read

Matukio Muhimu Ya Ukhalifa Wa Abu Bakr

Vita vya Kwanza vya wenyewe kwa wenyewe katika Uislamu.

Mara tu baada ya taarifa za kifo cha Muhammad Mustafa zilipoenea nje ya viunga vya Madina, mitume wa uongo walitokea katika sehemu nyingi za nchi. Waliojulikana zaidi miongoni mwao walikuwa ni Musailama huko Yamama; Tulaiha Asadi huko Najd; Laqait bin Malik huko Oman; na Aswad Ansi huko Yemen. Baadhi yao walitaka serikali ya Madina kushirikiana madaraka nao, na baadhi ya wengine walitaka “kujitawala” katika maeneo yao. Abu Bakr alituma vikosi vyake dhidi yao ambavyo viliwazimisha.

Msafara Wa Usamah.

Kama ilivyoelezwa mapema, Mtume (s.a.w.) alikuwa ameandaa, akiwa kwenye kitanda chake cha mauti, jeshi jipya la kushambulia Syria. Alikuwa amemteua Usamah, kijana wa miaka 18, kama kiongozi wa jeshi hili, na aliwaweka maswahaba zake wote chini ya amri yake huyo. Maagizo yake kwa jeshi hili yalikuwa ni waondoke Madina haraka. Lakini maswahaba hawakutaka kuondoka Madina, na hawakuondoka – mpaka Mtume (s.a.w.) akafariki.

Lakini baada ya kifo cha Mtume, wakati Abu Bakr alipohisi usalama kwenye kiti chake cha madaraka, alionyesha uharaka mkubwa sana katika kutuma jeshi la Usamah kwenda Syria. Alisema kwamba kitu kimoja ambacho asingeweza kukifanya ni kutangua amri ya bwana wake aliyefariki.

Abu Bakr alitembea na jeshi la Usamah kwa mwendo kidogo kujipatia “sifa” mwenyewe binafsi. Alipofikiria kwamba amejipatia sifa za kutosha, alimuomba yule Jenerali ruksa ya kurudi mjini. Alimuomba pia Jenerali huyo amruhusu Umar kubaki pamoja naye (Abu Bakr) hapo Madina kwa vile atahitaji ushauri wake katika kuiendesha serikali.

Usamah aliyakubalia maombi yote na Abu Bakr na Umar wakarudi Madina. Kwa urefu, Usamah aliondoka Madina na akatembea kuelekea kaskazini mbele ya jeshi lake bila Abu Bakr na Umar. Lakini jeshi lake lilikuwa limepoteza uchangamfu wake. Yeye sasa labda hakujua la kufanya, na alirudi Madina baada ya kutokuwepo kwa miezi miwili.

Sir John Glubb:

“Mnamo Septemba 632, baada ya miezi miwili ya kutokuwepo, Usamah alirejea Madina na kondoo na ngamia waliotekwa nyara, ingawa ni maelezo machache juu ya oparesheni yake yaliyotufikia. Inaonekana kwamba alishambulia makabila ya Kibedui badala ya vikosi vya Byzantine.”
(The Great Arab Conquests, 1963)

Usamah bin Zayd bin Haritha, kipenzi cha Muhammad (s.a.w.), na Jenerali wa msafara wa kwenda Syria, anaonekana kupotea mara moja kwenye historia; ni kidogo sana kinachosikika kuhusu yeye baada ya kurudi kutoka kwenye msafara wake. Anaweza kuwa ameshiriki katika kampeni za Abu Bakr na Umar katika viwango vya chini.

Malik Ibn Nuweira Na Mauwaji Ya Kabila Lake.

Ibn Khalikan, yule mwanahistoria, anasema kwamba Malik ibn Nuweira alikuwa ni mtu mwenye hadhi kubwa katika Arabia. Alikuwa ni mpanda farasi maarufu, shujaa wa ukoo, mshairi maarufu, na rafiki yake Muhammad Mustafa (s.a.w.).

Ibn Hajar Asqalani anasema katika kitabu chake cha wasifa wa maswahaba kwamba wakati Malik aliposilimu, Mtume (s.a.w.) alimteua kama Mkusanya Mapato wa kabila lake la Banu Yirbo. Alikusanya Zaka kutoka kwenye kabila lake, na akazipeleka Madina.

Lakini aliposikia habari za kifo cha Mtume (s.a.w.), aliacha kukusanya Zaka hizo, na akawaambia watu wake kwamba kabla ya kupeleka makusanyo yoyote Madina, alitaka kujua hiyo serikali mpya katika mji huo imekaaje.
Malik hakulipa Zaka kwa serikali hiyo mpya huko Madina, na Abu Bakr akatuma jeshi la kuadhibu chini ya uongozi wa Khalid bin al-Walid kuonyesha madaraka yake, na kukusanya ile Zaka iliyoshindikana kulipwa.

Khalid alikuwa na mazungumzo mafupi na Malik, na huyu Malik alijua kwamba atauawa. Baadhi ya wanahistoria wanasema kwamba Khalid alimpenda mke wa Malik, na akaamuru kuuawa kwake. Malik alimgeukia mke wake, na akasema: “Wewe ndiye utakayesababisha kifo juu yangu mimi.” Lakini Khalid alilikataa hili na kusema: “Hapana, umekuwa murtad, na urtad wako ndio unaosababisha kifo chako.” Ingawa Malik alilalami- ka kwamba alikuwa ni Mwislam, Khalid hakumsikiliza, na Malik akauawa.

Abu Qatada Ansari alikuwa ni sahaba wa Mtume (s.a.w.). Alikuja na Khalid kutoka Madina. Alishitushwa sana na kuuawa kwa Malik na Khalid kiasi kwamba alirudi mara moja Madina, na akamwambia Abu Bakr kwamba hatatumika chini ya kamanda ambaye ameua mwislamu.

Baada ya kumuua Malik ibn Nuwaira, Khalid “akamuoa” mjane wake. Huko Madina, Umar alikuwa ameshituka sana kiasi kwamba alidai, kutoka kwa Abu Bakr, ufukuzwaji wa mara moja wa Khalid. Alisema kwamba Khalid alipaswa kushitakiwa kwa makosa yote mawili, ya mauwaji na zinaa. Kwa mujibu wa sheria za Kiislam, Khalid alikuwa apigwe mawe mpaka afe. Lakini Abu Bakr alimtetea Khalid, na akasema kwamba alifanya tu “kosa la maamuzi.”

Watu wa kabila la Bani Yirbu walikuwa wameishikilia Zaka lakini mbali na hilo walikuwa ni Waislamu katika kila hali ya neno hilo.

Abu Qatada mwenyewe alishuhudia kwamba aliisikia Adhana katika kijiji cha Malik, na aliwaona jamaa wa kabila lake wakiswali Sala za jamaa. Hata hivyo, Khalid aliamuru vikosi vyake kuwaangamiza.

Tabari anaandika katika Taarikh yake kwamba pale Khalid na vikosi vyake walipoingia kwenye nchi ya Bani Yirbu, waliwaambia watu wa kabila hilo: “Sisi ni Waislamu.” Wao wakasema: “Na sisi pia ni Waislamu.” Watu wa Khalid wakauliza: “Kama ninyi ni Waislamu, kwa nini mmebeba silaha? Hakuna vita kati yetu. Wekeni silaha zenu chini ili sisi wote tuweze kuswali.”

Watu wa kabila hili wakaweka chini silaha zao, lakini mara tu walipokwisha kufanya hivyo, wapiganaji wa Khalid wakawakamata, wakawafunga, na wakawaacha watetemeke kwenye usiku ule wa baridi. Asubuhi iliyofuata, wote waliuawa. Kisha Khalid akazipora nyumba zao, akawateka wanawake zao na watoto, na wakawapeleka Madina kama wafungwa wa kivita.

Sir John Glubb

“Abu Bakr alimtuma Khalid bin Walid kwenda Najid pamoja na watu 4000. Koo nyingi za Bani Tamim, ziliharakisha kumtembelea Khalid lakini tawi la Bani Yirbu la kabila hilo, chini ya mkuu wao, Malik ibn Nuwaira, lilibaki nyuma. Malik alikuwa ni chifu mwenye heshima maalum, mpiganaji, aliyejulikana kwa ukarimu wake na mshairi maarufu. Ujasiri, ukarimu na ushairi zilikuwa ndio sifa tatu zilizopendwa sana miongoni mwa Waarabu. Kwa kutokupenda kujidhalilisha mwenyewe kwa kumnyenyekea Khalid, aliwaamuru wafuasi wake kutawanyika na yeye mwenyewe inavyoonekana akaenda upande wa pili wa jangwa peke yake pamoja na familia yake.

Abu Bakr alikuwa ametoa maagizo kwamba mtihani utakaotumika kwa waasi wanaoshukiwa ulikuwa kwamba watakiwe kurudia utaratibu wa shahada ya Kiislam na kwamba waitikie kwenye wito wa Swala. Khalid, hata hivyo, alipendelea njia za shari zaidi na akatuma vikundi vya wapanda farasi kuwazunguka wale watoro na kupora mali zao.

Kikundi kimoja kama hicho kilimkamata Malik ibn Nuwaira na familia yake na wakawaleta kwa Khalid, ingawa walitamka kwa dhati kwamba walikuwa ni Waislamu. Watu wa Madina ambao walikuwa pamoja na jeshi hilo walipinga kwa nguvu sana dhidi ya ukatili wa Khalid, lakini bila mafanikio.

Wafungwa hao waliwekwa chini ya ulinzi lakini, wakati wa usiku, Malik ibn Nuwaira na wafuasi wake waliuawa kikatili. Ndani ya masaa 24 Khalid alikuwa amemuoa mjane wa mwathirika wake.

Malik ibn Nuwaira aliuawa wakati akishuhudia kwamba ni mu’min. Kwa hakika ndoa ya Khalid na mrembo Laila ilizusha wasiwasi kwamba Malik aliuawa pamoja na kusudi la kumfanya apatikane kwa mtekaji.

Wale watu wa Madina, ambao walikuwa tayari wamepinga vitendo vya kikatili vya Khalid, walikuja juu kwa hasira kwa kifo cha Malik. Mtu mmoja, Abu Qatada, rafiki wa zamani na sahaba wa Mtume, aliharakishia Madina kulalamika kwa Abu Bakr, ambaye alimwita Khalid kujibu shutuma hizo. Umar ibn al-Khattab alimshinikiza khalifa kumnyang’anya Khalid ukamanda wake. Khalid akirejea Madina, alidai kwamba hakuamuru kuuawa kwa Malik, bali kwamba maagizo yake kwa walinzi wake yalikuwa hayakueleweka. Mweye hekima Abu Bakr, chochote ambacho angekifikiria juu ya maadili ya wakili wake, alikuwa anatambua umahiri wake. ‘sitaurudisha kwenye ala upanga ambao Allah ameuchomoa kwa ajili ya utumishi Wake,’ alitamka kwa mshangao. Visingizio vya Khalid vikakubalika.”
(The Great Arab Conquests, 1963, uk.112)

Wale jamaa wa kikabila wa Banu Yirbu walitamka kwamba Allah ni Mmoja, na Muhammad ni Mjumbe Wake, na waliswali Swala zao kama kawaida. Waliukubali pia ule utaratibu wa kulipa Zaka, na walikuwa wakiilipa kwa Mtume (s.a.w.).

Lakini wakasi- mamisha malipo ya Zaka kwa serikali ya Abu Bakr ndipo akasema kwamba wamekuwa murtadi, na akatangaza vita juu yao.

Wakiwa wanafuata masharti rasmi, wanahistoria wa Sunni wamewaweka kundi moja wale jamaa wote wa kikabila ambao walizuia kodi zao kwa serikali ya Saqifah kama “murtad.” Hivi walikuwa ni murtad kweli?

Mafaqihi wa Kiislam wameifafanua “murtadi” kama ukanusho wa Uislamu. Lakini kushindwa kuswali au kufunga wakati wa Ramadhani au kwenda kuhiji Makka au kutoa Zaka, sio ukanusho wa Uislamu.

Mtu ambaye hatekelezi wajibu wa lazima uliowekwa juu yake na Uislamu lakini anatamka kwamba ni mwislamu, hawezi kuitwa murtad. Kama mtu angekuwa awe murtadi kwa kukosa Swala au funga au kutoa Zaka, basi Waislamu wengi wa kila kizazi wangekuwa waitwe murtadi. Lakini hawakuitwa hivyo.

Hakuna Aya ndani ya Qur’an inayoitaka serikali ya Kiislamu kuwaua wale Waislamu ambao hawatoi Zaka. Hakuna Hadith ya Mtume wa Uislamu (s.a.w.) inayoeleza kwamba adhabu ya kukataa kutoa Zaka ni kifo.

Mbali na kutowaua Waislamu kwa kushindwa kwao kutoa Zaka, Mtume (s.a.w.) kwa kweli alitoa msamaha wa kulipa kodi (Zakat), angalau katika kadhia moja. Hiki ndicho mwanahistoria wa Sunni wa wakati huu, Dr. Muhammad Hamidullah, anachoandika kati- ka kitabu chake, Introduction to Islam, (Kuwait, 1977):

“... ujumbe kutoka Taif ulikuja Madina ukiahidi kujisalimisha (kusilimu). Lakini uliomba kusamehewa kwenye Swala, kodi na utumishi wa kijeshi… Mtume aliridhia kuruhusu msamaha kwenye malipo ya kodi na utoaji wa utumishi wa kijeshi… kiten- do hiki cha Mtume kinaonyesha kwamba tahafifu inaweza kutolewa kwa wafuasi wapya…”

Hapa ulikuwepo mfano wa jambo lililowahi kutokea. Mtume (s.a.w.) alitoa msamaha kwa wakazi wa Taif kwenye malipo ya kodi. Lakini Abu Bakr hakufuata ule mfano wa kiutume uliotangulia; aliamua kufanya mfano wake mwenyewe; watu wote wa kabila la Malik ibn Nuwaira walikuwa wauawe, na wanawake na watoto kufanywa wafungwa wa kivita.

Mbali na Qur’an na Hadithi, Waislamu wa Sunni pia wanayakubali mamlaka ya “makubaliano” (ijma). Kwa kweli, makubaliano katika fiqihi ya Sunni ni kanuni muhimu sana kiasi kwamba yanakadiriwa kama ni kitu takriban kisicho na makosa. Kulikuwa na makubaliano ya Waislamu wote pamoja na Umar mwenyewe katika kupinga uamuzi wa Abu Bakr wa kupigana dhidi ya wale Waislamu ambao hawakulipa kodi zao.

Lakini Abu Bakr aliyapuuza makubaliano yao na akasema kwamba kama makabila yangezuia hata kile kipande cha kamba ambacho walifungia ndama, katika sehemu ya Zaka, angepigana dhidi yao, na angekichukua kutoka kwao. Maagizo yake kwa vikosi vyake yalikuwa dhahiri: Waangamizeni wale watu wote ambao hawalipi Zaka.

Vikosi vya Abu Bakr vilitekeleza maagizo yake. Waliwafanyia wale Waislamu wa makabila vitisho visivyosemeka, na kufanya vitendo vya ukatili mkubwa juu yao kwa kuzuia Zaka.

Hivyo vinavyoitwa “vita vya murtad” vilivyopiganwa katika ukhalifa wa Abu Bakr, vilikuwa kwa kweli ni vita vya wenyewe kwa wenyewe – vya kwanza katika Uislamu. Vita hivi vilipiganwa na Waislamu dhidi ya Waislamu – kisa cha vita hivyo kwa upande wao kikiwa ni kukataa kwa baadhi ya makabila kulipa Zaka kwenye serikali ya Abu Bakr.

Abu Bakr alianza utawala wake na vita ya wenyewe kwa wenyewe lakini akaiita ni vita ya murtad. Pale vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipopewa jina vita vya murtad, viligeuka kuwa vya “kuheshimika” na “vitukufu,” na ikawa ni wajibu kwa Waislamu wote kushiriki ndani yake.

Katika shauku yao ya kumtetea Khalid, Waislamu wengi kwa utulivu kabisa wanadai kwamba baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.), Malik na kabila lake waliritad, na adhabu iliyoagizwa katika Uislamu kwa ajili ya murtad ni kifo. Kama sababu yao ya kumtetea Khalid ni kwamba alikuwa sahaba wa Mtume (s.a.w.), basi Malik alikuwa pia ni sahaba wa Mtume (s.a.w.). Usahaba wa Mtume, kwa hiyo, hauwezi kuwa ndio sababu yao ya kumtetea Khalid. Lazima iwepo sababu nyingine au ziwepo sababu zingine.

Kwa kweli walimtetea Khalid kwa sababu alikuwa ni chombo cha sera ya serikali ya Saqifah. Malik aligongana na serikali ya Saqifah alipozuia kuipa kodi. Mbali na hili, yeye na jamaa wa kabila lake walikuwa ni Waislamu wa vitendo. Lakini kwa sababu ya “kuvunja miiko yake” kwao, walilipa malipo ya adhabu yanayotisha – waliangamizwa!

Mbele ya kuzongwa na ushahidi dhidi ya Khalid, Abu Bakr alilazimika kumkosoa yeye lakini kama bwana mwenye shukrani, alimtetea na akaupachika uhalifu wake kwenye “kosa la maamuzi.” Kama zawadi kwa kitendo chake cha ujasiri wake wa harakaharaka, alimpachika jina la “upanga wa Allah,” na mwaka mmoja baadae, wakati peninsula yote ilipokuwa chini ya mamlaka yake, yeye (Abu Bakr) alimteua Khalid kama kamanda mkuu wa majeshi yake huko Syria.

Hatia kama uzinzi na mauaji ya halaiki ya Waislamu hazikuweza kusamehewa tu kama “makosa ya maamuzi” madogo tu bali zingeweza kwa kweli kuzawadiwa kama watendaji wake wangetoa uungaji mkono wao wa kupita kiasi kwa serikali ya Saqifah.

Hilo hitimisho la “kosa la maamuzi” umeonekana kuwa ni ugunduzi muafaka kwa Waislamu wengi.

Uliwawezesha kuidhinisha kila jinai, na kumlinda kila mhalifu. Katika miaka iliyofuatia, walificha baadhi ya vitendo vya kutisha mno na matendo mabaya kupi- ta kiasi, katika historia ya Kiislam kwa maelezo kwamba yalikuwa ni “makosa ya utendaji” tu.

Hapa mtu anaweza kuona jambo la kuvutia katika matumizi ya unafiki huu ujulikanao sana. Katika ukhalifa wa Abu Bakr, wale Waislamu wote waliozuia Zaka, walishutumiwa naye na wanahistoria wa Sunni kama “murtadi,” na waliuawa. Lakini (wanahistoria hao hao ) katika ukhalifa wa Ali ibn Abi Talib, wale watu wote waliofanya uasi dhidi ya mamlaka yaliyowekwa kihalali, na ambao walisababisha vifo vya makumi ya maelfu ya Waislamu, walitolewa kwenye lawama na kuondolewa tuhuma kwa sababu walifanya “kosa la maamuzi” tu, na “walitubia.”

Hili “kosa la utendaji” lilikuwa ni blanketi pana ajabu!

Kama ilivyoelezwa hapo juu, Abu Bakr aliuanzisha ukhalifa wake kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Lakini aliweza kuigeuza kama vita vya murtad, na kwa kudhamiria, alifanikiwa kuugandamiza upinzani wote juu yake mwenyewe.

Ushindi Mwingine Wa Abu Bakr

Mtume wa Allah (s.a.w.w) alimteua mtu mmoja, Ziad bin Labiid kama gavana wa Hadhramaut na Kinda. Wakati alipokufa, mtu mmoja, Ash’ath bin Qays aliamsha maasi dhidi ya serikali ya Madina ambayo sasa ilikuwa ikiongozwa na Abu Bakr. Abu Bakr alimtuma jenerali wake, Ikrima bin Jahl, kurudisha mamlaka yake huko Kusini mwa Arabia.
Ikrima alimshinda Ash’ath, akamteka na akampeleka kama mfungwa huko Madina. Ash’ath aliomba msamaha. Abu Bakr sio tu alimsamehe yeye bali pia alimuoza dada yake kwake.

Huko Bahrain, makabila ya Banu Bakr na Banu Abdul-Qays yalikuwa yamekataa kulipa kodi. Hatua za kuwaadhibu zilichukuliwa dhidi yao, na walilazimishwa kulipa kodi zao.

Vita hivi vinajulikana kwa jina la kijenasi (la kubatiza), la vita vya “Ridda” (yaani, vita dhidi ya murtad ili kuficha ukweli wenyewe wa mambo).

Abu Bakr alimaliza mwaka mzima kupigana dhidi ya Ahl-er-Ridda - watu walioritadi na mitume wa uongo. Mwishoni mwa mwaka wote hao walikuwa wametiishwa, na mamlaka yake yakaimarika katika nchi hiyo. Hata hivyo, katika mwisho wenye mafanikio wa vita hivi, hakutaka vikosi vyake kukaa bure; alivituma kwenda kuvamia nchi jirani za Syria na Uajemi.

John Alden Williams

“Wakati Abu Bakr alipomalizana na suala la wale walioritadi, aliona vema kuvituma vikosi vyake dhidi ya Syria. Kwa kulitekeleza hili, aliwaandikia watu wa Makka, al- Taif, al-Yaman, na Waarabu wote huko Najdi na Hijazi kuwaita kwenye vita vya jiha- di na kuamsha tamaa zao juu yake na katika ngawira inayoweza kupatikana kutoka kwa Wagiriki (Byzantines). Kwa sababu hiyo, watu ukichanganya na wale ambao walisukumwa na uroho na vile vile wale waliokuwa na matumaini ya ujira wa mbingnii, walikwenda kwa wingi huko Madina. Imesimuliwa kutoka kwa al-Waqidi kwamba Abu Bakr alimpeleka Amr ibn al-Aas Palestina; Shurahbil ibn Hasana na Yazid ibn Abu Sufyan huko Damascus.”
(Themes of Islamic Civilization, 1971)

Mapambano dhidi ya Syria na Uajemi yalianzishwa na Abu Bakr lakini alikufa kabla hajaweza kuyamalizia. Yalifikishwa kwenye mwisho wenye mafanikio na mrithi wake, Umar ibn al-Khattab.

Kukamatwa Kwa Shamba La Fadak Na Abu Bakr

Fadak lilikuwa ni moja ya mashamba aliyoyapata Mtume wa Uislamu baada ya ushindi wa Khaybar kwenye mwaka wa 7 Hijiria. Lakini kwa vile vikosi vyake havikulazimika kulipigania, na lilitolewa kwake kwa hiari, lilichukuliwa kwamba ni mali ya Allah (s.w.t.) na Mtume Wake (s.a.w.).

Kama ilivyoonyeshwa kabla, Mtume wa Allah (s.w.t.) aliifanya Fadak kuwa zawadi kwa binti yake, kwa upande mmoja ikiwa kama fidia kwa mihanga mingi mama yake, Khadija, aliyoitoa kwa ajili ya Uislamu.

Abu Bakr alipoikamata serikali ya Waislamu, moja ya vitendo vyake ilikuwa ni kuchukua umiliki wa nguvu wa Fadak. Aliwafukuza wapangaji wa Fatima Zahra kutoka shambani kwake, na pia alimnyang’anya mali ambayo baba yake alimpa hapo Madina penyewe. Wakati Fatima alipolalamika dhidi ya kukamatwa huku, Abu Bakr alimjibu kwa “Hadith” ya baba yake. Alisema kwamba alikuwa amemsikia Mtume wa Allah akisema kwamba Mitume hawana warithi wowote, na utajiri kama huo, mali au vitu wanavyokuwa navyo wakati wa uhai wao, baada ya kufa kwao vinakuwa sio mali ya watoto wao, bali ya umma.

Fatima akasema kwamba Fadak sio mirathi ya baba yake; ilikuwa ni zawadi. Alinena kwa dhati kwamba Fadak ilikuwa ni mali binafsi ya Mtume wa Allah, na ilikuwa kama mali binafsi ambayo alimpa yeye Fatima.

Abu Bakr akauliza kama kulikuwa na mashahidi wowote.

Hii ilikuwa ni ajabu kweli. Ni miaka minne tu imepita baada ya ushindi wa Khaybar. Abu Bakr sio tu alikuwepo wakati wa kuizingira bali pia alifanya jaribio lisilofanikiwa la kuiteka hiyo ngome. Alikuwa ameona kwa macho yake kile ambacho Mtume (s.a.w.) alikifanya na Fadak. Sasa miaka minne baadae, alikuwa akijifanya kama hana anachokijua. Kulingana na Bukhari, yule mkusanyaji wa Hadith, mahojiano yafuatayo yalitokea kati ya mdai na mtetezi.

Fatima: Ewe Abu Bakr, kama baba yako atafariki, nani atakayekuwa mrithi wake?
Abu Bakr: Ni mimi, ambaye ni mwanae.
Fatima: Ni nani mrithi wa baba yangu mimi?
Abu Bakr: Ni wewe, binti yake.
Fatima: Kama mimi ndiye mrithi wake, basi kwa nini uliikamata Fadak?
Abu Bakr: Nimemsikia Mtume wa Allah (s.w.t.) akisema: “Sisi ni kundi la Mitume, na hatuna warithi wowote wa kurithi mali zetu. Mali yoyote tuliyonayo, inakuwa ni mali ya umma pale tunapofariki.”
Fatima: Lakini baba yangu aliiweka Fadak juu yangu mimi kama zawadi wakati wa uhai wake, na ilikuwa mikononi mwangu miaka yote hii.
Abu Bakr: Unao mashahidi wowote?
Fatima: Ali na Ummu Ayman ndio mashahidi wangu.
Abu Bakr: Ushahidi wa mwanaume mmoja na mwanamke mmoja hautoshi. Lazima wawepo ama wanaume wawili au mwanaume mmoja na wanawake wawili. Lakini kwa vile sio hivyo, kesi hii imefutwa.

Masikio ambayo Fatima alikuwa akiongea nayo, hayakuwa tayari kusikiliza hoja yoyote au sababu. Mashahidi hao wasingeleta tofauti yoyote kwa wale ambao walikuwa wameamua kutoshawishika.

Kundi linaloshitakiwa lilikuwa na hoja moja yenye kuthubutu kabisa kwa upande wao! Ilikuwa ni hoja ambayo ilikuwa na nguvu ya kuzima hoja nyingine yoyote, na iliweza.

Kutilia nguvu utekelezaji wake katika kukamata lile shamba la Fadak, Abu Bakr alinukuu “Hadith” ya Mtume wa Allah (s.w.t.) Lakini ni ajabu kwamba yeye peke yake aliisikia “Hadith” hii. Na ni ajabu kama hiyo kwamba Muhammad hakuwaambia watu wa familia yake kwamba hawatarithi mali yake baada ya kifo chake kwa sababu alikuwa Mtume wa Allah, bali alizunguka akinong’oneza “Hadith” kwenye masikio ya watu wa nje.

Abu Bakr ndiye mtu pekee katika umma wa Muhammad (s.a.w.) aliyeisimulia “Hadith” hii na ambaye aliyeiweka kinyume na mamlaka ya Qur’an Tukufu. Fatwa ya Qur’an ni kama ifuatavyo:

لِلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ وَلِلنِّسَاءِ نَصِيبٌ مِمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ مِمَّا قَلَّ مِنْهُ أَوْ كَثُرَ ۚ نَصِيبًا مَفْرُوضًا {7}

“Wanaume wanayo sehemu katika wanayoyaacha wazazi na jamaa wa karibu, na wanawake wanayo sehemu katika waliyoyaacha wazazi na jamaa wa karibu; ikiwa mali hiyo ni kidogo au nyingi – hizi ni sehemu zilizofaridhiwa. (Sura ya 4; Aya ya 7)

Na kila mmoja tumemwekea warithi katika waliyoyaacha wazazi wawili na jamaa wa karibu. Na kwa wale pia ambao mikono yenu ya kulia imewaahidi, wapeni fungu lao.

إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدًا {33}

Hakika Allah ni Shahidi wa kila kitu.(Sura ya 4; Aya ya 33)

Kwa mujibu wa Aya hizi, Allah (s.w.t.) amewapa watoto haki ya kurithi mali iliyoachwa na wazazi wao. Kuna Aya nyingine ambayo inayonyima haki hiyo kwa watoto wa mitume wa Allah (s.w.t.) hususan, kwa binti wa Muhammad (s.a.w.)?

Hata kama ikichukuliwa kwamba “Hadith” hiyo iliyonukuliwa na Abu Bakr sio ya uongo, na warithi wa Mitume hawawezi kurithi mali zao, basi “sheria” hii ilipaswa kutumika kwa watoto wa Mitume wote, na sio tu kwa binti ya Muhammad. Lakini kwa mujibu wa Qur’an, Mitume waliopita walikuwa na warithi wao, na warithi wale walirithi mali iliyoachwa na Mitume wao – baba zao.

وَوَرِثَ سُلَيْمَانُ دَاوُودَ ۖ{16}

“Na Suleiman alikuwa mrithi wa Daudi.” (Sura ya 27; Aya ya 16)

Maelezo ya Mfasiri kwenye Aya hii:
Hoja hapa ni kwamba Sulaiman sio tu kwamba alirithi ufalme wa baba yake bali na umaizi wake wa kiroho na cheo cha utume, ambacho sio lazima kiende kutoka kwa baba kwenda kwa mtoto. (A . Yusuf Ali)

Kwa kiasi chochote, haikuwa ni lazima kwa Fatumah Zahra kuleta mashahidi. Yeye tayari alikuwa akiimiliki Fadak. Umiliki wake wa Fadak ulitegemea kwenye agizo lenye uzito au idhini yenye muwazo yakinifu ya Muhammad Mustafa (s.a.w.) kama Mtume wa Allah (s.w.t.) na mkuu wa Waislamu wote, na haiwezi kupingwa kisheria.

Mzigo wa uthibitisho kwamba umiliki wa Fatima wa shamba hilo sio wa haki, ulikuwa juu ya Abu Bakr.

Jambo la muhimu ni kwamba mahakama itengwe na wenye mamlaka, na wenye mamlaka wasije wakaiingilia mahakama. Lakini katika suala la Fadak. Abu Bakr ambaye alikuwa ndiye anayelalamikiwa, alikuwa yeye mwenyewe ndiye hakimu, na mzee wa baraza la mahakama, na hukumu yake lazima ilikwenda dhidi ya mlalamikaji kama ambavyo ingefanya katika mahakama isiyorasmi au chemba ya kidhalimu.

Kukamatwa kwa Fadak kilikuwa ni kitendo cha udhalimu mkubwa mno. Si muda mrefu baada ya Fadak, Abu Bakr alikabiliwa na matatizo mengi mapya na magumu. Ili kuyatatua hayo, aliweka vigezo viwili. Kimoja kilikuwa ni uteuzi wa maswahaba kama mahakimu. Kwa nafasi hizi, alichagua watu waliokuwa wakitambulika kwa ujuzi wao na uamuzi mzuri.

Kama angekuwa muadilifu, alipaswa kulipeleka suala la Fadak kwa mmoja wa mahakimu wake kwa ajili ya hukumu badala ya kuchukuwa hatua za upande mmoja katika kulikamata.

Kigezo cha pili kilikuwa ni kushauriana na maswahaba. Kama Abu Bakr alikuwa na tatizo gumu, alikaa Msikitini, akawaita maswahaba wakubwa, na akaliweka tatizo hilo mbele yao. Baada ya kujadiliana, walilifumbua tatizo hilo. Kama Abu Bakr angekuwa muadilifu, angepaswa kuwaomba wao watoe uamuzi wao wenye haki juu ya Fadak. Lakini hakufanya hivyo.

Hii “Hadith” aliyoinukuu Abu Bakr kama “sababu” yake ya kuchukua umiliki wa Fadak, ilikuwa kwa kweli ni muundo wa kisheria wenye kusudi maalum ulioundwa kukidhi hali ambayo ilitishia kuhatarisha nafasi yake. Ulikuwa ni “utaratibu” uliobuniwa kwa mara ya kwanza na ya mwisho. Mara mgogoro huo ulipopita, utaratibu huo ulizikwa, usije kufukuliwa tena kamwe.

Katika makabiliano yake ya kisheria na serikali ya Saqifah, juu ya kukamatwa kwa Fadak, Fatima Zahra hakutegemea haki hata kidogo. Kifo cha baba yake, bila shaka, kilikuwa ndio mshituko mkubwa na huzuni kuu juu yake yeye.

Lakini baadhi ya maswahaba zake Mtume (s.a.w.) hawakufikiri kwamba huzuni yake ilikuwa kubwa vya kutosha, na walitafuta kufanya wa kwao “mchango” juu yake. Ilikuwa ni pale alipokuwa katikati tu ya maombolezo juu ya baba yake ambapo Abu Bakr alipomfukuza meneja wake wa shamba kutoka Fadak, na mawakala wake wakachukua umiliki wake.

Muda mrefu baada ya mlalamikaji na watetezi katika suala la shamba la Fadak wakiwa wameiaga dunia, Umar ibn Abdul Aziz, khalifa wa Bani Umayya, akalirudisha kwa warithi wa Fatima Zahra. Alikuwa mwadilifu na mcha-mungu, na alitambua kwamba ule ukamatwaji wa Fadak ulikuwa ni kitendo cha kikorofi na unyang’anyi wa dhahiri.

Kitendo cha serikali ya Saqifah katika kuikamata Fadak hakikuhusika hata kidogo na sheria au tafsiri yake.Viongozi wake walishawishiwa na lengo moja, yaani, kuwakosesha watoto wa Muhammad Mustafa (s.a.w.) uwezo wao wa maisha. Sadaka ilikuwa ni haramu juu yao, na hawawezi kuipokea. Rasilimali iliyokuwa ikiwapatia, waliinyang’anywa, na haki yao ya urithi ilikuwa haitambuliwi.