read

Kuzaliwa Kwa Ali Ibn Abi Talib

Ali alizaliwa tarehe 13 Rajab ya mwaka wa thelathini wa Tembo (A.D. 600). Binamu yake, Muhammad, alikuwa ana miaka thelathini wakti huo. Wazazi wa Ali walikuwa ni Abu Talib Ibn Abdul Muttalib, na Fatima, binti Asad, wote wa ukoo wa Bani Hashim.

Ali alizaliwa ndani ya Al-Kaaba huko Makka.Yule mwanahistoria maarufu, Masud, Herodotus wa Waarabu anaandika kwenye ukurasa wa 76 wa juzuu ya 2 ya kitabu chake, Murujudh-Dhahab kwamba moja ya ubora ambao Ali alikuwa nao ulikuwa kwamba alizaliwa ndani ya Nyumba ya Allah (s.w.t.) Baadhi ya mabingwa wengine ambao wathibitisha kuzaliwa kwa Ali ndani ya Al-Kaaba, ni :-

1. Muhammad Ibn Talha Shafii katika Matalibul-usul uk 11.
2. Hakim katika Mustadrak, uk. 483, Juz. 111.
3. Al- Umari katika Sharh Ainia uk. 15.
4. Halabi katika Sira, uk. 165, Juz. 1.
5. Sibt Ibnul- Jauzi katika Tadhkira Khawaisil Umma, uk.7.
6. Ibn Sabagh Malik katika Fusuulul Muhimma uk.14
7. Muhammad Ibn Yusuf Shafi’i katika KifAyatut-Talib uk. 261.
8. Shablanji katika Nurul Absar, uk. 76.
9. Ibn Zahra katika Ghiyathul Ikhtisar, uk.97.
10. Edvi katika Nafahatul Qudsia uk. 41.

Miongoni mwa wanahistoria wa kisasa, Abbas Mahmud al-Akkad wa Misri anaandika katika kitabu chake Al-Abqariyat ul-Imam Ali, (Cairo, 1970) kwamba Ali Ibn Abi Talib alizaliwa ndani ya Al-Kaaba.
Mwanahistoria mwingine wa sasa, Mahmud Said at-Tantawi, wa Supreme council of Islamic Affairs (Baraza la juu la Mashauri ya Kiislamu), Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, anaandika katika ukurasa wa 186 wa kitabu chake kiitwacho Min Fadha-il al-Ashrat al- Mubashirina bil-Janna, kilichochapishwa mwaka 1976 na Matab’a al-Ahram at-Tijariyya, Cairo, Misri hivi:- “Rehma za Allah (s.w.t.) ziwe juu ya Ali Ibn Abi Talib. Alizaliwa ndani ya Al-Kaaba. Alishuhudia kuchipuka kwa Uislamu; alishuhudia Da’wa ya Muhammad na alikuwa ni shahidi wa Wahyi (kushuka kwa Qur’an al-Majid). Mara moja tu aliukubali Uislamu ingawa alikuwa bado mtoto, na alipigana maisha yake yote ili kwamba Neno la Mungu liwe juu kabisa.”

Mshairi wa Kiarabu alitunga ubeti ufuatao juu ya kuzaliwa kwa Ali: Yeye (Ali) ndiye yule ambaye ile Nyumba ya Allah (s.w.t.), iligeuzwa kuwa wodi ya wazazi; Na yeye ndiye aliyeyatupa masanamu nje ya Nyumba hiyo; Ali alikuwa mtoto wa kwanza na wa mwisho, daima kuzaliwa ndani ya Al-Kaaba.

Ilikuwa ni desturi ya Waarabu kwamba wakati mtoto anapozaliwa, aliwekwa chini ya miguu ya sanamu au masanamu ya ukoo huo, hivyo kuashiria “kumkabidhi” kwa huyo mungu wa kipagani. Watoto wote wa Kiarabu “walitolewa” kwa masanamu isipokuwa Ali Ibn Abu Talib. Wakati watoto wengine wa Kiarabu walipozaliwa, mmoja wa waabudu sanamu alikuja kuwasalimia na kuwabeba mikononi mwake.

Lakini Ali alipozaliwa, Muhammad, mjumbe wa baadae wa Allah (s.w.t.) alikuja kwenye eneo la Al-Kaaba kumsalimia. Alimbeba mtoto huyo mikononi mwake, na kumtoa kwenye kumtumikia Allah (s.w.t.) Mtume huyu wa baadae lazima awe alikwishajua kwamba yule mtoto aliyekuwa mikononi mwake siku moja atakujakuwa adui asiyeshindika wa wanaoabudu masanamu wote na washirikina na wa miungu yao na miungu ya kike. Wakati Ali alipokua, aling’oa uabudu masanamu na ushirikina kutoka Arabia kwa upanga wake.

Kuzaliwa ndani ya Al-Kaaba kulikuwa ni moja kati ya sifa nyingi ambazo Mungu amez- ijaalia juu ya Ali. Sifa nyingine aliyokuwa nayo ni kwamba kamwe hakuabudu masanamu. Hii nayo inamfanya awe wa kipekee kwa vile Waarabu wote waliabudu masanamu kwa miaka na miaka kabla ya kukana uabudu masanamu na kuukubali Uislamu. Ni kwa sababu hii ambapo anaitwa, “Karama llahu waj-hahu” (Ambaye Allah (s.w.t.) ameutukuza uso wake.”)

Uso wake ulitukuzwa hasa na Allah (s.w.t.) kwani ulikuwa ndio uso pekee katika maswa- haba ambao kamwe haukuinama mbele ya Sanamu lolote.

Ali alikuwa ndiye mtoto mdogo kabisa katika familia hiyo. Kati ya kaka zake watatu, Talib na Aqil, walikuwa wakubwa kwa miaka kumi zaidi yake.

Kuzaliwa kwa Ali kuliujaza moyo wa nabii wa baadaye furaha isiyo kifani. Mtoto huyu alikuwa ni mtu mmoja “maalum” kwake yeye. Ingawaje Muhammad alikuwa na binamu wengi wengine na walikuwa na watoto wao mwenyewe, na Ali mwenyewe alikuwa na kaka zake wakubwa watatu; lakini hakuonyesha mvuto wowote juu ya yeyote kati yao.

Ali, na Ali peke yake ndiye alikuwa kitovu cha mvuto wake na mapenzi.

Wakati Ali alipokuwa na miaka mitano, Muhammad alimchukua kama mtoto wake wa kupanga, na kuanzia hapo tena hawakutengana tena daima. Kuna Hadith kwamba wakati mmoja kulitokea njaa huko Makka, na maeneo yanayoizunguka, na Abu Talib, akiwa katika dhiki kubwa wakati huo, alikuwa akiona ugumu kutunza kundi kubwa la watu. Ilimjia Muhammad kwamba alipashwa kujaribu kupunguza baadhi ya uzito wa majukumu ya ami yake, na alishawishika kwa hiyo, kumchukua Ali.

Ni kweli kwamba Muhammad alimchukuwa Ali lakini sio kwa sababu iliyoelezwa hapo juu. Katika nafasi ya kwanza kabisa, Abu Talib hakuwa kwenye hali ya dhiki kubwa kiasi kwamba hakuweza kumlisha mtoto wa miaka mitano; alikuwa ni mtu mwenye hadhi na uwezo, na misafara yake ilikwenda na kurudi kati ya Hijaz na Syria au kati ya Hijaz na Yemen.

Katika nafasi ya pili, kulisha mtoto wa miaka mitano kungekuwa vigumu kuleta tofauti yoyote kwa mtu ambaye alilisha hata wageni kama wangekuwa na njaa.

Muhammad na Khadija walimchukua Ali baada ya kufa kwa watoto wao wenyewe wa kiume. Ali kwa hiyo aliziba uwazi katika maisha yao. Lakini Muhammad, Mtume wa baadae, pia alikuwa na sababu nyingine ya kumchukua Ali. Alimchagua Ali kumlea, kumuelimisha na kumuandaa kwa ajili ya takdir kubwa iliyokuwa ikimngojea katika nyakati zijazo.

Dr. Taha Hussein wa Mirsi anasema kwamba Mtume wa Allah (s.w.t.) mwenyewe alikuwa kiongozi wa Ali, mwalimu na mwelekezaji, na hii ni sifa moja nyingine zaidi ambayo anayo Ali, na ambayo hakuna mwingine yeyote anayeshirikiana naye kwayo.

Kuhusu Uislamu imesemekana kwamba kati ya dini zote za dunia, ni hii moja pekee iliyokuwa katika mwanga wa historia, na hakuna sehemu ya Hadith yake iliyoko gizani.

Bernard Lewis Asema:

“Katika insha juu ya Muhammad na chanzo cha Uislamu, Ernest Renan anazungumzia kwamba, tofauti na dini zingine ambazo zilianzishwa kwa usirisiri, Uislamu ulizaliwa katika mwanga kamili wa historia. “Mizizi yake iko kwenye usawa wa ardhi, na maisha ya Mwanzilishi wake yanafahamika vema kwetu sisi kama ya wale waleta mabadiliko wa karne ya kumi na sita. (The Arabs in History, 1960)

G. E. Von Grunebaum:

“Uislamu unaweka tamasha la maendeleo ya dini ya ulimwengu katika mwanga wa historia.”
(Uislamu, 1969)

Kadhalika, inaweza kusemwa kwamba kati ya marafiki na Masahaba wote wa Muhammad, Mtume wa Uislamu, Ali ndiye pekee aliyekua katika mwanga kamili wa historia.

Hakuna sehemu ya maisha yake, ama katika uchanga wake, utoto wake, uvulana wake ujana wake, uanaume wake au kupevuka, ambayo imefichikana kutoka kwenye mwangaza wa historia. Alikuwa ndio kivutio kikuu cha macho yote tangu kuzaliwa kwake mpaka kufa kwake. Kwa upande mwingine maswahaba waliobakia wa Mtume (s.a.w.) wanakuja kwenye mvuto wa nadhari ya mwanafunzi wa historia baada tu walivyokubali Uislamu, na kidogo, kama kipo, kinajulikana mpaka kufikia hapo.

Ali alijaaliwa kuwa mkono wa kuume wa Uislamu, na ngao na kingio la Muhammad, Mtume wa Allah (s.w.t.) Takdira au maajaliwa yake yalikuwa kiungo kisichotenganishwa na takdira ya Uislamu, na maisha ya Mtume wake. Alikuwepo katika kila hali ya mambo katika historia ya harakati hii mpya, na alishika nafasi ya kuwa nyota ndani yake. Ilikuwa, kwa dharura, ni nafasi ambayo yeye pekee ndiye angeweza kuishika.

Aliakisi “taswira” ya Muhammad. Kitabu cha Allah (s.w.t.) chenyewe kimemuita “nafsi” au mwandani (nafsi ya pili) ya Muhammad katika Aya ya 61 ya Sura ya tatu, na alionyesha jina lake maarufu toka upande mmoja hadi mwengine, wa historia.

Katika miaka ijayo, muundo wa ufanyaji kazi pamoja wa Muhammad na Ali - amir na mfuasi – utakuja kuweka “Ufalme wa Mbingnii” katika ramani ya dunia.