read

Kuuawa Kwa Ali

Kuanzia kwenye nusu ya pili ya mwaka 658, Mu’awiyah, gavana wa Syria, alikuwa akiendeleza kwa makini vurugu dhidi ya miliki za Ali. Uvamizi wake mwingine ulifika Ain-at-Tamar na Anbar, maili 170 tu kaskazini ya Kufa. Watu wa Kufa walikuwa hawapendi kupigana na watu wa Syria kiasi kwamba Ali aliona vigumu kuchukua hatua za kuadhibu zenye kufaa. Mu’awiyah binafsi aliongoza shambulizi kukatiza Jazirah kutoka Raqqa hakdi Mosul, na hakukutana na upinzani wowote mahali popote pake.

Mwishowe, Ali alitangaza ndani ya msikiti wa Kufa kwamba yeye ataondoka mjini hapo pamoja na wafuasi wake waaminifu wachache katika jaribio la kusimamisha uvamizi wa Syria dhidi ya Iraqi, hata kama itagharimu maisha yake.

Kitishio hiki kiliwaamsha raia wa Kufa kwenye tishio la kuachwa bila kiongozi kama Ali atakuwa auawe wakati akipigana dhidi ya Wasyria. Walichokozwa na kuchukua hatua na walianza kuhamasishana kwa ajili ya ulinzi.
Vita vya Siffin vilikuwa ni jaribio la kwanza la nguvu kati ya Ali na Mu’awiyah. Kimapambano, vita hivyo vilikuwa ni ushindi wa karibu kwa Ali, lakini kisiasa, viligeuka kuwa mvutano. Baada ya muda fulani ilionekana kwamba Ali angeishinda changamoto ya Mu’awiyah. Lakini mara tu Ali akauawa ndani ya Msikiti wa Kufa, na lile jaribio la pili la nguvu halikutokea kamwe.

Kwa mujibu wa maelezo ya kihistoria ambayo baadhi yao ni yenye kukubalika kabisa, Makhariji watatu walikutana hapo Kufa (wengine wanasema ni huko Makka) kubuni njama. Kila mmoja wao alijitolea kuwaua kila mmoja kati ya viongozi watatu mashuhuri katika Dar-ul-Islam – Ali, Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas. Kwa kuwauwa hao, inadaiwa, walitumainia kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya Uislamu, na kurudisha amani kwa umma wa Waislamu.

Mmoja wa wala-njama hao watatu alikuwa ni mtu mmoja aitwaye Abdur Rahman bin Muljim (La’natullah Alayhi.). Alikaa huko Kufa ili kumuua Ali, na wale wengine wawiliwakaenda Syria na Misri kumuua Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas. Mipango ya mauaji hayo ambayo yangetokea ya Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas, kwa mujibu wa Hadith zilizoko kwenye mzunguko, ilikwenda kombo, na wao walikamatwa na wakauawa.

Makhariji walikuwa wameshindwa pale Nahrwan, na wengi wao walikufa katika mapam- bano lakini wachache walikuwa wametoroka. Abdur Rahman bin Muljim (L.A.) alikuwa ni mmojawapo wa wale waliokuwa wametoroka. Alijawa na tamaa ya kumuua Ali, na alikuwa anaitafuta fursa hiyo ya kufanya hivyo. Kwa kutukizia, alikutana na mwanamke wa Kikhariji, aitwaye Qattama, ambaye baba yake na kaka zake waliuawa pia huko Nahrwan, na yeye pia alikuwa amelea chuki isiyokwisha juu ya Ali.

Abdur Rahman akatokea kumpenda Qattama, na akamposa. Mwanamke huyo akamwambia kwamba thamani ya mahari yake ilikuwa ni kichwa cha Ali ibn Abi Talib. Hii ilimuimarisha tu Abdur Rahman katika azma yake. Alimuahidi mpenzi wake mwezi kama angeuomba, lakini yeye akasema kwamba hakuna chochote ambacho kingemvutia yeye kama asingeweza kukipata kichwa cha Ali ibn Abi Talib!

Abdur Rahman bin Muljim (L.A.) aliitengeneza kwa uangalifu mipango yake ya kumuua Ali. Makhariji wengine waaminifu wachache walijitolea huduma zao kwake, na kwa pamoja walikariri mazoezi ya mauaji hayo. Abdur Rahman bin Muljim (L.A.) alichukua tahadhari moja zaidi – aliuloweka upanga wake kwenye sumu kali, na akiacha inywee kwenye upanga huo kwa siku tatu.

Asubuhi ya mwezi 19 Ramadhani ya mwaka wa 40 H.A., Ali alikuja kwenye Msikiti Mkuu wa Kufa, na akaadhini (mwito wa Swala). Yeye akachukua nafasi yake kwenye mihirabu, na baada ya muda waumini wakaanza kuwasili. Walisimama nyuma yake katika safu zilizofuatana, na Swala ikaanza. Waliosimama katika safu ya mbele, pamoja na waumini wengine, walikuwa ni Abdur Rahman ibn Muljim na wale alioungana nao (L.A.). Walikuwa wakiangalia nyendo za Ali.

Katika mikunjo ya majoho yao, walikuwa wamebeba panga zilizokuwa zimeng’arishwa kwa mng’ao wa hali ya juu, na zilizokuwa zimelowekwa kwenye sumu. Mara tu pale Ali alipogusa ardhi kwa paji lake la uso kwa ajili ya sajdah, Abdur Rahman bin Muljim (L.A.) alichomoka kwenye safu yake, na akanyemelea kwenye mimbari. Na mara tu Ali aliponyanyua kichwa chake kutoka ardhini, ibn Muljim (L.A.) akampiga dhoruba mbaya sana kwenye paji lake la uso kwa nguvu kubwa sana kiasi kwamba likapasu- ka.

Damu ilitoka kutoka kwenye paji la uso la Ali katika michirizi kadhaa, na yeye akaguta kwa mshangao: “Kwa jina la Mola wa al-Al-Kaaba, mimi nimefuzu!”

Watu waliokuwa kwenye jamaa ile walitambua kile kilichokuwa kimetokea, na mara tu walipohitimisha Swala hiyo, wakamzunguka. Wanawe, Hasan na Husein, wakambeba hadi nyumbani kwake. Mganga akaja, na akajaribu kulifunga lile jeraha la kutisha lakini hakuweza kuzuia kule kuvuja kwa damu. Dhoruba hiyo ya upanga ilikuwa mbaya sana kwa vyovyote vile, lakini ile sumu kutoka kwenye bapa lake ilikuwa pia ikienea kwa haraka sana katika mwili wake. Wanahistoria wa Kiarabu wanasema kwamba ilikuwa ni mara ya pili ambapo Ali alijeruhiwa katika paji la uso, mara ya kwanza ikiwa ni pale, katika vita vya Handaki vilivyopiganwa mwaka wa 627, upanga wa Amr bin Abd Wudd ulipasua kupita kwenye ngao na helmeti yake, na ukapiga kwenye hilo paji la uso. Paji lake la uso lilikuwa bado lina kovu lililoachwa na upanga wa Amr.

Haya ndio maelezo yaliyoachwa na wanahistoria wa Kiarabu juu ya kuuawa kwa Ali, na yamekubalika kuwa ni ya kweli na makundi makubwa ya Waislamu walio wengi. Ingawa maelezo haya yana idhini ya “makubaliano” (ijma) ya wanahistoria wengi nyuma yake, ukweli wake, hata hivyo, una mashaka kwa misingi ya “ushahidi wa kimazingira.” Kuna “migongano” mingi sana ndani yake.

Hakuna mtu anayetilia shaka ule ukweli kwamba alikuwa ni ibn Muljim aliyemuua Ali. Lakini je, lilikuwa ni wazo lake mwenyewe binafsi la kumuua yeye? Inawezekana kabisa kwamba wazo hilo lilipandikizwa akilini mwake na mtu mwingine ambaye alitumia mbinu zisizoelezeka ili kufanya hivyo. Ibn Muljim (L.A.) hakujua kwamba alikuwa ni mtumwa wa mtu, na aliendelea mbele na akamuua Ali.

Kwa wakati huu hakuna mtu katika Dar-ul-Islam aliyevutiwa sana na kuuawa kwa Ali kuliko Mu’awiyah. Mpango wa kumuua Ali, ustadi ulioonyeshwa katika utekelezaji wake, na mafanikio yake, vinaonyesha mguso wa werevu kamili na kiwango cha juu sana cha utaalam ambavyo vilikuwa ni sifa bainifu za Mu’awiyah pekee, ambapo ibn Muljim alikuwa si chochote zaidi ya boga. Mu’awiyah alitumia “ustadi” huo huo katika kuondoa kutoka kwenye mazingira, vitisho vya kweli au vya kudhaniwa, kwenye usalama na madaraka yake mwenyewe, katika matukio mengine mengi ya nyakati za baadae, pamoja na matokeo kama hayo hayo.

Wapelelezi wa Mu’awiyah walimwambia kwamba Ali alikuwa anafanya maandalizi kwa ajili ya kuishambulia Syria. Katika vita vya Siffin, Mu’awiyah alikuwa hakukubali busara aliyotendewa na Ali.

Safari hii, kwa hiyo, Ali alikuwa ameamua kutopigana vita vya kusitasita bali vya haraka haraka ambavyo vingekomesha maasi ya Mu’awiyah, na ambavyo vingerudisha amani kwenye himaya ya Waislamu yenye kujihami. Mu’awiyay pia alijua kwamba Ali alikuwa, safari hii, na vyote, uwezo na uamuzi wa kuufikisha mgogoro huo kwenye hatma ya haraka na ya mafanikio.

Tegemeo lake pekee, kwa ajili ya usalama wake hapo baadae, kwa hiyo, kama huko nyuma, lilikuwa kwenye msaada ambao angeweza kuupata kutoka kwa “marafiki” zake wa siku nyingi na wa kuaminika – usaliti na njama. Yeye kwa hiyo, akawahamasisha hao, na wao hawakumvunja matumaini.

Mu’awiyah alikifanya kile kitendo cha mauaji ya Ali kionekane ni cha papo hapo na cha kusadikika kwa kujifanya yeye mwenyewe na shoga yake, Amr bin Al-Aas, kuwa “waathirika” wenye uwezekano na waliokusudiwa wa njama na imani iliyopindukia ya wapinzani wa aina yoyote ya serikali wa Kikhariji.

Wote wawili “walikwepa” kuuawa kwa “mkupuo wa bahati njema” isiyo ya kawaida. Mmoja wao “alishikwa na maradhi” katika siku ile ambayo alikuwa “auawe,” na hakwenda Msikitini; mwingine hakuugua, lakini aliingia ndani ya Msikiti akiwa amevaa deraya yake chini ya joho lake. Yeye “alishambuliwa” na “muuaji” wake lakini “aliokolewa” na deraya yake. “Kuugua” kungekuwa ni kitendo kisichokuwa cha hadhari, na kingewafichua “waathirika” wote. Kwa namna hii, “ugonjwa” na “deraya” viliwaokoa wote Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas kutoka kwenye majambia ya “wauaji” wao wa Kikhariji.

Lakini Ali hakuwa na “bahati” sana. Hakuugua, na hakuvaa deraya yake wakati alipoingia Msikitini. Humo ndani ya Msikiti, Ibn Muljim alikuwa akimsubiri pamoja na upanga uliolowekwa kwenye sumu. Pindi Ali aliponyanyuka kutoka kwenye sajdah, alimpiga kwenye paji lake la uso, na akalitia ufa. Dhoruba hiyo ilionekana ya kufisha.

Wengi wa wanahistoria wa Kiarabu waliandika historia ambazo zilikuwa “zimepandikizwa” na Mu’awiyah na wafuasi wake. Yeye kwa kweli alikuwa huru kuingiza maelezo yoyote katika historia zile. Kwa hiyo, yeye alimudu kujiokoa yeye binafsi na Amr bin Al-Aas kutokana na mashtaka rasmi ya maandishi ya historia, na alikuwa ni ibn Muljim pekee aliyeingia kwenye vitabu vya historia kama mhalifu wa kweli na wa peke yake wa kosa hilo.

Kwa utukizi, mauaji ya Ali yalifanyika katika mkesha wa uvamizi wake wa Syria. Ingawa wapinzani wa aina yoyote ya serikali wa Kikhariji walikuwa wamelenga majambia yao kwa viongozi wote watatu mashuhuri wa kisiasa wa ulimwengu wa Kiislamu, yaani, Ali, Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas, kwa utukizi, hawa wawili wa mwisho waliyakwepa majaribio hayo juu ya maisha yao, na Ali peke yake ndiye aliyeuawa.

Kwa utukizi mwingine tena, hawa wawili waliokwepa, yaani, Mu’awiyah na Amr bin Al- Aas, walikuwa ni marafiki mwandani wa kila mmoja wao, na wote wawili walikuwa – utukizi tena – maadui wa kudumu milele wa huyu wa tatu, yaani, Ali, ambaye alikuwa ndie mmoja pekee aliyeuawa.

Kuna utukizi mwingi sana wa ajabu ambao uliokoa maisha ya Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas lakini ukachukua uhai wa Ali.

Ali alitumia muda uliokuwa umebakia kwake katika Swala na uchaji; katika kusoma imla ya wasia wake; katika kutoa maagizo kwa wanawe, mawaziri na makamanda kuhusu mwenendo wa serikali; na katika kuwasihi wote wasije kamwe wakawasahau wazee, wag- onjwa, masikini, wajane na mayatima kwa wakati wowote ule. Ali alitangaza kwamba mwanawe mkubwa, Hasan, atamrithi yeye kama kiongozi wa Mamlaka ya dini na ya dunia, na kama mtawala wa Waislamu wote.

Ingawa Ali alikuwa akizinduka taratibu kutokana na kuporeza damu na nguvu ya sumu, akili yake timamu ilikuwa elekevu na safi mpaka dakiki ya mwisho. Kwa wale watu wote waliokuja kumuona yeye, alisema kwamba walipaswa kutambua, kwa wakati wote, juu ya kuwepo kwa Muumba wao katika maisha yao, kumpenda Yeye, na kutumikia Viumbe Vyake.

Ile sumu ilikuwa imefanya kazi yake, na asubuhi ya mwezi 21 Ramadhani ya mwaka wa 40 H.A., Ali ibn Abi Talib aliiaga dunia hii kwenda mbele za Muumba wake ambaye alikuwa akimpenda na kumtumikia maisha yake yote. Alikuwa “amelewa mapenzi ya Mungu.” Shauku yake kubwa sana katika maisha ilikuwa ni kuwa na subira juu ya Muumba wake, kila wakati wa uhai wake, na aliifanikisha, na hii ndio maana ya ule mguto wake wa mshangao pale katika mihirabu ya msikiti pindi alipoihisi ile ncha ya upanga kwenye paji la uso wake: “Kwa Jina la Mola wa al-Al-Kaaba, mimi nimefuzu.”

Hasan na Husein waliosha mwili wa baba yao, wakaufunika kwenye sanda, wakaswali Swala ya jeneza kwa ajili ya mwili huo, na kisha wakauzika kimya kimya wakati wa usiku huko Najaf Ashraf, kwenye umbali kidogo kutoka Kufa. Hakuna alama zozote zilizowekwa kwenye kaburi hilo, na eneo la kaburi likafanywa siri, kama ilivyotakiwa na Ali mwenyewe.

Ali, mtu mwema sana wa Uislamu, shujaa, bingwa wa kuongoza shughuli za kiserikali, mwanafalsafa na shahidi, aliiaga dunia hii, na dunia haikuweza kupata mtu wa fahari kama yeye milele yote.

Wengi miongoni mwa Waislamu walikuwa ni waombolezaji wa kifo cha Ali lakini hakuna aliyemuomboleza yeye kwa majonzi sana kuliko ma-Dhimmi (Wayahudi, Wakristo, na Mamajusi). Wao walivunjika mioyo kabisa. Na pale wagonjwa, wasiokuwa na uwezo, walemavu, na mayatima na wajane katika dola hiyo waliposikia kwamba amefariki, walihisi kwamba dunia yao ilikuwa imeanguka. Yeye alikuwa ni baba kwao wote. Alikuwa amewashika wote mkononi. Aliwajumuisha wote katika Swala zake. Wengi miongoni mwao hawakuwa wakijua mpaka baada ya kifo chake kwamba alikuwa ni yeye aliyekuwa akiwalisha na kuwatunza. Yeye alikuwa amewashikilia wanadamu wote mkononi mwake.

Wakati ambapo Ali alikuwa akipatikana wakati wote kwa masikini na wanyonge, shauku na hofu yake kubwa yeye mwenyewe ilikuwa ni endapo mmoja wao akawa yeye hawezi kumfikia. Ilikuwa ni kwenye utawala wake tu ambapo ma-Dhimmi (wasiokuwa Waislamu), wasio na nguvu na wasio na ulinzi walipata usalama kamili. Hakuna hata mtu mmoja aliyeweza kuwatishia au kuwanyonya. Kwa kifo chake, usalama wao ulikuwa ume- toweka daima!

Ni kauli ya kweli kabisa kwamba matumizi ya madaraka hayawezi kuchanganyika na ufasihi wa wema, kwani mara tu mtu anapotwaa madaraka ya mambo ya umma, yale mafundisho mepesi ya maadili ambayo ndani yake inawezekana kabisa, kwa bahati, kuweza kuendesha maisha binafsi, mara yanafumba vya kutisha kwa kiasi kwamba yanazuia tofauti zote za wazi kati ya haki na batili.

Ukweli huu, hata hivyo, unalo kinzano lake lenyewe pekee – ndani ya Ali. Alitetea kanuni, katika maisha ya kijamii kama katika maisha binafsi, bila ya kujali gharama. Yeye siku zote aliweka jambo la sawa mbele ya jambo la werevu, bila ya kujali gharama. Chanzo cha kanuni hizo ambazo ziliongoza maisha yake ya binafsi na ya kijamii, kilikuwa ni Al-Qur’an al-Majid kama ilivyokuwa pia chanzo cha falsafa yake ya kisiasa.

Ali alikuwa na wakosoaji na maadui wengi lakini hawakuweza kuonyesha hata mfano mmoja ambapo alipotoka kutoka kwenye kanuni yoyote. Hawawezi kuonyesha mgongano wowote kati ya fikra na maneno yake kwa upande mmoja, au kati ya maneno yake na vitendo kwa upande mwingine. Kwa kawaida alikuwa na msimamo katika fikra, maneno na vitendo.

Ali alionyesha ushindi mkubwa kabisa wa tabia na itikadi. Alikuwa ni mkusanyiko wa nadra wa mapenzi juu ya Allah, bidii ya kazi, nguvu iliyoimarishwa na upendo, mpachano wa mpangilio, na uadilifu madhubuti.
Urithi wake mkubwa sana kwa ulimwengu wa Kiislamu utabakia daima kuwa ni tabia yake adhimu.