read

“Mgawanyo Wa Lazima” Wa Uislamu

Miaka ya awali ya Uislamu ilikuwa ni wakati wa majaribu magumu na mitihani mizito kwa Waumini. Kila siku iliwaletea makabilano mapya na, na changamoto mpya kutoka kwa washirikina, na pambano lisilokwisha, likiwa kwenye mazingira ya kikatili tu.

Kazi yote ya Muhammad kama Mtume wa Mwisho wa Allah kwenye dunia hii, ambayo ilidumu kwa miaka 23 ya mwisho ya maisha yake, ilivunikwa na pambano hili.

Lilikuwa ni pambano kubwa sana. Ni wanaume na wanawake wa imani isiyoshindika, ujasiri thabiti, na nguvu zisizochoka tu ambao wangeweza kuishi katika mfadhaiko na wasiwasi wake. Ili kukabiana nalo, kwa hiyo, Uislamu ulitoa “majitu maarufu” yake wenyewe.

Hayo “majitu maarufu” ya Uislamu yalikuwa watu binafsi wawili na vikundi viwili. Watu binafsi hao wawili walikuwa ni Abu Talib ibn Abdul-Muttalib na mwanawe Ali; na vikundi viwili hivyo vilikuwa ni Banu Hashim huko Makka, na Ansar huko Madina.

“Kituo cha uendeshaji” cha Abu Talib na Banu Hashim kilikuwa Makka ambapo “jukwaa” la migogoro ambamo Ali na Ansari walivutwa lilikuwa Madina. Kwa pamoja, wao waliunda kile kinachoweza kuitwa “Mgawanyo wa Lazima” wa Uislamu. Kila kimojawapo cha vijenzi hivyo vinne vya “mgawanyo” huu kilikuwa na lazima kwa uhai wa Uislamu, na kila kimojawapo kilijaaliwa kutimiza wajibu maalum katika historia yake.

Kijenzi cha kwanza cha mgawanyo huu kilikuwa ni Abu Talib. Allah swt. alimpa kazi ya kumlinda Muhammad na kuutetea Uislamu. Nyumba yake huko Makka ilikuwa ndio chim- buko la Uislamu. Muhammad, Mtume wa wakati ujao, alizaliwa katika nyumba yake. Baadae, nyumba hiyo hiyo ikawa, kwanza “chuo” cha Muhammad, na kisha “ngome” ya Uislamu.

Abu Talib alikuwa mtu wa heshima kubwa, werevu na mamlaka lakini matatizo aliyokumbana nayo, kama mtetezi wa Uislamu, yalikuwa makubwa kiasi kwamba hakuweza kuyashinda yote yeye peke yake. Ilimbidi, kwa hiyo, apate msaada. Lakini ni nani hapo Makka ambaye angeweza kumsaidia yeye dhidi ya Makuraish isipokuwa watu wa ukoo wake mwenyewe – Banu Hashim? Aliwakusanya hao, na ilikuwa ni msaada wao wa pamo- ja uliohakikisha uwepo na uhai wa Uislamu hapo Makka.

Ukoo wa Banu Hashim ulikuwa na msimamo na mtazamo mmoja katika kumuunga mkono Muhammad na Uislamu. Watu wake walithubutu miaka mitatu ya hatari na ya kunyimwa kama wakimbizi katika bonde la mlima lakini hawakumtelekeza Muhammad. Hao washirikina walikatishwa tamaa na kufadhaishwa na umoja na mkabala wa kijasiri ulioonyeshwa na Banu Hashim kwao wao, na kwa dunia yote.

Siku alipokufa Abu Talib, ilielekea kwa Muhammad kwamba ile ngao yenye nguvu ya Uislamu ilikuwa imebomoka. Kifo cha Abu Talib hakikukatisha hata hivyo, ule utaratibu wa kumlinda Muhammad na kuutetea Uislamu ambao alikuwa ameuanzisha; uliendelezwa na mwanawe Ali, ambaye alijaaliwa kujipatia sifa zaidi hata kuliko baba yake maarufu katika utumishi kwa Uislamu.

Kipaji chake kilijitokeza hapo Madina. Aliuvunja kabisa mtazamo wa kipagani wa Arabia. Lakini kama vile tu msaada wa Banu Hashim ulivy- oonekana kuwa wa lazima kwa ajili ya Uislamu hapo Makka, msaada wa Ansari ulionekana kuwa wa lazima kwa ajili hiyo hapo Madina. Maansari walijikusanya nyuma ya Muhammad hapo Madina kama vile Banu Hashim walivyokuwa wamejikusanya nyuma yake huko Makka.
Abu Talib na Ali, na wanaume na wanawake wa Banu Hashim na Ansari walikuwa wa kipekee kwa viwango vya wakati wao na vile vile kwa wakati wetu wenyewe. Wao walikabiliana na kila changamoto kwa Uislamu, na waliushinda kila mgogoro katika muda wake.

Wao peke yao walilinda na kutetea kanuni, heshima na urithi wa Uislamu. Majina ya mashujaa wote hawa hayajulikani kwenye historia lakini kila mmoja wao alikuwa na lazima kwa Uislamu. Kila mmoja wao, mwanaume au mwanamke aliunda ule “mgawanyo wa lazima” wa Uislamu. Bali ya mchango katika utumishi wa kila mmoja wao, huo “mgawanyo” wa Uislamu usingeweza “kutengemaa” kabisa.

Walikuwepo Waislamu wengine pia – masahaba wa Mtume – ambao walichukua majukumu wao wenyewe kwa viwango tofauti vya umuhimu katika historia ya Uislamu.

Wengine wao walifanya majukumu makubwa na wengine madogo lakini hakuna hata mmoja kati yao aliyefanya majukumu ambayo yalikuwa makubwa vya kutosha kuyafanya yawe ya lazima. Wengi wao walijipatia sifa wenyewe baada ya kifo cha Mtume lakini kama wangekufa wakati wa uhai wake, wasingesikika kabisa. Katika wakati wa uhai wake, walikuwa ni watu wanaofuatia na wa pembeni ambao waliupata ukweli binafsi na kujik- weza baada tu ya kifo cha bwana wao.

John Kenneth Galbraith, mchumi na mwanadiplomasia wa Kimarekani, wakati mmoja aliutenga ule ugonjwa wa kiuandishi wa habari aliouita “uundaji.” Kiini cha uundaji huo, yeye alisema, ni kumbadili mtu wa sifa za kawaida na kuwa mfano wa kihistoria usiosahaulika milele. Hili linaoneka kufanyika kuwahusu wengi wa Muhajirin. Sifa zisizo na kifani zimetolewa kwa wingi sana juu yao, na katika masuala mengi, sifa hiyo imehusish- wa kwa Mtume mwenyewe, na kwa hiyo ikapewa “hadhi” ya Hadith (sunnah ya Mtume). Kwa kweli, nyingi ya “Hadith” hizi au sunnah zisizo na idadi si chochote zaidi ya upigaji chuku wa ajabu wa mawazo bunifu yenye hamasa ya mpenzi au wapenzi fulani wa masahaba.

Mifano ya “Hadith” zinazowatukuza baadhi ya masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) ni mingi lakini hapa inawezekana kunukuu mmoja tu kati ya hiyo. Moja ya “Hadith” maarufu sana ni ile inayoitwa Hadith Ashara Mubaashara “Hadith ya masahaba kumi waliobashiriwa pepo.” Mtukufu Mtume anadaiwa kutoa uhakikisho wake binafsi kwa masahaba wake wakuu kumi kwamba wote hao wataingia peponi. Hao walikuwa ni:

1. Abu Bakr
2. Umar
3. Uthman
4. Ali
5. Talha
6. Zubeir
7. Abdur Rahman bin Auf
8. Saad bin Abi Waqqas
9. Abu Ubaidah Aamir bin al-Jarrah
10. Said bin Zayd

Usahihi wa Hadith hii unatia mashaka kwa sababu zifuatazo:

(1). Masahaba wote hawa ni Muhajirin na hakuna hata mmoja ambaye ni Ansari – kutelekezwa kunakoshangaza kweli! Kama vile tu Ansari walivyokuwa hawana nafasi katika serikali ya Saqifah, sasa itaonekana kwamba hawakuwa na nafasi huko peponi pia. Ni ajabu kweli kwamba Mtume hakuweza kumpata hata Ansari mmoja aliyekuwa anastahili kuwa kwenye kundi hili la watu kumi. Na bado, hata hivyo, walikuwa ni Ansari ambao walikuwa wametoa hifadhi kwa Uislamu na kwa hao Muhajirin wenyewe.

Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) hakuwa ama mtovu wa shukurani au msahaulifu. Asingeweza kusahau ukarimu ulioonyeshwa na Ansari kwake. Kwa kweli, alikuwa ameupokea ukarimu wa Ansari kwa furaha kubwa. Kwa upande mwingine, yeye alikuwa na mashaka mengi katika kukubali wajibu wowote kutoka kwa Muhajirin yeyote, na kamwe hakukubali. Kama hakuwa mtovu wa shukurani, na hakuwa hivyo, basi hii “Hadith” haiwezi kuwa ya kweli.

(2). Baadhi ya hawa wakazi wa peponi, walipokuwa wanaishi kwenye dunia hii, walikuwa
wakipigana mmoja dhidi ya mwingine, na walikuwa wakijaribu kuuana. Wawili wa hao–
Talha na Zubeir–walikuwa wakiwachochea watu kumuua khalifa aliyekuwa madarakani–
Uthman–ambaye pia alikuwa mmoja wa kundi hilo hilo. Baadaye, wote hao walivunja kiapo
chao cha utii kwa khalifa mwingine aliyekuwa madarakani–Ali –na wakamwaga damu ya maelfu ya Waislamu waliokuwa hawana hatia. Kwa kweli, Ali alijaribu kuwaokoa Waislamu hao hao wasiuliwe.

Na bado, kulingana na Hadith hii, wauaji hawa waliofichika na waathirika waliofichika – wote wataingia peponi!

(3). Hata miongoni mwa Muhajirin, walikuwepo watu ambao walikuwa na sifa kubwa kuliko baadhi ya hawa watu kumi lakini Mtume hakuwahakikishia hata mmoja wao kwamba ataingia peponi. Mas’ab ibn Umayr, Abdallah ibn Mas’ud, Bilal ibn Ribah, Zayd ibn Haritha, na mwanawe Usamah, na Abdallah ibn Rawaha, walikuwa na sifa nyingi kabisa kuliko Uthman, Abdur Rahman ibn Auf, Ubaidullah bin Aamir al-Jarrah, na Said bin Zayd, na bado Mtume hakuwapa uhakikisho wowote kwamba wataingia peponi.

Ilikuwa haijulikani ni kipimo gani cha kuamulia ni nani atakayeingia peponi, na ni nani atakayenyimwa ruksa ya kuingia. Kama uchamungu ndio kigezo cha kuingilia peponi, basi miongoni mwa masahaba – Muhajirin na Ansari pia – walikuwemo wengine wengi ambao walikuwa wachamungu zaidi na watiifu zaidi kuliko baadhi ya hawa watu kumi. Watano kati yao hawa walikuwa ni makabaila wakubwa. Walikuwa ndio nguzo za mfumo wa kikabaila wa Waislamu.

Hakuna ubaya katika kuwa kabaila kama hivyo; lakini ukabaila, hususan katika muundo wake mtupu, ulikuwa ndio mfano wa mfumo wa kiuchumi dhidi yake ambao, Muhammad, Mtume wa Allah swt. alikuwa akipigana nao maisha yake yote. Alipigana dhidi yake kwa sababu ulisimama katika msingi wa unyonyaji wa kikatili na mwingi kwa masikini. Aliukuta ukabaila wa uporaji ukitumiwa na kulindwa na muungano wa wakiritimba wa Makuraish wa Makka. Muungano huo wa wakiritimba ulikuwa madhubuti, imara na usioshindika lakini kupitia juhudi za muda mrefu na za mfululizo, hatimae aliweza kuubo- moa.

Muhammad kamwe hakujihusisha na hao walezi wa mfumo wa kikabaila. Kwa upande mwingine, yeye alijihusisha na masikini. Mara kwa mara alikuwa akisema: Alfaqru fakhri (Umasikini ndio fakhari yangu). Lakini baada ya kifo chake, ule mfumo wa kikabaila ulichimbuka na ukafufuliwa. Ile Kamati ya Uchaguzi ambayo Umar aliyokuwa ameiteuwa ili kuchagua khalifa mpya, ilikuwa ni muungano wa ukiritimba wa makabaila (wapya), ulioanzishwa upya katika nyakati za Kiislamu. Ni kweli kwamba alimfanya Ali kuwa mmoja wa wachaguzi lakini baadae hakuwa kwenye kundi hilo. Kwa kweli. Uhusiano wake na muungano huu wa wakiritimba ulikuwa sawa sawa na ule wa Muhammad kwa muungano wa wakiritimba wa Makuraish kule Makka.

Miungano yote hii ilikuwa ni maalum (kwa watu fulani tu). Ule muungano wa Makka uli- watenga wale wasiokuwa Makuraish na masikini kutoka kwenye uanachama wake; ule muungano wa Madina uliwatenga Ansari na masikini kutoka kwenye uanachama wake. Miungano yote iliendeshwa na Makuraish kwa manufaa pekee ya Makuraish.

Ukabaila huu mpya “ulitakaswa” kwa sababu ya uhusiano wake na masahaba mashuhuri wa Mtume, na haraka sana ukapanda kwenye mahali pa utawala katika Dar-ul-Islam kiasi kwamba haikuwezekana kuung’oa tena.

Pale Ali alipojaribu kuung’oa, walezi wake (wa mfumo huo) walimpinga yeye, na Dola ya Kiislamu ikalipuka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Muda si mrefu Ali akauawa, na baada ya kuuawa kwake, ukabaila wa unyang’anyi uka- jikuta uko huru kutamba bila kuzuiwa na kwa jeuri juu ya mandhari ya Uislamu.

Waislamu wa Shi’ah wanaichukulia “Ashara Mubashara” kama ni Hadith ya uongo kwa sababu haikubaliani na akili, na chini zaidi, pamoja na maadili ya kijamii ya Kiislamu. Wanaichukulia kama ni matokeo ya ule ugonjwa unaoitwa “uundaji.” Kiini chake, wao Shi’ah wanaamini, kilikuwa ni kuwabadili watu wa kawaida kuwa mfano hasa wa kihistoria usiosahaulika milele.