read

Kuzgombea Madaraka – 2 Mkutano Wa Ansari Ndani Ya Saqifah

Mnamo A.D.622, ansari walimkaribisha muhammad (s.a.w.w.), mtume wa Allah (s.a.w.w) aliyebarikiwa, huko Madina, na walimkubali kama kiongozi wao wa kiroho na kidunia. Waislamu wengine wa Makka, yaani Muhajirina, pia walihamia Madina, na Ansari wakawakaribisha kwa mikono miwili. Walishirikiana nao majumba yao na chakula chao. Katika nyakati nyingi, waliwanyima watoto wao wenyewe chakula ambacho walikitoa kwa Muhajirina wenye njaa.

Muhammad (s.a.w.) aliifanya Madina kuwa makao makuu ya Uislamu, na kwa wakati huo, mji huo ukaanza kuchukua sifa bainifu za dola. Jinsi muda ulivyoendelea, ule mji mdogo dola ulikua na kuwa serikali imara yenye vyanzo vyake vya mapato, hazina yake, jeshi, mfumo wa sheria na utawala na vyombo vya kidiplomasia.

Ilikuwa haikwepeki kwamba itakuja kutokea kwa Ansari (na Waislamu wengine) kwamba siku itafika ambapo Muhammad (s.a.w.), mwanzilishi wa Dola ya Madina, atakuja kuwaaga na atakuja kuiaga dunia hii. Uwezekano huu uliwakabili pamoja na maswali mapya au hasa magumu kama vile:

1. Kifo cha Muhammad Mustafa (s.a.w.) kitakuwa na athari gani kwa Dola changa ya Madina na kwa umma wa Kiislam?

2. Ni nani atakayemrithi Muhammad (s.a.w.) kama kiongozi mpya wa Dola ya Madina wakati atakapofariki?

3. Ni ipi itakayokuwa hali ya Ansari baada ya kifo cha Muhammad (s.a.w.)? Huyo kiongozi mpya atakuwa maridhawa tu na muadilifu kama alivyo yeye?

4. Hivi Ansari wataendelea kuwa mabwana katika nchi yao wenyewe – Madina – baada ya kifo cha Muhammad (s.a.w.)?

Ansari walikuwa wamesikia ile hotuba ya Mtume. wa Allah (s.a.w.w) pale Ghadir-Khum akimteua Ali kama mrithi wake, na waliuunga mkono kwa moyo wote utaratibu huu. Lakini pia waliuhisi ule mkondo wa kichinichini wa uadui wa Muhajirina kwa Ali, na hawakuwa na hakika kama urithi wake utakuwa salama au kama utafanyika kamwe. Ilikuwa ni dhahiri kabisa kwao kwamba kulikuwa na upinzani mkubwa, miongoni mwa Muhajirina, juu ya urithi wake, na kwamba, miongoni mwao, alikuwa yu peke yake. Mara tu Ansari walipoupata ukweli huu, walianza kujishughulikia wao wenyewe. Ilikuwa ni kwa sababu hii ndipo wakajikusanya ndani ya Saqifah.

Mtu anaweza akakipuuza kitendo hiki cha Ansari hata kama mtu hatakisifu kwa sababu wazo kubwa sana katika akili zao, kufuatia kifo cha bwana wao, Muhammad (s.a.w.), lilikuwa ni la kujilinda. Ingawa walipaswa kuahirisha mkusanyiko wao wa kisiasa mpaka baada ya mazishi ya mwili wa bwana wao, kwa wakati huo ilijitokeza kwao kwamba walipaswa kushughulika mara moja, vinginevyo watakuwa wamechelewa sana.

Kama ilivyoelezwa kabla, Ansari walikuwa wametoa hifadhi kwa Uislamu katika wakati ambapo hali yake ilikuwa nyonge sana. Kwa ajili ya Uislamu, wamewafanya Waarabu wote kuwa maadui zao. Kwa ajili ya Uislamu, wamejidharaulisha mbele ya Arabia yote. Katika kila vita ya Kiislam, walijitoa wenyewe kwa heshima kabisa. Wengi wa vijana wao wameuawa kwenye vita hivi. (Katika vita vya Uhud, Waislamu 75 waliuawa; kati yao wanne walikuwa Muhajirina, na waliobakia wote walikuwa Ansari). Walionyesha mapen- zi yao kwa Uislamu na utii wao kwa Mtume (s.a.w.) katika kila sehemu.

Ansari walijua kwamba Ukhalifa ulikuwa ni haki ya Ali lakini walijua pia kuhusu “azimio” la Waarabu la kuuondoa ukhalifa nje ya nyumba ya Mtume (s.a.w.).

Tafsiri yao juu ya “azimio” hili lilikuwa kwamba Muhajirina hawatamuachia Ali akifikie kiti cha ukhalifa.

Lakini kama sio Ali, basi ni nani mwingine atakayekuwa mrithi wa Muhammad (s.a.w.)? Jibu pekee la wazi kwa swali hili lilikuwa: Ni Muhajirina mwingine. Lakini Muhajirina yeyote mwingine mbali na Ali alikuwa hakubaliki kwao – kwa Maansari. Wao, kwa hiyo, waliamua kuweka mgombea wao wa uongozi wa umma. Hata hivyo, ilikuwa ni msaada wao, uliokuwa sababu, na sio msaada wa Muhajirina, ambao uliofanya Uislamu kuwepo.

Wasiwasi wa Ansari ni wenye kueleweka vizuri sana. Kwao wao, matarajio ya Dola ya Madina kuangukia kwenye mikono ya Bani Umayya, maadui wa jadi wa Allah (s.w.t.) na Mtume Wake (s.a.w.), ambao sasa wamekuwa Waislamu, yalikuwa ya kuchukiza sana. Wao (Ansari) walikuwa wamewaua wengi wao katika vita vya Kiislam. Kama Dola ya Madina ambayo iliimarika kwa msaada wao, ikawa kamwe imetekwa na watoto wa wale wapagani ambao wao Ansari waliwaua, watawatendea vipi hao Ansari, lilikuwa ndio swali lisilotamkika lililo ndani ya moyo wa kila Ansari. Matukio yalithibitisha kwamba hofu yao haikuzalika kutokana na ndoto yoyote ile.

Bani Umayya walipigana kwa chuki sana dhidi ya Uislamu na Mtume Wake. Wakati Mtume (s.a.w.) alipoiteka Makka, wao “walisilimu” kwa sababu hakukuwa na chochote cha kufanya tena. Kama ilivyoelezwa kabla, Mtume (s.a.w.) hakuwapa kamwe nafasi yoyote ya madaraka ingawa aliwapa sehemu kubwa kutoka kwenye ngawira ya vita ya Hunayn. Kwa upande wake yeye, ilikuwa ni kitendo cha ishara ya mapatano lakini haikupunguza uadui wao kwa Uislamu.

Lakini Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Allah (s.w.t.) hakuwa amekufa kwa muda mrefu wakati Abu Bakr alipowainua hawa maadui wa jadi wa Uislamu, na maadui wa kiukoo wa Mtume wake (s.a.w.), kwenye vyeo vikubwa ndani ya jeshi. Alimfanya Yazid, mtoto wa Abu Sufyan, kuwa jenerali katika jeshi lake.

Wakati Syria ilipotekwa, Umar ambaye alimrithi Abu Bakr kama khalifa, alimfanya huyo Yazid kuwa gavana wa kwanza huko. Yazid alikufa miaka michache baadae ambapo Umar akamfanya mdogo wake, Mu’awiyyah, kuwa gavana mpya wa Syria. Kana kwamba alikuwa hajafanya ya kutosha kwa Bani Umayya, Umar, akiwa kwenye kitanda cha mauti yake, aliitengeneza hali katika namna ambayo ilihakikisha urithi wa Uthman, Bani Umayya mwingine. Katika ukhalifa wa Uthman, watu wa ukoo wake, Bani Umayya, walikuwa wakitawala kila jimbo katika himaya hiyo na walikuwa wakiongoza kila idara katika jeshi.

Ansari walihofia pia kwamba kama Muhajirina wataitwaa Dola ya Madina, basi wao (Muhajirina) wataidhalilisha misaada yao Ansari kwa Uislamu, na watawashusha kutekeleza wajibu, kama utakuwepo wowote, mdogo sana ndani ya Uislamu.

Kwa kujaaliwa na ujuzi wa kubashiri hali ya mambo kama walivyokuwa, Ansari walifanya uchambuzi sahihi na wa kweli wa hali hiyo. Mkusanyiko wao pale Saqifah ulikuwa moja kwa moja ni wa asili ya kujilinda. Ulichochewa na hisia tu za kupona. Lakini kwa bahati mbaya, waling’ang’ania husuda yao wenyewe. Husuda yao ilisababisha malengo yao yasifanikiwe. Tabaka zao za kikabila – Aus na Khazraji – zilitiliana shaka, na ilikuwa ni shaka hii ambayo iliwafichua kwa Muhajirina.

Kama ilivyokwisha kuelezwa, kitendo kile cha Ansari cha kukusanyika pale Saqifah kinaleta wasiwasi, lakini hisia yao ilikuwa na maana. Matukio ya baadae yalithibitisha vyakulitosha kwamba walikuwa sahihi na walikuwa na sababu ya kuhoji nia za Muhajirina juu yao. Miongoni mwa Muhajirina, mlinzi pekee wa maslahi yao alikuwa ni Ali ibn Abi Talib.
Lakini pale Maquraishi walipofanikiwa katika kumpinga asiingie madarakani, wal- ifanikiwa pia katika kuwateremsha hadhi hao Ansari mpaka kwenye hali ya watu wa kawaida tu.

Muhammad (s.a.w.) alipokufa, na urithi wa Ali kuzuiwa, Ansari walikoma kuwa mabwana nyumbani kwao wenyewe – Madina!