bakr wasingeweza kuwashambulia Khuza’a bila ya kula njama na kutiwa moyo kama sio kuungwa mkono kwa uwazi na Maquraishi.

Tabari, yule mwanahistoria, anasema kwamba Ikrima bin Abu Jahl, Safwan bin Umayya na Suhayl bin Amr, wote watu mashuhuri wa Quraishi, walijibadili wenyewe na kupigana kwenye upande wa Banu Bakr dhidi ya Khuza’a. Kati ya hawa watatu, huyu wa mwisho kutajwa ndiye mweka saini mkuu wa Maquraishi kwenye Mkataba wa Hudaybiyya.

Maxime Rodinson

Katika Rajabu ya mwaka wa 8 (Novemba 629), katika mfululizo wa kisasi cha kurithi baina ya koo ambacho kilikuwa kikiendelea kwa miongo kadhaa, baadhi ya wale waliotaharuki sana katika Maquraishi kule nyuma yao, walishambulia kikundi cha kabila la Khuza’a, washirika wa Muhammad, sio mbali sana kutoka Makka. Mtu mmoja aliuawa na waliobakia waliumizwa vibaya na kulazimishwa kukimbilia ndani ya eneo tukufu la Makka. Wakifuatiliwa hata huko walichukua hifadhi kwenye nyumba mbili za kirafiki. Kwa aibu sana hawa Banu Bakr waliweka mzingiro kwenye nyumba hizo. Kwa jumla watu ishirini wa Khuza’a waliuliwa.
(Mohammed, kilichotafsiriwa na Anne Carter)

Mmoja wa wakuu wa Khuza’a, Amr bin Salim, alikwenda Madina na kumsihi Mtume (s.a.w.) kuingilia kati. Mtume alishituka kusikia habari hizo za ufisadi. Kama mshirika wa hao Khuza’a, alipaswa kuwalinda kutokana na maadui zao. Lakini kabla ya kufikiria hatua za kijeshi, alijaribu kutumia njia za amani ili kupata marekebisho na haki. Alituma mjumbe kwa Maquraishi, na akashauri kwamba:

• Wale wateja wa Maquraishi, yaani, Banu Bakr, au Maquraishi wenyewe walipe fidia ya damu kwa Banu Khuza’a, au;

• Maquraishi wabatilishe ulinzi wao wa Banu Bakr, au;

• Watangaze ule Mkataba wa Hudaybiyya kuwa umefutwa.

Zarqani anasema kwamba mtu aliyewajibia Maquraishi alikuwa ni Qurtaba bin Umar. Alimwambia mjumbe wa Mtume (s.a.w.) kwamba lile la mwisho tu kati ya masharti yale matatu ndio lililokuwa linakubalika kwao. Kwa maneno mengine, Maquraishi walimwambia kwamba ule Mkataba wa Hudaybiyya pamoja na makubaliano yake ya miaka kumi ya kusimamisha vita, tayari ni “kanuni isiyo na nguvu” kiasi wao walivyohusika.

Wale wakaidi wa Maquraishi walikuwa wepesi kuukana ule Mkataba wa Hudaybiyya lakini haraka sana wale viongozi wao wakweli zaidi na makinifu walitambua kwamba lile jibu walilopeleka Madina lilikuwa ni kosa la kijinga kwani lilitamkwa, sio kwa busara na hekima, bali kwa ufedhuli na ujinga.

Na pale walipofikiria juu ya matokeo gani ya kitendo chao yatakayokuwa, waliamua kuchukua hatua haraka sana kuzuia maafa. Lakini vipi? Baada ya mjadiala wa kusisimua, walikubaliana kwamba Abu Sufyan aende Madina, na ajaribu kumshawishi Mtume (s.a.w.) kurudia upya ule Mkataba wa Hudaybiyya.

Wakati Abu Sufyan alipowasili Madina, alikwenda kwanza kumuona binti yake, Ummu Habiba – mmoja wa wake zake Mtume. Alipokuwa anataka kukaa juu ya zulia, binti yake akalivuta kutoka chini yake, na akasema: “Wewe ni muabudu masanamu usiye na tohara, na siwezi kukuruhusu kukalia zulia la Mtume wa Allah (s.a.w.)” Alimfanya kama mtu aliyetengwa na jamii, asiyegusika.

Akishtushwa na mapokezi kama hayo, alimuacha na kuondoka na akaenda Msikitini akitegemea kumuona Mtume (s.a.w.) mwenyewe. Lakini Mtume (s.a.w.) hakumpa fursa ya kuonana naye. Baadae aliomba msaada wa Abu Bakr, Umar na Ali lakini wote walimwambia kwamba hawawezi kumuombea yeye kwa Mtume, na akarudi Makka mikono mitupu.

Maquraishi waliuvunja ule mkataba, na wajumbe wa Khuza’a walikuwa bado wapo Madina, wakidai haki. Kama Mtume (s.a.w.) angesamehe lile kosa la Maquraishi, angeiabisha vibaya sana heshima yake machoni mwa Waarabu wote. Asingeweza kukubali hili litokee. Hatimae, Mtume (s.a.w.) aliamua kuiteka Makka, na aliwaamuru Waislamu wakusanyike.

Jeshi hilo la Uislamu liliondoka Madina mnamo mwezi kumi ya Ramadhini ya mwaka wa 8 H.A. (1 Feb.630). Habari kwamba kuna jeshi lililokuwa linaelekea upande wa Kusini, zilienea haraka sana humo jangwani, na hata zikafika Makka kwenyewe.

Wale watu wa ukoo wa Bani Hashim ambao walikuwa bado wako Makka, wakaamua, baada ya kusikia habari hizi, kuondoka hapo mjini na kukutana na hilo jeshi linalokuja. Miongoni mwao walikuwa ni Abbas bin Abdul Muttalib, yule ami yake Mtume; Aqiil bin Abi Talib, na Abu Sufyan bin al-Harith bin Abdul Muttalib, binamu zake. Walijiunga na jeshi hilo la Uislamu, na wakaingia tena Makka pamoja nalo.

Mnamo mchana wa mwezi 19 Ramadhan, jeshi hilo liliwasili Merr ad-Dharan kaskazini ya Makka, na likasimama hapo ili kuupitisha usiku huo. Usiku Mtume (s.a.w.) aliwaamuru wapiganaji wake kuwasha mioto midogo midogo, na uwanda wote ukamulikwa na maelfu ya mioto.

Abu Sufyan na Hakim bin Hizam walikuwa wameondoka pia Makka kwenda kuchunguza zile taarifa za uvamizi wa Waislamu. Wakielekea kaskazini kwenye njia iendayo Madina, wao pia waliwasili Merr ad-Dharan, na walipigwa na butwaa kuona mioto midogodogo isiyo na idadi ikiwaka ndani ya bonde hilo. Walipotambua kwamba wako kwenye kambi ya Waislamu, walipata taabu sana wasijue chakufanya kujiokoa wao wenyewe au mji wao.

Abbas bin Abdul Muttalib pia alikuwa na wasiwasi mkubwa juu ya usalama wa watu wa Makka. Alihofia kwamba kama watatoa upinzani, watauawa kwa wingi. Alikuwa amempanda yule farasi mweupe wa Mtume (s.a.w.) kupita mle kambini, ambapo katika mpaka wake wa Kusini, alikumbana ghafla na Abu Sufyan na Hakim bin Hizam. Aliwaambia kwamba wanaweza kuona ile idadi ya Waislamu, na kwamba Maquraishi hawakuwa na uwezo wa kushindana nao. Abu Sufyan alimuuliza ni nini yeye angepaswa kufanya.

Abbas akamwambia afuate nyuma yake juu ya farasi wake mwenyewe, na kwamba atampeleka kwa Mtume, na atajaribu kupata hati ya usalama kwa ajili yake. Hakim bin Hizam akarudi Makka kwenda kuelezea juu ya kile alichokiona na kusikia. Abbas na Abu Sufyan waliwapanda farasi wao kuingia kwenye kambi ya Waislamu wakati huo huo, walipita karibu na hema la Umar, naye Umar akataka kujua ni akina nani hao wageni wawili.

Pale Umar alipomtambua Abu Sufyan, alisisimka, na akamwambia: “Ewe adui wa Allah (s.w.t.) hatimae uko kwenye mamlaka yangu, na sasa nitakuua.” Lakini Abbas akamwambia kwamba yeye (Abu Sufyan) yuko chini ya ulinzi wake. Pale pale Umar alikimbia kwenda kumuona Mtume (s.a.w.) na kumuomba ruhusa yake ili amuue (Abu Sufyan). Lakini Mtume (s.a.w.) alimwambia tu Abbas amlete asubuhi itakayofuata.

Mapema sana asubuhi iliyofuata, Abbas, Abu Sufyan na Umar, wote watatu walitokea mbele ya hema la Mtume. Umar alikuwa na hamu ya kumuua Abu Sufyan lakini Mtume (s.a.w.) alimzuia, na akamualika Abu Sufyan kusilimu. Abu Sufyan hakuwa na moyo sana wa kuukubali Uislamu lakini Abbas alimwambia kama hakusilimu, basi Umar atamuua, na hatarudi kamwe Makka. Akikabiliwa na tishio la kifo, Abu Sufyan aliitamka Shahada ambayo ilimwingiza rasmi kwenye jamii ya Waislamu.

Abbas pia alimuomba Mtume (s.a.w.) kumpa Abu Sufyan upendeleo fulani ambao angeulinganisha na “heshima maalum.” Mtume (s.a.w.) akasema wale watu wote wa Makka watakaoingia kwenye nyumba ya Abu Sufyan, au watakaokaa kwenye nyumba zao wenyewe, au watakaoingia kwenye maeneo ya Al-Kaaba, watakuwa salama kutokana na madhara yote.

Abu Sufyan alijivuna sana kwamba Mtume (s.a.w.) ameitangaza nyumba yake kuwa kimbilio la waabudu masanamu wa Makka. Marafiki zake wa baadae na wapenzi wanaringia ile “heshima maalum” yake mpaka leo.

Ilikuwa ni Ijumaa, Ramadhan 20, 8 A.H. (Feb.11, 630) pale jeshi la Waislamu lilipovunja kambi pale Merr ad-Dharan, na kuelekea Makka. Abbas na Abu Sufyan walisimama juu ya ukingo wa kilima kuangalia vile vikosi vikipita mbele yao. Huyu Abu Sufyan alivutiwa sana na utaratibu huo, na nidhamu, ile idadi na moyo wa mshikamano wa mipangilio, na akamwambia Abbas:

“Mpwa wako kwa hakika amepata ufalme mkubwa na mamlaka makubwa.” Abbas akamkaripia: “Ole wako! Huu ni Utume na sio ufalme.” Abu Sufyan alikuwa hajawahi kuona mandhari ya kutisha kama hii hapo kabla, na kwa hisia zake za kipagani, na uono wake wenye kikomo kabisa, aliweza kuitafsiri tu katika istilahi za mamlaka yakinifu. Lakini alitambua kwamba mchezo wake na waabudu masanamu umekwisha hatimae, na kitu muhimu sasa kilikuwa ni kuokoa maisha yake na yao.

Abu Sufyan aliharakisha kurudi Makka, na akiingia kwenye maeneo ya Al-Kaaba, alikemea kwa sauti kubwa: “Enyi watu wa Makka! Muhammad amewasili pamoja na jeshi lake, na hamna uwezo wa kumpinga yeye. Wale miongoni mwenu watakaoingia nyumbani kwangu, watakuwa salama kutokana na madhara yote, na sasa ni kusalimu amri kwenu tu bila ya masharti kutakakoweza kuwaokoeni na mauaji ya halaiki.”

Mke wa Abu Sufyan, Hinda, aliusikia mwito wake huo. Alishikwa na hasira kali, akatoka kwa kasi nje ya nyumba yake, akamshika kwenye ndevu zake, na akapiga mayowe: “Enyi watu wa Makka! Muueni huyu mpumbavu asiye na bahati. Ana upungufu wa akili. Muondoeni yeye na mlinde mji wenu kutokana na adui yenu.”

Lakini ni nani anayeweza kuilinda Makka na vipi? Sasa hivi, Abu Sufyan alikuwa amezungukwa na raia wengine wa Makka, na mmoja wao akamuuliza: “Nyumba yako inaweza kuchukua watu wachache tu. Ni vipi watu wengi watakavyopata kimbilio ndani yake?” Akasema: “Wale wote watakaokaa ndani ya nyumba zao au watakaoingia kwenye viwanja vya Al-Kaaba, watakuwa pia salama.”

Amri hii ilikuwa na maana kwamba kile ambacho waabudu masanamu hao wanachoweza kufanya kuokoa maisha yao, kilikuwa ni kubaki ndani ya nyumba zao, na kuepuka kushindana na wale wavamizi.

Washington Irving

Muhammad aliandaa msafara wa siri wa kuishtukiza Makka. Njia zote zinazoelekea Makka zilifungwa kuzui taarifa zozote za harakati zake kubebwa na kupelekwa Makka. Lakini miongoni mwa wakimbizi kutoka Makka, alikuwepo mtu mmoja, Hatib, ambaye familia yake ilibakia nyuma, na walikuwa bila kiunganisho au marafi- ki wa kuweza kujali juu ya ustawi wao. Hatib sasa alifikiria kupata msaada kwa ajili yao miongoni mwa Maquraishi, kwa kuisaliti mipango ya Muhammad. Yeye kwa hiyo, aliandika barua inayofichua lile jambo kubwa lililokusudiwa, na akaitoa mikononi mwa mwanamke anayeimba, ambaye alijitolea kuipeleka Makka. Mwanamke huyo alikuwa tayari njiani wakati Muhammad alipofahamishwa juu ya usaliti huo.

Ali na watu wengine watano, wenye vipando vizuri, walitumwa kumfukuzia huyo mjumbe. Walimkuta mara moja, lakini wakampekua mwili mzima bila mafanikio. Wengi wao wangejiachia huo upekuzi na kurudi lakini Ali alikuwa na hakika kwamba Mtume wa Allah (s.a.w.) asingeweza kukosea wala kupewa taarifa za uongo. Akichomoa upanga wake, aliapia kumuua huyo mjumbe labda barua ikitole- wa. Tishio hilo lilileta athari. Aliitoa barua hiyo kutoka kati ya nywele zake.

Hatib, katika kulaumiwa kwa usaliti wake, aliukubali; lakini alikiri shauku ya kupata msaada kwa ajili ya familia yake masikini, na uhakika wake kwamba barua ile isingekuwa na madhara, na isiyo na mafanikio dhidi ya malengo ya Mtume wa Allah (s.a.w.).

Umar alizikataa sababu hizo na angemkata kichwa chake; lakini Muhammad, akikumbuka kwamba Hatib alipigana kishujaa katika kuitetea dini katika vita vya Badr, alimsamehe.

Muhammad, ambaye alikuwa hajui ni upinzani gani atakaokutana nao, alifanya ugawaji wa uangalifu wa vikosi vyake alipokuwa akikaribia Makka. Wakati kikosi kikubwa kilisonga mbele moja kwa moja, vikosi imara vilisonga juu ya vilima kwenye pande zote. Kwa Ali ambaye aliongoza kikosi kikubwa cha wapanda farasi, alikabidhiwa ile bendera tukufu, ambayo ilikuwa aisimike juu ya Mlima Hadjun, na kuibakisha hapo mpaka Mtume (s.a.w.) atakapoungana naye. Amri dhahiri zilitolewa kwa majenerali wote kuwa wenye subira, na kwa namna yoyote ile wasiwe wa kwanza kushambulia. (The Life of Muhammad)

Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) aliingia Makka tokea upande wa kaskazini. Usamah, mtoto wa rafiki yake na shahidi wa Muutah, Zayd bin Haritha, alikuwa amepanda nyuma ya farasi pamoja naye. Kichwa cha Muhammad kilikuwa kimeinamishwa chini, na alikuwa akisoma ile Sura kutoka ndani ya Qur’an iitwayo “Ushindi”

Ali alibeba ile bendera ya Uislamu alivyokuwa juu ya farasi mbele ya kile kikosi cha wapanda farasi. Mtume (s.a.w.) alimuamuru Zubayr bin al-Awwam kuingia mjini hapo kutokea upande wa Magharibi, na Khalid bin al-Walid kutokea upande wa Kusini. Alitoa amri kali kwa jeshi lake wasimuue mtu yoyote isipokuwa katika kujihami. Alitamani siku nyingi kuyaharibu yale masanamu ndani ya Al-Kaaba lakini alitaka kufanya hivyo bila ya umwagaji damu wowote. Amri zake zilikuwa wazi na dhahiri; hata hivyo, Khalid aliuwa watu wa Makka 28 kwenye lango la Kusini la mji huo. Alisema kwamba alikutana na upinzani.

Sir John Glubb

Utwaaji wa Waislamu, wa Makka ulikuwa kwa kweli si wa kumwaga damu. Yule mwenye harara, Khalid bin al-Walid aliua watu wachache kwenye lango la Kusini na alikaripiwa vikali na Muhammad kwa kufanya hivyo. (The Great Arab Conquests)

Miaka nane kabla Muhammad aliondoka Makka kama mkimbizi pamoja na kunadiwa kichwa chake, na sasa alikuwa anaingia mji huo huo kama mtekaji wake. Tabia yake, hata hivyo, haikuashiria kiburi au hata kushangilia sana bali shukrani na unyenyekevu – shukrani kwa Allah (s.w.t.) kwa neema zake katika kuweka mafanikio juu ya Mtumwa wake mnyenyekevu, na unyenyekevu katika kuzingatia kiburi cha fahari za kidunia, na kufifia kwa vitu vyote vya kibinadamu.

Mtume (s.a.w.) aliingia na ngamia wake ndani ya viwanja vya Al-Kaaba, akashuka kwenye ngamia wake, akamwita binamu yake, Ali ibn Abi Talib, na wote wakingia ndani ya Al-Kaaba, wakizitambua zile Amri Tukufu kwa wale Mitume, Ibrahim na Ismail:

وَعَهِدْنَا إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ أَنْ طَهِّرَا {125}

“...na tuliagana na Ibrahim na Ismail kwamba itakaseni Nyumba Yangu …” (Sura ya 2; Aya ya 125)

Mtume (s.a.w.) pamoja na Ali waliikuta ile Nyumba ya Allah (s.w.t.), (Al-Kaaba) katika hali ya unajisi; ilikuwa imegeuzwa kuwa hekalu la masanamu 360, na ilibidi itakaswe. Mtume (s.a.w.) aliangusha chini kila sanamu huku akisoma Aya ifuatayo kutoka kwenye Qur’an:

وَقُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ ۚ إِنَّ الْبَاطِلَ كَانَ زَهُوقًا {81}

“Ukweli umefika, na uongo umetoweka. Hakika ya uongo(kwa asili yake) lazima utoweke.”
(Sura ya 17; Aya ya 81)

Sanamu kubwa sana ndani ya hekalu hilo lilikuwa ni lile la Hubal, mungu wa kifamilia wa ukoo wa Banu Umayya.

Abu Sufyan alikwenda nalo juu ya ngamia kwenye vita vya Uhud kuwatia moyo wale wapiganaji kwa kuwepo kwake. Hubal aliwekwa juu ya kiegemeo kirefu, na Mtume (s.a.w.) hakuweza kumfikia. Yeye, kwa hiyo, alimwamuru Ali kupanda juu ya mabega yake, na kuliangusha chini.
Katika kutii ile amri ya Kitume, ilimbidi Ali kusimama juu ya mabega ya Mtume; alilenga pigo kwenye yule mungu mkuu wa waabudu masanamu, na akamvunja vipande vipande. Kwa pigo lile kubwa, Ali aliweka mwisho wa kudumu kwa uabudu masanamu ndani ya ile Al-Kaaba! Al-Kaaba, Nyumba ya Allah (s.w.t.) ikawa imetakaswa!

Abul Kalam Azad

Baadhi ya masanamu yalikuwa yamewekwa juu ya viegemeo virefu na Mtume (s.a.w.) hakuweza kuyakuta. Alimuamuru Ali kupanda juu ya mabega yake na kuyaangusha chini. Ali akapanda juu ya mabega ya Mtume, na akayaangusha chini yale masanamu. Yeye kwa hiyo aliondoa uchafu wa uabudu masanamu kutoka kwenye Al-Kaaba kwa zama zote. (The Messenger of Mercy, Lahore, Pakistan, 1970)

Wakati masanamu yote yalipokuwa yameharibiwa, taswira zote zilikuwa zimefutwa, na dalili zote zilizobakia za ushirikina zilikuwa zimefutiliwa mbali kabisa. Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) alimtuma Bilal kupiga Adhana. Bilal alipiga Adhana na bonde la Makka likavuma kwa ile takbir yake yenye nguvu na ya kuvutia. Mtume (s.a.w.) ndipo akafanya mizunguko saba ya Al-Kaaba, na akaswali Swala ya kutoa shukruni kwa Muumba wake.

Wakati huo huo, Maquraishi walikuwa wamekusanyika katika baraza ya Al-Kaaba wakimsubiri Mtume. Walitegemea kwamba angeonana nao kabla ya kutoa fatwa juu ya hatima yao.

Hapo Mtume (s.a.w.) alitokea kwenye kizingiti cha Al-Kaaba. Alilitazama lile kundi la watu lililokuwa mbele yake na akawahutubia kama ifuatavyo: “Hakuna mungu ila Allah (s.w.t.) Yeye ni Mmoja na Mpweke kabisa, na Yeye hana washirika. Sifa zote na shukrani ni Kwake. Yeye ametimiza ahadi Yake. Amemsaidia mja wake kupata ushindi, na Ameyatawanya makundi ya maadui zake.

‘Enyi watu! Nisikilizeni! Kiburi chote, majisifu, majivuno, na madai yote ya damu ya Nyakati za Ujahiliya yako chini ya miguu yangu leo.

‘Enyi Maquraishi! Allah (s.w.t.) amevunja kiburi cha Zama za Ujahilia, na Yeye amevunja majivuno ya ukabila. Watu wote ni wana wa Adam, na Adam alikuwa ni ukafi tu udongo.”

Mtume (s.a.w.) kisha akasoma Aya ifuatayo kutoka kwenye Qur’an:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُمْ مِنْ ذَكَرٍ وَأُنْثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِنْدَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ {13}

“Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mbora zaidi kati yenu mbele ya Allah ni yule mchamungu zaidi miongoni mwenu. Hakika Allah ni Mwenye kujua, Mwenye habari.” (Sura ya 49; Aya ya 13)

Aya hii ndio waraka wa usawa na udugu wa watu wote katika Uislamu. Hapawezi kuwa na tofauti yoyote kati ya watu kwa misingi ya ukabila, rangi, utaifa, ukoo wala utajiri.

Bali wakati ambapo Uislamu unavunja tofauti za aina nyingine zote, unatetea sifa yake ya kipekee, na hiyo ni sifa ya imani na tabia.

Muhammad ndipo akawauliza swali Maquraishi: “Mnafikiri nitawafanya nini sasa?” Wakasema: “Wewe ni ndugu mkarimu, na mtoto wa ndugu mkarimu. Tunategemea wema na msamaha tu kutoka kwako.” Akasema: “Nitawaambia kile Yusufu alichowaambia ndugu zake, ‘hakuna lawama juu yenu leo.
(Qur’an. Sura ya 12 Aya ya 92). Ondokeni sasa, nyote ni waachwa huru wangu.”

Mtume (s.a.w.) alitangaza msamaha wa jumla hapo Makka. Msamaha huo uliwafikia na makafiri pia. Alilikataza jeshi lake kuteka nyara za mji huo au kuzuia kitu chochote kili- chokuwa mali ya Maquraishi. Hao Maquraishi hawakuacha kukamilisha kitu chochote kuzingira uharibifu wake, na uharibifu wa Uislamu; lakini katika saa yake ya ushindi alisamehe makosa yao yote na uhalifu wao.

Maquraishi, hapo mwanzoni, walikuwa hawasadiki. Hawakuweza kuamini masikio yao wenyewe. Vipi Muhammad anaweza kuzuia vishawishi vya kuwaua wote, baada ya yote yale ambayo wamemtendea kwa zaidi ya miongo miwili, na hasa sasa hivi ambapo alikuwa ana mamlaka makubwa kiasi hicho mikononi mwake? Kule kutokupenda kwake Muhammad kutumia madaraka yake kulikuwa ni kitu ambacho kabisa kilizipita akili-tam-buzi za washirikina wa Makka. Muda mwingi ulipita kabla ya maana ya dhamira ya Muhammad kuingia akilini mwao, na ule msamaha ukaanza kuonekana wenye kuwezekana na wa kweli kwao.

Nia ya Muhammad, Mtume wa Amani, ilikuwa ni kuiteka Makka bila ya umwagaji wa damu, na katika hili alifanikiwa. Ilikuwa ni hapa ambapo alijidhihirisha mwenyewe, kwa maneno ya Qur’an Tukufu “…rehma kwa wanadamu wote.” Historia haiwezi kutoa mfano wa uvumilivu kama huo. Sio kwamba wapagani hawakuangamizwa tu; sio tu kwamba hawakuwa walipe fidia yoyote kwa makosa yao ya wakati uliopita; hawakuingiliwa katika umiliki wa zile nyumba ambazo Muhajiriin waliziacha hapo Makka, na ambazo walizikalia.

Kutoka pale kwenye al-Al-Kaaba, Mtume (s.a.w.) alikwenda kwenye Mlima Safa, na watu wa Makka walikuja kumthibitisha kama mkuu wao katika hali zake mbili – kama Mtume wa Allah (s.w.t.) na kama mtawala wao wa kidunia. Watu wote walitoa kiapo cha uaminifu kwa Muhammad kwa kuweka mikono yao juu ya mkono wake. Baadae ikaja zamu ya wanawake kutoa hicho kiapo cha uaminifu. Lakini hakutaka kugusa mkono wa mwanamke yeyote ambaye hakuwa mke wake,. Yeye, kwa hiyo, alimtuma Umar ibn al-Khattab kupokea hicho kiapo cha wanawake kwa niaba yake.

Sir John Glubb

Mtume (s.a.w.) kisha akamtuma Umar ibn al-Khattab kupokea hivyo viapo vya wanawake.
(The Great Arab Conquests)

Wakati kula viapo kulipokwisha, Mtume wa Allah (s.a.w.) alijishughulisha na yale masuala mapya ya kisiasa na kiutawala yaliyotokana na ule ushindi wa Makka.

Ile Hadith nzito ya kuvutia ambayo ilianza mnamo Februari 12, mwaka 610, katika pango la Hira, ilifikia kileleni mnamo Februari 11, mwaka 630, katika baraza ya Al-Kaaba. Ilikuwa ni siku ya hisia, ahadi na sherehe, na siku kubwa katika historia, yenye umuhimu na uashiriaji. Ile hamu iliyoelekea kutokuwa na matumaini mwaka 620 kule Taif, imekuwa jambo kamilifu mwaka 630 hapo Makka.

Maquraishi waliendeleza mapambano marefu na makali dhidi ya Uislamu kwa miaka ishirini lakini wengi miongoni mwao sasa waliweza kuona kwamba yale masanamu ambayo waliyaabudu kama miungu yao, yalikuwa ni vitu bure kabisa. Wao, kwa hiyo, waliukubali Uislamu. Miongoni mwao, kulikuwemo na aina zote za watu waliosilimu: wachache ambao waliridhika kwamba Muhammad alikuwa ndiye Mtume wa kweli wa Allah (s.w.t.) na walimkubali yeye kama hivyo.

Lakini kulikuwa na wengine wengi ambao waliukubali Uislamu kwa sababu walikuwa na kidogo sana cha kuchagua kutokana nacho. Walitambua kwamba ilikuwa hakuna sababu ya kupingana na kundi la wengi, na vile vile waliona kwamba hayakuwa maafikiano mabaya hata hivyo kujitangaza kuwa Waislamu, na walifanya hivyo, kwa mashaka gani, lilikuwa ni swali la kujibiwa na hali yenyewe ya baadae.

Watu wote wa ukoo wa Banu Umayya, pamoja na Hinda, mke wa Abu Sufyan, yule mla watu wa Uhud, pia “waliukubali” Uislamu.

Hapa mtu anaweza kuweka kituo kutafakari juu ya “kuukubali” Uislamu kwa Banu Umayya. Mtu anaweza kujisalimisha kwa adui kwa sababu ya hofu, na hofu pia inaweza kuufunga mdomo wake. Hofu inaweza kufanya mambo mengi lakini kuna kitu kimoja hai- wezi kukifanya – haiwezi kubadilisha chuki kuwa upendo. Kwa miaka ishirini, Banu Umayya wameongoza upinzani wa mapagani kwa Uislamu. Walifanya vita vya kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kisaikolojia dhidi ya Mtume Wake, na dhidi ya wafuasi wake.

Sasa kufikiria kwamba onyesho moja la nguvu za kijeshi lililoonyeshwa na Muhammad “liliwaridhisha” wao kwamba yeye alikuwa ni Mtume wa kweli wa Allah (s.w.t.) litakuwa ni vigumu kulitegemea kutoka kwenye asili ya mwanadamu.
Hilo onyesho moja la uwezo la Waislamu halikubadili ile chuki, kinyongo na uchungu wa Banu Umayya kuwa upendo na haiba, hususan katika wakati ambao Uislamu umewanyima wao sio tu yale masanamu waliokuwa wakiyaabudu kama miungu yao bali pia umewanyima hadhi yao, fursa, uluwa na mamlaka. Walikuwa, kwa hiyo, na hali ile ile ya mawazo ambayo kila taifa linaloshindwa linakuwa nayo. Mioyo yao ilikuwa imejaa chuki, kinyongo na hisia za kulipa kisasi dhidi ya walezi wa Uislamu.

Hawa Bani Umayya waliukubali Uislamu kwa kujirejea katika kuogopa sana kuvunjika kwa juhudi zote za upagani hapo Makka. Juhudi zao za kuokoa kale yao, na mapambano ili kudumisha uhusiano wao na upagani kama wapagani yameshindwa lakini pengine wangeweza kufanya kitu hicho hicho kama Waislamu. Mabingwa wa hayo masanamu, kwa hiyo, waliingia kwenye safu za waumini wakijifanya kama ni Waislamu. Hili liliwafanya wao kuwa hatari zaidi kuliko hapo kabla wakati upinzani wao kwa Uislamu ulipokuwa dhahiri. Wakati huu, hata hivyo, walikwenda “kichinichini” wakivuta muda kusubiri fursa ya kujitokeza watakapouvunja Uislamu, kama ikiwezekana; la sivyo, basi watazibadili sifa-bainifu zake zinazoutambulisha, na wangerudisha desturi nyingi za Zama za Ujahilia kiasi iwezekanavyo.

Bani Umayya hawakuweza kuuharibu Uislamu wakati wa uhai wa Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) kwa sababu alichukua tahadhari zenye nguvu dhidi ya kuzuka tena kwa upagani. Alikuwa macho wakati wote, na hawakuweza kutoa mshitukizo wa ghafla kwake. Yeye pia alichukua tahadhari ya kutowapa nafasi yoyote ya madaraka ambayo wangeweza kuitumia kama msingi wao wa kujiongezea wenyewe.

Baadhi ya wanahistoria wamedai kwamba Mtume (s.a.w.) alikuwa na shauku ya kuwaingiza Bani Umayya katika utumishi wa Uislamu kwa vile walikuwa na ujuzi mwingi adimu na vipaji. Von Grunebaum, kwa mfano, anaandika hivi: Muhammad kwa upande wake alihitaji uzoefu wa tabaka la watawala wa Makka; upanuzi wa umma na zaidi ya yote mfumo wake wa asili usingeweza kuendeshwa bila ya msaada wa wale watu wa mji huo. (Classical Islam – A History 600-1258,1970)

Hili ni moja ya yale madai ambayo hayawezi kuthibitika mbele ya uchunguzi makini. Hakuna ushahidi kama Mtume (s.a.w.) aliwahi kamwe kuweka “uzoefu” wa Bani Umayya kwenye kazi yoyote.

Lisilo na maana kama hilo hilo ni lile dai kwamba upanuzi wa umma na mfumo wake wa asili usingeweza kuendeshwa bila wao. Kama hao Bani Umayya walikuwa na uwezo huo wanaohusishwa nao, kwa nini hawakuutumia katika vita vyao beuzi dhidi ya Muhammad na Uislamu, na kwa nini walishindwa? Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) aliunda na kuimarisha ile Dola ya Kiislamu kwenye meno ya upinzani wa Bani Umayya. Hiyo Dola ya Kiislamu isingeweza kuishi pamoja kwa amani na utawala wa wachache wa kipagani uliokuwa ukiongozwa na Bani Umayya, na ilimbidi auangamize.

Hakuwa amevutiwa na huo “uzoefu” wao kabla au baada ya kuukubali Uislamu, na hakumchagua yeyote kati yao kama jenerali au kama mtawala au hakimu au chochote kile. Hii sehemu ya sera yake juu yao haingeweza kuwa wazi zaidi.

Baadhi ya wanahistoria wa ki-Sunni wameeleza kwamba Mtume (s.a.w.) alimteua Mu’awiyyah, mtoto wa Abu Sufyan na Hinda, kuwa “mwandishi” wake wa kuandika Aya za Qur’an. Mu’awiyyah anaweza kuwa ameandika baadhi ya Aya za Qur’an lakini haina maana kwamba hazingeweza kuandikwa bila yeye. Wapo waandishi wengi wanaopatikana kwa Mtume.

Kwanza kabisa, wakati Mu’awiyyah alipoingia Uislamu, nyingi ya Aya za Qur’an zilikuwa tayari zimekwisha teremshwa, na kulikuwa na kidogo, kama kilikuwepo, kwa yeye kuandika. Katika nafasi ya pili, alikuwa ni mmoja tu kati ya waandishi wengi. Kama kuandika Aya za Qur’an ni “sifa” kwake, basi anashirikiana pamoja na wanakili wengine wengi.

Hata hivyo, Abdullah bin Saad bin Abi Sarh, yule ndugu wa kunyonya wa Uthman bin Affan pia alikuwa mwandishi. Alizibadilisha Aya za Qur’an alipokuwa anaziandika. Mtume (s.a.w.) alimtangaza yeye kama kafiri. Alikuwa auwawe lakini aliokolewa na Uthman. Mtume (s.a.w.) alimfukuza kutoka Madina.

Ujuzi wa Mu’awiyyah kama mwandishi, kwa hiyo, haukuwa mmoja ambao ulikuwa na upungufu katika baraza la Madina. Wanahistoria wamehifadhi majina 29 ya waandishi wa Mtume.

Hata hivyo, yale maelezo ya Von Grunebaum yaliyonukuliwa hapo juu, yanaweza, kwa kweli, kuwa sahihi, kama yakifanyiwa marekebisho kidogo kusomeka kwamba haikuwa Mtume (s.a.w.) wa Uislamu bali ni Abu Bakr na Umar waliohitaji uzoefu na ubingwa wa Bani Umayya, walikuwa ni wote hao ambao hawakuweza kuiongoza hiyo dola mpya bila ya msaada wao.

Hao Bani Umayya walikuwa wa muhimu sana kwa Abu Bakr na Umar. Hadithi ya kufufuka kwa Bani Umayya wakati wa ukhalifa wa Abu Bakr na Umar inaelezewa kwenye mlango mwingine.

Mtume (s.a.w.) hata hivyo, alijaribu kuwaridhisha kwa vitulizo kwa matumaini kwamba wangevua uadui wao kwa Uislamu, na siku moja, wao wenyewe au watoto wao wangekuwa Waislamu waaminifu.

Lakini juhudi zake hazikuzaa matunda. Hakuna alichowafanyia wao, ambacho kamwe kililainisha nyoyo zao kuelekea kwenye Uislamu. Kamwe hawakupata akili ya utambulisho na Uislamu au kuutii. Walikuwa kihisia, kiasili na kiitikadi hawawezi kukubaliana nao. Kwa kushindwa tu kufikia malengo yao kwa upanga, ndipo walipouona ulazima na kukubali amri ya amani. Lakini kwao wao, ni njia tu imebadilika, sio mwisho.

Hiyo siku Abu Sufyan; mke wake Hinda, mtoto wao Mu’awiyyah, na watu wengine wa ukoo wa Umayya walipoukubali Uislamu, Farasi mnafiki wa ushirikina pia aliingia kwenye ngome ya Uislamu. Ali ibn Abi Talib, yule mwana falsafa wa Uislamu, alitoa mukhtasari wa asili ya uingiaji kwenye Uislamu wa Bani Umayya kama ifuatavyo:

“Bani Umayya hawakuwa Waislamu wa kweli, walijisalimisha tu, kwenye nguvu kuu - iliyowazidi”

Katika kutoa fatwa hii juu ya kusilimu kwa Bani Umayya na kuwa Waislamu, Ali alikuwa anafasili Aya ifuatayo kutoka kwenye Kitabu cha Allah (s.w.t.):

قَالَتِ الْأَعْرَابُ آمَنَّا ۖ قُلْ لَمْ تُؤْمِنُوا وَلَٰكِنْ قُولُوا أَسْلَمْنَا وَلَمَّا يَدْخُلِ الْإِيمَانُ فِي قُلُوبِكُمْ ۖ {14}

Mabedui wanasema: ‘Tumeamini’. Sema (uwaambie) “Ninyi bado hamjaamini, bali semeni, ‘Tumesilimu’, kwani imani haijaingia katika nyoyo zenu.” (Sura ya 49; Aya ya 14)

Mtume (s.a.w.) wa Uislamu alitumia majuma mawili hapo Makka kuwaelimisha wale watu wapya wa Makka walioingia katika Uislamu, na katika kuanzisha serikali ya mji ule.

Alikuwa amekwisha “twahirisha” ile Al-Kaaba, na Waislamu sasa walikuwa wanaumiliki huo mji ambao ulikuwa ndio kitovu cha kijamii, kisiasa, kiutamaduni, kibiashara na kidini cha Arabia. Makabila yote ya Kiarabu sasa yaliyatambua mamlaka ya serikali yake kama yenye umuhimu mkubwa.

Mtume (s.a.w.) aliimarisha yale maeneo mapya yaliyopatikana kati ya Makka na Madina na sehemu zilizo karibu ya Makka. Ndipo yeye akaanza kazi ya kuitengeneza upya ile jamii ya Ki-Arabu. Huko nyuma, Waarabu walikuwa na uzoefu wa miundo ya asili ya ukabila na ukoo tu katika mfumo wao wa kijamii lakini sasa wamekuwa “taifa” (umma) chini ya uongozi wake. Uwajibikaji wao kama Waislamu, haukuangalia asili ya rangi zao, ushirikishwaji wa kikabila, uhusiano wa kitaifa au kilugha au hata mipaka ya kijografia.

Uwajibikaji wa Waislamu ulivuka vikwazo vyote vya asili na tofauti zilizowekwa na binadamu. Walipaswa kutoa uaminifu wao mpya kwenye Jumuiya ya Waumini ambayo ilimkiri Allah (s.w.t.) kwamba ni Mmoja, na Muhammad kama Mtume Wake.

Makabila mengi karibu ya Makka yalikuwa bado ni wapagani, na Mtume (s.a.w.) alitaka kuwalingania kwenye Uislamu. Pia, yalikuwepo makabila mengine ambayo yalikuwa yameupokea Uislamu lakini yalikuwa bado Hayajalipa Zaka zao kwenye Hazina ya Umma, na alitaka awakumbushe kulipa madeni yao yale. Yeye, kwa hiyo, alituma wajumbe wakakusanye Zaka katika pande mbalimbali, pamoja na maagizo maalum juu ya kazi zao, wajibu na madaraka yao.

Mmoja wa hawa wakusanyaji wa Zaka alikuwa ni Khalid bin al-Walid. Mtume (s.a.w.) alimtuma kwa kabila la Banu Jadhima kukusanya Zaka zilizokuwa hazijalipwa lakini alivuka mipaka ya madaraka yake, na akaitia doa mikono yake kwa damu ya Waislamu wasio na hatia!

Muhammad ibn Ishaq

Msafara wa Khalid baada ya kutekwa Makka, kwa Bani Jadhima wa Kinana, na msafara wa Ali kusahihisha makosa ya Khalid.

Hakim aliniambia kwamba Mtume (s.a.w.) alimwita Ali na akamwambia aende kwa hawa watu na kuliangalia suala lao, na kukomesha vile vitendo vya zama za upagani. Hivyo Ali alikwenda kwao pamoja na fedha ambazo Mtume (s.a.w.) alizituma na akalipa fidia ya damu na akafidia hasara zao za kifedha. Wakati damu na mali vyote vilipokuwa vimekwisha kulipiwa bado alikuwa na pesa zilizobakia. Aliuliza kama kuna fidia yoyote ambayo ilikuwa haijalipiwa bado na waliposema hakuna, aliwapa zile pesa zilizobakia kwa niaba ya Mtume. Kisha alirudi na kutoa taarifa kwa Mtume (s.a.w.) alichokuwa amekifanya naye akamsifu. Kisha Mtume (s.a.w.) akasimama na akielekea Qibla, akanyanyua mikono yake juu, na akasema: Ewe Allah (s.w.t.)! Mimi sina hatia mbele Yako kwa aliyoyafanya Khalid. Haya ameyafanya mara tatu.

Khalid na Abdur Rahman ibn Auf walijibizana kwa maneno makali kuhusu jambo hili. Huyu Abdur Rahman akamwambia Khalid: “Umefanya kitendo cha kipagani katika Uislamu.” Khalid akasema kwamba alikuwa amelipiza tu kisasi cha baba yake Abdur Rahman. Yeye akamjibu kwamba ni muongo kwa sababu yeye Abdur Rahman mwenyewe alimuua yule muuaji wa baba yake, lakini Khalid alilipiza kisasi cha ami yake hivyo kwamba kulikuwa na hisia mbaya kati yao.

Katika kuyasikia haya Mtume (s.a.w.) akamwambia Khalid: “Waache maswahaba wangu, kwani Wallahi kama ungekuwa na mlima wa dhahabu na ukautumia katika njia ya Allah (s.w.t.) usingeweza kukaribia sifa njema za maswahaba wangu.” (The Life of the Prophet)

Washington Irving

Akiwa kwenye ujumbe maalum (akiwa njiani kuelekea Tehama) Khalid bin Walid ilimbidi apitie kwenye nchi ya kabila la Jadhima. Alikuwa na watu 350 pamoja naye na alikuwa amefuatana na Abdur Rahman, mmoja wa waliosilimu mapema sana.

Maagizo yake kutoka kwa Mtume (s.a.w.) yalikuwa ni kuhubiri amani na mapenzi, kufundisha dini, na kujiepusha na vurugu, vinginevyo labda wakishambuliwa.

Sehemu kubwa ya hilo kabila la Jadhima walikuwa wameingia kwenye Uislamu lakini baadhi yao walikuwa bado ni wa dini ya Sabean. Katika wakati uliopita kabila hili lilipora na kumuua ami yake Khalid, pia na baba wa Abdur Rahman, walipokuwa wakirejea kutoka Arabia ya shangwe. Wakiogopa kwamba Khalid na jeshi lake wanaweza kulipiza kisasi kwa matendo yale mabaya, walijiandaa na silaha katika kuwasogelea kwao. Khalid kwa siri alifurahia katika kuwaona wakija (juu ya vipando vyao) kuwalaki katika mpango huu wa kivita. Akiwasalimia kwa sauti ya haraka haraka, aliwauliza kama walikuwa Waislamu au makafiri.

Walijibu kwa mkazo wa sauti ya kugugumia, “Waislamu.” “Kwa nini basi mnakuja kutulaki mkiwa na silaha mkononi?” “Kwa sababu tunao maadui miongoni mwa makabila ambao wanaweza kutushambulia sisi kwa ghafla,” walisema. Khalid kwa ukali kabisa aliwaamuru kushuka chini na kuweka silaha zao pembeni. Baadhi yao walikubali. Na mara moja walikamatwa na kufungwa kamba; wale waliobakia wakakimbia. Akichukulia kukimbia kwao kama kukiri makosa yao, aliwaandama kwa mauaji makubwa; akaiharibu nchi hiyo, na katika kuchemka kwa raghba yake aliwaua hata baadhi ya wale wafungwa.

Muhammad, wakati aliposikia juu ya hiki kitendo kiovu na cha kikatili, alinyanyua mikono yake juu mbinguni, na akamuomba Allah (s.w.t.) Ashuhudie kwamba yeye hakuwa na hatia juu ya hilo. Khalid wakati alipolaumiwa nalo wakati aliporudi, hakuwa na jibu akahamishia lawama zote kwa Abdur Rahman, lakini Muhammad akakataa kwa hasira tuhuma zozote dhidi ya mmoja wa wafuasi wake wa awali na mashuhuri. Yule Ali mkarimu alitumwa mara moja kwenda kurudisha kwa watu wa Judham kile ambacho Khalid alikinyang’anya kutoka kwao, na kufanya fidia ya kifedha kwa ndugu wa wale waliouawa.

Ilikuwa ni kazi inayoendana na tabia ya Ali, na aliitekeleza kwa uaminifu. Akiulizia juu ya hasara na mateso ya kila mtu mmoja, alimlipa mpaka akaridhika kabisa. Wakati kila hasara ilipokuwa imefidiwa, na damu yote kulipiwa, aligawanya zile pesa zilizobakia miongoni mwa watu, akifurahisha kila moyo kwa ukarimu wake.
Hivyo Ali alizipokea shukurani na sifa za Mtume, lakini huyu mlipiza kisasi Khalid alilaumiwa na hata wale aliofikiria kuwafurahisha. “Tazama” alimwambia Abdur Rahman, “Nimelipiza kisasi cha kifo cha baba yako.” “Badala yake sema,” huyu mwingine alimjibu kwa hasira, “umelipiza kifo cha ami yako. Umeifedhehesha dini kwa kitendo kinachomstahili muabudu sanamu.” (The Life of Muhammad)

Sir John Glubb

Baada ya kuikalia Makka, wajumbe walitumwa kwa yale makabila yanayoizunguka kuwasisitiza wao wAyaharibu masanamu yao ya kienyeji na madhabahu ya kipagani. Kikundi kimoja kama hicho kiliongozwa na Khalid bin Walid, yule mshindi wa Uhud. Khalid alikuwa ni mpiganaji mwenye mafanikio makubwa lakini mtu mkaidi, mwenye vurugu na mwenye kiu ya damu. Alitumwa kwa Bani Jadhima, ukoo wa Banu Kinana, katika ukanda wa Pwani Kusini-Magharibi ya Makka.

Kwa majonzi yaliyoingiliana wakati mmoja, hawa Bani Jadhima walikuwa wamemuua ami yake Khalid miaka mingi kabla, wakati alipokuwa anarudi kutoka kwenye safari ya kibiashara ya Yemen. Mtume, ambaye yumkini alikuwa hajui kwamba Khalid ana ugomvi binafsi na wale watu aliotumwa kuwasilimisha, alimwambia aepuke umwagaji damu. Wakati alipowakuta. Bani Jadhima, Khalid aliwaambia waweke silaha zao chini kwani vita ilikuwa imekwisha na kila mmoja sasa ameukubali Uislamu. Wakati walipokuwa wamefanya hivyo, hata hivyo, yeye ghafla alikamata idadi kadhaa ya watu hao, akawafunga mikono yao nyuma ya migongo yao, na akatoa amri kwamba wakatwe vichwa vyao, kama kisasi kwa ajili ya kuuawa kwa ami yake.

Mpanda farasi mmoja wa Kiarabu aliyekuwa pamoja na jeshi la Khalid, baadaye alieleza jinsi kijana mmoja wa Bani Jadhima, mikono yake ikiwa imefungwa, alivyomuomba yeye amruhusu kuongea na wanawake kadhaa waliokuwa wamesimama mbali kidogo.

Yule mwislamu alikubali na akamuongoza yule mfungwa kuelekea kwa wale wanawake. “Kwa heri, Hubaisha,” yule kijana alimwambia msichana mmoja miongoni mwao, “ maisha yangu yako mwishoni sasa.” Lakini msichana alipiga kelele, “Hapana, hapana, maisha yako yarefushwe kwa miaka mingi ijayo.” Yule mfungwa aliongozwa kurudishwa na mara moja akakatwa kichwa chake.

Alipokuwa anaanguka, yule msichana alitoka kwenye lile kundi la wanawake na akamkimbilia. Akimuinamia, alimgubika na mabusu mengi, akikataa kumuachia mpaka walipomuua na yeye pia.

Mtume (s.a.w.) kwa kweli alishitushwa pale aliposikia juu ya kitendo cha Khalid. Akiwa amesimama kwenye uwanja wa Al-Kaaba, alinyanyua mikono yake juu ya kichwa chake na akakemea kwa sauti: “ Ewe Allah! Mimi sina hatia mbele Yako kwa kile Khalid alichokifanya.” Ali alitumwa mara moja pamoja na fungu kubwa la pesa kulipa fidia ya damu kwa ajili ya wale wote waliokuwa wameuawa, na fidia ya ukarimu kwa ajili ya hasara yoyote ya mali. (The Life and Times of Muhammad, 1970, uk.320)

Muhammad Husein Haykal

Muhammad alikaa Makka kwa siku kumi na tano wakati ambapo alisimamia mambo ya mji huo na akawaelekeza watu wake kwenye Uislamu. Katika kipindi hiki, alitu- ma wajumbe kuwalingania watu kwa amani kwenye Uislamu na kuharibu masanamu bila ya kumwaga damu yoyote. Khalid ibn al-Walid alitumwa huko Nakhlah kumharibu al-Uzza, mungu wa kike wa Banu Shayban. Kazi yake ilipokamilika, ibn al-Walid aliendelea kuelekea Jadhimah. Kule, hata hivyo, watu walikamata silaha wakati wa kukaribia kwake. Khalid aliwaambia waweke silaha zao chini kwani watu wote walikuwa wameukubali Uislamu. Mmoja wa wale watu wa kabila la Jadhima aliwaambia watu wake: “Ole wenu, Banu Jadhima! Ninyi hamjui kwamba huyu ni Khalid? Wallah hakuna kinachowangojeni ninyi mara mtakapokuwa mmeweka chini silaha zenu isipokuwa utekwaji, na mara mtakapokuwa mateka, msitegemee chochote bali kifo.”

Baadhi ya watu wake wakajibu: “Unatafuta kutufanya sisi wote tuuawe? Wewe hujui kwamba watu wengi wameingia kwenye Uislamu, kwamba vita vimek- wisha, na kwamba usalama umerudishwa tena?” Wale walioshikilia wazo hili walien- delea kuongea na watu wa kabila lao mpaka wakasalimisha silaha zao. Papo hapo, ibn al-Walid akaamuru wafungwe kamba, na akawauwa baadhi yao.

Wakati alipozisikia habari hizi, Mtume (s.a.w.) alinyanyua mikono yake kuelekea juu mbinguni na akaomba: “Ewe Allah! Ninakishutumu kile Khalid ibn al-Walid alichokifanya.”

Mtume (s.a.w.) alimpa pesa Ali ibn Abi Talib na akamtuma kwenda kuchunguza mambo ya kabila hili, na kumtahadharisha kupuuza desturi zote za kabla ya Uislamu. Alipofika, Ali alilipa fidia ya damu ya waathirika wote na akafidia wenye mali zao kwa kuharibiwa kwao.

Kabla ya kuondoka, alizitoa zile pesa zote ambazo Mtume (s.a.w.) alimpa kwa kabila hilo kiasi tu kwamba kama kulikuweko na hasara zozote zile ambazo zingeweza kukosa kuonekana kwa wakati ule.
(The Life of Muhammad, Cairo,1935)

Ule ujumbe wa kidiplomasia ambao Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) alioufanya kwa kabila la Jadhima, kupitia kwa Ali, ulikuwa wa muhimu kabisa, Khalid alikuwa ameua watu ambao hawakuwa ni Waislamu tu bali pia walikuwa hawana hatia ya kosa lolote. Kukosa kufanya marekebisho ya maovu yake kungeweza kuwapatia Waislamu sifa sio tu kwa ukatili usio na maana na matumizi mabaya tele ya madaraka, bali pia kwa usaliti. Wapagani na wale Waarabu ambao wangeweza kuitwa Waislamu, katika tarehe hizi za mwanzo, kwa heshima tu, wangeweza, bila kukwepa, kuunganisha vitendo viovu vya Khalid na Mtume (s.a.w.) mwenyewe. Ilikuwepo hata hatari kwamba wataweza kuukana Uislamu na kurudi tena kwenye uabudu masanamu, kwa kumchukia Khalid tu. Mtume, kwa hiyo, aliingia ndani ya Al-Kaaba, na mara tatu akakikana hadharani kitendo cha Khalid, na akaiomba Mbingu iwe ni Shahidi kwamba hakuwa na lawama juu ya hilo.

Hawa Bani Jadhima waliachwa wamekongolewa na kuvunjwa kabisa na Khalid. Mtume (s.a.w.) alitaka sio kuwafariji tu na kuwajenga upya, bali pia kurudisha imani na mapenzi yao. Ilikuwa ni kazi ngumu na yenye kuhitaji uangalifu sana, na alimchagua Ali kuitekeleza. Khalid alikuwa ameharibu picha ya Uislamu, na Mtume (s.a.w.) alijua kwam- ba hakuna yoyote miongoni mwa maswahaba wake isipokuwa Ali aliyekuwa na uwezo wa kuirudishia mng’ao wake halisi. Ali alithibitisha mara nyingine tena kwamba bwana wake asingeweza kumchagua mtu yeyote bora kuliko yeye kwa kazi hii nyeti, na alidhihirisha mara nyingine tena kwamba alikuwa wa kwanza katika vita, na alikuwa pia ni wa kwanza katika amani.

Aliwashangaza na kuwavutia sana Bani Jadhima kwa uadilifu wake, ukarimu wake, wema wake, na kujihusisha kwake juu ya furaha yao na ustawi wao.

Kwa ubora wake wa kuhutubia, Ali alizikamata tena nyoyo za Bani Jadhima kwa ajili ya bwana wake, Muhammad Mustafa, na kwa Uislamu. Huu ulikuwa ni wajibu ambao ulikuwa “unaafikiana” na yeye kuutimiza. Aliupenda wajibu huu zaidi kuliko mtu mwingine yeyote. Alipenda kufunga vidonda vya kisaikolojia vya watu wengine, na alipenda kuleta furaha na faraja kwenye mioyo iliyo na majonzi. Alijaaliwa na kila kipawa maalum kutekeleza wajibu kama huu.