read

Mihanga Ya Muhammad Kwa Ajili Ya Uislamu

Malengo Makubwa, ili yafatimie, yanahitaji mihanga, na kufanikiwa katika kupata hali halisi kutokana nayo kunakuja kwa gharama kubwa. Lengo kubwa zaidi, gharama kubwa zaidi atakayolipia mtu kulifanikisha.

Mapambano ya mwanadamu kujikomboa kutoka kwenye minyororo ya utumwa na udhalimu yana umri wa maelfu ya miaka, na yamechukua maisha ya watu yasiyo idadi. Mapambano yanaendelea leo hii kama yalivyokuwa huko nyuma, na Hadith yake haina mwisho kwa sababu mapambano yenyewe hayana mwisho.

Matatu kati ya matukio muhimu katika mapambano ya mwanadamu kwa ajili ya uhuru ni yale Mapinduzi ya ki-Faransa ya mwaka 1789, Mapinduzi ya ki-Russi ya mwaka 1917, na Mapinduzi ya ki-China ya mwaka 1949. Haya pia ni matatu kati matukio ya maana sana katika historia ya ulimwengu.

Mikondo ya damu iliibuka kufuatia mapinduzi haya, na yalivyokuwa yakipungua, yaliibeba ile mifumo na mifano ya kizamani ya ukandamizaji na unyonyaji pamoja nayo. Mapinduzi haya yalianzisha nguvu mpya ambazo hadi leo hii zinaisukasuka dunia yote. Yalikuwa ndio gharama mwanadamu alikuwa ailipe kununua uhuru wake wa kisiasa na kiuchumi.

(Mapinduzi ya Kirusi na Dola ya Sovieti yalianguka, katika hayo, baada ya miaka 73 – mnamo mwaka 1990. Yalithibitika kutowezekana.)

Karne nyingi baadaye, yaani, katika karne ya saba, mapinduzi mengine yalibadili mwelekeo wa historia. Yalikuwa ni moja ya mapinduzi makubwa ya nyakati zote lakini jambo la kipekee kuhusu mapinduzi haya ni kwamba yalikuwa ya amani. Hayakutengeneza mikondo yoyote ya damu, na kwa kweli, yanapaswa kuitwa mapinduzi “yasiyo na umwagaji damu.” Yalikuwa ni ujumbe wa amani. Amani ilikuwa ndio beji yake, na amani au Uislamu lilikuwa ndio jina lake.

Ingawa Uislamu ulitetea amani katika ulimwengu, haukuwa umewezekana bila ya mapambano. Ulikuwa, kwa kweli, umefungwa, kwa miaka 23, katika mapambano ya kumwaga damu kwa ajili ya uhai wake, na kama vile tu mavuguvugu makubwa juu ya ukombozi, ulihitaji vilevile mihanga. Ni ajabu kwamba Muhammad - Mjumbe wa Allah swt. na Mtume wa Uislamu – hakuwaiga viongozi wengine ambao wanawasukuma wafuasi wao kwenye milipuko ya vita kwa jina la “muhanga” kwa ajili ya mfano bora. Yeye mwenyewe alikuwa ndiye mtu wa kwanza kutoa makafara kwa ajili ya Uislamu.

Ufafanuzi wa Webster wa muhanga ni kupata hasara kwa ajili ya kuweka mfano bora. Mtu kutoa mali yake anayoithamini sana kwa ajili ya mfano mwema kunafanya kafara.

Wengi wa manabii na mitume waliishi maisha ya muhanga. Ibrahim alimtoa mwanawe, Ismail, kama kafara; na Yahya (Yohana) alijitolea maisha yake mwenyewe kama kafara. Ismail angeweza kuuawa lakini akabadilishwa wakati ule ule na mwana kondoo. Yahya hata hivyo, yeye aliuawa, na kichwa chake kikabidhiwa kwa mwanamke fasiki kutuliza kiburi chake. Yeye ni mmojawapo wa wahanga (shahiid) wakubwa wa nyakati zote.

Hii ni miwili kati ya mifano mingi ya kafara ambayo ilihitaji ujasiri mkubwa na imani kubwa. Lakini yote kwa mtazamo wa ubora na ukubwa, ile mihanga Muhammad aliyotoa kwa ajili ya Uislamu, inabakia kutolinganishika katika historia.

Tofauti lazima ionyeshwe hapa kati ya makafara ya mali na makafara ya uhai. Muhammad (s.a.w.w.) alifanya yote. Alitoa muhanga hali njema zake binafsi zote, na mali zote alizokuwa akimiliki kwa ajili ya Uislamu. Hili, bila shaka kila mtu analijua. Ambacho labda hakijulikani sana, ni ule ukweli kwamba baadhi ya jamaa zake wa karibu na wapenzi wake walikuwa wameuawa katika ketetea Uislamu. Ndugu zake Muhammad waliofanya maisha yao dhabihu kwa ajili ya Uislamu, ni kama wafuatao:

1. Al-Harith ibn Abi Hala, mwana wa kulelewa, na mpwawe Khadija. Aliuawa huko Makka.
2. Ubaidullah ibn al-Harith ibn Abdul-Muttalib, binamu yake. Aliuawa katika vita vya Badr.
3. Hamza ibn Abdul-Muttalib, ami yake. Aliuawa katika vita vya Uhud.
4. Mas’ab ibn Umayr, ami yake. Aliuawa katika vita vya Uhud.
5. Abdallah ibn Jahash, binamu yake. Aliuawa huko Uhud.
6. Zayd ibn Haritha, mwana wa kulea na rafiki. Yeye aliuawa katika vita vya Muutah.
7. Jaafar Tayyar ibn Abi Talib, binamu yake. Yeye aliuawa katika vita vya Muutah.
8. Ayman ibn Ubayd, kaka wa kunyonya. Huyu aliuawa katika vita vya Hunayn.

Hii ni orodha ya baadhi ya majina yanayotambulika sana katika Uislamu wote, na inajumuisha ami zake wawili, binamu watatu, watoto wa kutwaliwa wawili, na kaka wa kunyonya mmoja wa Muhammad (s.a.w.w.). Ilikuwa ni kwa kupitia mihanga hii ambapo aliufanya Uislamu kutodhurika na kutoharibika.

Muhammad (s.a.w.w.) kamwe hakufanya jaribio la kutaka kuwalinda wale aliwapenda yeye mwenyewe. Walikuwa, kwa kweli, ni wale wapenzi wake ambao ndio walikuwa wa mbele kabisa katika kukabiliana na changamoto ya adui. Hakuna aliyekuwa akimpenda kuliko Ali, na bado, nafasi ya hatari kubwa zaidi katika kila makabiliano na wapagani – ndani ya Makka au Madina – ilikuwa siku zote imewekewa yeye.

Makafara makubwa kabisa kwa ajili ya Uislamu yote yalitolewa na Muhammad na Ali. Kwa upande mwingine, Abu Bakr na Umar hawakufanya makafara yoyote. Kwa jinsi makafara kwa ajili ya Uislamu yanavyohusika, wao hawana chochote cha kuonyesha. Wakati wowote ilipotokea changamoto kutoka kwa wapagani, kama ilivyokuja wakati wa vita vya Badr, Uhud na Khandaq, wao (Abu Bakr na Umar) hawakuipokea; na hakuna mtu wa familia zao aliyeuawa katika utetezi wa Uislamu katika wakati wowote ule. Ndugu pekee ambaye Umar alimpoteza kamwe kwenye mapambano ya Uislamu na upa- gani alikuwa ni mjomba wake, Abu Jahl, ambaye aliuawa katika vita vya Badr.

Taji la shahada ndio heshima kubwa na sifa kubwa ambayo Uislamu unaweza kuitoa juu ya Muislamu katika dunia hii. Wapendwa wa Muhammad na Ali walipata shahada nane katika uhai wa Muhammad (s.a.w.w.), na walitakiwa kupata nyingine nyingi zaidi baada ya kifo chake. Allah swt. awarehemu wote hao.