read

Kuzaliwa Kwa Hasan Na Husein

Mnamo tarehe 15 ya mwezi wa Ramadhani ya mwaka wa 3 H.A. (Machi, 625), Allah (s.w.t.) aliridhia kumbariki binti ya Mtume Wake, Muhammad, kwa kuzaa mtoto wake wa kwanza. Muhammad Mustafa alikuja akionyesha furaha; alimchukua mtoto mchanga huyo mikononi mwake, akambusu, akamsomea adhana kwenye sikio lake la kulia, na iqamah kwenye sikio lake la kushoto; na akamwita Hasan.

Mwaka mmoja baadae, yaani, mnamo tarehe 3 Shaaban ya mwaka wa 4 H.A. (Februari, 626), Allah (s.w.t.) aliridhia kumpa binti ya Mtume Wake, mwanae wa pili. Mtume (s.a.w.) akaja, mwenye tabasamu na furaha, akamchukua mtoto huyo mikononi mwake, akambusu, akamsomea adhana kwenye sikio lake la kulia, na iqamah kwenye sikio lake la kushoto, na akamwita Husein.

Kuzaliwa kwa kila mmoja wa mabwana hawa kulikuwa ni tukio la kufurahia kwa Muhammad. Aliwachukulia kama miongoni mwa baraka kubwa za Allah (s.w.t.) na akamshukuru Yeye kwa ajili yao. Katika kuzaliwa kwa kila mmoja wao, Waislamu walim- iminika kwenye ule Msikiti Mkubwa na kumpongeza yeye. Aliwapokea kwa tabasamu na shukurani, na akashirikiana furaha yake pamoja nao.

Hapakuwa kamwe na siku ambayo Mtume (s.a.w.) hakutembelea nyumba ya binti yake kuwaona watoto wake. Alipendelea kuwaona wao wakitabasamu, hivyo aliwachekesha na kuwarusharusha; Aliwakumbatia na kuwadekeza, na alichukulia kila hatua yao na kila neno kama shani.

Wakati mabwana hawa wawili walipokua kidogo, na wakawa wanaweza kutembea hapa na pale, mara nyingi sana walitoka nje ya nyumba yao kuingia Msikitini. Kama babu yao alikuwa katikati ya hotuba, aliacha mara moja, akateremka kutoka kwenye mimbari, akawachukua mikononi mwake, akawabeba na kurudi nao, akawakalisha karibu naye mwenyewe juu ya mimbari, na kisha akaendelea na hotuba yake. Kama alikuwa anaongoza Swala ya jamaa, na alikuwa kwenye sijdah, watoto hawa wote, mara kwa mara, walipan- da juu ya shingo na mgongo wake.

Alipendelea kurefusha sijdah hiyo kuliko kuwavuruga, na kunyanyuka kutoka kwenye sajdah pale tu waliposhuka kutoka kwenye shingo au mgongo wake kwa hiari yao. Kama alitoka nje ya nyumba yake au Msikitini, walipanda mabegani mwake. Watu wa Madina waliwaita “Wapandaji wa Mabega ya Mtume wa Allah (s.a.w.),” walikuwa wamemganda sana yeye kuliko walivyowaganda wazazi wao wenyewe.

Muhammad, Mtume wa Uislamu, kamwe hakuwa na furaha zaidi kuliko alipokuwa na Hasan na Husein. Walikuwa ni matunda ya macho yake, na furaha ya moyo wake, na katika kuwa pamoja nao peke yao yeye alipata burudani ya kweli na kamilifu.

Alicheza pamoja nao mchezo wa kujificha na kutafutana, na kama walikuwa wanacheza na watoto wengine, alikaa karibu nao kiasi tu cha kusikia uzuri wa sauti ya kicheko chao. Kwa ajili yao, aliweza kuacha hata mambo muhimu ya nchi. Walipotabasamu, alisahau usumbufu na wasiwasi wote wa nchi na serikali. Alipenda kusoma kila ujumbe ambao walimwandikia katika tabasamu zao za kimalaika.

Mwanzoni, Mtume wa Allah (s.a.w.) alimlea binti yake mwenyewe, Fatima Zahrah, ambaye alimwita Bibi wa Peponi. Sasa alichukua wajibu wa kuwalea watoto wake wawili – Hasan na Husein – ambao aliwaita Mabwana wa Vijana wa Peponi. Kwake yeye elimu yao ilikuwa ni jambo lenye umuhimu mkubwa, na yeye mwenyewe alishughulikia kila jambo ndani yake. Lengo lake lilikuwa wazi: aliwataka wao kuwa mazao bora kabisa ya Uislamu, na walikuwa hivyo. Aliijenga tabia yake mwenyewe kwenye tabia zao, na akawafanya kuwa mfano kwa umma wake ambao ulikuwa uigize mpaka mwisho wa wakati wenyewe.

Ali na Fatmah Zahrah pia walikuwa na mabinti wawili – Zainab na Ummu Kulthum. Walipokua, waliolewa na binamu zao – watoto wa Jafar ibn Abi Talib, yule Shahidi mwenye Mbawa (Tayaar) wa Uislamu. Zainab aliolewa na Abdullah ibn Jafar, na Ummu Kulthum aliolewa na Muhammad ibn Jafar.

Hasan, Husain, Zainab na Ummu Kulthum, watoto wote wanne walistareheshwa na babu yao, Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) na siku za furaha sana katika maisha yao wote watano ni zile walizokuwa pamoja.

Kifo Cha Fatima Binti Asad, Mama Yake Ali Ibn Abi Talib

Katika mwaka wa 4 A.H (626 A.D.) Fatima binti Asad, mjane wa Abu Talib na mama yake Ali, alifariki hapo Madina.

Alimlea Muhammad, Mtume (s.a.w.) wa baadae, kama mwanae mwenyewe, naye Muhammad alimwita yeye mama yake. Alikuwa ndiye mwanamke wa pili katika Arabia kuukubali Uislamu, wa kwanza akiwa ni Khadija, mke wa Mtume.

Muhammad alimkosa mama yake mapema sana maishani lakini mara akapata mama wa pili kwa Fatima binti Asad. Yeye, kwa hiyo, hakukosa mapenzi na upendo ambavyo ni mama peke yake anayeweza kuvitoa. Wakati mama yake wa kunyonya alipofariki, alihudhuria mazishi, na akasema: “Allah (s.w.t.) airehemu roho yako tukufu. Ulikuwa kwangu mimi kama mama yangu mwenyewe. Ulinilisha mimi wakati wewe mwenyewe ukikaa na njaa. Lengo lako katika kufanya hivyo lilikuwa ni kumridhisha Allah (s.w.t.) kwa maten- do yako.” Alitoa shuka lake mwenyewe kwa ajili ya sanda yake, na alizikwa nalo. Alikuwa mara kwa mara akisema, “Nilikuwa yatima na akanifanya mimi ni mwanae. Alikuwa ndiye mtu mpole sana kwangu baada ya Abu Talib.”

Kaburi lilipochimbwa tayari, Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) aliliingia; alilala ndani yake, na akasema: “Ewe Allah! Uhai na mauti viko mikononi Mwako. Wewe peke yako ndiye hutakufa kamwe. Mrehemu mama yangu, Fatima binti Asad, na umpe jumba kubwa huko Peponi. Wewe ni Mwingi wa Rehema.” Wakati Fatima binti Asad alipozikwa, Muhammad Mustafa alirudia Allah-u-Akbar mara arobaini, na akaomba: “Ewe Allah! Muweke kwenye Nuru, na ujaze moyo wake na Nuru.”

Muhammad Mustafa alikuwa ndiye Mtekelezaji wa hati ya wosia ya Fatima binti Asad. Fatima binti Asad alikuwa ni mwanamke wa kipekee sana kwa vile watoto wawili kati ya watoto aliowakuza, Muhammad, na Ali, walitokea kuwa watu wa kipekee katika historia ya Uislamu. Nyumbani kwake ndipo chimbuko halisi la Uislamu. Wote Muhammad, Mtume (s.a.w.) wa baadae wa Uislamu, na Ali, shujaa wa baadae wa Uislamu, walizaliwa katika nyumba yake, na walikulia ndani yake. Wote walikuwa “Matunda” ya elimu yake.

Fatima binti Asad pia ni mama yake Jafar, yule shujaa wa vita vya Muutah, na Shahidi mwenye Mbawa (Tayaar) wa Uislamu. Hili jina la mumewe, Abu Talib, linajitokeza kwenye historia kama mfadhili mkubwa sana wa Uislamu, lakini nafasi yake Fatima katika Uislamu si ya umuhimu wa chini kuliko ya mumewe.

Anachangia sifa hiyo pamoja naye ya kumlea na kumsomesha Muhammad, Mtume (s.a.w.) wa baadae wa Allah (s.w.t.) Kama mumewe alimlinda Muhammad kutokana na maadui zake huko nje, yeye Fatima alimpa upendo, faraja na usalama huko nyumbani. Ilikuwa ni ndani ya nyumba yake ambamo Muhammad alipata usalama wa kihisia na ukaribu wa hisia wa familia.

Kama Khadija alikuwa ndiye mwanamke wa kwanza mwislamu na mfadhili mkubwa sana (mwanamke) wa Uislamu, Fatima binti Asad alikuwa mwanamke wa pili mwislamu, na mfadhili wa pili (mwanamke) mkubwa sana wa Uislamu. Allah (s.w.t.) awawie radhi waja Wake, Khadija na Fatima binti Asad, na Awarehemu hao.