read

Kuzaliwa Kwa Muhammad Na Miaka Ya Mwanzo Ya Uhai Wake

Abdullah alikuwa ndiye mtoto kipenzi cha Abdul Muttalib. Alipokuwa na umri wa miaka kumi na saba, alimuoa Amina, bibi wa uzao bora wa Yathrib, mji ulioko Kaskazini ya Makka. Hakuwa hata hivyo, amekadiriwa kuishi muda mrefu, na akafa miezi saba tu baada ya ndoa yake. Muhammad, Mtume wa Mungu wa wakati ujao, alikuwa bado mimbani. Sheikh Muhammad el-Khidhri Buck, profesa wa historia ya Kiislamu, chuo kikuu cha Misri, Cairo, anasema katika kitabu chake, Nur-ul-Yaqin fi-sirat Sayyid al-Murasalin (1953) hivi:

“Yeye (Muhammad Ibn Abdullah) alizaliwa katika nyumba ya ami yake, Abu Talib, katika “mtaa wa Bani Hashim” huko Makka, tarehe 12 Rabil-awal ya ule Mwaka wa Tembo, tarehe ambayo inaoana na tarehe 8 Juni 570. Mkunga wake alikuwa ni mama yake Abdur Rahmani Ibn Auf. Mama yake, Amina, alituma habari za uzazi huu wa kheri kwa babu yake, Abdul Muttalib, ambaye alikuja, akamchukuwa mikononi mwake, na akampa jina hili la Muhammad.”

Mgao wa Muhammad katika urithi wake ulikuwa ni mtumwa mmoja wa kike, Ummu Ayman; ngamia watano na kondoo kumi. Huu ni ushahidi kwamba Mitume wanaweza kurithi mali, na kama wanaweza kurithi mali toka kwa wazazi wao, wanaweza pia kurithisha mali kwa watoto wao wenyewe.

Kuwa mitume hakuwabatilishii wao katika kupokea urithi wao wenyewe wala hakuwabatilishii watoto wao kupokea wa kwao. Kauli hii inaweza kuonekana kama isiyofuata mantiki katika muktadha huu lakini sio. Muhammad, Mtume wa Uislamu, alitoa kwa mwanae, Fatima kama zawadi, shamba la Fadak.

Lakini alipofariki; Abu Bakr, aliyekuwa Khalifa, na Umar, Mshauri wake, walilikamata shamba hilo kwa kisingizio kwamba Mitume hawarithishi mali yoyote kwa watoto wao wenyewe, na mali yeyote wanayomiliki, inahusika baada ya kifo chao, sio kwa watoto wao, bali kwa umma wao. Ni faini kali ambayo mtu anapaswa kulipa katika Uislamu kwa kuwa tu mtoto au binti wa Mtume wake. Mtu mwingine yoyote katika umma huu anayo haki ya kurithi utajiri au mali ya baba yake lakini sio binti wa Muhammad, Mtume wa Allah (s.w.t.)!

Ilikuwa ni desturi miongoni mwa Maquraish kuwapeleka watoto wao jangwani kupitisha miaka yao ya mwanzo katika hali ya hewa ambayo ilikuwa ni yenye kutia afya kuliko ile ya Makka. Watoto walijenga miili yenye nguvu zaidi katika maeneo ya wazi na hewa safi ya jangwani kuliko ambavyo wangekuwa katika hewa ya mjini yenye kusonga na kukirihi.

Kulikuwa na sababu nyingine moja zaidi ya kwanini Waarabu wa koo bora waliwapeleka watoto wao kuishi jangwani. Walikuwa wanasisitiza ufasaha katika kuongea na walikuwa “washabiki” wakubwa wa maneno.

Walivutiwa na lugha ya Kiarabu, maneno yake, maana zao na tofauti ndogo ndogo katika maana zao; na walijivunia sana katika ufasaha wao binafsi. Kwa kweli, matabaka ya juu katika Makka walipata mamlaka yao juu ya uwezo wao wa balagha. Makka ilikuwa ndio sehemu ya makutano ya misafara mingi na Kiarabu chake kilikuwa kimechafuliwa na kuwa “Kiarabu pijini” (chenye maneno mchanganyiko).

Waarabu wa koo bora hawakutaka watoto wao kujifunza na kuongea kiarabu pijini cha Makka; waliwataka wazungumze tu lugha safi na isiyochanganywa ya jangwani. Wao, kwa hiyo, waliwapeleka watoto wao mbali na Makka ili kuwakinga kutokana na athari zote haribifu kama hizi katika miaka yao ya awali ya maisha yao.

Amina alimtoa mwanae, Muhammad, kwa Halima, mwanamke wa kabila la Banu Asad, aliyekuwa akiishi Mashariki ya Makka, kwa ajili ya malezi. Mtoto mchanga huyu, Muhammad aliishi miaka yake minne ya kwanza ya maisha yake huko jangwani na mama mnyonyeshaji wake. Wakati fulani katika mwaka wake wa tano wa maisha yake, mama huyu anasemekana alimrudhisha kwa mama yake huko Makka.

Muhammad alikuwa na umri wa miaka sita wakati Amina, mama yake, alipofariki. Alichukuliwa baadae na Abdul Muttalib, babu yake, mpaka nyumbani kwake. Lakini miaka miwili tu ilipita wakati Abdul Muttalib naye alipofariki.

Kabla tu ya kifo chake, Abdul Muttalib aliwaita watoto wake wote pamoja, na akawaambia kwamba anaacha “urithi” namna mbili kwao; mmoja ulikuwa uongozi wa ukoo wa Bani Hashim, na mwingine ulikuwa ni Muhammad Ibn Abdullah, mpwa wao, yatima wa miaka nane.

Kisha akawauliza ni nani miongoni mwao alitaka uwezo wake na mamlaka kama kiongozi wa kabila hilo, na ninani miongoni mwao atachukuwa dhima ya kijana huyo ambaye amepoteza shauku kubwa ya kufanywa kiongozi wa kabila lakini hata mmoja hakujitolea kuchukua dhima juu ya Muhammad.

Kama Abdul Muttalib alivyolitazama kusanyiko hilo na kutafakari maisha ya baadaye ya kijana huyo, Muhammad, ukimya wa wasiwasi ukatanda mahali hapo. Lakini haukuchukua muda mrefu. Abu Talib, mmoja wa watoto wake, alijitokeza mbele na akasema kwamba alimtaka yule mwana wa marehemu kaka yake, Abdullah, na kwamba hakuwa na haja yoyote ya mamlaka na madaraka.

Tamko hili la wazi la Abu Talib lilikamilisha suala hilo kwa Abdul Muttalib. Aliamua kumfanya Abu Talib sio tu mlezi wa Muhammad bali pia mlezi wa ukoo wa Bani Hashim.

Abdul Muttalib alitangaza, alipokaribaia kufariki, kwamba mwanae, Abu Talib, atamfuatia yeye kama kiongozi mpya wa Bani Hashim, na kwamba atakuwa pia mlezi wa Muhammad. Kisha akaliamuru kusanyiko hilo kumtambua Abu Talib kama kiongozi mpya wa Bani Hashim. Wao wakakubaliana, na akawaruhusu kuondoka.

Historia ilithibitisha uamuzi wa Abdul Muttalib. Mwanae na mirthi wake, Abu Talib, alitekeleza kazi zote kwa heshima sana.

Sir John Glubb:

“Katika mwaka wa 578 Abdul Muttalib alifariki. Kabla ya kifo chake, alimkabidhisha mwanawe, Abu Talib, kumuangalia Muhammad. Abdullah, baba yake Muhammad, alikuwa ndugu wa Abu Talib kwa baba na mama yao. Watoto wengine wa Abdul Muttalib ni dhahiri walitokana na wake wengine tofauti.
(The life and Times of Muhammad, 1970)

Abu Talib na mkewe walifurahi sana na kumpokea Muhammad kwenye familia yao. Hawakumchukua nyumbani kwao tu, bali mioyoni mwao pia, na walimpenda zaidi ya walivyowapenda watoto wao wenyewe.

Abu Talib alikuwa ni mtu mwenye hadhi kubwa na mwenye kuheshimika. Wakati wa wajibu wake kama kiongozi wa Bani Hashim alibeba vyeo vya “Bwana wa Quraish,” na “Kiongozi wa bonde”. Kama watu wengine wa kabila lake alikuwa pia ni mfanyabiashara, na misafara yake ilisafiri kwenda na kurudi hadi Syria na Yemen.

Katika kila msimu, misafara ya Abu Talib iliondoka Makka kwenda vituo mbalimbali. Mara chache, yeye mwenyewe aliandamana na msafara kusimamia mauzo na ununuzi wa bidhaa katika masoko ya kigeni. Muhammad akiwa bado mdogo anasemekana kasafiri naye kwenda Syria pamoja na msafara mmojawapo alipokuwa na miaka kumi na miwili.

Mapema katika maisha, Muhammad, nabii wa baadae alijenga sifa ya ukweli, uaminifu na maamuzi yenye busara. Kwa vile hakukuwa na mabenki siku zile, alikuja kuwa “benki” ya watu wa Makka. Walileta fedha zao, mapambo ya vito, na vitu vinginevyo vya thamani kwake kwa uhifadhi wa salama, na wakati wowote walipotaka kurudishiwa kitu chochote, aliwarudishia. Walimuita yeye al-Amin (Mwaminifu) na as-Sadiq (Mkweli).

Sir William Muir:

“Kwa kujaaliwa na akili safi adilifu na tamaa dhaifu, mkimya na mwenye mazingatio, yeye (Muhammad) aliishi zaidi kiupweke, na tafakari ya moyoni mwake ilimpa- tia shughuli kwa masaa ya mapumziko yaliyotumiwa na watu wenye tabia duni katika michezo ya kikatili na ufisadi. Tabia njema na muelekeo wa heshima wa kijana huyu asiyejionyesha vilimletea kukubalika kwa wananchi wenzie; na alipata lile jina, kwa kuafikiana kwa jumla, la Al-Amin, ‘mwaminifu.’ Hivyo aliheshimiwa na kutukuzwa, Muhammad aliishi maisha ya utulivu na ya kitawa katika familia ya Abu Talib.” (The life of Muhammad 1887, uk 20)

Wakati Muhammad alipokuwa na umri wa miaka ishirini, ilizuka vita miongoni mwa Maquraish, kabila lake, na kabila la Hawazin. Ingawa alikuwapo katika kampeni za vita hii, hakushiriki kwenye nafasi yoyote katika mapigano.

Hakuua au kujeruhi mtu yoyote, hivyo kuonyesha katika kipindi hiki cha mwanzo cha maisha yake, kuchukia kwake umwagaji wa damu. Anasemekana, hata hivyo, kuwahi kuokota mishale kutoka uwanjani, na kuitoa kwa ami zake ambao walikuwa wanapigana.

Miaka michache baadae, Muhammad aliingizwa kama mwanachama wa lile Shirikisho la Wenye Maadili. Kama ilivyotajwa mapema, hili Shirikisho limejiapia lenyewe kuwalinda wayonge, kuwapinga madhalimu na waonevu, kukomesha unyonyaji wa namna yoyote ile.

Ikumbukwe kwamba ulikuwa ni ukoo wa Bani Hashim, ambao Muhammad nabii wa baadae alitokana nao, ambao ndio ulioanzisha lile Shirikisho la Wenye Maadili. Lilikuwa ni jambo lililotukia tu! Hakuna njia ya kujibu swali hili. Lakini kwa taratibu zao za kisiasa, Bani Hashim walikwishatangaza vita juu ya udhalimu na dhulma. Waliweka wazi kwamba hawatakula njama na wenye nguvu dhidi ya wanyonge; wala hawangeridhia katika unyonyaji wa maskini kwa Maquraishi wa Makka.

Sio miaka mingi baadae, Muhammad alikuwa aanzishe utaratibu wa ujenzi upya wa jamii ya wanadamu, sehemu ya uchumi ambayo itatambua wazi uharibifu wa unyonyaji. Angezichukua zile “fursa” za Maquraishi na “haki “ zao za kunyonya maskini na wanyonge, kutoka kwao.

Montgomery Watt:

“Lile Shirikisho la Wenye Maadili linaelekea kuchukua sehemu muhimu sana kati- ka maisha ya Makka, na kwa sehemu kubwa kuelekezwa kwa watu na sera ambazo baadae Muhammad alijikuta anapingana nazo. Hususan ukoo wake wa Bani Hashim ulikuja kuwa na wajibu mkubwa katika Shirikisho la Wenye Maadili. (Muhammad, Prophet and Statesman, 1961)