read

Montgomery

Lengo la mkakati la watu wa Makka halikuwa ni chochote pungufu zaidi ya kuiangamiza jamii ya Waislamu kama hivyo, au – kile kinacholingana na jambo hilo hilo – kumuondoa Muhammad kutoka kwenye nafasi yake ya mamlaka. (Muhammad, Prophet and Statesman)

Wakisukumwa na lengo hili, na kwa nguvu ya shauku ya kufanya fidia kwa ajili ya kushindwa kwa siku zilizopita, hawa viongozi wa Makka walianza maandalizi kwa ajili ya vita vya juhudi zote; vita ambavyo vitakuwa ni mwisho wa vita nyingine zote kwa kuuteketeza kabisa Uislamu!

Ndani ya miaka miwili Maquraishi waliunda jeshi la mapambano la wapiganaji elfu kumi. Hili lilikuwa ndio jeshi kubwa kabisa lililowahi kukusanywa na Waarabu mpaka wakati huo. Pamoja na shangwe kubwa na kujiamini, jeshi hili la kutisha liliondoka Makka mwezi wa Februari, 627A.D. kwenda kuiteka Madina na kufutilia mbali Uislamu.

Muhammad Husein Haykal

Wakati habari za uhamasishaji huu mkubwa mno zilipomfikia Muhammad na Waislamu huko Madina, ziliwatia wote wasiwasi. Uhamasishaji wa Arabia yote dhidi yao uliingiza hofu ndani ya mioyo yao kwani walikuwa wanakabiliwa na matarajio sio tu ya kushindwa bali kuteketezwa kabisa. Uzito halisi wa hali hiyo ulikuwa dhahiri katika ukweli kwamba lile jeshi ambalo makabila ya Kiarabu sasa walikuwa wameliunda lilikuwa limezidi katika idadi na zana, kitu chochote ambacho Peninsula hiyo imewahi kushuhudia kabla…. (The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Mtume (s.a.w.) aliitisha mkutano wa dharura wa maswahaba wake wakuu kushauriana nao katika suala la kuulinda mji. Kitu kimoja kilikuwa wazi. Waislamu walikuwa wachache sana kwa idadi na wadhaifu sana katika zana kwamba walikuwa hawawezi kukutana na lile jeshi linalovamia kwenye ardhi ya wazi. Madina ilikuwa ilindwe kutoka ndani yake. Lakini vipi? Vipi askari wa ulinzi wachache wa Waislamu wataweza kulizuia jeshi la Makka kutokana na kuivamia na kuizagaa Madina ambayo ingekuwa imejaa idadi ya watu wasio- fuzu, lilikuwa ndio swali katika akili ya kila mtu.

Mmoja wa marafiki wa karibu wa Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) alikuwa ni Salman yule Muajemi. Alizaliwa na kukulia huko Uajemi (Iran) lakini aliishi kwa miaka mingi huko Syria na Palestina, na alikuwa na uzoefu wa vita na operesheni za kuzingira za wote, Waajemi na Warumi. Madina ilikuwa na ulinzi wa asili au uliotengenezwa na watu katika pande tatu lakini ilikuwa wazi katika upande mmoja, yaani, ule upande wa kaskazini. Salman alimwambia Mtume (s.a.w.) kwamba kama handaki lingechimbwa katika upande wa kaskazini, mji ule pengine ungeweza kulindwa kwa mafanikio.

Wazo hili, ingawa ni geni na lisilo la kawaida katika Arabia, lilimvutia Mtume. Akalikubali na kuwaamuru Waislamu kulichimba handaki hilo.

Muhammad Husein Haykal

Salman al-Farsi, aliyejua vizuri zaidi juu ya mbinu za vita kuliko ilivyokuwa kawai- da hapo katika Peninsula. Alishauri kuchimbwa kwa handaki kavu kuzunguka Madina na kuimarisha kwa majengo yaliyomo ndani yake. Waislamu waliharakisha kutekeleza ushauri huo.

Handaki lilichimbwa na Mtume – rehema na amani za Allah (s.w.t.) ziwe juu yake – alifanya kazi kwa mikono yake sambamba na maswahaba zake kutoa uchafu, kuwatia moyo wale Waislamu wanaofanya kazi, na kumshawishi kila mtu kuongeza juhudi zake. (The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Kwa kuwa lile jeshi la Makka lilijulikana kwamba linasogelea Madina kwa haraka, hapakuwa na muda wa kupoteza, na Waislamu walifanya kazi kwa harakati kubwa – kwa kupokezana.

Ndani ya siku sita handaki hilo likawa limechimbwa, mapema tu kuwazuia wavamizi kuuchukua mji kwa uvamizi.

Kikosi cha wapanda farasi wa Makka kilikuja kama kimbunga lakini ghafla kikazuiwa, katika kasi yake, na handaki hilo. Wapanda farasi hao waliwasimamisha farasi wao kwenye ukingo wake. Mkakati wao mkuu ulikuwa ni kuiteka kwa nguvu Madina kwa masaa machache lakini sasa ilionekana kwao kwamba hawawezi kufanya hivyo. Hapa kulikuwa na handaki, kikwazo kipya ambacho hawakuweza kukipita. Limeingia vipi kwenye mkakati wao? Waliduwazwa kabisa na handaki hilo.

Hatimae, na baada ya majadiliano marefu, makamanda wa Makka waliamua kuizingira Madina, na kuwalazimisha Waislamu kuswalimu amri, kwa msuguano (kuwadhoofisha). Walifunga njia zote za kutoka nje ya Madina, na kuwazunguka Waislamu. Madina ilikuwa katika hali ya kuzingirwa!

Ingawa alikuwa ni Abu Sufyan ambaye aliongoza kampeni hiyo nzima, na alikuwa ndiye mkurugenzi wake wa utendaji, hakuwa mtu mpiganaji yeye mwenyewe. Mpiganaji wa jeshi lake alikuwa ni Amr ibn Abd Wudd, mkali zaidi kati ya wapiganaji wa wapagani wa Arabia. Matumaini ya Abu Sufyan ya ushindi wa haraka na wenye uamuzi juu ya Waislamu yalikuwa juu yake huyu. M. Shibli, yule mwanahistoria wa kihindi, na Abbas Mahmud Al-Akkad, yule mwanahistoria wa Misri, wanasema kwamba Amr ibn Abd Wudd alihesabiwa, na Waarabu wa wakati huo, kuwa zaidi ya usawa na askari wa farasi elfu moja.

Amr ibn Abd Wudd hakuwa akipendezewa na vita tulivu au mzingiro (karantini). Alitweta kwa kutaka vitendo. Wakati siku chache zilipokuwa zimepita, na hakuna chochote kilichotokea, alipoteza subira, na akaamua kuiteka Madina kwa vitendo vyake mwenyewe. Siku moja, akiranda kuzunguka Madina kwa kuvizia, yeye pamoja na mashujaa wengine watatu wa Makka waligundua sehemu yenye mawemawe ambapo lile handaki halikuwa pana sana. Waliwatia chonjo farasi wao kutoka kwenye sehemu hiyo, na wakafanikiwa katika kulivuka lile handaki!

Sasa Amr alikuwa ndani ya mzingo wa Madina. Kwa ujasiri kabisa akasonga mbele kwenye kambi ya Waislamu, na kuwapa changamoto mashujaa wa Kiislam kutoka na kupigana dhidi yake katika desturi ya jadi ya Kiarabu ya mapambano ya watu wawili wawili.

Changamoto ya kwanza ya Amr ilipita bila kujibiwa kwa hiyo akairudia lakini bado hakupata jibu. Hiyo ndiyo fahari kuu ya jina lake kwamba hakuna yeyote katika kambi ya Waislamu aliyethubutu kukabiliana naye katika kupimana nguvu. Kama waabudu masanamu waliyaona kwake matumaini ya ushindi, Waislamu waliona katika changamoto yake hukumu ya kifo chao.

Amr ibn Abd Wudd alitoa changamoto yake yenye dharau kwa mara ya tatu na akawadhihaki Waislamu wakati huo huo kwa woga wao.

Kwa Amr lazima itakuwa imeelekea kwamba Waislamu walikuwa wameishiwa na nguvu kwa woga, ambavyo wengi wao, kwa kweli, walikuwa hivyo. Qur’an Tukufu pia imechora picha ya hali ya Waislamu katika kuzingirwa Madina katika Aya zifatazo:

إِذْ جَاءُوكُمْ مِنْ فَوْقِكُمْ وَمِنْ أَسْفَلَ مِنْكُمْ وَإِذْ زَاغَتِ الْأَبْصَارُ وَبَلَغَتِ الْقُلُوبُ الْحَنَاجِرَ وَتَظُنُّونَ بِاللَّهِ الظُّنُونَا {10}

“Tazama! Walikujieni kutoka juu yenu, na kutoka chini yenu, na tazama; macho yalipofifia, na nyoyo zikapanda kooni, nanyi mkamdhania Allah dhana mbalimbali.” (Sura ya 33; Aya ya 10)

وَإِذْ قَالَتْ طَائِفَةٌ مِنْهُمْ يَا أَهْلَ يَثْرِبَ لَا مُقَامَ لَكُمْ فَارْجِعُوا ۚ وَيَسْتَأْذِنُ فَرِيقٌ مِنْهُمُ النَّبِيَّ يَقُولُونَ إِنَّ بُيُوتَنَا عَوْرَةٌ وَمَا هِيَ بِعَوْرَةٍ ۖ إِنْ يُرِيدُونَ إِلَّا فِرَارًا {13}

“Tazama! Na kundi moja kati yao likasema: ‘Enyi watu wa Yathrib! Hamuwezi kuhimili (shambulizi). Hivyo rudini’ na kundi jingine kati yao likaomba ruhusa kwa Mtume (s.a.w.) likisema: ‘Hakika nyumba zetu ni tupu na wazi’ Wala hazikuwa wazi; hawakutaka chochote ila kukimbia tu.” (Sura ya 33; Aya ya 13)

Amr ibn Abd Wudd pia alionyesha mshangao kwamba wale Waislamu hawakuwa wakionyesha shauku yoyote ya kuingia peponi ambako alikuwa tayari kuwapeleka.

Ni kweli kwamba wengi wa Waislamu walikuwa wamekumbwa na hofu lakini alikuwepo mmoja kati yao ambaye hakuwa hivyo.
Alikuwa, kwa kweli, amejitolea kuikubali changamoto ya kwanza kabisa ya Amr lakini Mtume (s.a.w.) alimzuia, akitegemea kwamba mtu mwingine yeyote angependa kumkabili Amr. Lakini aliweza kuona kwamba hakuna hata mmoja aliyethubutu kunyoosheana panga naye.

Huyu kijana mdogo aliyekuwa tayari kuipokea changamoto ya Amr hakuwa mwingine yoyote mbali na Ali ibn Abi Talib, yule shujaa wa Uislamu. Pale Amr alipotupa changamoto yake ya tatu, na hapakuwa na mtu aliyemjibu, Ali alisimama na kuomba ruhusa ya Mtume (s.a.w.) ya kutoka na kupigana dhidi yake.

Mtume wa Uislamu hakuwa na budi tena sasa ila kumruhusu binamu yake, Ali, yule Simba wa Uislamu, kwenda na kunyamazisha zile dhihaka na kejeli za Amr Ibn Abd Wudd.

Ali alivaa lile vazi la vita la Mtume wa Uislamu. Mtume (s.a.w.) mwenyewe akaning’inizia Dhu’l-Fiqar (upanga wake) pembeni mwake, na kumuombea kwa ajili ya ushindi wake, akisema: “Ewe Allah! Ulimwita kwenye huduma yako, Ubaida ibn al-Harith, ile siku ambayo vita vya Badr vilipopiganwa, na Hamza ibn Abdul-Muttalib, siku ambayo vita vya Uhud vilipopiganwa. Sasa ni Ali pekee aliyebakia nami. Kuwa Wewe Mlinzi wake, mpatie yeye ushindi, na mrudishe salama kwangu.”

Wakati Mtume (s.a.w.) alipomwona Ali akienda kuelekea kwa adui yake, alisema: “Yeye ndiye tashihisi wa Imani yote ambaye anakwenda kupambana na tashihisi ya Ukafiri wote.”

Muda mchache baadae, Ali alikuwa amesimama mbele ya Amr. Mashujaa wawili hawa wakatambulishana, na wakapimana. Ali alikuwa na seti ya kanuni ambazo alizitumia katika hali zote ama za vita au za amani. Kwenye vita vya handaki, Waislamu na wapagani waliona maonyesho ya matumizi ya kanuni hizo. Wakati wowote alipokabiliana na adui, alimpa hiari ya kuchagua kati mambo matatu. Nayo yalikuwa ni:

1. Ali aliutambulisha rasmi Uislamu kwa adui yake. Alimualika kuacha uabudu-sanamu na kuukubali Uislamu. Mwaliko huu ulimfanya Ali mubaligh wa Uislamu katika uwanja wa vita wenyewe.

2. Kama adui huyo hakuukubali mwaliko wa Ali wa kuukubali Uislamu, alimshauri yeye kujiondoa kutoka kwenye vita, na asipigane dhidi ya Allah (s.w.t.) na Mtume wake. Kupigana dhidi yao, alimuonya, kutamletea tu laana ya milele juu yake katika dunia zote mbili.

3. Kama adui huyo hakukubali chaguo hili la pili pia, na akakataa kujiondoa kwenye vita, basi Ali alimkaribisha kutupa dhoruba ya kwanza. Ali mwenyewe kamwe hakuwa wa kwanza kushambulia adui.

Amr ibn Abd Wudd alidharau hata kufikiria lile chaguo la kwanza na la pili lakini akakubali hili la tatu, na akapiga dhoruba kubwa kwa upanga wake mkubwa sana ambao ulikata kupita kwenye ngao, kofia ya chuma na kilemba cha Ali, na kufanya jeraha kubwa sana kwenye paji lake la uso.

Damu iliruka kutoka kwenye jeraha hilo katika mchirizi lakini Ali hakuvunjika moyo. Alipata nguvu, na kisha akatupa pigo la kujibu kwa upanga ule maarufu Dhu’l-Fiqar, na ukampasua yule mpiganaji wa kutisha wa Arabia katika vipande viwili!

Wakati Amr alipouawa, wale mashujaa watatu katika msafara wake waligeuka na kuwatia chonjo farasi wao kukimbia. Ali akawaacha wakimbie. Ilikuwa ni moja ya kanuni zake kutomfukuza adui anayekimbia. Yeyote yule aliyetaka kuokoa maisha yake, Ali alimwacha ayaokoe.

Kifo cha Amr ibn Abd Wudd kilivunja mgongo wa mashambulizi ya Makka dhidi ya Uislamu, na kuvunja hamasa yao. Nguvu za asili pia zilitangaza vita dhidi yao. Joto lilishuka kufikia kiwango cha kuganda, na wingu la vumbi lilinyanyuka ambalo lilivuma kwenye nyuso zao.

Wakiwa wamekata tamaa na kuvunjika moyo, wale jamaa wa makabila wenye kigeugeu walianza kuwaacha marafiki zao wa Makka, kwanza mmoja mmoja na wawili wawili na watatu watatu, na kisha kwa makumi na ishirini ishirini, na baadae kidogo, kwa mamia. Ule muungano ukaanza kutoweka polepole kwa uwazi kabisa. Abu Sufyan alilazimika kuacha kuzingira, na akatoa ishara kwa jeshi lake kurudi nyuma kutoka Madina. Jeshi lake lilitawanyika, na kampeni yake ilikuwa imeshindwa vibaya. Madina ilikuwa imeokolewa.
Kushindwa kwa mzingiro (karantini) wa Madina kwa waabudu-masanamu wa Makka lilikuwa ni tukio muhimu sana katika historia ya Arabia. Ilimaanisha kwamba watakuwa hawawezi kamwe kuandaa uvamizi mwingine wa Madina. Baada ya vile vita vya handaki, uamuzi ukahama, hatimae na kwa dhahiri kabisa, kutoka kwa waabudu-sanamu wa Makka kwenda kwa Waislamu wa Madina.

Madina na Uislamu viliokolewa na wazo na shujaa. Wazo lilikuwa ni lile handaki ambalo liliwazuia askari wa farasi wa Makka. Ilikuwa ni fikra mpya kabisa katika vita vya Uarabuni, na Waarabu hawakuwa na uzoefu nayo. Bila ya hilo handaki, wale watu elfu kumi wa kabila la majambazi wangeweza kuivamia na kuizagaa Madina, na wangemuua kila mtu humo. Heshima ya kuiokoa Madina-tun-Nabi, mji wa Mtume, na makao makuu ya Uislamu, inakwenda kwa Salman yule Muajemi, na kwa bwana wake, Mtume (s.a.w.) mwenyewe. Huyu wa kwanza alianzisha wazo jipya katika kanuni za kijeshi; na huyu mwingine alionekana tayari ni mwenye kulisikiliza, na papo hapo akalitekeleza.

Kila mmoja hapo Madina alidai kuwa ni rafiki au sahaba wa Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) Mji huo ulikuwa na fungu lake wenyewe la watu wenye kutafuta umaarufu. Lakini walikuwepo wachache, kwa kweli wachache sana, watu ambao Muhammad mwenyewe amewakiri kama marafiki zake. Salman, yule Muajemi alihusika kwenye kundi hili teule, ule mzunguko wa ndani kabisa wa marafiki wa Mtume wa Allah (s.a.w.)

Salman alikuwa mtu wa kimo kirefu sana na nguvu za kimwili nyingi mno. Wakati handaki lilipokuwa linachimbwa, alifanya kazi kama ya watu sita wengine. Hili lilimshawishi mmoja wa Muhajirina kutangaza kwamba Salman alikuwa mmoja wao, yaani alikuwa Muhajirina. Lakini alipingwa mara moja na Ansari ambao mmoja wao alisema kwamba Salman alikuwa ni Ansari na sio Muhajir. Makundi mawili hayo yalikuwa bado yanabishana wakati Mtume (s.a.w.) alipowasili hapo kwenye tukio. Yeye pia aliyasikia madai ya pande zote mbili na ali- furahishwa nayo. Lakini aliyakatisha mabishano hayo kwa kutoa “fatwa” yake binafsi. Alisema kwamba Salman hakuwa Muhajir wala Ansari bali alikuwa ni mtu wa nyumba yake mwenyewe – ni Ahlul-Bayt – mtu wa nyumba ya Muhammad Mustafa mwenyewe!

Yule mwanahistoria wa Kiarabu, Ibn Athir, amemnukuu Mtume (s.a.w.) ndani ya kitabu chake, Tarikh Kamil, juz. 2, uk.122, kwamba alisema: “Salman ni mmoja wetu. Yeye ni mtu wa Nyumba yetu.” Hii ndio heshima kubwa kabisa ambayo kamwe haijawahi kutole- wa kwa sahaba wake yeyote na Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.)

Salman alikuwa ni mkristo aliyekuwa akiishi huko Ammuria-Asia Ndogo, wakati aliposikia kwa mara ya kwanza habari zisizokuwa na yakini za kutokea kwa Mtume (s.a.w.) huko Hijazi.

Ili kuhakikisha habari hizi, alikuja Madina. Wakati alipouangalia kwa mara ya kwanza uso wa Mtume, aliguta kwa mshangao: “Huu hauwezi kuwa uso wa mtu ambaye amewahi kamwe kusema uongo,” na papo hapo akasilimu.

Uislamu ulimkubali Salman kama vile yeye “alivyoukubali” Uislamu. Uislamu ukawa ni kiunganisho cha hisia zake, naye akawa ni sehemu yake ya “mtiririko wa damu.” Huko Madina, safari moja mgeni mmoja akamuuliza yeye jina la baba yake. Jibu lake lilikuwa ni: “Uislamu! Jina la baba yangu ni Uislamu. Mimi ni Salman mtoto wa Uislamu.” Salman “alichanganyika” kwenye Uislamu kwelikweli kiasi kwamba alikuwa hatofautishiki nao.

Tishio kwenye usalama wa Madina, hata hivyo, halikwisha kwa kuchimbwa kwa hilo handaki. Madini ilikuwa bado sio salama. Kwenye sehemu ambayo lile handaki lilikuwa jem- bamba, yule jenerali wa jeshi la Makka na mashujaa wengine watatu, waliweza kuruka juu yake na kwenda (kwa farasi) kwenye kambi ya Waislamu.

Kama walifanikiwa kuanzisha daraja ya kuvukia juu ya handaki hilo, jeshi la farasi lote la Makka na askari wa miguu, na maharamia wasiotabirika wangeweza kuingia mjini humo na kuuteka. Lakini Ali aliwazuia na kuwashinda kabisa. Hivyo werevu wa Salman, busara za Muhammad na upanga wa Ali vilithubutu kuwa ulinzi bora wa Uislamu dhidi ya muungano wa kutisha wa washirikina katika historia ya Uarabuni.

Ilikuwa ni desturi katika vita za Kiarabu kumpora adui aliyeshindwa silaha zake, mavazi ya chuma – deraya na farasi wake. Katika kuizingira Madina, Amr alikuwa amevaa deraya nzuri sana katika Arabuni yote.
Ali alimuua lakini hakugusa kitu chochote ambacho kilikuwa mali yake, kwa mshangao mkubwa sana wa Umar ibn al-Khattab. Baadae, wakati dada yake Amr alipokuja kwenye maiti yake kumlilia kifo chake, yeye pia alishangaa kugundua kwamba silaha zake na mavazi viko salama. Alipoambiwa kwamba alikuwa ni Ali aliyemuua, alitunga beti kadhaa za kumsifia yeye (Ali).

Beti hizi zimenakiliwa na yule mwanahistoria wa Misri, Abbas Mahmud Al-Akkad, katika kitabu chake, Al-Abqariyyat Imam Ali (kipaji cha Imam Ali), na zinaweza kutarjumiwa kijuujuu kama ifuatavyo: “Kama mtu mwingine mbali na Ali angemuua Amr, Ningehuzunikia kifo chake maisha yangu yote. Lakini mtu aliyemuua yeye ni shujaa na hana kifani. Baba yake pia alikuwa ni muungwana.”

Akitoa maelezo juu ya mistari hii, Abbas Mahmud Al-Akkad anasema kwamba kabila halikuchukulia kuwa ni fedheha kama mmojawapo wa mashujaa wao aliuawa na Ali.

Ali alikuwa ndiye jasiri zaidi na muungwana zaidi kwa maadui, na pia alikuwa asiyeshindika. Baada ya kushindwa kwa kule kuizingira Madina, yale makabila yote kati ya Madina na Bahari Nyekundu na kati ya Madina na Yammama kwa upande wa Mashariki, yaliweka saini mikataba ya amani na Mtume wa Uislamu.

Katika mwaka huo huo, yaani mwaka wa 5 H.A. (627 A.D.), Hajj (kwenda kuhiji Makka) ilifanywa ni lazima kwa wale Waislamu wote waliokuwa na hali nzuri ya kifedha na walio na afya njema.