read

Maeneo Mapya Ya Uislamu

Yathrib ulikuwa ni mji kwenye chemchem karibu maili 250 kaskazini ya Makka. Mnamo mwaka wa 620 A.D., watu sita wa Yathrib walitembelea Makka kwa ajili ya Hija. Kukutana kwao kwa bahati na Muhammad kulisababisha kuingia kwao kwenye Uislamu. Walimwambia yeye kuwa waliiacha Yathrib katika hali ya kutokota na kwamba inaweza kulipuka wakati wowote kwenye vita.

Lakini walionyesha matumaini kwamba Allah (s.w.t.) atairudisha amani kwenye mji wao kupitia kwa Mtume Wake. Waliahidi pia kurudi Makka na kukutana naye mwaka unaofuata. Huu ulikuwa ndio mwanzo wa Uislamu huko Yathrib.

Wakati hawa Waislamu wapya sita waliporejea Yathrib, waliongea na jamaa zao na marafiki kuhusu Uislamu, na wakawaona wanaridhia, hata kuwa na shauku ya kusikiliza. Mwaka mmoja baadae, wakati msimu wa hija ulipofika, wenyeji kumi na wawili wa Yathrib, pamoja na wale sita wa mwanzo, walitembelea Makka. Miongoni mwao walikuwemo wanawake wawili pia.

Walikutana na Mtume wa Allah (s.w.t.) huko Aghaba. Aliwaelezea juu ya Shuruti za Imani katika Uislamu, na wote wakaukubali Uislamu. Wakati huo huo, walimpa pia kiapo chao cha utii. Hiki kinaitwa Kiapo cha Kwanza cha Aghaba.

Waislamu hawa walimhakikishia kwa dhati Mtume wa Allah (s.w.t.) kwamba:

Hawatamshirikisha Allah (s.w.t.) kamwe na yeyote, hawatamuabudu yeyote isipokuwa Allah (s.w.t.); hawatanyang’anya na kuiba kamwe; hawatawaua kamwe watoto wao wachanga wa kike; hawatawatukana watu wengine kamwe; hawatawakashifu tena wanawake; watakuwa sahihi na safi daima; watamtii Allah (s.w.t.) na Mtume Wake; na watakuwa waaminifu kwake wakati wote.

Hawa waumini wapya walimuomba Mtume (s.a.w.) kuwapa mwalimu wa kwenda naye Yathrib kuwafundisha Qur’an na maadili ya Uislamu. Alimtuma Mas’ab ibn Umayr, mmoja wa ami zake (Mas’ab alikuwa binamu ya baba yake), pamoja na kikundi hicho kwenda kuutangaza Uislamu huko Yathrib. Ujumbe wa Mas’ab ulifanikiwa, na familia nyingi huko Yathrib ziliukubali Uislamu.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Muhammad kuchagua mtumishi. Profesa Margliouth anasema kwamba Mas’ab ibn Umayr alikuwa chaguo la kwanza la mtumishi katika Uislamu.

Kiapo Cha Pili Cha Aghaba

Mwaka 622 A.D., wenyeji wa Yathrib sabini na watano walikuja Makka katika msimu wa hija.

Mtume (s.a.w.) alikutana nao mahali palepale huko Aghaba ambako alikutana na lile kundi la watu kumi na wawili mwaka uliopita. Watu hawa 75 waume kwa wake pia waliukubali Uislamu. Walimpa kiapo chao cha utii, na wakamkaribisha Yathrib.

Ami yake Mtume, Abbas ibn Abdul Muttalib, alikuwa pamoja naye safari hii. Anasemekana kwamba aliwaambia wale “wenyeji” kutoka Yathrib kuwa: “Muhammad anatukuzwa sana na watu wake mwenyewe. Kama mtaweza kusimama naye kwa heri na shari, mchukueni mwende naye Yathrib; la sivyo, basi liacheni suala zima.”

Mmoja wa viongozi wa watu wa Yathrib alikuwa ni Bira’a ibn Ma’ruur. Alisema: “Tulipokuwa watoto, wanasesere wetu tuliokuwa tukiwapenda sana walikuwa ni panga na mikuki.” Mkuu mwingine, Abul Haithum, alimkatisha, na akasema: “Ewe Mjumbe wa Allah (s.w.t.)! Kitatokea nini wakati Uislamu utakapokuwa mkubwa na wenye nguvu? Hapo tena wewe utaondoka Yathrib na kurejea Makka?”

Muhammad Mustafa akatabasamu na kusema: “La hasha. damu yenu ni damu yangu na damu yangu ni damu yenu. Tokea siku ya leo ninyi ni wangu na mimi ni wenu, na sitaten- gana nanyi kamwe.”

Waislamu wale wa Yathrib waliridhika na uhakikisho waliopewa na Muhammad Mustafa, na wakarudi Yathrib kuueneza Uislamu miongoni mwa jamaa zao. Uislamu ukaanza kupa- ta maendeleo imara huko Yathrib. Ilipoonekana kwamba imani hii mpya imepata mahali pa usalama katika mji ule, Mtume (s.a.w.) aliwashauri wale waathirika wa mateso pale Makka kuhamia pale. Kwa kufuata ushauri wake, Waislamu wakaanza kuondoka Makka, katika vikundi vidogo vidogo, na kuanza makazi katika majumba yao mapya hapo Yathrib.

Kile Kiapo cha Pili cha Aghaba ni tukio muhimu katika historia ya Uislamu. Kilikuwa ndio nanga ambayo juu yake kile chombo dhaifu kilikuja kupumzika mwishoe, baada ya kurushwa huku na kule kwa miaka kumi na tatu katika bahari zisizodhibitika za upagani ndani ya Arabia.

Hajira (Kuhama)

Wakati wengi wa Waislamu walipoondoka Makkah na kufanya makazi huko Yathrib, ilionekana kwa waabudu masanamu kwamba kama Uislamu utapata mizizi katika ile Nchi ya CHEMCHEM iliyopo kaskzini mwao, na ukaweza kujitegemea, itakujaleta tishio kwenye maslahi yao ya kibiashara huko Syria. Waliuona Uislamu kama “hatari kubwa” mpya inayonyanyua kichwa chake huko kaskazini. Kwa hiyo, waliitisha mkutano katika ukumbi wao wa jiji ambamo walifikiria njia yenye kufaa zaidi ya kuivuruga mapema hii “hatari kubwa”. Baada ya majadiliano kiasi, walikubaliana, kwa pamoja, kwamba njia ya pekee ya kuizuia hii hatari kubwa mpya, ni kwa kumuua mwanzilishi wake – Muhammad mwenyewe – akiwa angali bado yupo Makka.
Uamuzi huu ukazua maswali mengine machache kama vile ni nani atakayemuua, vipi, lini na wapi. Wakayajadili zaidi maswali haya, wakafikiria uwezekano wa namna nyingi, na hatimae wakaamua, kwa pamoja tena, kwamba mpiganaji mmoja kutoka kila ukoo wa kila kabila linaloishi Makka na viunga vyake, atachaguliwa; wote watashambulia nyumba ya Muhammad kwa wakati mmoja, na watamuua, kabla tu ya alfajiri ya siku inayofuatia. Tendo lililofanywa kwa pamoja kama hilo, waliamini, “lingewakwamisha” Bani Hashim ambao hawangeweza kuwa na uwezo wa kupigana dhidi ya koo zote hizo kwa wakati mmoja kwa kulipiza kisasi cha kuuawa kwa Muhammad.

Mtume, hata hivyo, alikuwa tayari kukutana na dharura kama hii. Kwa kuarifiwa wakati wa mpango wa Maquraishi wa kumuua, na mtu aliyesilimu kwa siri. Alimwita binamu yake mpendwa, Ali ibn Abi Talib, akamfahamisha ule mpango wa Maquraishi, na wa kwake mpango wa kuwazidi maarifa. Mpango wake ulikuwa ni kumuweka Ali kwenye kitanda chake yeye mwenyewe, na kisha kutoroka nje ya nyumba hiyo wakati wowote wenye fursa. Hao Maquraishi, kwa kumuona Ali akiwa amefunikwa na shuka, watadhania kwamba Muhammad alikuwa amelala, alimueleza.

Alimuomba Ali pia kurudisha dhamana zote za wapagani kwa wenyewe, na kisha kuondoka Makka na kumkuta yeye huko Yathrib. Ali alielewa kila kitu, na Mtume (s.a.w.) akamdhamini kwenye ulinzi wa Allah (s.w.t.)

Muhammad Husein Haykal

Wale vijana ambao Maquraishi waliwaandaa kwa ajili ya kutekeleza mauaji ya Muhammad walikuwa wamezingira nyumba yake wakati wa usiku ili asije akatoroka. Katika huo usiku wa Hajira, Muhammad alitoa siri ya mpango wake kwa Ali ibn Abi Talib na akamuomba ajifunike shuka la kijani la Mtume, na alale kwenye kitan- da cha Mtume. Alimuomba tena akae hapo Makka mpaka atakapokuwa amerudisha vitu vyote vya thamani vilivyokuwa vimewekwa kwa Muhammad, kwa wenyewe.
(The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Marmaduke Pickthall:

“Wauaji walikuwa mbele ya nyumba yake (Muhammad). Alitoa shuka lake kwa Ali, akimtaka alale kwenye kitanda hicho ili kwamba yeyote atakayekuwa anatazama ndani angefikiria kwamba Muhammad amelala pale. (Introduction to the Translation of Holy Qur’an, Lahore, 1975)

Washirikina waliizunguka nyumba ya Muhammad. Walichungulia ndani wakaona mtu aliyelala amefunikwa na blanketi, na wakaridhika kwamba “windo” lao liko salama. Ule wasaa wa fursa kwa ajili ya Mtume (s.a.w.) kutoroka ulifika muda baada ya usiku wa manane wakati ambapo wale askari wa doria wamesinzia. Alitembea kimya kimya na kuwapita na kutoka nje ya maeneo ya nyumba yake.

Wale askari wa doria wa kipagani walikutwa wamejisahau, na Mtume wa Allah (s.w.t.) alifanikiwa katika kuukwepa kwa hila uchunguzi wao!

Ali alilala kwenye kitanda cha Mtume (s.a.w.) usiku mzima. Kabla tu ya mapambazuko, wale wauaji wa kipagani wenye kuhifadhi vichwa vya maadui, walivamia ndani ya nyum- ba panga zikiwa zimechomolewa kwenda kumuua Mtume. Lakini mshangao wao na mfadhaiko havikuwa na mipaka pale walipotambua kwamba alikuwa ni Ali na sio Muhammad ambaye alikuwa amelala pale kitandani. Wakamkamata Ali kwa kumhoji na pengine kwa kumtesa.

Lakini mkuu wa wale askari wa doria akawaambia kwamba Muhammad hawezi kuwa amekwenda mbali sana, na kwamba wanaweza bado kumkamata kama hawatapoteza muda wao wenye thamani katika kumhoji Ali, hapo ndipo wakamuachia. Tukio hili linaitwa katika historia ya Kiislam Hajira au Kuhama.

M. Shibli, mwanahistoria ya Kiislam mashuhuri wa Kihindi, anaandika katika wasifa juu ya Mtume wa Allah (s.a.w.): “Wapagani wa Makka walimchukia Muhammad, na bado walimuamini. Yeyote aliyekuwa na vitu vya thamani, alivileta na kuvihifadhi kwake. Alikuwa ndiye “mwenyebenki” wao. Alitambua juu ya mpango wa Maquraishi wa kumuua yeye. Kwa hiyo, yeye, akamwita Ali na akasema: “Allah (s.w.t.) ameniamuru mimi kwenda Yathrib. Wewe utalala kwenye kitanda changu na kesho urudishe amana za watu wa Makka kwa wenyewe.”
Hii ilikuwa ni hali yenye kuleta maafa na yenye hatari mbaya sana. Ali pia alijua kwamba Quraishi wamekusudia kumuua Mtume wa Allah (s.a.w.) usiku ule, na kwamba kulala kwenye kitanda chake ni kulala katika meno ya kifo. Lakini ni lini ambapo Ali alikiogopa kifo? Yule shujaa wa Khaibar akalala kwenye meno ya kifo usingizi mzito ambao hajawahi kuulala maishani mwake mwote.
(Life of the Apostle of God, Azamgarh, India, 1976)

Mtume (s.a.w.) hakuwa na muda wa kumwelezea Ali kwa kinaganaga ni amana ngapi alikuwa nazo na zilikuwa zikadhiwe kwa nani. Ilitosha kwake yeye kumwambia Ali arudishe amana zote kwa (wapagani) wenye mali zao, na yeye (Ali) akafanya hivyo. Ilikuwa kama vile tu kwenye karamu ya Dhul-Ashiira wakati kile ambacho Mtume (s.a.w.) alikuwa afanye, kilikuwa ni kumwambia tu Ali awakaribishe kwenye chakula watu wazima wote wa ukoo wa Bani Hashim.

Hakukuwa na maelekezo ya kina yaliyokuwa lazima. Ali bila ya kufikiri alielewa nini bwana wake alichokitegemea kutoka kwake. Kule kukabidhiwa kurudisha zile amana za watu wa Makka kwao, ni ushahidi tosha kwamba Ali alikuwa msiri na “mwandishi binafsi” wa Mtume wa Uislamu hata kabla ya kule Kuhama kwenda Yathrib.

Ikiwa Hajira inasisitiza uaminifu wa Ali usio na mjadala kwa bwana wake, Muhammad, inaonyesha pia ujasiri wake wa ajabu. Wale askari wa doria wa maadui wangeweza kumuua ama kwa kuamini kwamba alikuwa ni Muhammad, au katika kugundua kwamba siye, kwa kuvunjika moyo tu.

Alilijua hili vizuri sana, lakini kwake yeye hakuna hatari iliyokuwa kubwa sana kama angeweza kuokoa maisha ya Mtume wa Allah (s.a.w.). Ilikuwa ni kujitolea huku na ujasiri huu kuliko mpatia ushindi yeye wa sifa nyingi za Qur’an Tukufu. Qur’an imetoa sifa kwenye uaminifu wake na ujasiri wake alioonyesha katika usiku ule wa majaaliwa wa Hajira (Kuhama) kama ifuatavyo:

وَمِنَ النَّاسِ مَنْ يَشْرِي نَفْسَهُ ابْتِغَاءَ مَرْضَاتِ اللَّهِ ۗ وَاللَّهُ رَءُوفٌ بِالْعِبَادِ {207}

“Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Allah. Allah ni mpole kwa waja wake.”(Sura ya 2; Aya ya 207)

Razi, yule mfasiri maarufu wa Qur’an, anasema ndani ya Tafsir Kabir yake (juz. 2,uk.189) kwamba Aya hii ilishuka hasa kwa kutambua kazi kubwa na tukufu ya Ali katika usiku wa Hijiria alipomuwezesha Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) kuondoka Makka. Kwa sababu ya Ali, aliweza kuondoka kwa usalama.

Katika usiku ule wa kihistoria, ilifanyika shughuli ya kibiashara ya ajabu na ya kimuujiza, ya kwanza na ya mwisho ya aina yake katika historia nzima ya Maumbile. Yalikuwa ni mapatano ya kuuza-na-kununua kati ya Allah (s.w.t.) na mmoja wa waja Wake. Mja aliyehusika hapa ni Ali ibn Abi Talib.

Katika usiku mkimya na usio na mbaramwezi, Allah (s.w.t.) alikuja kwenye “soko” kama “Mteja.” Alikuja kununua bidhaa maalum. Mja Wake, Ali, alikuja kwenye “soko” kama “mfanyabiashara.” Shughuli yake: kuuza ile bidhaa ambayo Allah (s.w.t.) alikuwa anaitafuta. Hiyo “bidhaa” ilikuwa ni roho yake, maisha yake!

Allah (s.w.t.) huyo “Mteja” aliangalia sana sifa ya “bidhaa” hiyo, na akaiona ni bora sana. Yeye, kwa hiyo, aliamua kuinunua papo hapo. Alilipa “thamani” yake kwa huyo “mfanyabiashara,” na bidhaa ikabadilishanwa, sawasawa kama kwenye mapatano ya biashara nyingineyo ile. Kutokea muda ule, ile “bidhaa” – maisha ya Ali – ikakoma kuwa yake, na ikawa mali pekee ya Allah (s.w.t.) Yale mapatano ya kuuza na kununua kati ya Bwana na mtumwa kwa hiyo yakakamilika, kwa ridhaa kamili ya pande zote.

Walikuwepo “mashahidi” pia wa mapatano haya. Walikuwa ni Malaika na nyota – wengi mno – wakiangalia kutoka kwenye “majumba yao ya kisanii” ya mbinguni.

Walitazama kwa kimya cha mshangao na kimya cha uvutiwaji vile Ali alivyouza maisha yake kwa Allah (s.w.t.) Qur’an Tukufu ikawa ndio “msemaji” wao kwa watu wa dunia hii, na ikaandika kile wao – hao mashahidi – walichokiona katika usiku ule wa kukumbukwa.

“Kumbukumbu” ya mapatano haya, kama ilivyohifadhiwa na Qur’an, tunayo hivi sasa, na ni ya kudumu na isiyoweza kuharibiwa. Itadumu kwenye dunia hii kwa muda ambao wale Malaika na zile nyota – “wale mashahidi” wa mapatano hayo – watakavyodumu huko Mbinguni!

Ali aliuza ile “bidhaa” kwa Allah (s.w.t.) Sasa akiwa ameondokana na ule “wasiwasi” kwa ajili ya usalama wa ile “bidhaa,” angeweza kulala, na akaenda kulala – kwenye kitanda cha Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.). Katika Usiku ule wa Majaaliwa, alilala fofofo. Wakati wa alfajiri, alipoamka, au kwa usahihi zaidi, alipoamshwa na sauti kubwa na mgongano wa mikuki na panga za wale wauaji wenye kuhifadhi vichwa vya maadui, waliotumwa na Maquraishi, kumuua Muhammad, alikwishapata uzima!

Katika waja Wake wote, Allah (s.w.t.) alimchagua Ali kutekeleza Mpango Wake. Mpango ule ulikuwa ni kumlinda Mtume Wake, kutokana na maadui zake. Hawa maadui walik- wishaandaa mpango kwa ajili ya kuangamiza Uislamu. Waliamini kwamba kama wangemuua Muhammad, Uislamu ungeangamia. Wao, kwa hiyo, wakapanga na kula njama za kumuua Muhammad. Bali hawakujua kwamba Allah (s.w.t.) alikuwa na mpango wake mwenyewe – Mpango-Tibuzi (wenye kutibua) – tayari kwa ajili ya tukio hili.Ulikuwa ni Mpango-Tibuzi wa Allah (s.w.t.) ambao ulikuwa uje kuwakwamisha Maquraishi kwa kuokoa maisha ya Mtume Wake. Rejea ya Qur’an kwenye Mpango-Tibuzi wa Allah (s.w.t.) inapatikana kwenye Aya ifuatayo:

وَمَكَرُوا وَمَكَرَ اللَّهُ ۖ وَاللَّهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ {54}

“Na makafiri walipanga mipango na Allah akapamnga mipango, na Allah ndiye mbora wa wenye kupanga.” (Sura ya 3: 54)

Ali ibn Abi Talib alikuwa ndiye “kiungo muhimu” katika Mpango-Tibuzi wa Allah (s.w.t.) Jukumu la Ali lilihakikisha mafanikio ya Hajira (Kuhama) ya Muhammad, na mafanikio hayo ya Hijira peke yake yalifanya kuanzishwa kwa dola ya kisiasa ya Madina kuwezekana. Kama Hajira ingeshindwa, hiyo Dola ya Madina kamwe isingekuja kuwepo. Hiyo Dola ya Madina ndio lilkuwa chombo cha kimaada cha Utawala wa Mbinguni wa mwanzo na wa mwisho Duniani. Allah (s.w.t.) alimfanya mja Wake, Ali ibn Abi Talib, kuwa chombo ambacho kupitia hicho Aliuweka ule Utawala katika dunia hii.

Wakati Muhammad alipokuwa ametoka nje ya mzingo wa nyumba yake, alikwenda kwenye nyumba ya Abu Bakr, na akamwambia kwamba Allah (s.w.t.) amemuamuru kuon- doka Makka usiku uleule. Kwa vile hawakuwa na muda wa kusita, waliuondoka mji mara moja, na wakaenda kwenye pango linaloitwa Thaur Kusini ya Makka. Walilifikia pango hilo na wakaingia kukiwa bado kuna giza.

Walikuwa wamejificha ndani ya pango hilo wakati, masaa machache baadae, wale wauaji walipotokea pia katika ufukuzaji wao. Kwa mujibu wa Hadith, buibui alitanda utando kwenye mlango wa pango, na ndege alitaga yai hapo mlangoni. Wale wauaji walihoji kwamba kama mtu yeyote angeingia ndani ya pango, ule utando na yai vingevunjika, lakini kwa vile vyote ni vizima, hakuna aliyeingia humo. Hivyo kwa kuridhika kwamba wale watoro hawakuwa ndani ya pango lile, waliacha msako wao na wakarudi Makka.

Wakati wale wauaji wakiwa wanajadili ile hoja ya kama waingie au wasiingie kule pangoni kuwakamata hao watoro ambao wanaweza kuwa wamejificha ndani yake, Abu Bakr alishikwa na hofu, na akamwambia Mtume: “Sisi tupo wawili tu na maadui zetu ni wengi sana. Tuna nafasi gani ya kuokoa maisha yetu kama wataingia hapa pangoni?”

Mtume (s.a.w.) akasema: “Hapana. Hatupo wawili. Yupo Wa Tatu pamoja nasi, naye ni Allah (s.w.t.)” Tukio hili limetajwa ndani ya Qur’an Tukufu kama ifuatavyo:

إِلَّا تَنْصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّهَ مَعَنَا ۖ فَأَنْزَلَ اللَّهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ{40}

“Na Allah alimnusuru Mtume Wake walipomtoa waliokufuru. Na walipokuwa pangoni, alimwambia sahibu yake: “usihuzunike. Hakika Allah yuko pamoja nasi.” Na Allah akamteremshia utulivu juu yake (Mtume).” (Sura ya 9; Aya ya 40)

Mtume (s.a.w.) pamoja na Abu Bakr walikaa kwa siku tatu ndani ya pango hilo. Huko Makka, kwa wakati huu, shauku ya kumkamata Mtume (s.a.w.) imepungua. Katika siku ya nne, Abdullah, mtoto wa Abu Bakr, alikuja na ngamia wawili kwa ajili ya kupanda wao. Abu Bakr alimtoa mmoja wa ngamia hao kwa Mtume (s.a.w.) lakini akakataa kumpokea kama zawadi, na akalipa bei yake kabla ya kumpanda. Yeye na Abu Bakr ndipo wakapan- da ngamia hawa, na wakiiambaa Makka kuelekea kaskazini na Mashariki, walisafiri kuelekea Yathrib upande wa kaskazini.

Muhammad ibn Ishaq:

“Pale Abu Bakr alipoleta wale ngamia wawili kwa Mtume, alimtoa yule mbora zaidi kwake na akamuomba ampande. Lakini Mtume (s.a.w.) alikataa kumpanda mnyama ambae hakuwa wake binafsi, na wakati Abu Bakr alipotaka kumpa ngamia huyo, alitaka kujua alichokuwa amelipa kumnunua, na akamnunua kutoka kwake.” (Life of the Messenger of God)

Wasafiri hawa wawili wakatembea umbali kati ya Makka na Yathrib kwa siku tisa, na siku ya kumi wakafika Quba, mahali palipo maili mbili Kusini ya Yathrib ambapo walikaa kati- ka nyumba ya Kulthum bin Hind, kama wageni wake. Mtume (s.a.w.) aliamua kusubiri kuwasili kwa Ali kutoka Makka kabla ya kuingia Yathrib. Katika wakati huo, alijenga msingi wa Msikiti hapo Quba. Lilikuwa ni jengo lisilokamilika ambalo kwisha kwake kunasemekana kulichukua siku kumi na nne.

Mtume wa Allah (s.a.w.) alifika Quba siku ya Jumatatu. Siku ya Alhamisi Ali naye akawasili. Alikuwa amekwisha rudisha fedha na vito, nyaraka na vitu vingine vya thamani vya watu wa Makka kwao wenyewe. Bwana wake alifurahi sana kumuona yeye, na akamshukuru Allah (s.w.t.) Ambaye alimtoa salama kwenye mji wa Makka.

Muhammad ibn Ishaq:

“Ali alibakia Makka kwa siku tatu, usiku na mchana mpaka akawa amerudisha zile amana ambazo Mtume (s.a.w.) alikuwa amezishikilia. Hili lilipokwisha kutendeka, alijiunga na Mtume, na akakaa naye katika nyumba ya Kulthum.” (The Life of the Messenger of God)

S. Margoliouth:

“Siku ya Jumatatu tarehe 8 ya mwezi wa Rabi ul Awwal wa mwaka wa 1 H.A., kulingana na Septemba 20 ya mwaka 622 A.D, Mtume (s.a.w.) alifika Quba, hivi sasa ikiwa ni mahali pakubwa kwa bustani na miti ya matunda. Ukarimu ulitolewa na mfuasi mmoja mtu mzima, Kulthum ibn Hind, jina la ambaye “mafanikio” ya utumwa wake yalielekea kwa Mtume (s.a.w.) kuwa ya ishara njema (Isabah, iii, 1138). Ulikubalika, ingawa kwa mapokezi ya wageni nyumba ya mfuasi mwingine ilionekana kuwa yenye kufaa zaidi. Hapo Quba, Mtume (s.a.w.) aliamua kubaki mpaka Ali atakapojiunga naye ambapo ilitokea siku ya Alhamisi; pamoja naye alikuwepo Suhaib ibn Sinan, ambaye alilazimishwa kukabidhi akiba zake kwa Maquraishi. Siku ya Ijumaa, Mtume (s.a.w.) alisafiri kutoka Quba kuelekea Yathrib, na anasemekana alifanya ibada ndani ya Wadi Ra’unah. (Muhammad and the Rise of Islam, London, 1931)

Njia ilikuwa imejipanga kundi kubwa lenye furaha la watu wa Yathrib waliokuwa wamevaa mavazi yao ya sikukuu. Wanawake na watoto walikuwa wakiimba nyimbo za makaribisho kutoka kwenye mapaa ya nyumba zao. Yalikuwa ni mandhari ambayo ni vigumu sana kuweza kuwa yamebuniwa katika njozi. Muhammad, Mtume wa Allah (s.w.t.) lazima awe alivutiwa sana na mapokezi ya namna ile.

Kila mkazi (wa Kiarabu) wa Yathrib alikuwa na shauku ya kuwa mwenyeji wa Mtume wa Uislamu ambaye alikuwa anaingia mjini kwake kama mgeni.

Lakini kwa kutokutaka kumkatisha tamaa hata yule mkazi mnyonge zaidi, alishusha hatamu za yule ngamia-jike, na akatangaza kwamba angekaa popote pale atakaposimama. Yule ngamiajike akatembea polepole kupita nyumba nyingi, na kisha akasimama mbele ya nyumba ya Abu Ayyub, baadae akawa ndiye mwenyeji mwenye fahari wa Mtume wa Allah (s.a.w.), Abu Ayyub alikuwa mwenyeji maarufu wa Yathrib, na alitokana na ukoo wa Bani Najjar. Wote Amina, mama yake Mtume, na mama wa babu yake, Abdul Muttalib, walitokana na ukoo huu.